- Wanaharakati wanaopinga kawi inayotokana na mafuta na watetezi wa mazingira nchini Uganda wanakabiliwa na unyanyasaji wa mara kwa mara, ikiwa ni pamoja na kukamatwa kiholela kwa sababu ya kupinga mpango wa ujenzi wa bomba la mafuta.
- Mradi huo umeharibu maisha ya maelfu nchini Uganda na utazalisha hewa ukaa kwa miongo kadhaa na kuchangia katika changamoto ya kimazingira duniani.
- Serikali ya Uganda haina budi kuheshimu haki za wanaharakati na kuondoa mashtaka ya jinai kwa watu wanaotumia uhuru wao wa kukusanyika na kujieleza.
(Nairobi) – Watetezi wa mazingira na wanaharakati wanaopinga kawi ya mafuta nchini Uganda mara kwa mara wamekumbana na vitendo vya kukamatwa kiholela, manyanyaso na vitisho kwa kupaza sauti dhidi ya mipango ya kujenga bomba la mafuta la Afrika Mashariki, Shirika la Human Rights Watch limesema katika ripoti iliyotolewa leo.
Ripoti hiyo yenye kurasa 22 kwa jina “‘Working On Oil is Forbidden’: Crackdown Against Environmental Defenders in Uganda” Kufanya kazi kwenye Mafuta kwakatazwa: Msako Dhidi ya Watetezi wa Mazingira Uganda inataja vikwazo vya Serikali ya Uganda juu ya uhuru wa kujieleza, kujihusisha na kukusanyika kuhusiana na shughuli za mafuta ikiwa ni pamoja na Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP). Asasi za Kiraia na watetezi wa mazingira mara kwa mara wameripoti kunyanyaswa na kutishwa, kutiwa kizuizini kinyume cha sheria au kukamatwa kiholela.
“Msako huu umesababisha kuwepo kwa mazingira magumu yanayotatiza uhuru wa kujieleza na kuzungumzia mojawapo ya miradi tata ya uchimbaji mafuta duniani,” anasema Felix Horne, mtafiti mwandamizi wa mazingira Shirika la Human Rights Watch. “Serikali ya Uganda yafaa kukoma mara moja kuwakamata hiholela wanaharakati wanaopinga mradi wa bomba la mafuta na kulinda haki zao za kujieleza kuambatana na kanuni za haki za binadamu kimataifa.”
Human Rights Watch walilifanya mahojiano na watu 31 nchini Uganda kati ya mwezi Machi na Oktoba 2023 wakiwemo watetezi 21 wa mazingira.
Bomba hili la mafuta ni miongoni mwa miradi kwenye miundombinu mikubwa ya kawi ya mafuta ambalo ujenzi wake unaendelezwa kwa sasa ulimwenguni. Mpango huo utahusisha mamia ya visima, mamia ya kilomita za barabara, kambi na miundombinu mingine na bomba la mafuta lenye urefu wa kilomita 1,443. Bomba hilo litakuwa ndilo refu duniani lenye mafuta yasiyosafishwa yenye kupashwa moto na litaunganisha visiwa vya Uganda magharibi na bandari ya Tanga -mashariki mwa Tanzania.
Kampuni ya Ufaransa ya mafuta TotalEnergies ndiyo mwenye hisa mkuu na ina ushirikiano na Kampuni ya Uchina- National Offshore Oil Company (CNOOC). Kampuni hizi mbili za kigeni zinashirikiana na kampuni za mafuta za Uganda na Tanzania.
Jopo la Serikali mbalimbali kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (IPCC), ambalo ndilo lenye mamlaka makuu duniani kuhusu sayansi ya tabianchi na mashirika wengine wameonya kwamba ikiwa dunia inataka kufikia malengo ya Mkataba wa Paris na kupunguza madhara ya mabadiliko ya tabianchi ni lazima kukoma kujenga miradi mipya ya uchimbaji mafuta.
Wanaharakati wanapinga ujenzi wa bomba la mafuta na namna watu wanaoathirika kwa mradi huo wanavyoshughulikiwa. Zaidi ya watu 100,000 Uganda na Tanzania watapoteza ardhi zao kwa ajili ya mradi huu. Wanaharakati wengi wamewaambia Human Rights Watch kuwa mwendelezo wa vitisho kutoka serikali na maafisa wa usalama unafanya kazi ya kusaidia wale wanaopoteza ardhi kuwa ngumu zaidi.
Mamlaka nchini Uganda zimekuwa zikiwatia kizuizini na kuwakamata wanaharakati na watetezi wa haki za binadamu kwa mashtaka ya kisiasa. Mtetezi wa Mazingira, Maxwell Atahura anaelezea alivyokamatwa mwaka 2021 katika eneo la Bullisa: “[Polisi] waliniuliza maswali kuhusu mafuta … kuna wakati waliniita gaidi, mhujumu wa mipango ya serikali … mwishowe walianiandikia dhamana ya polisi kwa kosa la kukusanyika kinyume cha sheria.” Atahura pia alisema amekuwa akipokea vitisho na mwishowe alihamia Kampala kwa usalama wake.
Rais Yoweri Museveni, mtetezi mkubwa wa bomba la mafuta la EACOP alitahadharisha kuwa “hatoruhusu yoyote kuleta mchezo … [na mafuta yake].”
Tangu Oktoba 2021, watu 30 waliopinga au kujaribu kuangazia madhara ya miradi ya mafuta wamekumbana na visa vya kukamatwa kisiasa Kampala na maeneo mengine Uganda. Mwaka 2021, serikali iliyafunga mashirika yasiyo ya serikali 54 kwa kile kilitajwa kuwa makosa ya kutumia lugha mbadala kinyume cha Sheria ya Mashirika yasiyo ya serikali 2016. Mashirika hayo yalijumuisha yale yanayohusika kwenye sekta ya mafuta na masuala mengine ya mazingira. Mashirika ya ndani yanayoendelea kupinga mpango huo yanahudumu katika mazingira magumu huku serikali na maafisa wa usalama wakitoa shinikizo kwao kukomesha harakati zao, hupigiwa simu na kutembelewa kusitishiwa.
Kutokana na ugumu wa kushawishi sera za serikali baadhi ya makundi yasiyo ya serikali Uganda yameungana na washirika wao kimataifa kufungua kesi nchini Ufaransa dhidi ya TotalEnergies. Watu wawili waliosafiri kwenda Ufaransa kwa ajili ya kesi kusikilizwa mwezi Disemba 2019 baada ya kurudi wamekumbana na mwendelezo wa unyanyasaji kutoka kwa maafisa wa serikali na wa usalama.
Wanaharakati nchini Uganda wameukosoa mradi huu kutokana na madhara yake kwenye mazingira, jamii na mchango wake kwenye mabadiliko ya tabianchi.Wanaharakati wameikosoa Serikali kwa kuidhinisha mradi pamoja na makampuni ya kimataifa na yale ya Uganda ambayo yanajihusisha na ufadhili, bima, ujenzi na uendeshaji wa mradi.
Mashirika ya umma ya ndani ya nchi yamekuwa msaada mkubwa kuwasaidia watu ambao ardhi zao zimechukuliwa kwa ajili ya kujenga mradi huu wa bomba la mafuta waelewe utaratibu wa fidia na njia nyinginezo za kuwasaidia kupata fidia stahiki, Human Rights Watch wamesema.
Mwezi Julai Human Rights Watch waliripoti ukiukaji wa haki za binadamu unaohusishwa na utaratibu wa kuchukua ardhi kwa ajili ya mradi wa bomba la mafuta ikijumuisha masuala ya fidia pungufu na shinikizo kutoka kwa maafisa, vitisho vya kushtakiwa na vitisho kutoka serikali za mtaa na maafisa wa usalama kwa wale ambao wamekataa fidia iliyotolewa.
Katika barua ya Oktoba 23 iliyotumiwa Human Rights Watch, kampuni ya TotalEnergies ilijieleza kwamba inatambua “umuhimu wa kuwalinda watetezi wa Haki za Binadamu na wala haiungi mkono unyanyasaji dhidi ya watu wanaoandamana kwa amani kwa mujibu wa sheria kutetea haki za binadamu.”
Human Rights Watch pia wameiandikia Ofisi ya Taifa ya Mashirika Yasiyo ya Serikali Uganda, ofisi iliyopo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani, Shirika la Usalama wa Ndani na Jeshi la Polisi la Uganda lakini hadi leo barua hizo bado kujibiwa.
Kutokana na pingamizi zinazokumba mradi wa bomba la mafuta zinazoendeshwa na asasi za raia na wanaharakati wa maswala ya mabadiliko ya tabianchi nchini Uganda na maeneo mengine duniani, taasisi nyingi za kifedha na kampuni za bima zimeweka wazi nia yao ya kutoshiriki katika mradi huu. Mchakato wa kupata fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mradi bado haujakamilika ijapokuwa mwezi Machi, afisa wa TotalEnergies alisema kuwa kampuni inatarajia kukamilisha masuala ya fedha kufikia mwisho wa mwaka 2023.
“Ujenzi na uendeshaji wa EACOP unaweza kuwa na madhara makubwa kwa mazingira, haki za binadamu na unachangia katika changamoto ya mabadiliko ya tabianchi.” Alisema Horne. “Taasisi za fedha na kampuni za bima zinafaa kukataa kushiriki kwenye mradi wa bomba la mafuta Uganda kutokana na madhara ya mafuta kwenye mabadiliko ya tabianchi pamoja na hatari ya baadaye ya madhara makubwa kwa haki za binadamu.”