‘’Adam’’ [jina bandia] aliyekamatwa na kushtakiwa kutokana na uvumi kwa ‘’hatia ya kushiriki vitendo vinavyokwenda kinyume na maumbile’’ akipekua hati za polisi.

Suala Nyeti ni Vurugu

Mashambulizi dhidi ya Wana LGBT katika Pwani ya Kenya

‘’Adam’’ [jina bandia] aliyekamatwa na kushtakiwa kutokana na uvumi kwa ‘’hatia ya kushiriki vitendo vinavyokwenda kinyume na maumbile’’ akipekua hati za polisi.   © 2015 Zoe Flood

I: Muhtasari

[1]

"Kuwa msagaji au shoga si hoja. Kuumizwa kwa sababu ya utambulisho wetu ni suala kubwa."

-Lorna Dias, Mratibu Mkuu wa Gay and Lesbian Coalition of Kenya, Nairobi,Julai 2015

Mnamo Februari 18, 2015, wanaume wawili katika kaunti ya Kwale iliyo katika pwani ya Kenya, walitiwa mbaroni na polisi, na kushtakiwa kwa "hatia zisizoambatana na maumbile" na ulanguzi wa "matini machafu." Wakazi wa eneo hilo walikuwa wamewashinikiza polisi kuwakamata kufuatia kuchapishwa kwa picha kwenye mitandao ya kijamii zilizowaonyesha wanaume kutoka jamii hiyo wakifanya ngono. Polisi walitishia kuwahujumu wanaume hao wawili ili kuwashurutisha kukiri mashtaka, na madaktari wakawafanyia uchunguzi wa lazima kwenye mikundu yao kwa lengo la kuthibitisha kama walikuwa wameshiriki ngono na wanaume wenzao. Kesi dhidi yao ilikuwa ikiendelea wakati wa kuiandika ripoti hii.

Kufuatia malalamiko makali kutoka kwa umma kuhusu madai ya mapenzi ya jinsia moja na picha za baadhi ya wahusika wakiwa wanashiriki ngono, wanaume kadhaa wanaofanya mapenzi na wanaume wenzao, pamoja na wanawake waliobadilisha jinsia zao, walihofia hujuma na kutoroka makazi yao. Wakazi wa Kwale katika miji ya Ukunda na Diani waliwashambulia wanaume wawili au zaidi waliotuhumiwa kufanya mapenzi na wanaume wenzao, ambao hawakuweza kutafuta msaada wa polisi kwa sababu waliogopa hatua hiyo ingewaweka katika hatari ya kukamatwa.

Tukio hilo la Kwale ni moja ya kesi chache tu zinazojulikana ambapo waendesha mashtaka wa Kenya humshtaki mtu yeyote kwa kushiriki mapenzi ya jinsia moja kwa hiari. Ingawa kesi hii inaonekana kama si jambo la kawaida katika mkondo wa mahakama, ni ishara ya jinsi ubaguzi, hujuma, na mateso yametawala maisha ya Wakenya wenye ujinsia usiolingamana au wanaoonekana kuwa wanahusika katika mapenzi ya jinsia moja.
Ripoti hii inaangazia ukiukaji wa haki za wana LGBT (lesbian, gay, bisexual and transgender – wasagaji, mashoga, watu wanaovutiwa kimapenzi kwa jinsia zote mbili, na watu ambao wamebadilisha ama wanatamani kubadilisha jinsia zao) katika mkoa wa pwani, ikiwa ni pamoja na hujuma, uchochezi wa hujuma na kutopewa ulinzi wa kutosha, na inabainisha jinsi serikali ya Kenya inaweza kuushughulikia ukiukaji huu kwa njia bora zaidi na kutekeleza wajibu wake wa kuwalinda Wakenya wote. Ripoti imejikita katika utafiti uliofanywa na shirika la Human Rights Watch kati ya Januari 2014 na Agosti 2015, kwa ushirikiano na wanachama wa shirika la Persons Marginalized and Aggrieved (PEMA Kenya), ambalo ni shirika la kijamii lenye makao yake jijini Mombasa na hutoa msaada katika maswala ya haki za kibinadamu, afya, VVU / UKIMWI, na kiuchumi na ustawi kwa walio wachache kijinsia na kimapenzi. Human Rights Watch liliwahoji wana LGBT 65 wakiwa miongoni mwao wanaume mashoga, wanaume wanaovutiwa kimapenzi na jinsia zote mbili, wanawake wanaofanya mapenzi na wanawake, na wanawake waliobadilisha jinsia zao, pamoja na zaidi ya watu wengine 20, wakiwa miongoni mwao viongozi wa kidini, viongozi wa serikali ya kaunti, maafisa wa polisi, mawakili, wahudumu wa afya na wanaharakati wa jamii.

Huku ripoti hii ikilenga kwa kiasi kikubwa kuiangazia hali inayowakabili wana LGBT katika eneo la pwani, ambalo limekuwa eneo la milipuko ya mara kwa mara ya ghasia dhidi ya wana LGBT, pia inatathmini mienendo katika ngazi ya kitaifa ambayo imeathiri au ina uwezo wa kuathiri maisha ya wana LGBT nchini kote.

Sehemu ya 162 katika Sheria ya Adhabu ya Kenya, ambayo sheria yenyewe ni moja ya masalio ya enzi za Ukoloni, inaharamisha "mapenzi kinyume na maumbile" (“carnal knowledge against the order of nature”), kipengee kinachoeleweka kuashiria kijumla ngono kati ya wanaume. Vyombo vya serikali vimeyanyima baadhi ya mashirika yanayowawakilisha Wakenya LGBT haki ya kujiandikisha ili kutekeleza shughuli zao kisheria, kwa misingi kuwa mashirika hayo yanaendeleza tabia haramu, ingawa ushindi kwenye mahakama wa hivi karibuni umeilazimisha serikali kuyasajili mawili baadhi ya mashirika haya. Wanasiasa na viongozi wa kidini wenye misimamo mikali wanataka kuimarisha nafasi zao katika jamii kwa kupendekeza sheria na kuhubiri chuki dhidi ya Wakenya wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja. Vyombo vya habari hushiriki katika utoaji wa taarifa za kusisimua kuhusu "kashfa," ambazo wakati mwingine huwa za kubuni kabisa, zinazowashirikisha wana LGBT. Ingawa wana LGBT wengi huungwa mkono na marafiki pamoja na jamaa na kujitengea mahali ambapo wanaweza kuishi kwa usalama kiasi, hatari ya hujuma dhidi yao bado ipo.
Katika matukio yasiyopungua sita kati ya mwaka 2008 na 2015, makundi ya wana LGBT katika kaunti za pwani kama vile Kilifi, Kwale, na Mombasa wametishiwa kushambuliwa na wakati mwengine hata wameshambuliwa na magenge. Matamshi yanayowashutumu wana LGBT, aghalabu kutoka kwa viongozi wa kidini, yameenea hasa katika pwani, na huathiri mtizamo wa umma kuhusu wana LGBT.

Msimamo wa polisi nao unakanganya. Katika baadhi ya matukio, wamewalinda wana LGBT dhidi ya hujuma kutoka kwa magenge – jukumu linalotambuliwa na kupata shukurani kutoka kwa wanaharakati wa LGBT katika pwani – lakini hawajawachukulia hatua yoyote ya kisheria waliozua ghasia hizo. Katika matukio mengine, wameshindwa waziwazi katika wajibu wao wa kutoa ulinzi: wakiwanyima msaada waathiriwa kutokana na jinsi watu wanavyodhani utambulisho wao wa kijinsia au hisia ya kimapenzi, wakiwakamata kiholela, au hata kuwahujumu wenyewe.

Kuharamishwa kwa mapenzi kati ya watu wa jinsia moja kunawafanya wana LGBT kuwa katika hatari ya kushambuliwa mikononi mwa wananchi wa kawaida na maafisa wa kutekeleza sheria. Wale ambao hushiriki katika biashara ya ngono wamo hata katika hatari zaidi: wanakumbana na ubakaji na unyanyasaji mwingine mikononi mwa wateja, polisi, na maafisa wa kutekeleza sheria za serikali za kaunti. Waathiriwa wengi wa unyanyasaji ambao ni wana LGBT wanaamini kuwa hawana njia ya kupata haki, na kwamba kuna uwezekano mkubwa wa polisi kuwatesa sawia na kuwalinda. Wana LGBT walituambia kwamba baada ya kesi ya Kwale ambayo muhtasari wake umetolewa hapo juu – ambapo wanaume wanaofanya mapenzi na wanaume na wanawake waliobadilisha jinsia zao na ambao wamo katika hatari ya kushambuliwa walihisi kuwa hawawezi kutafuta msaada kutoka kwa polisi baada ya polisi kuwakamata kiholela kuchu wengine wawili – imetokomeza zaidi matumaini kidogo ambayo Wakenya walio wana LGBT katika Pwani wanayo kwa serikali ya Kenya.

Uharamishaji, ubaguzi, na hujuma pia huzuia upatikanaji wa huduma za kuzuia maambukizi ya VVU na matibabu. Wanaume wanaofanya mapenzi na wanaume (men who have sex with men, MSM) wana uwezekano mkubwa zaidi wa kuambukizwa VVU kuliko watu wengine nchini Kenya na wametambuliwa na mashirika ya afya kama kundi maalum katika kulishughulikia janga la UKIMWI. Mombasa, jiji kubwa katika Pwani, pia lina viwango vya juu vya maambukizi ya VVU kuliko kiwango cha jumla nchini Kenya. Mafanikio katika kushughulikia VVU jijini Mombasa, ambalo lina idadi kubwa ya wahamiaji, ni muhimu katika kushughulikia suala la VVU katika kiwango cha kitaifa.

Lakini huduma za VVU kwa MSM katika eneo la Mombasa zinakabiliwa na vitisho. Makundi yanayoongozwa na chuki dhidi ya mapenzi ya jinsia moja yalizishambulia au yalitishia kuzishambulia kliniki na warsha za VVU kwa MSM katika Pwani mnamo mwaka wa 2008, 2010, na 2012. Mapendekezo ya Februari 2014 ya kukaza sheria dhidi ya mapenzi ya jinsia moja yalichochea hofu ya mashambulizi, na hivyo kusababisha kupungua kwa idadi ya watu wanaoendea huduma za VVU na kusababisha wahudumu wa afya kufunga kwa muda kliniki chache zilizokuwa zikitoa huduma za VVU kwa MSM. Wakati wa misako ya Februari 2015 dhidi ya mashoga kule Kwale, MSM kadhaa waliokuwa na VVU hawakuweza kutoka nyumbani kwao kwa siku nyingi. Ilibidi marafiki zao wawachukulie dawa zao za kupunguza makali ya VVU na kuwapelekea hadi nyumbani – ishara ya umoja unaostahili kushangiliwa katika jamii, lakini si mbinu inayoweza kudumu kuhakikisha haki ya kupata huduma bora za afya.

Katiba mpya na endelevu ya Kenya, iliyotangazwa rasmi mwaka wa 2010, inawahakikishia Wakenya wote haki ya faragha, usawa, heshima, na kutobaguliwa. Inatangaza orodha ya maadili ya kitaifa ambayo ni pamoja na "haki za kibinadamu, kutobaguliwa, na ulinzi wa makundi yaliyotengwa." Zaidi ya hayo, katiba inashirikisha katika sheria za Kenya sheria ya kimataifa – ikiwa ni pamoja na mikataba ya kimataifa iliyoidhinishwa na Kenya ambayo inazuia ubaguzi kwa misingi ya hisia ya kimapenzi. Masharti haya yanaipa serikali ya Kenya fursa ya kufutilia mbali sheria na tabia zinazobagua kwa misingi ya utambulisho wa kijinsia na hisia ya kimapenzi.


Kwenye Mfumo wa Kimataifa wa Mapitio ya Haki za Binadamu (Universal Periodic Review – UPR) katika Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa mwezi Januari mwaka 2015, Kenya ilikataa pendekezo la kuhalalisha mapenzi ya jinsia moja kati ya watu wazima kwa hiari, lakini ilikubalika pendekezo la "kupitisha sheria kamilifu dhidi ya ubaguzi hivyo kutoa ulinzi kwa watu wote, bila kujali hisia yao ya kimapenzi au utambulisho wa kijinsia." Wanaharakati wa Kenya wanaishinikiza serikali kutekeleza ahadi hii na pia kuhalalisha mapenzi ya jinsia moja.


Mbinu ya Kenya ya kuishughulikia hatari wazi ya mashambulizi inayowakumba wana LGBT na kutotengemaa inafaa kuongozwa na azimio la kihistoria lililopitishwa na Tume ya Afrika kuhusu Haki za Kibinadamu na Haki za Watu ya mwaka 2013, ambalo lilitoa wito kwa nchi wanachama wa "kukomesha vitendo vyote vya ukatili na unyanyasaji, iwe kutoka serikalini au kutoka kwa watu wasiokuwa serikalini" dhidi ya watu kwa misingi ya kweli au kukisiwa kuwa na hisia ya kimapenzi au utambulisho wa kijinsia.

Azimio la Tume ya Afrika hasa linataka mataifa:

 • kutunga na kutekeleza sheria mwafaka za kuzuia na kuadhibu aina zote za ukatili ikiwa ni pamoja na ule unaowalenga watu kwa misingi ya kukisiwa au ya kweli ya hisia yao ya kimapenzi au utambulisho wa kijinsia,
 • kuhakikisha uchunguzi sahihi na kuwashtaki ipasavyo wakosaji, na
 • kuanzisha taratibu za mahakama zinazowiana na mahitaji ya waathiriwa.
 • Kenya, kama nchi mwanachama, inahitajika kutekeleza azimio hili kwa kuchukua hatua ya kuzuia unyanyasaji dhidi ya wana LGBT, kutoa ulinzi unaotakikana, na kuwafungulia mashtaka wanaoendeleza unyanyasaji huo.

Ili kufanya hivyo, serikali ya Kenya katika ngazi ya kitaifa na hasa katika Kaunti za Mombasa, Kwale, na Kilifi inapaswa kutangaza hadharani msimamo wake kamili kwa maafisa wa kutekeleza sheria sawia na wananchi wa kawaida kuwa Wakenya wote, bila kujali utambulisho wao wa kijinsia au hisia za kimapenzi, wanastahili heshima sawa, ulinzi, na utambuzi wa haki zao.

Maafisa wa kutekeleza sheria wanapaswa kukomesha aina zote za unyanyasaji na ubaguzi dhidi ya wana LGBT (ikiwa ni pamoja na kusitisha mashtaka dhidi ya wanaume waliokamatwa Kwale), na wanatakiwa kuhakikisha kuwa wana LGBT wako huru kuwasilisha malalamiko yao dhidi ya maafisa wote wa kutekeleza sheria na wananchi wa kawaida bila hofu ya kulipiziwa kisasi. Bunge la Kenya na mabunge ya kaunti lazima yatupitilie mbali sheria ambazo zinaendeleza ubaguzi kwa misingi ya hisia ya kimapenzi, utambulisho wa kijinsia, au hadhi ya mfanyabiashara wa ngono. Wanapaswa kupitisha sheria kamilifu dhidi ya ubaguzi ambazo zinawalinda vilivyo watu wa hisia zote za kimapenzi na utambulisho wa kijinsia. Ni wajibu wa serikali ya Kenya kuhakikisha usalama wa raia wote, ikiwa ni pamoja na kushughulikia kwa njia bora zaidi hujuma na ukosefu wa usalama dhidi ya wasagaji, mashoga, wanaovutiwa kimapenzi na jinsia zote mbili, na waliobadilisha jinsia zao.

II: Mapendekezo Muhimu

Kwa Rais na Naibu Rais wa Jamhuri ya Kenya na Magavana wa Kaunti za Mombasa, Kilifi, na Kwale

 • Washutumu hadharani mashambulizi yoyote yatokanayo na chuki dhidi ya wale wanaoshiriki katika mapenzi ya jinsia moja ama wale wanaobadilisha jinsia zao yanayotokea nchini Kenya au katika kaunti zao, ikiwa ni pamoja na mashambulizi dhidi ya watu binafsi na mashirika.
 • Wajiiepushe na kutoa matamshi yoyote hadharani yanayowadhalilisha wanawake wana LGBT.

Kwa Serikali ya Kaunti za Mombasa, Kilifi, na Kwale

 • Tathmini sheria zote ndogo za kaunti ili kuhakikisha kuwa zinawiana na hakikisho la kikatiba la faragha, kutobaguliwa, na ulinzi sawa wa kisheria.

Kwa Bunge la Kenya

 • Lipitishe sheria kamilifu kuhusu ubaguzi ambayo inaukataza kwa misingi ya utambulisho wa kijinsia na hisia ya kimapenzi na inayohusisha hatua madhubuti ya kutambua na kushughulikia ubaguzi kama huo.
 • Kutupilia mbali vifungu 162, 163, na 165 vya Sheria ya Adhabu ya Kenya, ambavyo vinaharamisha mapenzi ya jinsia moja kati ya watu wazima waliokubaliana.
   

Kwa Tume ya Kitaifa ya Huduma za Polisi

 • Kuwatambua hadharani na kuwapongeza maafisa wa polisi ambao wanajitahidi kuwalinda wana LGBT dhidi ya mashambulizi, ili kuimarisha ujumbe kwamba polisi wanapaswa kutekeleza wajibu wao wa kuwalinda watu wote ndani ya Kenya.
 • Kuwakataza maafisa wa polisi kuagiza, kushiriki katika, au kufanya uchunguzi wa mikundu ya wanaotuhumiwa kushiriki katika mapenzi ya jinsia moja.
 • Kuchukua hatua zote zinazofaa ili kuhakikisha kwamba maafisa wote wa polisi wanaziheshimu haki ya kutobaguliwa, usawa, na faragha, na hawabagui katika utekelezaji wa majukumu yao.

Kwa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma

 • Kusitisha mashtaka dhidi ya watu wawili katika kaunti ya Kwale walioshtakiwa kwa tuhuma ya kushiriki katika mapenzi ya jinsia moja.

III: Ukosefu wa Ulinzi: Mashambulizi ya Magenge na Mashambulizi kutoka kwa Watu Binafsi katika Pwani


Serikali ya Kenya ina jukumu la kuchukua hatua zote muhimu ili kuwahakikishia usalama raia wake wote na watu wengine ndani ya mipaka yake. Lakini serikali ya Kenya haijitahidi vilivyo ili kuzuia na kuadhibu hujuma dhidi ya wana LGBT.

Katika Pwani, mfululizo wa mashambulizi yanayochochewa na chuki dhidi ya wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja na wale waliobadilisha jinsia zao hutokea kutokana na kauli za viongozi wa kidini wenye msimamo mkali. Hali hii imesababisha kuwepo kwa mawimbi ya kichinichini ya ukosefu wa usalama. Katika matukio yasiyopungua sita kati ya mwaka 2008 na 2015, magenge yamewashambulia au kutishia kuwashambulia wana LGBT au wahudumu wa afya wanaowahudumia wana LGBT. Maafisa wachache wa serikali wameyalaani mashambulizi, nao polisi – wakati mwingine wamewalinda waathiriwa kutokana na tishio la kushambuliwa – ila hawajamkamata mtu yeyote kwa kushiriki katika au kuchochea mashambulizi haya.

Wana LGBT pia wanahujumiwa na watu binafsi, ikiwa ni pamoja na kushambuliwa na kubakwa. Waathiriwa wengi tuliowahoji walisema wao hawaripoti uhalifu kwa polisi, kwa kuamini kwamba polisi hawawezi kuwasaidia au, vibaya zaidi, wanaweza kuwakamata.

Mnamo Julai 2015, Rais Uhuru Kenyatta alirejelea haki za makuchu kama "suala lisilo muhimu" – juhudi za wazi za kukwepa mjadala mkali kuhusu masuala ya LGBT katika muktadha wa ziara ya Rais wa Marekani, Barack Obama.
[2] Ikiwa baadhi ya wanaharakati wa haki za wana LGBT walitiwa motisha kwa kauli hiyo, wakiitafsiri kama ahadi kwamba serikali haitajiingiza kwenye ajenda ya hujuma inayochochewa na chuki dhidi ya watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja, wengine waliona kuwa inaweza kufasiriwa kama hali ya kutojali ubaguzi na ghasia zinazoendelea kwa misingi ya utambulisho wa kijinsia au hisia ya kimapenzi.[3]

Mashambulizi ya Magenge na Hatua za Polisi Zisizowiana

Polisi katika Pwani, ambao wana wajibu wa kuzuia vurugu na kuwalinda waathiriwa, wanachukua hatua zisizowiana katika kukabiliana na mashambulizi ya magenge dhidi ya wana LGBT. Katika nne kati ya visa sita vinavyofuata, polisi walichukua hatua na kuwalinda wana LGBT (katika Likoni, Mtwapa, Mombasa, na Watamu), lakini hakuna hata kimoja kati ya visa hivyo sita ambapo waliwakamata waliotenda ghasia hizo. Katika kisa kimoja (Malindi), polisi hawakujuzwa. Katika kisa cha hivi karibuni (Kwale), polisi hawakuwajibika ipasavyo kwa kuitikia hamasa za umma na kuwasingizia watu wawili kisha kuwakamatwa bila sababu.

Katika tatu kati ya visa hivyo, hujuma au vitisho vya hujuma dhidi ya wana LGBT kutoka kwa wakazi na viongozi wa kidini uliwafanya watoa huduma za afya waliowahudumia wanachama wa MSM kusitisha warsha zao kwa muda au kabisa.

Kwale, Februari 2015: Mashambulizi na Kukamatwa Kufuatia Usambazaji wa Picha
Mnamo Februari 2015, mfululizo wa picha na video zinazowaonyesha wanaume wanaoshiriki ngono na wanaume wenzao zilisambazwa kwenye mitandao ya kijamii, na kusababisha hasira miongoni mwa umma na msako uliofanywa na makundi dhidi ya wanaume wanaofanya mapenzi na wanaume katika Diani na Ukunda, miji miwili jirani katika Kaunti ya Kwale. Badala ya kuchukua hatua za kuwahakikishia usalama wakazi wana LGBT, polisi walitekeleza ukiukaji mbaya wa haki za binadamu kwa kuwakamata kiholela watu wawili waliodaiwa kufanya mapenzi na wanaume wenzao na kuwafanyiza uchunguzi wa kudhalilisha kwenye mikundu; uchunguzi udhalilishaji ambao vilevile ulikuwa kinyume na sheria. Gavana wa kaunti alitoa kauli za kushutumu mapenzi ya jinsia moja na hivyo kuchochea woga miongoni mwa wana LGBT.

Chanzo cha picha na video, pamoja na mazingira ambamo zilichukuliwa, bado ni tata. Vyombo vya habari nchini Kenya vilitoa taarifa kwamba baadhi ya wale waliopigwa picha walikuwa watoto walio chini ya miaka 18, huku shirika moja la habari likidai kwamba "vitu hivyo vilijumuisha picha zaidi ya 800 za watoto waliodanganywa na kuingizwa katika ulanguzi wa ngono."[4] Human Rights Watch lilizungumza na watu wazima kadhaa ambao ni wanaume waliosema kuwa walipigwa picha hizo kwa hiari – ingawa mmoja alisema kuwa baadhi ya picha zilichukuliwa katika sherehe na hazikukusudiwa kusambazwa kwa umma – na kwa mujibu wa mwanamume mmoja, vijana kadhaa chini ya umri wa miaka 18 walishirikishwa pia na washiriki walilipwa na mpiga picha za ponografia kutoka Ulaya.[5]

Dhuluma katika biashara ya ngono inayowashirikisha watoto, ambayo ni pamoja na uzalishaji wa picha za ngono zinazowahusisha watoto, ni kosa la jinai chini ya sheria ya Kenya, na serikali ya Kenya ina wajibu chini ya sheria za kimataifa kuzuia vitendo kama hivyo.[6] Hata hivyo, katika kisa hiki, inaonekana kuwa uchapishaji wa picha hizi ulisababisha msako kwa sababu ya chuki sio dhidi ya wale waliohusika kuwadhulumu watoto, lakini dhidi ya kundi pana la wakazi wa Diani na Ukunda wanaoshukiwa kufanya mapenzi na wanaume wenzao au wale wanaotamani kubadilisha jinsia zao. Hadi sasa, hakuna yeyote amekamatwa kwa tuhuma za unyonyaji katika biashara ya ngono ya watoto.

Mapema Februari, Adam,[7] mkazi wa Diani aliye na umri wa miaka 30, alikuwa anatembea kuelekea nyumbani jioni wakati genge la watu ambao aliwatambua kama wakazi wa Diani walimshambulia. Adam aliliambia shirika la Human Rights Watch kuwa ingawa hakuonekana katika picha hizo, majirani zake walimtuhumu kushiriki katika mapenzi ya jinsia moja.


Walikuja kwangu wakinitishia na kusema 'Nyinyi washoga mnawaharibia wanaume heshima yao. Mnawezaji kulala na wanaume?' Mmoja wao alipiga hatua nyuma na kuchukua chupa iliyokuwa imetupwa hapo. Nilimwona ameivunja chini, na kisha kuiinua. Nilijaribu kurudi nyuma, lakini alinikata kwa chupa hiyo shingoni na kwenye mtulinga, [na kuacha damu] ikitiririka kifuani mwangu.

Adam alianguka chini na kupoteza ufahamu. Mwendeshaji wa pikipiki ambaye alishuhudia shambulizi hilo alikimbia na kumjulisha rafikiye Adam, ambaye alimpeleka hospitalini. Adam alisema, "Kama rafiki yangu hakuja haraka hivyo, mimi ningekufa." Alilazwa hospitalini kwa siku tatu na kidonda kushonwa. Alipotoka hospitalini, Adam aliwazia kupiga ripoti kwa polisi, lakini alihofia: "Ningeenda kuwaambia polisi ni kwa sababu gani nilishambuliwa?"[8]

Mnamo Februari 11, Tony, mwanamume anayefanya mapenzi na wanaume, alipigwa kichwani kwa chupa akiwa barabarani Ukunda. "Walikuwa wamenitambua," alisema Tony, akirejelea zile picha. Alienda hospitalini kwa matibabu kutokana na shambulizi hilo, na kisha akaenda mafichoni Nairobi. Alisema, "Mimi niliondoka tu, sikuweza hata kuthubutu kwenda kwa polisi au kufanya kitu chochote kwa sababu nilijua hawangenisaidia.[9]

Charles, mwanaharakati katika Ukunda, aliliambia Human Rights Watch kwamba viongozi wa kidini, wazee wa kijiji, na "wawakilishi wa usalama katika jamii" walifanya mikutano kadhaa ya kijamii yenye lengo la kujadili jinsi ya kukabiliana na wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja.[10] Kundi la wakazi lilianza kwenda nyumba hadi nyumba wakiwasaka watu waliodaiwa kushiriki katika mapenzi ya jinsia moja, bila kujali ikiwa walionekana katika picha hizo au la.[11]

Mnamo Februari 18, polisi, baada ya kupashwa habari na raia, waliwatia mbaroni watu wawili, Bryan na yule Adam–aliyetajwa hapo juu ambaye alikuwa amekatwa kwa chupa na ambaye alikuwa bado anayauguza majeraha hayo–na kuwapeleka katika Kituo cha Polisi cha Diani.[12] Polisi waliwashtaki kwa "hatia ya kushiriki vitendo vinavyokwenda kinyume na maumbile" licha ya kutokuwa na ushahidi wowote kwamba wanaume hao walikuwa wameshiriki katika mapenzi ya jinsia moja.[13] Pia polisi waliwashtaki wanaume hao wawili kwa kosa la kuwa na picha chafu kwa lengo la kuzisambaza, chini ya kifungu cha 181 cha Sheria ya Adhabu ya Kenya[14] – tena, licha ya kutokuwa na ushahidi kwamba wanaume hao wawili walikuwa na picha hizo au walikuwa wakisambaza picha zozote.[15] Polisi walifanya msako katika nyumba za wanaume hao wawili, bila kibali, na katika moja ya nyumba hizo, wakapata DVD ya kipindi cha televisheni katika Uingereza almaarufu, "Queer as Folk," ambacho kilishinda matuzo mengi iliyochukuliwa kama "ushahidi."[16]

Bryan aliliambia Human Rights Watch kuwa polisi walitishia kumpiga ikiwa wawili hao hawangekiri mashtaka dhidi yao, lakini alikataa kukiri, na badala yake akawasiliana na wakili.[17] Kwa mujibu wa Adam, polisi walimtaka atoe hongo ya shilingi za Kenya 100,000 (karibu Dola za Marekani 1,000) ili mashtaka dhidi yao yatupiliwe mbali. Alipokataa, walisema "Tunaenda tu kukutupa barabarani kule Ukunda ambapo umati wa watu utakupiga mawe hadi ufe. Tia saini hapa." Aliendelea kukana mashtaka.[18]

Polisi waliwapeleka wanaume hao katika Mahakama ya Wilaya ya Kwale, ambapo mwendesha mashtaka aliomba mahakama ruhusa ya kuwafanyia wanaume hao "uchunguzi wa kimatibabu." Hakimu, Christine Njagi, alikubali. Baadaye aliliambia Human Rights Watch kwamba hakumbuki kutoa agizo hilo, na hangeweza kusema kamili ni aina gani ya uchunguzi mahakama ilitarajia wanaume wale wafanyiwe.[19]

Wakiwa wamejihami kwa agizo la mahakama, polisi waliwasindikiza wanaume hao hadi Hospitali Kuu ya Pwani, hospitali ya umma ya pili kwa ukubwa nchini Kenya, ili kufanyiwa uchunguzi wa lazima kwenye mikundu yao.[20] Uchunguzi wa mkundu ni njia iliyokataliwa kisayansi ya kutafuta "ushahidi" wa kufanya mapenzi ya jinsia moja, na imeshutumiwa na Kamati ya Umoja wa Mataifa dhidi ya Mateso.[21] Daktari aliyewafanyia uchunguzii, Dkt.

Stephen Kalai, aliliambia Human Rights Watch kwamba aliwaelekeza wanaume hao kulala chali juu ya meza na kuweka miguu yao kikuku kisha kukohoa, huku akitumia kiookuzi kuchunguza mikundu yao. Hatimaye alitoa ripoti yake, kwa kutumia "Fomu ya Kurekodi Visa vya Ubakaji" (Post Rape Care Form)–fomu iliyotengwa kwa kurekodi dhuluma dhidi ya manusura wa ubakaji lakini iliyokusudiwa kuripoti matokeo ya uchunguzi wa mkundu. Moja kati ya ripoti hizo inasema "misuli ya mkundu haikuharibiwa / hakuna dalili ya ngono kati ya wanaume,"[22] wakati fomu nyingine ikidai kuwepo kwa ushahidi wa "upenywaji wa mara kwa mara wa mkundu kwa kifaa butu.”[23] Dkt. Kalai alisema kuwa aliweza kuafikia mahitimisho haya kwa kufanya uchunguzi wa kutazama tu.[24]

Huku ripoti hii ikiandikwa, kesi dhidi ya wanaume hao wawili bado inaendelea. Mwanamume mmoja aliachiliwa kwa dhamana baada ya miezi miwili kutoka Gereza lenya ulinzi mkali kadiri la Kwale, huku mwingine akiachiliwa baada ya miezi minne.[25] Hata kama mashtaka yatatupiliwa mbali hatimaye wanaume hao wawili wanahofia kwamba maisha yao yatakuwa yameathirika kiasi kwamba hawataweza kurejea maisha yao ya zamani kulingana na jinsi habari juu ya kesi hii ilivyokuwa imeenezwa pakubwa. Mmoja wao tayari amefurushwa kutoka kwa nyumba aliyokuwa amekodi mjini Mombasa baada ya kutoka gerezani. Alisema, "mwenye nyumba aliniambia, 'Hatuwezi kuwa na aina ya kiumbe kama wewe hapa.’"[26]
 

Tishio la kushambuliwa na kukamatwa liliwatia wana LGBT katika Kaunti ya Kwale kwenye hali ya msukosuko. Tony, ambaye alishambuliwa kwa chupa, alirudi Ukunda, lakini aliliambia Human Rights Watch mnamo Machi 2015 kwamba:

Sisi sote tulilazimika kwenda mafichoni. Mimi bado niko mafichoni. Siwezi kwenda nje, wala kufanya chochote.

Magazeti yanachapisha habari zetu; wakati picha hizi zilipofichuliwa, tulitembelewa na wanahabari. Polisi wanatuwinda sana. Polisi wa Kenya wanataka kuonyesha umma kuwa wanafanya kazi. Viongozi wa kijamii – Waislamu na Wakristo – wanawashinikiza polisi.
[27]

Charles, mwanaharakati mwenye makao yake kule Ukunda, alisema kuwa takriban wanaume 50 walikimbia makazi yao kutokana na mashambulizi na kukamatwa.[28] Mnamo mwezi Mei, miezi mitatu baada ya tukio hilo, alieleza kuwa:

Baadhi ya wale ambao walitoroka wamerudi, wale ambao walikuwa wameajiriwa. Wale ambao walikuwa wanaishi na wazazi wao hawawezi kurudi. Sasa hawana budi ila kutafuta ajira zao wenyewe. Walifukuzwa na jamaa zao pamoja na kijiji kizima.[29]

Mmoja wa wale ambao walikimbia makazi yao, Francis, alisema kuwa vitisho kutoka kwa majirani zake vilimlazimisha kuondoka. "Sina picha yoyote ya kuonyesha uchi, [lakini] walikuwa wanasema 'wewe unaendeleza ponografia.' Hawakuwa hata wakichukua muda kuchunguza kile kilichokuwa kikiendelea."[30]
 

Baada ya kupokea vitisho vya kuuawa kwa njia ya simu, Francis alikimbilia Nairobi, huku akiamini kwamba hangeweza kuwatarajia polisi kumlinda. "Kilichonitia hofu zaidi ni kwamba polisi waliwatia mbaroni watu wawili. Lazima nikimbie sasa, ikiwa polisi wanafanya hivyo na hawezi kusaidia, basi mimi sina budi ila kukimbia. "[31]

Wengine, kama Leonard, walibaki katika Kaunti ya Kwale lakini walikwenda mafichoni: "Nimekaa ndani kwa muda wa majuma matatu na ninahofia kutoka nje; huwezi kujua ni nini watu wamekupangia. ... Sasa hivi wanaume wanaofanya mapenzi na wanaume hawana haki."[32]

Mashambulizi ya Kwale na baadaye kuhamishwa kwa wana MSM na wanawake wanaotamani kubadilisha jinsia zao kutoka kwa makazi yao kumedhuru jitihada za kuzuia na kutoa matibabu ya VVU. Evans Gichuru wa Taasisi ya Utafiti wa Madawa ya Kenya (Kenya Medical Researc Institute, KEMRI) alidhihirisha hofu yake kuwa "watu wanaotumia dawa [ya kupunguza makali ya VVU] hawawezi kupata dawa" ikiwa wamo mafichoni.[33]

UKWELI, shirika la kijamii la wanaume wanaofanya mapenzi na wanaume, lilisitisha shughuli zake za kuzuia kuenea kwa VVU baada ya polisi kuanza kuwakamata wana LGBT. Mmoja wa wanachama wake, ambaye alikimbia nyumbani kwake Ukunda kwa sababu ya vitisho vya kuuawa kutoka kwa majirani, alisema:

Wao hututishia – walituambia kwamba sisi tukirudi nyumbani, wanapanga kutuua.

Tuna kundi linaloitwa UKWELI. ... Tunajaribu kufundishana sisi wenyewe jinsi ya kutumia kondomu na kuzuia VVU / UKIMWI. Lakini hatuwezi kufanya hivyo sasa. Wakituona pamoja wanafikiri tunapanga kuwafundisha wavulana jinsi ya kufanya mapenzi na wanaume. Kwa hivyo hatukutani tena.
[34]

Watamu (Kaunti ya Kilifi), Februari 2015: Vitisho Dhidi ya Waombolezaji wana LGBT Waliokuwa katika Mazishi
Mnamo mwezi wa Februari 2015, wakati mwanamume mmoja huko Watamu (Kaunti ya Kilifi) alifariki kutokana na ugonjwa, marafiki zake – wakiwa ni pamoja na baadhi ya wana LGBT –walipanga mazishi. Kulingana na Douglas Masinde, mwanaharakati wa Kilifi, wakazi wa mtaa huo "walianza kughadhabishwa" na kuwepo kwa waombolezaji wenye mienendo isiyoambatana na mahusiano ya kawaida ya kijinsia, na kutishia kuwashambulia. Mtu fulani aliwaita polisi, ambao walikuja kuwapa ulinzi waombolezaji waliokuwa wana LGBT.

Masinde, ambaye amewahi kupanga warsha kuwafunza polisi wa Kilifi kuhusu haki za kibinadamu za wana LGBT, alisema tukio hilo lilidhihirisha haja ya umma kuhamasishwa pia:

Hakuna mtu aliyepigwa, lakini kama hatua haingechukuliwa, baadhi yao wangepigwa.

Hatua ambayo polisi walichukua ilikuwa sahihi. Lakini kuna haja ya kuhamasisha jamii kijumla kuhusu ujinsia wetu. Ikiwa polisi hawangekuwapo, basi kungetokea nini?[35]

Gazeti la The Standard lilichapisha makala chochezi likidai kwamba waombolezaji hao wana LGBT walikuwa wakishiriki katika "matambiko ya mashoga" katika mazishi. Makala hiyo kwa sasa imefutwa kutoka kwenye tovuti ya gazeti la The Standard.[36]

Mombasa, Oktoba 2014: Kupigwa na Vitisho Kufuatia Ripoti kuhusu "Ponografia"

Mnamo Oktoba 2014, wakazi wa Kisauni, kitongoji cha Mombasa, waliwashambulia na kuwatishia wakazi wana LGBT baada ya video ya ngono, ambayo inadaiwa iliwashirikisha wakazi wanaume wanaofanya mapenzi na wanaume, kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii.

Samir, mkaaji wa Kisauni ambaye ni kuchu, alisema kuwa kundi la wakazi waliokusanyika kwa hiari lilimpiga kijana mmoja ambaye inadaiwa alishiriki katika video hiyo. Kwa mujibu wa Samir:

Ilikuwa hali ngumu sana. Walisema walitaka kuwapiga wanaume wote katika eneo hilo waliofanya mapenzi na wanaume. [Mwathiriwa] hakuenda kwa polisi. Sijui kama yeye alikwenda hospitalini kwa sababu mimi pia nilikimbilia usalama wangu – nikaelekea kwa rafiki yangu huko Kilifi. Nilikaa huko kwa wiki mbili. Watu wengi walikimbia wakati huo.

Samir alikariri pia ukosefu wa msimamo kamili wa polisi katika kukabiliana na mashambulizi dhidi ya watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja:


Jamii ilitaka kuandamana na kwenda nyumba hadi nyumba kuwasaka wanaume wanaofanya mapenzi na wanaume. Polisi waliingilia kati na kusitisha mpango huo. Lakini hawakuwakamata watu waliompiga [mwaathiriwa].[37]

Bettina, mwanamke aliyebadilisha jinsia yake, alisema kuwa ghadhabu zinazohusishwa na video husika ilitumiwa kama kisingizio cha wakazi wanaotawaliwa na chuki dhidi ya wanaotamani kubadilisha jinsia zao kushambulia kibanda ambapo alikuwa akiuzia chakula. "Walikuwa wanatafuta kisingizio cha kunishambulia lakini hawakuwa na ushahidi wowote," alisema Bettina.[38] Aliongezea kuwa:

Sikufahamu kuhusu video yoyote. Mimi siye niliye katika video hiyo. [Lakini] watu walikuja na kushambulia kibanda changu, walitupa kila kitu nje. Walikifunga. Hivyo ilibidi nipoteze kila kitu.

Bettina aliambiwa na jamaa wa mmiliki wa kibanda hicho kwamba genge la watu walikuja siku iliyotangulia, na kutishia kuvifunga kabisa vibanda vyake; wakati mmiliki huyo alipokosa kuchukua hatua yoyote ya kumwondoa, genge hilo lilichukua sheria

mikononi mwao.[39]
 

Bettina alienda kwa polisi. Lakini polisi walikataa kumpa nambari kwa kesi yake, nambari ambayo waathiriwa wa uhalifu lazima wapewe ili kufuatilia kesi zao, inaonekana kwa sababu ya utambulisho wake wa kijinsia.

Nilikwenda katika Kituo cha Polisi cha Central, na nikaandika taarifa. Polisi aliniuliza: 'Je, wewe ni mwanamume au mwanamke?'

Nami nikasema, 'Wewe unaona nini?' Halafu alikataa kunipa nambari ya OB [nambari ya kesi].

Hivyo niliondoka kwa sababu hakukuwa na kitu chochote pale cha kunifaidi na ilinibidi kuondoka.
[40]

Likoni (Kaunti ya Mombasa), Februari 2012: Mashambulizi dhidi ya Warsha ya VVU

Katika mwezi wa Februari 2012, Muungano wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali yanayopambana na UKIMWI nchini Kenya (Kenya AIDS NGO Consortium, KANCO) liliandaa warsha ya siku nne ya elimu mwenza kuhusu VVU/UKIMWI kwa wanaume wanaofanya mapenzi na wanaume wenzao (MSM) katika kituo cha jamii huko Likoni, mji ulio kusini mwa Mombasa.

Mnamo Februari 23, siku ya mwisho ya warsha, wakazi wa mji walipata kujua kuwa kituo hicho kilikuwa mwenyeji wa warsha kwa wana MSM. Kwa mujibu wa chombo cha habari, "vijana wapatao 100, wakiongozwa na viongozi wa kidini na wazee wa kijiji waliingia katika ukumbi huo kwa lazima."[41]

Esther Adhiambo wa PEMA Kenya anaeleza kuwa alipokea “simu kadhaa za kuomba usaidizi wa dharura kutoka kwa washiriki ambao alisema waliweza kutoroka kupitia dari ya ukumbi huo wa warsha na kuruka nje kupitia ua la nyuma, na kuwa walikuwa wamewaacha baadhi ya watu katika ukumbi wa warsha.”[42] KANCO na mashirika mengine yaliyoshiriki katika warsha hiyo, yaliripoti kuwa umati “ulivamia jengo hilo kwa lengo la 'kuwafurusha mashoga.’”[43]

Shirika la KANCO lilipanga matatu (basi la usafiri wa umma) kuwasalimisha baadhi ya washiriki. Wakili wa PEMA Kenya aliwasiliana na polisi wa Likoni, ambao waliwasili katika eneo la tukio na kuwasindikiza washiriki waliobaki hadi eneo salama. Hata hivyo, umati uliwafuata polisi hadi wakati walimshusha mmoja wa wanaume hao nyumbani kwao. Alilazimishwa kuhama siku iliyofuata kutokana na vitisho. Mwanamume mwengine kuchu, ambaye picha yake ilionyeshwa kwenye televisheni, alifurushwa na mwenye nyumba ambapo alikuwa amekodi siku tatu baadaye.[44]


Polisi hawakumkamata yeyote kati ya waliotekeleza shambulizi hilo, wala hawakuwakamata viongozi wa kidini ambao walichochea shambulizi husika. Hawa walikuwa ni pamoja na kiongozi wa Kiislamu ambaye, kwa mujibu wa ripoti katika vyombo vya habari, "alitishia kuhamasisha jamii kuwapiga viboko mashoga kama wangethubutu kupanga mkutano kama huo tena."[45]

Afisa wa wilaya kutoka Wizara ya Vijana na Michezo alitetea warsha hiyo, huku akiwaambia maripota "Wana haki ya ngono salama. Kwa kufanya hivi, sisi hatuendelezi mapenzi ya jinsia moja ila tunatoa elimu."[46]

Mtwapa (Kaunti ya Kilifi), Februari 2010: Mashambulizi dhidi ya wana LGBT na Kituo cha Afya
Mnamo mwezi Februari 2010, viongozi wa Kikristo na Kiislamu jijini Mombasa walieneza uvumi kwamba "harusi ya mashoga" ilikuwa imepangwa kufanywa Mtwapa.[47] Tarehe 11 Februari, walifanya mkutano na waandishi wa habari na kusema kuwa walikusudia kusitisha kufanyika kwa harusi hiyo kwa mbinu zozote zile, na kufunga ofisi ya Taasisi ya Utafiti wa Madawa ya Kenya (KEMRI) katika eneo hilo, asasi ya umma ambalo hutoa huduma za VVU kwa MSM, ambalo walilituhumu kutoa ushauri nasaha kwa "wahalifu."[48]

Mnamo Februari 12, genge la takriban watu 200 lilizingira KEMRI. Wakawashambulia wana LGBT wengi waliokuwa waelimishaji rika katika shirika hilo.[49]

Kalisa, mmoja wa waelimishaji rika aliyeshambuliwa, alisema kuwa alipigwa na genge la watu kama 100.
 

Walinichoma moto kwa viberiti na sigara. Nilijaribu kukimbia, lakini nina ugonjwa wa pumu, hivyo nikaanguka. ... Nilipigwa mpaka nikazimia. Mtu fulani aliwaita polisi, ambao walikuja. Nilipewa ulinzi na kuchukuliwa na polisi.[50]

Richard, mwanamume ambaye ni shoga, alikuwa katika KEMRI wakati huo, alikumbuka:
 

Watu walikuwa wakipiga mayowe, ‘Tunataka kukichoma kituo hiki. KEMRI linaendeleza ushoga.’ Umati ulikuwa na hamasa sana na uliongozwa na viongozi wa kidini.[51]

Polisi waliutawanya umati na kumchukua Kalisa na wana LGBT wengine waliokuwa wamekusanyika katika kituo cha KEMRI na kuwapeleka kwenye kituo cha polisi kwa ajili usalama wao.[52] Washambuliaji hao, wakiwemo viongozi kadhaa wa kidini, waliwafuata, na kutishia kukichoma kituo cha polisi kama polisi hangewakabidhi Kalisa.[53] Kalisa alikumbuka Imamu mmoja akisema kuwa alitaka "kuwamaliza mashoga wote nchini Kenya."[54]

Wanaharakati wa haki za kibinadamu walifaulu kumtorosha Kalisa kisirisiri kutoka katika kituo cha polisi baadaye siku hiyo. Alikwenda mafichoni jijini Nairobi kwa miezi saba. Wengine ambao waliponea chupuchupu shambulizi hilo pia walikimbia eneo hilo kwa majuma au miezi kadhaa.[55]

Kwa mujibu wa Tume ya Haki za Kibinadamu ya Kenya, polisi hawakufanya jitihada zozote kuchunguza na kuwashtaki wale waliochochea shambulizi la Mtwapa, ikiwa ni pamoja na viongozi wa kidini.[56]

Malindi (Kaunti ya Kilifi), Juni 2008: Kufungwa kwa Kituo cha Afya Kinachowahudumia wana MSM
Mnamo Juni 2008, shirika linalotoa huduma za afya kwa wanaume wanaofanya mapenzi na wanaume (MSM) huko Malindi, sehemu ya Kaunti ya Kilifi, lilifungwa kwa nguvu na maafisa wa serikali katika eneo hilo.[57] Tawi la Kenya la International Centre for Reproductive Health – (ICRH-Kenya), kituo cha utafiti chenye makao yake jijini Mombasa ambacho huendesha utafiti na miradi ya kinga katika nyanja mbalimbali ikiwa ni pamoja na afya ya ngono na VVU, walifungua tawi katika Malindi kwa lengo la kutoa elimu rika na ushauri nasaha sawia na kutoa huduma za uchunguzi kuhusu VVU na magonjwa ya zinaa miongoni mwa wanaume wanaofanya mapenzi na wanaume. Nzioki King'ola, Naibu wa Mkurugenzi Mkuu wa ICRH-Kenya, alikumbuka:


Kituo hicho kilikuwa kimekuwepo pale kwa miezi miwili. Hata hatukuwa tumekizindua kirasmi. Wakati viongozi wa Kiislamu walipata habari kukihusu, na kuwaona wana MSM vijana wakikutana huko, walipinga kuwepo kwake na kutishia kuwapiga waelimishaji rika na kukichoma kituo hicho kwa petroli.[58]

Evans Gichuru alikuwa anafanya kazi na ICRH wakati huo. Alikumbuka:

Vijana, wapatao 40 hivi, walikuja hata na mafuta ya gesi. Baadhi yao hata walibeba panga. Nililazimika kuzungumza nao mimi mwenyewe ili kuwatuliza. Walisema kuwa walidhani shirika hili lilikuwa likiendeleza mapenzi ya jinsia moja.[59]

ICRH lilifanya mkutano na viongozi wa Kiislamu, chini ya usimamizi wa chifu wa eneo hilo, afisa wa serikali ya mitaa, kwa lengo la kuweka makubaliano kuhusu shughuli za kituo hicho. Viongozi wa kidini walisisitiza kuwa kituo kifungwe. Maafisa wa ICRH, walipohisi kuwa hawana kingine cha kufanya, wakakubali. Walianzisha mitandao ya elimu ya kihirimu iliyoendelea kufanya kazi walipoondoka, lakini halikuweza kufanikisha mipango ya kuweka kituo cha huduma za kupima virusi vya ukimwi na kutoa huduma nyingine za msaada kwa walio na VVU.[60]

Mashambulizi mengine dhidi ya Wana LGBT
Mbali na mashambulizi dhidi ya makundi yaliyotajwa hapo juu, mashambulizi dhidi ya watu binafsi walio wana LGBT pia hufanyika Pwani. Wanaume wasiopungua wawili wanaojulikana kushiriki mapenzi ya jinsia moja wameuawa pwani katika miaka mitatu iliyopita. Kumi na sita kati ya wale tuliowahoji walikuwa wamewahi kushambuliwa na raia ambao wengine wao hawakuwajua nao wengine wanajuana nao, katika mashambulizi ambayo waliamini kuwa yalitokana na utambulisho wao wa kijinsia au hisia za kimapenzi. Watu wenye mienendo ya kijinsia inayokwenda kinyume na kawaida, wakiwemo wanaume ambao huchukuliwa kuwa na tabia kama za kike, ni miongoni mwa wale wanaolengwa mara nyingi na unyanyasaji.[61]

Polisi na maafisa wengine wa usalama wana wajibu wa kutoa usaidizi kwa wana LGBT ambao ni waathiriwa wa uhalifu, lakini mara kwa mara polisi hawawajibiki ipasavyo. Sio wana LGBT pekee ndio wanaonyimwa ulinzi wa kutosha na polisi. Shirika la Human Rights Watch limerekodi ulinzi duni na polisi katika muktadha wa mashambulizi ya kigaidi, vita vya kikabila, na visa vingine vya vurugu kubwa.[62] Kwa wakati mwengine, huenda inaonekana kama wana LGBT wanashughulikiwa na polisi kwa njia bora kidogo kuliko makundi mengine yaliyo hatarini. Polisi wakati mwingine wamewahi kuwaokoa wana LGBT kuepuka mashambulizi ya magenge huko pwani, kama ilivyokuwa mwaka 2010 wakati wa kisa kilichotokea Mtwapa, warsha ya KANCO ya mwaka 2012 huko Likoni, na mashambulizi kwenye mazishi huko Watamu mwaka 2015, visa vyote vikiwa vimefafanuliwa hapo juu.

Mara nyingi, hata hivyo, polisi walio maeneo ya pwani wameitikia visa vya mashambulizi dhidi ya wana LGBT kwa kuwashughulikia waathiriwa kinyanyapaa na kibaguzi, kukataa kuchukua taarifa zao wala kuwapa msaada. Wengi miongoni mwa wana LGBT tuliowahoji walituelezea kwamba wao huwaogopa polisi, na hawakuwa na nia ya hata kujaribu kuwasilisha malalamiko, kama ilivyorekodiwa hapa chini.

Hata jinsi polisi walivyoshughulikia mashambulizi ya Mtwapa ya mwaka 2010, ambapo polisi walitoa ulinzi kwa KEMRI na waelimishaji rika wake MSM na waliobadilisha jinsia zao, ilituma ujumbe mchanganyiko. Mwanaharakati mmoja ambaye ni shoga alisema kuwa moja ya mafunzo ya mashambulizi ya Mtwapa ilikuwa "Ikiwa mimi ni shoga na nishambuliwe, polisi wataniokoa hatarini. Lakini hakuna hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wakosaji."
[63]

Wakati Walinda Usalama Wanapogeuka kuwa Wahalifu
Mashirika ya kitaifa na yale ya kimataifa yanayotetea haki za kibinadamu, ikiwa ni pamoja na Human Rights Watch, yamerekodi kwa miaka kadhaa ruwaza ya mwenendo dhalimu wa polisi wa Kenya dhidi ya makundi yaliyo hatarini, wakiwemo wakimbizi, kabila la Wasomali, jamii za wafugaji wa kuhamahama, na wakazi wa mitaa ya mabanda.[64] Ripoti hizo zinadhihirisha hali ya kutojali sheria na kutowajibika kutoka kwa serikali ya Kenya.

Wana LGBT pia – hasa wale ambao hushiriki katika biashara ya ngono – wanakabiliwa na unyanyasaji mikononi mwa polisi. Wengi wa mashoga na wanawake waliobadilisha jinsia zao katika pwani – wakiwemo 39 kati ya 58 tuliowahoji – wanashiriki katika biashara ya ngono mara kwa mara au wakati mmoja mmoja. Hii kwa kiasi fulani ni kutokana na ukosefu wa nafasi za ajira. Ukosefu wa ajira kwa vijana wote uko katika viwango vya juu zaidi hasa jijini Mombasa.
[65] Kwa wale ambao wanakabiliwa na ubaguzi katika ajira au ambao hawakuwahi kukamilisha masomo kwa sababu ya ubaguzi kwa misingi ya hisia za kimapenzi au utambulisho wao wa kijinsia, fursa za ajira ni chache.[66]

Kama wafanyakazi ya ngono wa kike, wafanyakazi ya ngono wa kiume na wafanyabiashara ya ngono waliobadilisha jinsia zao pia wanakabiliwa na dhuluma za kingono na unyang’anyi mikononi mwa maafisa wa polisi na maafisa wa kutekeleza sheria za serikali ya kaunti, wanaojulikana kwa lugha ya mitaani kama kanjoo ama makanjoo. Miongoni mwa waliohojiwa 39 ambao wakati mwingine hushiriki katika biashara ya ngono, 15 kati yao walisema kuwa maafisa wa polisi au kanjoo hutishia kuwakamata ikiwa watakataa kufanya ngono nao. Kwa mujibu wa sheria ya Kenya, kufanya mapenzi na mtu kwa lazima "kwa kutumia nguvu au kwa njia ya vitisho vya aina yoyote" ni ubakaji.[67]
David, mwenye umri wa miaka 25, aliliambia shirika la Human Rights Watch kwamba amesumbuliwa na polisi mara nyingi kwa sababu ya kazi ya ngono lakini hakuwa kazini usiku ambapo polisi walimshika. Alisema:
 

Nilikamatwa mnamo Septemba 2013 nikiwa ninatembea kukutana na rafiki yangu wakati wa usiku. Polisi walitaka niwahonge lakini sikuwa na fedha za kutosha, hivyo walinipeleka hadi Fort Jesus, eneo lenye kasri zee la makumbusho ambapo kuna giza. Kisha walinibaka: maafisa wawili wa polisi walifanya hivyo.[68]

Maafisa wa kutekeleza sheria za serikali ya kaunti – kitengo tofauti na polisi – pia huwabaka na kuwanyanyasa wanaume wafanyi biashara ya ngono. Guyo alieleza jinsi alivyobakwa na kundi la maafisa wa kutekeleza sheria za serikali ya kaunti [“makanjoo”] mnamo mwezi Novemba 2014:
 

Makanjoo walinipata barabarani na wakanichukua kwa lori ambalo hutumika kwa kawaida [kufanyia misako]. Walikuwa wakinibaka ndani ya lori walipokuwa wakizunguka jijini Mombasa. Takriban watano kati yao walinibaka. Hawakutumia kondomu. Walinizungusha kotekote kwa karibu masaa manne. Walinikamata mwendo wa usiku wa manane au saa saba usiku, lakini walinipeleka katika kituo cha polisi cha Central mwendo wa saa kumi na nusu alfajiri. Nilipelekwa mahakamani na kushtakiwa kwa kosa la kuzua kero na kuzurura.[69]

Ubakaji unaotekelezwa na maafisa wa kutekeleza sheria ni ukiukaji mkubwa wa haki za kibinadamu. Ingawa Human Rights Watch lilirekodi baadhi ya visa hivyo, hilo si lengo la kimsingi la ripoti hii. Kwanza, visa hivi vinahitaji uchunguzi zaidi ili kutathmini ni tawi jipi la utekelezaji sheria linalostahili kulaumiwa zaidi. Pili, mashirika mengine yamerekodi visa sawa vya ubakaji wa wafanyabiashara wa ngono wa kike unaofanywa na maafisa wa usalama, katika pwani na kwingineko.[70] Si wazi kwamba watu tuliowahoji, ambao walielezea ukiukaji huo, walinyanyaswa kwa misingi ya hisia zao za kimapenzi au utambulisho wao wa kijinsia, au kwa sababu tu, kama wafanyabiashara wa ngono, maafisa wa usalama waliwachukulia kama windo jepesi. Katika ripoti hii, tuliamua kuangazia zaidi ukiukaji unaofanywa waziwazi kwa misingi ya utambulisho wa kijinsia wa mwathiriwa au hisia ya kimapenzi, huku tukitambua kwamba kwa wafanyabiashara wa ngono wa kiume na waliobadilisha jinsia zao, kuna uwezekano wa kuwepo kwa utata kiasi kuhusu kile kinachowachochea wanaoutekeleza unyanyasaji huo.

Hata wakati ambapo hawajachochewa na hisia za kimapenzi au utambulisho wa kijinsia, ubakaji unaofanywa na maafisa wa usalama, pamoja na aina zingine za unyanyasaji ambao maafisa wale hutekeleza dhidi ya wana LGBT, una madhara makubwa kwa uaminifu kati ya waathiriwa wa unyanyasaji wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja na taasisi za kutekeleza sheria ambazo zahitajika kuwepo ili kuwalinda waathiriwa.

Ishmael, mwanaharakati, alidhihirisha utata ulioko katika jukumu la polisi katika kuwalinda au kukosa kuwalinda wana LGBT:

Katika Malindi kulikuwa na mazishi ya mwanamume aliyejulikana kama shoga. Polisi walikuja kuwaokoa wavulana hao dhidi ya umati wa watu. Sasa kukitokea mashambulizi, polisi watawapeleka wavulana hao kituoni [na] kusubiri umati kutawanyika.

Hivyo kama ni suala lililo hadharani, machoni pa umma, polisi wanatoa ulinzi. Kama ni suala la faragha, basi polisi wanakudhulumu na ni wafisadi.... Ikiwa utashukiwa [kuwa wewe ni shoga], basi umo hatarini, kisha wanaangalia iwapo kuna uwezo wa hao kukutumia kwa ajili ya ngono au fedha, na watatumia nafasi hiyo kukunyanyasa au kukudhulumu.[71]

Ubaguzi wa Polisi na Kukataa Kwao Kuandikisha Taarifa Kutoka kwa wana LGBT
Mnamo Juni 21, 2013, wakati wa kile ambacho shirika la Gay and Lesbian Coalition of Kenya (GALCK) baadaye ilielezea kuongezeka kwa vurugu za wazi dhidi ya wana LGBT, mwanamume mmoja ambaye ni shoga jijini Mombasa alikatwakatwa kwa upanga shingoni na kooni na mshambuliaji asiyejulikana. Mwathiriwa alinusurika kifo kutokana na shambulizi hilo na kupokea matibabu.[72]

Jo, rafiki ya mwathiriwa ambaye ni msagaji, alimpeleka katika kituo cha Polisi cha Central jijini Mombasa kuandikisha ripoti. Lakini polisi walikataa kupokea kesi hiyo, alisema Jo: "Waliichukulia kesi hiyo kijuujuu. Walisema 'Mashoga hawa ni wezi' na kusema hawangeweza kuishughulikia kesi hiyo. Hawakuaandika taarifa."[73]

Kama hao polisi wangekubali kuchukua ripoti ya mhasiriwa, wangeokoa maisha ya mtu mmoja. Siku tatu baadaye, tarehe 24 Juni, shoga mwingine aliuawa katika shambulizi sawa jijini Mombasa; naye pia alipatikana na majeraha ya kukatwakatwa shingoni na kooni.[74] Upungufu katika uchunguzi wa polisi umechangia kutobaini ikiwa waathiriwa walilengwa kutokana na hisia zao za kimapenzi ama na utambulisho wao wa kijinsia au kwa sababu nyinginezo.[75]

Polisi pia humlaumu mwathiriwa, wakati waathirika wa uhalifu ni wachache kijinsia ama kimapenzi. Samir alibakwa na genge la wanaume mnamo mwaka wa 2011 akiwa na umri wa miaka 20, alipokuwa akisubiria usafiri saa sita na nusu usiku huko Bamburi, Kaunti ya Mombasa. Mwanamume fulani alimnyaka Samir, akamwekea kifaa baridi shingoni, na kumwonya asithubutu kupiga mayowe. Mwanamume huyo alimshurutisha Samir kuvuka barabara hadi kwenye eneo faragha, ambapo wanaume wengine sita walijiunga naye. Walimwibia Samir simu yake na shilingi 5000 hela za Kenya (karibu Dola 50 za Marekani). Kisha, Samir alisema:

Waligundua kuwa mimi ni kuchu na kunivua uchi, huku wakinipiga sana. Nilibakwa kwa zamu. 'Wewe unapenda lolote unalofanyiwa na wanaume. Sasa tutakufanyia hayo.'
Baada ya kubakwa, Samir alimwarifu mamake, ambaye alimchukua hadi Kituo cha Polisi cha Nyali. Lakini polisi wa zamu alikataa kuchukua taarifa yake.
Polisi aliuliza, 'Kwa nini umeleta mtu mwenye madai kama haya? Mwangalie, hawa ni wasichana wanaocheza tu kwenye baa. Anastahili alichokipata.'
 
'Na je kama angekuwa mwanako?' Mama yangu aliuliza.
 
'Ningependa afe,' polisi alisema.[76]
Samir aliondoka kituoni bila kuandikisha kesi yake.

Kisa cha Bettina, mwanamke aliobadilisha jinsia yake na mwenye kibanda cha kuuza vyakula jijini Mombasa na kilichovamiwa na genge la watu mnamo Oktoba 2014, tayari kimeelezwa hapo juu: alipokwenda kuripoti uhalifu huo, polisi walikataa hata kumpa nambari ya kesi, na badala yake kuzidi kumhoji iwapo alikuwa mwanamume au mwanamke. Bettina tena aliwahi kupatana na mabaya mikononi mwa polisi baada ya kupigwa na genge la wanaume wanne mnamo Januari 2010, alipokuwa akishiriki katika biashara ya ngono. Aliliambia Human Rights Watch:
Genge la wanaume wanne lilifika pale nilikuwa nimesimama na kuuliza ni kitu gani nilikuwa nikifanya. Nilikuwa nimevaa tayari kwa kazi, sikujua niwaambie nini. Hivyo walianza kunitukana, huku wakinipiga. Nilipigwa makofi, mateke, na kutukanwa. Waliniacha nimelala hapo baada ya kunipiga, nikiwa nimejeruhiwa na nikitokwa na damu .... Baadhi ya marafiki zangu wafanyakazi wa ngono walinipata na kunipeleka hospitalini ambako nililazwa kwa wiki moja.
Nilipiga ripoti kwa polisi lakini hakuna chochote kilichofanyika. Nadhani kwamba ni kawaida nchini Kenya, unaweza kupiga ripoti kwa polisi lakini hawawezi kukushughulikia kama wewe ni mfanyakazi wa ngono bila kuwapa pesa.[77]

Huku mashambulizi yakiwa ndiyo hatari kubwa zaidi inayowakabili wana LGBT katika pwani, aina nyinginezo za ukiukaji wa haki za kibinadamu, ikiwa ni pamoja na kufurushwa na wamiliki nyumba wanaochukia mapenzi ya jinsia moja, kunachangia ukosefu wa usalama.
Douglas, mwanaharakati wa Kilifi, aliliambia Human Rights Watch kuwa polisi walikataa kuyashughulikia malalamiko yake alipofurushwa nyumbani kinyume na sheria kwenye misingi ya hisia yake ya kimapenzi:

Nimefurushwa sasa kutoka kwa kama nyumba 10. Nimejaribu kuwaarifu polisi lakini walichosema ni kwamba, 'Hatuwezi kwenda kuwashurutisha wamiliki wa nyumba kukuweka katika nyumba hiyo; unachofanya si halali.'[78]

Hofu ya Kukamatwa kama Kikwazo dhidi ya Haki
Sheria zinazoharamisha mapenzi ya jinsia moja nchini Kenya, katika kesi chache ambapo zimewahi kutumika, zimetumika vibaya: Washukiwa wanakamatwa kwa kushukiwa tu kuwa ni wapenzi wa jinsia moja, si kwa sababu kuna ushahidi wowote wa kutosha wa kuonyesha kuwa wamevunja sheria. Hofu ya kukamatwa kwa sababu ya kushiriki mapenzi ya jinsia moja huwa ni kikwazo kwa mtu yeyote ambaye angetaka kuripoti uhalifu kutokana na chuki dhidi ya wana LGBT, kwa sababu katika kufanya hivyo, watahitajika kufichua kwa polisi hisia yao ya kimapenzi au utambulisho wao wa kijinsia.
Baada ya wakazi kuanza kuwashambulia na kuwadhulumu watuhumiwa wana LGBT katika Kaunti ya Kwale mnamo mwezi wa Februari mwaka 2015, Patrick, ambaye ni shoga, alionywa na afisa wa polisi dhidi ya kutafuta msaada kutoka kwa polisi, kwa sababu polisi labda walikuwa wakiwatafuta mashoga ili kuwakamata kufuatia kusambaa kwa ripoti kuhusu picha za ponografia. Patrick alikuwa na rafiki yake Tony wakati Tony alipigwa kwa chupa barabarani, kama inavyoelezwa hapo juu:

Mtu fulani alimrushia [Tony] chupa na ikabidi tumpeleke hospitalini. Tulimpigia simu mmoja wa 'polisi rafiki’ ya wana LGBT, [lakini akasema,] 'Tayari jambo hili [kashfa ya ponografia] lipo – mkienda kupiga ripoti mnaweza kukamatwa.' Tulisitisha mpango huo tukiwa njiani kuelekea kituo cha polisi.[79]
Matukio haya, pamoja na mtazamo wa kijumla miongoni mwa wana LGBT kuwa polisi huenda wakawanyanyasa wala si kuwalinda, yanachochea hofu ya kuripoti uhalifu kwa polisi, hasa miongoni mwa wafanyakazi wa ngono wa kiume.
Ahmed, mfanyakazi wa ngono wa kiume, alisema kuwa mnamo mwaka wa 2012, kundi la vijana wanane au tisa wanaozurura mitaani kule jijini Mombasa walimburura hadi ufuoni, ambako walimpiga na kumbaka. Aliliambia Human Rights Watch, "Singeweza kuripoti kwa polisi kilichotokea, kwa sababu wangeniuliza nilichokuwa nikifanya nje wakati wa usiku."[80]

Vile vile, Daudi alibakwa mnamo mwaka wa 2009 na mteja ambaye alikataa kumlipa. Alieleza:
Nilihisi singeweza kwenda kwa polisi kwa sababu wangesema, 'Sababu wewe ni shoga, hiki ndicho unachopata.' Mwenzangu mmoja, mfanyibiashara wa ngono wa kiume aliambiwa hivi wakati aliripoti kubakwa. Hivyo sitapiga ripoti.[81]

Charles, mwanaharakati wa Ukunda, alielezea shambulizi la mwaka wa 2011 ambapo wakazi wa Mombasa walimvua uchi mfanyakazi wa ngono wa kiume akiwa barabarani. Charles alisema, "Yeye hakwenda kwa polisi. Huo ndio uhusiano uliovunjika – watu wanasema, afadhali niteseke kimyakimya kuliko kwenda kwa polisi."[82]

Athari za Mashambulizi na Ubaguzi dhidi ya wana LGBT kwa Haki ya kuwa na Afya

Wataalamu wa afya wanakubaliana kwamba ubaguzi, mashambulizi, na sheria za jinai dhidi ya wana LGBT zinajumuisha vikwazo dhidi ya kufanikisha kinga na matibabu ya VVU na UKIMWI. Kama Shirika la Umoja wa Mataifa la Kupambana na UKIMWI (UNAIDS) ilivyohitimisha:

Kuharamishwa kwa watu walio katika hatari kubwa ya maambukizi, kama vile wanaume wanaofanya mapenzi na wanaume, wafanyakazi wa ngono, waliobadilisha jinsia zao, na watu wanaotumia madawa ya kulevya, kunawalazimisha kwenda mafichoni na mbali na huduma za VVU. Hii huongeza uwezekano wa kuambukizwa VVU, sawia na unyanyapaa, ubaguzi, kutengwa na mashambulizi.[83]

Katika mwaka wa 2014, shirika la UNAIDS lilibainisha kuenea sana kwa "dhuluma, udhalilishaji, ubaguzi, na mashambulizi dhidi ya mashoga na wanaume wengine wanaofanya mapenzi na wanaume, ikiwa ni pamoja na ubakaji, kwenye misingi ya hisia ya kimapenzi na utambulisho wa kijinsia" kote ulimwenguni. Kwa mujibu wa UNAIDS:

Katika nchi nyingi, vitendo hivyo vinatekelezwa au kukubaliwa na maafisa wa serikali ya nchi, ikiwa ni pamoja na maafisa wa kutekeleza sheria. Hii inasababisha mazingira ya woga ambayo yanachochea zaidi ukiukaji wa haki za kibinadamu na ambayo huwazuia mashoga na wanaume wengine wanaofanya mapenzi na wanaume kutafuta na kuendelea kuzingatia taratibu za kuzuia VVU, matibabu, pamoja na huduma nyingine na msaada wa kujitunza.[84]

Mwongozo wa Mikakati dhidi ya UKIMWI nchini Kenya (Kenya AIDS Strategic Framework, KASF), uliochapishwa na Baraza la Taifa la Kudhibiti UKIMWI (National AIDS Control Council, NACC), unawatambua MSM na wafanyabiashara wa ngono kama kundi maalum katika kuunda miradi ya kudhibiti VVU. Huku kiwango cha maambukizi ya VVU nchini Kenya miongoni mwa watu wengine walio kati ya miaka 15 na 49 kikikadiriwa kuwa asilimia 5.6, kiwango cha maambukizi miongoni mwa wanaume wanaofanya mapenzi na wanaume ni asilimia 18.2.[85] Mwongozo wa mikakati unatambua kuwa dhuluma dhidi ya makundi maalum ni kikwazo kwa juhudi za kupunguza maambukizi mapya.[86] Kwa hiyo unatoa wito kwa serikali za kaunti na taasisi za kitaifa za kudhibiti ugonjwa wa UKIMWI kushughulikia hujuma dhidi ya jamii muhimu, na unapendekeza zaidi kupitishwa katika ngazi ya kitaifa na kaunti "mwongozo wa kisheria unaofutilia mbali uharamishaji wa shughuli za makundi maalum, hivyo basi, kuongeza ari yao ya kutafuta na upatikanaji wa huduma za kudhibiti VVU."[87]

Katika pwani ya Kenya, mashambulizi na ubaguzi dhidi ya wana LGBT yamekuwa na athari wazi juu kwa miradi ya VVU. Katika visa vitatu kati ya visa vya mashambulizi ya magenge vilivyoelezwa hapo juu, mashambulizi au vitisho vya mashambulizi kutoka kwa wakazi na viongozi wa kidini yalisababisha watoa huduma za afya kwa wana MSM kusitisha huduma hizo kwa muda au kuzikomesha kabisa au pia kufunga warsha zao. Hata wakati walengwa wa mashambulizi ni watu binafsi wala si taasisi, miradi ya kuzuia VVU na kuendelea na tiba kwa watu wanaoishi na VVU inaathirika vibaya. Wakati wanaume wengine walioshtakiwa kuwa mashoga walikamatwa na wengine kushambuliwa katika Kwale mnamo mwezi Februari mwaka wa 2015, wengi walikimbia eneo hilo au kukaa katika nyumba zao bila kutoka nje kwa majuma kadhaa, na hivyo kusababisha kupungua sana katika kiwango cha kushiriki katika shughuli za kuzuia VVU kwenye kituo cha afya chenye makao yake jijini Mombasa ambacho kiliwahudumia wana LGBT.[88]

Parinita Bhattacharjee, mtaalamu wa VVU, alikuwa jijini Mombasa kwa mkutano kati ya Shirika la Kitaifa la Udhibiti wa UKIMWI na Magonjwa ya Zinaa (NASCOP) na wanachama wa makundi maalum muda mfupi baada ya kupitia kwa Sheria ya Kupambana na Mapenzi ya Jinsia Moja nchini Uganda mnamo Februari 2014, wakati muswada sawia ulipendekezwa na wabunge nchini Kenya. Alieleza:

­­­­­­­­­­­­­­­

Wanaharakati wa huko walikuwa na hofu ya kutembea popote, na jinsi ya kufika nyumbani. Waelimishaji rika walikuwa na hofu ya kutoka na kujionyesha kwamba wao ni waelimishaji rika. Afya kamwe si jambo muhimu wakati kuna hofu. ... Kama una wasiwasi kuhusu maisha yako, VVU / UKIMWI linakuwa suala la kushughulikiwa baadaye kabisa.[89]

Sheria zinazoharamisha mapenzi ya jinsia moja zinaweza pia kuwa kikwazo dhidi ya watoaji wa huduma za afya ambao wanaweza kuwa wanahusika katika jitihada za kuzuia maambukizi ya VVU miongoni mwa makundi maalum. Dkt. Eduard Sanders wa KEMRI aliliambia Human Rights Watch:

Mafunzo ni muhimu. Mtu ambaye hajapokea mafunzo anaweza kufikiria: 'Je, tunaivunja sheria kwa kumsaidia mtu ambaye anashiriki mapenzi ya jinsia moja?' ... Ukuzaji wa uwezo huzuiwa na sheria za jinai; ikiwa tutaonekana kama watu wanaovumilia jambo ambalo ni kinyume na sheria, hii inaweza kuwazuia baadhi ya wale wanaotaka kushiriki.[90]

IV: Sheria za Kenya na za Kimataifa
 

Serikali ya Kenya haina budi, chini ya sheria za kitaifa na zile za kimataifa, kuhakikisha kuwa kuna haki na usawa kwa wana LGBT. Zaidi ya yote, serikali ndiyo mdhamini mkuu wa haki yao ya usalama na ya maisha – haki ambazo, kwa wana LGBT wengi ambao walihojiwa na Human Rights Watch, bado ni ndoto.

Wajibu wa Kenya katika Kutekeleza Haki za Kibinadamu
Katiba ya Kenya, Mkataba wa Afrika kuhusu Haki za Kibinadamu na Watu, na mikataba mingi ya Umoja wa Mataifa ambayo Kenya ni mwanachama, yote inashughulikia ulinzi wa haki muhimu za kibinadamu, bila kujali hisia za kimapenzi au utambulisho wa kijinsia.

Wajibu wa Kutoa Ulinzi chini ya Sheria za Kimataifa
Azimio la kihistoria lililopitishwa mnamo Novemba 2013 na Tume ya Afrika kuhusu Haki za Kibinadamu na Watu, juu ya "Ulinzi dhidi ya Kuvamiwa na Ukiukaji mwingine wa Haki za Kibinadamu unaotekelezwa dhidi ya watu kwa misingi ya Hisia ya kimapenzi au Utambulisho wa kijinsia wa kukisiwa au wa kweli," linalaani dhuluma na mashambulizi ya kupangwa yanayotekelezwa kwa misingi ya hisia ya kimapenzi na utambulisho wa kijinsia.[91] Azimio hilo linatoa wito kwa nchi wanachama kufanya yafuatayo:

Kumaliza vitendo vyote vya hujuma na unyanyasaji, iwe vinavyofanywa na wahusika serikalini au wale wasio serikalini, ikiwa ni pamoja na kutunga na kutekeleza barabara sheria mwafaka za kuzuia na kuadhibu aina zote za dhuluma ikiwa ni pamoja na zile zinazowalenga watu kwa misingi ya hisia ya kimapenzi au utambulisho wa kijinsia wa kukisiwa au wa kweli, kuhakikisha uchunguzi mwafaka na kuwashtaki vilivyo wakosaji, na kuanzisha taratibu za mahakama zinazowiana na mahitaji ya waathiriwa.[92]

Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa (The International Covenant on Civil and Political Rights, ICCPR) pia unailazimisha Kenya, ambalo ni taifa mwanachama, kuwalinda watu ndani ya mipaka au mamlaka yake, ikiwa ni pamoja na wanachama wa makundi yaliyotengwa, dhidi ya dhuluma, kwa kuunga mkono haki zao ya kuishi, usalama na kuwa huru kutokana na kudhulumiwa au kudhalilishwa. Mkataba huo unayapa mataifa wajibu wa kuchunguza na kuwafungulia mashtaka watekelezaji wa dhuluma, wawe ni wahusika kutoka serikalini au nje ya serikali.[93]

Ili kutekeleza azimio la Tume ya Afrika sawia na majukumu yake kama yalivyobainishwa chini ya ICCPR, Kenya inapaswa kuchukua hatua za kuzuia kabisa na kuwaadhibu watekelezaji wa mashambulizi hayo kila wakati. Kenya pia inapaswa kuwajibika kwa kuwalazimisha maafisa wa polisi wanaokataa kuchukua taarifa kutoka kwa waathiriwa wa uhalifu kwa misingi ya utambulisho wao wa kijinsia au hisia yao ya kimapenzi kuwajibika.

Usawa na Kutobaguliwa chini ya Sheria za Kimataifa
Mkataba wa Afrika kuhusu Haki za Kibinadamu na Watu, na Mkataba wa Kimataifa kuhusu Haki za Kiraia na Kisiasa yote inaitaka Kenya kuwahakikisha haki ya usawa na kutobaguliwa mbele ya sheria. Tume ya Afrika ya Haki za Kibinadamu na Watu hasa imeweka wazi kuwa ubaguzi kwa misingi ya hisia ya kimapenzi unakwenda kinyume na vigezo dhidi ya ubaguzi kwenye Mkataba huo.[94]

Faragha chini ya Sheria za Kimataifa
Kuharamishwa kwa mapenzi ya jinsia moja kati ya watu wazima waliokubaliana kunakiuka haki ya faragha, iliyotolewa chini ya ICCPR.[95] Kumkamata mtu kwa misingi ya kufanya mapenzi ya jinsia moja kwa hiari pia ni ukiukaji wa kanuni inayokataza kuzuiliwa kiholela.[96]
 

Human Rights Watch linaamini kuwa kuharamishwa kwa ubadilishanaji wa huduma za ngono kwa sababu za kibiashara kati ya watu wazima waliokubaliana, kama katika biashara ya ngono, pia inakiuka haki ya faragha, ikiwa ni pamoja na uhuru wa kujitawala mambo.[97]

Marufuku dhidi ya Uchunguzi wa Lazima wa Mkundu
Tendo la kufanya uchunguzi wa lazima wa mkundu kama njia ya “kuthibitisha” ngono kati ya wanaume unakiuka sheria za haki za kibinadamu, na Kenya inapaswa kuupiga marufuku kabisa uchunguzi huo. Kamati ya Umoja wa Mataifa dhidi ya Mateso imegundua kwamba uchunguzi wa mkundu unaweza kujumuishwa kama tabia ya udhalilishaji, iliyopigwa marufuku na Mkataba dhidi ya Mateso (Convention against Torture, CAT) na Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa (ICCPR).[98] Sheria ya Kenya haijapiga marufuku waziwazi uchunguzi wa lazima wa mkundu, lakini katiba inapiga marufuku ukatili, unyama, na udhalilishaji.[99] Sheria inatoa nafasi ya ukusanyaji wa sampuli za kimatibabu kwa ajili ya upimaji na mahakama kwa kufanya uchunguzi kutoka kwa watuhumiwa walioshtakiwa kwa makosa chini ya Sheria ya Uhalifu wa Kijinsia (Sexual Offences Act), lakini sheria hiyo haipigi marufuku mapenzi ya jinsia moja kwa hiari.[100] Tume ya Kitaifa kuhusu Haki za Mashoga na Wasagaji (The National Gay and Lesbian Human Rights Commission, NGLHRC) inaandaa kesi ya kikatiba dhidi ya matumizi ya uchunguzi wa mkundu katika kesi ya Kwale.[101]

Mnamo mwaka wa 2011, Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Kibinadamu ilisema ifuatavyo:

Suala moja lililodhihirishwa na wataalam wa Umoja wa Mataifa ni tabia "isiyo na maana kimatibabu" ya kuwalazimisha wanaume watuhumiwa wa mapenzi ya jinsia moja kufanyiwa uchunguzi wa mkundu bila idhini yao "kuthibitisha" kushiriki ngono na wanaume wenzao. Uchunguzi kama huo umelaaniwa na Kamati dhidi ya Mateso, Katibu Maalum wa Mateso (the Special Rapporteur on Torture) na Kamati ya Kuchunguza Uzuiliaji wa Kiholela (Working Group on Arbitrary Detention) ambazo zimeshikilia kwamba zoezi hilo linakwenda kinyume na marufuku dhidi ya mateso na ukatili.[102]

Haki ya Kupata Matibabu ya Kiwango cha Juu Iwezekanavyo

Haki ya kupata huduma bora za matibabu imehakikishwa chini ya Mkataba wa Afrika kuhusu Haki za Kibinadamu na Watu, Mkataba wa Kimataifa kuhusu Haki za Kiuchumi, Kijamii na Kitamaduni (International Covenant on Economic, Social and Cultural Rights), na Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Kutokomeza Aina zote za Ubaguzi dhidi ya Wanawake (UN Convention on the Elimination of all Forms of Discrimination against Women).[103] Serikali haziwezi kubagua kwa misingi ya hisia ya kimapenzi au utambulisho wa kijinsia katika kutekeleza haki ya matibabu.[104]


Haki hii inalazimisha mataifa kuchukua hatua zinazohitajika kwa ajili ya kuzuia, kutibu na kudhibiti maambukizi ya virusi vya ukimwi na magonjwa mengine. Kamati ya Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Kiuchumi, Kijamii, na Kitamaduni ilipata kuwa haki ya afya inahusiana na haki zingine, kama haki za "faragha, upatikanaji wa habari, na uhuru wa mahusiano, kujumuika, na kusafiri popote" – haki ambazo huwa hatarini wakati wa mashambulizi au vitisho vya mashambulizi, kama ilivyorekodiwa katika ripoti hii, huwazuia wahudumu wa afya, wanaharakati wa LGBT, na wengine dhidi ya kujumuika ili kubadilishana taarifa kuhusu VVU na afya ya ujinsia.[105] Haki ya afya hasa inahusisha "upatikanaji wa habari kuhusu elimu ya kiafya, ikiwa ni pamoja na afya ya ngono."[106]

Haki ya Makazi
Kenya ni nchi mwanachama wa Mkataba wa Kimataifa kuhusu Haki za Kiuchumi, Kijamii na Kitamaduni (ICESCR), ambao unahitaji mataifa kutekeleza hatua kwa hatua "haki ya kila mtu kumudu gharama ya maisha yake mwenyewe na jamaa yake, na kupata chakula cha kutosha, mavazi na makazi, na pamoja na kuendelea kuboresha hali ya maisha."[107] Katibu Maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu makazi yanayofaa kama sehemu ya haki ya kuishi maisha bora, na pamoja na haki ya kutobaguliwa katika hali hii, ametoa wito kwa mataifa kutoa ulinzi dhidi ya ukiukaji wa haki za kibinadamu unaofanywa na watu wengine, kama vile ubaguzi na kufurushwa, ambayo huchangia ukiukaji wa haki ya makazi kwa makundi yaliyotengwa, kwa mfano wana LGBT.[108]

Haki za Kikatiba nchini Kenya

Idadi kubwa ya haki ambazo zinalindwa na sheria za kimataifa zimehakikishwa pia katika katiba ya Kenya iliyopiganiwa kwa muda mrefu na kupitishwa mnamo Agosti 2010, ambayo ina muswada thabiti kuhusu sheria ya haki za kibinadamu. Katiba inalinda haki ya usawa na kutobaguliwa (kipengee cha 27) na haki ya kupewa utu (kipengee cha 28). Inalinda haki ya uhuru na usalama wa mtu (kipengee cha 29), ambayo inajumuisha haki ya kutokamatwa kiholela na haki ya "kutokakabiliwa na aina yoyote ya shambulizi kutoka kwa umma au watu binafsi." Inatoa hakikisho la haki ya faragha (kipengee cha 31), uhuru wa kujieleza (kipengee cha 33), uhuru wa kujumuika (kipengee cha 36), na haki ya makazi (kipengee cha 43. (1) (b)), na inatoa ulinzi maalum kwa "makundi ya walio wachache na waliotengwa" (kipengee cha 56).[109] Katiba ya Kenya pia inaharamisha mateso na ukatili, unyama au udhalilishaji (kipengee cha 29 (f)).[110]

Aidha, kipengee cha 2 (5) na 2 (6) cha katiba vinajumuisha sheria za kimataifa na mikataba yote ya kimataifa iliyoidhinishwa na Kenya kama sehemu ya sheria za nchi. [111] Hii inajumuisha mikataba ya Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika iliyoidhinishwa na Kenya kuhusu haki za kibinadamu.

Aprili 2015 Mahakama Kuu iliamua juu ya ombi lililowasilishwa na NGLHRC hatua iliyoonyesha kuwa hakuna shaka kwamba haki za kimsingi zilizolindwa na katiba yanawahusu Wakenya wote, bila kujali hisia zao za kimapenzi au utambulisho wao wa kijinsia.
[112]

Majukumu ya Kenya chini ya Mchakato wa UPR
Wakati wa Mfumo wa Kimataifa wa Mapitio ya Haki za Binadamu (UPR) katika Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa kule Geneva mnamo Januari 2015, serikali ya Kenya ilikataa mapendekezo kadhaa ya kuhalalisha mapenzi ya jinsia moja. Hata hivyo, ilikubali mapendekezo mawili ambayo huenda yakachangia pakubwa kuboresha utekelezaji wa haki za kibinadamu za wana LGBT. Haya yalijumuisha: "kubadilisha Sheria yake ya Adhabu ili kuifanya iwiane na katiba,"[113] na "kutunga sheria ya kupambana kwa kina na ubaguzi na hivyo kutoa ulinzi kwa watu wote, bila kujali hisia yao ya kimapenzi au utambulisho wao wa kijinsia."[114] Kwa sababu katiba ya Kenya inahakikisha haki ya faragha na haki ya kutobaguliwa, uhakiki mwafaka wa Sheria ya Adhabu ungeweza kubainisha kwamba sehemu 162, 163, na 165, ambazo zinaharamisha mapenzi kwa hiari kati ya watu wazima wa jinsia moja, zinakwenda kinyume na katiba.[115]
 

Hata bila kuhalalisha mapenzi ya jinsia moja, sheria ya kina na mwafaka dhidi ya ubaguzi itakuwa ni hatua nzuri ya kuchangia hakikisho kuwa waathirika wa dhuluma ambao ni wana LGBT wanaweza kuripoti hujuma bila kukabiliwa na ubaguzi. Waliokamatwa kiholela, kufurushwa kinyume na sheria, ubaguzi katika sekta ya huduma za afya, na visa vingine vya unyanyasaji vilivyorekodiwa katika ripoti hii, vitapata pia suluhisho la kisheria.

Bettina, mwanamke aliobadilisha jinsia yake jijini Mombasa ambaye vilevile amekabiliwa na ghasia kutoka kwa majirani na ubaguzi wa polisi, alisema:

Serikali inapaswa kuelewa kwamba kuna wana LGBT nchini Kenya na kuwa wazi kuhusu suala hilo. Hatua hii pia itawezesha jamii kuwa wazi na yenye kustahimili zaidi watu tofauti. Jamii hutumia sheria za kitaifa na zile sheria ndogo zilizopo za maeneo kuchukua mwenendo wa kutovumiliana kutoka serikalini [kama sababu] ya kutunyanyasa, na kuendeleza ubaguzi [dhidi] yetu.[116]

Maafisa wa serikali, katika ngazi ya kitaifa na za kaunti, watafanya vizuri kuuitikia ushauri wake Bettina, la sivyo, orodha ya visa vya dhuluma dhidi ya wana LGBT itaendelea kuwa ndefu zaidi.

 

[1] Ripoti hii ni tafsiri fupi ya ile ndefu zaidi. Ripoti Kamilifu katika Kiingereza inapatikana kwenye mtandao kwa www.hrw.org.

[2] “Gay rights ‘non-issue,’ says Kenytta,” AFP, Julai 21, 2015, http://www.iol.co.za/news/africa/gay-rights-non-issue-says-kenyatta-1.1888414#.Vbd3M6Sqqko (Iliangaliwa Julai 28, 2015).

[3] Mahojiano kati ya Human Rights Watch na wanaharakti wa haki za wana LGBT, Nairobi, August 3, 2015.

[4] Elkana Jacob, “Two gay men arrested in Kwale as Police hunt for suspects behind Diani child porn videos,” The Star, Februari 19, 2015, http://www.the-star.co.ke/news/2015/02/19/two-gay-men-arrested-in-kwale-as-police-hunt-for-suspects-behind-diani_c1088086 (Iliangaliwa Juni 9, 2015).

[5] Mahojiano ya Human Rights Watch, Mombasa, Agosti 5 na 6, 2015.

[6] Sheria za Kenya, Sheria ya Uhalifu wa Kijinsia, Na. 3 ya mwaka 2006, ibara. 16; Mkataba wa Haki za Watoto (CRC), uliopitishwa Novemba 20, 1989, GA Res. 44/25, kiambatisho, 44 cha Umoja wa Mataifa GAOR Supp (Na. 49) katika stakabadhi ya 167 Umoja wa Mataifa A / 44/49 (1989), aliyoanza kutekelezwa Septemba 2, 1990, kwa mujibu wa ibara 49, iliyoidhinishwa na Kenya mwaka 1990, ibara. 34 (c).

[7] Majina yamebadilishwa kulinda siri za waathirika.

[8] Mahojiano ya simu kati ya Human Rights Watch na Adam, Julai 13, 2015.

[9] Mahojiano ya simu kati ya Human Rights Watch na Tony, Machi 29, 2015.

[10] Mahojiano ya simu kati ya Human Rights Watch na Charles, Mei 7, 2015.

[11] Keshatajwa, na mahojiano ya simu kati ya Human Rights Watch na Esther Adhiambo, PEMA Kenya, Julai 10, 2015.

[12] Ingawa mashtaka dhidi ya wanaume wawili yamo kwenye rekodi ya umma, wana matumaini ya kurejesha kiasi fulani cha faragha yao wakati kesi dhidi yao itakapofungwa na hivyo majina yaliyotumika hapa ni bandia.

[13] Mahojiano ya simu kati ya Human Rights Watch na Bryan, Mei 26, 2015, na Adam, Julai 13, 2015.

[14] Sheria za Kenya, Sura. 63, Sheria ya Adhabu. Kipengele cha 181 inasema, "(1) Mtu yeyote ambaye - (a) kwa lengo la au kwa njia ya biashara au kwa madhumuni ya usambazaji au maonyesho kwa umma, huunda, kuzalisha au anamiliki matini moja au zaidi za kiponografia kati ya michoro, machapisho, michoro ya rangi, picha, mabango, nembo, filamu za sinema au vifaa vingine vyovyote vya kiponografia, au kitu kingine chochote kinachopotosha maadili; ... ana kosa dogo na anastahili kifungo cha jela cha miaka miwili au faini ya shilingi elfu saba."

[15] Polisi wa Kenya, Karatasi ya Mashtaka, O.B. 54/18/02/15, kwenye faili la Human Rights Watch.

[16] Mahojiano ya Human Rights Watch, Mombasa, Agosti 5 na 6, 2015.

[17] Mahojiano ya simu kati ya Human Rights Watch na Bryan, Mei 26, 2015.

[18] Mahojiano ya simu kati ya Human Rights Watch na Adam, Julai 13, 2015.

[19] Mahojiano ya simu kati ya Human Rights Watch na Christine Njagi, Kwale, Agosti 7, 2015.

[20] Keshatajwa; “Arrested Diani gays to remain in police custody,” News24Kenya, http://m.news24.com/kenya/MyNews24/Arrested-Diani-gays-to-remain-in-police-custody-20150220 (Iliangaliwa Julai 13 2014).

[21] 19 Kamati ya Umoja wa Mataifa dhidi ya Mateso, katika tathmini yake ya Misri ya mwaka 2002, ilichunguza suala la uchunguzi wa jinai na mikundu, ikatoa wito kwa serikali "kuzuia vitendo vyote vya udhalilishaji wakati wa upekuzi wa mwili." Kamati dhidi ya Mateso, “Consideration of Reports Submitted by States Parties Under Article 19 of the Convention: Conclusions and recommendations of the Committee against Torture, Egypt,” CAT / C / CR / 29/4, Desemba 23, 2002.

[22] Fomu ya Huduma kwa waathirika wa Ubakaji (muathirika wa kwanza), Februari 24, 2015, iliyosainiwa na Kalai S.M. (afisa wa kuchunguza) na Salim Yunus (afisa wa polisi), kwenye faili ya Human Rights Watch.

[23] Keshatajwa.

[24] Mahojiano kati ya Human Rights Watch na Dkt. Stephen Kalai, Mombasa, Agosti 7, 2015.

[25] Mahojiano ya simu kati ya Human Rights Watch na Esther Adhiambo, PEMA Kenya, Julai 10, 2015.

[26] Mahojiano ya simu kati ya Human Rights Watch na Adam, Julai 13, 2015.

[27] Mahojiano ya simu kati ya Human Rights Watch na Tony, Machi 29, 2015.

[28] Mahojiano ya simu kati ya Human Rights Watch na Charles, Machi 30, 2015.

[29] Mahojiano ya simu kati ya Human Rights Watch na Charles, Mei 7, 2015.

[30] Mahojiano kati ya Human Rights Watch na Francis, Mombasa, Machi 26, 2015.

[31] Keshatajwa.

[32] Mahojiano kati ya Human Rights Watch na Leonard, Mombasa, Machi 26, 2015.

[33] Mahojiano kati ya Human Rights Watch na Evans Gichuru, Mombasa, Machi 26, 2015.

[34] Mahojiano ya simu kati ya Human Rights Watch na Hamil, Machi 29, 2015.

[35] Mahojiano ya simu kati ya Human Rights Watch na Douglas Masinde, Tamba Pwani, Mei 11, 2015.

[36] Mtafiti wa Human Rights Watch lilitazama makala ya awali kwenye tovuti ya Standard mnamo Februari 25, 2015, katika kiungo http://www.standardmedia.co.ke/thecounties/article/2000152821/suspected-gays-attacked-for-lewd-acts-at-colleague-s-funeral?pageNo=1. Kiungo baadaye kiliondolewa. Makala imechapishwa, bila kusifia Standard, kwenye tovuti ya Out and Proud Diamond Group katika http://www.opdg.org/index.php/11-latest-news/130-suspected-gays-attacked-for-lewd-acts-at-colleague-s-funeral (iliangaliwa Mei 20, 2015).

[37] Mahojiano ya simu kati ya Human Rights Watch na Samir, Mei 14, 2015.

[38] Mahojiano ya simu kati ya Human Rights Watch na Bettina, Mei 3, 2015.

[39] Keshatajwa.

[40] Mahojiano kati ya Human Rights Watch na Bettina, Mombasa, Machi 27, 2015.

[41] Daniel Nyassy, “Gays flee as irate residents storm Likoni seminar,” Africa Review, Februari 24, 2012. http://www.africareview.com/News/Gays+flee+as+irate+residents+storm+Likoni+seminar+/-/979180/1334234/-/a7k5ovz/-/index.html (Iliangaliwa Mei 20, 2015). Angalia pia NTV Kenya, "Mkutano wa mashoga na wasagaji watibuka Mjini Mombasa," Februari 23, 2012, https://www.youtube.com/watch?v=dcGSnWbeY6k&feature=youtu.be (iliangaliwa Juni 9, 2015), kwa video ya mashambulizi.

[42] Esther Adhiambo, “A Report PEMA Kenya on the MSM Attacks in Likoni,” Februari 24, 2012, kwenye faili ya Human Rights Watch.

[43] Shirika la Kitaifa ya Kudhibiti Maambukizi ya UKIMWI & Magonjwa ya Zinaa (NASCOP), KenyaKenya Sex Workers Alliance (KESWA), Muungano wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali yanayopambana na UKIMWI nchini Kenya (KANCO), Mtandao wa Taifa wa Kutoa Uwezo kwa Watu Wanaoishi na VVU/UKIMWI nchini Kenya (NEPHAK), na Jarida la Identity Kenya, "“Joint Press Release: Likoni Attack on MSM Training,” Februari 29, 2012, kwenye faili ya Human Rights Watch.

[44] Adhiambo, “A Report PEMA Kenya on the MSM Attacks in Likoni,” Februari 24, 2012.

[45] Nyassy, “Gays flee as irate residents storm Likoni seminar,” keshatajwa awali.

[46] Keshatajwa.

[47] Askofu Lawrence Chai wa Kanisa la Free Kenya Apostolic Church katika Mtwapa aliliambia Human Rights Watch mnamo mwaka wa 2014 kwamba alikuwa miongoni mwa wale ambao walisambaza uvumi kuhusu "ndoa kati ya makuchu." Mahojiano ya Human Rights Watch, Mombasa, Januari 17, 2014.

[48] Galgalo Bocha, “Gay wedding here? No way, vow preachers,” Daily Nation, Februari 11, 2012, http://humanrightshouse.org/noop/page.php?p=Articles/13392.html&d=1 (Iliangaliwa Mei 20, 2015).

[49] Human Rights Watch, "Kenya: Halt Anti-Gay Campaign,” Februari 18, 2010, http://www.hrw.org/news/2010/02/17/kenya-halt-anti-gay-campaign.

[50] Mahojiano kati ya Human Rights Watch na Kalisa, Mombasa, Januari 14, 2014.

[51] Mahojiano kati ya Human Rights Watch na Richard, Kilifi, Januari 21, 2014.

[52] Mahojiano kati ya Human Rights Watch na Bettina, Mombasa, Januari 13, 2014.

[53] Mahojiano kati ya Human Rights Watch na Kalisa, Mombasa, Januari 14, 2014

[54] Keshatajwa.

[55] Mahojiano kati ya Human Rights Watch na Richard, Kilifi, Januari 21, 2014.

[56] Tume ya Haki za Binadamu Kenya (KHRC), The Outlawed Among Us, uk. 31, tanbihi 45.

[57] Gay and Lesbian Coalition of Kenya, “Kenya: Gay and Lesbian Coalition of Kenya Condemns Closure of Centre in Malindi,” Juni 27, 2008, http://iglhrc.org/content/kenya-gay-and-lesbian-coalition-kenya-condemns-closure-centre-malindi (Iliangaliwa Mei 20, 2015).

[58] Mahojiano ya simu kati ya Human Rights Watch na Nzioki King'ola, ICRH-Kenya, Mei 19, 2015.

[59] Mahojiano ya simu kati ya Human Rights Watch na Evans Gichuru, Mei 25, 2015.

[60] Keshatajwa.

[61] Mahojiano ya simu kati ya Human Rights Watch na Ishmael, Mombasa, Machi 25, 2015.

[62] Human Rights Watch na Tume ya Haki za Binadamu Kenya (KHRC), Insult to Injury: The 2014 Lamu and Tana River Attacks and Kenya’s Abusive Response, Juni 15, 2015, http://www.hrw.org/report/2015/06/15/insult-injury/2014-lamu-and-tana-river-attacks-and-kenyas-abusive-response; Human Rights Watch, "We Were Sent to Kill You"Gang Attacks in Western Kenya and the Government’s Failed Response, Aprili 24, 2014, http://www.hrw.org/report/2014/04/24/we-were-sent-kill-you/gang-attacks-western-kenya-and-governments-failed-response.

[63] Mahojiano kati ya Human Rights Watch na Charles, Mombasa, Machi 15, 2012.

[64] Human Rights Watch na Tume ya Haki za Binadamu Kenya (KHRC), Insult to Injury: The 2014 Lamu and Tana River Attacks and Kenya’s Abusive Response, keshatajwa awali; Human Rights Watch, "You Are All Terrorists" Kenyan Police Abuse of Refugees in Nairobi, Mei 29, 2013, http://www.hrw.org/report/2013/05/29/you-are-all-terrorists/kenyan-police-abuse-refugees-nairobi; Criminal Reprisals: Kenyan Police and Military Abuses against Ethnic Somalis, Mei 4, 2012, https://www.hrw.org/report/2012/05/04/criminal-reprisals/kenyan-police-and-military-abuses-against-ethnic-somalis; "Bring the Gun or You’ll Die" Torture, Rape, and Other Serious Human Rights Violations by Kenyan Security Forces in the Mandera Triangle, Juni 29, 2009, https://www.hrw.org/report/2009/06/29/bring-gun-or-youll-die/torture-rape-and-other-serious-human-rights-violations; Amnesty International, “We are Like Rubbish in This Country”: Forced Evictions in Nairobi, Kenya, Oktoba 7, 2013, https://www.amnesty.org/en/documents/AFR32/005/2013/en/.

[65] Kwa mujibu wa takwimu za Benki ya Dunia, ukosefu wa kijumla wa ajira kwa vijana nchini Kenya – kwa kurejelea nguvukazi katika kundi la umri wa miaka 15-24 wasio na kazi lakini ambao wanatafuta ajira – ni asilimia 17, huku shirika la wachanganuzi la Adam Smith International linakadiria ukosefu wa ajira kwa vijana mjini Mombasa kuwa asilimia 44. Takwimu za Benki ya Dunia, “Unemployment, youth total (percent of total labor force ages 15-24) (modeled ILO estimate),” haina tarehe, http://data.worldbank.org/indicator/SL.UEM.1524.ZS (iliangaliwa Julai 30, 2105); Adam Smith International, “Creating employment opportunities for young people in Mombasa,” haina tarehe, http://www.adamsmithinternational.com/explore-our-work/east-africa/kenya/mombasa-county-youth-employment-programme (Iliangaliwa Julai 30, 2015).

[66] Vijana wengi waliliambia Human Rights Watch kuwa walifutwa kazi au kutoajiriwa kutokana na makisio ya hisia yao ya kimapenzi. Mahojiano kati ya Human Rights Watch na Samir, Mombasa, Januari 13, 2014; Haroun, Diani, Januari 18, 2014; Morris, Diani, Januari 18, 2014.

[67] Sheria ya Uhalifu wa Kijinsia, ibara. 3.

[68] Mahojiano kati ya Human Rights Watch na Daudi, Mombasa, Januari 13, 2014.

[69] Mahojiano ya simu kati ya Human Rights Watch na Guyo, Juni 25, 2015.

[70] FIDA Kenya, Documenting Human Rights Violations of Sex Workers in Kenya, 2008, http://www.opensocietyfoundations.org/sites/default/files/fida_20081201.pdf (iliangaliwa Mei 20, 2015); Kenya Sex Worker Alliance (KESWA), mahojiano ambayo hayajachapishwa yaliyofanywa mwaka wa 2015, kwenye faili ya Human Rights Watch.

[71] Mahojiano kati ya Human Rights Watch na Ishmael, Mombasa, Machi 25, 2015.

[72] “The Value of a Life,” toleo la habari za GALCK, Julai 17, 2013, http://76crimes.com/2013/07/18/kenya-making-progress-but-anti-gay-violence-continues/ (iliangaliwa Aprili 9, 2015). Kwa mujibu wa GALCK, kipindi cha majadiliano kwenye kituo cha redio mjini Mombasa kilipokea simu za wakazi mnamo Juni 23 na 24 ambao walisema kuwa walikuwa katika safari ya "kusafisha" Mombasa kwa kuwaondoa wanaume wote wanaofanya biashara ya ngono.

[73] Mahojiano ya simu kati ya Human Rights Watch na Jo, Juni 26, 2015.

[74] “The Value of a Life,” toleo la habari za GALCK.

[75] Katika kisa kingine kinachojulikana cha mauaji ya mwana LGBT katika pwani, mnamo Machi 23, 2012, kuchu mmoja aliyeitwa Jimmy, ambaye alifanya kazi kama mwelimishaji rika wa Tamba Pwani, alipigwa hadi kufa huko Malindi. Jamaa za Jimmy waliliambia shirika la Tamba Pwani kwamba Jimmy alipokea simu usiku, akaenda nje kukutana na mtu fulani, na hakurudi kamwe. Jirani aliupata mwili wake katika eneo wazi karibu na nyumbani kwake. Afisa mmoja wa Tamba Pwani alirekodi taarifa kwa polisi na aliwaambia kuwa yeye alishuku kuwa Jimmy aliuawa katika shambulizi la hasama dhidi ya makuchu, lakini akasema kuwa polisi hawakufanya uchunguzi kamwe. Mahojiano ya simu kati ya Human Rights Watch na afisa wa Tamba Pwani (jina limewekwa siri), Mei 11, 2015.

[76] Mahojiano kati ya Human Rights Watch na Samir, Januari 13, 2014, Mombasa, na mahojiano ya simu, Mei 14, 2015.

[77] Mahojiano kati ya Human Rights Watch na Bettina, Mombasa, Januari 14, 2014.

[78] Mahojiano kati ya Human Rights Watch na Douglas Masinde, Kilifi, Machi 24, 2015.

[79] Mahojiano kati ya Human Rights Watch na Patrick, Mombasa, Machi 26, 2015.

[80] Mahojiano kati ya Human Rights Watch na Ahmed, Diani, Januari 18, 2014.

[81] Mahojiano kati ya Human Rights Watch na Daudi, Mombasa, Januari 13, 2014.

[82] Mahojiano kati ya Human Rights Watch na Charles, Mombasa, Machi 15, 2012.

[83] Shirika la Umoja wa Mataifa la Kupambana na UKIMWI (UNAIDS), “Guidance Note 2012: Key Programmes to Reduce Stigma and Discrimination and Increase Access to Justice in National HIV Responses,” uk.5, http://www.unaids.org/en/media/unaids/contentassets/documents/document/2012/Key_Human_Rights_Programmes_en_May2012.pdf (iliangaliwa Mei 31, 2013; tafsiti kutoka kiingereza ilifanywa na Human Rights Watch). Tazama pia Benki ya Dunia, “Increased Targeting of Key Populations Can Accelerate End of Global HIV Epidemic,” Novemba 28, 2012, http://www.worldbank.org/en/news/press-release/2012/11/28/increased-targeting-key-populations-can-accelerate-end-global-hiv-epidemic (iliangaliwa Mei 31, 2013).

[84] Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Ukimwi (UNAIDS), “The Gap Report 2014: Gay men and other men who have sex with men,” http://www.unaids.org/sites/default/files/media_asset/07_Gaymenandothermenwhohavesexwithmen.pdf (iliangaliwa Juni 22, 2015). UNAIDS pia lina taarifa kwamba "unyanyapaa, ubaguzi, na dhuluma za kijinsia na kingono, na ukosefu wa kutambuliwa kisheria kwa jinsia wanazoshikilia, na kutengwa kijamii na kiuchumi, ikiwa ni pamoja na kutokana na nafasi katika elimu na ajira, huwakilisha vichochezi vya kimsingi vya VVU vinavyowafanya wanawake waliobadilisha jinsia zao kuwa katika hatari zaid kote ulimwenguni." UNAIDS, “The Gap Report 2014: Transgender people,” http://www.unaids.org/sites/default/files/media_asset/08_Transgenderpeople.pdf (iliangaliwa Juni 22, 2015).

[85] Mwongozo wa Mikakati dhidi ya UKIMWI nchini Kenya (KASF), 2014 / 2015-2018 / 2019, http://www.nacc.or.ke/images/KASF_F_web.compressed.pdf, uk.8. Mambo yaliyochangia kiwango cha juu cha maambukizi ya VVU miongoni mwa MSM ikilinganishwa na watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia tofauti ni ya kibayolojia (ngono ya mkundu ina hatari kubwa ya maambukizi kuliko ngono ya ukeni) na ya kijamii (ubaguzi wa kisheria na kijamii dhidi ya MSM hufanya iwe vigumu kwao kupata huduma za kinga na matibabu).

[86] KASF 2014/2015-2018 /2019, uk. 15.

[87] Keshatajwa.

[88] Mahojiano ya simu kati ya Human Rights Watch na Nzioki King'ola, ICRH-Kenya, Mei 19, 2015.

[89] Mahojiano kati ya Human Rights Watch na Parinita Bhatacharjee, Mshauri Mkuu wa Kiufundi, Chuo Kikuu cha Manitoba, Nairobi, Aprili 30, 2015.

[90] Mahojiano kati ya Human Rights Watch na Eduard Sanders, KEMRI, Kilifi, Machi 31, 2015.

[91] Tume inaweza kufuatilia kama nchi wanachama zinazingatia maazimio, lakini haina mamlaka ya utekelezaji.

[92] Azimio la 275 la ACHPR, “Protection against Violence and other Human Rights Violations against Persons on the basis of their real or imputed Sexual Orientation or Gender Identity,” http://www.achpr.org/sessions/55th/resolutions/275/ (iliangaliwa Mei 21, 2015; tafsiri kutoka kiingereza ilifanywa na Human Rights Watch).

[93] Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa (ICCPR), uliopitishwa Desemba 16, 1966, GA Res. 2200A (XXI), 21 U.N. GAOR Supp. (Na. 16) katika stakabadhi ya Umoja wa Mataifa ya 52, A / 6316 (1966), 999 U.N.T.S. 171, ulioanza kutekelezwa Machi 23, 1976, ulioidhinishwa na Kenya Machi 23, 1976, ibara. 2,7,17.

[94] Mkataba wa Afrika [Banjul] kuhusu Haki za Kibinadamu na Watu, uliopitishwa Juni 27 1981, stakabadhi ya Shirika la Umoja wa nchi Huru za Kiafrika (OAU) CAB/LEG/67/3 rev.5, 21I.L.M. 58 (1982), ulioanza kutekelezwa Oktoba 21, 1986, ulioidhinishwa na Kenya mnamo Januari 23, 1992, ibara. 2. Tazama Tume ya Afrika ya Haki za Kibinadamu na Watu, Zimbabwe Human Rights NGO Forum v. Zimbabwe, kipengele cha 169, AHRLR 128 (ACHPR 2006).

[95] ICCPR, ibara. 17. Tazama pia Toonen v. Australia, awamu ya 50, Mawasiliano Na.488/1992, Stakabadhi ya Umoja wa Mataifa CCPR / C / 50 / D / 488/1992, Aprili 14, 1994, kipengele 8.7.

[96] Tazama François Ayissi na wengine. v. Cameroon, Kamati Tendakazi kuhusu Kuzuiliwa Kiholela (Working Group on Arbitrary Detention), Maoni Na. 22/2006, Stakabadhi ya Umoja wa Mataifa A / HRC / 4/40 / Add.1 katika 91 (2006), kwenye faili ya Human Rights Watch.

[97] ICCPR, ibara ya 17.

[98] Tazama tanbihi 17.

[99] Katiba ya Kenya, ibara ya 25.

[100] "Pale ambapo mtu ameshtakiwa kwa kutenda kosa chini ya Sheria hii, mahakama inaweza kuamuru kwamba sampuli mwafaka ichukuliwe au zichukuliwe kutoka kwa mshtakiwa, katika mahali au chini ya masharti ambayo mahakama inaweza kuamuru kwa lengo la uchunguzi wa jinai au tafiti nyingine za kisayansi, ikiwa ni pamoja na vipimo vya DNA, ili kukusanya ushahidi na kujua ikiwa mshtakiwa alitenda kosa au la." Sheria ya Uhalifu wa Kijinsia, ibara ya 36.

[101] Mahojiano ya simu kati ya Human Rights Watch na Eric Gitari, Julai 13, 2015.

[102] Kamishna wa Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Kibinadamu, “Discriminatory laws and practices and acts of violence against individuals based on their sexual orientation and gender identity,” Novemba 17, 2011, A / HRC / 19/41, http://www2.ohchr.org/Kiingereza/miili/hrcouncil/docs/19session/A.HRC.19.41_English.pdf, aya ya 37. (Tafsiri kutoka kiingereza imefanywa na Human Rights Watch.)

[103] Mkataba wa Afrika [Banjul] kuhusu Haki za Kibinadamu na Watu, keshatajwa awali, ibara ya 16; Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiuchumi, Kijamii na Kiutamaduni (ICESCR), uliopitishwa Desemba 16, 1966, GA Res. 2200A (XXI), 21 Umoja wa Mataifa GAOR Supp. (Na. 16) katika 49, Stakabadhi ya Umoja wa Mataifa A / 6316 (1966), 993 U.N.T.S. 3, ulioanza kutekelezwa Januari 3, 1976, ulioidhinishwa na Kenya tarehe 1 Mei 1972, ibara ya 12; Mkataba wa Kutokomeza Aina zote za Ubaguzi dhidi ya Wanawake (CEDAW), uliopitishwa Desemba 18, 1979, GA Res. 34/180, Stakabadhi ya Umoja wa Mataifa /34/46, ulianza kutekelezwa Septemba 3, 1981 na ulioidhinishwa na Kenya tarehe 9 Machi 1984, ibara ya 12.

[104] Tazama Kamati ya Umoja wa Mataifa kuhusu Uchumi, Jamii na Haki za Utamaduni, Kauli ya Kijumla Na. 20: Kutobaguliwa katika haki za kiuchumi, kijamii na kiutamaduni (ibara ya 2, aya ya 2, ya Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiuchumi, Kijamii na Kitamaduni), Julai 2, 2009, aya ya. 32. Huku ibara ya 12 inahakikisha haki ya afya, ibara ya 2 (2) inawalinda watu binafsi dhidi ya ubaguzi katika utekelezaji wa haki zote zilizotolewa na mkataba. Kauli ya kijumla ya 20 inafafanua kuwa ubaguzi unaotekelezwa kwa misingi ya hisia ya kimapenzi na utambulisho wa kijinsia ni marufuku.

[105] Kamati ya Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Kiuchumi, Kijamii na Kitamaduni, kauli ya kijumla Na. 14 (2000): haki ya kupata huduma bora za afya, aya ya 3.

[106] Keshatajwa, aya ya 11.

[107] Mkataba wa Kimataifa kuhusu Haki za Kiuchumi, Kijamii na Kitamaduni, ibara ya 11.

[108] Baraza la Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Kibinadamu (UNHRC), A / HRC / 25/54 / Add.1, "Report of the Special Rapporteur on adequate housing as a component of the right to an adequate standard of living, and on the right to non-discrimination in this context," Raquel Rolnik, 26 Desemba 2013.

[109] Katiba ya Kenya, 2010.

[110] Keshatajwa.

[111] Keshatajwa.

[112] Eric Gitari v Non- Governmental Organisations Co-ordination Board & 4 others.

[113] UNHRC, "Draft report of the Working Group on the Universal Periodic Review," Januari 26, 2015, https://www.privacyinternational.org/sites/default/files/Report%20A_HRC_WG.6_21_L.7_Kenya%20(1)_0.pdf, aya ya 5.4.

[114] "Draft report of the Working Group on the Universal Periodic Review," aya ya 5.41.

[115] Tazama Eric Gitari v Non- Governmental Organisations Co-ordination Board & 4 others. Mahakama Kuu ilirejelea uamuzi wa Afrika Kusini ambao ulipelekea kuhalalishwa kwa mapenzi ya jinsia moja nchini humo: "Nchini Afrika Kusini, Mahakama ya Kikatiba imeamua kwamba National Coalition for Gay and Lesbian Equality v Minister of Justice 1999 (1) SA 6: [136] 'Taifa linalotambua mienendo tofauti haimaanishi taifa lisilo na maadili au moja lisilo na mwelekeo. Halikomeshi dhana ya sahihi na si sahihi, wala kutazamia ulimwengu usio na wema na uovu. Taifa hilo halina mapendeleo katika kuwashughulikia watu na makundi, lakini sio lisilo na msimamo wa maadili. Katiba bila shaka haizuilii serikali dhidi ya utekelezaji wa maadili. Kwa hakika, Kanuni za Haki si chochote kama si hati iliyotungwa kwa misingi ya maadili ya kina ya kisiasa. Kilicho muhimu katika shughuli na mienendo ya serikali, hata hivyo, ni kwamba matakwa ya kimaadili ambayo inayatekeleza, na kina ambacho utekelezaji huo unaweza kufikia, vinafaa kupatikana katika maandishi na mtazamo wa Katiba yenyewe." (Tafsiri kutoka kiingereza imefanywa na Human Rights Watch.)

[116] Mahojiano kati ya Human Rights Watch na Bettina, Mombasa, Januari 14, 2014.

Region / Country