(Nairobi) – Ukandamizaji wa vyombo vya habari, watetezi wa haki za binadamu na vyama vya upinzani umeongezeka nchini Tanzania tangu mwaka 2015, haya yamesemwa na Shirika na Kimataifa la Amnesty na Human rights Watch katika ripoti mbili tofauti leo.
Ripoti zote mbili zimebainisha kwamba serikali ya Rais John Magufuli imepitisha au kutekeleza mlolongo wa sheria kandamizi zinazo zuia uhuru wa uandishi wa habari na kupinga vikali shughuli za asasi zisizo za kiserikali na upinzani wa kisiasa.
“Wakati Rais Magufuli anaadhimisha miaka minne madarakani mwezi ujao ni lazima atafakari kwa umakini rekodi ya serikali yake kutengua mfumo wa haki za binadamu nchini humo,” alisema Rolande Ebole, mtafiti wa Shirika la Kimataifa la Amnesty Tanzania. “Serikali yake haina budi kufutilia mbali sheria zote kandamizi zinazotumika kuwabana wapinzani na kukomesha kwa haraka ukiukwaji wa haki za binadamu na dhuluma.”
“Tanzania inapaswa kuonyesha nia ya dhati ya kulinda na kutimiza haki ya uhuru wa kujieleza na ya ushirika,” anasema Oryem Nyeko, mtafiti wa Afrika kutoka Human Rights Watch. “Mamlaka inapaswa kukomesha unyanyasaji, vitisho na ukamataji holela wa wanaharakati, waandishi wa habari na wanachama wa upinzani.”
Ripoti kutoka Shirika la Kimataifa la Amnesty, “Gharama ya upinzani: Kuwindwa na Serikali,” na ile ya Human Rights Watch, “Kadiri ninavyokuwa kimya, nakuwa salama: Vitisho kwa Vyombo vya Habari na Asasi za Kiraia nchini Tanzania,” zilifanyiwa utafiti na kuandikwa tofauti lakini matokeo yake yanafanana. Taasisi zote zilifanya tafiti nchini Tanzania mwaka 2018.
Human Rights Watch ilifanya mahojiano na waandishi wa habari 80, waandishi wa blogu, wanasheria, wawakilishi wa asasi zisizo za kiserikali na wanachama wa vyama vya siasa. Shirika la Kimataifa la Amnesty lilifanya mahojiano na maafisa wa serikali 68, wawakilishi wa asasi zisizo za kiserikali na kiserikali, wanasheria, wanataaluma, viongozi wa dini, wanadiplomasia na kupitia maamuzi ya mahakama, sheria za nchi, motisi za serikali na maagizo.
Rais na maafisa waandamizi wa serikali mara kwa mara wametoa matamko yanayopingana na haki za binadamu na wakati mwingine kufuatiwa na kukamatwa kwa watu au kuvamiwa kwa taasisi. Matamko haya ya hatari yakifuatiwa na ukamataji holela na vitisho vya kufungia makundi ya asasi zisizo za kiserikali yamekwamisha utoaji taarifa ulio huru kutoka kwa waandishi wa habari na mijadala ya umma juu ya uvunjifu wa haki za binadamu na unyanyasaji ikiwa ni pamoja na muktadha wa uchaguzi ujao.
Matokeo ya tafiti zilizofanywa na taasisi zote yameonyesha mamlaka za Tanzania zimekiuka haki ya uhuru wa kujieleza, uhuru wa kushirikiana na uhuru wa vyombo vya habari kwa kusimamia sheria kandamizi mpya na zilizokuwepo na kanuni zinazosimamia vyombo vya habari, asasi zisizo za kiserikali na vyama vya siasa.
Tangu mwaka 2015, serikali imeongezeka udhibiti kwa kufungia au kufuta walau magazeti matano kwa kuandika maudhui yaliyoonekana kukosoa. Magazeti haya ni pamoja na gazeti mashuhuri la kila siku la Kiingereza, The Citizen, mwaka 2019 na magazeti mengine manne mwaka 2017. Tume ya Matangazo Zanzibar ilifungia kituo cha radio, Swahiba FM, mwezi Oktoba 2015 kwa kuripoti kufutwa na baadae kufanyika upya kwa uchaguzi wa mwaka 2015.
Mamlaka zilitumia sheria ya Mitandao ya mwaka 2015 kuwahukumu waandishi wa habari na wanaharakati kwa kuandika maudhui mbalimbali katika mitandao ya kijamii. Mwezi Novemba 2017 mahakama katika Jiji la Dar es Salaam ilimhukumu Bob Chacha Wangwe, mwanaharakati wa haki za binadamu kwa “kuchapisha habari za uongo” kwa mujibu wa sheria hii kutokana na kuiita Zanzibar koloni la Tanzania Bara katika ukurasa wake wa Facebook. Hukumu yake ilitenguliwa na Mahakama Kuu kwa maelezo kwamba mahakama haikueleza bayana viashiria vya makosa.
Kanuni za Mawasiliano ya Kieletroniki na ya Posta (Maudhui ya Mtandaoni) zilizopitishwa 2018 zinamtaka kila anaemiliki blogu au tovuti kulipa ada ya leseni hadi shilingi za kitanzania milioni 2.1 (zaidi ya Dola za Marekani 900). Sheria hii pia inadhibiti maudhui ya mtandaoni na kuruhusu uchunguzi wa mitandao bila usimamizi wa mahakama.
Serikali ya Tanzania pia inadhibiti utafiti binafsi na upatikanaji wa taarifa za takwimu kwa umma kupitia sheria ya Takwimu ya mwaka 2015, ambayo inawanyima wananchi vyanzo mbadala vya taarifa huru zilizothibitishwa. Wakati marekebisho ya sheria hii yaliyoletwa mwaka 2019 yameondoa dhima ya jinai kwa kuchapisha takwimu zisizo rasmi, mamlaka bado inadhibiti nani anayeweza kukusanya na kusambaza taarifa za takwimu na kuamua kipi ni sahihi au sio sahihi.
“Tunaona hali ya hatari ya ukandamizaji ikikuwa nchini Tanzania,” anasema Roland Ebole. “Mamlaka zinawanyima wananchi haki yao ya kupata taarifa kwa kutoa zile taarifa ambazo tu zimeidhinishwa na serikali.”
Mwaka 2018, Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) iliwaeleza Twaweza, taasisi iliyopo Tanzania, kwamba hairuhusiwi kuchapisha matokeo ya tafiti ya Sauti za Wananchi. Tafiti hiyo ilionyesha kupungua kwa umaarufu wa Magufuli kwa kiasi kikubwa mwaka 2018. Mwaka 2017, COSTECH na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi iliwazuia Human Rights Watch kuitishwa mkutano na waandishi wa habari juu ya ripoti yao iliyoainisha unyanyasaji wa watumishi wa ndani wa Kitanzania katika nchi za Oman na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).
Januari 2019, Bunge lilifanya marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa na kuweka vikwazo vingi zaidi vya haki ya uhuru wa kushiriki na kukusanyika kwa amani. Marekebisho haya yalimpa Msajili wa Vyama vya Siasa nguvu ya kufuta vyama vya siasa, kuitisha taarifa kutoka vyama vya siasa na kusimamisha wanachama. Pia ilianzisha hitaji la mashirika na watu binafsi kupata kibali kabla ya kutoa elimu ya uraia, jambo ambalo linazuia haki ya mwananchi kupata taarifa.
Mwezi Julai 2016, Magufuli alitangaza kupiga marufuku ya jumla shughuli zote za kisiasa mpaka 2020 kinyume na sheria za nchi. Marufuku hii imetekelezwa dhidi ya vyama vya upinzani pekee. Wanasiasa kadhaa wa upinzani wamekamatwa na kushtakiwa kwa mashtaka yasiyo ya ukweli.
Mwaka 2017, watu wasiojulikana walimpiga risasi mbunge wa upinzani, Tundu Lissu na mwaka 2018 watu wasiojulikana waliua maafisa wawili, Daniel John na Godfrey Luena, wote wa chama kikuu cha upinzani, Chadema. Ijapokuwa polisi wanasema wanafanya uchunguzi wa mauaji hayo, hakuna aliekamatwa mpaka sasa.
Serikali ya Tanzania haina budi kufutilia mbali mashtaka dhidi ya waandishi wa habari na wanasiasa ambao walikuwa wanatekeleza haki yao ya uhuru wa kujieleza na kushiriki, wanasema Shirika la kimataifa la Amnesty na Human Rights Watch.
“Sera na matukio kandamizi yamenyamazisha vyombo vya habari, kupandikiza hofu kwa asasi za kiraia na kuzuia usawa kwa vyama vya siasa kufanya siasa kuelekea katika uchaguzi,” anasema Nyeko. “Ikiwa bado mwaka mmoja tu kufikia uchaguzi, serikali hii inabidi ibadili vitendo vya unyanyasaji na kuonyesha nia ya dhati ya kulinda uhuru wa kujieleza, kushiriki, mikutano au makusanyiko ya amani kama yanavyolindwa na katiba na mikataba ya haki za binadamu ambayo Tanzania ni nchi mwanachama.”