Skip to main content

(Nairobi) - Mamia ya wanawake na wasichana waliobakwa wakati wa ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007-2008 nchini Kenya, wanateseka katika hali duni ya afya ya kimwili na kisaikolojia, umaskini, na kutengwa na jamii, shirika la Human Rights Watch lilisema katika ripoti iliyotolewa leo. Serikali ya Kenya haijatoa msaada wa kimsingi na haki kwa waathirika wa ubakaji.


Katika ripoti hiyo ya kurasa 104 "Naketi Tu na Kungoja Kufa: Fidia kwa Waathirika wa Unyanyasaji wa Kijinsia katika Ghasia za baada ya Uchaguzi wa 2007-2008 Nchini Kenya imejikita katika mahojiano na wanawake na wasichana 163, na waathirika 9 wa kiume. Wengine kati ya wanaume hawa  walishuhudia ubakaji au unyanyasaji mwingine wa kijinsia wakati wa ghasia hizo. Human Rights Watch liligundua kuwa wengi wa waathirika waliohojiwa walikuwa bado wanahitaji sana matibabu, hivyo kuwaacha katika hali ya kushindwa kufanya kazi au kuendelea na masomo, na kuwaongezea umaskini na njaa. Serikali, hivi majuzi iliahidi kutoa fidia, ambayo sharti iamuliwe kwa kushauriana na waathirika wa unyanyasaji wa kijinsia ili kuhakikisha kwamba wameshirikishwa vilivyo katika mipango yote.

Fatma W. na mtoto wake wa kiume mwenye umri wa miaka saba aliyezaliwa baada ya Fatma kubakwa na kundi la wanaume watatu katika nyumba yao, Nairobi. Wanaume wale walimshtaki kuwaficha  wanaume kutoka katika jamii/kabila “adui”. Aliacha kuenda shuleni baada ya kubakwa. Fatma alisema kuwa majirani zake humshutumu mtoto wake kwa kuwa alizaliwa kutokana na ubakaji.   © 2015 Samer Muscati/Human Rights Watch


"Tulishtuka tulipogundua idadi ya waathirika waliokuwa wagonjwa, wanaoishi katika umaskini na unyanyapaa, kupuuzwa na mara nyingi kukataliwa badala ya kusaidiwa na serikali," alisema Agnes Odhiambo, mtafiti mwandamizi wa haki za wanawake katika Afrika kwenye Human Rights Watch. "Ahadi ya hivi karibuni ya Rais Kenyatta yatoa fursa muhimu ya kuyashughulikia mahitaji ya waathirika wa unyanyasaji wa kijinsia za baada ya uchaguzi nchini Kenya."

Ghasia zilizoanza baada ya uchaguzi wa urais wa mwaka 2007 zilijumuisha mauaji ya kikabila na ulipaji kisasi uliotekelezwa na wafuasi wa chama tawala na vyama vya upinzani, na matumizi ya nguvu kupita kiasi na polisi dhidi ya waandamanaji. Takriban watu 1,133 walipoteza maisha yao na wengine 600,000 wakapoteza makazi yao. Maafisa wanasema kuwa angalau visa 900 vya unyanyasaji wa kijinsia vilitokea, lakini inawezekana kuwa idadi hii ni ndogo.


Wengi kati ya wale waliohojiwa walikuwa wamebakwa kikatili wakati wa ghasia, hasa katika magenge ya wabakaji zaidi ya 4 – zaidi ya 10 katika visa vichache. Wanawake walisema walipenyezwa sehemu zao za siri kwa bunduki, vijiti, chupa, na vitu vingine. Wengi walibakwa mbele ya wanafamilia wao, ikiwa ni pamoja na watoto wadogo. Baadhi ya wanaume na wavulana walitahiriwa au kuhasiwa kwa lazima. Washambuliaji walijumuisha wanachama wa vikosi vya usalama nchini Kenya pamoja na raia na magenge ya wanamgambo.

"Nilibakwa na wanaume watano—walikuwa wakinipiga, huku wakiivuta miguu yangu pande tofauti," alisema Njeri N. ambaye aliugua ugonjwa wa fistula, jeraha ambalo mara nyingi husababisha mkojo na kinyesi kuvuja na bado ana kidonda mguuni na maumivu mgongoni. "Niliumizwa sana. Nina tatizo la kudhibiti mkojo. Nina aibu sana."

Serikali ya Kenya imetoa fidia ndogo tu kwa watu waliopoteza makazi au mali yao, kwa kuwapa kiasi fulani cha fedha, makazi, na ardhi. Waathirika wa ubakaji na unyanyasaji  mwingine wa kijinsia, kwa kiasi kikubwa ,wametengwa, na ni machache sana yaliyofanywa kuyashughulikia mahitaji yao maalum ya kimatibabu au mengineyo.
 

Tulishtuka tulipogundua idadi ya waathirika waliokuwa wagonjwa, wanaoishi katika umaskini na unyanyapaa, kupuuzwa na mara nyingi kukataliwa badala ya kusaidiwa na serikali. Ahadi ya hivi karibuni ya Rais Kenyatta yatoa fursa muhimu ya kuyashughulikia mahitaji ya waathirika wa unyanyasaji wa kijinsia za baada ya uchaguzi nchini Kenya.
Agnes Odhiambo

mtafiti mwandamizi wa haki za wanawake katika Afrika

Mnamo Machi mwaka 2015, Rais Uhuru Kenyatta alitangaza mfuko wa shilingi bilioni 10 za Kenya (dola milioni 9.8 za Kimarekani) ili kutoa "haki yenye marekebisho" kwa waathirika. Mpango huu unaweza kuwa fursa muhimu kwa ajili ya waathirika wa ubakaji na unyanyasaji wa kijinsia, ikiwa mahitaji yao yatatambuliwa vizuri na utoaji wa fidia kufanywa kwa mujibu wa viwango vya kimataifa vya taratibu nzuri na matendo mema, Human Rights Watch lilisema. Serikali ya Kenya inahitaji kuipa kipaumbele mpango wa kuwatafuta waathirika ambao wanahitaji matibabu ya dharura na kukubaliana na kuweka sera mwafaka ili kuhakikisha kuwa wanapata huduma za kimatibabu bure na kwa hiari pamoja na zile za kisaikolojia na kijamii.

Waathirika wanaojitokeza, iwe wametambuliwa kama waathiriwa kufuatia ufanisi wa mashtaka au la, wanapaswa kupata utambuzi, fidia, na hakikisho kwamba watapewa ulinzi dhidi ya unyanyasaji kama huo tena. Mfuko huu haufai kutumiwa na serikali kama njia ya kuepuka uwajibikaji wa kijinai.

Baadhi ya wanawake na wasichana waliambukizwa Virusi vya Ukimwi na magonjwa mengine ya zinaa lakini wamekuwa maskini sana kuweza kusafiri ili kupata dawa za bure au kupata chakula cha kutosha ili kuwawezesha kunywa au kumeza dawa hizo.

Athari ya unyanyasaji huo kwa afya ya akili zimeharibu maisha. Katika karibu kila kisa, waathirika walielezea hisia kubwa za kutamaushwa, kujichukia, aibu, hasira, na huzuni, hisia ambazo mara nyingi ziliongezwa na kutengwa kwao kutokana unyanyapaa dhidi yao kama waathirika wa ubakaji. Baadhi yao waliwazia kujiua. Serikali haiwapi msaada wa kutosha wa huduma za kisaikolojia na kijamii.

Wanawake na wasichana pia wamekumbana na matatizo ya kifamilia au kijamii, ikiwa ni pamoja na kukataliwa na kutengwa, kama matokeo ya moja kwa moja ya kubakwa au unyanyasaji mwingine. Wengi hunyanyaswa vibaya kwa kutukanwa au kupigwa na waume wao au wanafamilia wengine.

Miongoni mwa wanawake waliohojiwa, 37 walisema kuwa walipata ujauzito kutokana na ubakaji. Wengi waliamua kujifungua kwa sababu uavyaji mimba ni kinyume cha sheria na huchukuliwa kama uvunjaji wa maadili nchini Kenya. Wanawake hawa mara nyingi hukabiliwa na hisia tata au hasira dhidi ya watoto wao ambao wenyewe pia wanakabiliwa na unyanyapaa, kukataliwa, na kupigwa au kutukanwa na familia zao. Baadhi ya watoto pia wamekuwa wakibaguliwa wakati wa kutafuta vyeti vya kuzaliwa kwani mama zao hawawezi kutoa majina ya baba zao. Kina mama hawa na watoto wao hawatambuliwi ipasavyo na serikali pamoja na watu wengine, na hata mahitaji yao maalum, ambayo yanastahili kushughulikiwa katika mchakato wa kufidiwa na kutendewa haki.

Ni watu wachache tu ambao wameshtakiwa kwa unyanyasaji wa kijinsia uliofanyika wakati wa mgogoro wa baada ya uchaguzi. Ripoti ya Tume ya Ukweli, Haki na Maridhiano iliyokamilika mwaka 2013 bado haijapitishwa na bunge. Matokeo ya uchunguzi kuhusu utovu wa nidhamu wa polisi, ikiwa ni pamoja na unyanyasaji wa kijinsia, wakati wa ghasia za baada ya uchaguzi, hayajawahi kutangazwa kwa umma.

"Serikali ya Kenya imekwepa wajibu wake kwa waathiriwa wa unyanyasaji wa kijinsia wa baada ya uchaguzi," Odhiambo alisema. "Ni muhimu sana kwa serikali kupanga kwa makini na kutoa fidia kwa waathirika hawa ili kupunguza mateso yao."

Your tax deductible gift can help stop human rights violations and save lives around the world.