Skip to main content

Kenya: Undanganyifu Waathiri Ugawaji Pesa Za Janga La Korona

Tume Ya Kukabiliana Na Ufisadi Inafaa Kuanzisha Uchunguzi

(Nairobi) — Serikali ya Kenya ilishindwa kuweka mipango kabambe ya kuwalinda raia, ambayo ingehakikishia wakenya wote, wala sio watu wachache tu, wanamudu viwango bora vya maisha, msimu wa janga la Korona, Shirika la Human Rights Watch limesema kwenye ripoti iliyotolewa leo.

Ripoti hiyo yenye kurasa 77 iitwayo, We Are All Vulnerable Here: Kenya’s Pandemic Cash Transfer Program Riddled with Irregularities” inasema kwamba kati ya jamii zilizokumbwa na changamoto mbali mbali kutokana na janga la korona jijini Nairobi, ni familia chache tu zilizolinufaika na mpango huo wa msaada wa kifedha. Uchunguzi wetu umebaini kuwa mpango huo uliathirika na ukosefu wa uwazi, usaidizi kutolewa kwa kujuana, ukabila na mapendeleo. Aidha imebainika kwamba,maafisa wa serikali walishindwa kufuata utaratibu uliowekwa kuamua jamii zinazohitaji msaada, au kutoa habari ambazo zingewezesha jamii zilizoathirika zaidi kuorodheshwa kwa msaada. 

“Inasikitisha kwamba mpango wenye nia nzuri na muhimu kwa jamii unaweza kuharibiwa kwa sababu ya mwenendo mbaya wa kutojali, na ukosefu wa usimamizi thabiti kutoka kwa serikali,” asema Otsieno Namwaya, mkurugenzi wa shirika la Human Rights Watch tawi la Afrika Mashariki. “Maafisa wakuu serikalini, akiwemo Rais Uhuru Kenyatta, wanafaa kuonyesha kujitolea kwao kusaidia jamii zilizoathirika.Wanafaa kuzungumzia waziwazi swala la ubadhirifu wa pesa za umma na usimamizi mbaya wa mpango wa kusambaza pesa za msaada, na kuhakikishia wakenya kwamba uchunguzi utaanzishwa kuhusu matumizi mabaya ya pesa hizo.”

Shirika la Human Rights Watch liliwahoji jumla ya watu 136 kati ya mwezi Julai 2020 na Februari 2021,wakiwemo maafisa wa serikali na vile vile wakazi wa mitaa ya mapato ya chini. Ingawa ripoti hii iliwalenga zaidi wakazi wa mitaa ya mapato ya chini jijini Nairobi, maafisa wa serikali walidai kwamba pesa hizo za msaada zilitolewa kwa kaunti 21 kati ya kaunti 47 nchini Kenya.

Mnamo tarehe 23 Mei, 2020, Rais Kenyatta alitangaza kwamba alikuwa ametenga shilingi bilioni 10 (Dola milioni 100) kwa matumizi ya kusaidia jamii zilizoathiriwa na changamoto za kiuchumi kutokana na janga la Korona.

Shirika la Human Rights Watch lilibaini kwamba, tangu mwezi Machi 2020 serikali ilipotangaza kisa cha kwanza cha Korona nchini Kenya,idadi kubwa ya watu wamepoteza riziki yao.Punde baada ya kugundua kisa hicho, serikali ilitangaza masharti makali kukabili msambao wa ugonjwa huo wa Korona, ikiwemo kutolewa kwa amri ya kafyu,kuwaagiza wakenya kusalia nyumbani, na kanuni zilizokomesha mikutano ya halaiki au kukaribiana kiholela. Maelfu ya watu waliopoteza riziki yao, hasa kutokana na kufungwa kwa biashara na wengine kufutwa kazi, walikumbwa na tishio la njaa na fedheha za kufurushwa kwenye makazi yao.

Shirika la Human Rights Watch lilibainisha kwamba kulikuwa na utepetevu kwa upande wa maafisa wa serikali katika kuwasaidia raia na hasa jamii zilizoathirika vibaya.Baadaye serikali ilipoanzisha mpango wa kusambaza pesa uliochukua miezi minane, changamoto mpya ziliibuka ikiwemo uhaba wa pesa zilizotolewa,muda mfupi wa usaidizi,na ukosefu wa uwazi. Mpango huo wa usaidizi, haukuwa na njia mwafaka za kufahamisha raia kuhusu nani anafaa kusaidiwa, raia waliofaa kusaidiwa walivyotambuliwa, au ni kwa nini maelfu ya watu ambao walihitaji kusaidiwa walitengwa wakati wa kutolewa kwa msaada huo. 

Kwa mujibu wa Shirika la Human Rights Watch, ni jukumu la serikali kuhakikisha kwamba wananchi walioathiriwa vibaya na janga la Korona hawatengwi wakati wa kutekeleza mpango wa kutoa ufadhili wa kifedha. Kwa hivyo serikali ingefaa kurahisisha namna raia wangepata usaidizi, au kuwawezesha waliotengwa kuwasilisha malalamishi yao.

Licha ya kwamba baadhi ya masharti yaliyotangazwa kukabili Korona yangalipo, huku ugonjwa huo ukizidi kusambaa kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa, serikali ilikomesha mpango wa kutoa pesa za msaada na afueni ya kupunguza kiwango cha ushuru mwezi disemba mwaka uliopita.Badala yake, serikali imetangaza ushuru mpya kwa bidhaa na huduma za kimsingi, ikiwemo chakula cha watoto, mafuta, mikopo ya benki, katika harakati za kuongeza mapato ya kufadhili shughuli na mipango ya serikali.

Waziri wa Hazina na mipango, Ukur Yatani, aliliambia Shirika la Human Rights Watch kwamba katika kuamua watu wanaohitaji msaada,serikali ililenga zaidi maeneo yenye umaskini mkubwa, wengi wao wakiwa katika mitaa ya mabanda jijini Nairobi. Vile vile mpango huo ulilenga jamii zinazokabiliwa na changamoto mbali mbali ikiwemo magonjwa hatari,ulemavu, miongoni mwa matatizo mengine. 

Waziri Yatani alisema kuwa wazee wa vijiji wakisaidiwa na wahudumu wa afya wa kujitolea na viongozi wa vijana walihusishwa katika kutekeleza mpango huo wa msaada wa kifedha ambao ulisimamiwa na Machifu.

Hata hivyo wachunguzi wa Shirika la Human Rights Watchwalibainisha kwamba machifu wengi walipuuza kanuni zilizowekwa na serikali na badala yake wakawasajili jamaa na marafiki zao wasiokuwa wakazi wa Nairobi.

“Maboma 25,000 kati ya karibu maboma 40,000 katika eneo langu yalikuwa na matatizo mengi. Kwa hivyo yalihitaji usaidizi wa dharura,” chifu mmoja alisema. “Hata hivyo nilitengewa pesa za kutosheleza maboma 350 pekee. Sijui ni kwa nini wakubwa wetu waliamua kutuma kiwango hicho maana hawakutuuliza maoni yetu. Vile vile kati ya maboma 350 yaliyolengwa, ni karibu maboma 100 tu ndiyo yaliyopata msaada. Hatujui jinsi wakubwa wetu walifikia uamuzi huo.”

Mfanyikazi mmoja wa shirika lisilokuwa la serikali jijini Nairobi, ambalo lilihusika katika kuorodhesha familia zilizoathirika, alisema: “Tungependa kujua kwenye orodha ambazo tuliandaa na kuwasilisha kwa serikali ni nani walipewa fedha hizo. Njia iliyotumiwa kwenye mpango mzima haikuwa ya uwazi kwa hivyo ingevurugwa.”

Serikali ya Kenya imetetea njia za siri zilizotumika. “Watu wenye mahitaji na waliofaa kusaidiwa hapa ni wengi na wangefurika katika afisi yangu,” afisa mmoja msimamizi alisema. “Je ningewashughulikiaje?”

Wakazi pia walisema kwamba idadi ya waliopata usaidizi kupitia mpango huo haiwiani na idadi iliyotangazwa na serikali. Ilikuwa imetangazwa kwamba pesa zitatolewa kwa awamu 35 kwa wiki, lakini wakati wa kutoa ufadhili huo, watu walipata pesa hizo kwa awamu 2 au 3 pekee. 

Kwa mujibu wa shirika la Slum Dwellers International (SDINET), makazi nane ya watu wenye mapato ya chini hapa jijini Nairobi, yanakisiwa kuwa na maboma 600,000, yanayohitaji usaidizi, hasa ikizingatiwa kwamba wakazi wengi walipoteza kazi zao na wnegine kulazimika kufunga biashara zao ndogo ndogo kutokana na athari za janga la korona.Lakini, idadi ya wakazi waliosaidiwa na serikali jijini Nairobi ni takriban asilimia 4.8 tu ya watu wote wenye mapato ya chini.

Kulingana na Shirika la Human Rights Watch, serikali inafaa kubadilisha kanuni zinazotumika kutekeleza mipango ya misaada ikiwemo jinsi ya kubainisha jamii zilizoathirika zaidi. Mpango unaofaa ni ule unaohakikisha uwajibikaji, usimamizi thabiti, kuwapa mafunzo maafisa wanaohusika juu ya jinsi ya kutambua watu wanaohitaji msaada na vile vile kuweka kanuni zifaazo za kupokea na kushughulikia malalamiko. 

Mbali na mipango ya kutoa misaada ya kifedha wakati wa msimu wa janga la Korona, serikali pia iliendelea kutoa pesa kupitia mpango wa awali wa “Inua Jamii”. Kufikia tarehe 23 Mei, 2020, Rais Uhuru Kenyatta alisema kwamba serikali ilikuwa ikitumia shilingi milioni 250 (Dola milioni 2.5) kila wiki kusaidia watu walioathirika zaidi. Hata hivyo Rais hakudokeza ni lini serikali ilianza kutoa pesa hizo. Vile vile, Rais alisema kuwa serikali ilikuwa na mpango wa kuwasaidia wenye biashara ndogo ndogo, hata hivyo Shirika la Human Rights Watch halikupata ushahidi wowote kuonyesha ufadhili huo kwa wenye biashara ndogo ndogo katika mitaa ya mabanda.

Shirika la Human Rights Watch lilisema kwamba serikali ya Kenya inafaa kubainisha mahitaji ya watu walioathirika zaidi kote nchini ili kuhakikisha kwamba hakuna mwananchi yeyote anayekosa chakula na kwamba usaidizi ambao serikali inatoa unatosheleza mahitaji ya kimsingi ya maisha.

Kenya, ni mshirika wa mkataba wa kimataifa kuhusu Uchumi, Haki za Kijamii na Tamaduni (ICESCR) kwa hivyo ina wajibu wa kuhakikisha kwamba kila raia anafurahia haki ya kuishi maisha yanayofaa binadamu, ikiwemo chakula cha kutosha, makao na haki za kimsingi kama vile kutokumbwa na njaa. 

“Serikali ya Kenya inafaa kupata funzo kutokana na changamoto zilizokumba mpango wa kutoa pesa za msaada katika msimu wa janga la Korona na kuchukua hatua za kuanzisha taratibu za muda za kukabili majanga ya dharura ” Asema Namwaya. “Serikali inafaa kuchukua hatua thabiti kuhakikisha kwamba ilmuradi masharti ya kukabili Korona yangalipo,jamii zilizoathirika zaidi ikiwemo mitaa ya mabanda jijini Nairobi, zinapata mahitaji ya kimsingi ya chakula, kodi ya nyumba, na mahitaji mengine ya kimsingi kwa mwanadamu.”

Your tax deductible gift can help stop human rights violations and save lives around the world.

Region / Country