(London) – Mamia ya maelfu ya watu wenye matatizo ya akili wamefungwa kwa minyororo katika maeneo mengi duniani, Shirika la Human Rights Watch limesema kwenye ripoti iliyotolewa leo.
Wanaume, wanawake na watoto wenye tatizo hilo baadhi wakiwa wa umri mdogo wa miaka 10 hufungwa kwa minyororo kwenye vyumba au mahala palipozingirwa, kwa wiki kadhaa, miezi au hata miaka. Hii ni hali inayoziathiri karibu nchi 60 barani Asia, Afrika, bara Ulaya, Mashariki ya kati na Amerika.
Ripoti hiyo yenye kurasa 56, “Kuishi kifungoni: Kuwafunga watu wenye matatizo ya akili duniani,” inaangazia namna familia huwafungia nyumbani watu wenye maradhi ya akili au kuwazuia kwa lazima kwenye makao machafu tena yenye msongamano wa watu huku wakiwa wamefungwa minyororo. Hii ni kutokana na unyanyapaa na sifa mbaya ambayo familia huipata katika jamii punde inapojulikana kwamba ina jamaa wa maradhi ya akili. Vilevile kuna ukosefu wa matibabu katika nchi nyingi. Waathiriwa wengi hulazimika kula, kulala, kwenda haja ndogo na kubwa pale walipofungiwa. Katika vituo vya serikali, vituo binafsi au vituo vya kijamii na kidini vya kuwatibu watu wenye matatizo ya akili, watu hao hulazimika kufanya mfungo wa kwenda bila chakula, kunywa dawa nyingine ikiwa ya kienyeji, huku wakipigwa au kudhulumiwa kimapenzi.
“Kuwafunga minyororo watu wenye matatizo ya akili hufanyika kote duniani miongoni mwa jamii nyingi wala sio siri,” asema Kriti Sharma, Mtafiti Mkuu wa Maswala ya Ulemavu katika shirika la Human Rights Watch ambaye pia ni Mwandishi wa ripoti hiyo. “Watu huishi miaka wakiwa wamefungiwa kwenye mti, katika kibanda maalum au katika zizi la kondoo kwa kuwa familia zao zinapambana na hali kama hiyo pekee yao huku serikali zikiwa zimeshindwa kutoa huduma kwa watu wenye maradhi ya akili.”
Huku baadhi ya nchi zikishughulikia maradhi ya akili kwa njia nyingi, fedheha ya kuwafunga minyororo watu wenye matatizo hayo ingali ipo katika jamii huku ikikosa kushughulikiwa. Bado hakuna takwimu zozote zilizotolewa kuhusu swala hilo au hata kampeni yoyote kimataifa na katika kanda za kukomesha mwenendo wa kuwafunga watu minyororo. Ili kulishughulikia swala hilo, shirika la Human Rights Watch limekuwa likishirikiana na watetezi wa watu wenye matatizo ya akili waliopitia hali hiyo na wanajua uchungu wa kufungwa minyororo. Vilevile shirika limeshirikiana na mashirika ya kupinga unyanyasaji duniani, ili kuanzisha kampeni ya #BreakTheChains ikiwa na nia ya kukomesha fedheha ya kuwafunga watu minyororo. Kampeni hii yafaa ianze kabla tarehe 10 Oktoba, Siku Kuu ya Kimataifa ya afya ya akili.
Shirika la Human Rights Watch limewahoji zaidi ya watu 350 wenye matatizo ya akili, wakiwemo watoto. Aidha watu 430 wa familia kadhaa, wafanyakazi wa vituo, wataalamu wa afya ya akili, waganga au matabibu wa tiba asili, maafisa wa serikali, na watetezi wa watu wenye ulemavu. Kwa kuzingatia utafiti uliofanywa katika nchi 110, shirika la Human Rights Watch lilipata ushahidi kwamba fedheha ya kuwafunga minyororo watu wenye matatizo ya akili hutendewa waathiriwa wa umri wowote, katika jamii zote, dini zote, bila kujali viwango tofauti vya kiuchumi iwe mashambani au mijini katika nchi 60 duniani.
Duniani angalau watu milioni 792, kwa wastani mtu mmoja kati ya kila watu 10, mtoto mmoja kati ya kila watoto 5, wana tatizo la akili. Licha ya hiyo serikali nyingi zinatumia asilimia 2 tu ya pesa zilizotengewa huduma za afya kwa sekta inayoshughulikia afya ya akili. Kwenye maswala ya bima ya afya ya kitaifa katika zaidi ya thuluthi mbili ya nchi, ni vigumu serikali kuwarejeshea watu pesa walizotumia kutibu maradhi ya akili. Hata kama utapata huduma za afya zikiwa za kutolewa bila malipo au zinatolewa kwa ada za chini, watu wengi hukumbwa na tatizo la usafiri hivi kwamba hawawezi kufika mahala palipo na huduma hizo.
Katika mazingira ya ukosefu wa huduma za kufaa za kutibu matatizo ya akili familia nyingi hulazimika kuwafunga minyororo jamaa zao wenye maradhi hayo. Kufungwa huko kunatokana na wasiwasi kwamba huenda wagonjwa hao wakatoroka au wanaweza kujidhuru wao wenyewe au wawadhuru watu wengine.
Fedheha ya kuwafunga minyororo watu wenye matatizo ya akili kimsingi imeletwa na imani katika familia zinazofanya hivyo kwamba maradhi ya akili yanatokana na mapepo au humpata mtu kwa sababu amefanya dhambi. Mara nyingi kukiwa na tatizo hilo katika familia, watu huwakimbilia wahubiri, waganga au matabibu wa tiba asili na hivyo kuanza kutafuta huduma za kisasa za matibabu wakiwa wamechelewa. Mtu kwa jina Mura, wa umri wa miaka 56 raia wa Bali, Indonesia, alipelekwa kwa wahubiri 103. Alipokosa kupona wakamfungia ndani ya chumba kwa minyororo kwa miaka kadhaa.
Katika nchi nyingi , familia huwapeleka jamaa zao wenye matatizo hayo, wakiwemo watoto wadogo wa miaka 10, kwa wahubiri au waganga au taasisi kama hizo. Huko wao hufungwa kwa minyororo ili wasitoroke. Watu hao huishi katika mazingira duni yasiyomfaa mwanadamu. Hulazimishwa kumeza dawa au hufanyiwa namna nyingi za tiba ikiwemo kunywa mchanganyiko wa dawa asili zinazodaiwa kuwa za miujiza, hulazimishwa kufanya mfungo wa kutokula kutimiza imani fulani, waganga huwapondaponda misuli, huwakariria maandiko ya Kurani kwenye masikio yao, na pia kuwalazimisha kuimba nyimbo za dini na vilevile kuoga kwa njia maalum.
Kuwafunga watu minyororo huathiri akili na afya ya kimwili. Mtu aliyefungwa hupata msongo wa mawazo hasa baada ya kuachiliwa, utapia mlo, maradhi ya kuambukizwa, mishipa ya mwilini kutatizika, misuli kuathirika, na vilevile matatizo ya moyo. Kuwafunga watu minyororo pia huwalazimisha waishi katika mazingira yanayoathiri uwezo wao wa kutembea na hata kusimama. Vipo visa ambapo mtu hufungwa kwa mtu mwingine, watu wawili kufungwa pamoja na hivyo wanalazimika kulala pamoja na kwenda haja pamoja.
Mtu mmoja nchini Kenya aliyefungwa minyororo alisema, “Hii sio sawa, mwanadamu hakuumbwa kuishi hivi. Mwanadamu anafaa kuwa huru.”
“Kwenye taasisi hizi, viwango vya usafi ni duni kwa sababu watu hawaruhusiwi kuoga au kubadilisha nguo. Vilevile wanaishi kwa kutengwa hivi kwamba wako umbali wa mita mbili kutoka kwa wenzao,” Asema Sharma. “Heshima za kibinadamu hazipo.”
Kutokana na kukosa usafi, kukosa sabuni, au hata huduma za afya za kimsingi, watu waliofungwa kwa minyororo wamo katika hatari ya kukumbwa na homa ya Korona (Covid-19). Na katika nchi ambapo janga la Korona (Covid-19) limevuruga huduma za matibabu ya akili, watu wanaoathirika kwa maradhi ya akili wamo katika hatari ya kufungwa kwa minyororo.
Serikali kadhaa zafaa kuchukua hatua za haraka kupiga marufuku mwenendo wa kuwafunga watu kwa minyororo, zipunguze unyanyapaa, na kuanzisha huduma zifaazo za kutibu maradhi ya akili. Huduma zifaazo ni zile ambazo waathiriwa wanaweza kuzifikia kwa gharama wanayoimudu. Serikali zinafaa kuagiza shughuli za ukaguzi na ufuatiliaji katika taasisi za serikali zinazotoa huduma za matibabu kwa maradhi ya akili. Vilevile zinafaa kufanya hivyo kwa taasisi binafsi ili zichukue hatua dhidi ya taasisi zenye dhuluma ndani mle, shirika la Human Rights Watch limesema.
“Ni jambo la kusikitisha kwamba mamia ya maelfu ya watu kote duniani wanaishi wakiwa wamefungwa kwa minyororo, wakiwa wametengwa, wanadhulumiwa, wakiwa pweke,” Asema Sharma. “Serikali zinafaa kukoma kupuuza tatizo hili na badala yake zichukue hatua zifaazo sasa.”
Anwani za ziada:
“Nimefungwa mnyororo kwa miaka mitano. Mnyororo ni mzito. Hii si haki; inanipa huzuni tele. Ninaishi kwenye chumba kimoja na wanaume saba. Siruhusiwi kuvaa nguo, nina chupi tu. Nanywa uji asubuhi na nikibahatika nitapata mkate jioni, lakini sio kila jioni.”
—Paul, jamaa mwenye maradhi ya akili, Kisumu , Kenya, Februari 2020
“Kuwafunga minyororo watu wenye maradhi ya akili kwafaa kukoma- lazima kukome.”
—Tina Mensah, naibu waziri wa afya Ghana, Accra, Novemba 8, 2019
“Nina huzuni, nimefungiwa kwenye seli hii. Ninataka kuangalia nje, niende kazini, nipande mpunga kwenye mashamba. Tafadhali fungua mlango. Tafadhali fungua mlango. Usiufunge kwa kufuli.”
—Made, jamaa wa maradhi ya akili aliyefungiwa katika seli maalum aliyojengewa miaka miwili iliyopita kwenye shamba la babake, Bali, Indonesia, Novemba 2019
“Niliingiwa na woga kwamba mtu angenivamia usiku, siwezi kujitetea kwa sababu nimefungwa kwa mnyororo.”
—Felipe, jamaa wa tatizo la akili ambaye alifungwa kwa mnyororo na kufuli, akiwa uchi katika hospitali ya maradhi ya akili mjini Puebla, Mexico, 2018
“Ninakwenda haja kubwa kwenye mifuko ya plastiki, na huwa inaondolewa usiku. Nilioga mara ya mwisho siku mbili zilizopita. Hapa ninakula mara moja kwa siku. Sina uhuru wa kutembea popote. Usiku ninalala ndani ya nyumba. Ninaishi mahala tofauti na pale wanaume wapo. Ninaichukia minyororo hii.”
—Mudinat, mwanamke wa ulemavu wa akili aliyefungwa katika kanisa moja, Abeokuta, Nigeria, Septemba 2019
“Utotoni, nilimwona shangazi yangu akiwa amefungiwa kwenye kibanda cha mbao na nilikatazwa kwenda kumwona au kumkaribia. Familia yangu iliamini kwamba tatizo lake la akili litaipatia sifa mbaya familia nzima. Daima nilitaka kumsaidia shangazi yangu lakini singeweza. Ilinivunja moyo sana.”
—Ying (sio jina lake haswa), mwanamke aliyekuzwa katika mkoa wa Goungdong, Uchina, Novemba 2019
“Majirani wanasema eti mimi ni mwendawazimu [maluca or n’lhanyi]. Nilipelekwa katika kituo cha tiba asili ambapo walikata mikono yangu ili kuweka dawa halafu nikapelekwa kwingine ambako mganga aliagiza nioge kwa damu ya kuku.”
—Fiera, 42, mwanamke mwenye ulemavu wa akili, Maputo, Msumbiji, Novemba 2019
“Inahuzunisha kwamba binamu zangu wawili wenye matatizo ya akili wamefungiwa pamoja kwenye chumba kimoja kwa miaka mingi. Shangazi yangu amejaribu kwa uwezo wake wote kuwasaidia kwa njia nyingi lakini anasumbuka kwa unyanyapaa unaomwandama, watu wanamchukulia vibaya. Nchi ya Oman haina huduma za matibabu kwa matatizo ya akili. Ni vyema kwa serikali kusaidia kwa namna ili familia zilizoathirika zisisumbuke sana.”
—Ridha, jamaa wa familia yenye jamaa waliofungwa minyororo nchini Oman, Septemba 2020
“Nilifungwa kwa minyororo, nikapigwa, na nikapewa dawa na vifaa vingine vinavyoaminika kufukuza shetani. Wanaamini kwamba umekumbwa na pepo kwa hivyo wanamwaga puani dawa ya kumfukuza.”
—Benjamin, 40, jamaa mtetezi wa waathiriwa wa matatizo ya akili ambaye aliwahi kufungwa minyororo katika kanisa la Monteserrado, Liberia, Februari 2020
“Familia huwafunga [watu wenye matatizo ya akili] kila mara. Waweza kujua mtu alifungwa kwa sababu ya alama kwenye mwili wake. Wana makovu mengi.”
—Afisa kutoka afisi ya mwendesha mashtaka wa kutetea watu wenye ulemavu nchini Mexico.