(Nairobi) – Kuondolewa kwa nguvu kwa jamii za Kimaasai kulikofanywa na Serikali ya Tanzania kutoka maeneo ya kaskazini mwa Tanzania ambayo wameishi kwa muda mrefu ni uvunjaji wa haki zao za ardhi, riziki, na utamaduni, limesema shirika la Human Rights Watch leo. Tangu Juni 2022, mamlaka zimejihusisha kwenye vitendo vya ukatili na njia zilizo kinyume cha sheria, ikiwa ni pamoja na kuwapiga, kuwafyatulia risasi, unyanyasaji wa kingono, na ukamataji wa kiholela ili kuwafukuza wakazi kutoka katika ardhi yao.
Mnamo tarehe 6 Juni 2022 serikali ilitangaza kwamba itagawa/itatenga kilometa za mraba 1,500 za ardhi ya kijiji kama hifadhi ya wanyama pori, ili kuwazuia jamii za kimaasai ambao haswa ni wachungaji wa mifugo na wakazi wa tarafa ya Loliondo, wilaya ya Ngorongoro, kuishi kwenye ardhi hiyo, kutumia kwa malisho, au hata kuingia eneo hilo kuyatafuta maji kwa matumizi ya nyumbani na kilimo. Wanavijiji wa eneo hilo waliiambia Human Rights Watch kwamba hawakushauriwa vya kutosha kabla ya uamuzi huo, kama inavyotakiwa na sheria za Tanzania.
"Uhamishaji wa Wamaasai kutoka kwenye ardhi yao ya jadi umesababisha madhara makubwa na kuweka hatarini kuendelea kuwepo kwa utamaduni wao," alisema Oryem Nyeko, mtafiti wa Tanzania wa shirika la Human Rights Watch. "Serikali inapaswa kuacha kuinyakuwa ardhi ya Wamaasai na kutumia mtindo wa uhifadhi unaoheshimu haki za jamii zinazoathiriwa."
Kati ya Juni na Desemba 2022, Human Rights Watch iliwahoji watu 45, ikiwa ni pamoja na waathirika wa ukatili na vitisho kutoka kwa vikosi vya usalama vya serikali na askari wa uhifadhi. Unyanyasaji huu unaendana na udhalilishaji wa mara kwa mara dhidi ya Wamaasai katika eneo hilo. Tangu angalau mwaka 2009, serikali imehamisha kwa nguvu maelfu ya watu kutoka Loliondo ili kuweka maeneo kwa ajili ya uhifadhi, utalii na uwindaji wa nyara. Uchambuzi wa picha za satelaiti wa eneo hilo uliofanywa na Human Rights Watch uligundua kwamba mwezi Julai 2022, takriban maboma 90 na mazizi ya ng'ombe yaliyokuwa ndani ya eneo tengefu yalichomwa moto.
Tarehe 8 Juni 2022, siku mbili baada ya tangazo la serikali, makundi ya polisi, wanajeshi, na askari wa hifadhi walifika Loliondo kugawa eneo pendekezwa la hifadhi.
Kwa siku kadhaa, vikosi vya usalama vilikamata na kuwaweka kizuizini kiholela viongozi 10 wa jamii na kufyatua mabomu ya machozi na risasi za mpira kwa waandamanaji na wapita njia, huku wakiwajeruhi takribani watu 30 wakiwemo wanawake, watoto na wazee. Mashahidi walisema polisi walimchukua mtu mwenye umri wa miaka 84 kutoka nyumbani kwake na hajulikani alipo hadi leo. Vikosi vya usalama pia viliharibu mali za wakazi na kuuwa mifugo kwa kuwapiga risasi. Hadi wakati huo, takribani wakazi 2,000 kutoka vijiji mbalimbali ndani ya Loliondo walikimbia kwenda kutafuta hifadhi na matibabu nchi jirani ya Kenya.
Mamlaka zilimkamata pia mtetezi wa haki za binadamu na mwanajamii ambaye alisambaza picha na video za vurugu na athari zake kwenye mitandao ya kijamii.
Tangu wakati huo, vikosi vya usalama vimeendelea kutekeleza unyanyasaji dhidi ya wakazi wa Loliondo, na waathirika na mashahidi wametoa maelezo ya mambo mbalimbali waliyofanyiwa ikiwa ni pamoja na ubakaji na vitendo vingine vya unyanyasaji wa kingono, kuvamia nyumba wakati wa usiku na kufyatua risasi ndani ya nyumba. Wakazi walisema kwamba askari wa wanyama pori, ambao wanafanya kazi chini ya mamlaka ya Wizara ya Maliasili na Utalii, walichukua mifugo ambayo ilikuwa imevuka mpaka wa eneo la wanyama pori, huku mwanzoni wakiwatoza ada kubwa kuwakomboa na baadae kuwapiga mnada.
Serikali inadai kuwa kuzuia matumizi ya watu na mifugo yao katika eneo hilo ni muhimu kulinda "mfumo wa ekolojia wa eneo zima la Serengeti Kuu," eneo la kaskazini mwa Tanzania, na ilitangaza kuwa "inawekeza katika kuboresha ardhi ya malisho, masoko ya mifugo na bidhaa za uwekezaji, pamoja na utoaji wa maji safi ya kunywa kwa watu na mifugo." Mwezi Juni 2022, Wizara ya Maliasili na Utalii ilisema kwamba “hakuna makazi” katika eneo hilo na "kwa hivyo hakuna uhamishaji wa watu wa lazima."
Human Rights Watch iliandikia Wizara za Maliasili na Utalii, Mambo ya Ndani, Afya na Ustawi wa Jamii, na Jeshi la Polisi kuwapatia matokeo ya utafiti wake na kuomba taarifa lakini haijapokea majibu bado.
Hatua za serikali zimesababisha kuendelea kwa kuhamishwa, kuvurugika kwa mifumo ya msaada wa kijamii, na kudhoofisha mifumo ya ulinzi wa kijamii. Wanajamii waliiambia Human Rights Watch kwamba wakazi maskini, hasa wazee na kaya zinazoongozwa na wanawake, wameathirika sana. Mamia ya wakazi wamepoteza maeneo ya malisho, nyumba na mifugo, na wako na wanajamii ambao hawajarudi tena tangu walivyokimbilia Kenya.
Wataalam huru wa Umoja wa Mataifa na Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu, wametoa wito kwa Tanzania kusitisha kuhamisha watu kwa nguvu huko Loliondo. Mwezi Januari 2023, Tume ya Afrika ilitembelea wilaya ya Ngorongoro na kuelezea wasiwasi wao kuhusu ukosefu wa mashauriano ya kutosha na ushirikishwaji wa jamii za eneo husika katika zoezi la ugawaji ardhi na matumizi ya nguvu na vitisho dhidi ya wanajamii wanaopinga.
Mikataba ya kimataifa na ya Afrika kuhusu haki za binadamu inalinda haki za umiliki wa mali na ardhi za watu binafsi na za jamii, ikiwa ni pamoja na wale wenye hati za kijadi za umiliki wa ardhi. Kwa mujibu wa sheria za kimataifa na kikanda, hasa Itifaki ya Kimataifa ya Haki za Kiuchumi, Kijamii na Kitamaduni na Mkataba wa Afrika kuhusu Haki za Binadamu na Watu, uhamishaji watu kwa nguvu hauruhusiwi. Kabla ya kutekeleza kuhamishwa kisheria, serikali inapaswa kutafuta mbinu mbadala zinazowezekana ikishauriana na watu watakaoathirika, huku "ikiepuka au angalau kupunguza haja ya kutumia nguvu," Kamati ya Haki za Kiuchumi, Kijamii na Kitamaduni inasema, na serikali inapaswa kulipa fidia ya kutosha, ikiwa ni pamoja na kupatikana kwa ardhi mbadala.
"Serikali ya Tanzania inapaswa kuacha mara moja mbinu zake za unyanyasaji za kuwahamisha jamii za Wamaasai," Nyeko alisema. "Serikali inapaswa kuwapa malipo ya fidia ya haraka watu na jamii walioondolewa katika maeneo yao na, muendelezo uwe ni kuwashirikisha kwa dhati jamii zilizoathirika na kulinda haki zao za ardhi, vyanzo vya kipato, na utamaduni."
‘Eneo la Hifadhi la Wanyama Pori’ la Loliondo
Takriban watu 70,000 wa jamii ya kifugaji ya Kimaasai - ambao maisha yao yanategemea ufugaji wa mifugo kama vile ng'ombe, kondoo, na mbuzi, na kilimo cha mazao ya kujikimu, kwa kiasi kikubwa na wanaishi katika eneo la kaskazini mwa Tanzania la Loliondo. Loliondo inajumuisha eneo la 'Loliondo Game Control Area' (LGCA), lililowekwa rasmi mwaka 1951 na serikali ya kikoloni ya Uingereza. LGCA ina ukubwa wa kilomita za mraba 4,000, na kwa miaka mingi lilikuwa eneo lililotengwa kwa minajili ya uangalizi na uwindaji wa wanyama pori na pia kuwaruhusu watu kuishi na kulima hapo.
Kwa muda wa miaka 30, Tanzania imekuwa ikipanga kutenga kilomita za mraba 1,500 za eneo la LGCA ibaki tu kwa ajili ya uangalizi na uwindaji wa wanyama pori. Mwaka 1992, serikali iliidhinisha leseni za uwindaji katika LGCA, ambazo ziliongezwa muda wake mwaka 2009. Mwaka1993, serikali ilitengeneza mpango uliotenga eneo la kilomita za mraba 1,500 kwa ajili ya utalii, ikiwa ni pamoja na uangalizi na uwindaji wa wanyama pori, ambapo matumizi ya hizo sehemu na jamii za wenyeji yangesitishwa.
Mwezi wa Aprili 2013, serikali ilitangaza kuwa ingewaruhusu wakazi wa eneo la Loliondo “uhuru wa kutumia” kilomita za mraba 2,500 kati ya zile kilomita 4,000 za mraba za LGCA “kwa ajili ya maendeleo yao ya kijamii” na kubakiza kilomita za mraba 1,500 kwa ajili ya matumizi ya hifadhi ya wanyama pori pekee. Kwa mujibu wa mashirika yasiyo ya kiserikali ya eneo hilo, serikali iliwaondoa kwa nguvu wakazi wa eneo lililopangwa kwa ajili ya hifadhi ya wanyama pori mwaka 2015 na 2017.
Mwaka 2022, serikali ilipitisha Sheria mpya ya Uhifadhi wa Wanyama Pori, inayotukuza mtindo wa uhifadhi unaokataza jamii za eneo husika, kuingia na kulisha mifugo yao kwenye hifadhi za wanyama pori. Sheria ya Tanzania inatoa ulinzi wa kiasi fulani kwa wakazi waliopo katika ardhi ya kijiji yenye hati ya umiliki wa kijadi. Inatambua kuwa "jamii za jadi" zimekuwa zikitumia ardhi inayokaliwa pia na wanyama pori kwa muda mrefu, na imeweka mwongozo juu ya unyang’anywaji wa ardhi kwa lazima. Lakini serikali imepuuza au haikutekeleza kikamilifu masharti husika.
Tarehe 12 Januari 2022, John Mongella, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, aliwajulisha wenyeviti wa vijiji na madiwani katika tarafa ya Loliondo juu ya uamuzi rasmi wa serikali wa kutenga eneo la kilomita za mraba 1,500, na kuweka kizuizi kama alama inayozuia watu kuingia katika ardhi hiyo.
Tarehe 15 Februari 2022, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitoa taarifa kwa umma katika “mkutano wa wadau wa uhifadhi’ huko Wasso, tarafa ya Loliondo, kufuatia mapendekezo kutoka kwa kamati ya kudumu ya bunge juu ya rasilimali za asili na utalii kwamba mamlaka zishauriane na jamii. Nooloropil Moko, mkazi wa Loliondo ambaye alihudhuria, aliiambia Human Rights Watch kuwa Majaliwa alitambua kabila la Maasai kuwa jamii “nzuri kwa uhifadhi” na kuahidi kuwa serikali haitowachukulia ardhi yao.
Ghasia za kati ya Juni 8 hadi 13, 2022
Mnamo Juni 6, 2022 Mongella, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, baada ya mkutano wa faragha na maafisa wengine, alithibitisha tena nia ya serikali ya kubadilisha na kudhibiti eneo la kilomita za mraba 1,500 kama hifadhi ya wanyama pori. Wakazi wanasema hakushauriana na jamii, ikiwa ni pamoja na jambo la kuwahamishia makazi katika ardhi nyingine au fidia, isipokuwa kwenye mkutano uliofanyika mwaka uliopita.
Asubuhi ya tarehe 8 Juni, magari kadhaa yaliyokuwa yamewabeba maafisa wa polisi, wanajeshi, na askari wa wanyama pori kadhaa walifika katika vijiji vya Arash, Oloipiri, Ololosokwan, na Piyaya, katika wilaya ya Loliondo.
Tarehe 9 Juni, mamlaka walikamata na kuweka kizuizini viongozi 10 wa jamii ya Loliondo.
Wakazi walisema kwamba siku hiyo hiyo, walikusanyika kupeana taarifa na kujadili jinsi ya kujibu hatua ya utengwaji wa ardhi. Walisema mkutano ulikwisha ghafla baada ya maafisa wa polisi wa Kikosi Maalum cha Kutuliza Ghasia kilifika na kuhitaji kuzungumza na viongozi wa jamii, wakajaribu kuchukua simu ya mkononi kutoka kwa mkazi ambaye alikuwa anarekodi mkutano, na kuwaambia hawakuwa na idhini ya kukutana. Mwanamke mmoja ambaye alihudhuria mkutano huo alisema kwamba polisi hao waliwaambia, "maandamano hayaruhusiwi nchini hapa."
Usiku huo, maafisa wa usalama na askari wa wanyama pori waliweka alama za mipaka
wa eneo la hifadhi ya wanyama pori lililopendekezwa. Walipoondoka, wakazi wa Ololosokwan waliondoa baadhi ya alama hizo, wakipinga serikali kuliwekea uzio eneo hilo. Mkazi mmoja alisema kwamba wenye mamlaka walipogundua alama hizo zimeondolewa, walifanya mashambulio yasiyokuwa na mpangilio kwa kufyatua bunduki kiholela usiku kucha, kwa lengo la kuonyesha nguvu.
Wanajamii walidai kwamba mnamo saa 10 asubuhi tarehe 10 Juni, wanavijiji walikusanyika karibu na alama za mipaka kupinga kuzuiwa kwa eneo hilo na kutafuta majadiliano na vikosi vya usalama vya serikali. Wakazi walisema wanawake walikuwa mstari wa mbele wa maandamano kumaanisha dhamira ya jamii ya kuzungumza na sio kupigana na vikosi vya usalama.
Hata hivyo, mashuhuda walisema, maafisa wa usalama walijibu kwa ghasia. Walifyatua mabomu ya machozi na risasi za mpira bila kujali, wakakata watu na mapanga kwenye mikono yao na kuharibu mali za wakazi, pamoja na pikipiki. Takribani watu 30 walijeruhiwa, ikiwa ni pamoja na wanawake na watoto. Polisi waliripoti kuwa Garlius Mwita, ofisa wa polisi, aliuawa kwa mshale na waandamanaji.
Wanawake wengi waliripoti kuwa maafisa wa usalama waliwafyatulia risasi, ikiwa ni pamoja na watu ambao walikuwa wameinua mikono yao kuonyesha kwamba hawakuwa na nia ya kupigana. Mwanamke mmoja mzee alisema: "Tulikuwa tunawaambia [polisi] 'acheni kuweka alama za mipaka.' Walikuwa wanatuambia lazima waziweke. Kisha wakaanza kufyatua risasi na mabomu ya machozi. Walifyatulia risasi mguuni kwangu. Na risasi ikaruka na kugonga jicho langu la kushoto na mguu. "
Maofisa walifukuza wakazi, kuwachoma kwa mishale, kuwakata kwa mapanga na kuwapiga watu walipokimbia, mashuhuda walisema. Maafisa pia walishambulia wale ambao hawakuwa wanaandamana, ikiwa ni pamoja na watu waliokuwa wanahudhuria harusi.
Mwanamke mmoja alisema kuwa aliwaona maafisa waliovaa sare za kijeshi wakipiga watu waliokuwa wakienda sokoni, katika eneo lingine Loliondo, katika kijiji cha Oloipiri, ambacho kina sehemu katika eneo jipya lililotengwa. Alisema walikuwa wakiwaambia watu waondoke katika eneo hilo lililotengwa, na kuwafyatulia risasi wale waliokataa.
Maafisa wa usalama walifyatua risasi na mabomu ya machozi katika mkutano wa hadhara wa jamii huko Engong'u Niarowua, kijiji kidogo eneo la Ololosokwan, huku wakimpiga risasi mtu mmoja mguuni.
Mzee mmoja mwenye umri wa miaka 72 alisema kuwa maafisa wa usalama walimshambulia yeye na wazee wengine wawili nyumbani kwake Ololosokwan:
Tulikuwa tumeketi pamoja, tukitafuna tumbaku. Ghafla tukaona magari mawili ya polisi yamejaa maafisa, na wakasema, 'Piga magoti! Inua mikono yako!' Walianza kutupiga. ... Nilipigwa mwili mzima. Walinichoma kwa mshale upande wa kulia wa goti langu. Marafiki zangu walianguka na kupoteza fahamu. Baada ya muda, nilipoteza fahamu pia. Nilijikuta kwenye kliniki huko Kenya, nikiwa na maumivu mengi mwilini mwangu.
Pia huko Olosokwan, maafisa wa usalama walimpiga risasi Orais Oleng'iyo, mwanaume mzee
mwenye umri wa miaka 84 nyumbani kwake, kisha wakamvuta hadi kwenye gari la polisi na kuondoka naye. Shahidi alisema maafisa hao walimvunja miguu Oleng'iyo. Hadi kufikia Aprili 2023, bado haijulikani mahali alipo Oleng'iyo.
Wakazi walisema maafisa wa usalama pia waliwapiga risasi na kuwaua mifugo. Kwa mfano, katika kijiji cha Arash, mamlaka zilipiga risasi na kuua kondoo nane na ndama mmoja wa mwanamke mmoja.
Kukataliwa huduma za afya huko Loliondo; Kukimbilia Kenya
Wakazi na mashuhuda walisema vurugu zilisababisha takriban watu 2,000 kukimbia umbali wa hadi kilomita 40 kusini mwa Kenya kwa ajili ya usalama na matibabu.
Wakazi kadhaa wa Loliondo walisema walikwenda Kenya kwa sababu hawakuweza kupata Fomu ya Uchunguzi wa Afya wa Polisi wa Tanzania, maarufu kama Police Form No.3 (PF3), ambayo hospitali za umma na vituo vya afya vinasisitiza lazima itolewe kabla ya kutoa matibabu kwa waathirika wa unyanyasaji, hata kama maisha yao yamo hatarini, ingawa fomu hii haihitajiki kisheria.
Mwanamke kutoka kijiji cha Lopolun alisema kuwa wafanyakazi katika vituo vya matibabu huko Loliondo hawakutaka kumtibu ndugu yake ambaye alibakwa na polisi mnamo Juni 14 kwa sababu polisi walikataa kumpatia fomu ya PF3:
Hospitalini, tuliambiwa kwenda kuchukua fomu ya PF3. Tuliwaomba polisi atupatie hiyo PF3, lakini polisi walisema, "Hakuna mtu anayeweza kulishitaki jeshi lililotumwa na serikali kutoa usalama." Haikuwa inawezekana kupata msaada wa matibabu kwa mwanamke aliyebakwa. Tunahofia, labda atakuwa mgonjwa (wa magonjwa ya zinaa) au akapata mimba.
Anaamini kuwa polisi walikuwa na wasiwasi juu ya kuwajibika kisheria:
Bila shaka, polisi wanahofia kwamba tutaitumia kulishtaki jeshi. Tulizungumza juu ya kwenda kwa mkuu wa wilaya. Polisi walipotuambia kwamba wanajeshi hao walitumwa na rais, tulikosa mbadala.
Unyanyasaji wa kingono
Wakazi waliripoti kuwa maafisa wa usalama waliwabaka angalau wanawake watatu huko Loliondo. Mwanamke kutoka Lopolun alisema maafisa wa polisi walimbaka ndugu yake mnamo Juni 14, wakati dada yake huyo na wanawake wengine walipokwenda kuchota maji katika chanzo kilichopo kijiji cha Oltulelei.
Mwanamke kutoka kijiji cha Lopolun alisema kuwa muda mfupi baada ya Juni 13, maafisa wa usalama walilazimisha jirani yake na binti yake wa shule ya sekondari kuvua nguo zao na kufanya vitendo vya ngono, wakisema walikuja nyumbani kwake baadaye, wakionyesha wazi kuwa wametaharuki.
Mwanamke kutoka Loliondo alielezea ubakaji wa kikundi uliofanywa na polisi mwezi Agosti, wakati wanaume wa kijiji hawakuwepo: "Wanawake walipoona polisi, walianza kukimbia. Polisi waliwakimbiza. ... Walikuwa polisi watano na wanawake wawili ... watatu walimbaka mwanamke mmoja na wawili walimbaka yule mwingine."
Wanawake wengine wanne pia walielezea kubakwa na kikundi.
Baadhi ya wakazi waliamini kwamba ubakaji ulitumiwa kwa makusudi kuwatisha na kuwadhalilisha na kwamba haukuwa wa bahati mbaya. Walisema vikosi vya usalama na askari wa Wanyama pori waliwahi kutenda ubakaji wakati wa uhamishaji wa nguvu katika wilaya ya Ngorongoro hapo awali.
Hakuna muathirika yeyote aliyeweza kupata huduma ya baada ya ubakaji, ikiwa ni pamoja na huduma za matibabu na afya ya akili.
Unyanyasaji wa Wakaazi
Wanaharakati na wakazi walisema kwamba tangu zoezi la kuweka mipaka, serikali imewatisha, kuwakamata na kuwashikilia watu kiholela ili kuwanyamazisha kuhusu ghasia.
Vitisho kutoka kwa Maafisa wa Ngazi za Juu
Tarehe 10 Juni, baada ya kuripotiwa sana kwa matukio ya Loliondo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akiongea mbele ya Bunge la Tanzania, alikanusha kwamba polisi waliwafyatulia raia risasi. Wakati wa kikao hicho, Spika wa Bunge, Tulia Ackson, aliiomba serikali kuchukua hatua dhidi ya watu waliorekodi na kusambaza video za vurugu za Loliondo, akiwashutumu kwa kusambaza habari za uongo.
Tarehe 13 Juni, msemaji wa serikali, Gerson Msigwa, alisema, "Watuhumiwa wa uchochezi na kuhamasisha wakazi kufanya vitendo vya uchokozi huko [Loliondo] watawajibishwa na watashughulikiwa kisheria."
Mtetezi mmoja wa haki za binadamu alisema alipokea vitisho kwa sababu shirika lake lisilo la kiserikali liliongea kuhusu tukio hilo: "Baada ya kuripoti kile kilichotokea tarehe 9 Juni, nilipata simu kadhaa, zikisema, 'Unachofanya kitakuletea matatizo makubwa. Acha unachofanya.' "Alisema maafisa kutoka kamati ya usalama ya mkoa wameendelea kumtishia.
Kukamatwa na Kuzuiliwa kiholela
Asubuhi ya Juni 9, mamlaka iliwaita viongozi 10 wa jamii ya Loliondo kwenye mkutano katika ofisi ya mkuu wa wilaya ya Ngorongoro huko Wasso. Kisha Polisi waliwakamata viongozi hao na kuwapeleka kituo cha polisi cha Chekereni, karibu kilomita 350 kutoka hapo. Mamlaka iliwashtaki kwa jaribio la mauaji na mauaji ya askari wa polisi yaliyotokea tarehe 10 Juni huko Ololosokwan, licha ya kwamba viongozi hao walikuwa tayari kizuizini Chekereni wakati huo.
Mamlaka iliwakamata watu wengine 17 katika wilaya hiyo katika kipindi cha wiki tatu zilizofuata, na kuwashikilia baadhi yao kwa miezi kadhaa. Mamlaka iliwatoa kwa dhamana watatu mnamo Agosti, na mwendesha mashtaka aliwaachilia huru watuhumiwa wote 24 mnamo Novemba 25, baada ya kuwafungia kwa miezi mitano.
Mmoja wa wale 27 alielezea kukamatwa kwake na polisi wakati akielekea nyumbani tarehe 15 Juni:
Nilifungwa mnyororo, nikapigwa. Na wakanipeleka kituo cha polisi cha Loliondo. Nilinyimwa chakula kwa siku mbili. Kisha wakanipeleka gerezani ambapo viongozi wengine walikuwa wanashikiliwa. Polisi waling’ang’ania kuniuliza niwaambie wako wapi viongozi wengine, kwa nini watu walikimbilia Kenya, nani anarekodi watu hao [huko Loliondo na kutuma picha hizo kwa vyombo vya habari], nani anaitisha mikutano ya jamii. Nilisema sijui. Kisha nilishtakiwa.
Mnamo Juni 10 saa saba mchana, polisi watano walimkamata mwanaharakati Isaya Olepose Laizer huko Arusha baada ya kuzungumza ClubHouse, programu ya mtandao wa kijamii unaotumia sauti, siku hiyo na kusema kuwa Waziri Mkuu Majaliwa alidanganya bungeni kuhusu kile kilichotokea Loliondo siku iliyopita.
Laizer aliiambia Human Rights Watch kwamba polisi walimshikilia akiwa amefungwa pingu kwa saa tano huko Usa River, kilomita 12 kutoka Arusha. Baadaye, walimpeleka kituo kikuu cha polisi cha Arusha, ambapo polisi wawili walimshambulia na kumpiga wakati wakimhoji kuhusu uhusiano wake na wanaharakati mashuhuri. Polisi walimwachilia Laizer bila mashtaka tarehe 12 Juni na kumwambia aripoti kila wiki kwa wiki tatu. Askari polisi alimwambia Laizer na mke wake kwamba akizungumza hadharani tena kuhusu Loliondo, watamuua.
Hali ya Hofu na Kushindwa Kurudi Nyumbani
Wakazi walisema kuwa tangu Juni 2022 maafisa wa usalama na askari wa wanyama pori wamekuwa na uwepo mkubwa katika eneo la Loliondo. Wale ambao wamekimbia hadi Kenya walisema wanaogopa kurudi, ikiwa ni pamoja na kutokana na kupokea habari mara kwa mara kwamba mamlaka zinawatafuta. Baadhi ya wakazi walisema wanatambua kuwa maafisa wa usalama wa Tanzania wamevuka mpaka kuwatafuta nchini Kenya.
Gharama za Kibinadamu za Kupoteza Matumizi ya Ardhi
Human Rights Watch ilipitia picha za satelaiti zenye ubora mkubwa na uwezo wa kuona eneo ambalo serikali imepiga marufuku. Ufuatiliaji wa mpaka huu ulianza kutoka kaskazini mnamo Juni 20, 2022, na kukamilika mnamo Julai 28, 2022. Uchambuzi wa Human Rights Watch wa picha za satelaiti za eneo hilo uligundua kuwa takriban boma 90 na mazizi ya mifugo yameharibiwa kwa moto ndani ya eneo hilo kati ya Julai 2 na Julai 30.
Human Rights Watch iligundua kuwa mpaka uliowekwa na ghasia zilizofuatia zimeathiri moja
kwa moja upatikanaji wa ardhi, maji, kipato na utamaduni wa wakaazi wa eneo hilo.
Wakazi ambao nyumba zao ziko katika hifadhi iliyozuiliwa kwa ajili ya wanyama pori walisema wanahofia kulipizwa kisasi na vikosi vya usalama ikiwa watataka kuingia katika eneo hilo. Baadhi walisema hawajaweza kuvuna mazao tangu walipokimbia Juni 2022.
Kuzuiliwa Kuzipata Rasilimali
Wakili anayewakilisha jamii alisema serikali haijalipa fidia yoyote kwa wanajamii walioathirika kwa hasara waliyopata.
Wakazi wa Loliondo walisema kuwa kutokana na hifadhi mpya iliyotengwa ya wanyama pori, wamepoteza ardhi waliyotumia awali kwa malisho ya mifugo na kilimo, na sasa wana upatikanaji mdogo wa vyanzo muhimu vya maji. Hali imefanywa kuwa mbaya zaidi katika miezi ya hivi karibuni kutokana na ukame ulioendelea, ambao umesababisha mito midogo, mifereji kukauka na kusababisha athari kwa ukuaji wa majani ya malisho. Baadhi ya wakazi walisema mifugo yao ilikufa kutokana na kupungua kwa upatikanaji wa vyanzo vya maji.
Wakazi waliokimbia pia walipoteza mifugo yao iliyobaki ikitangatanga pamoja na mali nyingine, ikiwa ni pamoja na nyumba ambazo serikali imezibomoa tangu wakati huo.
Mama mmoja asiyekuwa na mume aishiye Ololosokwan alielezea changamoto zake baada ya kupoteza nyumba yake na ng'ombe 7 kati ya 15: "Nina watoto watatu na wanapitia wakati mgumu sana. Wananitegemea mimi kwa elimu, chakula, na nguo. Mimi hutegemea mifugo kuwalipia gharama za shule, lakini sasa mifugo haiwezi kupata ardhi ya malisho na wanakufa."
Baadhi ya wakazi wa Loliondo walilazimika kuwaacha watoto wao nyuma walipokimbia. Wakazi walisema kuwa wazee wa jamii ambao hawakuweza kuondoka kwa sababu ya ukosefu wa usafiri rahisi, umbali mrefu na eneo gumu kupita, na hatari ya shambulio la wanyama walikuwa wakiwalea watoto hao, wakiachiwa mzigo wa kifedha na kijamii juu yao.
Mkazi mwingine wa Ololosokwan alipelekwa Kenya kwa matibabu baada ya maafisa wa usalama kumpiga risasi kwenye mguu tarehe 10 Juni. Alirudi miezi sita baadaye. Alisema: "Niliikuta nyumba yangu imeharibiwa. Watoto wangu walikuwa wametawanyika sehemu tofauti na mifugo ilikuwa imetawanyika. Ukame ni mbaya. Hakuna chakula. Mifugo inakufa. Hatimaye niliwapata watoto lakini sio mifugo. ”
Wakazi kadhaa walisema wanawake walilazimika kutafuta vyanzo vingine vya maji kwa matumizi ya kila siku, wakisafiri umbali mrefu na kuongeza hatari ya mashambulio ya vikosi vya usalama, ikiwa ni pamoja na ubakaji.
Unyang’anyi na Kupigwa Mnada kwa Mifugo
Tangu Juni, askari wa wanyama pori wamekuwa wakiikamata mara kwa mara mifugo inayoingia katika eneo jipya lililotengwa kama hifadhi ya wanyama pori na kutaka wamiliki kulipa faini nzito ya shilingi 100,000 ($ 43) kwa ng'ombe na shilingi 25,000 ($ 15) kwa kondoo au mbuzi ili kuachiwa. Baadhi ya wakazi wamelazimika kuacha mifugo yao kwa sababu hawawezi kulipa faini hizo.
Hii imeathiri kwa kiasi kikubwa kaya zinazoongozwa na wanawake, ambao kwa kawaida huwa na idadi ndogo ya mifugo na hawawezi kuthubutu kuuza mfugo yeyote ili kupata fedha za kurudisha mifugo yao. Mkazi wa Ololosokwan alisema alilazimishwa kulipa shilingi milioni 1.4 ($ 600) kurudisha mifugo yake na wengine katika kaya yake walilipa jumla ya shilingi milioni 9 ($ 3,850).
Mnamo mwezi Novemba, askari wa wanyama pori walianza kukamata na kusafirisha mifugo ya wakazi katika eneo ambalo haliruhusiwi kilomita kadhaa kutoka Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, na kupata amri za mahakama iliyosema mifugo hiyo haikuwa na mmiliki, na kuipiga mnada. Mashahidi walisema mnada hufanyika chini ya wiki moja baada ya mifugo kukamatwa, na kuwaacha wamiliki kuwa na muda mchache wa kupata kibali cha kufika Serengeti, na hivyo kupunguza zaidi uwezekano wa kurejesha mifugo yao.
Ukosefu wa Chakula
Hatua za serikali zimesababisha ukosefu mkubwa wa chakula kwa jamii ambazo tayari zimepoteza makazi, mazao, zinakabiliwa na ukame, na zinazotegemea mauzo ya mifugo kununua chakula ambacho hawakilimi wenyewe.
Wakazi wa Loliondo waliiambia Human Rights Watch kwamba ng'ombe wao wana kiu na njaa, na hivyo kupungua uzito au kufa. Na kwa sababu mifugo yenye miili midogo huleta bei ndogo, familia zao hazijapata pesa za kutosha kulipia mahitaji ya chakula, huduma za afya, na elimu. Hii hutokea zaidi kwa wale ambao ndugu zao walikimbia eneo hilo.
Mwanamke mmoja mkongwe alisema:
Mwezi Juni na Julai ni wakati wa mavuno. Kwa sababu ya yaliyotokea sikuweza kuvuna. Nilikuwa Kenya, mume wangu alikamatwa na kuzuiliwa, kitu pekee nilichokuwa nakiwaza ni swala la chakula. Watoto wetu walikuwa na njaa. Kundi letu la ng'ombe lilikuwa linapotea.
Haki ya Utamaduni
Ufugaji ndio njia kuu ya kuwaingizia kipato Wamaasai, na ni sehemu muhimu ya tamaduni yao. Human Rights Watch iligundua kuwa vizuizi vya serikali kwa upatikanaji wa ardhi na vyanzo vya maji kwa wakazi wa Loliondo vimeathiri vibaya mtindo wao wa maisha.
Wakazi walisema kuwa eneo la akiba ya hifadhi lina ardhi ambayo imekuwa ikitumiwa kwa muda mrefu kwa malisho ya mifugo; kwa ajili ya matambiko, ikiwa ni pamoja na sherehe za unyago; na kwa ajili ya kuwarithisha mbinu za uhifadhi za jadi kwa kizazi kipya/kinachofuata.
Mkazi wa Ololosokwan mwenye umri wa miaka 71 alielezea "uhusiano mkubwa" kati ya utamaduni wa Wamaasai na ardhi:
Tunailinda [ardhi] kwa kutumia maarifa yetu ya jadi ili kuweza kuendelea kuwa na malisho kwa miaka mingi. ... Ndani ya eneo lililotengwa ni mahali patakatifu panapoitwa Oltorotwa. Tunakwenda huko kutoa sadaka wakati wa nyakati ngumu, hasa wakati wa ukame. Wakati kama huu wa ukame, watu fulani walipaswa kuwa wameteuliwa [kutoa sadaka]. Lakini sasa hatuwezi kuingia eneo hilo.
Mapendekezo kwa Serikali ya Tanzania
• Simamisha mipango yote ya kuwafukuza watu kwa nguvu au kuwahamisha kwa njia isiyo halali kutoka eneo la Loliondo Game Control Area, na kupitisha miongozo ya usalama ya kudumu dhidi ya kuhamisha watu kwa nguvu.
• Toa msaada wa kibinadamu mara moja kwa familia zinazoishi ndani ya hifadhi ya Wanyama pori iliyotengwa upya, ikiwa ni pamoja na makazi mbadala.
• Fanya uchunguzi wa kuaminika na usio na upendeleo kuhusu unyanyasaji uliofanywa na vikosi vya usalama na askari wa wanyamapori huko Loliondo tangu Juni 6, 2022, ikiwa ni pamoja na unyanyasaji wa kingono, na kuhakikisha kuwa maafisa wa polisi na jeshi wanaohusika wanawajibishwa.
• Simamisha mara moja ukamataji wa mifugo kwa malipo na kuiuza kwenye minada, na badala yake wahifadhi wanyama wanaotorokea katika eneo lililotengwa kwenye zizi kwa ajili ya kuwarudisha kwa wamiliki wao.
• Rekebisha vipengele vya Sheria ya Uhifadhi wa Wanyama pori ili kulingana na historia ya Tanzania ya maeneo yaliyolindwa kwa matumizi ya watu na wanyama, ikiwa ni pamoja na eneo la LGCA, na kuhakikisha kuwa vipengele havivunji haki za watu za ardhi, mali, kipato na utamaduni.
• Fanya mashauriano yenye maana na jamii zilizoathirika, ikiwa ni pamoja na wanawake na watoto, kuhusu athari za mabadiliko yoyote yanayowezekana katika mtindo wa uhifadhi wa maeneo ya uhifadhi ambayo yanaweza kuathiri ardhi, mali, maisha ya kujikimu, usalama wa chakula, utamaduni, na elimu yao.
• Weka taarifa zote zinazohusiana na mabadiliko yoyote katika mtindo wa uhifadhi kuwa wazi kwa jamii zilizoathirika, wawakilishi wao, na wadau wanaohusika kabla ya mashauriano.
• Tambua kisheria ardhi na rasilimali ambazo jamii za wafugaji katika wilaya ya Ngorongoro wamevitumia na kuvitunza kwa vizazi vingi, kwa kuheshimu mfumo wao wa kisheria, mila, na mazoea, ikiwa ni pamoja na njia za ufugaji wa kienyeji na ibada zao.
• Kutambua kisheria ardhi na rasilimali ambazo jamii za wafugaji katika wilaya ya Ngorongoro wameitumia na kuisimamia kwa vizazi, kwa kuheshimu mifumo yao ya kisheria, mila na desturi, ikiwa ni pamoja na njia za ufugaji wa kiasili na sherehe.
• Toa maagizo ya wazi ya kisheria kwa wafanyakazi wa afya kwamba hakuna mahitaji ya kisheria kwa waathirika wa unyanyasaji ya kuleta fomu zilizosainiwa na polisi ili kupata matibabu, ikiwa ni pamoja na huduma ya baada ya ubakaji.
Mapendekezo kwa Tume ya Haki za Binadamu na Watu wa Afrika
• Kutoa mapendekezo maalum na yanayoheshimu haki kwa Tanzania, kama vile mwongozo wa kuhakikisha kwamba haki za Wamaasai zinatambuliwa kisheria eneo la Loliondo na kwamba wanaweza kupata tiba/fidia sahihi.
• Kushirikiana na maafisa wa Tanzania ili kutekeleza mapendekezo ya tume kuhusu kushughulikia uvunjaji wa haki za binadamu Loliondo.