- Mpango wa kampuni kubwa ya mafuta ya Kifaransa ya TotalEnergies kutekeleza mradi wa bomba la mafuta Afrika Mashariki umeharibu vyanzo vya kujipatia kipato kwa maelfu nchini Uganda na utachangia katika uchafuzi wa hali ya hewa duniani.
- Mradi huo utawaondoa makwao watu zaidi ya 100,000, tayaru umesababisha uhaba wa chakula huku wengi wakikumbwa na madeni, kufaya watoto kuacha shule na unaweza kusababisha uharibifu wa mazingira.
- Watu wanaoathiriwa kwa ujenzi wa mradi huo lazima wafidiwe kufungamana na Viwango vya Utekelezaji vya IFC. Kampuni nyingine zinafaa kupinga mradi huo na itafaa kama ujenzi wake ungekoma.
(Nairobi) – Mradi wa bomba la mafuta unaotekelezwa na kampuni kubwa ya mafuta ya Kifaransa ya TotalEnergies Afrika Mashariki umeharibu vyanzo vya kujipatia kipato kwa maelfu ya watu nchini Uganda. Mradi huo utachangia katika uchafuzi wa mazingira na hali ya hewa, limesema shirika la Human Rights Watch katika ripoti yake iliyotolewa leo. Utakapokamilika, Mradi wa bomba la mafuta la Afrika Mashariki (EACOP) utakuwa na visima kadhaa, mamia ya kilomita za barabara, kambi na miundombinu mingine pamoja na kilomita 1,443 za mabomba yanayounganisha visima vya mafuta magharibi mwa Uganda na bandari ya Tanga mashariki mwa Tanzania.
Ripoti yenye kurasa 47, “Uaminifu wetu umevunjwa”: Upotevu wa ardhi na vyanzo vya kujipatia kipato kwa ajili ya Maendeleo ya mradi wa Mafuta Uganda,” imekusanya taarifa za mchakato wa upatikanaji ardhi kwa ajili ya moja ya mradi mkubwa wa miundombinu ya mafuta kote duniani. Uendelezaji wa vitalu vya mafuta ambao utasababisha watu zaidi ya 100,000 kuhama nao upo katika hatua ya utekelezaji.Ijapokuwa asilimia 90 ya watu watakaopoteza ardhi zao kwa ajili ya mradi wamepokea fidia kutoka kampuni ya TotalEnergies EP Uganda, mradi umeathiriwa kwa kuchelewa kwa miaka mingi kulipwa fidia ikiwemo fidia isiyotosheleza hasara wanayopata waathiriwa.
“EACOP imekuwa ni maafa kwa makumi ya maelfu waliopoteza ardhi ambayo ilikuwa ikiwapatia chakula kwa ajili ya familia zao na kipato kwa ajili ya kuwapeleka watoto wao shule na sasa wamepokea fidia ndogo sana kutoka TotalEnergies,” anasema Felix Horne, mtafiti mwandamizi wa Human Rights Watch. “EACOP vile vile ni janga kwa dunia kwa hivyo inapaswa mradi huu ukomeshwe.”
Ripoti hii inatokana na mahojiano zaidi ya 90 yaliyofanywa na Human Rights Watch mapema mwaka 2023 ikijumuisha familia 75 zilizohama katika wilaya 5 nchini Uganda.
Human Rights Watch iligundua kuwa madhara ya ucheleweshaji wa miaka mingi yamechangiwa na mawasiliano yasiyoeleweka ikiwa wakulima wanaweza kuendelea kutumia ardhi kuvuna kahawa, ndizi na mazao mengine ya biashara katika kipindi cha mpito. Vilevile, utaratibu wa kuchukua ardhi umesababisha uhaba mkubwa wa fedha kwa maelfu ya wakulima wa Uganda na kusababisha madeni makubwa ya kinyumbani, ukosefu wa chakula cha kutosha na kukosa uwezo wa kulipa karo za shule hali inayofanya watoto wengi kuacha shule.
Wakulima walisema walihisi kushinikizwa kusaini mikataba ya fidia kwa lugha ya Kiingereza, ambayo wengi wao hawawezi kuisoma huku wengi wakisema walipewa fedha taslimu badala ya kupewa ardhi mbadala ili kuendana na viwango vya kimataifa. Ahadi zisizotimizwa kuhusu kuhamishwa kwa makaburi na kuboreshwa kwa ubora wa maisha ambazo ziliwekwa wakati wa mikutano mbalimbali ya awali kuonyesha kuwa mradi una manufaa na thamani ya EACOP umechochea kupotea kwa uaminifu baina ya jamii na kampuni ya TotalEnergies.
“Walikuja hapa huku wakituahidi kila kitu,” mkazi mmoja alisema. “Tuliwaamini. Sasa hatuna ardhi, fedha za fidia zimekwisha, maeneo machache yaliyobaki yamejaa na vumbi limezagaa hewani.”
Kampuni ya TotalEnergies ndio kampuni inayoongoza katika uwekezaji huu kupitia kampuni tanzu ya Uganda ya TotalEnergies EP Uganda pamoja na Kampuni ya China National Offshore Oil Company na kampuni za taifa za mafuta za Uganda na Tanzania. Kampuni ya Atacama Consulting na Newplan Group zinasimamia mchakato wa upatikanaji wa ardhi kwa niaba ya TotalEnergis EP Uganda.
Kampuni ya TotalEnergies iliahidi kuheshimu na kuzingatia viwango mbalimbali vya kimataifa ikiwa ni pamoja na viwango vya utendaji vya shirika la International Finance Corporation (IFC) ambavyo vinaitaka TotalEnergies na kampuni zake tanzu kurejesha maisha ya watu katika hali nzuri au kuboresha hali ya maisha yawe kama ilivyokuwa kabla ya usumbufu kutokea. Mradi wa bomba la mafuta haujapata asilimia 60 ya bajeti inayohitajika. Wakati mradi ukiendelea kutafuta fedha zaidi za uwekezaji, TotalEnergies na kampuni zake tanzu hazina budi kuongeza kiasi cha malipo ya fidia na mpango wa kurejesha maisha katika hali ya awali kuendana na viwango vya haki za binadamu.
Katika barua yao ya Juni 15 kwa Human Rights Watch, TotalEnergies ilieleza kuwa “wataendelea kufuatilia kwa karibu mazingatio ya haki za jamii zinazohusika” na kutoa majibu ya kina kuelezea maoni yao kuwa fidia iliyotolewa iliendana na viwango vya IFC. Kampuni ya Atacama Consulting ambayo ni ya ushauri ya masuala ya mazingira inayosimamia shughuli ya upatikanaji ardhi kwa niaba ya TotalEnergies EP Uganda katika vitalu vya mafuta vya Tilenga ilitoa majibu yake Juni 22. Ilikana tuhuma kuwa kulikuwa na hali ya kuwashinikiza watu kusaini mikataba ya fidia na kuelezea kuwa fidia iliyotolewa imekidhi mahitaji ya “gharama kamili za kuhama.”
Utafiti unaonesha kuwa ujenzi na uendeshaji wa mradi wa EACOP unaweza kuwa na madhara makubwa kwa mazingira. Bomba linapita katika maeneo nyeti ya ikolojia ikihusisha maeneo yaliyotengwa na maeneo oevu ya kimataifa, hali inayo hatarisha bioanuwai na ikolojia ambayo jamii za asili zinategemea kwa ajili ya kukidhi mahitaji yao.
EACOP inatekelezwa katika wakati ambao Jopo la Serikali Mbalimbali kuhusu mabadiliko ya Tabia nchi (IPCC), mamlaka ya juu ya dunia ya sayansi ya hali ya hewa; Shirika la Kimataifa la Nishati; na wengine wana tahadharisha kuwa hakuna mradi mpya wa mafuta unapaswa kufanyika ikiwa dunia inataka kufikia malengo ya Makubaliano ya Paris na kuzuia madhara makubwa ya tabia nchi. Mwezi Machi, IPCC ilithibitisha kuwa hali ya joto duniani inaongezeka kwa kiwango cha juu na kuhimiza serikali kupunguza uzalishaji wa sumu -hewa kwa kuondoa mafuta na kuhimiza nishati jadidifu.
Kutokana na upinzani mkubwa wa mradi wa EACOP kutoka kwa asasi za kiraia, mashirika ya kijamii na wanaharakati wa mazingira nchini Uganda na duniani kote, taasisi nyingi za fedha na kampuni za bima zimeweka dhamira ya kutotoa ushirikiano kwa mradi huu. Taasisi za fedha hazina budi kukataa kushirikiana na EACOP kutokana na madhara makubwa ya mafuta katika mabadiliko ya tabia nchi pamoja na hatari ya madhara makubwa zaidi kwa haki za binadamu, Human Rights Watch ilisema.
“Uchomaji wa mafuta unachochea janga la mabadiliko ya tabia nchi.” Horne alisema. “Taasisi za fedha zinazofikiria kutoa fedha kwa ajili ya mradi wa EACOP zinapaswa kuacha mara moja na badala yake kuisaidia Uganda kufaidika na uwezo wake mkubwa wa nishati safi.”