Tarehe Moja Desemba, Rais wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan alitangaza kuanzishwa kwa kamati mbili ili kushughulikia mgogoro wa ardhi katika wilaya ya Ngorongoro kaskazini mwa Tanzania inayojulikana kwa uhifadhi wake wa wanyamapori. Kamati ya kwanza itachunguza malalamiko kutoka kwa wananchi; na ya pili itachunguza uhamisho wa “hiari” wa wakazi kutoka eneo la hifadhi la Ngorongoro kwenda kijiji cha Msomera Handeni katika mkoa wa Tanga, zaidi ya kilomita mia sita kutoka Ngorongoro. Serikali ilitangaza kuwa “uhifadhi” ulikuwa ndio msingi wa uhamisho wa wakazi hao.
Tangu mwaka 2022, kulingana na shirika la Human Rights Watch, serikali imefanya maisha kuwa magumu zaidi kwa wenyeji wafugaji laki moja (100,000) wa kimaasai ambao wanaishi katika eneo hilo la uhifadhi kwa kupunguza huduma muhimu za umma, pamoja na shule na vituo vya afya. Hii imewalazimisha watu wengi kuhama. Askari wanyamapori wa Serikali pia waliwashambulia wakazi ambao walishindwa kuendana na utaratibu, kuwazuia kuingia ndani na kuzunguka eneo la hifadhi.
Rais alifungua uwanja wa uchunguzi huu mwezi Agosti alipoahidi kwamba huduma za elimu na za hospitali zitolewe kikamilifu, na vituo vya uchaguzi vianzishwe ili kuwawezesha wakazi kupiga kura katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwezi Novemba.
Tangu muda huo serikali imetenga pesa kwa ajili ya ujenzi wa bweni la shule katika eneo la uhifadhi na kuondoa gharama ya malipo ya magari kwa wakazi wa eneo hilo.
Hatua za Rais Samia mpaka sasa zina maana, lakini mengi yanahitajika kufanywa. Serikali inatakiwa isitishe mpango wake wa kuwahamisha watu kutoka kwenye hifadhi, kupiga marufuku uhamisho wa watu kinguvu, kushauriana na jamii ambazo zimeathirika. Ushauri huu uwe ni wa maana na uwajumuishe wanawake pia. Mamlaka nazo ni lazima ziwawajibishe kwa kupitia vyombo halali vya kinidhamu na vya kisheria, wahifadhi waangalizi pamoja na maafisa wakuu ambao wamewanyanyasa, wamepiga na hata kuwafanyia ukatili wakazi ambao ni lazima kwa haraka wapewe fidia.
Mwisho serikali inatakiwa kuheshimu haki za binadamu za jamii ya kimaasai kama jamii ya asili, na mifumo halali, mila na desturi ambazo imetumia katika kusimamia ardhi ya mababu zake kwa vizazi vingi.