(Nairobi) – Maafisa wa Polisi na wale wa kijeshi nchini Kenya wanawanyanyasa wanaharakati wa mazingira katika kaunti ya Lamu mkoani pwani, Shirika la kutetea haki za Kibinadamu - Human Rights Watch pamoja na Muungano wa Kitaifa wa Makundi ya kutetea haki za kibinadamu (National Coalition of Human Rights Defenders-Kenya) wamesema katika ripoti yao iliyotolewa hii leo.
Ripoti hiyo yenye kurasa 69, “Wanataka Kutunyamazisha: Unyanyasaji dhidi ya wanaharakati wa mazingira katika mkoa wa pwani” (They Just Want to Silence Us: Abuses Against Environmental Activists at Kenya’s Coast Region) inaelezea muktadha wa kampeni za uanaharakati katika kupinga ujenzi wa bandari ya Lamu na mradi wa barabara ya kutoka Kenya hadi Sudan Kusini na Uhabeshi, mradi ujulilikanao kama (The Lamu Port-South Sudan- Ethiopia Transport corridor project-LAPSSET) na miradi nyingine inayohusiana nayo . Ripoti hiyo inajumulisha nyaraka zinazo-onyesha vikwazo ambavyo wanaharakati wanakumbana navyo wanapotoa matamshi yao ya wazi kuhusu hofu yao katika mradi huo.
Takriban wanaharakati 35 wanaofanya kampeni dhidi ya miradi hii mikubwa kwenye ukanda huu ya barabara na ile ya bandari ya Lamu wamekabiliwa na vitisho, kupigwa, kukamatwa kiholela na kuzuiliwa.
“Serikali ya Kenya inapaswa kuangazia athari katika mazingira na yale ya kiafya ambayo huenda yakatokana na mradi wa LAPSSET, badala ya kuwanyanyasa wanaharakati wanaozungumzia maswala hayo,” alisema Otsieno Namwaya ambaye ni mtafiti katika shirika la Human Rights Watch anayehusika na masuala ya bara la Africa. “Kuwanyamazisha wanaharakati hakuwezi kutoa suluhisho kwa wasiwasi uliopo kuhusu uwezo wa miradi hiyo ya Serikali kuathiri mazingira na afya ya wakaazi wa eneo hilo’’.
Mradi huo ambao ndio mkubwa zaidi katika eneo la Afrika Mashariki na Kati hadi sasa, unakusudia kujenga maeneo 32 ya kuegesha meli katika bandari ya Lamu , viwanja vitatu vya kimataifa vya ndege, barabara za magari na ile ya reli, miji mitatau ya kitalii pamoja na miradi mingine husika kama vile mradi wa umeme wa mkaa, unaofadhiliwa na kampuni mbili za kibinafsi Amu Power na Centum Investment. Mamlaka inayosimamia mradi huo inayojulikana kama LAPSSET Corridor Development Authority, ambayo inamilikiwa na Serikali ya Kenya, imetoa msaada wa ekari 394 za ardhi kwa ujenzi wa mradi huo wa umeme kutoka kwa mkaa.
Mnamo mwezi Mei na Agosti 2018, shirika la kutetea haki za kibinadamu la Human Rights Watch lilirekodi nyaraka za visa vya unyanyasaji, vitisho, na ukiukwaji mwengine dhidi ya takriban wanaharakati 35 katika kipindi cha miaka mitano iliopita. Katika visa vingi, wanaharakati walikamatwa ama hata kuzuiliwa kuhusiana na uanaharakati wao, na baadaye wakaachiliwa bila kufunguliwa mashtaka. Vikosi vya usalama vimevunja maandamano, kuzuia mikutano ya hadhara na kutoa vitisho, kukamata na kuwashtaki wanaharakati kwa mashtaka mbalimbali.
Katika takriban visa 15, maafisa wa polisi waliwatuhumu wanaharakati kwa kuwa na uhusiano na kundi la wapiganaji la Al-Shabab,kutoka Somalia. Vitendo hivi vilifanyika sana kati ya mwaka 2013 na 2016, huku serikali ikichunguza na kuyasaka mashirika ya haki za kibinadamu na wanaharakati katika eneo hilo lenye Waislamu wengi.
“Serikali imekuwa ikiwataja kama magaidi wanaharakati ambao wamekuwa wakipinga mradi huo,” alisema mwalimu mwenye umri wa miaka 32, ambaye amekuwa kifua mbele katika kuandaa mikutano ya kijamii kuhusu athari za kimazingira za mradi wa LAPSSET. “Polisi huwakamata na kuwazuia na hata kuwahoji wanaharakati kwa lengo la kuwatishia’’.
Huku serikali ikiendelea na utekelezaji wa mradi huo wa bandari ya Lamu, jamii katika Mwambao wa Pwani pamoja na mashirika yanayowaunga mkono wameendelea kuzungumzia wazi kuhusu athari za kiafya na zile za kimazingira zitakazotokana na mradi huo. Aidha, wameimarisha kampeni yao dhidi ya mradi wa umeme utakaozalishwa na mkaa , wakisema kuwa utachafua hewa na maji na hivyo basi kuathiri maisha ya wakaazi.
Wanaharakati wanasema kwamba mradi huo wa umeme utatoa moshi ulio na sumu mbalimbali na kuchafua bahari, hali ambayo inaweza kuwaua samaki na wanyama wengine wa baharini. Pamoja na hayo wanasema mradi huo utatoa jivu la mkaa ambalo huenda likawa na hatari ya kusababisha saratani kwa watu wanaoishi karibu na eneo hilo. Pia wana wasiwasi kwamba ujenzi wa bandari hiyo unaharibu mikoko na maeneo ya kuzalisha samaki na wanyama wengine wa baharini. Wanaharakati hao pia wameonyesha wasiwasi wao kuhusu hatua ya serikali kuchukuwa mashamba huku wamiliki wake wakikosa kulipwa fidia kufikia sasa, wakikabiliwa na hatari ya uchafuzi wa maji yao kutoka kwa uchafu mbali na mabadiliko ya hali ya hewa nchini yaliosababishwa na gesi ya kijani (greenhouse gas emissions).
Mwanaharakati mwenye umri wa miaka 34 ambaye amekuwa kifua mbele katika kuhakikisha kuwa raia wanashirikishwa katika kila uamuzi unaochukuliwa alikamatwa mnamo mwezi October 2015 katika kijiji cha Ndau na maafisa 10 wa jinai. Walimchukua na kumpeleka kwa ofisi ya naibu Kamishna wa kaunti wa eneo hilo ambapo alizuiliwa kwa saa chache. “Maafisa wa polisi baadaye waliniambia nikome kupinga miradi ya serikali kwa sababu ina lengo la kuwafaidi wakaazi”, alisema.
Serikali ya Kenya inafaa kuchukua hatua mwafaka za kuheshimu uhuru wa kujieleza, uhuru wa kufanya mikutano, na ule wa uhusiano. Pia Kenya inapaswa kuheshimu mikataba ya Kimataifa ya haki za kibinadamu katika muktadha wa maendeleo, kama wayanavyoshinikiza mashirika ya Human Rights watch na Muungano wa kitaifa wa makundi ya kutetea haki za Kibinadamu (National Coalition of Human Rights Defenders).
“Jinsi Serikali ya Kenya inavyowajibikia na kuyakabili maswala haya ya wanaharakati wa mazingira katika kaunti ya Lamu, ni jaribio na funzo kubwa katika jitihada za Kenya kuheshimu na kulinda haki za kibinadamu wakati wa Ujenzi wa miradi mikubwa ya maendeleo,” alisema Kamau Ngugi, Mkurugenzi mkuu wa Muungano wa Kitaifa wa Mashirika ya kutetea haki za Kibinadamu (National Coalition of Human Rights Defenders). “Serikali ya Kenya ina wajibu wa kuheshimu jukumu la wanaharakati na kuheshimu haki za kibinadamu kama ilivyo katika mikataba ya kimataifa”, alimalizia.