(Nairobi) – Mamlaka nchini Kenya imetekeleza unyanyasaji unaofanyiwa waandishi wa habari wanaoripoti maswala tata, hatua inayotishia uhuru wa kujieleza wakati ambapo taifa hilo linakaribia uchaguzi mkuu mnamo mwezi Agosti 8 2017 kulingana na ripoti iliotolewa na shirika la haki za kibinaadamu la Human Rights Watch na ofisi ya Shirika la ARTICLE 19 ya Afrika Mashariki. Waandishi wa habari pamoja na wanablogu wanaoripoti kuhusu maswala ya ufisadi, unyakuzi wa ardhi, operesheni za kukabiliana na ugaidi pamoja na ghasia za baada ya uchaguzi wa mwaka 2007-2008 pamoja na maswala mengineyo wamekabiliwa na vitisho, kupigwa pamoja na kupoteza kazi.
Ripoti hiyo yenye kurasa 53, kwa jina “‘Not Worth The Risk’: Threats To Free Expression Ahead of Kenya’s 2017 Elections,” imenakili unyanyasaji unaotekelezwa na maafisa wa serikali ,maafisa wa polisi, magavana pamoja na maafisa wengine wa serikali dhidi ya vyombo vya habari. Shirika la Human Rights Watch na ARTICLE 19 walichunguza majaribio ya serikali kuwazuia waandishi muhimu na wanablogu kupitia sheria, mamlaka na njia nyingine zisizo rasmi ikiwemo vitisho, unyanyasaji, kuwachunguza kupitia simu na mitandaoni na katika visa vingine, hata kupigwa.
“Lazima tukabiliane na ongezeko la ghasia, uvunjaji wa sheria dhidi ya Waandishi wa habari nchini Kenya’’, alisema Henry Maina ambaye ni mkurugenzi wa ARTICLE 19 Afrika Mashariki. ‘Hakuna sera za kukabiliana na hali hiyo zitafaulu iwapo hatua za kukabiliana na uchokozi na kuwalinda waandishi waliomo hatarini hazitaandamana na hatua kali za kisheria kuchukuliwa dhidi ya uhalifu wowote dhidi yao’’
Licha ya kupokea malalamishi rasmi kutoka kwa waandishi , ni nadra kwa maafisa wa polisi kufanya uchunguzi wowote wa vitisho hivyo. Tangu Rais Uhuru Kenyatta kuchukua mamlaka mnamo 2013 hakuna ushahidi wakuonyesha kwamba afisa yeyote wa polisi ama wa serikali ameshtakiwa kwa kutoa vitisho ama hata kuwapiga waandishi wa habari nchini Kenya.
Shirika la Human Rights Watch na ARTICLE 19 waliwahoji waandishi 92, wanaharakati wa haki za kibinaadamu,wanablogu na maafisa wa serikali nchini Kenya na kunakili visa 17 ambapo waandishi 23 na wanablogu walipigwa kati ya 2013 na 2017 na maafisa wa serikali ama watu binafsi wanaoaminika kushirikiana na maafisa wa serikali.
Angalau waandishi wawili walifariki katika hali inayohusishwa na kazi yao. Makundi hayo pia yalinakili visa 16 vya vitisho vya mauaji ya moja kwa moja dhidi vya waandishi na wanablogu nchini humo katika miaka ya hivi karibuni na visa ambavyo maafisa wa polisi waliwakamata ,kuwazuilia na baadaye kuwaachilia waandishi bila ya kuwafungulia mashtaka takriban waandishi 14 na wanablogu.
Kwa mfano mnamo Septemba 7 2016, watu wasiojulikana walivamia nyumba ya mwandishi Denis Otsieno katika mji wa Kitale mkoa wa Bonde la Ufa na kutaka picha kutoka kwa kamera yake na baadaye kumpiga risasi na kumuua. Otsieno alikuwa amewapiga picha maafisa wa polisi wakimpiga risasi na kumuua mwendesha bodaboda katika kituo cha basi cha Kitale siku chache kabla ya tukio hilo. Mmoja wa jamaa yake alisema kuwa kabla ya kifo chake Otsieno alikuwa amelalamika kuhusu vitisho alivyopata. Hakuna mtu aliyekamatwa kufuatia kifo chake.
Mhariri mmoja mwenye makao yake jijini Nairobi aliyaambia makundi hayo mawili: ‘Kila mara tunapoandika makala yanayoyakosoa mashirika ya usalama ama yanayofichua ufisadi katika serikali, waandishi wetu hupokea vitisho vya kuuawa kutoka kwa vitengo vya usalama pamoja na maafisa wa serikali. Hatua hiyo hufuatwa na serikali kuyaondoa matangazo kwenye vyombo hivyo vya habari au hata kususia kulipa malipo ya matangazo. Sasa inatulazimu kufikiria kwa kina sana kama habari hizo ni muhimu sana kuliko uhusiano wetu wa kibiashara unaotokana na matangazo ya kibiashara.’
Huku uchaguzi mkuu ukitarajiwa mnamo mwezi Agosti, vitengo vya usalama vya serikali vimeimarisha vitisho na vimekuwa vikitumia njia zenye utata ili kufanya uchunguzi bila ya vibali vya mahakama dhidi ya waandishi wanaoripoti kuhusu maswala nyeti. Kama anavyosema ripota mmoja ‘iwapo umeandika ripoti kuhusu vitengo vya usalama unapaswa kujua kwamba unafuatwa ama simu yako inasikizwa’.
‘Ili uchaguzi wa mwezi Agosti kuwa wa haki na huru , vyombo vya habari vinafaa kuripoti kuhusu maswala muhimu ya kitaifa bila upendeleo na hofu ya kushambuliwa,’ alisema Otsieno Namwaya ambaye ni mtafiti wa maswala ya Afrika katika Shirika la Human Rights Watch. ‘Rais Kenyatta anapaswa kusisitiza umuhimu wa uhuru wa kujieleza na kushutumu vitisho na mashambulizi dhidi ya waandishi na wanablogu’
Wakati waandishi wa Kenya wakinyanyaswa na serikali , wanahabari wa kigeni pia hawakusazwa kwa ripoti zao za ukosoaji. Mwaka 2015 Mamlaka ya Kenya ilitishia kuwapiga marufuku waandishi wawili wa habari wa kigeni kwa kuripoti kuhusu kikosi cha polisi cha Kenya kinachohusika na mauaji ya kiholela.
Licha ya kupokea malalamishi rasmi kutoka kwa waandishi, imekuwa nadra kwa polisi kuanzisha uchunguzi dhidi ya vitisho kwa vyombo vya habari, kama walivyobaini mashirika ya Human Rights Watch na ARTICLE 19. Mnamo mwaka wa 2015 mtu asiyejulikana na anayedaiwa kuwa afisa wa usalama wa serikali alimpiga mwanaharakati wa haki za kibinaadamu na mwanablogu Florence Wanjeri Nderu na kumuonya dhidi ya kuendelea na machapisho yake kuhusu ufisadi .‘Licha ya kuwasilisha maelezo ya malalamishi yake kuhusu shambulio hilo na mshukiwa kwa polisi, Maafisa hao hawajatembelea eneo la shambulio hilo ama hata kunijulia hali’’, alisema. ’Kisa hicho hakijawahi kuchunguzwa baada ya mimi kuwasilisha malalamishi yangu’’.
Uchunguzi wa kina na kuwashtaki wahusika wa mashambulio kama hayo ni muhimu katika kuhakikisha kuwa vyombo vya habari na wanabloga wanaripoti kuhusu maswala tofauti kabla ya uchaguzi wa 2017 wakiwa huru, kulingana na Human Rights Watch na ARTICLE 19.