Skip to main content

Afrika Mashariki na Upembe wa Afrika: Mahangaiko ya Raia katika Migogoro ya Kivita

Ukandamizaji wa Upinzani, Uhuru wa raia; Kutowajibikia Unyanyasaji

Wakimbizi wanasafirishwa kwa malori kutoka Joda, mpakani mwa Sudan, hadi Renk, Sudan Kusini. © 2024 Sipa kupitia Picha za AP.

(Nairobi) – Raia wa Afrika Mashariki na Upembe wa Afrika walikumbwa na athari mbaya za migogoro ya kivita kati ya majeshi ya serikali na vikundi vya waasi vya upinzani mwaka 2024, Shirika la Human Rights Watch limesema leo katika Ripoti yake ya World Report 2025. (Ripoti ya Dunia ya mwaka 2025). Katika eneo lote, mamlaka zimekuwa zikiwadhulumu na kuwanyanyasa wanaharakati na wakosoaji wa serikali, na kuukandamiza upinzani.

Katika ripoti hiyo ya dunia yenye kurasa 546, katika toleo lake la 35, Shirika la Human Rights Watch lilikagua shughuli za haki za binadamu katika zaidi ya nchi 100. Katika maeneo mengi duniani, Mkurugenzi Mtendaji Tirana Hassan anaandika katika insha yake ya utangulizi kwamba serikali zimekuwa zikikandamiza maoni ya upinzani, kuwakamata na kuwaweka gerezani wapinzani wa kisiasa, wanaharakati, na waandishi wa habari bila sababu ya msingi. Vikundi vya silaha na majeshi ya serikali vimekuwa vikiua raia kinyume cha sheria, kuwafurusha kutoka makazi yao, na kuzuia misaada ya kibinadamu. Katika chaguzi zaidi ya 70 za kitaifa mwaka 2024, viongozi wa kiimla waliongezeka kwa kutumia sera na kauli za kibaguzi.

“Vikosi vya jeshi na vikundi vyenye silaha nchini Sudan na Ethiopia vimewalenga raia na miundombinu muhimu kwa makusudi bila kuadhibiwa kabisa,” alisema Mausi Segun, Mkurugenzi wa Afrika wa Human Rights Watch. “Mashirika ya kikanda na kimataifa yanapaswa kuchukua hatua madhubuti kwa haraka kusaidia kuwalinda raia na kuwachunguza zaidi wale wanaohusika na ukiukaji mkubwa.”

  • Ukatili wa pande zinazopigana nchini Sudan na Ethiopia ulisababisha mauaji na kujeruhi maelfu ya raia, huku watu milioni 12 wakilazimika kuyahama makazi yao nchini Sudan pekee, huku miundombinu muhimu ya raia ikiharibiwa au kuvurugwa. Vitendo vya pande zinazopigana kuzuia kwa makusudi kutolewa kwa misaada ya kibinadamu vilipelekea kuongezeka kwa njaa nchini Sudan. Vikosi vya serikali ya Ethiopia katika eneo la Amhara vilifanya mashambulizi makubwa dhidi ya wataalamu wa afya, wagonjwa, na vituo vya afya.
  • Nchini Kenya, mamlaka iliwateka nyara na kuyaua makumi ya waandamanaji waliopinga Mswada wa Fedha, na kutishia kufunga asasi za kiraia na mashirika ya wafadhili kwa madai ya kufadhili maandamano hayo.
  • Nchini Ethiopia, mamlaka ilisimamisha mashirika ya kutetea haki za binadamu na kuzidisha unyanyasaji, vitisho, na kukamatwa kwa waandishi wa habari, watetezi wa haki za binadamu na viongozi wa upinzani, vilevile kuwalazimisha watu wengi kwenda mafichoni.
  • Nchini Eritrea, serikali iliendelea kuwalazimisha raia wake kusajiliwa kwa nguvu kufanya kazi ya lazima bila kikomo na kuongezea ukandamizaji dhidi ya raia wake walioko nje ya nchi.
  • Serikali ya mpito ya Sudan Kusini iliahirisha uchaguzi na kushindwa kutekeleza mageuzi muhimu, na hivyo kuzidisha kutoadhibiwa kwa ukiukaji wa haki za binadamu.
  • Jamii zilizobaguliwa kihistoria zilikabiliwa na ukandamizaji mkubwa wa haki zao. Mahakama ya Kikatiba ya Uganda iliidhinisha Sheria ya kibaguzi ya Kupinga Uhusiano wa Jinsia Moja ya 2023. Nchini Tanzania, serikali ilihamisha kwa nguvu jamii asilia za Wamasai kutoka ardhi za mababu zao huko Ngorongoro.
  • Mamlaka nchini Tanzania iliwakamata kiholela mamia ya wafuasi wa upinzani, kuweka vikwazo kwenye mitandao ya kijamii, kupiga marufuku uhuru wa vyombo vya habari, vilevile kuhusishwa na utekaji nyara na mauaji ya kiholela ya wakosoaji wanane wa serikali kabla ya uchaguzi wa serikali za mitaa mwezi Novemba.

“Serikali za Upembe wa Afrika na Afrika Mashariki zimepuuza waziwazi wajibu wao wa kimataifa wa sheria kwa kukandamiza upinzani na haki nyingine za msingi,” Segun alisema. “Mashirika ya kikanda na serikali husika zinapaswa kuchukua hatua kali zaidi kushinikiza wale wanaohusika kukomesha sera na mienendo kandamizi.”

 

 

Your tax deductible gift can help stop human rights violations and save lives around the world.