(Washington, DC) – Benki ya Dunia imeidhinisha mkopo wa elimu wa kiasi cha $500 milioni dola za kimarekani kwa Tanzania bila kuitaka serikali kuachana na sera yake ya kuwafukuza shule wasichana wajawazito, Human Rights Watch imesema leo. Tarehe 31 Machi 2020, Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya Dunia ilipiga kura kutoa mkopo ili kusaidia programu ya shule ya sekondari ya Tanzania
Rais wa Tanzania John Magufuli amekuwa mstari wa mbele kuunga mkono marufuku ya watoto wa kike shuleni na akaapa kuitekeleza katika kipindi chake chote cha uongozi. Mara kwa mara shule za Tanzania huwalazimisha wanafunzi wa kike kuwapima ujauzito na kuwafukuza moja kwa moja wale wanaopatikana kuwa wajawazito. Mamlaka pia zimewakamata baadhi ya wanafunzi wasichana kwa kuwa wajawazito. Takribani wanafunzi wajawazito 5,500 huacha kwenda shule kila mwaka, hata hivyo makisio ya nyuma yalionyesha kwamba takribani wanafunzi 8,000 wamelazimishwa kuacha shule kila mwaka.
“Benki ya Dunia inapaswa kufanya kazi na serikali kusukuma mifumo ya elimu kuwajumuisha wanafunzi wa jinsia zote na kuwaweka wanafunzi wote katika shule za umma, ikiwa ni pamoja na wale wajawazito au wazazi,” alisema Elin Martinez, mtafiti mwandamizi wa haki za watoto wa Human Rights Watch. “Badala yake, Benki ya Dunia imeshindwa kutumia ushawishi wake na kukubaliana na katazo na vitendo vingine vya kibaguzi vya Tanzania, na kupuuza ahadi yake ya kutokufanya vitendo vya kibaguzi.”
Mkopo wa Benki ya Dunia unajumuisha fedha kwa ajili ya kujenga mfumo wa “njia mbadala za elimu (alternative education pathways),” mfumo wa kulipia karo ulio sanjari na elimu ya kawaida na ulio na vituo vya elimu visivyo rasmi kwa watoto walioacha shule katika mfumo wa elimu rasmi, ambao ndio msingi mkuu wa Programu ya Kuboresha Elimu ya Sekondari ya Tanzania (SEQUIP). Programu hii ilianzishwa kufuatia hatua ya Benki ya Dunia kuzuia mkopo wa dola za kimarekani $300 milioni wa elimu ya sekondari nchini Tanzania kwa sehemu kwasababu ya ubaguzi wa serikali kwa wanafunzi wa kike wajawazito.
Chini ya SEQUIP, kusoma katika vituo hivi mbadala ndio chaguo pekee kwa wasichana waliofukuzwa shule kwa kuwa wajawazito. Lakini njia hizi za elimu mbadala haziwezi kuwekwa kama zinatoa elimu iliyo sawa na ile inayotolewa na elimu ya daraja la chini la shule za sekondari za umma. Vituo hivi havitakuwa vya bure, vitatoza ada, na vitatoa elimu ya mtaala uliofupishwa.
Katika kuidhinishwa kwake mkopo, Benki ya Dunia ilizingatia tu kwamba wasichana waopata ujauzito au kuwa na mtoto “wanaacha” tu shule wenyewe. Katika kuliweka swala hili katika mtindo huu, Benki ya Dunia ilipuuza ushahidi huru unaoonesha kwamba wasichana wanafukuzwa, wanadhalilishwa na maofisa wa shule na waalimu pale wanapolazimishwa kupimwa ujauzito au wanapogundulika kuwa wajawazito, na matokeo yake kukataliwa na wanafunzi wenzao.
Benki ya Dunia haikushughulikia/haikujibu wasiwasi uliopo juu ya marufuku wakati inaidhinisha mkopo, imesema Human Rights Watch. Serikali ya Tanzania haijaweka sera au amri inayoweka wazi haki ya wasichana kubaki shuleni pale wanapokuwa wajawazito au baada ya kujifungua au kutoa hakikisho kwamba itairudisha sera ya “kuwarejesha shuleni” wasichana wajawazito iliyofutwa na Bunge mnamo mwaka 2017.
Serikali zote zinapaswa kuchukua hatua za mara moja kuhakikisha kwamba elimu ya sekondari inapatikana na inatolewa bila malipo na kufanya elimu kuwa ya lazima hadi mwisho wa kidato cha nne, imesema Human Rights Watch.
Benki ya Dunia isitoe kiasi cha kwanza cha fedha za mkopo hadi pale serikali itakapo heshimu wajibu wake wa kuhakikisha upatikanaji wa bure na wa usawa wa elimu ya sekondari hadi kidato cha nne kwa wasichana. Serikali iachane mara moja na marufuku ya kibaguzi na kuanzisha amri ya kiwizara inayozitaka shule zote kuacha mara moja upimaji wa ujauzito na kuacha kuwafukuza wasichana wajawazito.
Tanzania ni moja ya nchi mbili barani Afrika ambazo zinawazuia waziwazi wasichana wajawazito au kina mama watoto kuhudhuria shule za umma. Miaka ya hivi karibuni, serikali nyingi za Afrika zimejiwekea ahadi ya uhakika ya kuhakikisha kwamba wasichana wajawazito na kina mama watoto wanahudhuria shule. Utafiti wa Human Rights Watch umegundua kwamba sheria, sera, na miongozo zinazolinda haki ya wasichana wajawazito na wakina mama watoto kupata elimu ni muhimu katika kuhakikisha kwamba wasichana hawabaguliwi shuleni.
Serikali zote za Afrika zinapaswa kuwa na sera zinazojali haki za binadamu za “muendelezo” ambazo zimewekwa nchi nzima, zikiweka wazi haki za wasichana ili kwamba shule na watumishi wa wizara wawe wana muongozo wa wazi juu ya kuwasaidia na kuwatunza ipasavyo wakina mama watoto shuleni, imesema Human Rights Watch.
Kurudi nyuma kwa Benki ya Dunia juu ya haki ya elimu ya wasichana wajawazito inaibua wasiwasi pia juu ya ahadi pana ya benki hiyo ya kutekeleza Mradi wa Mazingira na Jamii, ambao unaahidi kwamba mikopo ya benki haitatumika katika kuendeleza ubaguzi. Makundi mengine ambayo hubaguliwa na serikali nchini Tanzania ikiwa ni pamoja na watu wanaovutiwa kimapenzi na watu wenye jinsia kama zao (LGBT), yanaweza kuwa katika hatari zaidi ikiwa serikali itaona dalili za benki kutozingatia misingi yake ya kupiga vita ubaguzi.
“Kinyume na namna Benki ya Dunia inavyoonyesha mkopo wa Tanzania, “elimu mbadala” kamwe haiwezi kufanana na kile watoto wanachokipata katika elimu rasmi na ya lazima,” amesema Martinez. “Tofauti na watoto wengine wasiokuwa shuleni ambao wana uchaguzi wa kurudi shuleni, wasichana wajawazito hukataliwa kiholela haki ya kurudi shuleni na kulazimishwa kufuata mfumo mbadala.”