(Nairobi) – Mamlaka nchini Tanzania imewakamata au kuwatishia takribani watu 22 tangu Juni 10, 2023, ikiwa ni pamoja na waandamanaji, baada ya kulikosoa Bunge la Tanzania juu ya kuidhinisha mkataba wa usimamizi wa bandari za Tanzania, Shirika la Human Rights Watch limesema leo.
Mkataba huo unairuhusu kampuni ya masuala ya bandari inayosimamiwa na Emirati ya Dubai katika Umoja wa Falme za Kiarabu kusimamia bandari muhimu za Tanzania.Tanzania inapaswa kuacha kuwanyanyasa na kuwakamata wakosoaji wa mkataba huo.
"Unyanyasaji wa serikali ya Tanzania dhidi ya wakosoaji wake ni ishara mbaya ya kutokuwa na uvumilivu dhidi ya wale wenye maoni tofauti na serikali," alisema Oryem Nyeko, mtafiti wa Tanzania katika Human Rights Watch. "Badala ya kuwanyanyasa wakosoaji, serikali inapaswa kuheshimu haki ya uhuru wa kujieleza na kukusanyika, na kuwasikiliza."
Tarehe 10 Juni, bunge la Tanzania liliidhinisha "mkataba kati ya serikali mbili" ambao serikali ya Tanzania iliingia na Emirati ya Dubai mnamo Oktoba 2022 kwa lengo la "kukuza, kuboresha, kusimamia, na kuendesha bandari za baharini na katika maziwa, ikihusisha maeneo kama vile maeneo maalum ya uchumi (Special Economic Zone), maeneo ya mizigo na mengine ya kibiashara."
Tangu wakati huo, mamlaka zimekuwa zikiwanyanyasa waandamanaji na kuminya maoni ya wanaharakati ambao wamekosoa mkataba huo unaoipa nchi nyingine udhibiti mkubwa wa bandari za Tanzania. Wakosoaji wanadai kuwa hatua ya serikali ilikiuka sheria za Tanzania na za kimataifa.
Tarehe 19 Juni, polisi waliwakamata na kuwashikilia watu 18 kwa siku mbili wakati wa maandamano Dar es Salaam.
Tarehe 10 Julai, mkurugenzi wa upelelezi wa makosa ya jinai aliamuru Dr. Rugemeleza Nshala, mwanasheria na mwanaharakati, kuripoti polisi, akisema polisi wanafanya "uchunguzi" juu ya maoni aliyotoa siku chache kabla kwenye mtandao wa kijamii wa Clubhouse akikosoa makubaliano hayo. Nshala aliiambia Human Rights Watch kuwa alikimbia Tanzania baada ya kupokea vitisho dhidi ya uhai wake kwa sababu ya ukosoaji wake mkubwa kuhusu makubaliano hayo.
Tarehe 12 Julai, polisi walimuita Boniface Mwabukusi, ambaye pia ni mwanasheria, baada ya kufanya mkutano na mwanasiasa wa upinzani, Mdude Nyagali, Dar es Salaam kupinga makubaliano hayo. Tarehe 14 Julai, polisi walimkamata Mwabukusi na Nyagali, walipokuwa wakiitikia wito wa polisi.
Polisi waliichukua simu ya Mwabukusi na kumhoji kwa saa nane, kisha wakamwachilia bila mashtaka. Nyagali alibaki kizuizini hadi tarehe 17 Julai na kuachiliwa kwa dhamana ya polisi, pia bila mashtaka. Polisi walimpa Nyagali barua inayomtaka kukabidhi simu zake, kompyuta, na vifaa vingine vya umeme, hata hivyo Nyagali alikataa kufanya hivyo. Mwabukusi aliiambia Human Rights Watch kwamba alijificha kwa siku tatu alipoanza kupokea vitisho vya kuuwawa baada ya kutoa maoni yake juu ya mkataba huo mnamo mwezi Juni. Tarehe 14 Julai, mwanasheria mkuu aliwasilisha ombi kwa Kamati ya Mawakili - chombo cha nidhamu cha Tanzania kwa wanasheria – juu ya madai ya utovu wa nidhamu ya kiweledi uliyofanywa na Mwabukusi kwa sababu ya maoni aliyotoa katika mkutano na waandishi wa habari aliofanya tarehe 3 Julai kuhusu makubaliano hayo, akitaka kamati hiyo itoe tamko kwamba amefanya "utovu mkubwa wa nidhamu ya kiweledi" na amri ya kumzuia kufanya kazi za sheria.
Mwabukusi amefungua kesi mahakama kuu kupinga kuidhinishwa kwa mkataba huo. Hoja zake ni kwamba mkataba unakiuka sheria za Tanzania kwa sababu umma ulipewa siku mbili tu kuwasilisha maoni yao, na kwamba mkataba wenyewe unakiuka sheria za kimataifa na za ndani za Tanzania kwa kuipatia nchi nyingine usimamizi wa rasilimali za asili.
Tarehe 17 Julai, polisi walimkamata Peter Madeleka, pia mwanasheria, nje ya chumba cha mahakama Arusha muda mfupi baada ya mahakama kuu kufuta makubaliano ya kukiri kosa na kulipa fidia aliyofanya na mkurugenzi wa mashtaka ya umma kwa kesi ya uhujumu uchumi ya mwaka 2020, na kumfungulia mashtaka mapya. Wote Mwabukusi na Nshala waliiambia Human Rights Watch waliamini kuwa mamlaka zilikuwa zinamshikilia Madeleka kwa sababu alikuwa amekosoa hadharani makubaliano ya bandari.
Hali ya haki za binadamu nchini Tanzania, hasa kwa uhuru wa kujieleza na kukusanyika, ilidorora vibaya baada ya Rais John Magufuli kuingia madaraka mwaka 2015. Serikali ilitumia sheria kama Sheria ya Uhalifu wa Mtandao ya 2015 na Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari ya 2016 kuwanyamazisha wanasiasa wa upinzani, waandishi wa habari, na wanaharakati waliokosoa serikali na rais. Kipindi cha karibu na uchaguzi mkuu wa Oktoba 2020, wakati Magufuli alipochaguliwa tena, serikali iliongeza vizuizi hivi na kuwakamata kiholela viongozi wa vyama vya upinzani na wafuasi wao.
Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye aliteuliwa baada ya kifo cha Magufuli mnamo Machi 2021, amechukua hatua kadhaa kushughulikia wasiwasi juu ya masuala ya haki za binadamu. Mwezi Februari 2022 serikali iliyafungulia magazeti manne, na mwezi Machi ilifuta mashtaka na kumuachilia huru kiongozi mkuu wa upinzani nchini Tanzania, Freeman Mbowe, baada ya kushikiliwa kwa miezi saba. Mwezi Januari, Hassan aliondoa marufuku ya miaka sita kwa wanasiasa kufanya mikutano ya hadhara ya kisiasa nje ya kipindi cha uchaguzi.
Serikali bado haijafanya mapitio na marekebisho ya vipengele kadhaa kandamizi vya sheria mbalimbali zilizopitishwa na kutekelezwa baada ya Magufuli kuingia madaraka, zinazozuia uhuru wa kujieleza na kukusanyika.
Katiba ya Tanzania inalinda uhuru wa kujieleza na kukusanyika kwa mujibu wa Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu na Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa, na inahakikishia umma haki ya kupinga uvunjaji wa haki za binadamu za msingi kama suala lenye maslahi ya umma.
"Serikali ya Tanzania inapaswa kuacha ukamataji wa kiholela na kuchukua hatua zaidi kushughulikia changamoto za uhuru wa kujieleza," Nyeko alisema. "Serikali ya Hassan imepiga hatua muhimu kuhusu haki, na badala ya kurudi kwenye msimamo wa serikali iliyopita, inapaswa kuzuia wimbi hili la ukandamizaji."