Skip to main content

Tanzania: Maswali na Majibu juu ya Marufuku ya Wasichana Wajawazito na Mkopo wa Elimu kutoka Benki ya Dunia

Utangulizi

Mnamo Machi 31, 2020, Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya Dunia iliidhinisha mkopo wenye utata wa kiasi cha Dola za Marekani 500 Milioni kwa serikali ya Tanzania kwa ajili ya program ya elimu ya sekondari. Msingi wa utata huu ni utekelezaji wa marufuku ya shule huko Tanzania iliyowekwa na Rais John Magufuli tangu 2017 ambayo inawabagua wanafunzi wenye ujauzito, wenye watoto na walioolewa. Katika wiki za hivi karibuni, kumekuwa na mkanganyiko mkubwa juu ya msimamo wa serikali ya Tanzania katika suala la kuwaruhusu wasichana wajawazito kusoma katika shule za umma.

Benki ya Dunia pia imetoa taarifa zisizo sahihi zinazo kataa uwepo wa sera ya kufukuzwa shule, na kuwatambua wasichana wanaofukuzwa kanakwamba “walioacha shule”. Benki ya Dunia pia imeshindwa kusikiliza rufaa kutoka vikundi vya asasi za kiraia ambavyo vimekusanya na kuhifadhi madhara ya sera hii na kueleza wasiwasi wao kwa Benki ya Dunia, mfadhili mkubwa zaidi wa kimataifa wa Tanzania, kwa kuidhinisha vitendo na misimamo ya kibaguzi ya serikali kwa kuunga mkono mkopo mpya uliopitishwa. Maswali na Majibu haya yanaangazia ombwe la taarifa kuhusiana na mkopo, na kutoa taarifa zaidi za wajibu wa haki za binadamu kwa serikali na Benki ya Dunia, pamoja na mapendekezo ya kinachopaswa kufanywa na pande zote ili kurekebisha haki za wasichana wote kupata elimu nchini Tanzania.

Je, sera ya Tanzania ya kufukuza na kupiga marufuku shule inasemaje?

Maafisa wa Tanzania wamekuwa wakisema mara kwa mara kwamba hawana sera yenye kusema wazi kwamba wasichana wajawazito au walioolewa hawaruhusiwi kwenda shule. Hata hivyo, kufukuzwa kwa wasichana wajawazito kutoka shule za umma kunaruhusiwa chini ya kanuni za elimu Tanzania, ambayo inasema kwamba “kufukuzwa kwa mwanafunzi shule kunaweza kutokea pale … mwanafunzi huyo … ametenda kosa kinyume na maadili” au “alieingia kwenye ndoa.” Sera haitoi ufafanuzi ni yepi makosa ya kimaadili, lakini maafisa wa shule mara zote hutafsiri ujauzito kama mojawapo la kosa hilo.

Rais John Magufuli wa Tanzania ameunga mkono kwa nguvu marufuku ya wanafunzi wajawazito na kuapa kuisimamia kipindi chote cha awamu yake. Kama kulikuwa na ukosefu wowote wa uelewa juu ya sera hii, maneno ya Magufuli yameifanya kuwa sera rasmi ya serikali. Magufuli pia amezituhumu kimakosa taasisi zisizo za kiserikali ambazo zimekuwa zikiitaka serikali kuruhusu kinamama watoto kurudi shule kuwa “zinatumika na watu wa nje”. Waziri wa Mambo ya Ndani Mwigulu Nchemba alitishia kufuta usajili wa vikundi vinavyotetea elimu kwa wamama watoto. Mamlaka pia zimewakamata baadhi ya wasichana wa shule kwa kuwa wajawazito na kuzidhalilisha familia zao.  

Maafisa Waandamizi katika Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Tanzania wamewaambia Human Rights Watch kuwa kuwaruhusu wasichana wajawazito kuendelea kubaki shule kutafanya mimba za nje ya ndoa kuonekana jambo la kawaida, kuwaondolea adhabu wasichana na kupelekea “athari ya samaki mmoja akioza” ambapo wasichana wengi watashika mimba. Hoja hizo hazina mashiko yoyote ya kiutafiti. Maafisa wa Tanzania mara kwa mara wanachukua vipimo vya lazima vya ujauzito kwa wasichana kama hatua ya kinidhamu na kuwafukuza moja kwa moja wale wanaopatikana na ujauzito.

Vipimo vya lazima vya mimba pekee ni ukiukwaji mkubwa wa haki ya faragha kwa wasichana, usawa na uhuru, na inaweza kupelekea wengine kuacha shule wenyewe.

Wakati maoni mengi ya umma yamelenga wasichana wa shule za sekondari, kwa mujibu wa sera, wasichana wa shule za msingi ambao wanapata ujauzito au kuolewa pia wanafukuzwa na hawana mbadala wa uhakika kurudi katika mfumo rasmi wa shule.

Mnamo Aprili 6, 2020, taarifa iliyotolewa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuhusu Mkopo wa Benki ya Dunia ilithibitisha kwamba wasichana watanufaika na mpango wa Benki wa Kuboresha Elimu ya Sekondari Tanzania (SEQUIP) ambao unawezesha “njia mbadala ya elimu” (AEP), lakini haikueleza kwamba wasichana wajawazito wanaweza kurudi shule za umma. Marufuku ya Tanzania iko pale pale.

Wasichana wangapi wanaathirika na sera hii?

Hakuna takwimu sahihi, lakini vyanzo mbalimbali vinakadiria kwamba maelfu ya wasichana wameathirika na sera hii. Benki ya Dunia inakadiria wanafunzi wajawazito 5,500 wanaacha kwenda shule kila mwaka, ijapokuwa makadirio ya awali yalionyesha kwamba karibu wanafunzi 8,000 wamelazimika kuacha shule kila mwaka.

Kutokana na kuenea na kukomaa kwa utaratibu wa kuwafukuza wasichana wajawazito, tena katika njia za kudhalilisha, wasichana huacha kwenda shule kwa sababu wanajua watafukuzwa.

Fursa zipi zinapatikana kwa wasichana wajawazito au walioolewa ambao walifukuzwa kurudi katika mfumo rasmi wa elimu?

Mfumo wa elimu Tanzania unatoa njia mbadala chache ambazo ni halisia kwa maelfu ya wanafunzi ambao wanafukuzwa shule kutokana na ujauzito.

Kuna njia mbili za kuchagua kuendelea na elimu kwa watoto wote walioacha shule ili kuwawezesha kufanya mitihani ya taifa (kidato cha nne au Sekondari ngazi ya chini) kama wanafunzi waliohudhuria shule za sekondari za umma, wanapata cheti cha kumaliza shule ya sekondari na kuendelea shule za sekondari ngazi ya juu (A levels) ambayo siyo lazima. Wanaweza kujiunga na shule binafsi za sekondari au kujiunga na Shule za Wazi na Vyuo vya Maendeleo ya Watu Wazima, ambayo kwa sasa SEQUIP imeikusanya kama “njia mbadala ya elimu” (AEP).

Wanafunzi wanaotaka kumaliza sekondari ngazi ya chini (O Level), kama vile wasichana waliofukuzwa shule baada ya kupata ujauzito au wale walioacha shule ili kufanya kazi, wanapaswa kujisomea wenyewe au kujiandikisha na kulipa ada ambayo inaweza kufikia takribani Shilingi za Kitanzania (TZS) 500,000 (US$ 227) kwa mwaka kwa ajili ya kupata elimu katika vyuo binafsi. Wanafunzi wanaochagua njia hii humaliza masomo yao ambayo yamefupishwa kutoka miaka minne ya elimu ya sekondari ngazi ya chini (O Levels) kuwa miaka miwili. Kupata elimu nzuri ya ufundi stadi ni ngumu na gharama vilevile. Vijana wanaoacha ngazi ya chini ya sekondari kabla ya kumaliza wanakosa sifa,vigezo na masomo yanayotakiwa ili kusoma shahada ya elimu rasmi ya ufundi stadi na maarifa. Badala yake, vijana wanaoacha shule wanaweza kujiunga kwa kozi fupi za ufundi stadi na kupata cheti cha ujuzi. Wakati vituo vya elimu ya watu wazima vinawapa wanafunzi elimu ya msingi na ujuzi wa kujitegemea na kujiajiri, bado sio sawa na shahada kamili ya elimu ya ufundi stadi, ambayo hutolewa katika vituo vilivyothibitishwa vya Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA). Kwa sasa, kuna mgawanyo usio sawa wa shule za ufundi stadi- na zote zina ada ya malipo. Utafiti wa Human Rights Watch unaonyesha kwamba baadhi ya vijana wanajiunga na program za elimu ya ufundi stadi na ujuzi kupitia taasisi zisizo za kiserikali ambazo hutoa udhamini na kuwasaidia wanafunzi kushughulikia vikwazo vya kiutawala na mara kadhaa kuwalipia gharama za huduma za bweni.

Kuna maoni gani kuhusu mkopo wa Benki ya Dunia wa Dola za Marekani Milioni 500 wa elimu Tanzania?

Kuna maoni mengi kuhusiana na mkopo huu. Maoni haya ni pamoja na: msaada wa kifedha na kuidhinishwa kwa mfumo sambamba wa elimu ambao ni wa kibaguzi na utawaacha watoto wengi wakishindwa kupata elimu ya sekondari; kushindwa kutoa taarifa sahihi kuhusu sera ya serikali ya kufukuza, changamoto za ushiriki wa vikundi vya asasi za kiraia katika kufuatilia utekelezaji wa program ya SEQUIP; na kushindwa kwa Benki ya Dunia kufuata miongozi yake ya ndani kuhusu haki za binadamu.

Benki ya Dunia inapaswa kufanya kazi na serikali kusukuma mbele mfumo wa elimu ambao ni shirikishi kwa wote ikiwemo wasichana katika shule za umma, ikijumuisha wale ambao ni wajawazito au wazazi. Badala yake, Benki ya Dunia imeshindwa kutumia ushawishi/nguvu yake na sasa inaungana na mfumo wa kibaguzi wa serikali ya Tanzania wa muenendo wa kupiga marufuku.

Novemba 2018, Benki ya Dunia ilizuia mkopo wa Dola za Marekani milioni 300  kwa ajili ya elimu ya sekondari Tanzania sababu mojawapo ikiwa ni unyanyasaji kwa wasichana wajawazito unaofanywa na serikali. Katika kulishughulikia hilo, serikali ilikubali kukabiliana na ubaguzi dhidi ya wasichana, kurekebisha Sheria ya Takwimu ambayo ilitambua uchapishaji wa takwimu bila idhini ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu kama uhalifu, na kuzuia matamko ya maafisa wa serikali ya kuchochea ghasia dhidi ya jamii ya wanaovutiwa na wapenzi wa jinsia moja, wanaume wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja, wenye kuvutiwa kimapenzi na jinsia zote, na waliobadili jinsia  (LGBT).

Hafez Ghanem, makamu wa rais Benki ya Dunia Afrika, alinukuliwa akisema: “elimu kwa wasichana ni kitovu cha maendeleo, na sisi ni taasisi ya maendeleo, hatuwezi kukubali kwamba baadhi ya wasichana wananyimwa haki ya kupata elimu. Kama tukikubali hilo, hatutakuwa tunafanya maendeleo.”

Kutotimiza elimu ya lazima

Mkopo wa Benki ya Dunia umetoa fedha kwa ajili ya Programu ya Kuboresha Elimu ya Sekondari Tanzania (SEQUIP), ambayo inalenga kuongeza upatikanaji wa elimu ya sekondari kwa wasichana kwa kujenga madarasa zaidi, kuboresha vitabu vya kiada na utoaji elimu, kukabiliana na ukatili wa kijinsia mashuleni na njiani kuelekea shule, na kuhamasisha mazingira ya shule yenye kujali suala la jinsia. Hata hivyo, SEQUIP itakubali wasichana kusoma katika zinazojulikana kama “njia mbadala za elimu,” au vituo sambamba vya elimu, ambazo Benki ya Dunia imezitambua kama mbadala sahihi wa elimu ya sekondari. Lakini hizi njia mbadala za elimu haziwezi kuchukuliwa kana kwamba zinatoa elimu sawa na ile inayotolewa katika mfumo rasmi wa elimu kwa shule za sekondari ngazi ya chini.

  • Watoto ambao wako nje ya mfumo rasmi wa shule wanaweza kushiriki “njia mbadala ya elimu” AEP ili kuwa sawa na wale wa mfumo rasmi na kusoma mtaala uliofupishwa wa shule za sekondari. Human Rights Watch ilifanya utafiti katika programu hizi na kugundua matatizo makubwa katika ada, udhaifu katika ubora wa elimu na changamoto za upatikanaji kwa wale waliojaribu kupata.
  • Vituo vya AEP vinahitaji ada, wakati shule za msingi na sekondari ngazi ya chini hazihitaji ada wala gharama nyinginezo. Benki ya Dunia imesema inataka kuifanya elimu ya AEP kuwa nafuu zaidi lakini sio bure. Vile vile, wanafunzi wa shule za sekondari wanasoma masomo mbalimbali, wakati AEP itatoa mtaala uliofupishwa na hautofundisha masomo yote na kutoa elimu sawa na ile ya mfumo rasmi.
  • Kusoma katika vituo hivi mbadala ndio chaguo pekee la wasichana waliofukuzwa shule kwa kuwa wajawazito. Hawawezi kurudi katika mfumo rasmi wa elimu ya msingi au sekondari ngazi ya chini.

Ubaguzi na uwasilishwaji usio sahihi wa sera na mienendo ya serikali

Kwa kuidhinisha mkopo huu kwa Tanzania, Benki ya Dunia inaunga mkono moja kwa moja hatua zisizo sahihi kama zile za chaguo sambamba za elimu ambazo zinaendeleza ubaguzi na zinaweza kuchochea muendeleo wa sera za kibaguzi za serikali.

Benki ya Dunia pia imewasilisha taarifa zisizo sahihi juu ya sera ya kufukuza. Katika uidhinishaji wake wa mkopo, Benki ya Dunia iliangalia wasichana ambao ni wajawazito au wenye watoto kama wanaoacha shule kwa matakwa yao. Vile vile ilisema kwamba “hakuna sera ya serikali ambayo inaeleza kwamba wanafunzi wanaopata ujauzito lazima wafukuzwe katika shule za umma.” Katika kulielezea suala hili katika mtazamo huu, Benki ya Dunia ilipuuzia ushahidi huru ambao unaonyesha kwamba, kiutendaji, wasichana hufukuzwa shule na kudhalilishwa na maafisa wa shule na waalimu wanapolazimishwa kufanya vipimo vya mimba au kugundulika kuwa wajawazito, na matokeo yake mara nyingi kukataliwa na wenzao.

Kushindwa kuzingatia Mfumo wa Benki ya Dunia wa Mazingira na Jamii (ESF)

Kurudi nyuma kwa Benki ya Dunia juu ya haki za wasichana wajawazito kupata elimu kunaleta wasiwasi kuhusuu azma pana ya benki katika kutekeleza Mfumo wa Mazingira na Jamii ambao unahakikisha kwamba mikopo ya benki haitumiki kuchochea ubaguzi, na kwamba fedha kutoka Benki ya Dunia haziwezi kutumika kukandamiza vikundi vilivyotengwa.

Wasiwasi mkubwa juu ya dhuluma dhidi ya asasi za kiraia, uhuru wa kujieleza

Mafanikio ya mradi wa SEQUIP yanaweza kufikiwa kwa kushirikisha vikundi vya asasi za kiraia Tanzania katika kufuatilia utekelezaji wake. Taasisi zisizo za kiraia Tanzania zimeiandikia Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya Dunia kuelezea wasiwasi wao kufuatia kuundwa kwa mfumo mbadala wa elimu, na wakati huo huo wameelezea wasiwasi wao kufuatia Benki ya Dunia kuidhinisha program hii.

Hali ya sasa ya mazingira ya haki za binadamu Tanzania hairuhusu ufuatiliaji huru wa mkopo huu kupitia vikundi hivi. Tangu 2015, Tanzania imeongeza ukandamizaji kwa vyombo vya habari, watetezi wa haki za binadamu, na vyama vya upinzani. Serikali imezuia kwa kiasi kikubwa shughuli za taasisi zisizo za kiserikali, ikiwa ni pamoja na zile zinazopinga namna wasichana wajawazito na wamama watoto wanavyo baguliwa kwa kutishia kuondoa hadhi yao ya kuwa taasisi zisizo za kiserikali.

Mamlaka za Tanzania zifanye nini?

Serikali ya Tanzania haina budi kusitisha mara moja marufuku iliyowekwa kwa wasichana wajawazito na walioolewa au wamama watoto kurudi katika shule za umma. Inapaswa kufuata utekelezaji wa haki za binadamu wa sera ya “muendelezo” ambayo itaruhusu wasichana wajawazito kubaki shule kwa muda wanaotaka, na kutekeleza hatua za kuhakikisha wasichana wanabaki shule na kufanikiwa katika masomo yao. Rais Magufuli hana budi kufuta kauli zake za kichochezi dhidi ya elimu kwa wasichana wajawazito na kuiagiza serikali yake kuunga mkono wasichana wote kwenda shule.

Serikali pia inapaswa kuchukua mara moja hatua za kumaliza ukatili wa kijinsia ulioenea dhidi ya wasichana wa shule, kupitisha marufuku ya moja kwa moja dhidi ya adhabu za viboko mashuleni, kuhakikisha wanamaliza ndoa za utotoni kwa kubadili Sheria ya Tanzania ya Ndoa kwa kuongeza umri wa kuolewa kufikia miaka 18. Serikali pia inapaswa kuwawezesha vijana na taarifa sahihi na za kujitosheleza za elimu ya afya ya uzazi pamoja na huduma ili waweze kufanya maamuzi sahihi kuhusu ngono.

Benki ya Dunia ifanye nini?

Human Rights Watch inaelewa umuhimu wa kupanua ubora wa elimu ya sekondari nchini Tanzania, lakini inaamini kwa dhati jambo hili halipaswi kufanywa kwa kutozingatia maisha ya baadaye ya watoto wa kike. Haki ya watoto wa kike kupata elimu sio kitu cha kupuuzwa.

Serikali zote hazina budi kuchukua hatua kuhakikisha kwamba elimu ya sekondari inapatikana na kufikiwa na wote bure na kufanya elimu hadi sekondari ngazi ya chini (O-Level) kuwa lazima.

Benki ya Dunia inapaswa kuhakikisha kwamba wasichana wajawazito na wamama watoto wanapata elimu ya umma kwa ngazi ya shule za msingi na sekondari bila vikwazo au kulazimishwa kuchagua mfumo mbadala wa elimu, wakati huo huo wakihakikisha wamama watoto- ambao wanakuwa nje ya mfumo wa shule kwa kipindi kirefu kutokana na marufuku ya serikali- wanaweza kufikia na kupata AEP ili waweze kumaliza elimu ya msingi. Mkopo wa SEQUIP inabidi uruhusu machaguo yote, na kuhakikisha elimu bora inapatikana katika mifumo yote, wakati huo huo kuhakikisha azma ya mifumo yote kuwa bure.

Benki ya Dunia isitoe awamu ya kwanza ya mkopo, ambao umepangwa kutoka 2021, mpaka pale serikali itakapo heshimu wajibu wake wa kuhakikisha upatikanaji sawa wa elimu bure kwa elimu ya lazima ya msingi na elimu ya sekondari ngazi ya chini kwa wasichana. Mahitaji ya chini ni pamoja na kupitishwa notisi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia itakayo toa taarifa ya mwisho wa marufuku ya shule na kuwaagiza maafisa wa shule kuwasahili wasichana wajawazito na wamama vijana.  

Kama shemeu ya SEQUIP, Benki ya Dunia na washirika wengine wa maendeleo hawana budi kushirikiana na serikali ya Tanzania kuunda sera ya “muendelezo” ili kuhakikisha wanafunzi wajawazito na wamama vijana wanasaidiwa kubaki shule na kumaliza elimu ya sekondari. SEQUIP pia inapaswa kuweka kipaumbele utoaji wa elimu iliyojitosheleza ya afya ya uzazi kuhakikisha wanafunzi wote wanaweza kupata taarifa zinazojitosheleza, zinazoendana na viwango vya kimataifa vya haki za binadamu.

Your tax deductible gift can help stop human rights violations and save lives around the world.

Region / Country