Skip to main content

Kenya: Komesha oparesheni katili za polisi wakati wa maandamano

Uwajibikaji, Marekebisho ya kimsingi yanahitajika

Afisa wa polisi wa kitengo cha kukabili ghasia afyatua kitoza machozi dhidi ya waandamanaji wakati wa mkutano uliotishwa na kiongozi wa upinzani Raila Odinga kupinga gharama ya juu ya maisha jijini Nairobi, Jumatatu, Machi 27, 2023. © 2023 Picha za AP/ Patrick Ngugi

(Nairobi) –  Karibu miezi miwili tangu msururu wa maandamano kuanza nchini Kenya, Serikali ya Kenya  bado haijachukua  hatua zifaazo kuwaadhibu maafisa wa polisi na makamanda wao waliohusika na mauaji na mashambulizi dhidi ya waandamanaji na watu wengine, Mashirika ya Human Rights Watch na Amnesty International tawi la Kenya yamesema leo.

Mamlaka Huru ya Kufuatilia Utendakazi wa Polisi nchini Kenya (IPOA) yafaa kuharakisha uchunguzi wa visa ambapo watu kadhaa walidaiwa kuuawa kwa kupigwa risasi na polisi na vile vile tuhuma dhidi ya polisi kutumia nguvu kupita kiasi. Mashirika ya Human Rights Watch na Amnesty International yamesema. Yameongezea kwamba taasisi zote zenye mamlaka kwenye masuala ya usalama ikiwemo idara ya polisi, zafaa kuwatangazia raia, waziwazi, kwamba zinalinda haki ya kila raia kushiriki mikutano ya amani na maandamano ya amani katika siku zijazo.

 

Mwezi Agosti Mwaka 2022, Kenya ilifanya uchaguzi uliopingwa kortini.  Uchaguzi huo ulimpa Rais William Ruto kiti cha Urais na hivyo kuunda serikali. Tarehe 9 Mwezi Machi Mwaka 2023, Raila Odinga, kiongozi wa muungano wa upinzani -Azimio, alitoa hotuba akiitaka Serikali ya Ruto kushughulikia kuongezeka kwa gharama ya maisha nchini Kenya na udanganyifu kwenye uchaguzi mkuu wa Mwaka 2022, miongoni mwa maswala mengine. Maandamano ya kwanza yalianza tarehe 20 Mwezi Machi, 2023, halafu Odinga akatangaza maandamano hayo yatafanyika  mara mbili kwa wiki hadi pale Serikali ingeafikia matakwa yao.

Katikati ya mwezi Aprili, mazungumzo yaliyokuwa yameanza baina ya Serikali na upinzani yaligonga mwamba na hivyo maandamano mapya yakaanza Tarehe 2 Mwezi Mei. Keshoye, Odinga alitangaza kuahirisha maandamano ili kutoa nafasi kwa mazungumzo kati ya upinzani na Serikali ya Ruto, huku akiahidi kurejea kwenye maandamano iwapo mazungumzo yatavunjika.

“Serikali ya Kenya yafaa kukoma kuziba macho yake kuhusiana na suala la polisi kuwadhulumu waandamanaji na kuwavuruga kwa namna nyingine nyingi,” alisema Mausi Segun, Mkurugenzi  Shirika la Human Rights Watch tawi la Afrika. “Serikali inafaa kuanzisha uchunguzi wa kina kwa haraka kuhusiana na dhuluma na ukatili wa polisi uliojitokeza wakati wa maandamano ya hivi karibuni, ikiwemo kushindwa kuwalinda na kuwahakikishia waandamanaji usalama wao ili wasivamiwe na yeyote wanaposhiriki maandamano.”

Kati ya tarehe 7 Mwezi Aprili na tarehe 17 Mwezi uo huo, Mashirika ya Human Rights Watch na Amnesty International tawi la Kenya yaliwahoji watu 115. Waliohojiwa walikuwa watu walioshuhudia dhuluma wengine wakiwa waathiriwa wa dhuluma za polisi wakati wa maandamano ya Nairobi na  Kisumu, Migori, na Homa Bay. Mashirika hayo yalibaini kwamba serikali iliwatuma maafisa wa polisi wa kitengo cha kuzima ghasia ambao iwe waliwashambulia watu au walitumia nguvu kupita kiasi, ikiwemo nguvu ya kuhatarisha maisha kuzima ghasia za tarehe 20 Mwezi Machi, vilevile tarehe 27, na 30. Mashirika hayo yalirekodi visa vya mauaji, kutiwa nguvuni bila kuzingatia sheria, kuwapiga watu, kuharibu mali ya raia , kurusha vitoza machozi ovyo bila kujali paliporushwa, kuwapulizia watu maji kupitia mabomba ya lori zinazotumika kuzima ghasia na njia nyingine zinazokiuka haki za kimsingi za watu.

Vyombo vya habariTume ya kitaifa ya haki za binadamu , na mashirika ya kijamii wamenakili na kurekodi visa vya ukiukaji wa haki za kimsingi vilivyofanywa na Serikali wakati wa maandamano ya Mwezi Machi. Taasisis hizi vilevile zimeshutumu tangazo la Rais Ruto, kauli za Serikali yake na misimamo ya wakuu wa Polisi za Mwezi Machi kwamba maandamano yalikuwa kinyume cha sheria.

Mashirika ya Human Rights Watch na Amnesty International tawi la Kenya kwenye mahojiano waliyofanya,  kila shirika kivyake palikuwapo kufanana kwa visa 12 vya mauaji. Hii ilikuwa ni baada ya kuzungumza na familia za waathiriwa na watu kadhaa walioshuhudia. Licha ya kwamba baadhi ya waathiriwa wa mauaji hayo walishiriki kwenye maandamano, wengi wao, kwa mujibu wa Ushahidi ambao mashirika hayo yalipata, walikuwa watu waliopatwa tu kwa sababu ya kuwa karibu  na maeneo ya maandamano. Wapo waliokuwa wapita njia, wale waliokuwa kwenye shughuli zao za kibiashara na watu waliokuwa nyumbani mwao. Kwenye baadhi ya oparesheni za polisi mfano mjini Kisumu na Nairobi, watu kadhaa waliohojiwa walisema polisi walifyatua risasi kwenye maeneo ya makazi ya watu, ndani ya madarasa ya shule na vyuo.

Kwenye kisa kimoja, jamaa ya mwathiriwa kwa jina Elijah Okumu, wa umri wa miaka 26, walisema polisi walimpiga risasi wakati wa maandamano ya Tarehe 27 Mwezi Macchi. Okumu alikuwa akifunga duka lake mtaani Dandora jijini Nairobi. Jamaa zake walimkimbiza Okumu katika hospitali ya Mama Lucy mashariki ya Jiji la Nairobi na baadaye kumhamisha hadi hospitali ya kitaifa ya Kenyatta. Okumu alifariki kutokana na majeraha ya risasi punde baada ya kufika hospitali hiyo ya Kenyatta.

Jamaa yake mmoja alisema familia ilitoa habari kwa Mamlaka ya kufuatilia Utendakazi wa Polisi IPOA. Familia hiyo haijajua iwapo hatua zozote zilichukuliwa wala hakuna ujumbe wowote wamepata kutoka kwa IPOA. Hapakuwapo habari kuhusu iwapo uchunguzi ulifanywa.

Mashirika ya Human Rights Watch na Amnesty International tawi la Kenya vilevile yalinakili visa 30 vya  watu kujeruhiwa kwa kupigwa risasi  katika miji ya Kisumu na Nairobi.

Kwenye kisa kimoja, maafisa wa polisi walimtia nguvuni, wakampiga, na baadaye kumpiga risasi mwanafunzi wa sekondari, Brian Carlos Oduor, katika mtaa wa Korumba eneo la Riat mjini Kisumu Tarehe 30 Mwezi Machi. Ilikuwa ni baada ya kumshuku kuwa mwandamanaji. Mwathiriwa mwenyewe, Oduor na watu wengine walioshuhudia na wakazungumza na Mashirika ya Human Rights Watch na Amnesty International tawi la Kenya, alisema wakati alitiwa nguvuni alikuwa amebeba mtungi wa gesi. Aliwaelezea maafisa wa polisi kwamba alikuwa akienda kuujaza mtungi huo kwa gesi.

Baada ya kumweka kwenye gari lao baadaye polisi hao walimtupa nje ya gari hilo la Land Cruiser na kuanza kumpiga mateke. Hapo ndipo mojawapo ya bunduki ilifyatuliwa, Oduor akagundua kwamba alikuwa amepigwa risasi kwenye mkono wake wa kushoto. Polisi hao walitoroka na kumwacha Oduor pekee yake hapo akiwa na jeraha. Alipewa huduma ya kwanza na wapita njia halafu akakimbizwa hospitalini kutibiwa.

Watafiti wa mashirika haya pia walirekodi oparesheni za ukatili uliofanywa na polisi dhidi ya wanahabari kutoka vyumba mbalimbali vya habari. Wanahabari hao walikuwa wakikusanya habari za maandamano ya tarehe 30 Mwezi Machi kwenye barabara ya Outering karibu na mtaa wa Pipeline jijini Nairobi. Wanahabari hao walisema polisi walijitahidi kuwazuia wasiripoti maandamano hayo hasa kwa njia ya moja kwa moja. Walitumia mabomba ya maji ya kupuliza kuharibu kamera za televisheni. Waliwavuruga baadhi ya wanahabari, huku wakiwalazimisha wengine kufuta nakala za video walizokuwa wamerekodi. Wanahabari walisema wakati huo waliona kwamba wanalengwa, wanatishwa, wengi waliingiwa na hofu huku wakishindwa hata kuwasaidia watu waliokuwa wamejeruhiwa.

“Maandamano yalikuwa ya amani, watu waliimba nyimbo, watu walikuwa na furaha, walipungiana mikono ilivyo desturi ya salamu za umati. Lakini walipofika mahala ambapo walikuwapo polisi, polisi wakawarushia vitoza machozi,” mwanahabari mmoja alisema. “Polisi walizuia magari na waandamanaji waliokuwa wakitembea kwa miguu kutoka pande zote wakakosa pa kupitia. Halafu anga ikajaa moshi wa vitoza machozi na maji ya rangi yanayopulizwa na malori yanayotumika kuzuia ghasia … tulijipata tumenaswa kwenye maji chafu na moshi tukipambana kupumua.”

Maafisa wa polisi pia walifyatua vitoza machozi kwenye mitaa ya makao ya watu ikiwemo kwenye maboma na shuleni, hali iliyotatiza afya ya watu huku yamkini watoto wawili wakifariki, walisema mashahidi. Joyce Kemunto, wa umri wa miaka 39, alisema bintiye ambaye alikuwa mtoto wa miezi minne alifariki akiwa nyumbani mtaani Kibera baada ya polisi kurusha vitoza machozi pale mtaani tarere 30 Mwezi Machi.

“Vitoza machozi viliporushwa, baadhi ya vichupa vilianguka kwenye paa la nyumba huku moshi huo ukiingia ndani ya nyumba. Mtoto wangu Precious,wa miezi minne alikuwa amelala,” alisema Kemunto. “Mtoto wangu alianza kulia. Nilichukua kitambaa na maji nikaanza kumpanguza usoni na pia nyuso za watoto wangu wengine … Singeweza kutoka nje kwa sababu kulikuwa na moshi mwingi wa vitoza machozi hapakuwapo mahala pa kwenda. Kwa hivyo tulisalia nyumbani. Mtoto akalia hadi akanyamaza akashindwa kunyonya.” Kemunto alisema hali ya mtoto ilidhoofika, akaanza kutokwa damu kwenye pua. Alifariki wakiwa njiani kumpeleka hospitalini.

Katika kisa kingine, Jackline Moraa, wa umri wa miaka 31 mkazi wa mtaa wa Kibera, jijini Nairobi alimpoteza mwanaye wa kiume tarehe 4 Mwezi Aprili,baada ya kupumua moshi wa gesi ya vitoza machozi vilivyokuwa vimerushwa  mtaani tarehe 30 Mwezi Machi. Alisema madaktari katika hospitali ya Mbagathi walishuku kwamba gesi ya vitoza machozi ilikuwa imeathiri kifua chake na kumfanya ashindwe kupumua.

Licha ya kwamba maandamano yalikuwa ya amani, Mashirika ya Human Rights Watch na Amnesty International tawi la Kenya yalibaini kwamba wapo watu waliohusika kwenye visa vya vurugu wakati wa maandamano hayo. Visa hivyo vilijumuisha wizi, kupora, majaribio ya ubakaji na kuwajeruhi watu. Huku  vyombo vya habari vikiripoti baadhi ya visa, Mashirika ya Human Rights Watch na Amnesty International tawi la Kenya yalibaini kwamba polisi walishindwa kuingilia kati na kukomesha vurugu. Vilevile walishindwa kuanzisha uchunguzi kuhusiana na baadhi ya matendo ya vurugu.

Ali Said, wa umri wa miaka 17, alisema alishambuliwa na kundi la waandamanaji wakiwa na silaha butu mtaani Kaloleni, Kisumu tarehe 27 Mwezi Machi. Said alisema waandamanaji walimpiga vibaya na kumkata tumboni kwa kisu. Aliokolewa na mwendeshaji pikipiki aliyemkimbiza hospitalini. Alitoa habari za kuvamiwa kwa polisi, lakini hajaona hatua zozote zikichukuliwa.

Haki ya mtu kuwa hai, haki za watu kukutana kwa amani, haki za kushiriki pamoja, na haki ya kujieleza ni haki za kimsingi za mwanadamu ambazo zinatolewa na katiba ya Kenya. Haki hizo pia zinatolewa na mikataba ya kimataifa ya haki ambayo Kenya imetia Saini. Hali hii inamaanisha kwamba Serikali ya Kenya inawajibikia hitaji la kutii na kutimiza haki za kimsingi za waandamanaji wala haiwezi kukwepa. Mikataba hiyo inajumuisha Ratiba ya Bara la Afrika kuhusu Haki za binadamu na Haki za watu. Vilevile Mkataba wa kimataifa wa Haki za kijamii na Haki za Kisiasa.

Kanuni za Umoja wa Mataifa- UN, kuhusu utumiaji nguvu na utumiaji silaha zinawaruhusu polisi kutumia nguvu iwapo hamna njia nyingine ya kulinda usalama. Hata hivyo nguvu wanayoamua kutumia iwe ya kutimiza shughuli muhimu na yafaa iwe inayokubalika kisheria. Idara za usalama zinafaa kutumia vitoza machozi iwapo zimelazimika kufanya hivyo lakini zitumie bila kumjeruhi mtu yeyote na ikiwezekana vitoza machozi virushwe baada ya onyo kutolewa. Wakati wa maandamano yenye vurugu utumiaji vitoza machozi unafaa kuendana na kasi ya maandamano au viwango vya makosa yanayofanywa. Lazima pia vitoza machozi vitumike kwa kuzingatia malengo ya ulindaji sheria, kwa njia inayopunguza tishio la kudhuru. Utumiaji maksudi wa nguvu ya kupita kiasi huruhusiwa tu iwapo ndio njia ya pekee iliyopo ya kulinda maisha na uhai wa mtu.

Mashirika ya Amnesty International tawi la Kenya na Human Rights Watch awali kivyao na kwa ushirikiano yamerekodi suala la kuwepo mwingilio wa kisiasa kwenye juhudi za kuhakikisha kwamba maafisa wa polisi wanaohusika na kutekeleza dhuluma wanawajibikia makosa waliyofanya. Vilevile kwamba uchunguzi  uanzishwe dhidi ya kushindwa kwa Mamlaka zinazofaa kuwachukulia hatua polisi, pia suala la polisi kushindwa kutii utaratibu wa kuanzisha hatua hiyo lichunguzwe, ukosefu wa nia ya kisiasa miongoni mwa wakuu kwa lengo la kukomesha dhuluma dhidi ya watu ili kuhakikisha uwajibikaji huku kukiwapo marekebisho katika idara ya polisi.

Kuipa Huduma ya Polisi uhuru wa kusimamia pesa na bajeti zake huku pia Mamlaka ya kufuatilia Utendakazi wa Polisi IPOA ikipewa uhuru huo ni njia mojawapo ya kuhakikisha upo uhuru wa kufanya kazi katika taasisi hizo mbili. Hali kama hiyo itatoa nafasi ya mbele ya kupanda mbegu ya kutimiza mpango wa mabadiliko kwenye utendakazi wa polisi ikiwemo uwajibikaji ambapo polisi wanaohusika kwa kutenda makosa wanachukuliwa hatua, Mashirika ya Human Rights Watch na Amnesty International tawi la Kenya yamesema.

“Oparesheni katili za polisi dhidi ya maandamano ambayo yanaidhinishwa na katiba yetu hazikubaliki,” alisema Irũngũ Houghton, Mkurugenzi Mkuu katika Shirika la  Amnesty International tawi la Kenya. “Mamlaka nchini Kenya yanafaa kuchukua hatua muhimu kukomesha dhuluma ambazo hukumba maandamano na hilo litawezekana kupitia njia ya kuwachukulia hatua kali polisi wanaohusika na kufanya dhuluma- maafisa hao wanafaa kushtakiwa kwa makosa ya jinai kwa kufanya kazi yao bila kutii sheria. Kushindwa kuwachukulia hatua maafisa wa polisi waliohusika na ukatili huo wakati wa maandamano ya Mwezi Machi kutafungua mlango wa vurugu zaidi siku za usoni.”


Your tax deductible gift can help stop human rights violations and save lives around the world.

Region / Country
Topic