(Nairobi) – Marufuku ya serikali ya Tanzania dhidi ya wanafunzi wa kike wanaopata mimba na wale walio na watoto wachanga kuendelea na masomo imewanyima maelfu ya wasichana haki ya kupata elimu. Shirika la Human Rights Watch limesema leo. Shule za umma kote nchini Tanzania bara huwapima wasichana kwa lazima kubaini iwapo wana uja uzito. Wale wanaopatikana na mimba hufukuzwa shuleni kabla ya kumaliza masomo yao.
Marufuku hiyo ambayo imekuwa ikitekelezwa tangu mwezi Juni mwaka 2017, wakati wa utawala wa aliyekuwa Rais wa Tanzania, Marehemu John Magufuli, inaendelea kutekelezwa na mrithi wake, Rais Samia Suluhu, ambaye alishika hatamu mwezi Machi mwaka huu wa 2021.
“Wasichana wa Tanzania wanadhulumiwa sana kwa sababu serikali inaendeleza sera hiyo ambayo imezima ndoto yao ya kupata masomo. Sera hiyo inawadhalilisha na kuwatenga wasichana huku ikiathiri maisha yao ya usoni,” asema Elin Martinez, mtafiti mkuu wa masuala ya haki za watoto katika Shirika la Human Rights Watch. “Serikali ya Tanzania inafaa kusitisha sera hiyo dhalimu kwa haraka ili wanafunzi wa kike wajawazito na ambao ni wazazi waweze kurejelea masomo yao.”
Katika miezi ya Julai na Agosti, Shirika la Human Rights Watch liliwahoji wasichana na wanawake 30 wenye kati ya umri wa miaka 16 na 24. Wote walikuwa wamefukuzwa shuleni au kukoma kwenda shule za msingi au sekondari kati ya mwaka 2013 na 2021 kwa ajili ya ujauzito.
Maafisa wa elimu na walimu wana jukumu kubwa la kutekeleza sera hiyo ya serikali, na huitekeleza kwa njia zinazowadhalilisha wasichana na kuwasababishia maisha ya unyanyapaa. Hali hiyo huwaletea aibu wazazi na walezi wengine. Miongoni mwa wale ambao tumewahoji, wengi wao ni wale ambao walipimwa wakiwa shuleni na kupatikana wakiwa wajawazito au walipimwa katika zahanati zilozokaribu, kabla ya kufukuzwa shuleni.
Wasichana kadhaa walifukuzwa kabla ya kukamilisha masomo ya sekondari ya daraja ya kwanza – kumaliza masomo hayo huwa ni hatua nzuri kwa wasichana, hasa kwa kuwa nchini Tanzania kuna tatizo la wanafunzi wengi kushindwa kumaliza masomo. Baadhi walishindwa kufanya mtihani wa kitaifa kufuzu kidato cha 4, kwa sababu ukaguzi huo ulifanyika siku chache tu kabla ya mtihani au wakati mtihani ukiendelea.
Mnamo mwaka wa 2020, maafisa wa elimu katika Mkoa wa Morogoro walimfukuza shuleni msichana wa umri wa miaka 16 kabla ya kufanya mtihani wa mwisho wa kidato cha 4: “Walisema tu kwamba kwa sababu nilikuwa mja mzito … Ilifaa nifukuzwe shuleni hata kama nilikuwa nimesalia na mitihani miwili tu. Haki sikujua kile walikuwa wakifikiria …. Hata hawakutaka kunisikiza. Walinifukuza tu shuleni.”
Wasichana wengi na wanawake tuliowahoji hawakujiunga na vituo vingine vya mafunzo baada ya kufukuzwa shuleni. Badala yake walijiunga na vituo visivyo rasmi vya kufunza ushonaji wa nguo, huku wachache wakijiunga na shule binafsi, zinazosimamiwa na mashirika yasiyo ya serikali ambayo huwapokea wasichana ambao wamefukuzwa kutoka shule za umma.
Mwaka 2020, serikali ya Tanzania ilitangaza kwamba ingewaruhusu wanafunzi ambao walikuwa wajawazito au wazazi kujiunga kwenye programu sambamba za mafunzo ili kuwawezesha kuendeleza masomo kama “njia mbadala za masomo.” Programu hiyo iliwezeshwa kupitia ufadhili wa Benki ya dunia wa Dola za kimarekani milioni $180 kama sehemu ya mkopo wa dola milioni $500 kufadhili mipango ya kuboresha Viwango vya Masomo ya Shule za Sekondari nchini Tanzania (Secondary Education Quality Improvement Program (SEQUIP).
Katika kueleza programu hiyo, Benki ya Dunia ilisema kwamba “licha ya kuwa hakuna sera za serikali zinzoshurutisha wanafunzi wanaopata mimba kufukuzwa kutoka shule za umma, wasichana wengi wanaopata ujauzito husitisha masomo ya o kwa hiari.” Serikali ya Tanzania na Benki ya Dunia imelenga kuendeleza programu hiyo kama njia mbadala kwa wasichana ambao “wameondoka shuleni” kwa ajili ya kupata mimba.
Licha ya kwamba njia mbadala za masomo ni muhimu kwa wanafunzi ambao waliondoka shuleni mapema, Tanzania ina mfumo mbadala ambao ni wa kipekee ambapo wasichana waliofukuzwa shuleni na kunyimwa haki ya kupata elimu wanaweza kuutumia kupata masomo.
Lakini vituo vingi vinavyotoa mafunzo hayo huitisha ada, huku wanafunzi wakilazimika kusafiri mwendo mrefu kufikia vituo hivyo. Hali hii inadumisha vikwazo vikuu ikiwemo ukosefu wa pesa na ukosefu wa njia za kufikia masomo na kuathiri wasichana wengi katika shule za upili. Vituo vingi vya masomo havina njia zozote za kuwasaidia wasichana wazazi wenye umri mdogo, ikiwemo usaidizi wa namna ya kuwalea watoto hao.
Tanzania ni mojawapo ya nchi tatu zilizoko Kusini mwa Jangwa la Sahara ambazo Shirika la Human Rights Watch limebaini kwamba zinatekeleza marufuku rasmi dhidii ya wanafunzi wa kike ambao hupata mimba. Mnamo mwezi Machi mwaka 2020, Sierra Leone, ilibadilisha sera hiyo ambayo ilikuwa imetekelezwa kwa muda wa miaka 10. Mwezi Machi mwaka 2021, serikali ya Sierra Leone iliandaa sera mpya ya “kushirikisha mageuzi,” ambayo ilisisitiza haki za wasichana wajawazito na wazazi wachanga kupata elimu’. Shirika la Human Rights Watch limebaini kwamba yamkini nchi 30 barani Afrika sasa zina sheria, sera, na mikakati ya kulinda haki za wanafunzi wanaopata mimba na wazazi vijana kupata elimu.
Rais Suluhu anafaa kutoa agizo maalum ambalo litakomesha mfumo wa kuwafukuza shuleni wanafunzi waliopata mimba, na kuwaagiza maafisa wa serikali kukomesha taratibu za kibaguzi zinazowadhulumu wasichana, vile vile Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia inafaa kutunga sera ambayo italinda haki za wanafunzi waliopata mimba na wale ambao ni wazazi kuendelea na masomo yao katika shule za umma, Shirika la Human Rights Watch lilisema.
“Tanzania kwa sasa ndio nchi ya pekee yenye sera zinazowadhulumu wanafunzi wa kike wanaopata mimba, miongoni mwa nchi zilizoko kusini mwa jangwa la Sahara ambazo zimetunga sheria, sera na mikakati ambayo italinda haki za wanafunzi waliopata mimba na wale ambao ni wazazi,” Asema Martinez. “Rais Suluhu anafaa kukomesha marufuku dhidi ya wanafunzi wa kike wajawazito na wazazi vijana na kutangaza kujitolea kwake kulinda na kutekeleza haki za elimu kwa kila msichana.”
Mimba za mapema Tanzania
Tanzania ina rekodi ya juu sana ya vijana wa umri mdogo kupata mimba: asilimia 22 ya wanawake wenye kati ya umri wa miaka 20 na 24 hupata watoto kabla kutimu umri wa miaka 18. Kwa mujibu wa takwimu zilizoandaliwa na Shirika la Guttmacher, linaloangazia haki za mapenzi na uzazi, wasichana na wanawake wachanga 360,000 wenye umri wa kati ya miaka 15 na 19 hupata watoto kila mwaka; halafu 390,000, au asilimia 57 ya wasichana wa umri huu wanashindwa kutimiza mambo yanayohusu njia za kupanga uzazi au hata hawatumii njia hizi.
Kati ya Mwaka 2003 na 2011, zaidi ya wasichana wadogo 55,000 walilazimika kuacha shule huku baadhi wakifukuzwa kwa sababu ya uja uzito. Habari hizi ni kwa mujibu wa Shirika la kimataifa la kushughulikia haki za wanwake Center for Reproductive Rights. Benki ya Dunia inakisia kwamba wanafunzi 5,500 waliopata mimba huacha shule kila mwaka licha ya kwamba mashirika yasiyo ya serikali awali yamekisia kwamba takriban wanafunzi 8,000 wamelazimika kuacha shule kila mwaka kwa sababu ya mimba za mapema.
Takwimu za Tanzania zinazohusu mimba za mapema, ambazo ni za juu, zinazoonyesha kwamba watoto na vijana wa umri wa kubalehe wanahitaji habari muhimu za kuwasaidia kujikinga dhidi ya mimba za mapema, ilhali mafunzo kuhusu maswala ya mapenzi hayapo kwenye mtaala wa masomo nchini humo. Mwaka 2017, Shirika la Human Rights Watch limebaini kwamba wasichana wengi wanakosa habari za kimsingi kuhusu afya ya uzazi. Mara nyingi, wasichana na wanawake hupata habari muhimu kuhusu maswala ya mahusiano ya kimapenzi na afya ya uzazi wakiwa tayari wamepata mimba au hata baada ya kujifungua.
Hofu ya kufukuzwa shuleni huwaongezea wasichana wengi shinikizo huku wengi tayari wakiwa wanakumbana na changamoto nyingi. Wasichana na wanawake waliohojiwa wamezungumzia ugumu wa kupata pesa huku wanaume wengi wakitumia mapungufu hayo kuwashawishi kufanya nao mapenzi. Walisema wanaume wengi huwabeba kwenye magari na kuwapa pesa au kuwapa vifaa vya kimsingi, huku wakiitisha mahusiano ya kimapenzi. Miongoni mwa waliohojiwa, wengi wao walisema walipata mimba baada ya kunajisiwa au - kupitia njia nyingine za kuwatumia kimapenzi, mara nyingi watu wanaohusika ni waendeshaji boda boda, madereva wa magari ya uchukuzi au wanaume wengine wa mitaani na vijijini.
Marufuku ya Tanzania ya kuwa shuleni
Sheria ya Elimu nchini Tanzania ya Mwaka 2002 yenye masharti ya kuwafukuza wanafunzi shuleni, inaruhusu kufukuzwa iwapo “ mwanafunzi amefanya kosa la ukiukaji wa maadili” au iwapo mwanafunzi “ameolewa au kuoa.” Licha ya kwamba masharti hayo hayataji uja uzito, maafisa wa elimu na wasimamizi wa shule hufafanua sheria na masharti hayo kumaanisha kwamba uja uzito ni kosa la ukiukaji maadili. Mnamo mwaka 2013, Shirika la Center for Reproductive Rights lilipata kwamba hatua za kuwafukuza wasichana shuleni kwa sababu ya uja uzito ilikuwa ikifanyika karibu kote nchini Tanzania.
Utafiti wa Shirika la Human Rights Watch wa Mwaka 2014 na 2017 ulipata kwamba shule za umma hazikuwa zinatekeleza sera hii kwa njia sawa kote nchini Tanzania. Baadhi ya shule zilikuwa zinaruhusu wanafunzi wa kike waja wazito na wale ambao ni wazazi kusalia shuleni, huku baadhi ya walimu wakiwaunga mkono wanafunzi kama hao kuendelea na masomo. Hata hivyo, shule nyingi ziliwapima mimba wanafunzi wa kike kwa lazima na kuwafukuza shuleni waliopatikana kuwa wajawazito mara kwa mara. Licha ya kwamba hakuna masharti ya kuwapima mimba wanafunzi, shughuli hiyo ilitumika kwenye shule nyingi za sekondari na hivyo wanafunzi wengi waliopatikana kuwa wajawazito walifukuzwa shuleni. Shirika la Human Rights Watch limepata kwamba shughuli ya kupima mimba kwa lazima inakiuka haki za msichana -haki za faragha za mtu, heshima za kibinadamu, usawa, na uhuru wa mtu juu ya mwili wake.
Halafu ikafanyika kwamba –Rais Magufuli aliidhinisha kutupilia mbali kwa sera hiyo tarehe 22 Juni, 2017, akisema, “almuradi mimi ni rais, hakuna mwanafunzi ambaye ni mzazi au mwanafunzi mjamzito ataruhusiwa kurejea shuleni …idhini ya kwenda shule iwe shule za msingi au shule za sekondari sasa imepigwa marufuku.” Agizo hilo la Rais, lililoandamana na vitisho ambalo liliandaliwa na Waziri wa maswala ya ndani wa Tanzania dhidi ya mashirika ya kijamii na wakereketwa waliopinga marufuku hiyo, lilitekelezwa mara moja.
Binti kwa jina Imani A mwenye umri wa miaka,18, kutoka Mkoa wa Morogoro, alisema kwamba alikuwa na umri wa miaka 12 mwaka 2015 wakati alifukuzwa kutoka shule ya msingi aliyokuwa akisomea katika darasa la 6. “Na, hawakuniambia kwamba [ningerudi shule], kwa sababu rais alikuwa ametangaza waziwazi bila kusita kwamba yeyote anayeshika mimba asiruhusiwe kurejea shuleni,” alisema Imani. “Kwa kuwa walikuwa tu wakifwata amri ya rais.”
Maafisa wa serikali wamekuwa wakifuatilia kwa karibu utekelezaji wa amri ya rais ya Mwaka 2017, huku wakitangaza waziwazi kwamba shughuli za kupima mimba miongoni mwa wanafunzi wa kike zitaendelea huku wale wanaopatikana kuwa wajawazito wakifukuzwa shuleni.
Mnamo tarehe 29 mwezi Februari mwaka 2020, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Patrobas Katambi aliwaagiza wakuu wa shule na maafisa wa elimu kutoa habari kwa polisi kuhusu visa vya wanafunzi waliokuwa wamepata mimba:
Kwenye kila kipindi cha miezi mitatu, usimamizi wa shule … utaandaa taratibu za kusimamia shughuli ile … huku ukitenga siku ya kuwapima mimba wasichana kukiwemo kuwahamasisha kuhusu athari zinazoshirikishwa na mimba za mapema, vilevile athari na hatari iliyopo kwenye mahusiano ya mapenzi ya mapema.
Katambi aliongeza kwamba wakati wa siku ile ya kufanya shughuli, shule zinafaa:
Kuwatangaza wale[wanafunzi] ambao wamepatikana kuwa na mimba na hatua zilizochukuliwa dhidi yao. Wanafunzi ambao watapatikana kuwa na mimba siku hiyo ya ukaguzi watashtakiwa kwa polisi …Shughuli hii itakuwa kazi kuu kwa maafisa wa serikali na itatumika kutathmini utendakazi wetu … Ukiwa mtu anayevumilia visa vya uja uzito katika shule yako … bila shaka hilo linamaanisha kwamba wewe ni sehemu ya [matatizo yaliyopo], kwa hivyo tutaamini kwamba umechangia katika kujenga tatizo hilo.
Alielezea kuwa katika muda wa siku tano baada ya kuchukuliwa kwa hatua hizo, yafaa:
Awe amepokea ripoti kamili kuhusu visa 195 vya wanafunzi walioshika mimba vilivyomfikia, na ni wapi walipo, hatua zipi zimechukuliwa au hazijachukuliwa… hatua zipi zimeshughulikiwa, visa vingapi vingali vinasubiri kushughulikiwa … Kwenye suala hili, “ninalichukulia kwa mazingatio makubwa… Nitawakana wote wanaotuzuia kutekeleza jukumu hili. Iwapo ni idara ya mahakama, yafaa tuwe tunasema wazi kwamba ni mahakama, kwamba rais atapashwa habari hiyo.”
Tarehe 3 Aprili, Mwaka 2020, msemaji mkuu wa serikali Hassan Abbasi, alitoa taarifa ifuatayo kupitia ukurasa wake rasmi wa Twitter :
Swala la kuwazuia wanafunzi wa kike wajawazito kurudi shuleni kushiriki kwenye masomo rasmi sio la kuwahamasisha wanafunzi kuanza kushiriki mapenzi wakiwa katika umri mchanga … Msichana anayepata mimba hajanyimwa haki yake ya kupata elimu. Ataendelea na masomo yake kupitia mfumo tofauti na mfumo rasmi wa elimu ambao utajumuisha vituo vya kutoa mafunzo ya kiufundi vinavyompa maarifa ya kikazi anayohitaji.
Hali ya wasichana waliopata mimba kukoma kuendelea na masomo haikuanza leo, imekuwa sehemu ya taratibu za serikali kwa miaka mingi. Serikali ilianzisha mfumo mbadala wa elimu ili kuwafaa wanafunzi wa kike ambao wamepata mimba wakiwa shuleni.
Kinyume na Tanzania bara, katika kisiwa cha Zanzibar, wizara ya elimu na mafunzo ya kazi inazingatia utaratibu wa kisheria chini ya sera zinazozingatia masharti yaliyowekwa. Mwezi Aprili 2021, waziri wa elimu wa Zanzibar alisisitiza haki za wasichana kurudi shuleni baada ya kupata mimba na kujifungua.
Athari za marufuku kwa wasichana wa shule wajawazito.
Waathiriwa waliohijiwa ambao walikuwa wanafunzi walirejelea visa vingi vya kuwadhalilisha ikiwemo kulengwa na walimu wanaowatumia kama mifano darasani. Leyla M. mwenye umri wa miaka 23, kutoka Mkoa wa Kilimanjaro, alisema kwamba “Mwalimu mkuu alikuwa mkali sana … alisema nisiwahi kukanyaga pale shuleni tena.”
Esther A wa umri wa miaka 21, wa kutoka kijiji kilicho karibu na Kilimanjaro, alifukuzwa shuleni akiwa katika kidato cha 2 Mwaka 2017:
Mama yangu alijaribu kuwaomba [wasimamizi wa shule] kwamba ikiwezekana nirudi shuleni baada ya kupata mtoto. Lakini walimu walimwambia la, nisingerudi shuleni. Walisema hawawezi kukubali kuwa na mtu ambaye ni mama mzazi darasani. Walisema kwamba nitakuwa mfano mbaya kwa wanafunzi wengine.
Walimu walimpa majaribio Gladness M. wa umri wa miaka 19 sasa, akiwa shuleni pamoja na wanafunzi wenzake wa kike. Mwaka 2017, alifukuzwa kutoka shule ya sekondari Mkoani Morogoro, akiwa katika kidato cha 4 na mimba ya miezi minne. “Walimu waliwaambia wanafunzi wenzangu pale shuleni kwamba nilifukuzwa kwa sababu nilikuwa mja mzito,” alisema Gladness. “Halafu waliwaambia wanafunzi wengine kwamba iwapo watapata mimba wakiwa shuleni basi nao pia watafukuzwa.”
Wasichana kadhaa waliohojiwa walihadithia ajali za kupoteza mimba zao lakini hawakurejeshwa tena shuleni, licha ya kwamba sasa hawakuwa tena wajawazito. Aidha baadhi yao hawakuwa wazazi lakini wasingerudishwa. Mwaka 2015 katika Mkoa wa Arusha, Maria T.wa umri wa miaka, 21 sasa, alisema mimba yake ilitoka wakati ikiwa miezi minne akiwa katika kidato cha 2. Lakini hakuruhusiwa tena shuleni:
Nilifukuzwa shuleni nikiwa umri wa miaka 15 pekee. Nilikuwa mchanga … Sikujua lolote kuihusu .… dunia - mtu aliyenipa mimba naye alikuwa akinishinikiza [niitoe mimba ile]. Nilihofu kwamba huenda jambo baya likatokea, [na ] sikuwa naungwa mkono na familia yangu … sikuwa na mtu yeyote wa kunijali, singerudi shuleni.
Wasichana sita walielezea namna walikatazwa kufanya mtihani wao wa mwisho wa kidato cha 4. Bila kuufanya mtihani huo, wanafunzi hawawezi kupata cheti cha kukamilisha masomo ya daraja la kwanza la shule ya sekondari. Wengi wao walipimwa mimba siku chache kabla mitihani kuanza.
Mwaka 2017, akiwa na umri wa miaka 17, Glory R., alfukuzwa kutoka shule moja ya sekondari katika Mkoa wa Arusha akiwa kwenye mwisho mwisho wa muhula wa kumaliza kidato cha 4: “Kwa wanafunzi wa kidato cha 2 na 4 [madarasa ambayo hufanya mitihani ya kitaifa ya kufuzu], mwezi mmoja kabla kufanyika mitihani hiyo wangeleta wauguzi kuja kutupima mimba.” Wasichana pia walipimwa kila baada ya miezi mitatu au minne katika shule aliyosomea Glory.
Kwenye kisa sawa, mwaka huo huo, Rebecca C. wa umri wa miaka, 23 sasa, alifukuzwa kutoka kidato cha 4 kwenye shule moja ya sekondari katika Mkoa wa Arusha. Alipatikana kuwa na mimba kabla mitihani ya mwisho ya kidato cha 4: “Kwa sababu ilikuwa ndiyo desturi ya shule kupima uja uzito miongoni mwa wasichana. Sasa walipotupima, walitupata tukiwa wajawazito na hapo tukafukuzwa shuleni,” Alisema Rebecca. Alikumbwa na woga kuhusu namna wazazi wake wangechukulia swala hilo hata akatoroka nyumbani, na baadaye mimba hiyo ikatoka.
Baadaye Rebecca aliwauliza wasimamizi wa shule iwapo angerudi shuleni:
Waliniambia waziwazi kwamba sikutakikana pale shuleni. Iwe kwamba nilikuwa nimeitoa mimba ile au imetoka yenyewe, waliniambia kwamba wasingeniruhusu shuleni pale tena. Waliniambia kwamba nikirudi pale nitawafunza wanafunzi wengine mienendo mibaya.
Mwalimu mkuu wa kike mkoani Arusha alisema: “Sheria za Tanzania zinaelezea waziwazi kuhusu swala hilo wala haziyumbiyumbi. Akiwa mjamzito, atafukuzwa shuleni hata kama atakuwa amesalia na mwezi mmoja pekee [wa mitihani] … kwa kuwa sheria inanitaka mimi kumfukuza … mwalimu hawezi kwenda kinyume na hilo.”
Mwezi Juni Mwaka 2016, bunge la Tanzania lilipitisha marekebisho kwenye Sheria ya Elimu yaliyofanya iwe kosa kumwoa mwanafunzi wa shule ya msingi na shule ya sekondari, au kuwatia mimba wasichana ambao wangali wanafunzi. Adhabu ya kosa hilo ilitajwa kuwa kifungo cha kufikia miaka 30 jela. Mbali na hayo, sheria hiyo inamtaka kila mwalimu mkuu wa shule kuhifadhi rekodi za visa vya wasichana kuolewa na wale waliopata mimba. Vilevile mwalimu mkuu anafaa kuhakikisha kwamba wakuu wa mikoa wanafahamishwa habari hizi.
Shirika la Human Rights Watch lilipata kwamba shule hukusanya habari hizi kwa njia inayoongeza unyanyapaa katika jamii dhidi ya wasichana walioathirika. Kwenye Mkoa wa Simiyu , Salma H., wa umri wa miaka 19 sasa, alisema alikuwa na umri wa miaka 15 wakati mwanamume aliyekuwa anamfahamu alimnajisi. Baadaye aligundua kwamba alikuwa ameshika mimba. Rafiki yake wa karibu akamwambia Salma kwamba asiwaarifu wazazi wake na badala yake akampa dawa za kumsaidia aitoe mimba ile. Mpango wa kutoa mimba uliharibika, sasa Salma aliificha mimba ile kwa miezi michache akiwa katika kidato cha 1. Walimu walipata uvumi kutoka kwa wanafunzi wenzake na kulazimika kuwapima mimba wasichana wote shuleni. Salma alisema aliporejea walimu walianza kumuuliza maswali mengi kuhusu mwanamume aliyempa mimba ile:
Sikutaka kuwaambia lolote. Walimwita rafiki yangu na kuanza kumuuliza maswali yale yale. Rafiki yangu aliwapa majina ya wanaume ambao nilikuwa nimefanya nao mapenzi. Waliniita tena shuleni na kuniuliza tena mwanamume yupi kwenye orodha ile alikuwa amenipa mimba ile. Niliwaambia sikujua ni yupi.
Kwa hivyo walimu waliandika barua ya [kunifukuza shuleni] ambayo ilitaja majina ya wanaume watatu. Walikuwa wamepewa majina hayo na rafiki yangu. Halafu wakatuma nakala za barua ile kwa polisi, nyingine kwa idara ya mahakama na moja wakawatumia wazazi wangu.
Walimu walimfukuza Rose B. Mwenye umri wa miaka 20 sasa, kutoka Mkoa wa Arusha, akiwa katika kidato cha 3 Mwaka 2020. Rose alihojiwa shuleni:
Tulipimwa mimba shuleni na hivyo ndivyo walimu walipata kujua … Walinitaka kumtaja mtu aliyenipa mimba lakini nikakataa kuwaambia. Nilikuwa na woga na wasiwasi mwingi. Wazazi wangu waliitwa waje wanichukue shuleni … Nilisumbuka sana, nilikufa moyo si kidogo, na nilijutia sana kilichokuwa kimenitendekea.
Wasichana kadhaa walielezea visa vya kufukuzwa shule za binafsi pia. Katika mkoa wa Arusha, Maria T. wa umri wa miaka 21 sasa, alifukuzwa kutoka shule binafsi aliyokuwa akisomea Mwaka 2015, akiwa kwenye kidato cha 2:
Tulikuwa wawili tuliopatikana kuwa wajawazito baada ya shughuli ya kutupima. Walimu walituambia tu kwamba hatungeendelea na masomo kwa sababu ya sera za serikali kuhusu uja uzito shuleni … Baadaye walinipa barua niwapelekee wazazi wangu na huo ndio ukawa mwisho wa masomo yangu.
Hizo ni sera mbovu maana zinawadhalilisha watoto ... Wasichana wanafaa kuruhusiwa kuendelea na masomo baada ya kujifungua. Yafaa uwe uamuzi wa msichana kuhusu iwapo angetaka kurejea shuleni aendelee na masomo ama la. Lakini kwa kuwa ipo sheria inayowakataza wasichana kurejea shuleni wengine ambao wangependa kuendelea na masomo baada ya kukumbwa na changamoto ya mimba za mapema hushindwa. Mfano, ningepata nafasi ya kurudi tena shuleni baada ya mimba yangu kuharibika.
Esther A.,wa umri wa miaka 21 sasa, Mkoani Arusha, anasema:
Zipo changamoto nyingi sana hapa nje mitaani. Baadhi ya wasichana hupata watoto wakiwa wangali wadogo … msichana bado hajapata werevu wa kujitafutia riziki. Unapata hapati usaidizi kutoka kwa wazazi wake. Hao ndio wasichana ambao huamua kuzurura mitaani bila pa kwenda ... Yafaa wasichana wanaopata mimba wawe wanaruhusiwa kurejea masomoni punde wakishajifungua ili angalau ndoto zao maishani zisikatizwe.
Programu ya masomo mbadala ya serikali ya Tanzania inayofadhiliwa na Benki ya Dunia
Mwezi Machi Mwaka 2020, Benki ya dunia iliidhinisha mkopo wa dola milioni $500 za marekani kufadhili mpango wa serikali ya Tanzania wa kuboresha viwango vya elimu. Sehemu ya pesa hizo, Dola milioni $180 zilitengewa Programu za masomo mbadala (AEPs) na programu nyingine salama za masomo kwa wasichana. Shirika la Human Rights Watch na mashirika mengine yamekosoa uamuzi wa Benki ya dunia wa kuidhinisha mkopo huo licha ya kuwepo ushahidi mwingi kuhusu ubaguzi katika elimu nchini Tanzania. Suala hilo bila shaka linaibua malalamiko kuhusu iwapo Benki ya dunia inazingatia kanuni zake zinazoelezea kwamba itafadhili nchi zisizokuwa na ubaguzi wa namna yo yote..
Leonard Akwilapo, Katibu katika Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, amesema kwenye mahojiano kwamba serikali imekuwa ikiendesha shughuli zake “kuambatana na mkataba wake na Benki ya Dunia. Mkataba huo unaohusu mradi wa Elimu ambao benki hiyo kwa sasa inafadhili, unataka serikali kuwawezesha wasichana waliopata watoto wakiwa wadogo kupata njia za kuendeleza masomo.” Mwezi Machi Mwaka 2021, Akwilapo alitangaza kwamba vituo 54 vitaanza kuwasajili wanafunzi wa kike wenye mimba na wale ambao sasa ni wazazi kuanzia Januari 2022.
Wasichana waliofukuzwa shuleni wangali wanakumbwa na changamoto ya kufikia masomo hayo na pia ukosefu wa pesa ili kujisajili kwenye vituo vya programu za AEP. Shule za umma za msingi na sekondari hutoa masomo bila malipo, na hali programu za kutoa masomo mbadala kupitia vituo maalum huhitaji karo. Programu za masomo zinaweza kuhitaji takriban dola $150 kwa mwaka, kulingana na stakabadhi za miradi za Benki ya dunia. Stakabadhi hizo zinaonyesha kwamba vituo vya masomo mbadala vya AEP hupokea tu “idhini ya kutotozwa ushuru” kwa karo ili kuwafaa “wasichana walio hatarini.”
Utafiti uliofanywa na TENMET, shirika liliso la serikali nchini Tanzania linaloshughulikia masuala ya elimu, ulibaini kwamba safari ndefu ya kufikia vituo hivyo, na kujengwa kwenye maeneo ya miji, na gharama za kuvifikia imekuwa changamoto kuu kwa wasichana. Baadhi ya wasichana walisema kwamba kutokana na hali yao ya maisha, na muda ambao wamepoteza wakiwa nje ya shule, itafaa kama wangekamilisha masomo ya sekondari kupitia vituo mbadala au wapokee mafunzo kuhusu mbinu za kuanzisha biashara wajitegemee kwa shughuli ndogo ndogo za kibiashara. Lakini wengi walisema wanapitia ugumu kwa sababu wanalazimika kulipia karo na vilevile gharama za usafiri wa kila siku. Baadhi walisema wanaona hawawezi kuendeleza masomo kwa sababu hawakuwa na mtu wa kuwasaidia kuwatunza watoto.
Malika M. wa umri wa miaka 21 sasa, alisema: “Ningependa kurudi shule – hata ikiwezekana kesho. Nikipata mtu wa kunisaidia kulipa karo, nitarudi shule maana kwa sasa sijarudi kwa sababu tuna matatizo ya pesa nyumbani … Vituo hivi [vya mafunzo] vinaitisha karo ya masomo, lakini shule ya zamani niliyosomea haikuwa ikiitisha karo.” Lakini ameelezea masikitiko kwamba hapakuwa na vituo karibu na mahala anapoishi: “Na nikirudi masomoni, kutoka pale ninapoishi, nina hofu huenda nikajipata tena kwenye tatizo lililonifikisha hapa.”
Mpango wa masomo mbadala kwa wasichana wenye mimba unakumbwa na ubaguzi, limesema Shirika la Human Rights Watch. Mnamo mwezi Disemba Mwaka 2019, Mahakama ya Jumuia ya Uchumi ya Mataifa ya Afrika Magharibi (ECOWAS) iliamua kwamba sera za Sierra Leone ambazo zilitoa marufuku kwa wanafunzi wajawazito na wale ambao ni wazazi zilikuwa za kibaguzi. Mahakama hiyo pia iliamua kwamba programu ya serikali kuhusu shule mbadala za kuwafaa wanafunzi waliopata mimba na wengine ambao ni wazazi— inafanana na programu za serikali ya Tanzania za AEP – na kuu zaidi ni kwamba ni za kibaguzi na zinakiuka haki za wasichana kupata masomo.
Mapendekezo
- Afisi ya Rais inayosimamia utawala wa mikoa na serikali za mitaa yafaa kuwaagiza maafisa wote wakome kuwafukuza shuleni wanafunzi waliopata mimba au wale wenye watoto. Vilevile utaratibu wa kuwashtaki wanafunzi kama hao kwa idara ya polisi au wakuu wa wilaya na mikoa wafaa kukoma. Utaratibu huo umekuwa wa lazima nchini Tanzania.
- Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia yafaa:
- Itafute njia za kurekebisha Sheria ya Elimu, na kuandika upya masharti ya Mwaka 2002 ya kuwafukuza wanafunzi, na badala yake kuwe na masharti yanayowalinda wanafunzi ambao wamepata mimba na wale ambao ni wazazi. Yafaa kuiga mifano ya nchi zilizoandaa sheria nzuri zinazohamasisha njia zifaazo na zenye utu.
- Liwe jambo la dharura kuandaa sera ya kitaifa ya kuendeleza masomo, kupata maagizo yafaayo shuleni, na kuanzisha mafunzo ya kitaifa kuhusu mahusiano ya kimapenzi ikiwemo kuandaa mitaala inayowezesha mafunzo hayo kote nchini.
- Komesha shughuli ya lazima ya kuwapima mimba wanafunzi wasichana.
- Hakikisha kwamba wanafunzi wajawazito na wale ambao ni wazazi wanapewa nafasi ya kufanya mitihani ya mwaka ya kidato cha 2 na kidato cha 4.
- Hakikisha kwamba vituo vyote vya kutoa masomo mbadala AEP vinahudumu bila malipo, vilevile hakikisha kwamba vituo hivyo vimejengwa na kupangwa vyema ili kuwafaa wanafunzi ambao ni wazazi- kumaanisha vituo hivyo viwe na njia za kuwafaa watoto.
- Umoja wa Afrika AU, wafaa kuishawishi serikali ya Tanzania kuondoa marufuku kwa wasichana wanaoshika mimba kuendelea na masomo na kutoa wito wa serikali ile ikome kutatiza haki za wasichana hao za kupata elimu. AU yafaa kuishawishi serikali ya Tanzania kuandaa sera ya kuendeleza masomo ili kuhakikisha kwamba wanafunzi waliopata mimba wakiwa shuleni, hasa wale wanaotaka kusoma wanaendeleza masomo yao,- vilevile iwasaidie wasichana ambao ni wazazi kurejea shuleni
- Washirika wa Tanzania wa maendeleo ikiwemo Benki ya Dunia yafaa waishinikize serikali ya Tanzania kukomesha marufuku ya kutoendelea na masomo dhidi ya wasichana wanaopata mimba, na badala yake kutoa wito kwa serikali ile kutunga sera ambazo zitahakikisha kwamba wanafunzi waliopata mimba na wale ambao ni wazazi wanasaidiwa ifaavyo kuendelea na masomo hadi wamalize elimu ya sekondari.