Skip to main content

Kenya: Haki Iliyochelewa kwa Ukatili wa Maandamano ya 2023

Tekeleza Marekebisho ya Kimsingi na Sera Muhimu za Polisi, Fidia

Polisi wa kukabili ghasia wawatawanya wafwasi wa muungano wa upinzani Azimio La Umoja, wakati wa maandamano ya kulalamikia kupanda kwa gharama ya maisha na makosa kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2022, mtaani Mathare jijini Nairobi, Machi 27, 2023. © 2023 REUTERS/John Muchucha
  • Mamlaka za Kenya zimeshindwa kuhakikisha haki inatendeka kwa mauaji ya watu wasiopungua 31 na ukatili mwingine uliofanywa na polisi wakati wa maandamano kote nchini kuanzia Machi hadi Julai 2023.
  • Zaidi ya mwaka mmoja baadaye, uchunguzi haujakamilika wala hakuna afisa hata mmoja wa polisi au afisa wa serikali aliyeshtakiwa kwa mauaji hayo au ukiukaji mwingine wa haki.
  • Rais Willam Ruto anapaswa kuhakikisha kuwa Mamlaka ya Usimamizi wa Polisi (IPOA) inafanya kazi kwa uhuru na kutoa wito kwa taasisi zinazofaa kufuatilia mapendekezo yake. 


(Nairobi) – Mamlaka za Kenya zimeshindwa kuhakikisha haki kwa mauaji ya watu wasiopungua 31 na dhuluma nyingine zilizofanywa na polisi wakati wa maandamano kote nchini kuanzia Machi hadi Julai 2023, Amnesty International Kenya na Shirika la Human Rights Watch walisema katika ripoti iliyotolewa leo. Zaidi ya mwaka mmoja baadaye, uchunguzi haujakamilika, na hakuna afisa wa polisi au afisa wa serikali aliyeshtakiwa kwa mauaji hayo au ukiukaji mwingine wa haki za binadamu. 

Ripoti yenye kurasa 77, “Haki Iliyocheleweshwa: Ukandamazaji wa Maandamano ya 2023 Nchini Kenya ,” inaeleza jinsi polisi, chini ya utawala wa Rais William Ruto, walitekeleza ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu walipokabiliana na maandamano ya kitaifa yaliyoongozwa na vyama vya upinzani na ambayo kwa kiasi kikubwa yalikuwa ya amani. Maandamano hayo yalichochewa na gharama ya juu ya maisha na madai ya ukiukaji wa sheria za uchaguzi mkuu wa Agosti 2022.

“Polisi wa Kenya waliwaua watu kinyama na kinyume cha sheria, kuwajeruhi, na kuwanyanyasa waandamanaji na wapitanjia, wakiwamo watoto wengi,” alisema Otsieno Namwaya, Mkurugenzi Mshiriki wa Afrika katika Human Rights Watch. “Serikali inapaswa kuhakikisha kuwa Mamlaka Huru ya Usimamizi wa Polisi (IPOA) na mamlaka za mashtaka ya umma (ODPP) zina uwezo wa kufanya kazi kwa ufanisi, ili waathiriwa na familia zao wapate haki kwa uhalifu huu.” 

Ripoti hiyo inatokana na mahojiano ya watu 226 walionusurika na mashahidi katika kaunti za Nairobi, Kisumu, Nyamira, Machakos, Migori, Kisii, Siaya, Nakuru, Homa Bay, na Makueni. 

Amnesty International Kenya na Human Rights Watch waligundua kwamba kati ya Machi na Julai 2023, polisi walitumia nguvu nyingi na zisizohitajika dhidi ya waandamanaji na wapita njia, ikiwemo kutumia risasi za mauji, miripuko za athari za kimwili kama vile makombora ya mpira, mateso na unyanyasaji mwingine, kukamatwa koholela na kifungo kisicho cha kisheria, na kutekeleza ukiukaji mkubwa wa haki dhidi ya Watoto chini ya umri wa miaka 18. 

Mashirika hayo pia yaligundua kwamba polisi wa Kenya walitumia vitoza machozi kwa njia isiyo sahihi na kiholela, hasa katika maeneo ya shule, vituo vya afya, na maeneo ya makazi. Takriban watoto wawili walifariki kutokana na kufichuliwa vitoza machozi nyumbani kwao.

Wakati wa msako wa nyumba kwa nyumba kuwanasa wanaoshukiwa kuwa waandamanaji mnamo Julai 2023, polisi katika Kaunti ya Kisumu waliwapiga, kuwakandamiza na kuwatishia walioshukiwa, wakiwemo watu ambao hawakuwa sehemu ya maandamano. Waliwaua watu watatu wakati wa msako huo, wakiwamo binamu Brian Oniango’ na William Amulele, ambao walifariki kutokana na majeraha ya kupigwa na polisi. 

Jamaa wa familia alisema, “Nilikuwa nyumbani kwangu niliposikia kelele nje na sauti zikisema kwamba wanangu wanauliwa … nilifungua mlango na kuwaona wakipigwa. Nilipiga magoti, nikiwasihi wawaache wavulana hao kwa vile hawakuwa sehemu ya [maandamano], lakini afisa mmoja alikuja na kuniamuru nirudi nyumbani ... alinipiga teke hadi nikaanguka nyuma. [waliendelea] kuwapiga.”

Unyanyasaji wa polisi uliwadhuru waathiriwa na familia zao kimwili, kiakili, na kifedha. Wengi waliohojiwa katika siku na miezi iliyofuata walisema kwamba majeraha yao yameathiri afya na maisha yao. Mkulima mwenye umri wa miaka 50 ambaye mwanawe John aliuawa kwa kupigwa risasi Julai 7, 2023, Kisii, kwa madai ya polisi, alisema, “Mwanangu alinisaidia kwa kila kitu. Alipenda kunipigia simu na kuniuliza ikiwa nilihitaji usaidizi wowote. Alitaka kurudi nyumbani na kukaa ili anisaidie kuwasomesha ndugu zake. John alikuwa tegemeo langu. Tegemeo limeondoka…. Sijui la kufanya.”

Baadhi ya manusura na familia za waathiriwa wa dhuluma waliripoti kwamba walifukuzwa kutoka vituo vya polisi walipojaribu kuripoti dhuluma za polisi. Wengine walisema kwamba hawakuweza au hawakutoa ripoti kwa polisi kwa sababu walihofia kulipizwa kisasi au waliamini kwamba ripoti yao haingefwatiliwa.

Mamlaka Huru ya Usimamizi wa Polisi (IPOA), ambayo hutoa uangalizi wa kiraia wa mwenendo wa polisi, iliarifu Amnesty International Kenya na Human Rights Watch katika majibu ya barua ya tarehe Oktoba 29 kwamba watu wasiopungua 67 waliuawa wakati wa maandamano kati ya Machi na Julai, 2023. IPOA ilisema kwamba walipendekeza uchunguzi wa kesi sita ufanyike na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP), walifunga kesi nne na wanachunguza kwa makini kesi za wahasiriwa 57. IPOA ilisema kwamba walikumbana na changamoto nyingi ikiwemo ukosefu wa ushirikiano kutoka kwa mashahidi na tabia ya polisi kuficha utambulisho wao na kutumia magari yasiyo ya polisi, jambo lililofanya kuwa vigumu kubaini uwajibikaji.

Rais Ruto anapaswa kuhakikisha kwamba IPOA ina uwezo wa kufanya kazi yake kwa uhuru na kutoa wito kwa mamlaka zinazofaa kufuatilia mapendekezo ya IPOA. Pia anapaswa kuunda Tume ya Uchunguzi kuchunguza dhuluma za 2023 na ukatili unaoendelea kuhusiana na maandamano, ikiwa ni pamoja na kubaini ni vitengo vinavyohusika na unyanyasaji, kutambua maafisa waliohusika, na kubaini maagizo yaliyotolewa kwa maafisa wa polisi, kukomesha matumizi ya polisi wasio na sare katika maandamano, na matumizi ya maafisa wa polisi ya kuficha nyuso zao, mashirika hayo mawili yalisema.

Zaidi ya hayo, serikali ya Kenya inapaswa kushughulikia sababu kuu za maandamano ya zamani na yanayoendelea, ikiwa ni pamoja na sera za serikali za kiuchumi ambazo zinawanyima watu haki zao za kiuchumi, kijamii, na kitamaduni. Hii inaweza kujumuisha kutunga au kupanua hatua za kulinda jamii ili kuhakikisha usalama wa mapato ya wale waliojeruhiwa na mamlaka na wasioweza kufanya kazi, pamoja na wategemeaji waliobaki wa wale waliouliwa, mashirika hayo mawili yalisema.

“Mamlaka za Kenya zinapaswa kufanya kazi kwa bidii ili kurejesha imani ya umma na kuonyesha kwamba zinaweza kutekeleza mageuzi yanayozingatia watu na yenye muktadha wa haki za binadamu,” alisema Irungu Houghton, Mkurugenzi Mtendaji wa Amnesty International Kenya. “Wanaweza kuanza kwa kukomesha hali ya kutoadhibiwa kwa dhuluma za polisi wakati wa maandamano na kutunga njia za kipevu za kuitatua mashara mabaya ya sera za kiuchumi za serikali.” 

 

Your tax deductible gift can help stop human rights violations and save lives around the world.

Region / Country