Skip to main content

Tanzania: Wakimbizi wa Burundi ‘Wapotezwa’, Wateswa

Komesha Kurudishwa kwa Lazima; Peleleza Idara za Polisi, Ujasusi

(Nairobi) –Mamlaka za Tanzania zimewadharirisha kupindukia wakimbizi na watafuta hifadhi wa Burundi wapatao 18 tangu mwishoni mwa mwaka 2019, limesema shirika la Human Rights Watch leo. Wakimbizi waliopotezwa kwa nguvu hawajulikano waliko, na inawezekana Warundi wengine wakawa wamedharirishwa kwa namna hiyo.

Rais wa Burundi Évariste Ndayishimiye (kushoto) na Rais wa Tanzania John Magufuli walipokutana Kigoma, kaskazini magharibi mwa Tanzani, tarehe 19 Septemba 2020. Ilikuwa ni safari ya kwanza ya anje ya nchi ya Ndayishimiye tangu alipochaguliwa kuwa rais mwezi May 2020. © 2020 SOS Médias Burundi


Kati ya Oktoba 2019 na Agosti 2020, idara za polisi na ujasusi za Tanzania zimewapoteza kwa nguvu, zimewatesa na kuwaweka kizuizini pasipo utaratibu sahihi Warundi wapatao 11 kwa wiki kadhaa katika mazingira mabaya katika kituo cha polisi cha Kibondo, mkoa wa Kigoma. Watatu waliachiwa Tanzania, na mamlaka za Tanzania zikawarudisha kwa nguvu Warundi wengine wanane Burundi mwezi Agosti, ambako wamewekwa kizuizini pasipo kushtakiwa. Polisi wa Tanzania wamewashikiria na kuwapoteza kwa nguvu wakimbizi na watafuta hifadhi wengine saba tangu mwezi Januari 2020. Ukamatwaji ulifanyika katika kambi za wakimbizi wa Mtendeli na Nduta mkoani Kigoma, karibu na mpaka wa Burundi.

“Kutoweshwa kwa nguvu na mamlaka za Tanzania kwa wakimbizi na watafuta hifadhi wa Burundi ni uhalifu wa kupindukia, mbali na mateso na uchungu mkubwa waliosababishiwa wanafamilia, wengi wao wakiwa wamekimbia unyanyasaji wa namna hiyo hiyo kwao Burundi,” amesema Mausi Segun, Mkurugezi wa Afrika wa Human Rights Watch. “Serikali ya Tanzania inapaswa kuchunguza haraka na pasipo upendeleo madai kwamba Warundi wametekwa, wameteswa, na kurudiswa mikononi mwa mamlaka za Burundi kinyume cha sheria, na kuhakikisha kwamba wote waliohusika wanawajibishwa.”

Zaidi ya Warundi wakimbizi 150,000 wanaishi katika makambi nchini Tanzania , wengi wao wamekimbia ukaili nchini Burundi baada ya uamuzi wa aliyekuwa rais wa Burundi Pierre Nkurunziza kutaka kugombea awamu ya tatu iliyoleta mgogoro mnamo mwaka 2015. Serikali ya Tanzania imekuwa ikiwashinikiza wakimbizi kurejea kwao Burundi.

Ramani ya eneo la mpakani mwa Burundi na Tanzania. © 2020 John Emerson kwa ajili ya Human Rights Watch

 

Kati ya Agosti na Novemba 2020, Human Rights Watch ilifanya mahojiano ya simu na waathrika, mashuhuda, na wanafamilia wa waathirika wa unyanyasaji 23. Vyanzo vingine saba vinafanya kazi kambini ambao hawakupenda kutambulishwa walitoa ushuhuda uliofanana na ule wa waathirka na wanafamilia wa waathirika.

Kesi zote zilizonakiliwa zinaonyesha kwamba mamlaka za Tanzania zilihusika katika kupotezwa kwa nguvu kwa wakimbizi. Tisa ya waathirika walisema waliwekwa kizuizini kwa wiki kadhaa pasipo mawasiliano yoyote katika kituo cha polisi cha Kibondo na kwamba familia zao hazikujulishwa mahali walipo. Majasusi wa Tanzania au askari polisi  waliwahoji mahabusu kuhusu kushikiwa kwa ushirika wao na vikundi vya kiuanamgambo wa silaha na umiliki haramu wa silaha, shughuli zao katika makambi, na nyakati zingine, waliwaomba pesa ili wawaachie.

Warundi walisema kwamba polisi wa Tanzania waliwashikiria katika vyumba visivyokuwa na umeme wala madirisha, wakawapeleka katika jingo lingine la kituo cha polisi, na kuwaning’iniza katika dali kwa kutumia pingu walizokuwa wamewafunga. Wengine walisema kwamba askari polisi na majasusi waliwapiga shoti ya umeme, wakawapaka pilipili usoni na sehemu zao za siri, na kuwapiga na kuwachalaza viboko. Wakati mwingine, polisi na majasusi waliwaambia kwamba wamepokea taarifa kutoka mamlaka za Burundi kuhusu wao, ikiashiria ushirikiano kati ya maofisa wa nchi mbili.

Mfungwa wa Kirundi aliyekaa katika kituo cha polisi cha Kibondo kwa siku 23 mwezi Julai alielezea jinsi alivyoning’inizwa darini kwa kutumia pingu alizokuwa amefungwa: “Tulipiga kelele kama vile tunasulubiwa…. Walisema wanataka shilingi (za Kitanzania) milioni moja [US$430].” Aliposema kwamba hawezi kulipa, polisi walimshutumu kwa kuwazuia wakimbizi kurudi Burundi na kujaribu kuchochea ghasia Burundi. “Walitumia spoku za baiskeli kutuchoma nazo halafu kupaka pili pili sehemu zetu za siri,” alisema. “Tulikuwa tunakula mara moja tu kila baada ya siku tatu…. walisema watakwenda kutuua.”

Walipomwambia achague aidha kubaki kizuizini nchini Tanzania au kurudishwa kwa mamlaka za Burundi, aliwasihi wamrudishe Burundi. Yeye pamoja na Warundi wengine saba waliorudishwa mwezi Agosti wanashikiliwa tangu wakati huo katika magereza za Muramvya na Bubanza nchini Burundi. Walisema waofisa wa ujasusi wa Burundi waliwapeleka mbele ya ofisa wa mahakama kwa ufupi mwezi Agosti, pasipokuwa na mwanasheria yeyote yule kuwepo, ambapo walirudia mashtaka ya mamlaka za Tanzania ya kuchochea ghasia Burundi kabla ya kuamuru kurudishwa kwao magereza. Hakuna mahabusu yeyote kati yao ambaye amemuona hakimu au kuhukumiwa rasmi tangu wakati huo.

Katika kesi za wakimbzi na watafuta hifadhi wengine saba waliokamatwa na polisi, wanafamilia walisema hawajapata majibu yeyote yale kutoka kwa maofisa wa polisi wa kambini walipowauliza wapendwa wao wako wapi. Baadhi ya wanafamilia hata wamewasiliana na shirika la Umoja wa Mataifa la Wakimbizi (UNHCR).

Katika majibu yake kwa Human Rights Watch kuhusiana na maombi ya taarifa juu ya tuhuma hizi, UNHCR ilisema inashitushwa sana na taarifa za upotevu wa wakimbizi nchini Tanzania na kwamba wamekuwa wakizieleza mamlaka za Tanzania mara kwa mara juu ya hofu hizi kwa njia zote za mdomo na maandishi, wakiomba uchunguzi kamili na kutoa taarifa ya maandishi kwa serikali. UNHCR iliandika: “Baada ya maombi kadhaa, serikali iliitaarifu UNHCR mwezi Agosti kwamba uchunguzi wa ngazi ya juu ulikuwa ukiendelea. Hatujajulishwa juu ya matokeo yeyote ya uchunguzi huu. Bado tunaendelea kulizungumzia swala hili na serikali kama swala la dhalula.” UNHCR walihitimisha kwa kusema: “Ulinzi wa kimwili wa wakimbizi ni wajibu wa nchi wenyeji na kwasababu hiyo, UNHCR inatoa wito kwa mamlaka za Tanzania kuchukua kila hatua ziwezekanazo kuhakikisha usalama wa wakimbizi Warundi, kwa mujibu wa wajibu wao wa kimataifa.”

Human Rights Watch ilituma barua tarehe 26 Oktoba ikitoa taarifa juu ya visa vilivyonukuliwa na maombi ya utafiti kwa mkurugenzi wa mashtaka ya umma wa Tanzania, mkurugenzi wa idara ya wakimbizi katika Wizara ya Mambo ya Ndani, na kamanda mkuu wa polisi. Tarehe 18 Novemba, Human Rights watch iliziandikia wizara za mambo ya nje na ile ya sheria za Burundi kuomba taarifa za Warundi nane ambao wanashikiliwa katika magereza za Muramvya na Bubanza. Human Rights Watch haijapokea majibu yeyote yale.

Kuwasafirisha kwa Tanzania kwa mahabusu wakimbizi na watafuta hifadhi wa Burundi kwenda Burundi pasipo taratibu mahususi kunakiuka katazo la sheria la kimataifa, kurudishwa kwa nguvu kwa yeyote sehemu ambayo anaweza kuteswa au kuetendewa ubaya, au kwenye hatari ya maisha yake.

Nchini Burundi, ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu dhidi ya wafuasi au wadhaniwa wafuasi wa upinzani, ikiwa ni pamoja na wakimbizi wanaorejea nyumbani, huwaweka hatarini, limesema shirika la Human Rights Watch. Kamisheni ya Umoja wa Mataifa lenye jukumu la kushughulikia Haki za Binadamu liliripoti mwezi Septemba ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu uliokithiri tangu mwaka 2019. Kamisheni iliona kwamba baadhi ya waliorudi nyumbani waliendelea kukumbana na ukatili kutoka kwa maofisa wa nyumbani na kambi ya vijana ya chama tawala, ijulikanayo kama Imbonerakure, na kwamba “kuna wakati wanaorudi wamekuwa waathirika wa ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu uliofanya warudi uhamishoni.”

“Tuna hofu kwamba Warundi waliopotea wanakumbana na hali kama ile ambayo wanakutana nayo wale wanaorudishwa Burundi kinyume cha sharia, au mbaya Zaidi,” anasema Segun, “ We are concerned that the Burundians who have been disappeared face a fate like those already unlawfully returned to Burundi, or worse,” Segun said. “Mamlaka za Tanzania zinapaswa kufanya kila juhudi kuwapata watu hawa, kuwajulisha familia zao, na kuwapatia haki zao za msingi wanazostahili wakimbizi kote ulimwenguni.”

Kwa taarifa Zaidi juu ya mazingira kupotezwa kwa nguvu, unyanyasaji katika kituo cha polisi cha Kibondo, hali ilivyo Tanzania, na mapendekezo, tafadhari angalia hapa chini.
 

Wakimbizi wa Burundi nchini Tanzania

Tanzania imekuwa mwenyeji wa maelfu ya wakimbizi katika miongo kadhaa iliyopita na imewapatia uraia maelfu ya wakimbizi ambao wamekuwemo nchini tangu mwaka 1972. Hata hivyo, nchi hiyo ina historia mbaya ya kuwalazimisha wakimbizi kurudi kwao  na mwaka 2017 rilifuta  hadhi ya prima facie – ambayo ilitambua hadhi ya ukimbizi kwa kuzingatia tu uraia wa mkimbizi – kwa wakimbizi wa Burundi. Tangu mwaka 2018, Warundi wengi wanaotafuta hifadhi wamekumbana na vikwazo vya kujisajili.

Kufikia tarehe 31 Oktoba, 2020, zaidi ya wakimbizi 150,000 wa Burundi walikuwa katika kambi tatu – Nduta, Nyarugusu, and Mtendeli – katika mkoa wa Kigoma, Tanzania karibu na mpaka wa Burundi. Wengi walikimbia Burundi baada ya uamuzi wa aliyekuwa rais wa nchi hiyo Pierre Nkurunziza  kutaka kugombea awamu ya tatu iliyozua mvutano mwaka 2015 na kuibua mgogoro mkubwa wa haki za binadamu.

Kati ya Septemba 2017 na Septemba 2020, takribani Warundi 100,000 walirudi kutoka Tanzania kwenda Burundi chini ya makubaliano kati ya Burundi, Tanzania na UNHCR, ambayo ilitakiwa kufanya mahojiano ya kina na wakimbizi kuhakikisha kwamba wanaondoka Tanzania kwa hiari. Tangu mwaka 2019, n ahata hivi karibuni mnamo mwezi Septemba 2020, UNHCR imekuwa ikisisitiza kwamba “haihamasishi safari ya kurudi Burundi” lakini itaendelea kusaidia “kurudi kwa hiari” kwa wale walioelimika vizuri. Imesema pia kwamba “Tanzania ina mpango wa kufanikisha kurudishwa kwa wakimbizi wa Burundi wapatao 20,000 kati ya mwezi Septemba na Desemba 2020.”

Mwezi Machi 2018, Tanzania na Burundi walikubaiana kuwarudisha wakimbizi wa Burundi 2,000 kwa wiki, na Agosti 2019 makubaliano kati ya Tanzania na Burundi yalitangazwa kwamba wakimbizi wote “walipaswa kurejea nchini kwao aidha kwa hiari ama lah” ifikapo tarehe 31 Disemba ya mwaka huo.

Ripoti ya Human Rights Watch ya Disemba 2019 iligundua kwamba hofu ya ukatili, kukamatwa kiholela na kuondoshwa nchini kwa nguvu kulikuwa kunawasukuma wakimbizi na watafuta hifadhi wengi wa Burundi kuondoka nchini Tanzania. Mamlaka za Tanzania zilikuwa zikiwalenga Zaidi wakimbizi fulani wa Burundi ambao hadhi yao ya kisheria isiyokuwa kamili na kutokuwepo kwa msaada wa kisheria kuliwafanya kuwa hatarini Zaidi kulazimishwa kurudi Burundi. Human Rights Watch ilihitimisha kwamba mamlaka za Tanzania zilifanya ugumu kwa UNHCR kukagua ipasavyo ikiwa uamuzi wa mamia ya wakimbizi wa kurudi Burundi ulikuwa ni wa hiari.

Tarehe 3 Disemba, waziri wa mambo ya ndani wa Tanzania Kangi Lugola, alikanusha kwamba serikali ilikuwa “ikiwafukuza  wakimbizi” , na kusema kwamba mamlaka za Tanzania na Burundi “wanaratibu tu, na kuwatia moyo wale walioko tayari kurudi nyumbani kwa hiari yao wenyewe, kufanya hivyo”

Mamlaka za Burundi zilikuwa zikizungumzia sana suala la wakimbizi kurejea kutoka uhamishoni kabla na baada ya uchaguzi wa Mei 2020. Katika hotuba ya sherehe ya uapisho wake, Rais Evariste Ndayishimiye alisema: “Tunawasihi Warundi wote wanaopenda kurudi nchini kwao wafanye hivyo.” Hata hivyo katika hotuba hiyo hiyo, alizitishia nchi ambazo zinawaunga mkono “Warundi wanaojiingiza katika kuchochea ghasia,” inawezekana kabisa alikuwa akiwazungumzia wakimbizi waliokimbia nchi kutoka na harakati zao za kisiasa na haki za binadamu. Safari ya kwanza ya nje ya nchi ya rais Ndayishimiye taliifanya katika mpaka wa Burundi karibu na Kigoma, Tanzania, mnamo mwezi Septemba.

Mkataba wa Wakimbizi wa mwaka 1951 na Mkataba wa Wakimbizi wa Kiafrika wa mwaka 1969 unazuia kuwaadhibu, kuwarudisha wakimbizi kwa namna yoyote ile mahali ambapo maisha yao na uhuru wao utatishiwa. UNHCR wanasema kwamba adhabu hutokea  si tu pale ambapo serikali inapokataa moja kwa moja au kumfukuza mkimbizi, lakini hata pale ambapo shinikizo lisolo la moja kwa moja linapokuwa kubwa hata kupelekea watu kuamini kwamba hawana chaguo lingine lolote lile isipokuwa kurudi katika nchi ambayo wanakumbana na hatari kubwa. Kuzuiwa kwa kurudishwa kwa nguvu kunatokea pia pale ambapo wanaotafuta hifadhi wanakuwa bado hawajatambuliwa kama wakimbizi.

Kutokana na unyeti wa swala la hadhi ya wakimbizi wa Burundi wa Tanzania, Human Rights Watch imezuia taarifa za utambulisho wa waliotoa shuhuda zao kwa hofu za kushambuliwa kwa mashuhuda wenyewe na ndugu zao.

Kukamatwa, Kupotezwa Makambini

Kupotezwa kwingi ambako Human Rights Watch ilikunukuu kunafanana. Polisi wanafika katika nyumba ya muathirika kati ya usiku wa manane na saa tisa alfajiri na kusema Kiswahili: “Musihofu, musihofu, sisi ni polisi”. Wengi wanasema kwamba wanaume hao huwa wamevaa nguo za kijani za polisi lakini hawakuonyesha waraka wowote wa kukamata. Waathirika wawili wa kupotea na wanafamilia wawili wa waathirika waliwatambua makamanda wa polisi kutoka vituo vya Nduta na Mtendeli kuwa sehemu ya oparesheni hiyo.

Kambi ya Nduta nchini Tanzania kwasasa inahifadhi wakimbizi na watafuta hifadhi wa Burundi wapatao 70,109. Takribani Warundi 154,000 wanaishi katika kambi tatu – Nduta, Nyarugusu na Mtendeli – kaskazini magharibi mwa Tanzania katika mkoa wa Kigoma, ambapo baadhi yao wamekumbwa na ukamataji holela, kupotezwa kwa nguvu, na kuteswa. © 2020 SOS Médias Burundi

 

Mke wa mkimbizi mwenye umri wa miaka 42 anayeishi katika kambi ya Nduta alisema kwamba mume wake alikamatwa Februari 2020:

Walikuja wakavunja mlango. Walipoingia ndani ya nyumba, walisema, “Sisi ni polisi” na wakataka simu zetu…. Niliwasihi wamuache mume wangu avae nguo kwanza wakiwa wanamfunga pingu… Asubuhi tulikwenda kuwaona polisi wanaolinda kambi. Walituambia kwamba hapakuwa na polisi yeyote yule aliyeingia kambini usiku uliopita. Ni kama vile maafisa wote wa polisi wanashirikiana.

Jirani yake alithibitisha taarifa hii.

Mke mwingine wa mkimbizi, ambaye mume wake walikamatwa mwezi Julai katika kambi ya Mtendeli, alisema kwama alisikia sauti za wanaume karibu na nyumba yake majira ya saa nane usiku.: “Walivunja dirisha ya chumbani kwetu na kutumulika na tochi usoni kwetu. Walizungumza Kiswahili na kusema, “Sisi ni polisi, msiogope, fungueni mlango.” Baada ya mume wake kufungua mlango, alisema, “Walitaka simu zetu kisha wakamfunga pingu mume wangu. Walikuwa ni askari polisi waliovaa sare za kijani; mmoja wao alikuwa na bunduki. Nilimtambua mmoja wao – alikuwa ni mmoja wa askari wanaolinda kambi.”

Alipowauliza askari wa kambini hapo kuhusu alipo mume wake siku iliyofuata, aliwakuta wanawake wengine watano pale waliokwenda kwa swala hilo hilo: “Tulipowauliza waume zetu wako wapi, walisema hawakuwepo pale na kwamba hawakujua chochote kile….. Hadi leo sijamuona tena.”

Familia sita zilizoenda kuulizia kuhusu walipo wapendwa wao walisema polisi walikanusha kuwashikiria waathirika hao. Hakuna hata familia moja ya wakimbizi na watafuta hifadhi saba waliopotea ambao wamefanikiwa kujua walipo ndugu zao.

Katika kesi moja, mke wa muathirika alisema kwamba alitishiwa kwa kuuliza alipo mume wake: “Baada ya kuuliza mara kadhaa, nilikwenda tena kituo cha polisi cha kambi ya Nduta….lakini mara hii walisema; ‘Ukiendelea kutusumbua juu ya kesi ya mume wako, tutakupeleka kule alipo.’ Tangu siku hiyo, sijamuulizia tena, kwasababu sijui kama walimuua na kwamba wataniua na mimi pia.”

Chini ya sharia za kimataifa, kupotezwa kunatokea pale ambapo maofisa wa serikali, au watu au vikundi vinavyofanya kazi chini ya idhini ya serikali, vinapomnyima mtu uhuru na kukataa kwamba vinamnyima uhuru au kukubali pale mtu huyo alipo.

Kupotezwa kunaendelea kwa muda wote ambao mtu huyo hajulikani alipo, na taarifa za mahali alipo hazitolewi. Inakuwa pia na waathirika zaidi ya mmoja. Wale walio karibu na muathirika wanaugua uchungu kwa kutokua nini kimetokea kwa mpendwa wao, kitu ambacho ni ukatili wa hali ya juu.

Wanaweza kufanyiwa ukatili pia na mamlaka ambazo zimeshindwa kupeleleza au kutoa taarifa za mahali alipo ndugu yao. Sifa hizi hufanya kupotezwa huku kuwe kwa ukatili wa hali ya juu, na kudhihirisha namna ambavyo mamlaka zinapaswa kuwajibika katika kuzuia na kukomesha uhalifu.

Mahakama ya Afrika ya Haki za Watu na Binadamu, ambayo Tanzania iliitambua mwaka 1984, inakataza ukamatwaji na ushikiliwaji wa kiholela, na udharirishaji mwingine uliosawa na kupotezwa. Tanzania ni miongoni mwa nchi chache ambazo haziutambui Mkataba wa Umoja wa Mataifa unaopinga Ukatili, Udharirishaji, na aina zingine za Unyama au Adhabu za kikatili (Mkataba wa kupinga Utesaji”.)

Tanzania haijatia sahihi pia Mkataba wa Kimataifa Dhidi ya Kulinda Watu Dhidi ya Kupotezwa. Hata hivyo. Katazo la wazi dhidi ya utesaji ni sehemu ya Sheria za msingi za Kimataifa na zinahesabiwa kama uhalifu katika Mkataba wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu. Chini ya sharia ya kimataifa, utesaji na kupotezwa ni makossa makossa yaliyo ndani ya sharia za kimataifa, maana yake ni kwamba nchi yoyote inaweza kuyasimamia kisheria haijalishi yamefanyika wapi au uraia wa wale waliohusika au waathirika wa uhalifu huo.


Udharirishaji katika Kituo cha Polisi Kibondo

Human Rights Watch iliwahoji Warundi tisa ambao walipotezwa kwa nguvu na ambao walisema walipelekwa  kituo cha polisi cha Kibondo, takribani kilometa 11 kutoka kambi ya Nduta na kilometa 25 kutoka kambi ya Mtendeli.

Picha ya satelaiti ya kituo cha polisi cha Kibondo, kaskazini magharibi mwa Tanzania. © 2020 CNES/Airbus. Chanzo: Google Earth

 

Walisema waliwekwa kizuizini kwa wiki kadhaa kati ya Oktoba 2019 na Agosti 2020. Baadhi yao walikuwa kwanza katika kituo cha polisi cha kambini, na wote walieleza kupitia kituo cha polisi cha Kibondo, ambapo waliwekwa katika chumba cha giza, kisichokuwa na dirisha. Mahojiano na polisi yalifanyika katika jengo lingine lakini ndani ya uzio mmoja.

Mrundi mmoja walisema:

Tulipofika katika kituo cha polisi usiku huo, tuliwekwa katika chumba kidogo ambacho hakikuwa na taa wala dirisha. Hapakuwa na maji wala vyoo. Tulikuwa nan doo tu. Tulikula mara chache sana, na tulikuwa tukiteswa. Walikuwa wakitupigia katika nyumba nyingine ya jirani ndani ya uzio ule ule. Walipitisha kamba katikati ya mikono yetu iliyofungwa pingu na kutuning’iniza. Sijui nilitumia muda gani pale nikining’inia. Maumivu ni zaidi ya jinsi ambavyo niliweza kustahimili.

“Kwenye hii nyumba kuna fito ambazo watu huning’iniziwa,” alisema Mrundi mmoja mwenye umri wa miaka 32 aliyeshikiliwa katika kituo cha polisi kutoka Oktoba hadi Novemba 2019. “Wanatumia shoti ya umeme pia kama mbinu ya utesaji katika nyumba hii.” Maofisa wa polisi na ujasusi walimshutumu kwa kubeba silaha na kujaribu kuchochea ghasia ndani ya serikali ya Burundi:

Nilikanusha madai haya, hivyo wakaniambia nivue nguo zangu zote. Wakaifunga pingu miguu yangu kwenye mikono yangu na kunining’iniza, na kuanza kunichapa kwa kutumia waya [wa baiskeli] uliochubuliwa. Nilichapwa na fimbo….. walinipiga popote pale walipotaka, mwili mzima…. Nilipiga kelele pasipo msaada, hawakuwa na huruma kabisa….kwasababu sikuwaambia kile walichotaka kusikia, walinitundika juu tena na tena…. Nilisikia maumivu makali sana kiasi kwamba niliwaomba waniue – hata sijui walinipiga kwa muda gani.

Mrundi mmoja, aliyekamatwa na maofisa wa polisi wa kambini na kupelekwa kituo cha polisi cha Kibondo mwezi Novemba 2019 kwa wiki mbili, alisema askari polisi walimshutumu kwa kuwa na silaha na kumtesa mara kwa mara:

Waliichovya fimbo iliyokuwa na pamba mwishoni katika chupa yenye pilipili na kuingiza katika tundu langu la haja kubwa. Nilipoendelea kukataa kuwa na silaha, walimimina pilipili machoni na katika mwili wangu….. niliendelea kusema kuwa sikuwa na silaha yoyote ile, hivyo wakaunganisha nyaya mbili za umeme kwenye kifua change. Ilikuwa inauma kupindukia.

Mtu mwingine aliyeachiwa baada ya kukaa wiki mbili katika kituo cha polisi cha Kibondo mwezi Machi 2020, alisema:

Wakati wa kipindi hiki, nilipewa chakula mara mbili. Mahabusu wengine wa Kitanzania walikuwa wakitupa chakula kidogo walichopewa na ndugu zao. Nilimuona mahabusu mwingine aliyeitwa “Gervais” [si jina halisi]. Aliniambia kwamba amekuwa akishikiliwa pale kwa siku nne bila chakula. Aliniambia jina la mke wake, nilipoachiwa nilimjulisha mke wake kwamba nilimuona mumewe. Alikuwa akipigwa mara nyingi sana, akiwa uchi. Alikuwa akivuja damu mwili wake wote. Siku moja alitolewa rumande na sikumuona tena.

Human Rights Watch ilithibitisha taarifa hizi na mke wa Gervais, aliyesema kwamba askari polisi walimchukua mume wake majira ya saa tisa usiku tarehe 12 Machi katika kambi ya Nduta. Alisema alitoa taarifa juu ya kupotea kwake katika kituo cha polisi cha kambini, lakini walimwambia hakuna askari polisi aliyekwenda kambini hapo usiku ule: “Walisema wangefanya uchunguzi, lakini sikusikia chochote kutoka kwao tena.”

Ushirkiano kati ya Mamlaka za Burundi na Tanzania

Wakimbizi na watafuta hifadhi nane kutoka Burundi walikamatwa katika kambi za Nduta na Mtendeli kati ya Julai mwishoni na mwanzoni mwa Agosti na kuwekwa kizuizini pasipo mawasiliano kwa wiki kadhaa katika kituo cha polisi cha Kibondo, halafu wakapelekwa kwa maofisa wa ujasusi wa Burundi mpakani mwezi Agosti. Sita kati yao walisema maofisa wa polisi na ujasusi wa Tanzania waliwannyanyasa na kuwaomba wawapatie shilingi milioni moja za Kitanzania ($430) ili wawaachie. Baada ya kushindwa kulipa, wanaume hao walipewa kuchagua aidha kurudishwa Burundi au kufia kizuizini.

Mrundi mmoja alisema baada ya kushikiliwa kwa siku 23 katika kituo cha polisi cha Kibondo:

Walituweka kwenye gari, mikono ikiwa imefungwa, sura kufunikwa, na tukiwa wanane wakatupeleka mpakani, ambapo maofisa wa usalama wa [Burundi] walikuwa wakitusubiria. Hatukuwa tumeonana na hakimu bado…. Mpakani pale, tulimsikia polisi mmoja Mtanzania akiwaambia maofisa wa Burundi, “Fanya hii siri; tuondoke hapa mara moja kabla Uhamiaji hawajatukuta hapa.” …

Baada ya kukaa ndani ya gari kwa dakika 30 [tukiwa na maofisa wa Burundi], tulianza kupiga kelele kwasababu kamba tulizokuwa tumefungwa nazo zilikuwa zikiuma. Walizifungua lakini wakabakiza macho yetu yakiwa yamefungwa. Tulikaa siku nane katika ofisi ya idara ya ujasusi Bujumbura, ambapo tulikuwa tukihojiwa. Walitusainisha karatasi na kutuahidi kutuachia huru, lakini badala yake walitupeleka wote gerezani.

Kati ya kundi la watu wanane tuliorudishwa Burundi kwa nguvu kinyume na sharia za kimataifa, wane kati yatu wapo gereza la Bubanza na wane wengine wapo gereza la Muramvya.

Warundi wengine wawili ambao walikuwa wanashikiliwa kituo cha polisi cha Kibondo walisema pia kwamba wakati wa kuhojiwa, maafisa wa ujasusi wa Tanzania waliwaambia kwamba maafisa wa ujasusi wa Burundi waliwapatia taarifa zao. Bwana mmoja ambaye aliachiliwa baadae Tanzania, alisema kwamba alihojiwa kuhusu kuhudumu kwake jeshini Burundi:

Tayari walijua kwamba niliwahi kuwa jeshini, hata kabla sijawaambia…… niliwaambia sikuwa na silaha, lakini walisema kwamba wangeniua, na ikiwa hawatafanya hivyo, watanipeleka Burundi…..waliponiachia, waliniambia kwamba ikiwa serikali ya Burundi itanihitaji watakuja kunichukua.

 
Mapendekezo

Serikali ya Tanzania inapaswa:

  • Kumwachia mara moja au kumpeleka kwa hakimu yeyote aliyepotezwa na kuhakikisha kwamba kushikiliwa kwa yeyote yule kunazingatia sharia za kimataifa za haki za binadamu;
  • Kuhakikisha kwamba mamlaka zinajibu haraka maombi kutoka kwa familia za waliopotezwa kwa nguvu au wasiojulikana walipo, wakitoa taarifa zote zinazojulikana kuhusu mahali walipo au kilichowasibu na kutoa hatua zinazochukuliwa kuzipata taarifa hizo ikiwa hazipo bado;
  • Kuwaagiza mamlaka za kanda na taifa kuchunguza juu ya visa vyote vya watu kupotezwa, kutoa taarifa za uchunguzi hadharani, na kumchukulia hatua za kisheria yeyote aliyehusika na kupotezwa kwa watu hawa kwa nguvu;
  • Kutoa agizo la maandishi kwa maofisa wote wa serikali wanaohusika na maafisa wa usalama kuacha mara moja utesaji dhidi ya Warundi walioandikishwa na wale ambao hawajaandikishwa, ikiwa ni pamoja na ushikiliwaji wa holela, kupotezwa kwa nuvu, utesaji, kuwalazimisha kutoa pesa na kuwarudisha Burundi;
  • Kuingiza katika sharia mikataba yote kimataifa ya haki za binadamu, hasa Makataba wa kupinga Utesaji, na Mkataba wa Kimataifa wa Kuwalinda Watu Wote dhidi ya Kupotezwa kwa Nguvu;
  • Wajulishe UNHCR mara moja juu ya kukamatwa na kushikiliwa kwa mkimbizi na mtafuta hifadhi yeyote kutoka Burundi na sababu za kukamatwa kwao, na kuwaruhusu UNHCR kuwaona wakimbizi na watafuta hifadhi wote kabla ya kuanza kwa hatua zozote za kuwarudisha, kuchunguza vyema kwamba uamuzi wao wa kurudi Burundi ni wa hiari.

Serikali ya Burundi inapaswa:

  • Kuwaachia au kuwaleta mahakamani wakimbizi na watafuta hifadhi wote wanaoshikiliwa baada ya kurudishwa Burundi na kuhakikisha kwamba kushikiliwa zaidi kunazingatia sharia za kimataifa za haki za binadamu. Hakuna anayestahili kushikiliwa isipokuwa baada ya kushtakiwa kwa kosa la jinai, kuwashikilia watu kabla ya hukumu hakuna ulazima, na hatua zingine za muhimu na kushatikiwa kwa mujibu wa haki zao zinaheshimika;
  • Chunguza na wawajibishe maofisa wa ujasusi wanaohusika na uhamishaji wa kinyume na sheria na ushikiliwaji holela wa wakimbizi na watafuta hifadhi wa Burundi;
  • Kusitisha ushirikiano wowote na Tanzania wa kuwarudisha wakimbizi na watafuta hifadhi wa Burundi kinyume na sharia, walinde wote wanaotaka kurudi nyumbani kwa hiari dhidi ya kuadhibiwa kokote kule.

UNHCR inapaswa iseme hadharani kwamba kurudishwa kwa nguvu kunakofanywa na Tanzania kwa wakimbizi na watafuta hifadhi wa Burundi katika visa vyote vilivyonukuliwa ni kinyume na sharia, ni kinyume na Mkataba wa Wakimbizi, na inapaswa izisihi mamlaka za Tanzania kuacha mara moja kurudisha huku kwa nguvu.

Jumuiya ya Afrika Mashariki, Kamisheni ya Afrika ya Haki za Watu na Binadamu, na Umoja wa Afrika unapaswa uiambie Tanzania hadharani kuchunguza taarifa zote za kupotezwa kwa nguvu, kukamatwa kiholela, na kuteswa, na kuacha kulazimisha kurudi kwa wakimbizi na watafuta hifadhi kwa njia ya moja kwa moja ama vinginevyo.

 

Your tax deductible gift can help stop human rights violations and save lives around the world.

Region / Country