Skip to main content

Qatar: Hatua chache zimepigwa katika kuwalinda wafanyakazi wasio raia

Licha ya Michuano ya Kombe la Dunia la Soka kukaribia, serikali bado kutekeleza mageuzi makuu iliyoahidi

Wafanyakazi wasio raia huchangia asilimia 95 ya wafanyakazi wote wa nchini Qatar. Ndio wafanyakazi wanaojenga muundo msingi, hoteli, viwanja vya michezo, huku wakichangia pakubwa katika sekta ya huduma mbalimbali. © 2020 John Holmes for Human Rights Watch

(Beirut) - Juhudi za serikali ya Qatar  kulinda haki za wafanyakazi wasio raia katika kulipwa ujira wao ifaavyo na kwa wakati ufaao zimegonga mwamba, shirika la Human Rights Watch limesema leo kwenye ripoti iliyoandamana na kanda ya video.

Licha ya marekebisho machache kwenye sheria za kazi miaka ya hivi karibuni, visa vya waajiri kukatalia ujira ama kutoulipa kabisa, huku wakifanya dhuluma nyingine za malipo, vimeendelea kuwepo na kuenea miongoni mwa jumla ya kampuni na waajiri 60 nchini Qatar.

Ripoti ya kurasa 85 “How Can We Work Without Wages: Salary Abuses Facing Migrant Workers Ahead of Qatar’s FIFA World Cup 2022” “Tutafanyaje kazi bila ujira”: Dhuluma kwenye malipo ya wafanyakazi wasio raia msimu wa kabla ya Kombe la Dunia la Soka FIFA 2022inaonyesha kwamba waajiri kote Qatar mara kwa mara wanakiuka haki za wafanyakazi za malipo.

Kwamba Qatar imeshindwa kutimiza ahadi yake ya 2017 kwa Shirika la Kazi Duniani (ILO) ya kuwalinda wafanyakazi wasio raia dhidi ya dhuluma za malipo huku ikikomesha mfumo wa kafala ambao unawapokonya wafanyakazi hao hati zao za visa na kuwapa waajiri.

Shirika la Human Rights Watch limebaini kwamba visa baada ya visa vya dhuluma za malipo vipo katika aina zote za kazi zikiwemo ubawabu, uyaya na usaidizi, walinzi, wasafishaji, mameneja na wafanyakazi wa ujenzi.  

“Miaka kumi tangu Qatar ijishindie nafasi ya kuwa mwenyeji wa Michuano ya Kombe la Dunia la Soka, FIFA 2022, wafanyakazi wasio raia wangali wanaathirika kwa kucheleweshwa kwa malipo, mishahara kutolipwa kabisa, au hata mishahara kukatwa,” asema Michael Page, naibu mkurugenzi wa Human Rights Watch eneo la Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini.

“Tumepata habari za wafanyakazi kukosa chakula kwa sababu ya malipo yao kucheleweshwa, wafanyakazi kukumbwa na madeni, kulipwa mishahara midogo na vilevile kuna wale ambao wamejipata katika mazingira magumu ya kazi lakini wana uoga wa kulalamika wasije wakadhulumiwa zaidi.”

Shirika la Human Rights Watch limewahoji zaidi ya wafanyakazi 93 wasio raia katika kampuni zaidi ya 60. Shirika limesoma na kupitia stakabadhi za kisheria na ripoti kadhaa kabla ya kuandika ripoti hii.

Qatar imekuwa ikiwategemea wafanyazi milioni 2 wasio raia, idadi ambayo ni asilimia 95 ya wafanyakazi wake wote. Idadi kubwa ya wafanyakazi hao ni ya wale wanaojenga na kutoa huduma nyingine kwenye viwanja vya michezo, shughuli za uchukuzi - usafirishaji, hotelini, na kazi ya kujenga miundo misingi kwa maandalizi ya Kombe la Dunia la Soka - FIFA 2022 Qatar.

Wakienda Qatar, huwa na ndoto ya kupata kazi nzuri zenye mishahara inayowatosheleza, lakini hujipata kwenye dhuluma za malipo hali inayowaweka kwenye madeni. Hata hivyo hawawezi kuziacha kazi hizo kwa sababu ya kukosa namna huku wakikosa mahala pa kupeleka malalamiko na yasikizwe.

Wafanyakazi hamsini na tisa walisema kwamba malipo yao yamecheleweshwa, yameshikwa au kutolipwa; Wafanyakazi 9 walisema hawajalipwa kwa sababu waajiri waliwaambia kwamba hawana wateja wa kutosha; 55 wakasema hawajalipwa kwa kazi ya ziada licha ya kuwa walifanya kazi zaidi ya saa nane, wengi walifanya zaidi ya saa 10 kwa siku; na wafanyakazi 13 walisema waajiri walibadilisha mikataba yao ya kuajiriwa wakaandaa mikataba tofauti ambayo inawapendelea wao wenyewe. Wafanyakazi 20 walisema hawakupokea mafao ya kumaliza vipindi vyao vya kuhudumu; huku 12 wakisema waajiri walikata malipo yao bila kuwafahamisha.

Dhuluma za malipo zimeongezeka tangu kuanza kwa maradhi ya virusi vya Corona - Covid-19. Baadhi ya waajiri walitumia janga la Corona kuwa sababu ya kukatalia ujira au kukataa kuwalipa wafanyakazi wanaokamatwa na kurejeshwa kwao kwa nguvu. Baadhi ya wafanyakazi walisema hata hawawezi kununua chakula. Wengine wakasema walilazimika kukopa pesa ili waweze angalau kuishi.

Mtu mmoja wa umri wa miaka 38,meneja wa maswala ya wafanyakazi katika kampuni ya ujenzi - Qatar, yenye zabuni ya kujenga sehemu za nje za uwanja wa michuano hiyo ya Kombe la Dunia la Soka Qatar 2022, alisema mshahara wake umecheleweshwa kwa miezi minne karibu mara tano katika kipindi cha mwaka 2018 na 2019.

“Nimeathirika kwa sababu kucheleweshwa kwa mshahara kumetatiza malipo yangu ya deni la kadi za benki (credit card), kodi ya nyumba, na karo ya watoto,”  akasema. “Hata sasa mshahara wangu umechelewa kwa miezi miwili.… Ndio hali ya watumishi wote wa daraja langu na hata wafanyakazi. Ninawasikitikia wafanyakazi wa ngazi ya chini hasa nikifikiria namna wanavyojikimu katika mazingira kama haya – wao hawawezi kuchukua mikopo kwenye benki kama mimi”

Shirika la Human Rights Watch limebaini kwamba mfumo wa kafala ulikuwa sehemu ya vichocheo vya dhuluma. Mwaka 2017, Qatar iliahidi kukomesha mfumo huo wa kafala, na licha ya kuanzisha hatua kadhaa za kuubadilisha, mfumo huo ungali unawapa waajiri nguvu za kupita kiasi kuwadhibiti wafanyakazi wasio raia.

Dhuluma za malipo pia zinachochewa na njia za ujanja za kuwaajiri wafanyakazi nchini Qatar na katika nchi ambazo shughuli za kuwaajiri watu wa kuelekea Qatar zinafanyika. Mtu huhitajika kulipa ada ya dola kati ya 700- 2600 kusajiliwa kwa kazi nchini Qatar. Wakifika Qatar tayari wana deni la kulipa na hali wanapata kazi za ujira hata si za mshahara ulioahidiwa wakisajiliwa.

Shirika la Human Rights Watch limebaini kwamba watu 72 kati ya wafanyakazi waliohojiwa walichukua mikopo ili kulipa ada ya usajili. Kanuni za kikazi, kwa mfano ile iitwayo “pay when paid” “lipa ukishalipwa” inachangia katika kuongeza makali kwenye dhuluma za malipo. Kanuni hizi huwaruhusu wenye zabuni (waajiri) ambao hawajalipwa kuchelewesha malipo ya wafanyakazi.

“Tangu Agosti 2019, nimekuwa nikisubiri pesa,” alisema injinia wa umri wa miaka 34 aliyewasilisha kesi katika mahakama ya Kazi kudai malipo yaliyochelewa kwa zaidi ya miezi 7. Mtu huyo amelazimika kukopa pesa kutoka kwa marafiki nchini humo ili aitumie familia yake Nepal. Alikwenda mahakamani mara ya kwanza mwaka mmoja uliopita na angali anasubiri malipo yake: “Nipo katika hali mbaya kwa sasa maana nakosa pesa hata za chakula. Nitawezaje kulipia mikopo yangu iwapo silipwi mshahara [kwa njia za kisheria]?  Nafikiria kila mara kujiua ndio njia pekee.”

Dhuluma za malipo ndizo aina ya ukiukaji mkubwa wa haki za wafanyakazi wasio raia zinazofanywa kwa wingi sana nchini Qatar na eneo la ghuba ambapo mfumo wa kafala upo. Ili kupata suluhu ya swala hili serikali ya Qatar ilianzisha mipango iitwayo Mfumo wa Kulinda Malipo (Wage Protection System-WPS) mwaka 2015, Kamati za kutatua Mizozo ya Kazi (Labour Dispute Resolution Committees) mwaka 2017, na Hazina ya Bima ya Wafanyakazi (Workers’ Support and Insurance Fund) mwaka 2018.

Lakini shirika la Human Rights Watch limebaini kwamba mfumo wa Kulinda Malipo - WPS ni njia ya kufwatilia na kuangalia ujira na mishahara. Mfumo huo una mapungufu kadhaa kwenye utaratibu wake wa kufanya uchunguzi. Waajiri mara kwa mara huwapokonya wafanyakazi kadi zao za ATM. Kadi hizo zafaa kuwawezesha wafanyakazi kuchukua pesa zao za malipo kwenye benki. Vilevile, wafanyakazi kupeleka kesi zao mbele ya kamati za usuluhishi ni kazi ngumu yenye gharama za kifedha na huchukua muda mwingi. Ni shughuli isiyo na manufaa, huku wafanyakazi wakiogopa kulengwa na waajiri wao punde wakiwashtaki. Nayo hazina ya bima ya wafanyakazi inayofaa kuhakikisha wafanyakazi wanapata malipo wakati ambapo waajiri na kampuni hazijalipa mishahara, imeanza kuhudumu mapema mwaka huu.

Mwezi Oktoba 2019, serikali ilitangaza mageuzi ambayo yangetoa kiwango cha chini zaidi cha ujira au malipo kwa wafanyakazi wasio raia nchini Qatar na hivyo kuwaruhusu wafanyakazi kutafuta kazi nyingine au kuacha kazi bila idhini ya mwajiri. Licha ya hatua hiyo, baado kuna mbinu ambazo waajiri wanaweza kutumia kuwadhibiti wafanyakazi kwa njia wanayotaka na inaelekea zitasalia kuwepo kwenye mfumo huo. Mageuzi hayo yalifaa kuanza kutekelezwa mwezi Januari 2020.

Shirika la Human Rights Watch liliitumia wizara ya wafanyakazi nchini Qatar maswali kadhaa na mambo mengine ambayo lilikuwa limeyapata. Vilevile shirika liliitumia wizara ya maswala ya ndani, na shirika la soka la Kimataifa FIFA, na kamati kuu ya utekelezaji wa Michuano hiyo nchini Qatar . Tulipata majibu kutoka kwa kamati kuu, afisi ya mawasiliano ya Qatar (GCO) na shirika la FIFA.

Katika kujibu swali letu, shirika la FIFA kwa njia ya barua lilisema ‘FIFA na mshirika wake Kamati kuu ya Utekelezaji wa Michuano hii  (SC), zina sera thabiti zinazokataza ubaguzi wa namna yoyote na dhuluma za malipo. Kupitia juhudi zetu za kulinda haki za wafanyakazi kwenye miradi mingi ya maandalizi ya michuano ya Kombe la Dunia nchini Qatar, FIFA na mshirika wake Kamati kuu (SC), inafahamu umuhimu wa kuwepo njia za kulinda ujira wa wafanyakazi nchini Qatar. Hii ndio maana FIFA na washirika wengine kwenye maandalizi ya michuano ya Kombe la Dunia imeweka mifumo ya kukomesha dhuluma za malipo kwenye miradi ya maeneo yatakayotumiwa kwa michuano ya Kombe la Dunia. Vilevile FIFA imeandaa njia za kuwaruhusu wafanyakazi kutoa malalamiko yao ili kampuni zikishindwa kudumisha viwango vyetu basi swala hilo litashughulikiwa na kutatuliwa.

Shirika la FIFA limewaomba wafanyakazi na mashirika yasiyo ya serikali yawe yakitoa habari kuhusu yanayofanyika kwenye miradi ya Kombe la Dunia kupitia nambari maalum ya simu ya kamati kuu ya maswala ya wafanyakazi

“Imesalia miaka miwili kwa michuano ya Kombe la Dunia la Soka la FIFA kuanza nchini Qatar,” asema Page. “Muda unakwenda huku siku zikisonga kwa hivyo Qatar inafaa kuonyesha kwamba itatimiza ahadi yake ya kukomesha mfumo wa kafala, iboreshe njia zake za kufwatilia na kuchunguza malipo ya wafanyakazi, itunge njia za kupokea na kusuluhisha malalamiko, na kujipatia mifumo ya kukomesha dhuluma kwenye malipo ya wafanyakazi.”

Your tax deductible gift can help stop human rights violations and save lives around the world.

Region / Country