(Nairobi) – Janga la Korona (Covid-19) limeonyesha kwamba serikali za Afrika zinafaa kuimarisha mifumo ya ufadhili wa kijamii ili kutimiza mahitaji ya kimsingi ya watu -kwamba wanaweza kuitegemea serikali kuwapa maisha ya kuheshimika wakiwa wanadamu, Shirika la Human Rights Watch limesema leo. Serikali nyingi za Afrika zilianzisha mipango kadhaa ikiwemo programu za kuwafadhili raia kwa pesa, kutoa misaada ya chakula baada ya kuongezeka umaskini na njaa kutokana na athari za janga la Korona. Hata hivyo imetokea kwamba familia nyingi hazikupata usaidizi huo. Benki ya Dunia inatabiri kwamba janga la Korona litaongeza idadi ya watu maskini hivi kwamba kufikia mwisho wa Mwaka 2021, watu wengine milioni 29 barani Afrika watajiunga na kundi la watu wenye umaskini mkubwa.
“Janga la Korona (Covid-19) limevuruga njia za kujipatia riziki za mamilioni ya watu barani Afrika na hivyo kuwaacha wakitatizwa kwa ukosefu wa chakula hivi kwamba wanahitaji msaada wa dharura,” asema Mausi Segun, Mkurugenzi wa Afrika - Shirika la Human Right Watch. “Serikali za Afrika zinafaa kuimarisha mifumo ya ufadhili wa jamii inayohitajika kwa kuwa itawawezesha raia wa Afrika kustahimili athari za janga la Korona kwa uchumi na kusalia na heshima za kibinadamu.”
Kati ya Mwezi Machi 2020 na Agosti 2021, Shirika la Human Rights Watch liliwahoji zaidi ya watu 270 nchini Cameroon vilevile Ghana, Kenya, Nigeria, na Uganda kuhusiana na athari za janga la Korona na namna ambavyo zimeathiri njia zao za kujipaia riziki na chakula. Vilevile Shirika lilitaka kuelewa namna ambavyo serikali zimehusika kwenye utaratibu wa kuwasaidia raia. Watafiti waliwahoji waathiriwa na familia zilizoathirika, wahudumu wa afya, maafisa wa serikali, na wawakilishi wa mashirika yasiyo ya serikali. Aidha mashirika ya kimataifa ya fedha, wafadhili, na makundi mengine yalihojiwa.
Nchini Kenya na Nigeria, Shirika la Human Rights Watch limenakili visa vya watu kupoteza kazi, mishahara na faida kwenye shughuli zao. Njaa imeenea miongoni mwa watu wanaoishi maisha ya umaskini katika miji ya Nairobi na Lagos. Nchini Kenya, utafiti huo uliangazia ongezeko la dhuluma dhidi ya wanawake na wasichana katika msimu kafyu na maagizo ya kuwazuia watu kusafiri. Nchini Ghana na Uganda, watafiti wa Shirika la Human Rights Watch walifanya uchunguzi kuhusu ongezeko la mwenendo wa kuwatumia watoto kazini. Nchini Cameroon, utafiti huo uliangazia ufisadi na ukosefu wa uwazi kwenye utaratibu wa serikali wa kutumia pesa zilizokuwa zimeandaliwa kukabili athari za kiuchumi na kiafya za janga la Korona (Covid-19).
Mahojiano yaliyofanywa nchini Nigeria, Ghana, na Uganda yaliendeshwa kwa ushirikiano na mashirika washirika yakiwemo Justice & Empowerment Initiatives (lShirika lisilo la serikali nchini Nigeria), Shirika la Friends of the Nation (la nchini Ghana), na Shirika la Initiative for Social and Economic Rights (la nchini Uganda).
Watu waliohojiwa kwenye nchi zote tano walisema masrufuku ya kusafiri, agizo la kafyu na masharti mengine yaliyotangazwa na serikali kuzuia kuenea kwa virusi vya Korona, ukiongeza na kuharibika kwa biashara na ajira na hivyo kuvuruga uchumi kulitatiza njia zao za kupata chakula na mahitaji mengine ya kimsingi. Nchini Ghana, msichana wa umri wa miaka 14 alisema, alilazimika kuanza kufanya kazi ya kusafisha samaki, kwa muda was aa tisa kila siku. Alichukua hatua hiyo baada ya shule kufungwa na hivyo akashindwa kupata chakula ambacho alikuwa akikipata shuleni. “Nisipoifanya ile kazi, maisha yatakuwa magumu kwetu sote,” alisema.
Watu wengi waliohojiwa walisema kwamba hawakuwa wamepokea usaidizi wowote kutoka kwa serikali. “Serikali haijatusaidia,” alisema karani mmoja kwenye hoteli moja jijini Douala, Cameroon. Karani huyo alikuwa akipambana kuwaelimisha watoto wake na kupata chakula baada ya kupoteza thuluthi mbili ya mshahara wake- mwajiri wake alikuwa amelazimika kupunguza mshahara wake.
Ukosefu wa ufadhili kwa watu waliopoteza kazi, ufadhili kwa ajili ya watoto, na njia nyingine za kuwafadhili watu waliopoteza mapato iwe kwa pesa au hata ushauri nasaha, au michango umeonyesha kwamba mifumo ya serikali za Afrika ya ufadhili wa kijamii ina udhaifu mwingi. Takwimu za Shirika la Leba duniani (ILO) zimefichua kwamba sio zaidi ya asilimia 20 ya raia wa Afrika walipata ufadhili wa namna yoyote kutoka kwa serikali za nchi zao Mwaka 2020. Hata ukiangalia takwimu zilizoandaliwa na serikali zao awali unaona kwamba viwango hivyo vinasalia namna ile.
Serikali nyingi za Afrika zililenga kuondoa mapengo na matatizo madogo madogo yaliyokuwapo kwenye mifumo ya ufadhili wa kijamii wakati wa janga la Korona. Zilifanya hivyo kwa kuanzisha programu kama za kuwafadhili raia kwa pesa na pia kutoa msaada wa chakula. Lakini Shirika la Human Rights Watch likifanya uchunguzi wake nchini Ghana, Kenya, Nigeria, na Uganda lilipata kwamba programu zilizokuwa zimeanzishwa zilizifikia familia chache tu kati ya familia zilizohitaji usaidizi na zilizokuwa zimelengwa.
“Tumekuwa tukisikia uvumi kwamba serikali inatoa pesa na chakula, lakini binafsi sijaona mgao wowote wa namna ile katika eneo langu,” alisema mama wa watoto saba kutoka jimbo la Lagos, nchini Nigeria, ambaye alipoteza kazi ya kusafisha kwenye kampuni moja Mwezi Machi Mwaka 2020. Alikuwa miongoni mwa wengi walioathirika kwa kupoteza kazi baada ya kutangazwa masharti ya kukabili ueneaji wa virusi vya Korona.
Utafiti uliofanywa nchini Kenya na Nigeria umeonyesha kwamba ufisadi mara nyingi umeathiri shughuli za kuwasaidia raia. Kutokana na ufisadi misaada mingi haiwafikii raia haswa wanaohitaji usaidizi. Nchini Kenya, Shirika la Human Rights Watch lilipata ushahidi ulioonyesha kwamba maafisa waliosimamia usajili wa raia waliofaa kusaidiwa kwenye programu za kuwafadhili raia kwa pesa wakiwa na wanasiasa walipuuza utaratibu wa kuwasajili watu na badala yake kuwapa pesa jamaa zao na marafiki. Familia nyingi zilizofaa kupewa usadizi huo hazikusaidiwa. “Tulifanya maandamano hadi kwenye afisi ya chifu kwa sababu kulikuwa na watu waliokuwa wakipewa pesa na misaada mingine lakini sisi hatukuwa tukipata chochote,” alisema mwalimu mmoja mjini Nairobi, ambaye alikuwa amepoteza kazi kufuatia maagizo ya kufunga shule na shughuli nyingine wakati wa kafyu. Mwalimu huyo alikuwa akipata ugumu kuwalisha watoto wake wanne wote wakiwa wa umri wa kwenda shule.
Tishio la ufisadi limenawiri kwa sababu ya ukosefu wa ufuatiliaji wa kutosha ili kujua namna ambavyo pesa zilizotolewa na mashirika ya fedha ya kimataifa, mfano Shirika la fedha duniani IMF, zilivyotumika. Ufadhili huo wa kifedha ulitolewa kwa lengo la kuwezesha njia za kukabili athari za janga la Korona. Uchunguzi wa Shirika la Human Rights Watch wa masharti ya kukabili ufisadi kwenye mikopo ya dharura iliyotolewa kwa nchi za Cameroon na Nigeria, vilevile Ecuador na Misri, ulipata kwamba habari ambazo serikali zilitoa zilitofautiana pakubwa hivi kwamba hazingeelezea ukweli ambao ungesaidia katika kufuatilia namna pesa hizo zilitumika.
Chini ya sheria za kimataifa kuhusu haki za kibinadamu, serikali zina wajibu wa kutimiza haki za raia kupata kiwango cha maisha ya kuheshimika, ikiwemo haki ya kupata chakula, maji, na makao. Na haki ya kusaidiwa na serikali kukitokea dharura. Mahitaji haya yote yanatambuliwa chini ya Sheria ya Afrika ya Haki za kimsingi . Haki ya watu kusaidiwa kukitokea dharura au majanga inataka kwamba serikali za nchi ziwe zinawasaidia raia kimatibabu, ufadhili kwa wazee, watoto, watu wasio na kazi, na usaidizi mwingine ili mtu apate viwango vya maisha vya kumfaa mwanadamu – hata kama ni wakati wa misukosuku ya kiuchumi.
“Janga la Korona (Covid-19) lilizipa funzo serikali nyingi za Afrika kwamba ni muhimu kuwa na mifumo ya ufadhili wa kijamii ambayo inatengewa pesa sio tu eti kwa kuwahakikishia watu wanaendelea kupata chakula na mahitaji mengine ya kimsingi lakini pia kuimarisha nchi kiuchumi,” alisema Segun. “Sasa changamoto iliyopo ni kujenga na kuongeza mipango ambayo imewekwa msimu wajanga ili kuanzisha programu zenye uwazi ambazo zitalinda haki za watu kupata kiwango cha maisha kimfaacho mwanadamu.”
Ili kupata mambo kwa kina kutoja kwenye tafiti za Shirika la Human Rights Watch tafadhali angalia hapa.
Ongezeko la umaskini na njaa kwa ajili ya janga la Korona (Covid-19)
Kufikia Septemba 2021, mataifa ya Afrika yalikuwa yamerekodi watu milioni 7.95 kuambukizwa virusi vya Korona huku watu 200,762 wakifariki kutokana na maradhi hayo. Hata hivyo yawezekana idadi ya walioathiriwa ikawa ya juu zaidi kwa sababu mataifa mengi ya Afrika hayana hayajawezehwa kupima maambukizi iffavyo. Kwa hivyo upo uwezekano maambukizi yapo lakini watu wengi hawajapimwa.
Janga la Korona pia limevuruga uchumi wa nchi nyingi za Afrika na hivyo kusababisha kuongezeka kwa viwango vya umaskini kote barani Afrika. Wanauchumi wa Benki ya Dunia wanatabiri kwamba takriban watu nusu bilioni au milioni 500 barani Afrika wataishi maisha ya umaskini mkubwa kufikia mwisho wa mwaka 2021. Kiwango hichi ni takriban thuluthi mbili ya idadi nzima ya watu maskini sana duniani. Watu ambao hutajwa kuwa wanaoishi maisha ya kutumia chini ya dola $1.90 kwa siku.
Maeneo mengi ya dunia yakiwa yameanza kurejelea hali ya kawaida ya maisha huku uchumi ukiendelea kukua kama ulivyokuwa awali, namna ambavyo nchi tajiri duniani na mashirika yamekuwa yakilichukulia suala la Korona imesababisha tatizo la Afrika kushindwa kupata chanjo ya Korona kwa bei nafuu. Ukosefu wa chanjo ukijumuisha na serikali za Afrika kutenga pesa kidogo za kufufua uchumi, kumechelewesha ufufuaji wa uchumi wa mataifa ya Afrika. Benki ya Dunia inabashiri kwamba umaskini barani Afrika utaongezeka mwaka 2021 kwa kiwango ambacho ni mara mbili ya utabiri uliokuwapo kabla janga la Korona.
Ongezeko la umaskini limewafanya raia wengi barani Afrika kukosa chakula, maji na mambo mengine ambayo ni muhimu kuhesabika katika maisha yanayomfaa mwanadamu. Nchini Nigeria, shirika la utafiti na takwimu la taifa hilo (National Bureau of Statistics -NBS) lina takwimu zilizochunguzwa na Shirika la Human Rights Watch, ambazo zimeonyesha kwamba viwango vya njaa vimeongezeka mara mbili. “Watu wamekuwa wakijiokoa kwa kusaidiana miongoni mwao,” alisema mwanachama wa Shirika la wakazi wa mitaa ya mapato ya chini (Nigerian Slum/Informal Settlements Federation)linaloshughulikia maswala ya watu waishio mitaa ya mapato ya chini “Huwezi kumwangalia jirani yako akifa njaa, ni bora umpe ulichonacho, iwe ni chakula basi umpe umwokoe.”
Nchini Kenya, zaidi ya watu 90 ambao ni wakazi wa mitaa ya watu wa mapato ya chini katika mji mkuu wa nchi - Nairobi, waliliambia Shirika la Human Rights Watch kwamba marufuku za msimu wa Korona ambzo zilitatiza shughuli za kujitafutia riziki zilisababisha ukosefu mkubwa wa chakula, njaa na kupoteza kazi. Mwanamke wa umri wa miaka 75- nyanya ya watu aishie jijini Nairobi, ambaye anawatunza wajukuu wenye matatizo ya akili, alisimulia matatizo aliyoyapitia kupata dawa na chakula. “Agizo la kufunga shughuli nchini lilipotolewa, biashara yangu ndogo ya sabuni ilikuwa ngumu sana,” alisema. “Singeweza tena kununua dawa. Nilikuwa naomba chakula, omba omba , na kukopa bidhaa za chakula.”
Ukiangalia Kimataifa na hasa kote barani Afrika, athari za janga la Korona ziliwatatiza zaidi wanawake na wasichana kuliko watu wengine katika jamii. Kulikuwa na kuongezeka visa vya dhuluma za kijinsia. Shirika la Human Rights Watch limepata kwamba matatizo mengi yaliyoletwa na janga la Korona Nchini Kenya, yalihusu hata kushindwa kwa serikali kuhakikisha watu wanapata huduma za matibabu, kupata nafasi kujifufua kiuchumi, na ufadhili wa kijamii wakati wa maagizo ya kutosafiri, kulichangia pakubwa katika kuongezeka kwa dhuluma za kijinsia na dhuluma nyingine dhidi ya wanawake na wasichana. Umaskini na ukosefu wa njia ya kupata mahala pengine pa kuishi ulifanya iwe vigumu kwa wale waliokuwa wakidhulumiwa kimapenzi kuondoka pale walikuwa wakidhulumiwa kutafuta usaidizi. “Nililazimika kuishi nyumbani kwangu hata nilipokuwa nadhulumiwa kwa sababu sikuwa na pa kwenda,” alisema mwathiriwa wa dhuluma za kinyumbani katika kaunti ya Kisumu.
Baada ya familia nyingi kupoteza riziki, watoto wengi kwenye nchi nyingi za Afrika wamekuwa wakikosa chakula. Shirika la umoja wa mataifa kuhusu hazina ya watoto (UNICEF) lilikisia kwamba ukosefu mkubwa wa chakula uliongezeka barani Afrika kwa asilimia 15 katika miezi ya kwanza sita ya mwaka 2020. Kufikia Aprili 2020, zaidi ya watoto milioni 50 wa umri wa kwenda shule walikuwa wamepoteza ile nafasi ya kupata chakula shuleni. Kwenye idadi hiyo, milioni 40 waliathirika kwa ukosefu wa chakula kwa takriban miezi sita. “Zipo siku tulilala njaa kwa kuwa hatukuwa na chochote cha kula,” alisema kijana wa umri wa miaka 14- ambaye ni mfanyakazi nchini Uganda. Mwajiri wake katika timbo moja ya mawe alianza kuwalipa yeye na mamaye, kwa pombe badala ya pesa, baada biashara ile kuathirika msimu wa Korona.
Ukosefu wa usawa kwenye ufadhili wa kijamii duniani.
Kwa mujibu wa shirika la Leba duniani -ILO, ni asilimia 17 tu ya waafrika ndio walipata angalau usaidizi wa namna mmoja hivi wakati wa janga Mwaka 2020- kulingana na takwimu zilizopatikana. Takwimu hizi zinashirikisha asilimia 5 ya watu waliokuwa kazini na sasa hawana kazi na asilimia 13 ya watoto.
Kulikuwa pia na hitilafu nyingi katika programu za ufadhili kwenye nchi nyingi: karibu nusu ya raia wa Afrika Kusini wangepata angalau usaidizi wa namna moja wakati wa mipango ya ufadhili wa serikali ukilinganisha na asilimia 11 nchini Nigeria na asilimia 3 nchini Uganda. Suala la watu kushindwa kufikia usaidizi lilionyesha serikali kushindwa kutenga pesa kuwezesha mifumo ya kuwafadhili raia barani Afrika, hivi kwamba serikali nyingi zinatenga chini ya asilimia 4 ya pato lake nzima (gross domestic product -GDP) kwa ajili ya ufadhili wa kijamii, bila hata kujumuisha huduma za matibabu, ukilinganisha na kiwango cha kimataifa ambacho ni asilimia 13.
Suala la raia kushindwa kufikia ufadhili wa kijamii barani Afrika linaonyesha namna ambapo ukosefu wa usawa kwenye huduma kama hizi ulivyo kote duniani. Mataifa hutenga pesa kwa viwango vinavyotofautiana ajabu. Hali hii iliongezeka athari za janga la Korona. Mwezi Mei 2021, takwimu za Benki ya Dunia zilionyesha kwamba raia wa nchi zenye mapato mazuri ambazo ni tajiri walikuwa wamenufaika kwa ufadhili wa kijamii kupitia mipango ya kuwasaidia raia wakati wa janga la Korona, hivi kwamba kila raia alikuwa amepewa dola za Marekani $847. Lakini raia wa nchi za Afrika walikuwa wamepewa dola $28 mtu mmoja.
Ukuaji huu wa mapengo kwenye utaratibu wa raia wa nchi husaidiwa umesababisha wito kutoka kwa Muungano wa kimataifa wa mashirika yasiyo ya serikali, na mwandishi maalum wa umoja wa mataifa wa masuala ya umaskini na haki za kimsingi Olivier De Schutter, kwa serikali kote duniani kwamba zianzishe Hazina ya kimataifa ya kuwafadhili raia ikiwa njia ya kutatua tatizo la kuongeza ufadhili wa pesa kwenye miradi ya kuwafadhili raia kwenye nchi zenye mapato ya chini.
Juhudi za kuongeza ufadhili wa kijamii wakati wa janga la Korona
Ili kuondoa mapengo yaliyoonekana kwenye mipango ya ufadhili wa jamii kuwasaidia raia kwenye mwanzo wa janga la Korona, nchi 51 kati ya 55 wanachama wa Umoja wa Afrika kufikia mwezi Mei zilikuwa zimetangaza jumla ya hatua 238 zilizoongozwa za ufadhili wa jamii. Shirila la Leba Duniani-ILO lilisema kwamba asilimia 86 ya hatua zilizochukuliwa zilikuwa za ufadhili wa jamii au kuwa zisizohitaji watu kuchangia. Hatua ambazo zinafadhiliwa kwa ushuru unaotozwa na serikali wala sio michango ya watu wanaofaa kunufaika. Asilimia 21 ilihusu programu za kuwafadhili raia kwa pesa au njia nyingine za usadizi huku asilimia 16 ikiwa kupitia utoaji chakula na mahitaji mengine ya lishe.
Nchini Nigeria, ambapo zaidi ya asilimia 40 ya watu wake milioni 211 wanaishi maisha ya umaskini mkubwa, serikali ya taifa hilo imeongeza kiwango cha pesa kwenye programu za kuwafadhili raia ambapo ilikuwu ikitoa pesa za Nigeria almaarufu Naira -5,000 kiwango sawa na dola $12 za Marekani kwa kila familia kwa mwezi. Malipo hayo yalitolewa kwa karibu familia milioni 1 mwezi Juni mwaka 2020. Hata hivyo idadi ya familia zilizosaidiwa ilishuka hadi kufikia 400,000 mwezi Desemba Mwaka 2020. Serikali ya Nigeria pia ilianzisha mradi wa usaidizi wa haraka Mwezi Januari 2021 ikilenga familia nyingine milioni 1. Kwa mujibu wa takwimu za serikali, serikali zote za Nigeria, -serikali ya taufa ba serikali za majimbo zilizisaidia familia milioni 8.8 kwa misaada ya chakula ya muda mfupi.
Nchini Kenya, mwaka 2020 serikali ilitoa shilingi 4,000 za Kenya kwa kila raia miongoni mwa watu Milioni 1.1, kiwango sawa na dola 37 za Marekani kila baada ya miezi miwili. Zilitolewa chini ya programu za kuwafadhili raia kwa pesa. Mbali na hayo serikali ilianzisha njia mpya kwa ajili ya janga la Korona ya kuwasaidia raia kwa shilingi 1000 kiwango sawa na dola 9 za Marekani kwa wiki. Kwa mujibu wa takwimu za serikali usaidizi huo uliwafikia watu 332,563 kuanzia Mwezi Aprili hadi Novemba 2020.
Programu za kuwasaidia raia kwa pesa, ufadhili wa kijamii uliwaacha wengi bila usaidizi
Licha ya kuongeza usaidizi wa kijamii, serikali za Afrika zimeendelea kuwaacha watu wengi wakikosa ufadhili wa kifedha au usaidizi mwingine wa namna wakati wa janga la Korona. Shirika la maswala ya watoto la UNICEF lilikisia kwamba programu za kuwafadhili raia kwa pesa zilizoenezwa kati ya Mwezi Aprili na Septemba Mwaka 2020 ziliboresha njia za kuwasaidia raia kwa asilimia 8 hivi katika nchi 27 za barani Afrika. Kwa hivyo ziliyaacha mapengo makubwa baina ya viwango vya umaskini na juhudi za kueneza usaidizi kwa watu.
Nchini Nigeria, tathmini ya Shirika la Human Rights Watch ya takwimu za shirika la utafiti na takwimu -NBS ilifichua kwamba katika Miezi ya Mei, Agosti na Novemba Mwaka 2020 familia zilizopokea usaidizi wa pesa na chakula hazikuwa zaidi ya asilimia 15 kote nchini. Karibu nusu ya familia zilizofanyiwa ukaguzi zilikuwa zimepungukiwa chakula katika muda wa siku 30 zilizokuwa zimepita. “Walitangaza kupitia mitandao ya kijamii kwamba watu watapata Naira 5,000 [sawa na Dola 12 za Marekani] pesa kutoka programu za ufadhili,” alisema mwendeshaji teksi jijini Lagos. “Lakini ilikuwa tu ahadi bure isiyo ukweli. Watu wengi sana hawana njia za kukabili maisha, nao maafisa katika serikali walikuwa tu wakishughulikia mahitaji yao pekee.”
Usaidizi mdogo ambao watu waliupata wakati wa Korona uliwafanya watu wengi kuanza kuuliza maswali kuhusu namna serikali ya Nigeria ilitumia pesa zilizotengewa harakati za kukabili athari za Korona. “Tulipata habari za pesa ambazo serikali ilifaa kuzipata kushughulikia janga la Korona – yalikuwa mabilioni ya Naira— halafu serikali ilizungumzia chakula ambacho ilikuwa ikitoa, lakini jamii nyingi za watu hazikupata chakula hicho,” alisema mhudumu wa afya ambaye hufunza masuala ya afya mjini Lagos. Ripoti ya pamoja ya mashirika matatu yasiyo ya serikali inayohusu ugawaji chakula jijini Lagos katika msimu wa janga ilipata kwamba “wanasiasa walipora bidhaa za chakula mashinani” wala “hakukuwa na utaratibu wa kuwafaa wote wa kuwatambua watu wenye mahitaji mengi waliofaa zaidi kusaidiwa.”
Nchini Kenya, Shirika la Human Rights Watch lilihakikisha kwamba chini ya asilimia 5 ya familia 600,000 zinazoishi katika mitaa ya mapato ya chini jijini Nairobi zilinufaika kwa programu za kuwafadhili raia kwa pesa kati ya Mwezi Aprili na Novemba 2020. Wakazi wengi wa Nairobi ambao hawakupokea pesa za ufadhili waliliambia Shirika la Human Rights Watch kwamba kiwango cha pesa walichopokea kilikuwa kidogo. Vilevile walisema kwamba utoaji wa pesa haukujulikana utakuwa lini au mara ngapi kwa mwezi. “Nilianza kupokea shilingi 1,000, (dola 10 za Marekani) kwa wiki Mwezi Aprili 2020, lakini pesa hizo hazikutosha,” alisema mama ya watoto watatu. “Nilikuwa nikizitumia zote siku ile ile kwa mahitaji ya kinyumbani.”
Masharti yalikuwa mabaya zaidi kwa wale hawakupata pesa hizo hata kidogo. “Sikuwa na chakula cha kuwapa watoto wangu, hata wangelia mfululizo kwa siku kadhaa,” alisema mwanamke mmoja mwenye watoto wawili na asiye na mume. Alilazimika kukiuka masharti yaliyokuwa yamewekwa kwa ajili ya Korona, akaondoka mtaani kutafuta kazi ya kufua nguo ili alipwe ada kidogo.
Nchini Uganda, Shirika moja lisilo la serikali Initiative for Social and Economic Rights, lilikisia kwamba Mwezi Desemba Mwaka 2020 ufadhili wa kijamii ulikuwa unafanyika kwenye asilimia 3 ya watu Milioni 9.5 “waliohitaji misaada ya dharura kuwaweka katika hali ifaayo.” Watoto wengi, kati ya 32 ambao Shirika la Human Rights Watch liliwahoji kuhusu na athari za janga la Korona walisema kwamba walikuwa wametafuta kazi kwa sababu familia zao zilikuwa zimeshindwa kutimiza mahitaji ya kimsingi. Msichana mmoja wa umri wa miaka 13 alisema kwamba, kabla aanze kuuza vifagio kando kando ya barabara, familia yake ilikuwa inategemea chai na uji kuwa ndicho chakula chao. “Nilianza kufanya kazi kwa sababu tulikuwa katika hali mbaya ajabu,” alisema msichana huyo. “Njaa pale nyumbani ilikuwa nyingi hata hatungeketi tu tusubiri.”
Nchini Ghana, watoto 21 kati ya 24 waliohojiwa walisema familia zao hazikuwa zimepokea usaidizi wowote kutoka kwa serikali. Watoto wengi walikuwa wameanza awali kufanya kazi na waliongeza muda wa kufanya kazi msimu wa janga ili kujisaidia au kuzisaidia familia zao. “Nilitafuta kazi ili nijitunze mwenyewe,” alisema mvulana wa umri wa miaka 15. Alisema rafiki zake walimfahamisha kwamba zipo pesa na walikuwa wakizipata kwenye kazi ya kubeba bidhaa na mizigo.
Nchi zilizokuwa na mifumo ya ufadhili wa kijamii iliyokomaa hata kabla ya janga la Korona zimekuwa na ufanisi kwenye utaratibu wa kuwasaidia raia. Afrika Kusini imekuwa na mpango wa ufadhili wa kijamii kwa muda ilikuwa tayari ikitoa pesa kwa ajili ya watoto na jamii, kwa raia milioni 18 nchini . Baada ya kutangazwa janga, nchi hiyo ilitoa “nyongeza” kwenye malipo hayo kwa watu walioorodheshwa kufaa kusaidiwa kati ya Mwezi Mei na Oktoba Mwaka 2020.
Afrika Kusini pia ilianzisha ufadhili maalumu wa pesa (Randi) 350 sawa na dola 24 za Marekani kuanzia mwezi Mei Mwaka 2020 ambao ulionngeza ufadhili wa kijamii kwa watu milioni 6 ambao hawakuwa na kazi na hawakuwa wakipokea usaidizi mwingine wowote. Nchi hiyo ilikumbwa na ongezeko la kutisha la njaa mapema katika kipindi cha Korona, lakini usaidizi wa serikali na ufadhili ulizisaidia familia nyingi kupata ufadhili wa kijamii kutokana na athari mbaya za janga la Korona. Hatua hiyo ilichangia pakubwa kwenye mjadala wa kitaifa kuhusu kuanzisha kwa ufadhili wa kimsingi kwa wote.
Haja ya kupata mifumo ya kudumu ya ufadhili wa kijamii katika nch za Afrika
Kadri janga la Korona linapoendelea kuenea barani Afrika, serikali za Afrika zinafaa sasa kuanza kuongeza programu nyingi zilizoanzishwa kwa ajili ya Korona ili kupata mipango thabiti ya ufadhili wa raia kuhakikisha kwamba familia ambazo zimepoteza kazi na mapato zinaweza kudumisha viwango vya maisha yawafaayo wanadamu.
Serikali za Afrika zinafaa kushirikisha suala la ufadhili wa kijamii kwenye sheria zinazotungwa, ili liwe jukumu la lazima la serikali. Hali ikiwa hivyo itabidi serikali ziwe zikianzisha hazina, na kutoa nafasi kwa raia kusaidiwa kila mara dharura inaporipotiwa. Sheria kama itafaa ziangazie masuala kama, marupurupu kwa ajili ya watoto kwa kila raia wa nchi, usaidizi wa kifedha kwa watu wanaopoteza kazi na watu wa umri wa utu uzima wasio na kazi, ufadhili ufanyike kote katika sekta ya umma na sekta binafsi. Serikali zafaa kulinda hazina zinazoanzishwa zikilenga kufadhili jamii wakati wa majanga kama ya Korona ili hazina hiyo isiwe ikiathirika kwa hatua za serikali kupunguza viwango vya pesa mara zikiandaa bajeti mpya. Vilevile serikali zafaa kuandaa mapendekezo ya kutafuta pesa zaidi hasa kupitia ushuru unaokusanywa.
Taasisi za kimataifa za fedha na wafadhili zafaa pia kuongeza viwango vya ufadhili na hata ufadhili wa kiufundi ambao bila shaka utasaidia nchi nyingi za Afrika kujenga mifumo ifaayo ya ufadhili wa kijamii kote barani. Mashirika ya wafadhili pia yasiwe yanatangaza masharti na vikwazo ambavyo vitazilazimisha serikali za Afrika kupunguza viwango vya pesa ambazo zimetenga kwa ajili ya ufadhili wa kijamii katika msimu wa janga la Korona. Ufadhili wowote wa kutoka kwa jamii ya kimataifa uliolenga kuhamasisha usaidizi kwa kijamii barani Afrika wafaa kuandamana na vikwazo vya kukabili ufisadi na kufanya taasisi za serikali zilizopokea ufadhili ziwajibikie namna zilitumia pesa ambazo zilipokea kutoka kwa wafadhili.