Skip to main content
Maafisa wa polisi, kwenye barabara ya Likoni, wakijaribu kuwatawanya wafwasi wa kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga wa muungano wa National Super Alliance (NASA). Walikuwa wakiwazuia wafwasi hao kufika eneo la kati la Jiji la Nairobi, Kenya, Tarehe 17 Novemba mwaka 2017.  © REUTERS/Thomas Mukoya

(Nairobi) – Maafisa wa polisi na magenge yaliyojihami yaliwaua yamkini watu 37 jijini Nairobi katika msimu wa marudio ya uchaguzi kati ya mwezi Septemba na Novemba mwaka 2017, shirika la kimataifa la haki za binadamu Human Rights Watch limesema leo. Wito unatolewa kwa serikali ya Kenya kuchunguza mauaji haya ya kinyume cha sheria na mengine yaliyotokea msimu mzima wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2017 ili kuhakikisha waliohusika wamechukuliwa hatua za kisheria.

“Serikali ya Kenya yafaa kuwajibikia dhuluma nyingi zilizotekelezwa msimu wa uchaguzi na hivyo kuchunguza kila kisa cha mauaji,” asema mtafiti wa Human Rights Watch tawi la Afrika Otsieno Namwaya. “Familia za waliouawa zafaa kupata haki.”

Katika msimu wa uchaguzi wa marudio, polisi waliwaua takriban watu 23 katika mitaa mbali mbali ya jiji la Nairobi, wengi wao wakiwa wafwasi wa upinzani. Aidha magenge yaliyojihami nayo yakawaua takriban watu 14 msimu huo. Uchaguzi wa kwanza wa urais ulifanywa tarehe 8 mwezi Agosti lakini matokeo yakatupiliwa mbali na Mahakama ya Juu. Aidha kufwatia maagizo ya Mahakama hiyo uchaguzi wa marudio kwa wadhifa wa urais ulifanywa tena tarehe 26 mwezi Oktoba. Rais Uhuru Kenyatta aliapishwa kuanza muhula wa pili mwezi Novemba.

Kati ya mwezi Novemba 2017 na Januari 2018, watafiti wa Shirika la Human Rights Watch waliwahoji watu 67, wakiwemo 30 jamaa ya waliouawa, mashahidi 27, watetezi wa haki 2, maafisa wa mashirika ya misaada 3 ambao walizisaidia familia za waathiriwa, viongozi wa jamii 3 na maafisa wa polisi 2 waliokuwa kazini msimu huo. Watafiti vilevile waliziangalia rekodi za hospitalini na maiti kwenye mochari, aidha walikagua ripoti 32 za mwanapatholojia mkuu wa serikali, na kuwahoji wakazi wa mitaa ya Muthurwa, Kawangware, Kibera, Mathare, Dandora, Kariobangi, Babadogo na Riverside jijini Nairobi.

Ripoti za mwanapatholojia mkuu zilionyesha kwamba waathiriwa wengi waliuawa kwa risasi zilizofyatuliwa kwa karibu kwa kutumia bunduki za kisasa. Kwa mujibu wa Shirika la Human Rights Watch mauaji mengi yalitokea wakati polisi wakiwakabili waandamanaji kwa kuwarushia vitoza machozi na kuwafyatulia risasi. Vilevile kulikuwa na hali ambapo polisi waliwapiga risasi wakazi waliokuwa wakiendesha shughuli zao au hata kuwafyatulia risasi vijana waliokuwa kwenye makundi mitaani.

Utafiti wa Shirika la Human Rights Watch kuanzia mwezi Agosti wakati uchaguzi wa kwanza ulifanywa umebaini kwamba maafisa wa polisi na magenge yaliyojihami yaliwaua zaidi ya watu 100 katika kipindi kizima cha uchaguzi mkuu. Kwenye ripoti ya pamoja ya mwezi Oktoba Mashirika ya Human Rights Watch na Amnesty International yalisema kwamba takriban watu 67 waliuawa kote nchini katika awamu ya kwanza ya uchaguzi mwezi Agosti. Wengi waliuawa kwa kupigwa risasi au kupigwa hadi kufa na maafisa wa polisi. Katika awamu ya pili ya uchaguzi, Shirika la Human Rights Watch limenakili mauaji ya watu 37 zaidi, mengi yakiwa yamefanywa na polisi katika mitaa ya jiji la Nairobi kama vile Embakasi, Kawangware, Dandora, Mathare, Kibera, Kangemi, Kariobangi na Riverside. Magenge yaliyojihami nayo yaliwaua wale ambao yalikuwa yakiwanasibisha na upinzani kutokana na jamii zao.

Wakazi wa Mathare, Nairobi, watoroka huku polisi wakifukuza waandamanaji wa upinzani, tarehe 12 Agosti. © 2017 Thomas Mukoya/Reuters

Wakati wa uchaguzi mkuu wa Agosti na wa marudio mwezi Oktoba, na hata siku zilizofwata, wafwasi wa upinzani jijini Nairobi, maeneo ya Pwani na Magharibi ya Kenya walipinga kile walichodai kuwa wizi wa kura. Muungano wa vyama vya upinzani National Super Alliance (NASA) uliitisha maandamano ya kila wiki kote nchini mwezi Septemba na Oktoba kushinikiza yafanyike marekebisho kwenye taratibu za uchaguzi huku ukiwashawishi wafwasi wake kupuuza uchaguzi wa marudio. Mwanzo mwanzo wa maandamano hayo polisi hawakuyaingilia na hivyo mengi yakafanywa na kumalizika kwa njia ya amani.

Hata hivyo katika miezi ya Oktoba na Novemba maafisa wa polisi walianza kuwakabili waandamanaji kwa kutumia nguvu huku wakiwafyatulia risasi baadhi yao na kuwapiga wengine hadi kufa. Kwenye baadhi ya oparesheni polisi walifanya misako ya nyumba hadi nyumba katika mitaa yenye wakazi wengi wakiwa wa jamii zinazojitambulisha na upinzani kama vile Kariobangi, Dandora, Mathare na Kibera. Kwenye misako hiyo polisi waliwaua baadhi ya wakazi kwa kuwapiga risasi huku wakiwajeruhi wengine vibaya kwa kuwapiga kitutu. Mojawapo ya siku zilizoshuhudia dhuluma hizi ni wakati kiongozi wa upinzani Raila Odinga alikuwa akirejea nyumbani kutoka ng’ambo tarehe 17 mwezi Novemba. Dhuluma nyengine zilifanywa wakati Mahakama ya Juu ilitoa uamuzi ulioidhinisha ushindi wa rais Kenyatta tarehe 20 mwezi Novemba na vilevile ile siku ya kuapishwa kwake tarehe 28 mwezi Novemba.

Kwa mujibu wa kanuni za kimataifa za haki za binadamu polisi wanaruhusiwa kuyatawanya makundi yanayokusanyika bila idhini ama kukomesha mikutano ya hadhara isiyo na kibali, lakini wanafaa kuzingatia kanuni zao za utendakazi ili wasitumie nguvu za kupita kiasi. Iwapo wanakabili hali inayowalazimisha kutumia nguvu, basi nguvu hizo zafaa kuwa za kiasi kinachokubalika kisheria. Wanafaa kutumia bunduki ama kufyatua risasi katika mazingira yanayotishia maisha yao wenyewe ama yanayotishia kuwajeruhiwa. Licha ya hiyo risasi hutumika tu wakati njia nyengine zilizopo zikiwa zimejaribiwa zote na kushindwa. Utumiaji risasi huruhusiwa tu wapo ndiyo njia ya mwisho na ya pekee ya kuokoa maisha.

Serikali yafaa kuanzisha uchunguzi wa mauaji yote yaliyofanywa na polisi na kuwachukulia hatua maafisa waliohusika mauaji hayo ya kinyume cha sheria. Vyombo vya sheria nchini Kenya vimekuwa vikichelea na kujivuta kuhusu kuanzisha uchunguzi hasa wa mauaji ambayo yamethibitishwa na kunakiliwa.

Katika taarifa ya tarehe 14 mwezi Novemba, Mamlaka ya kutathmini utendakazi wa polisi (IPOA), ilisema kwamba imechunguza mauaji ya watu wawili pekee yaliyofanyika wakati wa uchaguzi - kwanza ni kifo cha mtoto wa umri wa miezi 6- Samantha Pendo, ambaye alipigwa kichwani akiwa mikononi mwa mamaye nyumbani kwao katika mojawapo ya mitaa ya Kisumu. Mtoto huyo alifariki tarehe 15 mwezi Agosti. Vilevile Mamlaka ya IPOA ilisema imechunguza mauaji ya msichana wa umri wa miaka 9 kwa jina Stephanie Moraa, ambaye alipigwa risasi na polisi akiwa nje ya nyumba yao kwenye orofa ya tatu ya jengo la makazi katika mtaa mmoja wa Nairobi. Alifariki tarehe 12 mwezi Agosti. Mamlaka ya IPOA imependekeza uchunguzi wa kina ufanywe kuhusu mauaji ya wawili hao ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya makamanda wa polisi waliokuwa wakiongoza oparesheni za mitaa hiyo. Uchunguzi wa mauaji ya Pendo ulianza mjini Kisumu tarehe 15 mwezi Februari.

Shirika la Human Rights Watch limetuma nyaraka rasmi kwa Mamlaka ya IPOA na Idara ya Polisi. Waraka mmoja umetumwa mwezi Januari na mwengine mwezi Februari. Nyaraka hizo zinaomba habari zaidi kuhusu mauaji hayo na maelezo kuhusu hali ya uchunguzi ikiwemo orodha ya majina ya waathiriwa. Vilevile tuliomba nafasi ya mahojiano kufwatia waraka mwengine wa maombi uliotumwa mwezi Agosti. Hadi wakati wa kuandaa ripoti hii Mamlaka ya IPOA na msemaji wa polisi walikuwa bado kutupa majibu ya maombi hayo.

Mashirika ya haki za binadamu ya Kenya na yale ya kimataifa kwa mara kadhaa yametoa wito kwa rais wa Kenya Uhuru Kenyatta kutoa nafasi kwa waliohusika mauaji ya kinyume cha sheria msimu mzima wa uchaguzi kuwajibikia makosa yao. Ripoti ya Tume ya Taifa kuhusu haki za binadamu (Kenya National Commission on Human Rights) ambayo ni tume inayotoa nguvu zake katika katiba ya Kenya, ilisema mwezi Desemba kwamba takriban watu 97 waliuawa kote nchini wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2017. Shirika la Haki za binadamu lisolo la serikali Independent Medico-legal Unit (IMLU), lilinakili mauaji ya watu 36 kufanywa na polisi kote nchini kati ya mwezi Agosti na Novemba. Mashirika hayo mawili kwa pamoja yametoa wito kwa serikali kuhakikisha waliohusika wanachukuliwa hatua za kisheria.

Kwa upande wake rais Kenyatta hajakiri kwamba vyombo vya usalama vilihusika katika mauaji ya kinyume cha sheria. Vilevile hajaagiza uchunguzi ufanywe na badala yake amewapongeza polisi kwa kile alikitaja kuwa kazi nzuri hata bila kuelezea sababu za kuwapa sifa hizo. Tarehe 2 mwezi Desemba, Mkurugenzi wa Oparesheni katika idara ya polisi, Benson Kibui, aliandika waraka kwa niaba ya rais akisema “rais Kenyatta anapongeza idara ya polisi kwa kuwa wakakamavu wakati wa kutekeleza majukumu yao ya kuuhudumia umma msimu wa uchaguzi”

Shirika la Human Rights Watch limesema serikali ya Kenya ina jukumu la kuchunguza mauaji yote yaliyotekelezwa siku chache kabla ya marudio ya uchaguzi wa urais mwezi Oktoba na baada ya uchaguzi huo, yawe yalifanywa na maafisa wa polisi au magenge yaliyojihami. Serikali yafaa kuhakikisha kwamba uchunguzi wa kina umefanywa ili wote waliohusika ukiukaji huu wa haki washtakiwe.

“Rais Uhuru Kenyatta anafaa kuonyesha kwa vitendo kwamba anaunga mkono msukumo wa utawala unaoheshimu sheria. Anafaa kulaani waziwazi mauaji yanayofanywa kinyume cha sheria huku akiagiza uchunguzi wa kina ufanywe,” Amesema Namwaya. “Ukosefu wa uwajibikaji ni mojawapo ya matatizo yanayoikumba Kenya, maafisa wa serikali wanafaa kuanza kuwasilisha ujumbe kuwa wamejitolea kuhakikisha kwamba walioathirika wamepata haki.”


Uchaguzi wa urais

Kenya ilifanya uchaguzi mkuu tarehe 8 mwezi Agosti. Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ikamtangaza rais Uhuru Kenya kuwa mshindi. Tangazo hilo lilifanywa wakati madai ya wizi wa kura yalikuwa yameanza kutolewa. Tarehe 1 mwezi Septemba, kufuatia kesi ya kupinga ushindi huo iliyowasilishwa na Raila Odinga, Mahakama ya Juu iliutupilia mbali uchaguzi wa urais na kuagiza ufanywe upya. Uchaguzi mpya ulifanywa tarehe 26 mwezi Oktoba, lakini Odinga alikuwa amejiondoa mashindanoni akisema serikali haikuwa imefanya marekebisho yafaayo kwenye taratibu zinazosimamia uchaguzi sawa na alivyokuwa ameitisha ili uchaguzi uwe huru na haki. Tarehe 30 mwezi Oktoba, Kenyatta alitangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi wa Oktoba 26.


Tarehe 7 mwezi Novemba, Odinga alisafiri nje ya nchi wakati ambapo joto la kisiasa lilikuwa limeongeza hali ya wasiwasi nchini. Alirejea nchini tarehe 17 mwezi Novemba ambapo alikosoa na kukataa kuutambua ushindi wa Kenyatta. Kufikia tarehe 30 Januari aliongoza sherehe zisizorasmi za kuapishwa na hivyo kujitangaza kuwa ‘rais wa watu’. Serikali ilivikanya vyombo vya habari kupeperusha hafla hiyo moja kwa moja na hivyo kuzima runinga nne na zikasalia hivyo kwa siku kadhaa. Vilevile serikali ilianza misako iliyowalenga wanasiasa wa upinzani waliohusika katika sherehe za kumwapisha Odinga. Ikawatia nguvuni takriban 5 na kuwapokonya wengine 15 hati zao za kusafiri nje ya nchi huku ikiwapokonya ulinzi wabunge 100 wa upinzani.

Kenya imekuwa na historia ya kukumbwa na machafuko na mapigano misimu ya uchaguzi kuanzia mwaka 1992. Machafuko mabaya zaidi yalitokea baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007 yaliyosababisha mauaji ya takriban watu 1,100 huku zaidi ya watu 600,000 wakifukuzwa makwao. Ripoti ya mwaka 2008 ya Shirika la Human Rights Watch na ripoti nyengine za taasisi za serikali zimeilaumu idara ya polisi na magenge yanayojihami kwa vurugu na vifo ambavyo hutokea wakati wa machafuko haya. Mwaka 2008, ripoti ya Tume maalum iliyoteuliwa kuchunguza asili ya machafuko ya baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007 Commission of Inquiry into the 2007 Post Election Violence (CIPEV) ilisema kundi lililopigwa marufuku la Mungiki liliwaua huku ikiwapasha wengine tohara ya lazima wafwasi wa upinzani katika miji ya Naivasha na Nakuru.

Mauaji yaliyotekelezwa na polisi jijini Nairobi Oktoba na Novemba

Shirika la Human Rights Watch lilitafiti na kunakili mauaji yaliyofanywa na maafisa wa polisi katika siku zifuatazo; tarehe 26 mwezi Oktoba, siku ya uchaguzi wa marudio; tarehe 17 hadi 19 Novemba, kufwatia kurejea nchini kwa Odinga baada ya ziara yake ya siku 10 nje ya nchi; Novemba 20, wakati Mahakama ya Juu iliidhinisha ushindi wa Kenyatta; na Novemba 28, wakati Kenyatta aliapishwa. Mauaji mengi yalitekelezwa wakati wa maandamano, vilevile kwenye mikutano ya hadhara, huku mengine yakifanywa ile siku ya Odinga kurejea nchini ambapo polisi walizuia msafara wake wa kutoka uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta hadi katika eneo la kati la Jiji la Nairobi, mahala ambapo mkutano wa hadhara ulikuwa umepangwa kufanyika.

Mashahidi tuliosema nao walisema kwamba tarehe 17 mwezi Novemba, maafisa wa polisi waliokuwa wametumwa katika uwanja wa ndege na kwenye barabara za kuingia eneo la kati la jiji la Nairobi, waliwalenga risasi wafwasi wa upinzani waliokuwa wamejumuika kumkaribisha Odinga na kuwafyatulia. Kamera za televisheni za Kenya vilevile ziliwanasa maafisa wa polisi wakiyapiga mawe magari yaliyokuwa kwenye msafara wa Odinga.

Maafisa wa polisi vilevile waliweka vizuizi barabarani, wakalipua vitoza machozi kuwatawanya waandamanaji, huku wakiyafyatulia risasi makundi au kuwafyatulia watembeaji wengine barabarani.

Magenge yaliyojihami, ambayo mashahidi waliyaelezea kuwa yanayoiunga mkono serikali yalisababisha mauaji ya watu 14 .Shirika la Human Rights Watch liliyanakili haya kwenye rekodi zake, mengi yakiwa yaliyofanywa ile Ijumaa ya kurejea nchini kwa Odinga na kuendelea wikendi nzima.
Mashahidi wanane wa mauaji ya watu sita waliouawa na magenge walisema kwamba tarehe 17 mwezi Novemba, wanaume waliojihami walikuwa karibu na markiti ya Muthurwa na kwenye barabara ya Landhies. Walitapakaa hadi katika uwanja wa michezo wa City, eneo la mashariki ya Jiji la Nairobi. Magenge hayo yalikuwa yakiitisha vitambulisho huku yakiwatenga wale wanaofikirika kuwa wafwasi wa upinzani kwa sababu ya jamii zao. Magenge hayo yalikuwa yakiwapiga huku yakiwakata kwa panga. Mashahidi watatu walisema kwamba waliona magenge yakiburura maiti mbili hadi barabara ya Landhies iliyo umbali wa mita wa kati mita 100 na 200 kutoka kituo cha polisi. Magenge hayo yaliziacha maiti hizo ambazo baadaye zilichukuliwa na polisi.

Mashahidi watano walisema kwamba waliona watu wakiuawa mbele ya maafisa wa polisi na hata kuwaona polisi wakikusanya maiti bila ya kuwatia nguvuni wauaji. Mashahidi hao walidai kwamba magenge hayo yalikuwa ya wafwasi wa kundi lililopigwa marufuku la Mungiki, linalosemekana kuunga mkono serikali. Kundi hilo lilihusika pakubwa katika vurugu zilizokumba taifa baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007.

Yamkini watu wawili waliuawa katika siku zilizofwatia uchaguzi wa marudio. Asubuhi ya tarehe 26 Oktoba polisi walimuua kwa risasi Willis Ojenge, mwenye umri wa miaka 30 mwenyeji wa Homabay. Nduguye wa kambo, aliyekuwa akiishi naye wakati huo, alisema nduguye aliondoka nyumbani saa tatu asubuhi kwenda kununua bidhaa fulani na baadaye akajumuika kwenye maandamano. Anasema alimwona afisa wa polisi akiwa amenyanyua bunduki akimwandama Ojenge. Alipomfikia Ojenge alipiga magoti, lakini polisi huyo alimwagiza asimame akimbie na hapo ndipo alimpiga risasi kutoka nyuma.

Tarehe 31 Oktoba, polisi walimuua kwa risasi Philip Mutisya Musyemi, mwenye umri wa miaka 31. Aliuawa nje ya nyumba yake katika mtaa wa Riverside - Ruaraka. Babaye, aliyeshuhudia mauaji hayo, alisema kuwa Mutisya Musyemi alikuwa ameketi nje ya nyumba yao akiwa na marafiki. Maafisa sita wa polisi wa kukabili ghasia waliokuwa kwenye zamu ya ushikaji doria walifika na kudai kwamba Mutisya na wenzake walikuwa miongoni mwa waandamanaji. Waliwafyatulia risasi huku Mutisya akipigwa tumboni. Wote walilazwa katika hospitali ya Taifa ya Kenyatta wakiwa na majeraha ya risasi, Mutisya Musyemi alifariki kutokana na majeraha hayo tarehe 21 Novemba huku wenzake wakipona.

Mauaji mengi yalitekelezwa tarehe 17 mwezi Novemba wakati wafwasi wengi wa upinzani walikusanyika kwenye barabara mbali mbali jijini Nairobi kumkaribisha Odinga aliyekuwa akirejea nyumbani kutoka ng’ambo.

Saa tano asubuhi, hata kabla Odinga kuwasili nchini, inadaiwa afisa mmoja wa polisi alimpiga risasi Patrick Muasya, wa umri wa miaka 39, alipokuwa akiondoka kwenye umati karibu na kampuni ya magari ya GM, barabara ya Nairobi-Mombasa. Umati huo ulikuwa ukitoka upande wa uwanja wa ndege. Rafiki ya Muasya aliyekuwa naye wakati huo, alisema Muasya aliyekuwa mchuuzi jijini Nairobi na mkazi wa mtaa wa mapato ya chini wa Mukuru Kwa Reuben, alikuwa akielekea kwao mashambani wakati polisi walimpiga risasi mbavuni na akafa papo hapo.

Saa nane alasiri, maafisa wa polisi walimuua kwa risasi Tom Atura, wa umri wa miaka 30, aliyekuwa amejumuika kwenye maandamano katika mtaa wa Kawangware area 56. Wakati wa maandamano hayo makundi ya vijana yaliwasha mioto na kuweka vizuizi barabarani. Mtu mmoja jamaa ya Atura alisema polisi walionekana kuwalenga risasi waandamanaji na wakazi wengine. Walikuwa pia wakifyatua risasi kwenye makao ya watu na maduka. Ripoti ya mwanapatholojia mkuu wa serikali, ya upasuaji wa maiti, ambayo Shirika la Human Rights Watch linayo kwenye faili zake, inaonyesha kwamba Atura alipigwa risasi nne kichwani na kifuani.

Mashahidi kumi na mmoja waliliambia Shirika la Human Rights Watch kwamba takriban vijana sita waliuawa kwenye barabara ya Landhies wakati msafara wa Odinga ukiandamana na wafwasi wake ulikuwa ukielekea eneo la kati la jiji la Nairobi. Mfanyabiashara mmoja wa kike pale Muthurwa alisema kwamba kwenye kisa kimoja, ikiwa karibu saa kumi jioni, alishuhudia polisi wakimuua kwa risasi Evans Owino, mwenye umri wa miaka 23, mwanafunzi wa chuo ambaye alikuwa amejumuika na umati uliokuwa unamkaribisha Odinga. Polisi walimpiga risasi mgongoni akafa. Babaye Owino, aliiambia Human Rights Watch kwamba polisi ama Mamlaka ya IPOA haijawahoji walioshuhudia mauaji ya mwanaye

Mtu mmoja aliyeshuhudia mauaji msimu huo alisema maafisa wa polisi vilevile walimuua kwa risasi Elisha Osenyo, wa umri wa miaka 25, mfanyakazi ya sulubu kwenye miradi ya ujenzi, ikiwa saa kumi jioni. Ilikuwa dakika chache kabla msafara wa Odinga kupita. Binamu ya Osenyo alisema Osenyo alikuwa ameondoka nyumbani kwake Kangemi asubuhi kuelekea kazini lakini akapiga simu kuiambia familia yake kwamba alikuwa anarudi nyumbani kwa sababu ya kuongezeka wasiwasi jijini. Hakurudi nyumbani kwake akiwa hai. Rekodi za mochari zinaonyesha kwamba polisi waliiokota maiti yake kwenye barabara ya Landhies karibu saa tatu usiku na kuipeleka katika mochari ya City. Ripoti ya mwanapatholojia mkuu wa serikali inaonyesha kwamba Osenyo alipigwa risasi kwenye kwapa, likajeruhi moyo wake na hivyo akafa papo hapo.

Jioni ya tarehe 17 mwezi Novemba, polisi wa kukabili ghasia walimfyatulia kitoza machozi Kennedy Owino, mwanamume wa umri wa miaka 30 mkazi wa eneo la Katwekera mtaa wa Kibera. Kifaa hicho kilimgonga kifuani. Nduguye anasema Owino alifariki papo hapo. Owino alikuwa ametoka uwanja wa ndege akiwa na kakaye alipojipata kwenye maandamano katika mtaa wake, akiwa njiani kurejea nyumbani. Mtu mmoja aliyeshuhudia mauaji hayo ambaye alikuwa mmoja wa waandamanaji alisema afisa mmoja wa polisi wa GSU aliyekuwa mmoja wa kikosi kilichokuwa kwenye oparesheni alifyatua mkebe wa kitoza machozi moja kwa moja kifuani mwa Owino.

Watu wengine waliouawa na polisi tarehe 17 Novemba walikuwa Josephat Sakas, wa umri wa miaka 39. Jamaa zake na walioshuhudia kifo chake wanasema polisi walimuua kwa risasi kwenye barabara ya Landhies; aidha kuna Maurice Otieno Odipo, wa umri wa miaka 23, mkazi wa Kawangware. Walioshuhudia walisema polisi walimuua kwa risasi akiwa kwenye mzunguko wa barabara ya Landhies. Shirika la Human Rights Watch liliziona rekodi za mochari katika chumba cha city zilizoonyesha kwamba polisi walileta maiti nyengine tano usiku wa Novemba 17 (siku ya Odinga kurejea nchini).

Tarehe 19 Novemba, asubuhi ya saa mbili na nusu maafisa wa polisi walimuua kwa risasi Gabriel Onyango Obiero, wa umri wa miaka 35, mfanyakazi wa kampuni ya magari, kwenye barabara ya Outer ring. Mkewe alisema kulikuwa na hali ya wasiwasi katika eneo hilo baada ya vyombo vya habari kutangaza kwamba watu watano walikuwa wamepigwa risasi au kukatwakatwa na miili yao kutupwa kwenye barabara za mtaa wa Riverside -Babadogo. Onyango Obiero, aliyekuwa akihofu kwamba vurugu zitazuka aliondoka nyumbani saa mbili asubuhi kwenda kutoa pesa kwenye benki. Mmiliki duka kwenye barabara ya outer-ring aliyeshuhudia mauaji hayo alisema kwamba Onyango Obiero alikumbana na polisi waliokuwa wakiokota maiti za watu waliokuwa wameuawa na kuachwa barabarani, afisa mmoja wa kike alimlenga risasi na kumuua alipokuwa akitembea.
Maafisa wa polisi, kwenye barabara ya Likoni, wakijaribu kuwatawanya wafwasi wa kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga wa muungano wa National Super Alliance (NASA). Walikuwa wakiwazuia wafwasi hao kufika eneo la kati la Jiji la Nairobi, Kenya, Tarehe 17 Novemba mwaka 2017.  © REUTERS/Thomas Mukoya
Vilevile tarehe 19 mwezi Novemba, ikiwa saa kumi jioni polisi katika mtaa wa Mathare 4A walimuua kwa kumpiga risasi mwanafunzi wa shule ya upili Stephen Mbaluka Mbui, wa umri wa miaka 17. Alikuwa njiani kumtembelea mjombake mtaani humo. Jamaa mmoja jirani alimwona Stephen akiwapita maafisa wa polisi wa kukabili ghasia. Walikuwa wakipambana na waandamanaji katika mtaa huo, na akamwona mmoja wao akimlenga risasi. Ilimpiga kichwani kutoka nyuma. Mjombake alisema kwamba Stephen alifariki dakika chache baadaye akiwa amekimbizwa katika kliniki ya MSF mtaani Eastleigh. Kasi ya maandamano iliongezeka baada ya habari za mauaji ya kijana huyo, huku maafisa wa polisi wakianza kufanya misako ya nyumba hadi nyumba katika mtaa wa Mathare 4A. Kwenye misako hiyo waliwapiga wakazi na hasa wanaume huku wakiwajeruhi vibaya.

Tarehe 20 mwezi Novemba ikiwa saa tatu usiku mtaani Kariobangi, maafisa wa polisi walimpiga risasi kifuani Elvis Otieno Ogutu, wa umri wa miaka 30. Ogutu alikuwa mfanyakazi kwenye miradi ya ujenzi na alifariki papo hapo. Wakazi wa mtaa huo walisema kwamba mtaa mzima ulikuwa umewekwa doria kali ya maafisa wa polisi wa kuzima ghasia. Polisi hao walikuwa wameletwa wakitazamia fujo, na walikuwa tayari kuizima. Jamaa ya mwathiriwa alisema Otieno Ogutu alikuwa ameondoka nyumbani kwenda kununua bidhaa za matumizi ya kinyumbani. Kuuawa kwake kulipalilia hasira mtaani na kuchochea vurugu na hivyo kuwafanya polisi kuanza oparesheni za nyumba hadi nyumba ambapo waliwapiga na kuwajeruhi wakazi wengi mtaani humo.

Aidha tarehe 20 mwezi Novemba, afisa wa polisi anayehudumu katika kituo cha polisi cha Ayany alimuua kwa kumpiga risasi David Omondi Otieno, wa umri wa miaka 22, mtaani Olympic Kibera. Nduguye aliyeshuhudia mauaji hayo aliwaambia haya watafiti wa Human Rights Watch. Aidha kutokana na kuanza fujo mtaani punde baada ya Mahakama ya Juu kuidhinisha ushindi wa rais Kenyatta, Omondi alikuwa amefunga duka lake ili kuepuka vurugu na hapo ndipo polisi walimpiga risasi. Rekodi za maafisa wa polisi ambazo watafiti wa Human Rights Watch waliziona zinasema kwamba polisi walimpiga risasi alipokuwa akipora mali ya wenyewe. Ripoti ya mwanapatholojia mkuu wa serikali ilipata kwamba Otieno Ogutu aliuawa kwa risasi moja iliyopigwa kwenye paji la uso. Familia yake iliandikisha taarifa katika kituo cha polisi cha Industrial Area na vilevile katika Mamlaka ya IPOA. Hata hivyo haijafahamishwa kuhusu uchunguzi wowote kuanzishwa. Sawa na ilivyo desturi, idara ya polisi haijajibu maombi na maswali ya watafiti wa Human Rights Watch kuhusu mauaji haya. Na imekuwa ndiyo hali kwenye visa vyote vya mauaji vilivyoripotiwa msimu mzima.

Maandamano na wasiwasi wa kisiasa uliendelea kutawala katika maeneo mengi yanayojitambulisha na upinzani jijini Nairobi hadi wakati Kenyatta aliapishwa tarehe 28 mwezi Novemba. Siku hiyo, polisi waliweka vizuizi barabarani, wakalipua vitoza kuwatawanya waandamanaji huku wakitumia risasi kumzuia Odinga kukutana na wafwasi wake katika mitaa ya mashariki ya Nairobi.

Watafiti wa Human Rights Watch walipata kwamba, siku ile katika mitaa ya Embakasi na Donholm, polisi waliwaua kwa risasi takriban watu watatu ambao ni wafwasi wa upinzani. Miongoni mwa waliouawa ni mvulana wa miaka 7 kwa jina Geoffrey Mutinda ambaye alikuwa amesimama kwenye ukafu wa nyumba yao iliyokuwa kwenye orofa mtaani Embakasi. Wakazi na mashahidi walisema kwamba kuanzia asubuhi polisi waliendeleza oparesheni mtaani wakiyakabili makundi ya vijana wanaojitambulisha na upinzani ambayo yalikuwa yakiwasha mioto na kuweka vizuizi barabarani huku yakirusha mawe. Walioshuhudia pia walisema maafisa wa polisi wa kuzima ghasia walikuwa wakifyatua risasi kulenga makazi ya watu na vilevile kuwafyatulia wapita njia, na waandamanaji.

Asubuhi ya saa tano, polisi katika mtaa wa Kawangware 56 terminus walimuua kwa kumpiga risasi Faith Oduor Onyango, wa umri wa miaka 30, alipokuwa akinunua bidhaa za kinyumbani. Jamaa ya Faith aliyeshuhudia mauaji, alisema: “alikutana na polisi hatua chache kutoka mlango wa nyumba yake. Afisa mmoja akamlenga risasi na kumfyatulia tumboni.” Ripoti ya mwanapatholojia mkuu wa serikali ambayo watafiti wa Human Rights Watch, waliiona ilionyesha kwamba risasi ilimpiga tumboni na kupasua utumbo wake.

Waathiriwa wengine waliouawa tarehe 28 mwezi Novemba walikuwa Erick Ochieng, wa umri wa miaka 28. Mashahidi walisema aliuawa katika eneo la Embakasi. Aidha wakati Kenyatta alikuwa akiapishwa, Odinga alijaribu kuongoza mkutano wa hadhara katika eneo hilo la Embakasi lakini polisi walizingira eneo zima na kuwatawanya wafwasi wa upinzani kwa kutumia vitoza machozi huku wakiwapiga wengine kwa rungu.

Mauaji yaliyofanywa na makundi haramu yenye silaha

Mashahidi wa baadhi ya matendo dhalimu waliwaarifu watafiti wa Human Rights Watch kwamba makundi yaliyojihami, ambayo wanaamini, yalikuwa ya kuiunga mkono serikali yaliwashambulia wakazi wanaoaminika kuunga mkono upinzani. Makundi hayo yaliendesha oparesheni zao kwa kulenga jamii katika mitaa mbali mbali ya jiji la Nairobi. Walioshuhudia walisema makundi hayo yaliwazaba watu makofi, yaliwapiga mateke, kuwapiga kitutu na kuwakata kwa panga. Walioshuhudia waliyataja makundi hayo kuwa ya wanachama wa kundli lililopigwa marufuku la mungiki ambalo wanachama wake huhusika kwenye visa vya uhalifu jijini Nairobi, eneo la kati la Kenya na baadhi ya maeneo ya Rift Valley.

Shirika la la Human Rights Watch limenakili mauaji ya watu 14 ambayo yanakisiwa kufanywa na makundi hayo. Tarehe 16 mwezi Novemba, wakati ambapo hali ya wasiwasi ilikuwa imeanza kupanda kwa sababu ilikuwa imesalia siku moja kabla kuwasili kwa Odinga nchini, mashahidi wanasema makundi yanayoiunga mkono serikali yalimshambulia Martin Otieno Olot, wa umri wa miaka 33, usiku. Alikuwa dukani mwake kwenye barabara ya River road akichapisha shati tao za kutumiwa na wafwasi wa upinzani NASA.

“Kundi la vijana liliingia kwenye duka lake na kumpiga hadi akapoteza fahamu," alisema mmoja wa mashahidi aliyekuwa kwenye afisi moja iliyo karibu jioni ile. “Baada ya kumpiga walifunga mlango kutoka nje na kurusha bomu la petroli ndani ya duka hilo.” Nduguye mwathiriwa alisema kwamba licha ya Otieno Olot kuondolewa kwenye moto na zimamoto waliowasili baada ya kutokea mlipuko huo, alifariki siku tatu baadaye. Kifo chake kilitokana na majeraha ya moto na yale ya kukatwa kwa panga. Rekodi za hospitali zilionyesha kwamba alikuwa ameungua zaidi ya asilimia 86 ya mwili wake.

Mauaji mengi ya namna hii yalitokea kati ya tarehe 17 mwezi Novemba na tarehe 20. Jioni ya tarehe 17, katika markiti ya Muthurwa jijini Nairobi, kundi la vijana barubaru waliojihami walimshambulia Stephen Omondi, wa umri wa miaka 20 aliyekuwa mwanafunzi. Stephen alikuwa akiuza kwenye duka la wazazi wake. Jamaa ya Stephen aliyeshuhudia uvamizi huo alisema: “kundi hilo liliiburura maiti yake na kuitoa katika markiti hiyo na kwenda kuitupa kando ya barabara huku polisi wakishuhudia.”

Tarehe 17 mwezi Novemba, mashahidi walidai kwamba ikiwa saa nane alasiri kwenye barabara ya Jogoo, polisi walimuua kwa risasi Kennedy Odhong Obel, wa umri wa miaka 30. Jamaa ya Obel aliyekuwa akiishi naye alisema Odhong Obel alikuwa miongoni mwa kundi la mamia ya vijana waliojumuika kwenye mapokezi ya Odinga aliyekuwa amerejea nchini kutoka ng’ambo. Na licha ya mashahidi kudai kwamba waliona polisi wakimpiga risasi shingoni, ripoti ya mwanapatholojia mkuu wa serikali ilitofautiana na taarifa za mashahidi. Ripoti inaonyesha kwamba alifariki kutokana na majeraha ya kifaa chenye ncha kali kilichomkata shingoni.

Siku ile ile, katika mtaa wa Shauri Moyo mashariki ya Nairobi, jamaa wa mwathiriwa kwa jina Collins Owino, walisema Owino, wa umri wa miaka 33, fundi bomba, hakurejea nyumbani baada ya kazi. Mwenzake kazini aliyeshuhudia mavamizi hayo alisema wafwasi wa chama cha Jubilee waliojihami kwa panga walimkaba na kupima mazungumzo yake ili kujua jamii yake, halafu wakamkata hadi kufa: “Wafwasi wa chama cha Jubilee kwanza walimtaka azungumze kwa lugha ya Kikuyu. Aliposhindwa walianza kumpiga huku wakimkata kwa kutumia panga huku polisi wakitizama.”

Siku mbili zilizofwata, familia yake iliipata maiti yake katika mochari ya City jijini Nairobi. Maiti hiyo ilikuwa imepelekwa hapo na afisa mmoja wa polisi. Ilikuwa na majeraha ya panga kichwani na kwenye mikono. Ripoti ya mwanapatholojia mkuu wa serikali ilionyesha kwamba Owino alifariki kutokana na majeraha na vilevile kupoteza damu nyingi.

Siku iyo hiyo, kundi la vijana waliojihami, ambalo mashahidi wanadai kuwa ni la kuunga mkono chama tawala cha Jubilee lilimuua John Omondi Ojwang, wa umri wa miaka 33, makanika karibu na markiti ya Burma. Aliuawa katika eneo lisilo mbali na kituo cha polisi cha Kamukunji, mashariki ya Nairobi. Watu wawili wa familia hiyo na mashahidi watatu, walisema magenge ya vijana yanayoiunga mkono serikali yaliwaua Kennedy Okoth Barasa, wa umri wa miaka 30, na Mary Atieno, wa umri wa miaka 31, wote wakiwa wakazi wa Kibera. Watu hao wawili walikuwa wamejumuika na umati ulioelekea katika uwanja wa ndege kumpokea Odinga aliyekuwa anarejea nchini kutoka ng’ambo. Wallivamiwa walipokuwa njiani kurejea nyumbani. Walioshuhudia walisema, wawili hao walifariki kutokana na majeraha waliyopata kwa kupigwa.

Shahidi mmoja alisema kwamba kijana mmoja mfwasi wa chama tawala alimvamia na kumpiga Kennedy Okoth Barasa, karibu na uwanja wa michezo wa City. Kennedy alifariki siku nne baadaye. Ripoti ya mwanapatholojia mkuu wa serikali ilionyesha kwamba kifo chake kilitokana na kuvuja damu nyingi kwa ndani. Jamaa ya mwathiriawa aliyekuwa na Atieno alisema naye alipigwa hadi kufa alipokuwa njiani kurejea nyumbani kwake katika mtaa wa Kibera.

Tarehe 19 mwezi Novemba, vyombo vya habari nchini Kenya viliripoti kwamba maiti za watu wanne, wakazi wa mitaa ya Riverside, Babadogo na Dandora zilipatikana kwenye barabara za mitaa huku ikiibuka kwamba zilikuwa za watu waliokuwa wameuawa na watu wasiojulikana. Wakazi wa mtaa, na bawabu mmoja aliyeepuka shambulizi la alfajiri waliwaambia watafiti wa Human Rights Watch kwamba waliomwona mtu mmoja aliyekuwa akipima wakazi kwa kusema nao lugha fulani huku akiwaua wale walioshindwa kuizungumza. Bawabu huyo alisema “Kwanza alinisalimu kwa lugha ya Kikuyu na nilipojibu kwa Kiswahili alinivamia kwa upanga,” alisema Bawabu “Alikuwa akimfyatulia risasi au kumkata mlengwa kwa upanga hasa iwapo aliyeshindwa kumjibu kwa lugha yake ya mama. Machoni mwake, yeyote aliyeshindwa kuzungumza lugha yake alikuwa mfwasi wa NASA.”

Siku ile ile katika mtaa wa Korogocho, mashahidi walisema watu wanaodaiwa kuwa wafwasi wa chama cha Jubilee walimuua kwa kumpiga George Owino Odhiambo, wa umri wa miaka 40. Nduguye mwathiriwa alisema kundi hilo baadaye liliirusha maiti yake katika daraja jipya la Kariobangi-Huruma kwenye barabara iliyojengwa upya ya Outering: “Tulipoiokota maiti yake, mifupa yote mwilini ilikuwa imevunjika –mikono yote, miguu, na mgongo ilikuwa imevunjika kutokana na kuanguka. Vilevile alikuwa na majeraha ya kukatwa kwa panga mwili mzima.”

Hapa na pale, makundi yaliyojihami yanayounga mkono upinzani yalikabiliana na wafwasi wa chama tawala, au kuwavamia. Tarehe 17 mwezi Novemba, punde baada ya vurugu za siku hiyo ambapo polisi walikuwa wamewaua watu kadhaa, kundi la vijana wanaojitambulisha na upinzani lilimuua Patrick Baariu Kathure, mfanyabiashara wa umri wa miaka 25, katika mtaa wa Viwandani (Industrial Area). Shangaziye alielezea namna ya majeraha yake punde walipoipata maiti yake katika mochari ya Hospitali ya kimishonari ya Matter: “Panapofaa kuwa na jicho la kushoto palikuwa na shimo. Jicho lilikuwa limeng’olewa. Shingoni pia kulikuwa na shimo lililokatwa huku kwenye mashavu kukiwa na majeraha ya kukatwa kwa panga.”

Shahidi mmoja alisema kundi lililojihami la vijana wanaojitambulisha na upinzani lilimuua George Mwambura, mfanyabiashara wa umri wa miaka 34, usiku wa tarehe 19 mwezi Novemba mtaani Dandora. “George alikuwa na majeraha mabaya mkononi, mgongoni, begani na upande mmoja wa kichwa chake” Babaye George alisema: “meno yake yote yalikuwa yameng’olewa.”

Shirika la Human Rights Watch bado kuthibitisha ni makundi yapi yalikuwa yakihusika dhuluma na uovu huu msimu mzima wa uchaguzi. Shirika la Human Rights Watch vilevile halijapata ushahidi wowote unaonyesha kwamba idara ya polisi imeanzisha uchunguzi dhidi ya makundi haya na shughuli zao za msimu wa uchaguzi. Mwezi Agosti, Waziri wa Maswala ya ndani, Fred Matiang’i, alikanusha habari za vyombo vya habari kwamba magenge yanayoiunga mkono serikali yaliwavamia wakazi wa mitaa yenye wafwasi wengi wa upinzani jijini Nairobi na badala waziri huyo akatisha kuwatia nguvuni wale waliokuwa wakitoa madai hayo.

Your tax deductible gift can help stop human rights violations and save lives around the world.

Region / Country