Skip to main content

Kenya: Vurugu dhidi ya Wapenzi wa Jinsia Moja Yaenea katika Pwani

Serikali Inapaswa Kuwalinda, Sio Kuwanyanyasa Walio Wachache Kijinsia

(Nairobi)- Magenge katika pwani ya Kenya yamewashambulia watu tena na tena kwenye misingi ya hisia ya kimapenzi na utambulisho wa kijinsia, mashirika ya PEMA Kenya na Human Rights Watch yasema katika ripoti iliyotolewa leo. Katika matukio yasiyopungua sita kati ya 2008 na 2015, magenge katika kaunti zilizopo pwani ya Kenya kama vile Mombasa, Kwale na Kilifi yamewashambulia au yametishia kuwashambulia wasagaji, mashoga, wanaovutiwa kimapenzi na jinsia zote mbili na waliobadilisha jinsia zao (lesbians, gays, bisexual and transgender people - wana LGBT) ama wahudumu wa afya wanaohudumia jamii ya wana LGBT bila hatua zifaazo kuchukuliwa na mamlaka.

Ripoti yenye kurasa 70 iitwayo “Suala Nyeti Ni Vurugu; Mashambulizi dhidi ya Wana LGBT katika Pwani ya Kenya, ‘’ imejikita katika utafiti uliofanywa katika mwaka wa 2014 na 2015 na mashirika ya Human Rights Watch na PEMA Kenya ambalo ni shirika la kijamii lenye makao yake jijini Mombasa na linawahudumia walio wachache kijinsia na kingono katika maswala ya haki za kibinadamu, afya , VVU/UKIMWI,  and maslahi ya kiuchumi. Mashirika hayo mawili yalirekodi ukiukaji wa haki za kibinadamu ya walio wachache kijinsia katika pwani ya Kenya kama vile mashambulizi ya magenge, ubakaji, kuchochea vurugu, na kutolindwa vilivyo. Mashirika vilevile yaliainisha jinsi serikali inavyoweza kukabiliana na ukiukaji huu.

‘’Kwa wana LGBT wengi walioko katika pwani ya Kenya, usalama ni jambo linawalotia wasiwasi kila siku,’’ alisema Esther Adhiambo, Mkurugenzi Mtendaji wa PEMA Kenya. ‘’Ingawa jinsi polisi wanavyowahudumia wana LGBT imeendelea kuimarika katika miaka ya hivi karibuni, ubaguzi bado ni changamoto kubwa. Kwa sababu ya hofu ya kweli ya wana LGBT kuhusu kuripoti uhalifu utokanao na chuki,  vurugu inaendelea bila kujali  sheria.’’

Hatua zinazochukuliwa na serikali baada ya mashambulizi ya magenge na mashambulizi mengine dhidi ya wapenzi wa jinsia moja hazitoshi. Maafisa wa serikali mara nyingi hawashutumu mashambulizi. Polisi nao hata katika visa vichache ambavyo wamewalinda manusura, hawajamkamata mtu yeyote kwa kuhusika au kuchochea mashambulizi hayo.

Manusura wengi hawatoi malalamiko yao kwa polisi, wakiamini kuwa  polisi hawatawasaidia, au labda mbaya zaidi, huenda wakawakamata badala yake. Katika visa vingi, wana LGBT waliojaribu kuripoti kwa polisi, walikabiliana na ubaguzi kutoka kwa polisi, waliwakejeli au waliwahangaisha ama walikataa kuchukua taarifa zao.

Sheria ya Kenya inatoa kifungo cha miaka 14 kwa kosa la ‘mapenzi kinyume na maumbile.’’  Ingawa mashtaka kwa mapenzi ya jinsia moja ni nadra nchini Kenya, polisi katika Kaunti ya Kwale waliwakamata wanaume wawili mnamo Februari 2015 kwa sababu ya uvumi tu na kuwafanyia uchunguzi unaodhalilisha kwenye mikundu kama jaribio lisilofaa la ‘’kuthibitisha’’ hisia zao za kimapenzi. Walinaswa katika msako wa kuwanasa mashoga uliofanywa na wakaazi wa Kaunti ya Kwale. Idadi ya wanaume isiyopungua wawili walivamiwa na kukatwa kwa chupa zilizovunjka, katika kipindi hicho cha uhalifu ulioonekana ulitokana na chuki dhidi ya mapenzi ya jinsia moja. Waliyaambia Human Rights Watch na PEMA kuwa waliogopa kuwa wangaliripoti matukio hayo kwa polisi, wangekamatwa.

Vurugu kwenye misingi ya hisia ya kimapenzi na utambulisho wa kijinsia isiyozuiliwa sio tu ukiukaji mbaya wa haki za kibinadamu, bali pia inahatarisha juhudi za Kenya za kukabiliana na janga la VVU lililoenea sana miongoni mwa wale walio hatarini kama wanawake waliobadilisha jinsia zao na wanaume wanaofanya mapenzi na wanaume(men who have sex with men, MSM), mashirika hayo yalisema. Katika mashambulizi matatu ya magenge, vurugu ama vitisho kutoka kwa wenyeji na viongozi wa kidini katika eneo la pwani viliwafanya wahudumu wa afya wanaowahudumia MSM kufunga vituo vyao kabisa au kwa muda. Mashambulizi dhidi ya mashoga katika Kwale mnamo Februari yaliwafanya wengi kutoroka eneo hilo au kukaa ndani ya nyumba zao kwa majuma, hatua iliyofanya idadi ya walioshriki katika juhudi za kupunguza VVU kupungua sana katika kituo kimoja cha afya jijini Mombasa.

 

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kupambana na UKIMWI (UNAIDS) limetoa wito wa kutoharamisha mapenzi ya jinsia moja, kwa kufafanua kuwa kuharamisha mapenzi ya jinsia moja kunafanya makundi yaliyoko hatarini kujificha na kutoendea huduma muhimu za kuzuia UKIMWI na ya kimatibabu.

Mashirika ya umma katika pwani ya Kenya likiwemo PEMA Kenya, yamechukua hatua za kuwaelimisha maafisa wa polisi, wahudumu wa afya na viongozi wa kidini katika maswala ya hisia ya kimapenzi na utambulisho wa kijinsia , na pia kuhusu umuhimu wa kutobagua katika utoaji wa huduma. Hatua hizi zimeboresha polepole mazingira wanamoishi wana LGBT katika pwani ya Kenya, lakini mashirika hayo ya umma yameeleza kuwa jukumu hili halipaswi kuwa lao wenyewe na kwamba serikali vilevile inapaswa kuchangia katika kukomesha vurugu na ubaguzi dhidi ya wale wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja na waliobadilisha jinsia zao.

‘’Rais Kenyatta hivi majuzi alielezea kuwa haki za mashoga nchini Kenya, ‘‘si suala muhimu,’” alisema Lorna Dias, Mratibu Mkuu wa shirika la Gay and Lesbian Coalition of Kenya, shirika linaloleta pamoja mashirika mengine kama PEMA Kenya. “Jibu letu ni kwamba kuwa shoga ama msagaji si hoja, lakini kuumizwa kwa sababu ya jinsi ulivyo ni suala kubwa. Na serikali haiwezi kukwepa jukumu lake la kushughulikia vurugu dhidi ya jamii zetu.”

Tume ya Afrika Kuhusu Haki za Kibinadamu na Watu ilipitisha azimio la kihistoria la 275 katika mwaka wa 2014, ikizihimiza serikali kuzuia na kuadhibu aina zote za vurugu zinazowalenga watu kwa misingi ya kweli au kukisiwa ya hisia yao kimapenzi au utambulisho wa kijinsia.

“Ikiwa baadhi ya viongozi wa Kenya wamejaribu kuonyesha ushoga kama ‘’sio tabia ya kiafrika,’ azimio la Tume ya Afrika linatilia mkazo tabia ambayo imetajwa kwa muda mrefu na wanaharakati wa haki za kibinadamu Waafrika  -  kuwa ni vurugu na kutengwa ndiko sio tabia za Kiafrika,’’ alisema Daniel Bekele, Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Human Rights Watch. “Kenya inapaswa kuliunga mkono azimio hilo na iwalinde badala ya kuwanyanyasa walio wachache kimapenzi na kijinsia, katika pwani ya Kenya na popote vurugu dhidi ya wana LGBT inapatikana.” 

Your tax deductible gift can help stop human rights violations and save lives around the world.

Region / Country
Topic