Skip to main content

Sudan: Mauaji mapya ya halaiki yanayoegemea kabila, uporaji Darfur

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lafaa kuchukua hatua kuwalinda raia, kuwaadhibu makamanda wa Jeshi la Rapid Support Forces.

Familia zikitoroka Ardamata Darfur Magharibi kuingia Adre, nchini Chad, kufuatia msururu wa vurugu za kikabila. Tarehe 7 Novemba. Manusura walielezea visa vya watu kuuawa na uporaji katika eneo la Ardamata, uliofanywa na jeshi la Rapid Support na wanamgambo wa kiarabu wanaoliunga mkono © 2023 REUTERS/El Tayeb Siddig
  • Jeshi la Rapid Support liliwaua mamia ya raia katika eneo la Darfur Magharibi mapema mwezi Novemba mwaka 2023.
  • Matukio mapya kabisa ya mauaji ya kikabila yanayolishirikisha jeshi la Rapid Support katika eneo la Darfur Magharibi yana ishara zote za kupangwa makusudi kupitia kampeni ya kutekeleza madhila dhidi ya raia wa jamii ya Massalit.
  • Baraza la Usalama la Umoja wa mataifa lafaa tena kwa haraka kuanza kuonyesha umakini wake kuhusu yanayoendelea Sudan ili kuzuia madhila zaidi na hivyo kuwalinda ifaavyo raia wa Darfur.

(Nairobi) – Jeshi la Rapid Support na wanamgambo wanaoshirikiana nalo waliwaua mamia ya raia katika eneo la Darfur Magharibi mapema mwezi Novemba mwaka 2023, Shirika la Human Rights Watch limesema leo. Jeshi hilo pia lilipora, likawapiga watu, na likawatia kizuizini wengine kinyume cha sheria watu wa jamii yenye idadi kubwa katika eneo la Ardamata ya Massalit, sehemu ya El Geneina Darfur Magharibi.

Kutokana na kuwepo mpango wa kufunga ubalozi wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan, huku nafasi hiyo ikipangwa kuchukuliwa na ujumbe maalum, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lafaa kwa haraka kutafuta njia za kutia guu lake nchini Sudan, ili kuzuia madhila zaidi  kwa lengo la kuwalinda raia wa eneo la Darfur. Baraza la Usalama linafaa kuunga mkono juhudi za kufuatilia matendo ya ukiukaji wa haki za binadamu kule Darfur ikiwemo kuongeza marufuku ya silaha kule na kuieneza kote nchini Sudan. Vilevile, Umoja huo unafaa kueneza marufuku hiyo kuwalenga wahusika wote kwenye mzozo unaoendelea Sudan. Mataifa ya Afrika wanachama wa Baraza la Usalama, Umoja wa Milki za Kiarabu (Imarati), na nchi zingine wanachama wa Baraza la Usalama zafaa kuunga mkono juhudi na hatua hizi na hatua nyingine ili kuhakikisha kwamba tawi lenye mamlaka zaidi la Umoja wa Mataifa linaunga mkono kutekelezwa kwa wajibu wake wa kulinda maisha ya raia wa Darfur Magharibi  na kote nchini Sudan.

“Matendo mapya dhalimu yaliyofanywa na jeshi la Rapid Support’ ambayo ni mauaji yanayowalenga watu wa jamii tofauti katika eneo la Darfur Magharibi, yana dalili zote za madhila yaliyopangwa chini ya kampeni makusudi ya kufanya maafa dhidi ya raia wa jamii ya Massalit,” alisema Mohamed Osman, Mtafiti wa Sudan wa Shirika la Human Rights Watch. “Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lafaa kukoma kupuuza suala muhimu la kuwalinda raia wa Darfur.”

Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Wakimbizi (UNHCR), yakadiriwa watu 800 waliuawa wakati wa mavamizi ya mapema mwezi Novemba katika eneo la Ardamata. Waangalizi wa mashirika ya haki wa eneo waliwahoji waathiriwa waliokuwa wakifika nchini Chad ambapo walikadiria idadi ya watu waliokuwa wameuawa na ambao walikuwa raia wasio na hatia kuwa kati ya 1,300 na 2,000, wakiwemo wengi waliouawa wakiwa njiani kutorokea Chad. Yamkini watu 8,000 wametorokea Chad, kujiunga na karibu watu 450,000, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, ambao wamefukuzwa makwao kutokana na mashambulizi Darfur Magharibi  kati ya mwezi Aprili na Juni.

Shirika la Human Rights Watch liliwahoji watu 20 wa jamii ya Massalit waliotoroka Ardamata kukimbilia Mashariki mwa Chad kati ya tarehe 1 hadi 10 mwezi Novemba, wakiwemo wanajeshi 3 wa Jeshi la taifa la Sudan (SAF). Wote walielezea msururu wa mauaji, ulipuaji wa mabomu, kuwazuilia watu kinyume cha sheria, dhuluma za kimapenzi, kuwatesa na kuwatumikisha watu, na uporaji. Watu wote waliohojiwa wametambuliwa kwa kutumia majina yasiyo yao haswa kwa madhumuni ya kuwalinda. Shirika la Human Rights Watch vilevile limekagua picha nane za video na picha zisizo za video ambazo zimetumwa kwenye mitandao ya kijamii zikionyesha jeshi ya Rapid Support likiwa limewazuilia zaidi ya wanaume na wavulana 200 katika eneo la Ardamata. Mojawapo ya video inaonyesha kundi la wanamgambo likilipiga wanaume walokuwa kwenye kundi moja.

Shirika la Human Rights Watch liliwatumia barua wanajeshi wa Rapid Support, kuwajulisha yale ambayo lilikuwa limeyapata huku likiwauliza maswali kuhusu matukio hayo, lakini halikupokea majibu hadi kufikia wakati wa kuchapisha ripoti hii.

Picha za satelaiti zilizochukuliwa juma la kwanza la mwezi Novemba zinaonyesha athari za urushaji mabomu miongoni mwa raia na pia kwenye miundo msingi ya majeshi na vilevile uporaji, na kuteketeza mali katika eneo la Ardamata kwenye kambi ya watu waliotoroka makwao. Picha za satelaiti vilevile zinaonyesha makaburi mapya katika eneo makaburi rasmi na vilevile maiti kwenye barabara za mji.

Mzozo ulizuka tarehe 15 mwezi Aprili nchini Sudan kati ya makundi mawili ya majeshi; Jeshi la Sudan (Sudanese Armed Forces) na Jeshi la Rapid Support Forces. Kati ya Aprili na Juni, jeshi ya Rapid Support  na makundi ya wanamgambo yanayoshirikiana na jeshi hilo yalitekeleza msururu wa dhuluma za kuwapiga watu wa jamii ya Massalit ambao ndio wengi katika eneo la El Geneina, na miji mingine na vijiji vya eneo huku raia wakiwa ndio waliolengwa zaidi.

Utafiti unaoendelea wa Shirika la Human Rights Watch na taarifa za vyombo vya habari umeashiria kwamba wanajeshi waliwaua maalfu ya raia, wakateketeza mitaa na vijiji ambapo watu waliokuwa wametoroka walikuwa wakiishi katika eneo la El Geneina. Uporaji ulifanywa kwa fujo kote kote, vilevile kuwabaka wanawake na wasichana. Mavamizi haya yaliwaondoa makwao kwa lazima mamia ya maalfu ya raia, na kuwafanya maalfu waanze kutafuta makao katika eneo la Ardamata. Ardamata kwa sasa ni makao ya jeshi la Sudan na kambi za makundi ya wakimbizi wa ndani.

Manusura na waangalizi wa eneo walisema tarehe 1 mwezi Novemba kwamba mapigano yalizuka tena baina ya jeshi la Rapid Support na jeshi la Sudan. Katika siku mbili za mapigano makali yaliyozuka, pande mbili za majeshi yaliyokuwa yakipigana zililipulia mabomu mitaa ya watu, ambapo katika baadhi ya mashambulizi raia waliathirika. Wakazi walisema baadhi ya wapiganaji wa jamii ya Massalit walijiunga na vita hivyo katika upande wa jeshi ya Sudan. Kuanzia tarehe 4 mwezi Novemba baada ya jeshi la Rapid Support na makundi ya wanamgambo yanayoyaunga mkono kuteka ngome ya jeshi la  Sudan, yaliingia kwa fujo katika kambi ya wakimbizi na maeneo mengine ya makazi, yote yakiwa yaliyokaliwa na watu wa jamii ya Massalit na jamii zingine za watu wasiokuwa wa asili ya Kiarabu.

Manusura walisema jeshi la Rapid Support na washirika wao yaliwafyatulia risasi raia waliokuwa wakitoroka na kuwaua watu waliokuwa manyumbani mwao, au katika Makazi yao na hata pia kwenye barabara za eneo hilo. Manusura walisema washambuliaji waliwatusi watu wa jamii ya Massalit, hapa na pale wakisema walitaka “kuwaua wa-Massalit.” Washambuliaji waliwalenga zaidi wanaume wa jamii ya Massalit, hata hivyo watu wawili waliohojiwa walisema hata watu kutoka wengine wa jamii zisizo za Kiarabu, na hasa jamii za Tama na Eringa, pia waliuawa huku wengine wakijeruhiwa.

Tarehe 7 mwezi Novemba, mkulima wa umri wa miaka 45 wa jamii ya Massalit alisema wanamgambo wa Kiarabu, wakiwa kwenye magari ya majeshi ya Rapid Support waliingia kwenye nyumba ambayo alikuwamo katika kambi ya Ardamata. Wavamizi waliwaleta watu saba mbele ya nyumba:

“Wavamizi waliniambia nitoke nje,” alisema mwanamume yule. “Nilipotoka nje, mmoja wa watu wawili wa Kiarabu aliwafyatulia risasi watu hao saba kwa karibu. Halafu kwa haraka wakawaua wote. Wote wakawa wamelala pale. Mmoja wa wavamizi akaniambia: ‘Hebu tizama namna tulivyowaua wengi?’ Halafu wakaniambia niondoke pale mjini.”

Namna ilivyokuwa wakati wa msururu wa vurugu katika eneo la El Geneina miezi mitano tu iliyopita, majeshi ya Rapid Support na washirika wao waliwalenga watu mashuhuri wa jamii ya Massalit. Miongoni mwao alikuwamo kiongozi wa kijamii, mzee wa umri wa miaka 85 kutoka mji wa Misterei ambaye aliripotiwa kuuawa pamoja na mwanaye na wajukuu wake saba tarehe nne mwezi Novemba.

Kundi kubwa la wanaume lalazimishwa kukimbia kuelekea uwanja wa ndege wa El Geneina, Mashariki ya Ardamata. © 2023 Private.

Picha za video na picha za kawaida ambazo zilisambazwa kwenye mitandao ya jamii mapema mwezi Novemba, ambazo zimethibitishwa na kukaguliwa na Shirika la Human Rights Watch zilionyesha majeshi ya Rapid Support yakishirikiana na wanamgambo wa Kiarabu waliwaweka kizuizini, zaidi ya watu 200 wanaume kwa wavulana katika maeneo matatu ya Ardamata.

Msururu wa picha 5 za video ambazo zilitundikwa kwenye Telegramu na mtandao wa Facebook kati ya tarehe 4 mwezi Novemba na tarehe 5 pia zinaonyesha kundi la takriban watu 125 wanaume kwa wavulana wakilazimishwa kukimbia kuelekea uwanja wa ndege wa El Geneina, Mashariki mwa Ardamata. Wanaume kadhaa wanaonekana wakiwa wamejeruhiwa, ambao wamo wanaoonekana wakichechemea upande, huku watu wanne wakionekana wakimbeba mtu mmoja. Shirika la Human Rights Watch halikuweza kubaini kilichowatendekea watu hao baadaye.

Wavamizi walipora vifaa kwenye nyumba, wakawa waibia watu kwa mabavu wakiwa wanatoroka, wakawapiga, huku wakiwatumikisha na kuwatesa. Ishara za kupora na kuharibu kwa kuteketeza zipo kupitia picha za satellite zilizonaswa katika kambi ya Ardamata kuanzia tarehe 5 mwezi Novemba hadi tarehe 7, huku moto ukionekana katika maeneo ya maziko ya kambi ile.

Picha za Satelaiti za Tarehe 7 Novemba zikionyesha kuwashwa moto ulioteketeza vitu katika kambi ya Ardamata. Image © 2023 Planet Labs PBC. Analysis and graphics. © 2023 Human Rights Watch.

Picha za video zilizoandikwa tarehe 4 mwezi Novemba kutoka kwenye ukurasa rasmi wa mtandao wa X (awali ukijulikana kama Twitter) wa majeshi ya Rapid Support uliokadiria na kunaswa na Shirika la Human Rights Watch unaonyesha Abdel Raheem Hamdan Dagalo, naibu kamanda wa majeshi ya Rapid Support ambaye pia ni ndugu ya kiongozi wa majeshi ya Rapid Support Mohamed Hamdan Dagalo “Hemedti,” akiwa eneo la Ardamata akisherehekea pamoja na majeshi yake, kutekwa kwa kambi ya majeshi ya Sudan, pamoja na Jenerali Abdel Rahman Joma’a, kamanda wa majeshi ya Rapid Support Darfur Magharibi. Kufuatia utekaji wa kambi ile, Abdel Raheem alitangaza kwamba Joma’a alikuwa ameteuliwa kuwa kamanda wa kikosi cha 15 cha jeshi hilo.

Nakala ya picha ya video ikionyesha Abdel Raheem Hamdan Dagalo (katikati kushoto) na Jenerali Abdel Rahman Joma’a (katikati kulia) wakisherehekea ufanisi wa jeshi la Rapid Support kuteka kambi ya jeshi la Sudan katika eneo la Ardamata.   © RSF Sudan on X (formerly known as Twitter)

Chini ya sheria za kimataifa, kuwavamia raia maksudi, ikiwemo kuwaua watu bila kufuata kanuni za sheria, kuwanyanyasa raia na watu wote ambao sio wahusika kwenye mapigano kama vile watu walio kizuizini na wale waliojeruhiwa; na kuwafukuza watu makwao kwa kutumia nguvu, kukiuka sharia zinazoongoza namna ya kufanya vita, na mhusika anaweza kuchukuliwa hatua kwa kuhusika makosa ya kivita. Kuhusika mauaji, ubakaji, kutesa watu, kuwafukuza watu, kudhulumu, na makosa mengine yaliyofanywa yakiwa sehemu ya mavamizi dhidi ya raia kufungamana na maagizo ya serikali au sera iliyotangazwa na kundi fulani zinatajwa chini ya sheria za kimataifa kuwa makosa dhidi ya binadamu na ubinadamu.

Tarehe 16 mwezi Novemba, Sudan iliomba umoja wa mataifa kuondoa ujumbe wake nchini humo na hivyo kazi zake kwenye maswala ya kisiasa ya nchi hiyo. Siku iliyofwata Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa aliteuwa mjumbe maalum na kumtuma Sudan na hivyo kupunguza uwezo wa Umoja wa Mataifa kufuatilia yaliyokuwa yakiendelea nchini Sudan na hasa mzozo uliokuwepo. Baraza la Usalama la Umoja wa mataifa na washirika wengine wanapaswa kushughulikia njia zote zilizopo kuzuia maangamizi yanayoendelea na hivyo kuwalinda raia. Ikiwa hatua ya kwanza, wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wanafaa kuandaa ziara ya kutembelea mashariki ya Chad kukutana na manusura  wa madhila ambayo yamekuwa yakiendelea katika eneo la Darfur, Shirika la Human Rights Watch limesema.

Mbali na hayo, mataifa wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na nchi nyingine zinazotatizwa na mzozo wa Sudan, zafaa kutangaza vikwazo dhidi ya yeyote anayevuruga marufuku ya Umoja wa Mataifa ya silaha dhidi ya Darfur, iliyotolewa mwaka  2004 kwamba yeyote asiuze silaha eneo hilo. Baraza la Usalama linafaa kuongeza makali ya marufuku hiyo kote nchini Sudan, Shirika la Human Rights Watch limesema. Vilevile wanafaa kuunga mkono uchunguzi unaoendelea wa Mahakama ya Kimataifa kuhusu uhalifu (ICC) kwenye uhalifu wa kivita unaoendelea katika eneo la Darfur. Shughuli za taasisi huru ya Umoja wa Mataifa kuhusu Sudan, ikiwemo kufanya mashauri na mashirika haya ili kuelewa aina ya usaidizi ambao mataifa hayo yanaweza kuutoa ziungwe mkono.

Uingereza, Umoja wa Ulaya, Umoja wa Afrika, Shirika la maendeleo baina ya Mataifa (IGAD) na mataifa mengine yanayotatizwa na mzozo wa Sudan yanafaa kutangaza vikwazo mara moja dhidi ya Abdel Raheem na Abdel Rahman, makamanda wakuu wa jeshi la Rapid Support ambao imethibitika kwamba walikuwepo wakati wa mauaji yaliyotekelezwa katika eneo la Ardamata. Vikwazo pia vyafaa kuwekewa kiongozi wa jeshi la Rapid Support Hemedti, kwa makosa ya ukiukaji mbaya wa haki za watu uliofanywa na jeshi analoongoza.

“Washirika wa kimaeneo na kimataifa wamekuwa wakipuuza wito unaotolewa na manusura kwa miezi kadhaa kuhusu uwezekano wa kuibuka madhila zaidi katika eneo la Darfur Magharibi,” alisema Osman. “Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linafaa kuchukua hatua thabiti kushughulikia hali tete katika eneo hilo, litangaze vikwazo dhidi ya makamanda wakuu, lipiganie kuachiliwa kwa watu waliowekwa vizuizini, na kuunga mkono kuanzishwa kwa njia za kuhakikisha wakosaji wamewajibikia makosa yao.”

 

Kuendelea kwa Kiingereza, ikiwa ni pamoja na taarifa zaidi za kina.

………….....

Your tax deductible gift can help stop human rights violations and save lives around the world.

Region / Country