(Nairobi) – Serikali ya Tanzania haijachukua hatua za kisheria na kisera za kutosha zinazohitajika katika kulinda haki ya wasichana wajawazito na wamama vijana ya kupata elimu na kurekebisha miaka ya ubaguzi wa kimfumo shuleni, limesema leo shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch katika Siku ya Elimu ya Kimataifa. Wasichana wa Kitanzania bado wako katika hatari kubwa ya unyanyapaa na ubaguzi shuleni ikiwa wana ujauzito au ni wamama.
Zaidi ya miaka mitatu tangu serikali ya Tanzania itangaze ukomo wa marufuku ya kibaguzi dhidi ya wanafunzi wenye ujauzito na wamama vijana, haijafanya mageuzi yoyote ya muhimu ya kisheria na kisera yanayohitajika ili kufafanua wajibu wa shule zote, maafisa elimu, na walimu katika kulinda na kukuza haki ya elimu kwa wanafunzi wenye ujauzito au wanaolea watoto. Serikali pia haijatoa msaada na mazingira bora yanayohitajika kwa wasichana wajawazito au wamama vijana ili wabaki shuleni na kuendelea na masomo.
“Kuondolewa kwa marufuku ya kibaguzi na yenye madhara dhidi ya wasichana wenye ujauzito na kinamama vijana mwaka 2021 kuliashiria mabadiliko muhimu ya mwelekeo na ahadi ya kurekebisha miaka ya ubaguzi, unyanyapaa, na vitendo vya udhalilishaji dhidi ya wasichana,” alisema Elin Martínez, mtafiti mwandamizi wa haki za watoto wa Human Rights Watch. “Tanzania inahitaji kumaliza ucheleweshaji wake wa mara kwa mara katika kupitisha mageuzi yanayohitajika ili kulinda haki ya wasichana kupata elimu na kuhakikisha kuwa wasichana vijana wengi zaidi wanabaki shuleni.”
Mwezi Novemba 2021, serikali ya Tanzania ilitangaza Waraka wa Waraka wa Elimu Na. 2 wa 2021, ambao ulielezea jinsi wanafunzi walioacha shule kwa sababu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na ujauzito, wanaweza kurudi shuleni. Kupitia muongozo huo, serikali iliachana na marufuku yake ya kibaguzi dhidi ya wasichana wajawazito na wamama vijana. Mwezi Februari 2022, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ya Tanzania ilichapisha "Miongozo ya kuwarejesha Wanafunzi waliokatiza masomo ya elimu ya msingi na sekondari kwa sababu mbalimbali."
Hata hivyo, hatua zote mbili zina vipengele vinavyokinzana na wajibu wa Tanzania wa haki za binadamu na vinapaswa kushughulikiwa kwa haraka, imesema Human Rights Watch. Hususan, miongozo ya mwaka 2022 ina vikwazo vya kiutawala kwa wasichana kurudi shuleni baada ya ujauzito na inahitaji kipindi cha hadi miaka miwili kwa wanafunzi wamama vijana ili kurudi shuleni. Pia inasema kuwa wasichana watakaopata ujauzito kwa mara ya pili hawataruhusiwa tena kurudi kwa elimu rasmi.
Mwaka 2022, Kamati ya Wataalamu wa Haki za Watoto na Ustawi wa Watoto ya Afrika, chombo huru cha wataalamu kinachosimamia ufanisi wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika katika kutii Mkataba wa haki za mtoto wa Afrika, ilibaini kuwa Tanzania ilikiuka haki ya wasichana ya kupata elimu, ikiwa ni pamoja na kwa kubagua wasichana kwa misingi ya ujauzito au uzazi. Kamati ilitoa matokeo yake kama jibu kwa kesi iliyofunguliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu na Kituo cha Haki za Uzazi Juni 2019 kwa niaba ya wasichana wa Kitanzania.
Mara kwa mara Serikali imekuwa ikichelewa kupitisha mapendekezo ya Kamati ya Afrika. Mapendekezo hayo ni pamoja na marekebisho ya Sheria ya Elimu Tanzania ili kueleza hatua madhubuti za kuzuia kufukuzwa shuleni kwa wasichana wajawazito na walioolewa, kutangaza marufuku ya kipimo cha lazima cha ujauzito, na kuondoa ndoa kama msingi wa kufukuzwa kwa wanafunzi katika Kanuni za Elimu (Kufukuzwa na Kusimamishwa kwa Wanafunzi Shuleni) Na. 295 za 2002.
Utafiti wa mashirika mbalimbali, ikiwemo Human Rights Watch, unaonyesha kuwa kipindi cha likizo ya lazima kinachowekwa kwa wamama vijana, hasa kwa vipindi virefu, kinapingana na juhudi za kuwasaidia wasichana warudi na kubaki shuleni. Kadiri wasichana wanavyokaa nje ya shule kwa muda mrefu, ndivyo inavyoongeza uwezekano wa wao kuacha shule kabisa. Mara wanapokuwa wameacha shule, wamama vijana wako katika hatari kubwa ya ndoa za utotoni na vitendo vingine vya ukiukaji wa haki za binadamu.
Ripoti za asasi za kiraia zinaonyesha kuwa wasichana wanaendelea kukutana na unyanyapaa nchini Tanzania wanaporudi shuleni, na bado wanakatishwa tamaa na kupuuzwa na baadhi ya wakuu wa shule na walimu katika mikoa mbalimbali. Maafisa wa shule hawana uelewa wa kutosha wa maagizo ya sasa ya wizara ya kusaidia wasichana kurudi shuleni, au hutumia mamlaka mapana wakati wa kutumia miongozo, hali inayosababisha wasichana kutorudi shuleni.
Mwezi Oktoba 2024, maafisa wa serikali ya Tanzania waliijulisha Kamati ya Afrika kuwa serikali itakamilisha mapitio ya Sheria yake ya Elimu ifikapo mwishoni mwa mwaka 2025. Kamati ya Afrika iliendelea kusisitiza wito wake kwa Tanzania kuhakikisha kuwa wasichana wenye ujauzito, wanaolea watoto, na walioolewa wanakuwa na haki ya kurudi shuleni bila vikwazo au ucheleweshaji, kuondoa kikomo cha miaka miwili cha kurudi shuleni, na kushughulikia misingi ya kufukuzwa inayohusiana na ndoa. Kamati pia ilipendekeza Tanzania kuhakikisha kuwepo kwa marufuku ya wazi na ya kisheria ya mtihani wa lazima wa ujauzito shuleni na katika vituo vya afya.
Serikali inapaswa kupitisha haraka sera ya taifa inayotoa miongozo inayozingatia haki za binadamu kwa maafisa wa shule kuhusu usimamizi wa ujauzito kwa mabinti shuleni, na kuainisha hatua mbalimbali za kuwasaidia wamama mabinti kurudi shuleni.
Serikali pia inapaswa kuharakisha mageuzi ya Sheria ya Elimu, ikiwa ni pamoja na kuingiza kinga bora za kulinda haki ya elimu kwa wanafunzi wenye ujauzito na wanaolea watoto, kuondoa vipengele vinavyoruhusu kufukuzwa kwa wasichana kwa misingi ya ndoa, na kuongeza marufuku ya wazi ya mtihani wa lazima wa ujauzito wa wanafunzi. Hatua hizi zitapelekea utendaji na mifumo ya sheria na sera za Tanzania kuwa sawa na zile za nchi nyingine za Afrika, alisema Human Rights Watch.
“Maelfu ya wasichana wamefanyiwa ubaguzi, unyanyapaa, na kutengwa katika shule za Tanzania,” alisema Martínez. “Serikali inapaswa kupitisha haraka sera ya kitaifa inayotaja majukumu ya shule kulinda haki ya kuwa shule kwa wasichana wenye ujauzito na wamama mabinti, kurekebisha Sheria ya Elimu ili kuhakikisha haki yao ya kupata elimu, na kuzuia vitendo vyote vinavyowatenga na kubagua wasichana.”