(Nairobi) – Katika karibu theluthi moja ya mataifa ya barani Afrika, wasichana wenye umri wa kubaleghe ambao ni wajawazito, wanakabiliwa na vikwazo vingi vya kisheria na sera dhidi ya kuendeleza masomo yao, Shirika la Human Rights Watch limesema leo. Hata hivyo, serikali nyingi barani Afrika, zimeweka sheria, sera na taratibu za kulinda haki za wanafunzi wajawazito au akina mama vijana.
Kielelezo kipya cha mwingiliano kilichoundwa na shirika la Human Rights Watch pamoja na mkusanyiko wa sheria na sera zinazohusiana na mimba za utotoni shuleni katika nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU), kinaonyesha kwa umakini sheria na sera zilizowekwa na vile vile changamoto za kulinda haki ya wasichana hao kupata elimu. Shirika la Human Rights Watch limesema kwamba, mifumo inayolinda haki za kibinadamu ni miongoni mwa hatua muhimu katika kulinda haki za wasichana wajawazito kupata elimu. Serikali zinafaa kuzingatia umuhimu wa utekelezaji na ufuatiliaji wa sera katika shule zote. Bila hatua hizo, maelfu ya wanafunzi barani Afrika wataendelea kunyimwa nafasi ya kuendeleza masomo yao.
“Wasichana wengi wajawazito na akina mama vijana barani Afrika bado wananyimwa haki yao ya kimsingi ya kupata elimu kwa sababu ambazo hazihusiani na azma ama uwezo wao wa kusoma,” alisema Adi Radhakrishnan, mwanachama wa taasisi ya Leonard H. Sandler katika kitengo cha haki za watoto katika Shirika la Human Rights Watch. “Serikali hazifai kusitisha haki ya wasichana kupata elimu kama adhabu ya kupata mimba.”
Shirika la Human Rights Watch lilihakiki zaidi ya sheria na sera 100 zinazohusu elimu, usawa wa jinsia, na vile vile sera na mipango inayohusiano na afya ya uzazi katika mataifa wanachama wa Umoja wa Afrika.
Mataifa thelathini na nane kati ya hamsini na nne barani Afrika, yana sheria, sera na taratibu za kulinda haki za wasichana wenye umri wa kubalehe kupata elimu wakiwa wajawazito na hata baada ya kupata watoto. Baadhi ya nchi hivi majuzi ziliondoa sera zinazohujumu haki ya wasichana kupata elimu. Mnamo mwezi Machi 2022, Togo ilifutilia mbali agizo la serikali la mwaka 1978 ambalo liliwapiga marufuku wanafunzi wajawazito na akina mama vijana dhidi ya kuendelea na masomo. Mwaka 2019, Niger ilibatilisha amri iliyokuwa inatumika kuwazuia kwa muda wasichana waliopata mimba kuhudhuria shule. Pia iliwapiga marufuku ya kuhudhuria shule wale walioelewa. Baada ya kubatilishwa kwa amri hiyo nchi hiyo ilitunga sera mpya ambayo inalinda haki ya wasichana ya kuendelea na masomo.
Takriban mataifa 10 wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) hayana sheria au sera zinazohusiana na uhuru wa wanafunzi wajawazito au akina mama vijana kuendelea na masomo. Vile vile mataifa mengi barani Afrika, hayana au yana sera hafifu za kuzuia na kusimamia mimba za utotoni, – hali ambayo inaathiri haki za watoto kufurahia haki za afya ya uzazi, ikiwemo haki ya kupata huduma ya afya ya uzazi na elimu ya jinsia.
Mengi ya mataifa haya ni ya ukanda wa Kaskazini au upembe wa Afrika ambayo yana sheria tatanishi na sera zinazoharamisha mahusiano ya kimapenzi nje ya ndoa, hatua ambayo inaweza athiri haki za watoto wa kike kupata elimu. Mataifa mengi katika eneo hilo hayana sera zinazohusiana na usimamizi wa mimba za utotoni na jinsi ya kushughulikia wasichana waja wazito shuleni.
Katika nchi za Libya, Mauritania, na Morocco, wasichana na wanawake wenye mahusiano ya kimapenzi nje ya ndoa wanakabiliwa na tishio la adhabu kali. Kwingineko katika Ukanda wa Afrika Kaskazini, wasichana na wanawake wanaopata watoto nje ya ndoa mara nyingi huchukuliwa kama wenye aibu na fedheha kwa familia zao. Wasichana wanaojipata katika hali kama hii mara nyingi hawaruhusiwi kuendelea au huogopa kuendelea na masomo kwa sababu ya unyanyapaa au kuhofia kejeli.
Mataifa mengine ya Afrika yameidhinisha taratibu zinazotoa nafasi ya kulinda watoto ili kukabili tatizo la mimba za utotoni, hata hivyo taratibu hizo mara nyingi hazitoshi kuhakikisha watoto wa kike wanapata elimu. Katika nchi ya Congo Brazaville, serikali inadai kwamba inahakikisha wanafunzi wajawazito hurejelea masomo yao baada ya kujifungua, kwa kuwafungulia mashtaka wanaume wanaowatia mimba wasichana na wanawake walio chini ya umri wa miaka 21 miongoni mwa hatua nyingine.
Adhabu ya mashtaka kwa mahusiano ya kimapenzi kati ya watu wazima wanaoelewana au baina ya watoto wenye umri sawa inahujumu haki za kimsingi za kufanya shughuli faraghani na haki ya kutobaguliwa na mara nyingi haisaidii kulinda haki za wanafunzi husika kupata elimu. Shirika la Human Rights Watch limebaini kwamba wanafunzi wajawazito au akina mama vijana wanaendelea kubaguliwa kutokana na ukosefu wa sera dhabiti zinazolinda haki ya kupata elimu, na kushughulikia vizuizi vya kijamii, kifedha au kielimu kwa kuendeleza masomo.
Kupitia idara ya elimu, Sayansi, Teknolojia na ubunifu, Umoja wa Afrika, unafaa kushirikiana na serikali kuelekeza mifumo ya elimu kuhusisha kikamilifu wasichana katika shule za umma, limesema Shirika la Human Rights Watch. Umoja wa Afrika unafaa kushinikiza serikali kurekebisha sheria zilizopo, ili kuondoa sera tatanishi zinazohujumu haki za watoto wote kupata elimu na kuasisi taratibu zinazoambatana na majukumu yao ya haki za kibinadamu – huku zikizingatia mifano bora katika mataifa mengi wanachama.
Umoja wa Afrika unafaa kuhimiza nchi wanachama wanaheshimu, kulinda na kutimiza haki za watoto wa umri wa kubalehe kupata elimu ya afya ya uzazi. Aidha Umoja huo unafaa kuhakikisha kwamba wanafunzi wajawazito na wale ambao ni wazazi wanaruhusiwa kuendelea na masomo jinsi wanavyotaka, na vile vile wanaweza kuendeleza masomo yao bila kufuata taratibu ngumu za kijiondoa au kurejelea masomo, mbali na kupewa msaada wa kutosha wa kifedha na kijamii kumaliza masomo yao.
“Ingawa mataifa mengi ya Afrika yameidhinisha sheria na sera zinazohusiana na masomo ya wasichana, mataifa mengi bado hayana mifumo mahsusi inayoruhusu wanafunzi wajawazito na akina mama vijana kusalia shuleni au kuendelea na masomo yao bila vizuizi,” Alisema Radhakrishnan. “Umoja wa Afrika unafaa kutoa ushauri mwafaka kwa serikali na nchi wanachama kuidhinisha sera zinazozingatia haki za kibinadamu na kuhakikisha wanafunzi wanaweza kuendelea na masomo yao wakati wa ujaa uzito na hata baada ya kupata watoto.”
Tafadhali angalia hapa kwa maelezo kamilifu na habari zaidi kuhusu aina ya sheria na sera barani Afrika.
Ili kuangalia kielezo cha mwingilio kuhusu sheria na sera miongoni mwa wanachama wa Umoja wa Afrika, tafadhali angalia hapa:
https://www.hrw.org/video-photos/interactive/2022/08/29/brighter-future-empowering-pregnant-girls-and-adolescent
Ili kupata nakala ya tafiti tafadhali tembelea:
https://features.hrw.org/features/african-union/files/African_Union_Education_Policies_Mothers_Pregnant_Students_Index.pdf
------
Yanayofanyika sasa katika nchi wanachama wa Umoja wa Afrika.
Nchi nyingi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) zimepitisha Mkataba wa Afrika kuhusu Haki na Maslahi ya Watoto (Mkataba wa Haki za Mtoto wa Kiafrika), na Itifaki ya Mkataba wa Afrika kuhusu Haki za Watu na Kibinadamu kuhusu Haki za Wanawake barani Afrika (Itifaki ya Maputo, au Mkataba wa Haki za wanawake wa Kiafrika), unaowajibisha serikali kuchukua hatua mahsusi kuhakikisha usawa wa kupata elimu kwa wasichana, kuongeza umri wa kuolewa hadi miaka 18, na kuchukua hatua zote zifaazo kuhakikisha kwamba wasichana wanaopata mimba wana haki ya kuendeleza na kukamilisha masomo yao.
Shirika la Human Rights Watch limeandaa kielezo cha mwingiliano na uchanganuzi wa taratibu na sera zinazotumika miongoni mwa wanachama wa Umoja wa Afrika kulinda au kuzuia wasichana wajawazito au akina mama vijana kupata elimu. Shirika la Human Rights Watch limehakiki zaidi ya sheria na sera 100 kutoka mabunge na Afrika na wizara za Elimu, Afya, Wanawake na Maswala ya kijamii kutoka nchi wanachama wa Umoja wa Afrika ili kuelewa jinsi serikali za mataifa ya Kiafrika zinavyolinda au kuzuia uwezo wa wanafunzi waja wazito au akina mama vijana kupata elimu.
Shirika la Human Rights Watch pia liliwahoji na kuzungumza na wataalamu wa masuala ya elimu, wanaharakati, mashirika yasiyo ya serikali ili kuelewa jinsi ambavyo sera zinavyotumika na vilevile lilizungumza na wizara na balozi za mataifa mbali mbali ili kupata uhakiki kamili wa malengo ya serikali.
Mataifa mengi wanachama wa Umoja wa Afrika –AU, yameidhinisha sheria na sera zinazolinda haki za mwanafunzi msichana kusalia shuleni wakati wa uja uzito au baada ya kupata mtoto. Utafiti wetu ulibaini kuwa mataifa mengi zaidi yana mifumo dhabiti inayolinda haki ya wasichana waja wazito na akina mama vijana kupata elimu kupitia sheria au sera kuliko idadi ya nchi ambazo hazina sera au zenye taratibu za kiubaguzi. Kufikia mwaka 2022, takriban nchi 38 wanachama wa Umoja wa Afrika-AU zilikuwa na utaratibu wa kulinda haki za wanafunzi wajawazito na akina mama vijana kupata elimu kwa viwango mbali mbali.
Shirika la Human Rights Watch limeratibu taratibu zilizopo kwa makundi matano: Sera za “maendelezo” sera za “kurejea shule”, ukosefu wa sera za kulinda haki za wasichana kupata elimu, sheria au taratibu zinazoharamisha wasichana wanaopata mimba nje ya ndoa, na sheria zinazowazuia kuendelea na masomo.
Sera za “Maendelezo” zinaruhusu wanafunzi wajawazito kuamua iwapo watasalia shuleni kuendelea na masomo bila kushurutishwa kutohudhuria masomo wakati wowote wakiwa waja wazito au hata baada ya kujifungua. Sera hizo pia zinawapa wanafunzi uwezo wa kusitisha masomo kwa muda ili kujifungua pamoja na mahitaji mengine ya afya ya kimawazo, na chaguo la kurejea shuleni baada ya kujifungua kwa wakati unaofaa kwao, bila kuwekewa masharti magumu. Sera hizo zinaonyesha kwa mapana wajibu wa serikali katika kutimiza haki za kibinadamu na kutilia mkazo uhuru wa wasichana kufanya maamuzi.
Sera za “kurejea shule” zinalinda haki ya msichana kuendelea na masomo, lakini zinaambatana na vizuizi kadhaa kwa wanafunzi. Baadhi ya vizuizi hivyo ni vipindi virefu vya likizo ya baada ya kujifungua, na masharti au mahitaji magumu ya kutimizwa, kama vile wanafunzi kuhamia shule nyingine au kuwasilisha barua kutoka maafisa mbali mbali wa elimu na afya. Shirika la Human Rights Watch lilibaini kwamba mahitaji haya yana athiri vibaya kujitolea na uwezo wa mwanafunzi aliyejifungua kuendelea na masomo huku wakiwa wanakabiliwa na mabadiliko makubwa katika maisha yao.
Nchi nyingi hadi sasa hazina mifumo angafu ya sera. Wasichana wajawazito na akina mama vijana wanaweza kukabiliwa na tisho la kuadhibiwa kisheria, maamuzi mabaya ya wakuu wa shule, na vile vile pingamizi za kijamii wanapojaribu kuendeleza masomo yao.
Katika mataifa 10 barani Afrika, ukosefu wa taratibu zenye mitizamo mizuri kuwalinda wanafunzi wajawazito, unahujumu uwezo wao wa kupata elimu ambapo wasimamizi wa shule wanaweza kuamua hatma ya mwanafunzi au mitazamo ya kiubaguzi na vizuizi vya kijamii huwashinikiza wasichana kuacha shule.
Mwaka 2018, Shirika la Human Rights Watch lilibaini kwamba nchi nne — Equatorial Guinea, Sierra Leone, Tanzania na Togo— zilikuwa na taratibu za kibaguzi ambazo ziliwapiga marufuku wasichana wajawazito ama wanafunzi wazazi kuendelea na masomo. Kufikia Agosti 2022, nchi hizo zote isipokuwa Equatorial Guinea zilikuwa zimebatilisha marufuku hizo. Mwaka 2020, Sierra Leone ilibadilisha sera yake ya kibaguzi kwa kuondoa marufuku ya miaka 10 iliyokuwa imewekwa dhidi ya wanafunzi wajawazito, na mnamo mwezi Machi 2021 nchi hiyo iliidhinisha sera ya “Kuwashirikisha kwa kasi” ambayo ilithibitisha haki ya wasichan wajawazito na akina mama vijana kupata elimu.
Mwezi Novemba Mwaka 2021, wizara ya Elimu ya Tanzania iliidhinisha Agizo rasmi almaarufu Circular No. 2 of 2021la kuwarejesha shule wanafunzi waliokuwa wameondoka shule za upili kwa sababu ya ujauzito. Agizo hilo lilisema moja kwa moja kwamba wasichana ambao ni wazazi wana haki ya kurejea katika shule za umma huku ikitoa maagizo kwa shule za umma kuwakaribisha na kuwapa nafasi wanafunzi hao kusoma. Mwezi Machi 2022, waziri wa Elimu wa Togo alikomesha agizo la Mwaka 1978 ambalo lilitoa nafasi ya kuwapa marufuku wanafunzi wajawazito kuwa shuleni. Togo na Tanzania bado hazijaidhinisha sera inayopinga kuwepo taratibu na hatua zinazohakikisha kwamba wanafunzi ambao ni wajawazito na wale ambao ni wazazi wanaendelea na masomo yao.
Nchi zenye Mitizamo sera za kuwalinda wasichana: Sera za maendelezo
Sera za maendelezo na kurejea shuleni, sio mifumo geni kwa serikali za nchi za Afrika. Baadhi ya mataifa kwa miaka mingi yamekuwa na mifumo dhabiti ya kulinda haki za elimu kwa wanafunzi wajawazito na akina mama vijana. Sera hizo zinahimiza na kuunga mkono elimu na hatua za kimasomo kwa wanafunzi hao, na vilevile kuzuia kuwaadhibu au kuwaondoa shuleni kwa sababu ni wajawazito. Hata hivyo, katika mataifa yenye mfumo wa sera za kurejea shuleni, wasichana wajawazito mara nyingi hushindwa kuendelea na masomo kwa sababu ya mitazamo ya kiubaguzi miongoni mwa wakuu wa shule, unyanyapaa unaohusiana na kupata watoto nje ya ndoa, na vilevile ukosefu wa mwongozo mwafaka unaozingatia tofauti za kijinsia kutoka kwa walimu.
Usheliseli
Nchi ya Ushelisheli imekuwa na sera tangu Mwaka 2005 inayotoa taratibu mahsusi za kuzingatiwa na shule na wazazi kuwasaidia wanafunzi wanaopata mimba ili kukamilisha yao. Mwanafunzi mwenye umri wa kwenda shule akipata mimba, “anaruhusiwa kusalia shuleni mwake kwa miezi sita ya kwanza ya uja uzito.” Baada ya miezi sita, mwanafunzi “anaweza kuondoka shuleni kwenda kujifungua” na anaruhusiwa kurejea shuleni baada ya kujifungua hatua ambayo inawapa wasichana nafasi ya kuamua iwapo wanafaa kuchukua likizo ya kujifungua badala ya kulazimishiwa likizo ya lazima. Hata hivyo, mwanafunzi ni sharti arejee shuleni mwaka mmoja baada ya kujifungua.
Sera hiyo vile vile inatoa mamlaka kwa wasimamizi wa shule na familia ya mwanafunzi mja mzito kumsaidia akiwa shuleni na hata baada ya kurejea shuleni. Sera hiyo inaorodhesha majukumu ya kila mhusika kuhakikisha kwamba mama huyo kijana anafanikiwa katika masomo yake. Taratibu maalum zinaeleza hali ambapo wanafunzi wanaojipata katika hali hii wanaweza kujiunga na ngazi inayofuata ya masomo, au kurudia darasa huku zikitoa matarajio mahsusi baada ya kurejea shuleni.
Ushelisheli inatambua vizuizi mahsusi vinavyowakabili baru baru katika kupata huduma za afya ya uzazi ikiwemo masharti ya kuonyesha idhini ya mzazi. Serikali ya Ushelisheli pia imechukua hatua zaidi za kutoa mafunzo ya afya ya uzazi, kuruhusu kutolewa kwa huduma za kuavya mimba na kuzuia mimba kwa vijana wenye umri wa kubalehe, na kuhakikisha vijana wanaweza kupata huduma hizo baada ya muda wa masomo.
Serikali ya ushelisheli ililiambia Shirika la Human Rights Watch kwamba taifa hilo liko mbioni kurekebisha sera ya Mwaka 2005. Katika kurekebisha sera zilizopo kuwalinda wasichana, serikali hiyo inafaa kuidhinisha sera zinazohakikisha utekelezaji wa majukumu yake ya kimataifa na kuhakikisha kwamba wasichana akina mama vijana wanaruhusiwa kurudi shuleni baada ya kujifungua bila kuwekewa masharti magumu.
Hatua mwafaka zilizochukuliwa na nchi zilizoathiriwa na mizozo na uongozi legevu.
Kunakotokea mizozo ya vita na mapigano, wasichana na wanawake hukabiliwa na dhuluma nyingi za kijinsia na ubaguzi wa kijinsia, kimsingi ni kwa sababu ya msambao wa dhuluma za kimapenzi zinzoendeshwa na majeshi ya serikali na makundi mengine yaliyojihami na vilevile umaskini mkubwa ambao huchangia dhuluma za kijinsia. Wahanga wa dhuluma za kimapenzi mara nyingi huogopa kurejea shuleni kwa sababu ya kejeli na unyanyapaa, na mara nyingi kwa sababuu ya ukosefu wa mipango ya dharura ya masomo inayoambatana na mahitaji yao. Wale ambao hurudi shuleni mara nyingi hukosa usaidizi wa kuwawezesha kuendelea na masomo yao. Mikutadha ya hali hiyo inatilia mkazo haja ya kuweko sera mwafaka za kuwalinda wanafunzi waja wazito na akina mama vijana, na ambazo huzingatia mahitaji ya waschana walioathirika kwa mizozo au kulazimika kutoka nyumbani.
Baadhi ya mataifa ya Kiafrika yaliyoathirika na mizozo ya kivita, ambayo mara nyingi huwa na viwango vya juu vya visa vya mimba za utotoni, hivi karibuni zimechukua hatua muhimu kulinda haki ya wasichana kuendelea na masomo na kutoa usaidizi kwa wanafunzi wajawazito au wale wanaolea watoto.
Burkina Faso
Tangu mwaka 1974, nchi ya Burkina Faso, imekuwa na sheria inayolinda wanafunzi wajawazito na wale wanaolea watoto dhidi ya kufukuzwa shuleni na inashurutisha shule kuwaruhusu wanafunzi hao kurejelea masomo yao baada ya kujifungua. Mnamo mwaka 2021, Wizara ya Elimu ya Burkina Faso ilichapisha mwongozo unaosimamia jinsi ya kuzuia “mahusiano ya kimapenzi ya mapema”, mimba za mapema na ndoa za mapema, katika shule.
Mwongozo huo unahimiza jinsi ambavyo wasichana wajawazito watalindwa, na vilevile unatoa maelezo jinsi ya kushughulikia visa vya mimba za mapema, viwango vya ukusanyaji wa takwimu na hatua za kufuata katika kutoa huduma za afya na ushauri nasaha mara tu wasimamizi wa shule wanagundua visa vya wanafunzi kupata mimba. Hata hivyo, mfumo uliopo sasa nchini Burkina Faso hauelezei taratibu za kuwarejesha wasichana shule, wala kutoa maelezo juu ya aina ya msaada wa kifedha,kielimu na kijamii ambao wanafunzi wajawazito au akina mama vijana wanapaswa kupewa katika mazingira ya kawaida ya masomo.
Niger
Nchi ya Niger kwa muda mrefu imekuwa na viwango vya juu vya ndoa za mapema na idadi kubwa ya watoto wanaozaliwa huku ikikumbwa na mzozo kuanzia mwaka 2012. Mnamo mwaka 2012, miongoni mwa wakati wa mwisho ambao takwimu zilichukuliwa, asili mia 48 ya wasichana nchini Niger walikuwa wamezaa watoto kufikia umri wa miaka 18. Kati ya Mwaka 2015 na 2020, asilimia 76 ya wasichana nchini huo waliolewa kufikia umri wa miaka 18. Takwimu hizi ni kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu idadi watu -UNPFA.
Mnamo mwezi Februari Mwaka 2019, serikali ya Niger ilibatilisha amri ya mwaka 1978 ambayo iliwalazimu wasichana wanaopata mimba kuacha masomo kwa muda na kuwapiga marufuku kabisa wanapoolewa. Mnamo mwezi Agosti Mwaka 2019, Niger ilianzisha sera mpya inayolinda haki za msichana mja mzito kupata elimu. Kifungu cha 8 cha agizo nambari 334 la Agosti 22, Mwaka 2019, kinatoa hakikisho kwamba mwanafunzi anaweza endelea na masomo iwapo atapata mimba au kuolewa. Aidha agizo hilo linasema kwamba hatua za kinidhamu zitachukuliwa dhidi ya mwalimu yeyote atakayekataa kumruhusu mwanafunzi aliyepata mimba kuendelea na masomo baada ya kujifungua.
Hata hivyo, mwanafunzi husika analazimika kurudi shuleni katika muda wa siku arobaini baada ya kujifungua isipokuwa wakati wa mazingira ya kipekee. Agizo hilo pia linatoa mamlaka kwa wizara ya Elimu kuidhinisha mwongozo unaofafanua vikwazo vinavyowekwa wasimamizi wa shule wanaokataa kuwaruhusu wanafunzi waliozaa kurejelea masomo. Serikali inafaa kuondoa vikwazo vya muda vya kuendelea na masomo na badala yake kutoa mwongozo mahsusi kwa shule kuelezea wajibu wao kuwasajilisha na kusaidia wanafunzi wajawazito na akina mama vijana ambao wanalea watoto.
Guinea-Bissau
Mnamo mwezi Machi Mwaka 2022, Serikali ya Guinea-Bissau iliwasilisha mswada wa sheria ya kuwalinda watoto uliojumuisha kanuni mahsusi za kulinda haki za wanafunzi waja wazito na akina mama vijana kupata masomo na kusaidiwa kuendeleza masomo yao. Vifungu nambari 67 na 68 vya mswada huo vinahakikisha kwamba mwanafunzi mjamzito au mama kijana hawezi kuzuiliwa kuendelea na masomo au kushurutishwa kusitisha masomo yake. Mswada huo pia unasema kwamba wanafunzi wajawazito, au wanafunzi wazazi, wanapaswa kusaidiwa kuhudhuria masomo kila siku. Shule zinafaa kuhakikisha kwamba mwanafunzi yeyote ambaye ni mzazi, licha ya ngazi yake ya masomo, anapewa fursa ya kumnyonyesha mtoto wake hadi wakati mtoto huyo aatfikisha umri wa miezi sita, kuambatana na mapendekezo ya shiirika la Afya Duniani- WHO.
Mnamo mwezi Mei Mwaka 2022, rais wa Guinea-Bissau alivunja bunge, hatua ambayo ilihujumu juhudi za kuidhinisha mswada huo wa sheria. Kutokana na ukosefu wa sheria za kuwalinda wasichana, wizara ya elimu ya Guinea-Bissau inafaa kutekeleza mwongozo wa sera ili kuweka kanuni za kuwalinda wasichaana katika sekta nzima ya elimu nchini humo.
Jamhuri ya Afrika ya Kati
Jamhuri ya Afrika kati hivi majuzi imechukua hatua za kuandaa kanuni zenye kulinda nguzo dhabiti kulinda haki ya watoto wasichana kupata elimu. Kifungu nambari 72 cha kanuni za kulinda watoto za Mwaka 2020 kinatoa hakikisho kwamba mwanafunzi anayepata mimba atakuwa na haki ya kurejelea masomo yake katika shule ya msingi au ya upili.
Nchini zenye sheria za maadili na zinazoharamisha mahusiano ya kimapenzi yanayoathiri elimu.
Shirika la Human Rights Watch limebaini kwamba nchi za ukanda wa kaskazini mwa bara la Afrika kwa jumla hazina sera za kusimamia suala la mimba za mapema katika shule. Kutokana na ukosefu wa mifumo, wasichana waja wazito na wale wanaolewa huenda wakakabiliwa na vizuizi vya kisheria na kijamii vinavyozuia nia yao ya kuendelea na masomo.
Wataalamu wa elimu na haki za watoto walisema kwamba kutokana na itikadi kali juu ya mimba nje ya ndoa, mataifa mengi ya Afrika kaskazini hayanakili takwimu juu ya visa vya wasichana kupata mimba, na mara nyingi takwimu zikinakiliwa kuhusu mimba za mapema, na viwango vya mimba za mapema katika shule haziwezi kutegemewa kuunda sera. Mitizamo kama hiyo na ukosefu wa takwimu huchangia ukosefu wa usawa na usiri na kupelekea ukosefu wa hatua za kushughulikia mahitaji ya wasichana wanaopata mimba na wale wanaojipata wakitekeleza majukumu ya kuwa mama.
Afrika Kaskazini
Katika ukanda mzima wa Afrika Kaskazini, mataifa mengi hutoa adhabu za “kimaadili”-dhidi ya wasichana na wanawake iwapo wamekiuka kanuni zilizopo- kupata mimba mapema hucukuliwa kuwa kosa la zina, neno la kisheria linalotokana na sheria za Kiislamu zinazopiga marufuku mahusiano ya kimapenzi nje ya ndoa. Nchi za Algeria, Misri, Libya, Mauritania, na Morocco zimeratibisha makosa ya uzinzi, ukosefu wa adabu, na mapenzi kabla ndoa kuwa njia zinazotishia maisha ya wasichana wanaobalehe. Katika nchi hizo kosa la zina limefungamanishwa na miiko mingine ya kijamii na vilevile mitizamo kwamba msichana anayepata mimba au kuzaa kabla ya kuolewa huileta fedheha kwa familia yake na jamii nzima.
Kifungu cha 307 cha sheria za adhabu nchini Mauritania kinaharamisha mahusiano ya kimapenzi kati ya mwanamume na mwanamke nje ya ndoa. Yeyote anayekiuka sheria hiyo huadhibiwa kwa kucharazwa viboko 100 na kifungo cha mwaka moja gerezani iwapo hajaolewa au kuoa. Adhabu ya kucharazwa viboko huahirishwa hadi wakati mwanamke husika amejifungua mtoto. Ingawa sheria hiyo inawalenga “watu wazima waaumini wa dini ya kiislamu,” utafiti uliofanywa na Shirika la Human Rights Watch Mwaka 2018 ulibainisha kwamba baadhi ya viongozi wa mashtaka huwashtaki wasichana kutumia sheria hiyo bila kujali kama ni wajawazito.
Cha kuzingatia hasa ni kwamba, msichana yeyote anayeonyesha dalili zozote za ujauzito anaweza kufanyiwa uchunguzi kwa tuhuma za kukiuka sheria ya zina. Kwa wasichana wengi na wanawake kwa ujumla, tishio la kufunguliwa mashtaka na unyanyapaa unaombatna na tuhuma kufanya kosa la zina ni adhabu tosha kivyake. Miiko ya kijamii inayotiliwa mkazo na adhabu za makossa mara nyingi hulazimisha jamii nyingi kuwafukuza nyumbani wasichana au kuwalazimisha kuolewa.
Kutokana na hali hiyo, huwa ni vigumu kwa wanafunzi waliozaa kuendelea na masomo. Mara nyingi hata mataifa yenye sera zinazohimiza elimu ya wasichana, ikiwemo sheria zinazofanya masomo kuwa lazima, serikali hukinzana na sera hizo kwa kuharahimisha mahusiano ya kimapenzi nje ya ndoa. Kutokana na hali hiyo, makosa ya zina yanaendeleza ubaguzi kwa misingi ya jinsia, kwa sababu mimba inaweza chukuliwa kama “ushahidi” wa kutosha kwa kosa hilo na vilevile inahujumu zaidi haki za msichana kupata elimu.
Nchini Mauritania, yeyote anayemzuia msichana mwenye umri chini ya miaka 18 kuendelea na masomo yake kwa sababu ya kupata mimba huchukuliwa hatua na kutozwa faini. Licha ya hayo kuharamishwa kwa mahusiano ya kimapenzi nje ni kizuizi kikubwa kwa juhudi za wasischana waja wazito na akina mama vijana kupata elimu wakati wa uja uzito au baada ya kujifungua.
Mataifa ya kanda ya kaskazini mwa Afrika nchi hazitoi adhabu haswa kwa kosa la zina. Nchini Algeria, sheria ya adhabu kimsingi haiharamishi mapenzi nje ya ndoa, lakini tishio la kushtakiwa chini ya sheria hizo zinazolenga kosa la uzinzi ni changamoto kubwa kwa vijana wenye umri wa kubalehe. Sawa na Algeria,Misri haiharamishi mahusiano ya kimapenzi nje ya ndoa, lakini inaharamisha kosa la uzinzi, “ukosefu wa adabu hadharani,” na “kuchochea ufisadi,” hali ambayo inaweza wazuia wasichana kwenda shuleni iwapo wamepata mimba kabla ya ndoa.
Tunisia
Ingawa Tunisia haiharamishi mahusiano ya kimapenzi nje ya ndoa, inaharamisha mapenzi kati ya watu waliooa au kuolewa,kukosa adabu hadharani na vile vile ukahaba. Ingawa baadhi ya wanawake wanaofanya mapenzi nje ya ndoa wamewahi kukamatwa, mwanasheria mmoja aliyehojiwa na shirika la Human Rights Watch alisema kwamba mashtaka hayo huenda hayakutumika kuwaadhibu wasichana wanaopata mimba nje ya ndoa kwa nia ya kuwazuia kupata elimu.
Hata kama hawakushtakiwa kwa makossa hayo, wasichana wanaopata mimba na akina mama vijana bado hawana ulinzi wa kutosha kuwawezesha kuendelea na masomo. Mwanafunzi anapopata mimba, maafisa wa elimu na maafisa wa kulinda haki za watoto mara nyingi huchukulia kwamba msichana husika alibakwa, mtaalamu mmoja wa maswala ya watoto aliliambia Shirika la Human Rights Watch. Ingawa hakuna sheria au sera inayowazuia wasichana wanaopata mimba au akina mama vijana kuhudhuria masomo, wasichana wengi huacha shule kwa sababu ya mitizamo ya kijamii inayochukulia mimba za utotoni kuwa aibu na fedheha na wanaruhusiwa tu kurejelea masomo iwapo wana usaidizi wa familia na cheti cha afya ama barua kutoka kwa afisa wa kijamii kueleza sababu za wao kutokuwa shuleni.
Viwango vya mimba za mapema nchini Tunisia ni cha chini ikilinganishwa na mataifa mengine ya Afrika Kaskazini. Kiwango cha wasichana waliopata mimba kilikuwa wasichana 7 kati ya kila 1,000 wenya umri wa kati ya miaka 15 na 19 kati ya mwaka 2004 na 2020, kwa mujibu wa takwimu za Hazina ya Umoja wa Mataifa kuhusu idadi ya watu-UNFPA. Viwango hivyo vya chini huenda ni kwa sababu ya kuwepo kwa huduma za kuwasaidia vijana kuzuia au kutoa mimba. Utoaji mimba ni halali na huduma hiyo hutolewa bure katika muda wa miezi mitatu ya kwanza ya mimba lakini ni sharti uwe na idhini ya mzazi ama mlezi kwa wasichana wenye umri wa chini ya miaka 18,kadhalika vijana wanaweza kabiliwa na changamoto kama vile ukosefu wa dawa,wahudumu wa afya kukataa kukuhudumia na ukosefu wa muda.
Hata hivyo, kiwango sahihi cha mimba miongoni mwa vijana, haswa nje ya ndoa, huenda ni juu kuliko takwimu zinavyoonyesha, alisema Samia Ben Messaoud, anayeongoza Shirika la Amal pour la Famille et l'Enfant (Amal kwa ajili ya familia na mtoto), ambalo hushughulikia haki za akina mama wasio na waume na watoto wao. Idadi ya wasichana wanaotafuta huduma za shirika hilo imekuwa ikiongezeka katika miaka ya hivi karibuni.
Nchi zenye mapungufu ya sera yanayochangia kutengwa
Shirika la Human Rights Watch lililibainisha kwamba nchi 15 za Afrika, ikiwemo Somalia na Ethiopia, hazitoi mamlaka kuwazuia wasichana waja wazito na akina mama vijana kusitisha masomo lakini hakuna sera za kuwawezesha kuendelea na masomo. Ukosefu wa sera za kuwalinda wasichana mara nyingi huchangia utekelezaji wa mfumo wa masomo ya lazima hatua ambayo inawapa wasimamizi wa shule na jukumu la kuamua iwapo wasichana waja wazito wanaweza kuendelea na masomo na kutoa mwanya kwa mitazamo ya kibaguzi a vizuizi vya kijamii vinavyowalizimisha wasichana wanaopata mimba kuacha shule.
Bila njia za kuwatetea na kuwalinda wasichana huku serikali ikiwa haijawekeza katika mifumo ya kuwasaidia kimasomo na kijamii, wasichana wajawazito na wale ambao ni wazazi hujipata hawana nafasi shuleni kwa hivyo wamefukuzwa daima. Wengi wao pia hukabiliwa na ukosefu wa usaidizi wowote kutoka shule zao, nyumbani pia au katika ngazi za jamii zao hamna usaidizi wa namna yoyote kuwawezesha waendelee na masomo.
Somalia
Nchini Somalia, kupata elimu ni changamoto kubwa kwa watoto wengi kwa sababu ya umaskini, kusafiri miendo mirefu kwenda shuleni na makabiliano ya vita vya silaha. Kuna tofauti kubwa kati ya idadi ya wavulana na wasichana waliosajiliwa katika shule za msingi na upili. Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na serikali ya Somalia hivi majuzi, idadi ya wasichana waliosajiliwa katika shule za upili katika maeneo ambayo yanayodhibitiwa na serikali ilikuwa ni asili mia 39 pekee kati ya mwaka 2015 na mwaka 2016.Hapakuwa na takwimu zo zote kwa wale wanaoishi katika maeneo yanayodhibitiwa na kundi la wapiganaji wa Al shabaab.
Wasichana na wanawake nchini Somalia wanabeba mzigo mkubwa wa ubaguzi kutokana na hali ngumu ya maisha inayosababishwa na umaskini, mizozo ya kivita, na vizuizi vya kitamaduni kuhusu majukumu ya wasichana na wanawake katika jamii. Wazazi wengi huhofia kuwapeleka mabinti zao katika shule zilizoko mbali na nyumbani kwa sababu ya hofu ya kudhulumiwa, ukosefu wa vyumba vya usafi, na karo za juu za shuleni. Wasichana hukabiliwa na vizuizi zaidi kwa sababu ya tamaduni za kijamii zinazowapendelea wavulana kupata elimu, upungufu wa walimu wa kike, na ukosefu wa habari muhimu kuhusu elimu ya uzazi na huduma shuleni.
Ingawa hakuna sheria au sera inayowabagua wasichana wajawazito na wale wanaolea, mkusanyiko wa gharama za kijamii na mzigo mingine huchangia idadi kubwa ya msichana kuacha masomo. Punde tu baada ya kuzaa, wasichana mara nyingi hutwikwa majukumu makubwa nyumbani. Wasichana, ambao huchukuliwa kana kwamba ni watu wazima baada ya kupata watoto na ambao wanatarajiwa kutekeleza majukumu yote ya nyumbani,wanahitaji kusaidiwa na jamii kutunza watoto wao,mtaalamu mmoja wa masuala ya usawa wa jinsia aliyetaka jina lake kubanwa aliliambia shirika la Human Rights Watch na tunamnukuu:
Kwa vyo vyote hakuna namna ambavyo [wasichana ambao sasa ni wazazi] wanaweza kurejea shuleni na kuhudhuria masomo kama wanafunzi wengine wa kawaida. Hakuna nafasi ya kufanya mambo mengine, wala usaidizi kuwezesha msichana huyo kunyonyesha akiwa shuleni, na kuna unyanyapaa unaombatana na mwanafunzi kuonekana shuleni na mtoto.… Mara nyingi, wasichana kama hao wakijaribu kwenda shule huweza tu kumudu masomo kwa muda wa saa sita pekee. Huwa wana majukumu mengi ya kinyumbani,na wanatakiwa kupika na kusafisha nyumba kabla ya kuelekea shuleni na wakati huo huo wanatarajiwa kuendelea kufanya vizuri katika masomo pia.
Msichana akipata mimba nje ya ndoa, anaweza kukabiliwa na shinikizo zaidi kuaacha shule ili aolewe. “Ni afadhali [msichana kama huyo] asalie nyumbani na aolewe kwa haraka ili kuhifadhi heshima zake katika jamii, na familia yake ili kujiepusha na mizigo,” mtalaamu wa masuala ya jinsia alisema kuhusu hali hiyo ya maisha nchini Somalia.
Ethiopia
Nchini Ethiopia, hakuna sheria au sera za kulinda haki ya wasichana au kuwaadhibu wanaohujumu masomo ya wanafunzi wanaopata mimba. Wasichana wajawazito na wale wanaoolewa kimsingi wanaweza kuendelea na masomo yao. Hata hivyo ni nadra kwa mwanafunzi mja mzito au aliyeolewa kurejea shuleni kuendeleza masomo yake kwa sababu ya Imani za kijamii, majukumu ya kulea mtoto, na changamoto za kiuchumi. Wasichana wajawazito ambao hawajaolewa hukabiliwa na unyanyapaa mkubwa kutoka kwa wenzao shuleni na jamii. Wataalamu wa masuala ya elimu walisema kwamba wakati mwingine, wanafunzi ambao wameolewa huendelea kwenda shule, lakini ili kurejea kwa shuleni hutegemea nia ya mume wake na iwapo wanaweza kumudu gharama za kuendelea na masomo
Badala yake, baadhi ya wanafunzi nchini Ethiopia wanakubaliwa kupata elimu kupitia njia mbadala za masomo bila kwenda shuleni, kama vile mipango ya masomo ya watu wazima ambayo hutoa maarifa ya kimsingi na mafunzo ya kikazi ambayo hutolewa kwa watoto “walioacha shule”. Hata hivyo, mipango hiyo haitoshelezi mahitaji ya serikali kutimiza majukumu ya haki za kibinadamu kutoa masomo ya upili kwa watoto wote. Wanafunzi wote wana haki ya kusoma katika shule rasmi za upili au kuamua njia mbadala yenye viwango sawa inayowapa nafasi ya mabadiliko ya hali na kupewa cheti cha shule ya upili wanapomaliza masomo.
Misri
Nchini Misri, wanafunzi walioolewa ambao ni wajawazito au ni wazazi tayari ,yamkini wanaruhusiwa kuendelea na masomo kupitia njia ya mafunzo ya nyumbani. Sera ya kitaifa nchini Misri kuhusu masomo ya nyumbani, hata hivyo, haizungumzii wanafunzi ambao tayari ni wazazi. Masomo ya nyumbani inafaa kuwa wazi kwa mwanafunzi ye yote anayetaka kusoma kupitia mfumo huo. Mfumo wa masomo ya nyumbani hautilii maanani mahitaji ya wanafunzi wajawazito au wale ambao ni wazazi. Ilihali wanafunzi ambao wameolewa kupitia usaidizi wa wazazi wao wanaweza kuagiza vitabu kwa matumizi ya nyumbani na kufanya mitihani ya mwaka.
Lakini Shirika la Human Rights Watch limebainisha kwamba wanafunzi wanaopata mimba nje ya ndoa hawapati usaidizi sawa na himizo la kuendelea na masomo hata wakiwa nyumbani. Wakati huo huo, wasichana hao wanakabiliwa na hatari kubwa ikiwemo kupigwa na kudhulumiwa na wakati mwingine hata kuuwawa na jamaa zao wa kiume kwa sababu ya kupata mimba wakiwa shuleni.
Congo Brazaville
Kwenye ripoti yake ya mwaka 2017 kwa Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Kuokomesha ubaguzi dhidi ya wanawake, serikali ya Congo Brazaville ilisema kwamba inaruhusu wanafunzi wanaopata mimba wakiwa shuleni kurejelea masomo yao baada ya kujifungua huku ikinukulu sheria zinazowaadhibu wanaume wanaowatia mimba wasichana na wanawake wenya umri wa chini ya miaka 21.Hata hivyo sheria zilizoko kama vile sheria ya kulinda watoto ya mwaka 2010 ambayo inatoa adhabu hiyo, hazijakomesha dhuluma za kimapenzi au mimba za mapema, ama kulinda haki ya wanafunzi waja wazito na akina mama vijana kuendelea na masomo. Congo Brazaville inaendelea kukabiliwa na viwango vya juu vya mimba za mapema, kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu idadi ya watu-UNFPA: wasichana 111 kati ya 1,000 wenye umri wa kati ya miaka 15-19 hupata mimba.
Serikali ya Congo Brazaville inafaa kuzingatia hatua kama vile mkakati wa mwaka 2016 wa kuimarisha masomo ya wasichana ambao unaelezea mbinu za kuzuia na kushughulikia suala la mimba za mapema ikiwemo kupitia upatikanaji wa huduma za bure za afya na kutolewa kwa habari, elimu na kampeni za mawasiliano kushughulikia dhuluma za kimapenzi, unyanyasaji wa kimapenzi na mimba za mapema.
Mapendekezo
Kwa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika
- Kuhakikisha kwamba wanafunzi ambao ni wajawazito, wale wanaolea watoto, au walioolewa wanawezeshwa kuendelea na masomo yao bila vikwazo au taratibu za kuwazuia –na kuhakikisha kwamba unyanyapaa na ubaguzi shuleni umekomeshwa.
- Mataifa ambayo hayana sera au sheria kuhusu wanafunzi waja wazito na akina mama vijana, yanaidhinisha sera zinazotimiza majukumu ya serikali ya haki za kibinadamu na kutilia mkazo uhuru wa wasichana kufanya maamuzi kuhusu maisha yao.
- Idhinisha Itifaki ya Maputo na kutekeleza vifungu nambari 9, 10, 17, na 19 ambavyo vinatilia mkazo uhuru wa wasichana kufanya maamuzi kuhusu maisha yao.
- Rekebisha sera zilizopo kuhusu wanafunzi waliozaa ili ziambatane na viwango vya kimataifa vya haki za kibinadamu zinazolinda haki ya wasichana wajawazito na akina mama vijana kuendelea na masomo ya msingi na upili, na vilevile kufuatilia shule kuhakikisha kwamba zinangatia sera hizo.
- Ili kutimiza mkakati wa, Umoja wa Afrika kuhusu Usawa wa jinsia na kuwawezesha wanawake, hakikisha kuwa wanafunzi wanaolea watoto wanapata ufadhili wa kifedha na kijamii kukamilisha masomo yao, ikiwemo kupata huduma kwa watoto wao, na ruzuku za kifedha kujimudu kijamii.
- Zingatia kuzuia mimba za mapema kwa kuhakikisha kwamba:
- Wanafunzi wote wanapata mafunzo kuhusu elimu ya afya ya uzazi, kufungamana na viwango vya kimataifa; na vilevile
- Watoto wote na vijana wanaweza kupata habari mahsusi za faragha kuhusu vijana na mapenzi na afya ya uzazi na huduma ya afya ikiwemo utoaji mimba kwa njia iliyo salama na ya kisheria, mbinu za kisasa za kuzuia mimba, na habari kuhusu haki za kuhusika mahusiano ya kimapenzi, haki za kupata afya ya uzazi bila kushurutisha kuhusika kwa wazazi.
- Ondoa vifungu vya sheria ya adhabu vinavyoharamisha mahusiano ya kimapenzi yanayotokana na maelewano na makosa mengine ya kimaadili.
- Weka rasmi umri wa kuolewa ama kuoa kuwa miaka 18 – kwa wanaume na wanawake bila kubagua.
Kwa Umoja wa Afrika.
- Asisi “sera mfano endelevu” ya haki za kibinadamu na miongozo inayoeleza mifumo ya kuhakikisha kwamba wanafunzi wajawazito na akina mama vijna wanapata elimu.
- Toa wito kwa mataifa wanachama kukomesha ubaguzi wa wanafunzi waja wazito shuleni na dhuluma nyingine zinazoandamana na hali hilo.
- Himiza serikali:
- Kutunga sera zinazowaruhusu wanafunzi waja wazito kuendelea na masomo jinsi wanavyotaka licha ya uja uzito bila kuwashurutishia likizo ya lazima baada ya kujifungua;na
- Zingatia utekelezaji na ufuatiliaji wa sera zilizopo katika shule.
Kwa Kamati ya Umoja wa Afrika kuhusu Haki za Watu na Kibinadamu na Kamati ya Wataalam kuhusu haki na maslahi ya mtoto
- Fanya utafiti kuhusu hali ya elimu kwa wanafunzi waja wazito, walioolewa na wale ambao ni wazazi.
- Kuzingatia hoja ya pamoja ya Mwaka 2018 kuhusu kukomesha ndoa za utotoni, toa mwongozo unaolenga majukumu ya kisheria ili kutoa elimu kwa usawa kwa wasichana na wanawake, ikiwemo wale ambao ni wajawazito au ni wazazi tayari, bila ubaguzi.
- Toa wito kwa serikali kubatilisha sheria na sera zinazowabagua wasichana waja wazito na akina mama vijana, zikiwemo sheria zinazoharamisha mapenzi nje ya ndoa.
- Fuatilia jinsi ambavyo serikali zinatekeleza sera zinazosaidia wasichana waja wazito na akina mama vijana wa kuendelea na masomo yao wakati wa uchunguzi kuambatana na mipango husika ya haki za kibinadamu.