Skip to main content

(Nairobi, Tarehe 29 Mei, 2013) – Polisi wa Kenya katika jiji la Nairobi waliwatesa, waliwabaka yaani walizikiuka haki za wakimbizi zaidi ya elfu moja pamoja na kuwazuilia kiholela kutoka katikati ya Novemba mwaka wa 2012 hadi karibu na mwisho wa Januari 2013, shirika la Human Rights Watch lilisema katika ripoti yake iliyotolewa leo. Serikali ya Kenya inapaswa kuanzisha mara moja uchunguzi ulio huru na wazi na shirika la Umoja wa Mataifa linalowasimamia wakimbizi(United Nations Refugee Agency) ambalo mpaka sasa halijatoa maoni yake waziwazi kuhusu swala hili vilevile  linapaswa kuweka hati na kutoa ripoti yake wazi kuhusu ukiukaji dhidi ya wakimbizi katika siku za usoni, shirika la Human Rights Watch lilisema.

Ripoti yenye kurasa 68, iitwayo “Nyinyi Nyote ni Magiadi: “Polisi wa Kenya Wakiuka Haki za Wakimbizi Nairobi” iliandikwa baada ya kuwahoji wakimbizi, wanaotafuta  kimbilio na Wakenya wenye asili ya Kisomalia 101. Ripoti inaonyesha jinsi polisi walivyotumia mashambulizi ya mabomu na mashambulizi mengine yaliyotekelezwa na watu wasiojulikana katika mtaa wa Eastleigh ambao wakazi wake wengi ni Wasomali na amri ya serikali ya kuwahamisha wakimbizi kutoka mijini hadi kwenye kambi za wakimbizi kama sababu ya kuwabaka, kuwapiga, kuwanyang’anya pesa na kuwazuilia kiholela zaidi ya watu elfu moja. Polisi waliwaita waathiriwa wao “magaidi” na kuwalazimu kuwapa pesa ili kuwaachilia. Shirika la Human Rights Watch aidha ilirekodi viwango vya juu vya ukiukaji katika kesi 50 ambao unaweza kuchukuliwa kama mateso.

“Wakimbizi walituelezea jinsi kwa muda wiki kumi mamia ya polisi wa Kenya waliwatendea unyama karibu na katikati ya jiji la Nairobi kwa kuwatesa, kukiuka haki zao, na kuwaibia baadhi ya wale walio maskini zaidi na walio katika hali mbaya kabisa,” alisema Gerry Simpson, mwandishi wa ripoti hii na aliye mtafiti mwandamizi katika maswala ya wakimbizi kwenye shirika la Human Rights Watch. “Kuwavamia wanaume, wanawake na watoto ovyovyo katika nyumba zao na barabarani si njia inayofaa hata kidogo kuulinda usalama wa Kenya.”

Mnamo Januari, Mahakama ya Juu ya Kenya iliziamrisha idara mbalimbali za serikali zilizohusika na shughuli hii ya kuwahamisha wakimbizi kuisimamisha kwa muda hadi korti iamue kama ni ya kisheria. Chini ya mpango huu, jumla ya wakimbizi na waliotafuta kimbilio 55,000 watahamishwa kutoka kwenye miji ya Kenya hadi katika kambi zilizochafu, zilizojaa kupita kiasi, na walimofungiwa ndani. Korti inatarajiwa kutoa uamuzi wake katika wiki zijazo baada ya kesi hii kusikilizwa mnamo tarehe 22 Mei.

Wakimbizi kutoka nchi za Somalia na Uhabeshi pamoja na wale wanaotafuta kimbilio waliokuwa wameishi na familia zao kwa miaka mingi katika mtaa wa Eastleigh waliliambia Shirika la Human Rights Watch kuwa polisi waliuvamia mtaa ule kwa fujo  kutoka tarehe 19 Novemba mwaka wa 2012 siku moja baada ya watu wasiojulikana kuilipua matwana moja na kuwaua watu 7 na kuwajeruhi wengine 30. Waliohojiwa walisema kuwa maafisa kutoka vitengo vinne vya polisi ya Kenya kama kile cha kuzima ghasia (General Services Unit), polisi wa kawaida, polisi wa utawala(Administration Police) na kile cha kufanya upelelezi(Criminal Investigation Department) waliwakiku. Kitengo kile cha GSU kilihusishwa na idadi kubwa ya kesi zile zilizoripotiwa.

Wanawake saba walielezea jinsi polisi waliwabaka makwao, kando ya barabara, na kwenye viwanja na vitendo hivi wakati mwingine viliendelea watoto wao wakiwa karibu nao. Mwanamke mmoja aliyebakwa aliongezea kuwa polisi waliwabaka wanawake wengine watatu pamoja naye. Wakimbizi arubaini wakiwemo wanawake  wengi walielezea walivyopigwa, walivyopigwa teke, walivyopigwa ngumi pamoja na watoto wao wakiwa nyumbani kwao, barabarani, ndani ya magari ya polisi na kujeruhiwa vibaya na kuwa na maumivu kwa muda mrefu. Wengi walisimulia jinsi polisi walivyoingia katika biashara na nyumba zao mara nyingi usiku wa manane na kuwaibia pesa nyingi na vitu vingine vya kibinafsi na kuwalazimu kuwapa pesa ili kuwaachilia.

Human Rights Watch pia iliweka hati ya karibu kesi 1000 kuhusu wakimbizi na waliotafuta kimbilio waliozuiliwa kiholela na polisi katika nyumba zao, barabarani, ndani ya magari ya polisi na katika vituo vya polisi. Hata wakati mwingine polisi waliwazuilia kwa siku nyingi katika mazingira mabaya na ya kudhalilisha wakitisha kuwashtaki bila ushahidi wowote, ama kwa ugaidi au mashtaka ya kuvuruga amani ya umma. Katika kesi moja polisi waliwashtaki karibu watu 100 bila ushahidi na mahakama ikalazimika kuifutilia mbali kesi ile baada ya miezi kwa kukosa ushahidi.

Serikali ya Kenya bado haijajibu ombi la Shirika la Human Rights Watch la kuitaka itoe maoni yake juu ya ripoti ile wala haijatangaza hatua zozote za kuchunguza ukiukaji ule hali ambayo inazidi kuiharibu sifa mbaya ya maafisa wa usalama wanaoivunja sheria bila kujali wala kuchukuliwa hatua zozote za kinidhamu. Kwa miaka mingi maafisa wale wamekuwa wakizikiuka haki za Wakenya wenye asili ya Kisomali na wakimbizi kutoka Somalia katika eneo la Kaskazini Mashariki na kambi kubwa ya wakimbizi ya Dadaab katika mpaka kati ya Kenya na Somalia. Nchi zinazotoa msaada kwa Kenya hazipaswi kutoa msaada wowote kwa vitengo vile vinne vya polisi vilivyohusika na ukiukaji haswa ule wa GSU, Human Rights Watch lilisema.

Kifungu cha kwanza katika Mkataba wa Umoja wa Mataifa dhidi ya Mateso unaoijumuisha Kenya kinafafanua mateso kama “kitendo chochote kinachomsababishia mwengine maumivu makali au taabu, kimwili au kiakili kimakusudi ili kumwadhibu kwa alichokitenda au kilichotendwa na mwengine au kwa mtuhumiwa au kumtisha au kumshurutisha ……. maumivu ama mateso kama hayo yakifanywa na ….... afisa wa umma.”

Polisi kule Eastleigh waliowabaka na kuwaumiza vibaya wakimbizi na waliotafuta kimbilio huku wakiwaita wakimbizi ama kuwanyang’anya pesa waliwaumiza kimakusudi kimwili na kiakili pamoja na kuwatesa kama adhabu kwa mashambulizi yaliyotekelezwa na wengine katika mtaa huo na kuwalazimisha kutoa pesa, shirika la Human Rights Watch lilisema. Mkataba dhidi ya Mateso unailazimisha serikali ya Kenya kuwachunguza mapema na kwa njia ya haki maafisa wa usalama pamoja na makamanda wao waliowatesa wakimbizi na kuwashtaki watakaopatikana na hatia.

“Sheria ya kimataifa inaishurutisha Kenya kuhakikisha kuwa maafisa waliowatesa wakimbizi, waliowabaka wanawake na kuwapiga watoto na wanaume hadi wakapoteza ufahamu wakisema ni wakimbizi wamechunguzwa na kuchukuliwa hatua.”

Jukumu la Shirika la Umoja wa Mataifa Linalowatetea Wakimbizi (UNHCR) la  kuwatetea waathiriwa hadharani ili kukomesha ukiukaji kama huu ni muhimu haswa kwa kuwa serikali haijamchukulia mtu yeyote hatua za kisheria, shirika la Human Rights Watch lilisema. “Shirika la UNHCR limekosa kuweka hati vilivyo na kuongea juu ya ukiukaji huu kwa hivyo linapaswa kuboresha ufuatiliaji wake wa ukiukaji dhidi ya wakimbizi na liweke kumbukumbu na kukashifu waziwazi ukiukaji utakaotokea baadaye.

“Kumekuwa na kimya cha ajabu kutoka kwa UNHCR kuhusu ukiukaji huu ingawa ulifanyika umbali wa nusu saa kwa gari kutoka kwenye afisi zao jijiniNairobi” Simpson alisema. “Kwa muda wa wiki 10 polisi walikuwa huru kubaka, kushambulia na kuwaibia zaidi ya wakimbizi na waliotafuta kimbilio 1000 bila shirika lililopewa jukuma kimataifa la kuwalinda wakimbizi kutoa sauti hata mara moja.

Jukumu la UNHCR la kuweka kumbukumbu na kukabiliana na ukiukaji wa polisi ni muhimu zaidi kwa sababu ya uwezekano wa ukiukaji mwingine kutokea katika siku za usoni serikali ikijaribu kuwahamisha tena wakimbizi walioko mijini hadi kwenye makambi, shirika la Human Rights Watch lilisema.

Mnamo tarehe 13 Desemba, idara inayosimamia maswala ya wakimbizi katika serikali ya Kenya ( Department of Refugee Affairs) ilitangaza kwamba kutokana na ongezeko la mashambulizi kwa gruneti pamoja na mashambulizi mengine jijini Nairobi na katika maeneo mengine nchini Kenya kutoka Oktoba 2011,  wakimbizi na waliotafuta kimbilio wote 55,000 waliokuwa wakiishi katika jiji la Nairobi walipaswa kurudi au wahamishwe kwa nguvu hadi kwenye kambi za wakimbizi zilizoko karibu na mipaka kati ya Kenya na Somalia na Sudan walimofungiwa. Idara hii pia ilisitisha mara moja usajili wa wakimbizi waliokuwa mijini pamoja na huduma zote ilizowapa.

Serikali ya Kenya inapaswa kuachana na mpango wake wa kuwahamisha, shirika la Human Rights Watch lilisema.

Tangazo la serikali la tarehe 13 Desemba halithibitishi itakikanavyo na sheria ya kimataifa kuwa mpango huu wa kuwalazimisha maelfu ya wakimbizi wanaoishi katika miji nchini Kenya kurudi kambini ni hatua inayohitajika ili kuboresha usalama wa kitaifa na ndio njia itakayowanyima wakimbizi uhuru kwa kiwango cha chini kabisa pamoja na kuwa utaratibu mwafaka zaidi wa kuushughulikia usalama wa kitaifa wa Kenya. Ni mmoja tu – Mkenya asiye wa asili ya Kisomali ndiye amewahi kushtakiwa na kupatikana na hatia ya kuhusika na moja kati ya mashambulizi zaidi ya  30 nchini Kenya toka Oktoba 2011, Kenya ilipotuma majeshi yake kule Somalia.

Uhamishaji huu pia unawabagua wakimbizi kwa kuwanyima uhuru wa kutembea kinyume na sheria ikilinganishwa na Wakenya. Pamoja na hayo, kuwahamisha maelfu ya wakimbizi kutoka mijini hadi kwenye kambi wanamofungiwa kutakiuka haki zao nyingine kama ile ya kutembea, kutohamishwa kwa nguvu kutoka kwao na ile ya kupunguziwa upatikanaji wa haki za kimsingi kama ya kupata chakula, kuchuma riziki, huduma za afya, na elimu. Kambi zenyewe kwa sasa hazina ufadhili wa kutosha kwa kiwango cha dola za Marekani milioni 100.

Ripoti hii vilevile inazungumzia shida katika msaada wa kibinadamu na kiusalama inayoendelea katika kambi za Kenya za wakimbizi kutoka Somalia karibu na mji wa Dadaab ulioko katika eneo la kaskazini mashariki ya Kenya na hali ya ukosefu wa usalama unaokumba karibu kila kona ya Somalia. Maafisa wa ngazi za juu nchini Kenya wamewahimiza mara nyingi wakimbizi wa Somalia warudi nchini mwao na wamesema kuwa kuwahamisha wakimbizi hadi kwenye makambi kutafuatwa mara moja na kurudishwa Somalia.

Eneo kubwa la Kusini ya Kati ya Somalia bado ni hatari  kutokana na vita inayoendelea, mauaji, utumiaji wa nguvu nyingi ovyoovyo dhidi ya raia na mashirika yanayotoa misaada kuweza kufikia eneo dogo tu.

Shirika la Human Rights Watch lilisema kuwa serikali ya Kenya isiwashinikize wakimbizi kurudi Somalia. Shinikizo hilo litakiuka jukumu la Kenya la kutowarudisha wakimbizi katika maeneo yenye mauaji au vita. Nchi zinazotoa ufadhili ziendelee kutoa msaada kwa makundi yanayowashughulikia wakimbizi kutoka Somalia nchini Kenya vilevile zihimize serikali ya Kenya ikomeshe kuwasukumiza wakimbizi kurudi Somalia   kabla ya wakati unaofaa.

“Serikali ya Kenya isiwashinikize Wasomali kuhatarisha maisha yao kwa kurudi nyumbani mapema zaidi.,” Simpson alisema. “Nchi zinazotoa msaada  zinapaswa kuyafadhili kwa ukarimu mashirika yanayofanya kazi na wakimbizi nchini Kenya.”

Your tax deductible gift can help stop human rights violations and save lives around the world.

Region / Country