(Nairobi) – Sera za afya za serikali ya Tanzania zinawanyima huduma za kutosha wanawake wanaovutiwa kimapenzi na wanawake wengine, wanaume wanaovutiwa kimapenzi na wanaume wengine, wanaovutiwa kimapenzi na jinsia zote, na wabadili jinsia wa kike/kiume (LGBT) pamoja na watu wengine ambao wako katika hatari zaidi ya kupata maambukizi ya VVU, zikihatarisha afya ya umma, Human Rights Watch imesema katika ripoti iliyozinduliwa leo. Tanzania inapaswa kuachana na sera hizi, kuacha ukamataji holela wa wana-LGBT, na kupiga marufuku upimwaji wa lazima wa njia ya haja kubwa ambao hutumika kama Ushahidi wa uongo wa vitendo vya mapenzi ya jinsia moja.
Ripoti yenye kurasa 95, “‘Tusipopata Huduma, Tutakufa’: Kuandamwa kwa LGBT na Kunyimwa Haki ya Afya Tanzania,” inanukuu namna ambavo, tangu mwaka 2016, serikali ya Tanzania imekuwa ikiwasaka wana-LGBT na mashirika ya kijamii yanayo wahudumia. Wizara ya Afya ya Tanzania bara imeyazuia mashirika ya kijamii kutoa mafunzo juu ya kujikinga na VVU kwa wanaume wanaofanya ngono na wanaume wenzao na makundi maalum mengine ambayo yapo hatarini zaidi kupata maambukizi ya VVU. Imevifungia vituo vya msaada ambavyo vinatoa upimaji wa VVU na huduma zingine maalum na jumuishi, na kupiga marufuku usambazaji wa vilainishi, ambavyo ni muhimu katika matumizi ya mipira ya kiume katika kujikinga na VVU kwa makundi maalum na jamii nzima kwa ujumla.
“Mamlaka za Tanzania zimeunda mashambulizi ya kimfumo dhidi ya haki za wana-LGBT, ikiwa ni pamoja na haki zao za afya,” amesema Neela Ghoshal, mtafiti mwandamizi wa haki za wana-LGBT wa Human Rights Watch. “Vitisho vya kutengeneza juu ya kile kinachoitwa ‘uchochezi wa mapenzi ya jinsia moja’ zimeondoa utendaji mzuri na ufanisi wenye ushahidi katika kuongoza sera ya VVU nchini Tanzania.”
Wizara ya Afya inadai kwamba huduma maalum na utoaji wa vilainishi vinahamasisha mapenzi ya jinsia moja. Inasema kwamba vituo vya afya vya umma vinatoa huduma bila ubaguzi hivyo hakuna haja ya kuwa na huduma maalum zinazotolewa na asasi za kiraia. Lakini utafiti wa Human Rights watch umegundua kwamba ubaguzi kwa misingi ya mwelekeo wa kijinsia na utambulisho wa kijinsia ni jambo la kawaida katika vituo vya afya vya serikali.
Utafiti unatokana na mahojiano yaliyofanywa na watu 35 waliojitambulisha kama Watanzania wana-LGBT kati ya Mei 2018 na Juni 2019. Ripoti hii pia imetokana na mahojiano rasmi na mazungumzo yasiyo rasmi na wanaharakati wa haki za LGBT wa Kitanzania, wanaharakati wa haki za binadamu na wanasheria kati ya mwaka 2014 na 2020, pamoja na majadiliano na wawakilishi wa mashirika zaidi ya 20 ya Kitanzania, kikanda na kimataifa ya afya na yale ya haki za binadamu na wataalamu, wafadhili na mashirika ya Umoja wa Mataifa.
Mamlaka za Tanzania pia zimekandamiza haki ya afya kupitia uvamizi wa polisi katika mikutano na mafunzo yaliyokuwa yakitolewa na wanaharakati wa haki na afya na washirika wao, ikiwa ni pamoja na mafunzo kuhusu VVU ambayo yanaweza kuokoa maisha, kuwakamata washiriki. Uvamizi umewapa hofu jamii ya wanaharakati na watoa huduma na wanufaika wao.
Mwezi Novemba 2018, wakati mkuu wa mkoa Paul Makonda alipotishia kukamata wanaume wote wanaovutiwa kimapenzi na wanaume wengine jijini Dar es Salaam, balozi na Benki ya Dunia walikataa. Matokeo yake, Rais Magufuli aliihakikishia Benki ya Dunia kwamba Tanzania haitafuata sera za namna hiyo. Lakini ukamataji na sera na matendo ya kibaguzi bado vimeendelea. Mwezi Aprili 2019, Bodi ya Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali iliyo chini ya serikali ilifutia usajili shirika la Community Health Education and Advocacy Services (CHESA), shirika muhimu linalohudumia wana-LGBT, kwa misingi kwamba lilikuwa “linachochea vitendo visivyo na maadili.” Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani Hamad Masauni alitoa wito hadharani wa kukamatwa kwa wanaume wote wanaovutiwa kimapenzi na wanaume wenzao alipokuwa akitembelea Zanzibar mwezi Septemba.
Polisi ilipofanya ukamataji chini ya sheria za Tanzania za kipindi cha ukoloni zinazokataza “ufanyaji mapenzi kinyume na maumbile,” kuna wakati wametoa maelekezo kwa watoa huduma za kitabibu kufanya vipimo vya lazima vya njia ya haja kubwa kukusanya “ushahidi” wa ngono kupitia njia ya haja kubwa. Vipimo hivi havina msingi wa kisayansi na ni aina ya ukatili, unyama na kitendo cha udhalilishaji ambao unaweza kutafsiriwa kuwa ni mateso.
Tanzania inatakiwa, kama mwanachama wa Mkataba wa Kimataifa juu ya Haki za Kiuchumi, Kijamii na Kitamaduni, kuchukua hatua kuhakikisha upatikanaji wa kiwango cha juu cha afya kwa watu wote. Ubaguzi kwa misingi ya muelekeo wa kingono na utambulisho wa kijinsia katika utoaji wa taarifa na huduma za afya haziruhusiwi chini ya sheria ya kimataifa. Tanzania ni mwanachama pia wa Jumuia ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), ambayo mwaka 2016 ilichapisha Viwango vya Chini vya VVU na afya vikizitaka nchi wanachama kuboresha upatikanaji wa huduma za afya na VVU kwa wana-LGBT.
Kamisheni ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu, katika Azimio la 275, lilizitaka serikali za Afrika kukomesha unyanyasaji na ubaguzi kwa misingi ya mwelekeo wa kijinsia na utambulisho wa kijinsia. Kamisheni ya Afrika imekemea wazi kabisa vipimo vya lazima vya njia ya haja kubwa kama aina ya mateso. Kukamata mtu kwa misingi ya kufanya kwa hiari mapenzi ya jinsia moja kati ya watu wazima wawili walio faragha ni ukiukwaji wa katazo la Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa juu ya ukamataji holela na uwekaji kizuizini.
“Mamlaka za Tanzania zinapaswa kuhakikisha kwamba hakuna Mtanzania hata mmoja anakamatwa kwa kuwa aidha mwanaume anayevutiwa kimapenzi na mwanaume mwenzake ama mbadili jinsia, au kwa kuhudhuria semina ya elimu juu ya masuala ya VVU,” alisema Ghoshal. “Hatua thabiti za mbeleni pia zinapaswa kuwa ni pamoja na kupiga marufuku upimwaji wa njia ya haja kubwa na kubadilisha sera za afya ili kwamba ziwe zinatokana na ushahidi, na si chuki.”
Baadhi ya Nukuu kutoka kwa Watu Tuliowahoji
“Osman,” mwanaume anayevutiwa kimapenzi na mwanaume mwngine, mwenye umri wa miaka 24 na muathirika wa VVU, juu ya kutafuta matibabu ya VVU katika hospitali ya serikali jijini Dar es Salaam, alisema:
[Waliniambia] “Wewe ni kijana mzuri, kwanini unafanya mapenzi ya jinsia moja? Ndio maana umepata UKIMWI, kwasababu hayo matendo yanamchukiza Mungu.” Waliniambia pia kwamba niache michezo hii na kuokoka, kumfukuza Sherani, anayenisababishia kufanya mapenzi ya jinsia moja, na kutafuta mke, nioe, na kuwa na familia.
“Medard,” mwanaume anayevutiwa kimapenzi na mwanaume mwenzake mwenye umri wa miaka 38 aishie jijini Dar es Salaam, juu ya kufungwa kwa vituo vya msaada rafiki kwa wana-LGBT, alisema:
Kila nilipokuwa na tatizo la kiafya, niliweza kwenda kwenye hivyo vituo kupata msaada au kuunganishwa na mtoa huduma za afya ambaye hakuwa mbaguzi, ambaye alinihudumia kama mtu mwingine yeyote. Siku hizi, hata kama nina tatizo la kiafya, sina sehemu ya kwenda ambapo naweza kuelezea tatizo langu, kwahivyo nanyamaza tu…… ningependa serikali ya Tanzania kuwaruhusu makuchu (wana-LGBT) kupata huduma za afya. Kama hatupati huduma hizi, tutakufa.
“Toni,” mwanamke aliyebadili jinsia aishie Dar es Salaam, juu ya kubadilika kwa maofisa wa afya wa serikali, alisema “Tulikuwa na mkutano na (maofisa wa afya wa serikali) na walisema hawataki kusikia chochote kuhusiana na masuala ya wana-LGBT. Walidai kwamba tunawaandikisha watu (kuwa wana-LGBT).”