Skip to main content

(Nairobi) – Ukandamizwaji unaofanywa na serikali za mataifa ya Afrika Mashariki katika maandamano ya amani na uhuru wa kujieleza ulitishia na kuhujumu haki za kibinadamu katika kanda hii mwaka wa 2016, Human Rights Watch imesema leo katika  Ripoti Yake ya Ulimwengu ya 2017.

Vikosi vya ulinzi vya serikali ya Uhabeshi (Ethopia), pamoja na vya mataifa ya Uganda na Kenya, vilitumia nguvu kupita kiasi na kwa njia zisizo stahili kuyatawanya maandamano ya amani na kusababisha vifo na majeraha. Nchini Ethiopia mamia ya waandamanaji waliuawa mwaka wa 2016. Serikali za mataifa ya Afrika Mashariki pia zilitumia mbinu kadha wa kadha kuzuia ukosowaji wa sera za serikali na kuzuia utendakazi wa wanahabari, haswa kwa kutumia nguvu, kukamatwa kiholela na kuwafungulia mashtaka ya kihalifu. Katika kanda hii, serikali zilishindwa kuchunguza na kuwafungulia mashtaka wale maafisa wa kijeshi waliohusika katika dhulma dhidi ya haki za kibinadamu. Wakimbizi, haswa nchini Kenya, walikabiliwa na tishio la kurudishwa makwao kwa lazima.

Maafisa wa usalama waliokuwa wamejihami waliwatazama waandamanaji waliokuwa wakiandamana dhidi ya serikali wakati wa sherehe za kitamaduni za Irreechaa huko Bishoftu, Uhabeshi tarehe mbili Octoba 2016. © 2016 Getty Images


“Katika mwaka wa 2016, Serikali za mataifa ya Afrika Mashariki zilionyesha kutojali haki za kimsingi za wananchi wao za uhuru wa kujieleza na kujumuika pamoja,” alisema Maria Burnett, mkurugenzi msaidizi wa Afrika katika Human Rights Watch. “Ushikaji doria na ukandamizaji wa haki za makundi ya waandamanaji huko Uhabeshi yaliyoshuhudiwa, ni mojawapo wa visa vya ukiukwaji wa haki za kibinadamu usiotajika katika kanda hii.”

Katika ripoti ya ulimwengu yenye kurasa 687, toleo lake la 27, shirika la kutetea haki za kibinadamu la Human Rights Watch limeweza kuhakiki mienendo ya haki za kibindamu katika mataifa zaidi ya tisini (90). Katika maelezo yake ya utangulizi, Mkurugenzi Mkuu Kenneth Roth ameandika ya kuwa kizazi kipya cha uongozi wa kiimla unaoungwa mkono na wengi unajaribu kuipindua ile dhana ya ulinzi wa haki za kibinadamu, na kuyachukulia maswala ya haki za kibinadamu kuwa kama kizuizi kwa nia ama maono ya wale walio wengi nchini mwao. Kwa wale ambao wanahisi kuachwa nyuma katika Uchumi wa ulimwengu na kuzidi kuyaogopa mashambulio ya kimabavu, mashirika ya kibinadamu, vyombo vya habari na umma kwa jumla yana majukumu ya kutekeleza ili kuhakiki yale maadili ambayo mataifa ya kidemokrasia yameyajenga na kuyaimarisha kwa miaka iliyopita.

Serikali katika eneo hilo zinashindwa mara kwa mara kuchunguza dhuluma zinazofanywa na vikosi vya ulinzi vya mataifa hayo, na hivyo basi kuhujumu uwezekano wa waathiriwa kudai fidia, Human Rights Watch ilisema. Nchini Uhabeshi vikosi vya ulinzi Viliyakandamiza kwa nguvu maandamano mengi dhidi ya sera za serikali, na kuishia kuwaua mamia ya watu na kuzuia makumi ya maelfu ya watu. Serikali baadaye iliweza kutangaza hali ya usalama  kote. Hali hio ya taharuki ilikuwa na maafa kwa haki za kibinadamu. Hilo lilitokana na kukanyagana na kuumuzana katika tamasha la kitamaduni lililosababishwa na vikosi vya usalama kuingia na kuwatawanya kwa fujo halaiki ya watu. Serikali ya Uhabeshi imeshindwa kuchunguza kwa umakini mauaji ya waandamanaji hao na dhuluma zingine.

Nchini Kenya, vikosi vya ulinzi vilisababisha kutoweka kwa lazima kwa watu angaa 34 katika kipindi cha  miaka miwili iliyopita katika oparesheni za kupambana na ugaidi eneo la Kaskazini Mashariki mwa Kenya na Nairobi. Wawili kati yao waliweza kuachiliwa hatimaye, ingawaje mmoja wao alishtakiwa kwa kosa la ugaidi. Polisi wa Uganda na maafisa wa jeshi waliwaua watu angaa 13 katika kile kinachokisiwa kuwa udumishaji wa sheria na kuwatia mbaroni wale wanaokiuka sheria kwenye eneo la Magharibi kule Ruwenzori. Nchini Somali, vurugu ambazo zilichochewa kisiasa ziliwaathiri pakubwa wananchi.

Migogoro na kuteswa kwa wananchi kule Sudan Kusini, Somalia na Burundi miongoni mwa nchi nyingine, kulisababisha nchi za Afrika Mashariki kuishia kuwa wenyeji wa wakimbizi maelfu ya mamia na kuzua hisia mseto Wakati Uganda imetafuta mbinu za kuwapokea na kutangamana na wakimbizi, ilhali serikali ya Kenya imekiuka majukumu yake yaliyomo katika sheria za Kimataifa zinzowalinda wakimbizi (International Refugee Law) kwa kutangaza azimio lake la kufunga kambi ya wakimbizi ya Daadab, inayowatumikia wakimbizi haswa wenye asili ya Kisomali. Uamuzi huo ulisababisha wakimbizi maelfu wa Somali kurudi nyumbani, licha ya makabiliano ya kivita yayanayoendelea kule, na wakawaacha wale waliosalia wakiwa wenye hofu juu ya usalama wao na siku za usoni.

Vitisho na vurugu vilivyopangwa na serikali na kuelekezwa katika vyombo vya habari vinabakia kuwepo sana Afrika Mashariki. Wanahabari kadha huru nchini Eritrea wamekuwa katika vizuizi vya pweke tangu Septemba 2001. Hakuna yeyote kati yao ambaye ameshtakiwa na kufunguliwa mashtaka na hakuna magazeti huru yanayochapishwa kule. Uhabeshi pia iliwazuilia wanahabari na wanabloga, mara nyingi chini ya vifungu vya sheria vya Kupambana na Ugaidi, na wengi wanabakia vizuizini. Serikali ya Uhabeshi ilizuilia upeperushwaji wa vipindi vya vituo vya televisheni vya kigeni na kuzuia ishara na mawasiliano ya vituo vya redio vya kimataifa kama vile Deutsche Welle na Voice of America.

Nchini Somalia, mamlaka ya shirikisho na kimaeneo na kundi lile la wapiganaji wa Kiislamu la Al Shabab liliweza kutekeleza mashambulizi yaliyolenga vyombo vya habari, ikiwemo pia unyanyasaji, na udhalilishaji. Angaa wanahabari wawili waliuawa katika mashambulizi yaliyowalenga wanahabari. Mnamo Mei, mahakama moja ya Kenya ilitangaza kuwa sehemu ya Kifungu cha Sheria ya Habari na Mawasiliano ambacho polisi walikuwa wakikitumia kuwakamata na kuwashtaki wanahabari kuwa kakikuambatana na kanuni za kikatiba.

Katika uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2016 kule Uganda, watumishi wa serikali na polisi walikamata na wakapiga zaidi ya wanahabari kumi na wawili – na wakati mwingine katika hali ya kupeperusha matangazo hewani. Angaa wanahabari na mabloga wanane wa Kenya walikamatwa na kushtakiwa kwa makosa yaliyobuniwa kwa njia isiyoeleweka kwa mujibu wa sheria mpya ya nchi hiyo. Katika mataifa ya Uhabeshi na Uganda, wakati ambapo serikali zilikosolewa sana, mamlaka yalizuia matumizi na huduma za mitandao  na mitandao ya kijamii wakisema kwamba kuzuia huko kulihitajika kwa ajili ya “sababu za kiusalama.”

Wakati mwingine, serikali pamoja na mahakama zilichukua hatua chanya kuboresha njia za kuwafidia waathiriwa wa dhuluma dhidi ya haki za kibinadamu. Rais wa Somalia alitia sahihi sheria inayobuni tume ya kitaifa ya haki za kibinadamu ambayo inaweza kupokea malalamishi na kufuatilia hali ilivyo katika magereza na hata sehemu za kuzuia watu bila kufuata sheria. Wachunguzi hao wanastahili kuwa na uwezo wa kuyatembelea magereza bila ya ilani ama idhini wakati wowote. Nchini Uganda, Mahakama ya  kikatiba ilitoa uamuzi na kusema kwamba kile kifungu cha sheria ya Tume ya Fursa Sawa kilikuwa kinyume na katiba kwani kiliiruhusu Tume kukataa malalamishi ya watu wanaodhaniwa kuwa “hawakubaliki kimaadili au kijamii” na wale walio wengi.

“Kwa kusingizia usalama, misururu ya udhalimu imeenea kote katika Afrika ya Mashariki. Hili limesababisha kutengwa kwa watu na jamii ambazo zilikuwa zimetengwa tayari,” Burnett alisema. “Serikali kwenye eneo na wabia wake wake wa kimataifa wanastahili kushika hatamu dhidi vikosi vya dhuluma na kukipa kipao mbele uwajibikaji na stahamala hasa kwa maoni mseto yanayotolewa na watu mbalimbali.”

Your tax deductible gift can help stop human rights violations and save lives around the world.