Serikali ya Kenya inapaswa kuusitisha mpango wake wa kuwatoa kwa nguvu wakimbizi na wale wanaotafuta hifadhi wanaokaa katika majiji na kuwarudisha kwenye makambi ya wakimbizi. Kwa jumla watu hawa ni hamsini na tano elfu.
Makambi yenyewe hayana hudumu muhimu ya kimsingi pamoja na kujaa kupita kiasi. Serikali inataja visa vingi vya vilipuzi au mabomu katika mwaka wa 2012 kama sababu ya mpango huu na inafikiria kuwa hatua hii itaboresha usalama wa kitaifa wa Kenya pamoja na kuwafanya wakimbizi kutoka Somali kurudi Somali.
Mpango huu ukitekelezwa utakiuka haki ya uhuru wa kutembea na kwa kiwango kikubwa utajumuisha kufukuzwa kwa maelfu ya wakimbizi kutoka katika nyumba zao. Shirika linalotetea haki za binadamu la Human Rights Watch lilisema kuwa hali mbaya sana katika makambi ya wakimbizi ambayo imedumu kwa muda mrefu inamaanisha kuwa kurudishwa kwa wakimbizi katika makambi kutaathiri uwezo wao wa kuchuma riziki na kupunguza nafasi zao za kupata chakula cha kutosha, mavazi, makao, huduma za afya na elimu.
"Kenyainatumia visa vya vilipuzi vya hivi majuzi kuwachukulia wakimbizi wote kama magaidi na kuwalazimisha maelfu wao kurudi kwenye makambi ambayo tayari yako katika hali mbaya sana pamoja na kuwa na idadi kubwa ya watu kupita kiasi." Haya yalisemwa na Gerry Simpson ambaye ni mtafiti mkuu katika maswala ya wakimbizi na wakili wa Shirika la Human Rights Watch. “Mpango wa kuwahamisha maelfu ya watu kutoka kwenye majiji ni kinyume na sheria na utasababisha taabu nyingi mno."
Mnamo tarehe 13 Disemba, serikali ya Kenya ilisema kuwa mpango wa kuwahamisha wakimbizi walioko mijini hadi kwenye makambi umetokana na visa vya mashambulizi vilivyotekelezwa na watu wasiojulikana kwa kuwatupia halaiki vilipuzi au makombora katika sehemu mbalimbali na kuwaua pamoja na kuwaaumiza wengine wengi wakiwemo polisi na wanajeshi.
Mnamo tarehe 16 Januari 2013, Wizara ya Utawala wa Mikoa na Usalama wa Ndani iliiandikia Wizara ya Mradi Maalum ikisema kuwa awamu ya kwanza ya msako ingeanza tarehe 21 Januari na iliwalenga watu 18,000 na iliendelea kuwa wangepelekwa katika uwanja wa michezo wa Manispaa ya Thika na wangewekwa kule wakisubiri kupelekwa katika makambi.
Mashirika na mawakili wanaowashughulikia wakimbizi katika jiji la Nairobi wamesema kuwa toka Disemba, polisi jijini Nairobi wamewakamata Wasomali wengi na kuwasingizia kuwa ni wanachama wa makundi ya kigaidi. Wote waliopelekwa kortini waliachiliwa kwa sababu serikali haikuwa na ushahidi.
Mnamo Mei 2012 shirika la Human Rights Watch liliripoti kuhusu visa vibaya sana vya unyanyasaji vilivyotekelezwa na vikosi vya usalama katika eneo la kaskazini mwa Kenya dhidi raia baada ya visa vya vilipuzi au makombora vilivyowaua maafisa wa usalama. Jeshi la Kenya liliahidi kukomesha visa hivyo vya kulipiza kisasi pia liliunda kamati la kuchunguza unyanyasaji ule. Shirika hili lina wasiwasi kuwa vikosi vya usalama bado vitatumia nguvu nyingi wakiwakamata na kuwasafirisha wakimbizi hadi kwenye makambi.
Mpango huu ukitekelezwa utakiuka wajibu wa kisheria wa Kenya kimataifa na kitaifa, shirika la Human Rights Watch liliongezea. Wajibu huu unaihitaji Kenya kuthibitisha kuwa kuuzuia uhuru wa kutembea ndio njia mwafaka zaidi inayoweza kuchukuliwa kuishughulikia hali ya usalama wa kitaifa Kenya.
Katika ripoti yake ya mwaka wa 2010 itwayo Welcome to Kenya, shirika la Human Rights Watch lilihitimisha kuwa matakwa ya Kenya kwamba wakimbizi nusu milioni wakae makambini ilienda kinyume na wajibu wake wa kisheria wa kuwahakikishia wakimbizi uhuru wa kutembea.
“Mpango wa Kenya wa kuwahamisha wakimbizi hamsini na tano elfu hadi makambini hauhitajiki wala haufai kama hatua ya kukabiliana na mashambulizi ya hivi karibuni.” Simpson alisema. “Kenya haipaswi kuwachukulia wakimbizi wote kama hatari/tishio la usalama hivyo basi kuipuuza haki za watu hamsini na tano elfu”.
Kwa mujibu wa shirika linalowashughulikia wakimbizi la United Nations High Commissioner for Refugees (UNHCR), hadi mwisho wa mwaka wa 2012 wakimbizi 46,540 walikuwa wameandikishwa nchini Kenya katika miji mbalimbali pamoja na wasomali 33,246 na wengine 6,832 raia wa nchi mbalimbali walioandikishwa na wanatafuta hifadhi waliotoka katika nchi mbalimbali pamoja na wasomali 447 walikuwa wakiishi Kenya.
Mnamo tarehe 13 Disemba idara ya maswala ya wakimbizi nchini Kenya ilitoa ripoti kwa vyombo vya habari kuwa serikali ilikuwa ikibuni sera ya kuunda kambi kwa sababu ya hali mbaya isiyovumilika wala dhibitika ambayo pia ilitishia usalama wa kitaifa. Hali hii iliyosababishwa na mashambulizi kwa makombora yaliyotekelezwa barabarani, makanisani, na vituo vya biashara yamewaua na kuwaumiza wengi.
Inasemekana kuwa wote wanaotafuta hifadhi pamoja na wakimbizi kutoka Somalia ambao wanaishi mijini wanapaswa kuhamia kambi la wakimbizi lililoko Dadaab karibu na mpaka wa Somalia na wote wanaotafuta hifadhi pamoja na wakimbizi kutoka nchi nyingine wanapaswa kuhamia kambi la wakimbizi la Kakuma karibu na mpaka wa Sudan.
Inasemekana kuwa uandikishaji wa wanaotafuta hifadhi na wa wakimbizi umesitishwa na vituo vya uandikishaji vimefungwa na kuwa shirika la UNHCR na mashirika mengine yanayowahudumia moja kwa moja yakome kuwahudumia.
Katika mkutano na wanahabari wa tarehe 13 Disemba kaimu afisa anayeyasimamia maswala ya wakimbizi, Badu Katelo, alisema kuwa uandikishaji wa wakimbizi na wanaotafuta hifadhi ulikuwa umesitishwa na kama wataendelea kukaa katika miji watafanya hivyo kinyume na sheria na kukamatwa na kutolewa katika miji ni jukumu la idara nyingine ya serikali labda ile ya polisi na ile ya uhamiaji.
Tangu Disemba UNHCR pamoja na mashirika mengine yameiomba idara za serikali nakala ya hati ambayo amri ile ya tarehe 13 Disemba ilijikita kwake bila mafanikio yoyote.
Toka mpango ule utangazwe, mashirika yasiyo ya kiserikali, mawakili wa wakimbizi katika jiji la Nairobi wanasema kuwa polisi wamewakamata kiholela raia wa Somalia na wengi wao wameachiliwa baada ya kutoa kiasi kikubwa cha rushwa. Ripoti kutoka ubalozi wa Somalia kampuni za ndege na wafanyakazi wa mashirika yanayotoa misaada katika mpaka kati ya Kenya na Somalia karibu na Dadaab zinasema kuwa tangu Disemba zaidi ya wakimbizi elfu moja wamekuwa wakirudi Somalia kila wiki kwa ndege au barabara. Wengine waliwaambia wafanya kazi wa mashirika yanayotoa misaada kuwa waliondoka kwa sababu waliogopa kuchukuliwa hatua kali ya kinidhamu nchini Kenya.
Mwisho wa Disemba shirika la Human Rights Watch pia lilipokea ripoti kuhusu kuongezeka katika visa vya dhuluma za kingono dhidi ya wanawake na wasichana katika kambi moja kule Daadab. Chanzo cha kuaminika kililiambia shirika hili kuwa polisi hawajakabiliana vilivyo na visa hivyo. Mashambulio haya yamesababisha uoga hali ambayo imewafanya mamia ya wakimbizi kutoka makambini na kuvuka mpaka na kuingia Somalia. Wengine wao wamehamia pembeni mwa makambi mengine karibu na Dadaab. Katika mwaka wa 2010 shirika lili hili lilitoa ripoti kuhusu polisi wa Kenya kukosa kuchunguza kwa muda mrefu swala la dhulma za kingono katika makambi ya Dadaab.
Katika mkutano na vyombo vya habari wa tarehe 13 Disemba, kamishna Katelo alisema kuwa kuwahamisha wakimbizi hadi kwenye makambi kutafuatiliwa na kuwarudisha wakimbizi kutoka Somalia makwao Somalia. Baadaye tarehe 21 Desemba, Rais Mwai Kibaki alisema kuwa ,” hakuna heshima katika kuishi kwenye makambi ya wakimbizi na kwamba nchi za Somalia na Kenya zitafanya kazi pamoja ili kuwawezesha mamia ya wakimbizi wa Somalia wanaoishi katika makambi ya wakimbizi kurudi makwao.
Shirika la Human Rights Watch lilisema kuwa hali katika eneo la kusini mwa kati ya Somalia bado halina usalama na kwamba hatua zozote za serikali ya Kenya ya kuwalazimu au kuwahimiza Wasomali kurudi Somalia itaivunja sheria ya Kenya na zile za kimataifa zinazopiga marufuku kuwarudisha wakimbizi kwa lazima katika maeneo ya mateso , mauaji na vurugu.
Hali duni sana katika makambi ya wakimbizi kule Dadaab ambamo zaidi ya wakimbizi 450,000 wamejazwa katika eneo lililonuiwa kuwachukua watu 170,000 , ukosefu wa makambi mapya yaliyojengwa vizuri karibu na Dadaab au Kakuma inamaanisha kuwa kuwahamisha wakimbizi kutoka mijini, Kenya itakosa kuyatimiza majukumu yake ya kisheria ya kimataifa. Majukumu haya yanahitaji Kenya isichukue hatua zozote zinazotatiza haki za wakimbizi ya kupata hali ya maisha inayofaa kama kupata chakula, mavazi, makao pamoja na huduma za afya na elimu.
Tarehe 28 Desemba shirika la Doctors Without Borders (MSF) linalosimamia huduma mbailimbali za afya katika makambi lilisema kwamba kwa sababu ya idadi kubwa ya watu kupita kiasi makambini hali ya afya na ya kibinadamu ya wakimbizi katika Dadaab tayari ilikuwa changamoto kubwa na ya kuogofya na shirika la MSF lilikuwa na wasiwasi mwingi kuhusu athari za kuongezeka kwa idadi ya wakimbizi makambini.
Human Rights Watch pia lilisema kuwa kuwalazimu maelfu ya watu kiholela kutoka makwao jijini ni kama kuwafukuza kwa lazima ambayo ni kinyume na sheria ya kimataifa.
Shirika hili liliyaomba wafadhili wa kimataifa na lile la UNCHR kuupinga hatua hii kwenye misingi ya kukiuka haki za wakimbikizi ya uhuru wa kutembea, haki za kimsingi za kijamii na kiuchumi na ya kutohamishwa kwa nguvu.
“Mpango huu utazivunja baadhi ya haki muhimu za wakimbizi na kuchangia ukosefu wa usalama ambao Kenya inasema inakabiliana nao,” Simpson alisema.
“Wafadhili wa kimataifa kwa Kenya na UNHCR wanapaswa kushawishi Kenya kuacha mpango huu.
Kwa maelezo ziadi kuhusu matatizo ya wakambizi kwenye makambi ya wakimbizi na jinsi mpango huu utakavyokiuka majukumu ya kisheria ya Kenya ya kimataifa ukitekelezwa, tafadhali soma hapa .
Kusoma ripoti ya Human Rights Watch ya Juni 2010, Welcome to Kenya: Police Abuse of Somali Refugees,” tafadhali angalia:
https://www.hrw.org/reports/2010/06/17/welcome-kenya-0
Kusoma ripoti ya Human Rights Watch ya Machi2009, “From Horror to Hopelessness: Kenya's Forgotten Somali Refugee Crisis,” tafadhali soma:
https://www.hrw.org/reports/2009/03/29/horror-hopelessness
Kusoma ripoti ya Mei 2012 Human Rights Watch report,“Criminal Reprisals: Kenyan Police and Military Abuses Against Ethnic Somalis,” tafadhali angalia:
https://www.hrw.org/news/2012/11/22/kenya-end-security-force-reprisals-north
Kwa maelezo zaidi kuhusu jinsi Kenya inavyowashughulikia wakimbizi kutoka Somalia tafadhali soma:
https://www.hrw.org/africa/kenya
Mazingira Mabaya Wanamoishi Wakimbizi Katika Makambi ya Wakimbizi ya Dadaab na Kakuma.
Shirika la Human Rights Watch lilisema kuwa makambi ya wakimbizi ya Kakuma na Dadaab hayafai kuwahamishia wakimbizi kutoka majiji ya Kenya. Tangu mwaka wa 2007, makambi haya ambayo shirika la UNHCR linasema yana uwezo wa kuwabeba watu 160,000 ingawa sasa hivi yana watu 450,000 yamekuwa na changamoto nyingi kwa muda mrefu. UNHCR linasema kuwa asilimia 96 ya wakimbizi katika makambi haya ni wasomali ilhali kambi la Kakuma lina wakimbizi zaidi kwa asilimia 10.
Katika mwezi wa tatu mwaka wa 2009, Human Rights Watch liliripoti kuhusu shida kubwa katika makambi ya wakimbizi ya Dadaab Kaskazini mwa Kenya. Makambi haya yalijengewa wakimbizi tisini elfu ingawa yalikuwa na idadi ya wakimbizi250,000. Vilevile mwaka huu wa 2009 shirika la UNHCR liliomba msaada wa dola za Marekani 92 ingawa lilipata kama dola za Marekani milioni 30 tu.
Na kutoka wakati ule idadi ya wakimbizi walioandikishwa imeongezeka maradufu na mpaka mwanzo wa Januari 2013 idadi ya wakimbizi kambini ilikuwa 450,000 katika ardhi iliyotengewa watu 170,000.
Mashirika yanayotoa misaada yanasema kuwa makambi yamekuwa yakikumbwa na shida moja baada ya nyingine nayo bajeti ya UNHCR daima haifadhiliwi vilivyo.
Kama njia ya kupunguza idadi ya watu makambini katikati ya mwaka wa 2011, serikali ya Kenya ilifungua kambi ya nne inayoitwa ifo 2 linalowabeba watu 70,000 ingawa lina uwezo wa kuwachukua watu 80,000.
Kwa sababu ya ukosefu wa nafasi makambini, maelfu ya wakimbizi wanaendelea kuishi nje ya yale makambi manne ambako wanatatizika kupata huduma hata zile za kimsingi kabisa.
Tangu katikati ya mwaka wa 2011, wakimbizi 18,000 pia wamehamia kambi la tano linaloitwa Kambios karibu na Dadaab.
Mnamo tarehe 18 Januari mwaka huu, shirika la UNHCR lilisema kuwa serikali ya Kenya ilikubali kulitambua Kambios kama kambi la tano. Kambi hili lina uwezo wa kuwachukua watu 20,000 ingawa shirika la UNHCR linasema kuwa likitengezwa vizuri kwa gharama ya mamilioni ya dola linaweza kuwachukua watu 80,000. Kambi hili linahitatji mamilioni ya dola kila mwaka kuliendesha.
UNHCR linasema kuwa wakimbizi katika kambi la Kambios wanapata msaada mdogo sana kwa mfano hawapokei chakula ,wanapata elimu na huduma za afya za hali ya chini katika vibanda. Hakuna soko la wakimbizi kulifanyia biashara na kupata hela za ziada pia hakuna kituo cha polisi.
Kambi la Kakuma katika wilaya ya Turkana Kaskazini Mashariki mwa Kenya vilevile ina idadi ya watu kupita kiasi. Hivi sasa lina watu 107,205 ingawa ilinuiwa kuwachukua watu 100,000.
Nusu yao ni Wasomali nayo asilimia 30 ni raia wa Sudan Kusini.
Kutoka mwaka wa 2012 shirika la UNHCR limekuwa likijadiliana na idara mbalimbali za serikali zikubali kambi la pili lifunguliwe karibu katika eneo la Kalobei na mnamo tarehe 18 Januari UNHCR lilisema kuwa idara zilikubali kuwa kambi lijengwe. UNHCR linakadiria kuwa ujenzi utagharimu dola za Marekani milioni 15 na litaweza kuwachukua watu elfu ishirini na mamilioni zaidi ya kulipanua hadi liweze kuwachukua watu elfu hamsini na kuliendesha kila mwaka.
Haki ya wakimbizi ya kutembea kwa uhuru.
Toka mwanzo wa miaka ya 90, Kenya imeweka sera isiyo rasmi inayowahitaji wengi wa wakimbizi kukaa katika makambi haya. Juni 2010 shirika la Human Rights Watch liliripoti kuwa sera ambayo sasa inawaathiri wakimbizi na wanaotaka hifadhi 560,000 makambini inakiuka haki za bindamu za Kenya na za kimataifa na sheria ya wakimbizi inayowahakikishia haki ya kutembea kwa uhuru katika nchi.
Chini ya sheria ya kimataifa na ile ya Kenya lazima ithibitike kuwa kuwaweka wakimbizi kambini ndio ya njia mwafaka zaidi inayohitajika kuulinda usalama wa kitaifa, utangamano katika umma,hali ya afya ya umma ambayo haijawai kuwatolea wakimbizi 560,000 waliolazimika kuishi Kenya kwenye makambi pia kuwa sera hiyo haitawabagua Wakenya na raia wa nchi nyingine.
Shirika la Human Rights Watch limesema kuwa idara mbalimbali za serikali hazijadhibitisha kuwa kuwazuilia wakimbizi kambini ndiko njia bora zaidi ya kuushughulikia usalama pia ni wazi kuwa itawabagua Wakenya na wakimbizi kwa sababu sera hii inawaruhusu Wakenya kutembea kwa uhuru na kuwanyima wakimizi haki hii.
Haki ya wakimbizi ya kufurahia haki yao ya kijamii na kiuchumi na kupiga marufuku kuhamishwa kwa lazima.
Kenya ni mojawapo ya nchi zile zilizouratibu mkataba wa kimataifa juu ya maswala ya uchumi, kijamii na kitamaduni unaobainisha haki sawa za kila mtu, raia wa nchi fulani, raia wa nchi nyingine ya kuishi katika mazingira inayofaa kama kupata chakula, mavazi na nyumba, huduma za afya na elimu.
Mkataba pamoja na kamati inayohakikisha ufuatiliaji wake inasema kuwa nchi zina wajibu muhimu na ni muhimu kuwa wajibu huu unatimizwa vilie vile. Mkataba na kamati inapiga marufuku nchi kuchukua hatua zinazoirudisha nyuma. Hatua zinazowanyima wakimbizi haki ambazo walikuwa wakifurahia. Hatua zilitatiza harakati za nchi za kuzifika malengo katika mkataba.
Mashirika yanayowatetea wakimbizi yanasema kuwa wakimbizi wengi ambao wameishi kwa miaka au hata miongo katika miji nchini Kenya wamepata riziki, nyumba zinazofaa, na huduma za afya. Human Rrights Watch lilisema kwamba kuwahamisha hadi ndani ya makambi yenye wakimbizi wengi kupita kiasi ni dhahiri kuwa ni hali mbovu itakayokiuka wajibu ulioko chini ya mkataba ule.
Kamati inayohakikisha ufuatiliaji wa mkataba inasema kwamba ibara ya kumi na moja inayomhakikishia kila mmoja haki ya kupata makao yanayofaa, inapiga marufuku kuhamishwa kwa nguvu. Inafafanua kuhamishwa kwa nguvu kama kuwatoa watu binafsi, familia, jamii kutoka nyumbani kwao, au na katika wanakoishi kwa muda au milele na kinyume na matakwa yao bila kuwa na ulinzi wa kisheria au ulinzi mwingine. Kuhamishwa kwa nguvu ni lazima kutekelezwe kulingana na sheria husika pia ni lazima zibainishe kindani hali inayostahili kuhamishwa kwa mtu. Sheria hizo ni lazima ziambatane na zile za kimataifa kuhusu haki za binadamu.
Shirika la Human Rights Watch lilisema kuwa kwa sababu mpango wa Kenya wa kuwahamisha wakimbizi wanaokaa mijini hauwezi kuthibitishwa katika msingi wa usalama wa kitaifa,uhamisho wowote utakaotekelezwa chini ya mpango huu hautaambatana na sheria za kitaifa kuhusu haki za binadamu na utakuwa sawa na kuhamishwa kwa nguvu.