Leo tarehe 23 Juni, ni Siku ya Wajane Kimataifa, ni siku ambayo mataifa duniani kote yanatambua vurugu, ubaguzi na unyanyapaaji unaofanywa dhidi ya wajane na kusherehekea mchango muhimu wa wajane. Ni siku ambayo serikali zote ikiwemo ya Tanzania zinatakiwa kuchukua hatua za makusudi kulinda haki za wajane.
Mwaka jana, yalifanyika maamuzi ya kihistoria ambapo kamati ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia haki za wanawake iligundua ukiukwaji wa haki za wajane uliofanywa na Serikali ya Tanzania. Wajane wawili, waliofungua majalada ya kesi kwa majina ya E.S na S.C, walipeleka kesi zao Umoja wa Mataifa baada ya mahakama za Tanzania kukataa madai yao ya haki sawa katika kurithi na kusimamia mali. Kamati ya Umoja wa Mataifa iligundua matatizo kadhaa kwa wanawake hawa na katika mfumo mzima wa sheria za Tanzania.
Hata hivyo ni mwaka sasa umepita tangu Tanzania iahidi kurekebisha matatizo hayo. Hatua za haraka zinahitajika ili kuwezesha wajane kupata haki zao.
Mume wa E.S alifariki dunia mwaka 1999. Shemeji yake alimfukuza nyumbani na kumlazimisha yeye na watoto wake wadogo watatu kuhamia kwa wazazi wake. S.C na mwanae mchanga waliachwa katika hali kama hiyo punde baada ya mumewe kufariki mwaka 2000 na wakwe zake kuchukua nyumba na mali nyingine.
Chini ya sheria za kimila katika mkoa wa Shinyanga ambapo wanawake hawa walikua wanaishi, wajane hawana haki ya kurithi kutoka kwa waume zao kama kuna mtoto wa kiume au ndugu wa damu wa mume. Sheria za kimila katika mkoa huo ambazo zilisimbikwa mwaka 1963, zinaeleza kwamba mjane “ hana mgao wa mirathi kama marehemu ameacha ndugu wa ukoo wake; mgao wake husimamiwa na wanawe kama anavyo watunza .” Sheria za kimila humtaka mrithi wa marehemu kumtunza mjane, lakini kiuhalisia, ndugu wa marehemu humfukuza mjane katika ardhi yao. Sheria za kimila pia huzuia wajane kusimamia mali zisizohamishika: husema kwamba mali hizo lazima zisimamiwe na kaka mkubwa wa marehemu, baba au ndugu wa kiume, au dada pale ambapo hakuna ndugu wa kiume. Hakuna mwanamke ambae anaweza kurithi au kumiliki ardhi ya ukoo, ikiwa ni pamoja na wajane.
Hali ni tofauti kwa wanaume, ingawa sheria za kimila zinatoa hisia kwamba mwanaume harithi kutoka kwa marehemu mkewe. Tume ya Marekebisho ya Sheria Tanzania inadokeza kwamba mwanaume hana haja ya kurithi kwa sababu ya dhana ya kimila kwamba “ mume pekee ndiyo mwenye maslahi katika mali ambayo imepatikana kwa pamoja na wanandoa katika kipindi cha ndoa.” Makala katika jarida la sheria juu ya mirathi Tanzania, inainukuu Tume ikisema kwamba dhana hii ndio inayopelekea kutokuwa na umuhimu wa kumteua mwanaume kuwa msimamizi wa mali au kugawa mirathi wakati wa kifo cha mke. Mume hana haja ya kurithi. Mke anapofariki tayari mume humiliki kila kitu. Mume anapofariki, mke hamiliki chochote na hivyo huhitaji kurithi kwa hali na mali ili kuendelea na maisha.
Katiba ya Tanzania inatambua na kulinda haki za wanawake. Ibara ya 13 inatoa dhamana ya usawa wa wanawake chini ya sheria bila ubaguzi wa kijinsia, na ibara ya 107A (2) inatoa dhamana ya fidia kwa waathirika wa uvunjifu wa sheria. Kwa kuzingatia hayo, E.S na S.C walitafuta msaada katika mahakama za Tanzania. Mahakama Kuu ilikuwa inatambua kwamba sheria za kimila zina ubaguzi dhidi ya wajane lakini hata hivyo ilikataa madai yao mwaka 2006. Mahakama ya Rufaa ilichukua miaka minne kusikiliza kesi na kisha kuitupilia mbali kwa sababu za kitaalamu.
E.S na S.C hawakukata tama. Wakiwakilishwa na Kituo cha Msaada wa Kisheria kwa Wanawake Tanzania, na Kliniki ya Kimataifa ya Haki za Wanawake ya Chuo cha Sheria cha Georgetown, Washington DC, wajane hawa walifikisha kesi zao mbele ya Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Kutokomeza Ubaguzi dhidi ya Wanawake ( Kamati ya CEDAW).
Katika maamuzi ya mwaka 2015, Kamati ya CEDAW iligundua kwamba serikali ya Tanzania ilikiuka haki za wajane hawa kwa kuwanyima “usawa katika kurithi na kushindwa kuwapatia aina nyingine ya suluhisho.” Pia iligundua kwamba mahakama za Tanzania zilikiuka haki za wajane hawa kupata haki za kisheria na fidia. Kamati ilipendekeza serikali ya Tanzania kufidia wajane wote wawili kwa kukiuka haki zao na kutoa wito wa marekebisho ya katiba na sheria za kimila na kuchukua hatua za vitendo kutokomeza ubaguzi wa aina hii.
Zaidi ya mwaka mmoja baadaye, Tanzania haijalipa fidia yoyote na wanasheria wanawake wanasema serikali haijapiga hatua juu ya marekebisho mapana ya sheria. Mwezi Machi, Kamati ya CEDAW kwa mara nyingine iliitaka Tanzania kuchukua hatua za haraka juu ya haki za wajane.
Mwezi Aprili, Taasisi inayoangalia Haki za Binadamu ilituma barua kwa serikali ikisisitiza kuchukua hatua. Muda mfupi baadaye, habari ziliripoti zikimnukuu Waziri wa mambo ya Nje, Dkt. Augustine Mahiga akisema kwamba haki za wanawake kurithi ni suala muhimu na kwamba serikali itafanyia marekebisho sheria husika. “ Ni suala ambalo linahitaji msukumo na tunahitaji kuliharakisha,” alisema Waziri.
Ni kipi kinachozuia?
Tanzania inapaswa kutambua wajibu wake wa kisheria chini ya mkataba lakini pia kufanya jambo sahihi kwa Taifa: kufidia wajane hawa na kuhakikisha kwamba wanawake na wanaume wanaweza kurithi na kusimamia mali kwa usawa.
Ni matumaini yetu kwamba katika Siku ya Wajane Kimataifa mwaka ujao Tanzania itakua na sababu za kusherehekea.