(Des Moines) - Serikali ya Tanzania inawahamisha kwa nguvu wamasai wenyeji kutoka katika makazi yao na ardhi ya mababu zao katika Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro (NCA), Human Rights Watch imesema katika ripoti iliyotolewa leo. Kabla ya uhamisho zaidi kupangwa au kufanywa, Mamlaka za Tanzania zinapaswa kurejesha huduma za muhimu za umma na kushauriana na jamii zilizo athirika ili kutafuta ridhaa huru, ya awali na yenye kuzingatia taarifa sahihi.
Ripoti ya kurasa 87-, “Ni kama Kuua Tamaduni,” inaandika mpango wa serikali ya Tanzania ulioanza mwaka 2022 kuhamisha zaidi ya watu 82,000 kutoka NCA kwenda kijiji cha Msomera, takribani kilometa 600, kutumia ardhi yao kwa madhumuni ya uhifadhi na utalii. Tangu mwaka 2021 mamlaka zimepunguza kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa huduma muhimu za umma zikiwemo, shule na vituo vya afya. Kupunguzwa huku kwa miundombinu na huduma, pamoja na kupunguza ufikiaji wa maeneo ya kitamaduni na maeneo ya malisho na kupiga marufuku kupanda mazao, kumefanya maisha kuwa magumu kwa wakaazi, na kuwalazimu wengi kuhama.
“Wamasai wanahamishwa kwa nguvu kwa kisingizio cha kuhama kwa hiari,” alisema Juliana Nnoko, mtafiti mkuu wa wanawake na ardhi wa Human Rights Watch. “Serikali ya Tanzania inapaswa kusitisha uhamishaji huu na kuheshimu haki za watu wa kiasili na jamii za vijijini kwa kuhakikisha ushiriki wao katika maamuzi yanayohusu haki zao na maisha yao kupitia mashauriano ya kweli, kupata habari, na ridhaa ya vikundi vya watu wa asili.
NCA, ambalo ni Eneo la Urithi wa Dunia la Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni inasimamiwa na Mamlaka ya Hifadhi la Eneo la Ngorongoro (NCAA), taasisi ya serikali. Eneo hilo limekua makazi ya Wamasai kwa vizazi kadhaa.
Serikali haijaomba ridhaa huru, ya awali, na yenye kuzingatia taarifa sahihi kwa wakazi wa Asili wa Kimasai katika eneo hilo kuhusu mpango wa serikali wa makazi mapya, Human Rights Watch iligundua. Wakazi hao hawakupata taarifa ya masuala yanayohusiana na mchakato wa kuhama, fidia, hali gani watarajie Msomera, na wanakijiji gani walijiandikisha kuhamishwa. Kwa kupuuza wajibu wake, serikali inaleta wasiwasi mkubwa kuhusu matarajio ya uwajibikaji, haki, na masuluhisho yanayohitajika chini ya sheria za kimataifa, kikanda na kitaifa.
Human Rights Watch iliwahoji takribani watu 100 kati ya Agosti 2022 na Desemba 2023, ikiwa ni pamoja ya wakazi wa sasa katika eneo la hifadhi, wakazi wa zamani ambao sasa wako kijiji cha Msomera, na wakazi wa Msomera ambao walikua wakiishi hapo tangu awali. Walielezea ukiukwaji wa haki zao za ardhi, elimu, afya na fidia na mashambulizi dhidi ya wakosoaji wa mchakato wa uhamisho.
“Hakuna kiongozi [wa serikali] aliyekuja kuwasikiliza wananchi wa Ngorongoro kujua matatizo yao ni nini,” alisema mjumbe wa baraza la kijiji la NCA. Ukosefu wa mashauriano umezuia ushiriki wa maana na kuzidisha madhara kwa wakazi katika maeneo yote mawili.
Mamlaka imeweka sheria mpya zinazozuia watu kuingia na kutoka nje ya eneo la hifadhi. Tangu 2022, maafisa usalama wa NCAA bila mpangilio maalumu wamewataka wakazi kuonyeshe aina mbalimbali za vitambulisho ili kuthibitisha wanapoishi ili kupata kibali cha kuingia, hata kama mkazi huyo anajulikana na mlinzi. Walinzi huwanyima wakazi kuingia au kuwalazimisha kulipa ada ya watalii ya gharama kubwa ikiwa hawana kitambulisho kinachohitajika.
Mamlaka imekataa kwa mashirika yasiyo ya kiserikali kuingia au kuwafuata na kuwafuatilia wawakilishi wao ambao wameruhusiwa kuingia. Mamlaka pia imeweka ada kubwa za kuingia kwa vikundi vya ndani: ada ya kila mwaka mnamo 2022, ada ya gari kwa kila mtu anaeingia mnamo 2023, na ada ya kwa kila mtu na kila gari kwa kila anayeingia mnamo 2024.
Vitendo hivi hufanya iwe ngumu kwa vikundi vya wenyeji kuendelea kusaidia jamii za Wamasai katika eneo hilo na kufanya iwe vigumu kwa wakazi kupata taarifa na usaidizi mwingine.
Wakazi waliwaambia Human Rights Watch kwamba uhusiano kati ya walinzi wa mamlaka ya uhifadhi, wanaolinda maeneo ya kuingilia na maeneo mengine ya NCA, na wanajamii umezorota sana tangu serikali kuanza mpango wa kuhamisha. Walinzi hao wamewashambulia, kuwapiga na kuwanyanyasa wakazi kwa kutokufuata kanuni za serikali. Human Rights Watch ilirekodi matukio 13 ya kupigwa na walinzi kati ya Septemba 2022 na Julai 2023.
Michakato ya serikali kuhamisha watu na makazi mapya umechochea ukosefu wa usawa wa kijinsia, Human Rights Watch ilisema. Mkuu wa kaya, kwa kawaida ni mwanaume, husajili familia kwa ajili ya kuhamishwa. Wakati wa kuhamishwa, serikali inaharibu makazi ya familia hiyo, na kuacha jamaa yoyote, ikiwa ni pamoja na wake walioamua kubaki, bila makazi na kuwa tegemezi kwa familia walizotoka. Human Rights Watch iliwatambua wanawake kadhaa ambao hawakuhusishwa katika kujiandikisha, walikataa kuhama na waume zao na waliachwa bila makazi.
Kushindwa kushauriana kumesababisha serikali kutoa nyumba moja ya vyumba vitatu kwa kila mkuu wa kaya wa kimasai aliyehamishwa, ambayo haiakisi mahitaji au mchangamano wa familia zao kubwa, za wake wengi, vizazi vingi na kaya nyingi. Mamlaka pia imehamisha wakazi wa Msomera ili kuzipa makazi familia zilizohamishwa kutoka eneo la hifadhi, ikiwaita wakazi wa Msomera “wahalifu” na “wakazi holela” na kuwatishia kukamatwa na kufukuzwa endapo wataandamana au kuzungumza na vyombo vya habari.
Wale wanaozungumza kupinga uhamisho wakiwemo wakazi wa NCA na Msomera na watetezi wa haki za binadamu wamekabiliwa na vitisho kutoka kwa walinzi na vyombo vya usalama, hali inayozua mazingira ya hofu. “Hauruhusiwi kusema lolote,” mkazi mmoja wa Msomera alisema, na kuongeza kua watu “wana hofu mioyoni mwao”.
Utaratibu wa serikali ya Tanzania kuhamisha watu unakiuka haki zinazolindwa na sheria na viwango vya kitaifa, kikanda na kimataifa, ikiwa ni pamoja Mkataba wa Afrika na Haki za Binadamu na Watu, Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiuchumi, Kijamii na Kitamaduni, Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa na Azimio la Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Watu wa Asili. Kufukuzwa kwa lazima kunajumuisha ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu zinazoambulika kimataifa, ikiwa ni pamoja na makazi yanayokidhi, chakula, maji, afya, elimu, kazi, usalama wa mtu, kuwa huru dhidi ya kufanyiwa ukatili, unyama na udhalilishaji, na uhuru wa kutembea.
“Umuhimu wa serikali ya Tanzania kuheshimu haki za jamii za Wamasai wa Asili ni wajibu wa kimaadili na pia wa kisheria,” Nnoko alisema. “Serikali inapaswa kuangalia upya kwa uharaka mbinu yake na kuhakikisha kuendelea kwa maisha, ustawi na utu wa wamasai, ambao kwa sasa unawekwa hatarini na mchakato huu wa kuwahamisha.”
Nukuu zaidi:
Mwenyekiti wa kijiji katika eneo la hifadhi alisema:
Serikali inaanza kutufanya tusifanye kazi kabisa. Wanajaribu kutudhoofisha katika njia zote za maisha. Kukata tamaa, kuto kupigana na kuondoka. Wanajaribu kuhakikisha kuwa ufugaji unafikia kikomo. Hatujawahi kuwafukuza wanyamapori. Sisi ni wahifadhi wazuri sana; hatuwachukii wanyama pori.
Kiongozi wa kimila katika eneo la hifadhi alielezea mkutano wa maafisa:
Hayo hayakua mashauriano kwa sababu [waziri mkuu] alizungumza tu na kuondoka. Hakukua na kitu kama kuchukua maoni na mashaka ya watu…. waziri mkuu alitembelea eneo hilo; watu wengi walienda, lakini wakanyimwa [ruhusa] ya kuingia. Alichagua watu wachache - maofisa wa kata na vijiji na alisema tu kile anachofikiria na kwenda zake.
Kiongozi wa vijana katika eneo la hifadhi alisema:
Hatujui lolote kuhusu Msomera. Tulichosikia ni kwamba watu wamepoteza mifugo yao. Je tunahakikishaje kwamba serikali inatoa dhamana kwamba katika kipindi cha miaka miwili hadi mitano ikiwa wakazi waliohamishwa watapoteza mifugo yao yote, watapewa mingine, kupata fidia, au msaada? Je, jamii inawezaje kuhakikisha kua serikali inatoa uhakikisho huu ikiwa hatuna taarifa?
Mkazi wa eneo hilo la hifadhi alisema, “pale Ngorongoro, Serikali iliipa jina operesheni ile ‘kuhama kwa hiari’ lakini hakuna kuhama kwa hiari. Serikali inatumia njia tofauti kutesa jamii yetu.”
Diwani katika kijiji cha Esere katika eneo la hifadhi alitoa mfano wa namna serikali imesitisha kusaidia huduma za afya katika eneo la NCA:
Siwezi kulinganisha Endulen [hospitali] sasa na hapo awali. Hapo awali serikali ilitoa msaada pamoja na kulipa baadhi ya wafanyakazi wa hospitali. Hapo awali, Endulen ilikua na huduma za mama na mtoto na dawa za kutosha. Sasa serikali imesitisha misaada yote; wamerudisha madaktari wao katika hospitali za serikali.
Kiongozi wa kimila katika eneo la hifadhi alielezea madhara ya kupungua kwa huduma za afya kwa wakazi wanaougua na hawawezi kumudu gharama za usafiri:
Kila mkazi anaumia. Ukiugua unafikiria gharama kubwa utakayotumia kutafuta huduma za afya. Watu maskini wapo katika hatari zaidi kwa sababu hawana pesa za kusafiri mbali, na zahanati za karibu hazina dawa. Unaweza kuuza mifugo na kupata huduma hizi. Njia nyingine ni kutumia mitishamba ya kitamaduni au kuomba Mungu kwa ajili ya muujiza.
Alikua anatembea, wakamuhadhibu tu. Walimfanya achutame kichura [mtindo wa chura], na wakampiga kwa kutumia fimbo. Alipata majeraha kwenye miguu yake. Hatuna mahali popote pa kutoa taarifa. Unaenda kwa polisi wale wale waliompiga, kwa hivyo huwezi kupata msaada wowote. Kuna kesi nyingi kama hizi. Walinzi hawa ni kama watu walio juu ya sheria.
Mkazi wa Msomera ambaye familia yake ilihamishwa na uhamisho huo uliofadhiliwa na serikali alisema:
Nilizaliwa hapa. Babu yangu alizaliwa hapa… Sisi ni familia ya takribani watu 72 yenye babu na bibi, wake, Watoto [leo hii]. Hakuna ardhi ya kutosha kulisha kila mtu katika familia yetu. Sasa tunategemea ng’ombe wetu pekee, ambao tunawaweka mbali na hapa kwa sababu hakuna mahali pa malisho.