(Nairobi) – Ahadi ya Tanzania kupitisha miongozo kuhakikisha shule zinahakikisha wamama vijana wanaweza kurudi shuleni kufikia mwezi Juni 2022 ni hatua muhimu kwa elimu ya wasichana, mashirika ya Human Rights Watch na Accountability Counsel yamesema leo hii.
Tarehe 8 Machi, serikali ya Tanzania na Benki ya Dunia ilichapisha makubaliano yao kuipanga upya Programu ya Kuboresha Elimu ya Sekondari nchini (Tanzania’s Secondary Education Quality Improvement Program (SEQUIP)), inayofadhiliwa kwa mkopo wa kiasi cha dola milioni 500 kutoka Benki ya Dunia, kuendana na hatua mpya za kuondokana na katazo dhidi ya wanafunzi waliopata ujauzito au wamama vijana kurudi shuleni.
“Serikali ya Tanzania imechukua hatua ya kwanza ya muhimu na ya kutia moyo kurekebisha uminywaji haki wa muda mrefu dhidi ya wasichana,” amesema Elin Martinez, mtafiti mwandamizi wa haki za watoto wa Human Rights Watch. “Mamlaka zinapaswa sasa kuharakisha upitishwaji wa miongozo inayozingatia haki na kujumuisha ulinzi wa kisheria na kisera kwa wanafunzi wajawazito au wamama.”
Tarehe 24 Novemba, 2021, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ilichapisha waraka ulioweka wazi kwamba ujauzito au kuwa mama si vigezo vya kumfukuza mwanafunzi katika shule za umma. Wasichana wadogo walio wamama wanaruhusiwa kurudi katika shule za umma na kuendelea na masomo yao. Tanzania ilikuwa kati ya nchi kadhaa Afrika ambazo zilipiga marufuku wasichana waliopata ujauzito au kuwa wamama kuwa shuleni.
Makubaliano ya marekebisho ambayo yanafungamanisha utolewaji wa fedha na utekelezwaji wa ahadi na malengo, yameweka wazi “miongozo ya kuendelea na shule” ambayo imeainisha ni kwa muda gani mwanafunzi mwenye ujauzito anaweza kubaki shuleni kabla hajachukua mapumziko ya muda kwa ajili ya kujifungua na kwa muda gani baada ya kujifungua mwanafunzi anaruhusiwa kurudi shuleni. Serikali iliahidi pia kukataza “upimwaji mimba usio wa hiari,” ambao hutekelezwa kwa lazima katika shule nyingi za sekondari na unatumika kuwafukuza wanafunzi wajawazito. Serikali pia iliahidi kwamba itaanzisha mfumo wa ufuatiliaji kwa wasichana wanaorudi katika shule za umma kuendelea na masomo yao na namna gani mamlaka husika zinazingatia miongozo.
Miongozo ya serikali na hatua za kuifuata zinapaswa kuwa wazi na za haraka ili kuondokana na vikwazo mbalimbali wanavyokabiliana navyo wasichana wajawazio na wamama. Lakini serikali itahitaji pia kupitisha hatua zingine kuondokana na vitendo vibaya vya kimfumo katika mfumo wake wa elimu, na kuongeza zaidi ulinzi kwa wasichana walio wajawazito au ambao ni wamama.
Serikali inapaswa kurekebisha Sheria ya Elimu kuondoa vifungu katika Miongozo ya Elimu ya mwaka 2002 (Ufukuzwaji na Utengwaji wa Wanafunzi Shuleni) ambavyo vinaruhusu shule kufukuza wanafunzi ambao “wametenda makosa ya kinidhamu” au “kuingia katika ndoa,” na marekebisho ya 2016 ya Sheria hii, yanayowapa mamlaka walimu wakuu kuripoti ndoa na ujauzito katika ofisi za wakuu wa wilaya na mikoa.
Utafiti wa kina wa Human Rights Watch juu ya sheria zinazolinda haki ya wanafunzi wajawazito katika zaidi ya nchi 30 za Umoja wa Afrika umegundua kwamba miongozo mingi ni hatua muhimu katika kupitisha sera za kitaifa zenye nguvu ya kisheria. Ili kuendana na haki za binadamu, miongozo au sera zinazoshughulikia kuendelea na shule kwa wasichana zinapaswa kujikita katika kuwasaidia wanafunzi kubaki shuleni, na kupunguza muda ambao wasichana wanakuwa nje ya shule.
Serikali zinapaswa kuepuka masharti magumu yanayowataka wanafunzi kujiunga tena na shule – kwa mfano, zikitoa muda maalumu au wa lazima wa kutokuwepo shuleni baada ya kujifungua. Sera pia inapaswa kutoa maeneo maalum kwa wazazi wanafunzi wanapokuwa shuleni, kwamfano muda wa kunyonyesha, muda wa kutokuja shuleni pale mtoto anapokuwa anaumwa au wamama wanapokuwa wanawapeleka watoto kliniki, na uwezo wa kuwapeleka watoto katika vituo vya watoto vilivyopo karibu na shule.
Makubaliano ya mabadiliko ya Benki ya Dunia yanataka pia kuanzishwa kwa kamati maalumu kutengeneza Programu ya Shule Salama za serikali, unaopangwa chini ya SEQUIP “kutengeneza mazingira salama ya kujifunza ya wanafunzi,” kupunguza ukatili katika shule za sekondari, na kuimarisha msaada kwa wasichana waliobalehe.
Serikali inapaswa kuanzisha pia mpango maalumu wa uwazi na uwajibikaji ukijumuisha mfumo wa kushughulikia malalamiko katika ngazi ya shule na ya taifa na kutoa fursa kwa wanafunzi, asasi za kiraia, jamii na “wadau” wengine kuibua matatizo mbalimbali yahusuyo elimu.
Marufuku ya awali nchini Tanzania kwa wanafunzi waliopata ujauzito au kuwa na mtoto yalikuwa na madhara mabaya sana. Benki ya Dunia inakadiria kwamba takribani wanafunzi 6,500 wenye ujauzito waliacha kwenda shuleni nchini Tanzania kila mwaka, wakati ambapo mashirika yasiyo ya kiserikali huko nyuma yalikadiria kwamba karibu wanafunzi 8,000 walilazimishwa kuacha shule kila mwaka.
“Ili kuhakikisha miongozo ya kuendelea na shule na vipengele vingine vinavyohusu programu ya SEQUIP inafanikiwa vizuri, serikali itapaswa kutengeneza fursa za kushauriana na kuzungumza mara kwa mara na asasi za kiraia, wanafunzi wamama na wengine wanaoguswa moja kwa moja na program hiyo,” amesema Teresa Mutua, afisa mwandamizi wa masuala ya jamii wa Accountability Counsel. “Ni muhimu kwa serikali kuhakikisha kwamba mianya yote ya mawasiliano inafanya kazi vizuri.”