Tarehe 4 Novemba 2018, baada ya matamko ya chuki kuripotiwa na vyombo vingi vya habari vya kimataifa, Wizara ya Mambo ya Nje ya Tanzania ilitoa taarifa kwamba kampeni ya chuki dhidi ya wapenzi wa jinsia moja iliyoanzishwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda ilikuwa ni “mawazo yake na sio msimamo wa serikali.” Wizara iliahidi “kuendelea kuheshimu na kulinda” haki za binadamu zinazotambulika kimataifa. Hata hivyo, siku hiyo hiyo, wanaharakati walieleza Human Rights Watch kwamba polisi kisiwani Zanzibar waliwakamata watu kadhaa kwa makosa ya kujihusisha na mapenzi ya jinsia moja.
“Inatia moyo kwamba serikali ya Tanzania imedhamiria kutunza wajibu wake wa kulinda haki za binadamu, ikiwa ni pamoja na zile zinazohusu mwelekeo wa kijinsia,” alisema Neela Ghoshal, mtafiti mkuu wa Human Rights Watch wa masuala ya haki za kijinsia (LGBT). “Lakini kauli hiyo ya serikali haitatoa ahueni yoyote kwa walio wachache kijinsia Tanzania ikiwa mamlaka nchini humo zinaendelea kuwakamata na kuwabagua.”
Makonda aliibua hofu miongoni mwa walio wachache kijinsia mnamo Oktoba 31, alipoitisha mkutano na waandishi wa habari ambapo alitangaza mpango wa kuwakamata wanaume wote wanaotuhumiwa wa vitendo vya mapenzi ya jinsia moja, na kuwafanyia uchunguzi kwa nguvu kupitia tundu la haja kubwa na kuwafanyia ushauri nasaha wa kuwabadilisha. Alisema angewakamata au kuwafukuza katika jiji, akitangaza, “Jijini Dar es Salaam, ushoga si haki ya binadamu.” Makonda aliwasihi watu kuwaripoti wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja katika vituo vya polisi, akidai kwamba tayari alikuwa amekusanya mamia ya majina ya watu hao.
Sheria za Tanzania dhidi ya mapenzi ya jinsia moja ni miongoni mwa sheria kali duniani, zikitoa adhabu ya kifungo kati ya miaka 30 hadi maishani kwa kufanya vitendo vya ngono “kinyume na maumbile.” Human Rights Watch na mashirika mengine huko Tanzania yanayotetea haki za walio wachache kijinsia, wamekusanya kesi nyingi za unyanyasaji wa polisi, vurugu kutoka kwa umma na kubaguliwa katika kupata huduma za afya katika ripoti yao ya mwaka 2013. Katika miaka miwili iliyofuata, kuna hatua chanya ambazo zimefikiwa. Mashirika ya serikali wanaodhibiti virusi vya UKIMWI nchini Tanzania yaliweza kuwafikia makundi maalum yaliyoathirika na virusi vya UKIMWI, na kuhakikisha kwamba yalikuwa yanashirikishwa katika maamuzi, huku mashirika ya afya ya kimataifa yakiongeza utoaji wa huduma za virusi vya UKIMWI kwa walio wachache kijinsia. Baadhi ya wanasiasa na maafisa wa polisi walionekana kuwa tayari kujadiliana kwa hili jambo. Mashirika mapya yakaanzishwa, ikiwa ni pamoja na yale yanayowawakilisha watu wenye jinsia tofauti na asili.
Hata hivyo, tangu kuchaguliwa kwa Rais John Magufuli mnamo Desemba 2015, heshima kwa haki ya kujieleza na kukusanyika imeporomoka nchini Tanzania, imesema Human Rights Watch. Matamko ya viongozi wa juu dhidi ya haki yameambatana na sheria kandamizi, unyanyasaji na ukamatwaji wa waandishi wa habari, wanasiasa wa upinzani na wakosoaji wa serikali, huku maendeleo juu ya maswala yahusuyo haki na afya ya walio wachache kijinsia yakirudishwa nyuma. Polisi wamevamia warsha kuhusu afya na haki za binadamu zinazowalenga walio wachache kijinsia na kuwakamata kiholela wahudhuriaji. Wamewakamata wanaume wanaotuhumiwa kuwa wana wapenzi wa jinsia lao barabarani, huku ikiripotiwa kwamba waliwalazimisha baadhi yao kufanyiwa vipimo vya nguvu kupitia njia ya haja kubwa, kipimo ambacho imepingwa kuthibitisha mahusiano ya ushoga na kuhesabiwa kuwa ni mateso na jumuiya ya Umoja wa Mataifa na Tume ya Afrika ya Haki za Kibinadamu na Haki za Watu.
Mamlaka zilifungia vituo vya afya vilivyokuwa vikitoa huduma kwa watu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja na kuzuia usambazaji wa vilainishi, kitu ambacho husaidia katika kuzuia maambukizi ya virusi vya UKIMWI. Walilisimamisha shirika moja lililoko Tanzania, na kuwahoji viongozi wake huku wengine wakiwekwa kizuizini na kuirudisha timu ya wanasheria nchini kwao Afrika Kusini, kwasababu tu ya kazi yao juu ya afya na haki za walio wachache kijinsia. Magufuli mwenyewe amenukuliwa akisema “hata ng’ombe” hawauungi mkono mapenzi ya jinsia moja.
Mkuu wa Mkoa, Makonda, amekuwa muungaji mkono mkubwa wa ukandamizaji huu. Katika mkutano wa hadhara mnamo Julai 2016, alitishia kuwakamata wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja na “wafuasi” wao katika mitandao ya kijamii na kufuta mashirika “yanayohamasisha mapenzi ya jinsia moja.” Katika mkutano wake na waandishi wa habari tarehe 31 Oktoba, Makonda alisema ametengeneza kikosi kitakacho tafuta wanaume wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja, wafanyabiashara wa ngono, wanaotengeneza filamu za ngono na wale wanaoendesha harambee za ulaghai katika mitandao ya kijamii.
Kampeni yake hii inaonekana ilitokana na video yenye maudhui ya ngono ya watu wa jinsia tofauti, lakini kiini cha mkutano wake na waandishi wa habari uliodumu kwa dakika 30 ulilenga katika kuamsha chuki dhidi ya wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja. Alitishia kuwapima wanaume wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja, kuwapatia ushauri nasaha kwa wale wanaotaka “kutoka kwa ushoga,” na kuwafunga wengine kifungo cha maisha, akisema kwamba kikosi chake kitaanza kazi Novemba 5.
Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje haisemi kinagaubaga ni kwa namna gani itachukua hatua za kuheshimu makubaliano ya kimataifa, ambayo sheria za Tanzania zinazopinga mapenzi ya jinsia moja na vitendo vingine vya unyanyasaji dhidi ya wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja zinayakiuka wazi wazi. Kamati ya Kutetea Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa, ambayo hutafsiri Mkataba ya Kimataifa ya Haki za Kiraia na Kisiasa, ambayo Tanzania imesaini, imeweka wazi kwamba kukamatwa kwa mtu kwa sababu ya mwelekeo wa kingono kunakiuka haki ya mtu ya faragha na haki ya kutobaguliwa. Tanzania pia imetia sahihi Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiuchumi, Kijamii na Utamaduni, ambao unalinda haki ya kupatiwa huduma ya hali ya juu ya afya, na kupinga ubaguzi katika kupata huduma hii kwa kigezo cha mwelekeo wa kingono.
“Ikiwa serikali inamaanisha kweli katika kukataa jumbe za Makonda za kupinga haki, inahitaji kuhakikisha kwamba watu wote nchini Tanzania wanafurahia haki sawa za binadamu bila kujali mwelekeo wao wa kingono ama utambulisho wao wa kijinsia,” amesema Ghoshal. “Hii ikiwa na maana ya kukomesha ukamatwaji na polisi na kulazimishwa vipimo kwa njia ya tundu la haja kubwa, kuyaruhusu mashirika yahusuyo wanaojihuisha na mapenzi ya jinsia moja na vituo vya afya vinavyotoa afya kwa wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja kuendelea kufanya kazi, na kuboresha sheria zinazoadhibu watu kwa jinsi walivyo au kutokana na wale wanaowapenda.”