(Nairobi) – Viongozi wa Afrika walishindwa kukabili dhuluma zilizofanywa na vyombo vya serikali na makundi yaliyojihami dhidi ya raia huku sera na mipango yao ikikosa kutoa nafasi ya kushughulikia masuala ya haki za waathiriwa, Shirika la Human Rights Watch limesema leo kwenye Ripoti yake ya Dunia (World Report 2023) Mwaka 2023. Ukiukaji haki za binadamu umefanyika katika mazingira ya kudorora viwango vilivyopo vya kuhakikisha jamii zinaongozwa kisheria.
Umoja wa Afrika (AU) na taasisi za umoja huo katika jumuiya za kanda zafaa kubuni njia za kuanzisha mifumo ya kuhakikisha masuala ya haki za binadamu yanafuatwa kwa umakini huku dhuluma zinazotokea kwenye maeneo ya mizozo zikifuatwa na kuripotiwa - ni muhimu jamii kulenga namna ya kuepuka michipuko ya majanga yanayowaathiri wanadamu.
“Juhudi za barani Afrika za kujaribu kushughulikia mizozo mingi ya barani mwaka 2022 zimekosa kuungwa mkono na viongozi wa kisiasa na hivyo kuacha raia wengi kuathirika vibaya, wengi wakikosa pa kutorokea ,” asema Mausi Segun, Mkurugenzi wa tawi la Afrika -Shirika la Human Rights Watch. “Njia bora ya kuhakikisha suluhu kwa matatizo ya Afrika kutoka ndani ya Afrika ni viongozi wa kisiasa barani kutumia vyombo vya serikali kuwalinda raia kutokana na dhuluma na ukiukaji wa haki za binadamu.”
Kwenye ripoti yake ya awamu ya 33 yenye kurasa 712 ya Dunia, World Report 2023, Shirika la Human Rights Watch limeangalia na kupitia masuala ya ukiukaji haki katika karibu nchi 100. Kwenye maandiko yake ya utangulizi, kaimu mkurugenzi mkuu Tirana Hassan anasema katika dunia ya sasa, yenye kubadilika kwa wenye nguvu na mamlaka, si bora tena kuzitegemea serikali za mataifa ya ulaya (ukanda wa kaskazini wa Dunia) kutetea haki za binadamu. Namna ambavyo Dunia imeshughulikia mzozo wa Urusi kuivamia Ukraine inatukumbusha uwezo uliopo katika serikali kuelewa majukumu yake ya kulinda haki za binadamu kote. Ni jukumu la nchi zote, ziwe kubwa au ndogo, kutunga sera zinazozingatia haki za binadamu na kushirikiana kuendeleza enzi ya kuongoza jamii kwa kutii haki za binadamu.
Kwenye mizozo katika mataifa takriban 15, ikiwemo Jamhuri ya Demokrasia ya Congo, Cameroon, Ethiopia, Msumbiji, Mali, Burkina Faso, na Sudan Kusini, majeshi ya serikali na makundi mengine yenye silaha yameshukiwa kuhusika kwenye dhuluma dhidi ya binadamu.
Kumekuwa na hatua chache kupigwa kwenye mpango wa kuhakikisha haki inapatikana hasa kuhusu makosa makubwa ya jinai, Shirika la Human Rights Watch limesema. Vikao vya kesi dhidi ya washukiwa vilianza katika Jamhuri ya Afrika -Kati na Guinea, huku Mahakama ya Kimataifa kuhusu jinai (ICC) ikifungua kesi zinazohusu makosa makubwa ya jinai dhidi ya viongozi wa kijeshi katika Jamhuri ya Afrika- Kati na Sudan.
Kaskazini mwa Ethiopia, mzozo unaokumba maeneo ya Tigray, Amhara, na Afar umekuwa na athari kubwa kwa mamia ya maelfu ya raia waishio kule. Sehemu kubwa ya watu wa jamii ya Tigray na watu waishio eneo la Tigray wangali kurejea kwao- mbali na hilo watu hao hawafikiwi na ufadhili wowote wa kibinadamu iwe kwa chakula au dawa. Katika eneo la Oromia, mapigano baina ya majeshi ya serikali ya Ethiopia na jeshi la wapinzani wa Oromo -Oromia Liberation Army yameongezeka. Juhudi za kuwachukulia hatua wanaohusika katika makosa makubwa ya jinai ikiwemo ukiukaji wa haki zilivurugwa.
Katika mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, kundi linaloungwa mkono na Rwandan - M23 limefanya upya dhuluma na mauaji mengi katika eneo la mashariki la Congo. Makundi mengine yaliyojihami kwa silaha, wakiwemo wanajeshi wa serikali ya Congo, wamekuwa wakifanya dhuluma kwa kuwa hamna hatua zinachukuliwa dhidi ya wanaohusika dhuluma hali ambayo imechochea msururu wa vurugu. Mwezi Agosti, serikali ya Burundi imewatuma wanajeshi mashariki ya Congo, huku wakipata usaidizi kutoka kwa vikosi kutoka Kenya mwezi Novemba. Oparesheni hiyo mpya ya Congo ilitokana na uamuzi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwamba liteuliwe jeshi rasmi la kurejesha amani na usalama katika Kongo.
Mwezi Novemba, mazungumzo yaliyokuwa yakiongozwa na Umoja wa Afrika yaliafikia kusainiwa kwa mkataba uliokomesha kwa muda mizozo baina ya serikali tanagamano ya Ethiopia na mamlaka yanayojitenga na kutangaza uhuru wa eneo la Tigray.
Kule Msumbiji, Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) ikishirikiana na a Rwanda waliunga mkono jeshi la Msumbiji kwenye mzozo baina yake na kundi la kiislamu lililojihami la Ansar al-Sunna Wa Jamma (ASWJ), ambalo linashirikishwa na kundi la awali la Islamic State. Mzozo huo umesababisha mapigano katika mkoa wa Cabo Delgado ambapo raia wamevamiwa huku zaidi ya 940,000 wakifukuzwa kwao - muda wa miaka minne iliyopita.
Katika ukanda wa Afrika Magharibi, kwenye mataifa ya Burkina Faso, Guinea, na Mali, hapajakuwa na kuboreka hali kwenye suala lililopalilia mapinduzi ya hivi majuzi.Umoja wa Afrika na vilevile Jumuiya ya kijamii na kiuchumi ya Magharibi ya Afrika ECOWAS kwa pamoja zilipinga mapinduzi hayo kwa kuzipokonya nchini zilizoathirika uanachama katika AU na ECOWAS huku zikitishia vikwazo zaidi.
Ukosoaji uliofanywa na wanajeshi wanaotawala Mali dhidi ya oparesheni za kutoka ng’ambo zinazonuia kukomesha ugaidi pamoja na vurugu zinazofanywa na makundi ya kiislamu nchini Mali kulisababisha kuondoka kwa jeshi la Ufaransa na majeshi mengine kutoka Umoja wa ulaya nchini humo.
Kuongezeka kwa mapigano nchini Mali na Jamhuri ya Afrika-Kati kulisadifiana na habari kuhusu ukiukaji mbaya wa haki za binadamu uliokuwa ukifanywa na wanamgambo kutoka nchi za nje waliofika nchi hizo. Wanamgambo hao walikuwemo wale wa kutoka Urusi - wanaoshirikishwa na kundi la Wagner.
Licha ya hiyo, namna ambavyo serikali za kanda zinafaa kushughulikia suala hilo kulifanywa bila mvuto hasa kwa kuwa viongozi Afrika walitumia njia za kisiasa na kikatiba kusalia mamlakani, waliwadhulumu au hata kuwaua wanahabari, kuwadhulumu wanaharakati wa haki za binadamu na watu wengine waliofikirika kuwa washindani wao.
Kwenye kongamano maalum lililoitishwa mwezi Mei kwa ajili ya kujadili masuala ya ugaidi na mapinduzi ya serikali, Umoja wa Afrika- AU, ulilaani na kukosoa vikali visa vya ugaidi, vurugu zinazofanywa na makundi yenye misimamo mikali, na namna zote za kuziondoa serikali mamlakani bila kufuata katiba za nchi. Viongozi waliohutubia kikao walitoa wito kundolewa kwa makundi ya ugaidi yanayotoka nje ya bara la Afrika yaliyopo barani na vilevile makundi ya mamluki -wapiganaji wa kulipwa. Kikao hicho cha AU kiliafikiana kwamba serikali zimejitolea kukabili mitandao ya kihalifu inayoeneza shughuli zao kimataifa.
Mamlaka kwenye baadhi ya nchi zenye serikali za mpito yaliwaandama wote wanaozikosoa serikali hizo au kuendeleza mawazo mbadala na ukosoaji dhidi ya serikali hizo. Mwezi Machi, jeshi la Chad liliwatawanya kwa ukatili maalfu ya waandamanaji waliokuwa wakieneza ujumbe wao kwa amani. Nchini Sudan, ukiwa wakati wa maandamano ambayo yametatiza nchi tangu mapinduzi ya Oktoba mwaka 2021, majeshi yamewauwa watu zaidi ya 100, yamewaweka kizuzini mamia ya watu bila kuwafungulia mashtaka, huku yakiwapoteza wengine. Umoja wa Afrika umesalia kimya muda wote ambapo haya yametokea.
Msururu wa misako na oparesheni dhidi ya watu wanaokosoa serikali hata hivyo haijawalenga raia katika nchi zinazoongozwa na serikali za mpito pekee. Nchini Burundi, Rwanda, Uganda, na Zimbabwe, wanaharakati, washindani, na wanahabari wamekuwa wakiwekwa kizuizini na kuteswa. Nchini Congo, mavamizi dhidi ya vyombo vya habari, kuendelea kushirikishwa kwa idara za ujasusi katika kuwatisha watu wanaopinga serikali na kuzikosoa, na kuendelea kukosa kwa uhuru wa watu kufanya shughuli zao kwa njia za demokasia kunapalilia wasiwasi kuhusu ni vipi msimu wa uchaguzi unaosubiriwa mwaka 2023 utakuwa.
Katika maeneo mengine barani Afrika, watu waliofukuzwa kwao, wakimbizi, na wahamiaji wametoroka kwao kutokana na kuzuka vurugu, dhuluma kufanywa na serikali, vurugu za kijamii, umaskini, na matatizo yanayoletwa na mabadiliko ya kimazingira. Nchini Eritrea na Cameroon, watu kadhaa waliokuwa wametoroka kutafuta maficho walirudishwa kwa nguvu na kutiwa kizuizini huku wakifanyiwa dhuluma nyingine. Nchini Nigeria, hatua ya serikali ya kuzifunga kambi zilizokuwa za kuishi wakimbizi iliwaweka maalfu katika hangaiko na ukosefu wa makao.
Ukosefu wa njia za kisheria za kuhama kutoka nchi moja hadi nyingine, ukosefu wa maficho kwa wanaotorokea usalama ndani na nje ya Afrika , ukijumuishwa na shinikizo kutoka Umoja wa Ulaya na mataifa wanachama, umesababisha vifo vya watu wanaohama, na kuongeza dhuluma dhidi yao kukiwemo kutumiwa vibaya na kubaguliwa.
Ikija kwenye suala la waathiriwa wa majanga kusaidiwa, upo mkanganyiko kwenye hatua inayopigwa, Limesema Shirika la Human Rights Watch.
Mwezi Julai, Umoja wa Afrika AU ulitangaza uanzishaji wa hazina ya kuwafidia waathiriwa wa utawala wenye dhuluma wa rais wa Chad Hissène Habré.
Nchini Guinea, kesi dhidi ya washukiwa wa maangamizi yaliyofanyika katika uwanja wa michezo Mwaka 2009 zilifunguliwa miaka 13 baadaye na hivyo kuonyesha umuhimu wa kuwepo njia za kufuatilia makosa ili kuwachukulia hatua wahusika wa makosa makubwa ya kihalifu.
Mwezi Oktoba, Mahakama maalum kuhusu uhalifu katika Jamhuri ya Afrika-Kati iliwapata na hatia Issa Sallet Adoum, Ousman Yaouba, na Tahir Mahamat, wa kundi la ugaidi la 3R kwa makosa ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu uliofanyika nchini humo Mwaka 2019.
Lakini wazo la Umoja wa Afrika (AU) la kubuni Mahakama maalum lililofikirika kwenye mkataba wa amani wa Mwaka 2015 halijatekelezwa ili kuanzishwe Mahakama na ianze kazi.
Mataifa ya Burundi na Ethiopia yameendelea kumnyima nafasi ya kuingia nchini mwao mjumbe wa Umoja wa Mataifa kuhusu masuala yanayofanyika nchini Burundi. Vilevile yameinyima fursa tume ya uchunguzi ya Umoja wa Afrika kuhusu haki za binadamu na masuala yote ambayo yamefanyika katika eneo la Tgray na hivyo kuwanyima fursa ya kuingia watalaamu wa tume ya Umoja wa mataifa kuhusu Ethiopia.
Mashirika ya kijami ya barani Afrika yamehusika pakubwa katika kuhakikisha kwamba taasisi hizi zimeanzishwa na kwamba zinahudumu kwa uhuru na umakini kwenye oparesheni zao
“Serikali za Afrika na taasisi za kanda barani Afrika zinafaa kutangaza waziwazi tena mbele ya umma kwamba zinapinga na kukataa kushirikishwa na dhuluma na oparesheni dhidi ya watu wanaozikosoa, hali iliyozagaa katika bara zima la Afrika,” Alisema Segun. “Juhudi za ukweli zenye nia ya kukabili tatizo la watu kufanya makosa bila kuchukuliwa hatua za kisheria zinafaa kufanyiwa uchunguzi na taasisi isioegemea upande wowote. Vilevile kesi zifunguliwe na kufanywa bila mapendeleo kuwahusu wale waliohusika katika ukiukaji wa haki za kimsingi ukiwemo uhalifu wa kivita kote barani Afrika.”