Skip to main content

Tanzania: Mahakama Kuamua juu ya Katazo la Elimu kwa Wanafunzi Wajawazito

Ushauri kutoka Watetezi wa Haki kwenda Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu

The flag of the United Republic of Tanzania. © 2010 TONY KARUMBA/AFP via Getty Images

(Nairobi) – Kesi ya muhimu juu ya katazo la Tanzania dhidi ya wanafunzi wajawazito, walioolewa, au ambao ni kina mama katika Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu inaweza kuathiri kwa kiasi kikubwa haki za wasichana kote Afrika, Initiative for Strategic Litigation in Africa, Women’s Link Worldwide, na  Human Rights Watch wamesema leo. Mashirika hayo matatu ya haki za binadamu yamewasilisha muhtasari wake wa ushauri kwa mahakama mnamo tarehe 17 Juni 2022.

Mwezi Novemba 2020, Equality Now, shirika la kimataifa linalotetea haki za wanawake, na Tike Mwambipile, mkurugenzi mtendaji wa Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania, walifungua kesi ya pamoja dhidi ya serikali ya Tanzania katika Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu, mahakama ya kikanda iliyopo Arusha, Tanzania. Wanatafuta uamuzi wa kimahakama wa kubatilisha katazo la Tanzania la kibaguzi la kuendelea na shule dhidi ya wanafunzi wajawazito, walioolewa au ambao ni kina mama

“Kesi hii inawakilisha hatua muhimu sana kama moja ya kesi katika Mahakama ya Afrika zihusuzo haki za wanawake na wasichana,” alisema Sibongile Ndashe, mkurugenzi mtendaji wa Initiative for Strategic Litigation in Africa. “Kutokuwa na elimu na upatikanaji mdogo wa elimu kwa wasichana barani Afrika una madhara ya muda mrefu kwa mtu binafsi na kwa jamii nzima kwa ujumla na unaweza kuathiri kwa kiasi kikubwa hatma ya maisha ya wasichana.”

Muhtasari wa ushauri umeweka wazi kwamba wajibu wa haki za binadamu wa Tanzania wa kitaifa, kikanda na kimataifa unaitaka kuondoa aina zote za ubaguzi dhidi ya wasichana na wanawake, kuzuia na kukabiliana na aina zote za unyanyasaji dhidi ya wasichana, ikiwa ni pamoja na shuleni, na kulinda afya ya kingono na uzazi na haki za wasichana na wanawake. Mkataba wa Afrika wa Haki na Maslahi ya Mtoto, ambao Tanzania iliupokea na kuufanya sheria mwaka 2003, mahsusi unalinda haki za wasichana wanaopata ujauzito kuendelea na kukamilisha elimu yao ya msingi na sekondari, pasipo kubaguliwa.

Hii ni mara ya pili kwa mahakama ya kikanda ya Afrika kusikiliza kesi ya msingi juu ya katazo la kibaguzi dhidi ya wanafunzi walio wajawazito au kina mama. Mwezi Desemba 2019, katika kesi iliyofunguliwa na muungano wa mashirika ya Sierra Leone na kimataifa, Mahakama ya Haki ya Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) iliamua kwamba marufuku ya nchini Sierra Leone iliyowazuia wasichana na kina mama watoto kuhudhuria shule za umma, iliyokuwepo kwa miaka 10, ilikuwa ya kibaguzi , na ikaamuru serikali kuiondoa. Mahakama iliona pia kwamba shule mbadala za wasichana wajawazito, ambazo nyingi zinafadhiliwa na wahisani, zilikuwa za kibaguzi .

Mashirika hayo, katika ushauri wao, walitoa taarifa za kutosha juu ya madhara ya kijinsia yatokanayo na kuwanyima elimu wanawake na wasichana, ikiwa ni pamoja na uhuru wao, maendeleo na ukuaji wao kimwili, na ukosefu wa muda mrefu wa mzunguko wa mapato na mali.

“Ni muhimu kwa wasichana na wanawake mahali popote wasikumbane na vizuizi vya kimfumo wanapotimiza malengo yao,” alisema  Achieng Orero, mwanasheria mwandamizi wa Women’s Link Worldwide, “Kama jamaa, tunatoa mtazamo wa kimataifa unaosisitiza umuhimu wa haki za kingono na uzazi na uwezo wa wasichana na wanawake katika kujitafutia miradi yao ya maisha, ikiwa ni pamoja na elimu ya juu iwezekanavyo.”

Benki ya Dunia inakadiria kwamba kila mwaka takribani wasichana 6500 wanaacha shule nchini Tanzania – yaani wanaondoka shule  au wanafukuzwa na hawarudi tena katika mfumo rasmi wa kujifunza – kwasababu ni wajawazito. Tarehe 24 Novemba, mwaka mmoja baada ya kesi kufunguliwa, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ya Tanzania ilibadilisha sera hiyo na kuchapisha waraka ukisema kwamba wasichana wajawazito na wale ambao ni kina mama wanaruhusiwa kurudi katika shule za umma kuendelea na masomo yao. Tanzania ilikuwa miongoni mwa nchi chache barani Afrika ambazo zilipiga marufuku wasichana waliopata ujauzito au kina mama katika shule zake.

“Tunafahamu kutoka kazi za Human Rights Watch ulimwenguni kote kwamba kuwakatalia wasichana wajawazito na kina mama watoto haki zao za kusoma katika shule za umma zinaathiri haki zao za binadamu na maisha yao ya baadae,” alisema Mausi Segun, Mkurugenzi wa Afrika wa Human Rights Watch. “Mahakama ya Afrika ina fursa ya pekee kuzingatia hatua za kimageuzi zinazoweza kusaidia kurekebisha upotevu wa kudumu wa elimu, unyanyapaa, na ubaguzi unaowakabili wasichana wanaotengwa kiholela shuleni.”

Wanasheria wanaoisimamia kesi hii kwa niaba ya mashirika, Nyokabi Njogu na Achieng Orero, ni wanasheria wa Feminist Litigation Network (FLN) ya Initiative for strategic Litigation. Kupitia kazi zao kama wanasheria wa mtandao huo, wana nafasi ya kipekee kuimarisha ujuzi wao katika kutetea kiumahiri na kikamilifu juu ya haki za binadamu za wanawake.

Your tax deductible gift can help stop human rights violations and save lives around the world.

Region / Country