(Nairobi, Oktoba 17, 2017) – Madaktari, wataalamu wa matibabu na vyama vya kitaifa vya matibabu hawana budi kutii maazimio ya Shirika la Matibabu la Kimataifa ya Oktoba 2017 juu ya kusitisha uchunguzi wa lazima wa njia ya haja kubwa, kwa watu wanaoshutumiwa kujihusisha na vitendo vya kushiriki mapenzi ya jinsia moja, Human Rights Watch wamesema haya hii leo. Mkutano Mkuu wa Shirika la Matibabu Kimataifa (WMA), taasisi ya kimataifa yenye jumla ya vyama vya kitaifa vya matibabu kutoka nchi 111 imelaani upimaji wa lazima wa njia ya haja kubwa kutafuta ushahidi wa mienendo ya uhusiano wa jinsia moja.
Vipimo vya lazima vya njia ya haja kubwa, kulingana na sayansi iliyokosa mashiko ya karne ya 19 mara nyingi inahusisha madaktari au wauguzi kuingiza kwa lazima vidole na wakati mwingine vifaa vingine katika njia ya haja kubwa kujaribu kung’amua kama mtu huyo ameshiriki mapenzi ya jinsia moja. Vipimo hivyo hutumika kama “ushahidi” katika mashtaka ya vitendo vya mapenzi ya jinsia moja kwa hiari katika baadhi ya nchi, vinakosa misingi ya kisayansi, vinakiuka maadili ya uuguzi na ni vitendo vya kinyama, vyenye kudhalilisha na visivyokuwa vya kibinadamu ambavyo vinapelekea mateso.
“Hakuna uamuzi katika hili. Hakuna sababu za msingi kwa serikali kuendelea kufanya vipimo vya lazima vya njia ya haja kubwa kwa watu wanaotuhumiwa kujihusisha na ushoga,” anasema Neela Ghoshal, mtafiti mwandamizi wa Human Rights Watch juu ya masuala ya haki za wasagaji, mashoga, wanaovutiwa na jinsia mbili na waliobadilisha jinsia (LGBT). “Shirika la Matibabu Kimataifa kimepaza sauti kuonyesha makubaliano ya pamoja kwamba vipimo vya lazima vya njia ya haja kubwa ni kinyume cha maadili, kinyume cha sayansi na hakina misingi yoyote.”
Maazimio ya Shirika la Matibabu Kimataifa yanawataka madaktari kusitisha uchukuaji wa vipimo hivi. Maazimio hayo yanahimiza vyama vya matibabu kitaifa kutoa tamko la maandishi kuwakataza wanachama wao kujihusisha na vipimo hivyo na kutoa elimu kwa madaktari na watumishi wa afya kuhusu “ukosefu wa ushahidi wa kisayansi na ubatili ya vipimo hivyo na ukweli kwamba ni aina ya mateso, vitendo vya kinyama na visivyo vya kibinadamu na vyenye kudhalilisha.” Pia inatoa rai kwa Shirika la Afya Duniani kutoa tamko rasmi kupinga vipimo vya lazima vya njia ya haja kubwa kwa kukosa vigezo vya kisayansi na kukiuka maadili ya uuguzi, tamko hili litakuwa ni muendelezo wa hatua za kupiga vita vitendo hivyo.
Maazimio haya yalipendekezwa na Shirika laMatibabu cha Afrika Kusini kwa kushirikiana na Human Rights Watch, yametathminiwa kwa kipindi cha mwaka mmoja na kupokea mrejesho na kuruhusu wanachama wote kutoa mapendekezo kabla ya kupitishwa. Mapendekezo yalipitishwa kwa makubaliano ya pamoja isipokuwa kwa wanachama wawili ambao hawakuhudhuria kikao.
Katika Mkutano Mkuu, chama pia kilipitisha marekebisho ya “Kiapo cha Madaktari,” ambacho kinawataka madaktari kujiepusha na ubaguzi unaotokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na mwelekeo wa kijinsia.
Nchi kadhaa ambazo bado hazijaondoa utaratibu wa kufanya vipimo vya lazima vya njia ya haja kubwa hivi karibuni zimeendelea kupiga hatua kuelekea kusitisha vipimo hivyo, walisema Human Rights Watch. Serikali za Lebanon na Tunisia zimechukua hatua kuzuia vipimo hivyo. Hivi karibuni Tunisia imekubali mapendekezo ya kusitisha vipimo hivyo wakati wa Tathmini ya Jumla ya Baraza la Haki la Umoja wa Mataifa, ijapokuwa utekelezaji wa zuio hilo kwa Tunisia unabaki mikononi mwao wenyewe. Katika hatua zote, vyama vya matibabu kitaifa vimefanikisha jukumu muhimu la kubadili mtizamo wa serikali zao. Mwezi Septemba, Chama cha Matibabu Kenya kimekuwa moja ya vyama vya matibabu hivi karibuni kukemea matumizi ya vipimo vya lazima vya njia ya haja kubwa, ijapokuwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imejaribu kutetea matumizi yake.
Nchi nyingine bado ziko nyuma. Huko Misri, wanaume na wanawake waliobadili jinsia waliokamatwa na makosa ya “kukiuka maadili” huingizwa katika utaratibu kupitia Mamlaka ya Uchunguzi wa Madawa, tawi la Wizara ya Sheria kwa ajili ya vipimo vya lazima vya njia ya haja kubwa na matokeo hutumika kortini kuwafunga watu kwa minajili ya mwelekeo wao wa kijinsia. Tangu mwishoni mwa Septemba, kwa mujibu wa wapigania haki za binadamu huko Misri, angalau Wamisri watano wamejikuta wakifanyiwa vipimo vya namna hii ikiwa ni sehemu ya kutafuta wakosaji baada ya vijana kadhaa kupeperusha bendera yenye rangi za upinde wa mvua (ambayo hutumika kama alama ya LGBT) katika tamasha.
Nchini Tanzania mwishoni mwa 2016, polisi waliamua kufanya uchunguzi wa lazima wa njia ya haja kubwa kutafuta “ushahidi” wa vitendo vya kishoga kwa mara ya kwanza, kwa kiasi ambacho Human Rights Watch wameweza kung’amua, ikiwa ni sehemu ya kampeni kubwa dhidi ya LGBT na wengine wanaowaunga mkono. Sio Chama cha Matibabu cha Misri wala Tanzania ambao wote ni wanachama wa WMA ambao wamejitokeza na kupinga vitendo hivi kwa wazi.
Nchi nyingine ambazo Human Rights Watch wameweka kumbukumbu ya matumizi ya vipimo vya lazima vya njia ya haja kubwa kati ya 2010 na 2015 ni pamoja na Cameroon, Turkmenistan, Uganda na Zambia. Human Rights Watch pia imepokea ripoti za mamlaka za serikali kutoa maagizo ya vipimo vya namna hiyo kufanyiwa watu wanaotuhumiwa kujihusisha na ushoga huko Syria na Umoja wa Falme za Kiarabu lakini haijaweza kuthibitisha madai haya kwa uhuru.
“Madaktari wanajukumu muhimu la kusimamia viwango vya maadili na mara nyingi wao huwa ndio dira ya maadili ya jamii,” anasema Ghoshal. “Nchini Misri, Tanzania na nchi nyingine zote ambapo watu hulazimishwa kufanya uchunguzi wa lazima wa njia ya haja kubwa madaktari hawana budi kuongoza vita dhidi ya unyanyasaji huu wa kikatili.