(Nairobi) – Mamlaka nchini Kenya zimetakiwa kurekebisha sharti linalotaka kila mtu anayetaka huduma za serikali kupokea chanjo kwa ukamilifu. Shirika la Human Rights Watch limesema leo kuwa huo ni ukiukaji wa haki za msingi za binadamu.
Masharti hayo yaliyopendekezwa, yalitangazwa mwezi uliopita. Yataanza kutekelezwa tarehe 21, Disemba 2021, ikizingatiwa kuwa asilimia 10 ya watu wazima nchini Kenya walikuwa wamepokea chanjo mwishoni mwa Novemba, kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Afya. Masharti hayo yanatishia kukiuka haki za kufanya kazi, kupokea huduma za afya, haki za elimu na mafao ya jamii kwa mamilioni ya Wakenya.
“Pamoja na kuwa serikali ina wajibu wa kuwalinda watu wake dhidi ya vitisho vya kiafya, masharti hayo yanastahili kuwa ya busara na yanayoweza kutekelezeka,” amesema Adi Radhakrishnan, Mhudumu wa Utafiti wa Human Rights Watch. “Usambazaji wa chanjo unategemea kupatikana kwake na masharti mapya ya serikali, yatawakosesha mamilioni ya wakenya huduma muhimu za serikali.”
Tarehe 21 Novemba, waziri wa afya nchini Kenya Mutahi Kagwe, alitangaza kuwa kuanzia tarehe 21 Disemba, mamlaka zitahitaji yeyote anayetafuta huduma za serikali kutoa cheti ya chanjo ya Covid-19. Huduma ambazo mtu atazikosa ni pamoja na uchukuzi wa umma, elimu, uhamiaji, huduma za hospitali na ziara magerezani. Cheti pia kitahitajika kwa wanaoingia katika mbuga za wanyama za taifa, hotelini na katika migahawa.
Kenya ina uhaba wa chanjo ya Covid-19 za kuhakikisha kuwa watu wote wazima wanapokea chanjo na kutimiza tarehe iliyowekwa na Wizara ya Afya. Hilo limetokana na ukosefu wa usawa na usambazaji wa dozi za chanjo hiyo duniani.
Kampeni za chanjo hiyo zilianza mwezi Machi nchini Kenya huku wahudumu wa afya, walimu, maafisa wa usalama na watu walio na umri wa miaka 58 na zaidi wakipewa kipa-umbele. Mwezi Juni idadi ya watu wazima ambao walistahili kupokea chanjo hiyo iliongezeka. Kwa sasa, chanjo za AstraZeneca, Moderna, Pfizer, Johnson & Johnson na Sinopharm zinapatikana nchini Kenya. Hata hivyo takwimu za Wizara ya Afya, zinaonesha kuwa kuna uhaba wa chanjo hizo. Taifa la Kenya, lenye idadi ya watu wazima milioni 27.2 na idadi ya watu milioni 55, limepokea takriban dozi milioni 23 kufikia Disemba 11 tangu kuanza kwa mpango wa chanjo.
Kenya, kama mataifa mengine yenye uchumi mdogo na wa wastani, haswa Afrika, imejitahidi kupata chanjo kwa sababu ya wananchi wake. Zaidi ya asilimia 80 ya chanjo zote duniani zimeelekezwa kwa mataifa yenye uwezo mkubwa kiuchumi ya G20, ilhali mataifa yenye uwezo mdogo wa kiuchumi, yamepokea tu asilimia 0.6 ya chanjo zote. Haya ni kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO). Kenya ilipokea dozi milioni 1.02 pekee ya chanjo ya AstraZeneca mwezi Machi kuanza mpango wa kuchanja idadi ya watu wake wazima milioni 27.2.
Idadi kubwa ya chanjo hizo haijasambazwa kwa usawa kote Duniani kama ilivyoripotiwa, kwa sababu ya kiwango kidogo cha viwanda katika mataifa machache. Kupo pia kukataa kwa mataifa na kampuni za dawa zilizotengeza chanjo hizo kushiriki teknolojia na kampuni nyingine na mashirika mengine ya WHO.
Wataalamu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, akiwemo mjumbe maalum wa afya Dkt. Tlaleng Mofokeng, amekosoa tabia hii ya kutoa chanjo kwa njia za ubaguzi ambayo inafanywa na mataifa tajiri. Wataalamu hao wanasema kuwa “hakuna nafasi ya uzalendo ya kukabiliana na janga hili. Janga hili la kiwango kikubwa na gharama kubwa, linahitaji ushirikiano kwa misingi ya kuzingatia haki za binadamu na ujasiri kutoka kwa mataifa yote.” Wataalamu hao pia wameelezea wasiwasi wao kuwa baadhi ya serikali zinajaribu kutafutia raia wake chanjo, hali ambayo huenda ikadhalilisha malengo ya kutoa chanjo hiyo kwa watu wengi.
Tangazo lililotolewa tarehe 21, Novemba, linalomtaka kila mkenya kupewa chanjo, halielezei jinsi masharti haya mapya yatakavyoendeshwa na kutekelezwa wala halijatoa njia mbadala, kwa wale ambao hawawezi kupokea ama wenye matatizo ya afya. Hilo linawafanya kukosa huduma. Alipoulizwa kutoa maelezo kwa kina, Waziri Kagwe alisema “ Pamoja na kwamba tungependa kutekeleza masharti haya, uwajibikaji wake unategemea watu binafsi.”
Vyombo vya habari nchini Kenya vimeripoti kuhusu uamuzi wa serikali wa kutoa ilani ya mwezi mmoja. Kwa mujibu wa Muongozo wa Maswali yanayoulizwa mara kwa mara kuhusu chanjo ya Covid-19 uliyochapishwa na Wizara ya Afya, masharti yatakayozingatiwa yatalenga idadi ya dozi inayohitajika kwa aina ya chanjo itakayotolewa.
Chanjo nyingi ambazo zinapatikana nchini Kenya kwa sasa zinahitaji mmoja kupokea dozi mbili ili kukamilisha utaratibu wa chanjo. Chanjo ya pili hutolewa kati ya majuma 4-12 baada ya ya kwanza kutolewa. Yote hutegemea aina ya chanjo aliyopewa mtu. Kuna uwezekano mkubwa kuwa hata watu watakaopokea chanjo hiyo tarehe 21 Disemba, watakabiliwa na vikwazo.
Serikali ya Kenya imesema kuwa, sera hiyo mpya inalenga kuwashawishi watu wengi kupokea chanjo. “Ni bayana kuwa, mataifa yanapokabiliana na janga hili, inasisitizwa kuwa iwepo haja ya kuwachanja watu wengi,” Waziri Kagwe alisema alipotangaza sera hiyo.
Chini ya sheria ya haki za kimataifa, serikali ya Kenya ina wajibu wa kuhakikisha kuwa kila mmoja ana haki ya kupata huduma za afya, bila ya ubaguzi. Serikali inastahili kuipigia debe chanjo hiyo kwa kutoa maelezo, manufaa na hatari zake kwa afya ya mtu kwa uwazi. Kuwataka watu kutoa thibitisho, ili wapate huduma za umma, huenda kukawachochea kupokea chanjo, lakini pia jinsi inavyoendeshwa, huenda kukachangia sababu nyingi za mtu kutopata chanjo hiyo kwa wakati ufaao, limesema Shirika la Human Rights Watch.
Sera ya busara inayoweza kutekelezeka inastahili kuwapa nafasi wale ambao hawajachanjwa ili wapate huduma muhimu kama vile za afya bila ya kuhatarisha maisha yao.
Wajibu wa serikali ya Kenya kwa haki za binadamu ni kuhakikisha kuwa chanjo ya Covid-19 inapatikana kwa kila mtu licha ya mataifa yenye utajiri mkubwa kushindwa kushirikiana na mataifa mengine na kampuni za kutengeza chanjo kushindwa kushiriki teknolojia hiyo. Kwa zaidi ya mwaka mmoja, juhudi za kuifanya chanjo ya Covid-19 kupatikana pamoja na tiba kwa kuondoa ushuru wa Mwafaka wa Biashara na haki miliki zimezuiliwa na mataifa yenye mapato makubwa.
Serikali zote zina wajibu wa kushirikiana, sio kuingilia uwezo wa mataifa mengine wa kutimiza wajibu wa haki za binadamu na kushiriki matokeo ya manufaa ya kisayansi, Shirika la Human Rights Watch limesema.
Serikali ya Kenya pia ina wajibu wa kuhakikisha kuwa sera kandamizi haziwazuii watu kupokea huduma za msingi ama kupata mahitaji yao ya kimsingi. Kupata haki ya afya kunajumuisha, wajibu wa kuzuia na kudhibiti janga ambalo chanjo ni ala muhimu. Lakini kila mtu ana haki ya kupata huduma za afya, bila ya kujali iwapo wamepokea chanjo au la. Mpango wa chanjo unastahili kubuniwa kwa kuzingatia changamoto za kijamii, kisiasa na kiuchumi ambazo huenda zikawakabili watu, zikiwemo upatikanaji wa chanjo hizo.
“Pamoja na kuwa chanjo huenda ikawa muhimu, zinastahili kutolewa kwa kuzingatia mkakati mpana wa afya ya umma ambao unasisitiza upatikanaji wa chanjo yenyewe na njia nyingine za kukinga Covid-19,” Radhakrishnan alisema. “Chanjo haifai kuwa mzigo kwa idadi au kundi lolote la watu ama ije kukiuka haki za binadamu.”