- Vikosi vya usalama vya Tanzania vimechukua hatua kali dhidi ya maandamano wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa 2025 na kuua na kujeruhi watu ambao hawakuwa wakishiriki kwenye maandamano.
- Kuhusiana na utafiti wa awali kuhusu mauaji hayo, Shirika la Uangalizi wa Haki za Binadamu linaamini kwamba mamia ya watu wanaweza kuwa wameuawa nchini kote.
- Mamlaka za Tanzania zinatakiwa kutambua kwamba kinga kwa ukiukwaji wa haki za binadamu inahamasisha vurugu zaidi za kisiasa. Wanatakiwa kukomesha ukandamizaji wa kisiasa unaoendelea na uzuiaji wa wakosoaji wa serikali,vyama vya kiraia na vyombo vya habari.
(Nairobi) - Vikosi vya usalama Tanzania katika operesheni kali ya kudhibiti maandamano wakati na baada ya uchaguzi mkuu uliopingwa wa 2025 waliua na kujeruhi watu ambao hawakuwa wakishiriki kwenye maandamano hayo,Shirika la Uangalizi wa Haki za Binadamu limesema leo.
Shirika la Uangalizi wa Haki za Binadamu limehifadhi mauji ya watu 31 ambao hawakuwa wakishiriki kwenye maandamano na walipokea taarifa nyingine za kuaminika za vifo hivyo. Kuhusiana na utafiti wa awali katika idadi ya watu waliokufa nchi nzima, Shirika la Uangalizi wa Haki za Binadamu linaamini kwamba mamia ya watu waliuwawa. Tume ya Taifa iliyoundwa kuchunguza matukio ya machafuko yanayohusiana na uchaguzi inatakiwa kuchunguza haya na ukiukwaji mwingine, na kuhakikisha uwajibikaji.
“Ukandamizaji mkali wa mamlaka ya Tanzania dhidi ya upinzani wakati wa uchaguzi uliharibu maisha ya watu wengi",alisema Oryem Nyeko, mtafiti mkuu wa Afrika katika Shirika la Uangalizi wa Haki za Binadamu,"Tume ya uchunguzi inatakiwa itoe haki kwa waathirika na uwajibikaji na ihakikishe kwamba machafuko kama hayo hayatokei tena."
Kufuatia wiki za kuchochea maandamano dhidi ya ukandamizaji uliozidi wa kisiasa, waandamanaji walionekana katika mitaa ya Dar es salaam na majiji mengine siku ya uchaguzi wa raisi na wabunge,mwezi Oktoba, 2025. Maafisa wa polisi walitumia vipigo, nguvu za ziada na mabomu ya machozi kuwatawanya waandamanaji na kulazimisha watu kufungiwa ndani nchi nzima kwa siku tano, wakiwaua na kuwajeruhi wengi ikiwa ni pamoja na watu ambao hawakuwa wanaandamana. Katika matukio mengine, mashahidi walisema, jeshi na maafisa wa polisi waliweka vizuizi vya barabarani na kuzuia majeruhi kufika hosipitalini. Baadhi yao walikufa.
Kati ya Oktoba 2025 and Februari 2026, Shirika la Uangalizi wa Haki za Binadamu liliwahoji watu 48, pamoja na mashahidi 34, waandishi wa habari 7, na wanachama wa mashirika ya kiraia pamoja na wanaharakati, katika mikoa 6 ya kiutawala- Arusha,Dar es salaam, Geita, Mwanza, Ruvuma na mjini magharibi huko Zanzibar, n kupitia nyaraka za mahakama na taarifa za vyombo vya habari. Watafiti walichambua picha 15 na video zilizotumwa kwa watafiti na mashahidi au kuchapishwa kwenye mitandao ya kijamii na kuthibitisha maelezo ya mashahidi.
Maafisa wa polisi waliokuwa wakitekeleza agizo la kutotoka ndani kwa nchi nzima walipiga na kuwafyatulia raia risasi, wakiwemo wafanyabiashara katika soko la Buhongwa, katika mitaa ya Mwanza, asubuhi ya Oktoba 30, na kuwaua angalau saba na kujeruhi wengine takriban 50, kulingana na mashahidi. "Polisi walikuwa wanapiga risasi moja kwa moja kwa kundi lolote la watu," shahidi mmoja alisema.
Mnamo Oktoba 30, mwanaume wa miaka 31 alisema kuwa maafisa wa polisi waliokuwa wanashughulikia maandamano huko Songea, kusini-magharibi mwa Tanzania, walimpiga risasi mida ya saa kumi jioni alipokuwa akirudi kutoka kazini: "Kwa sababu risasi zilipigwa hovyo, ungeweza kusikia tu mlio wa risasi wakati mwingine juu au ukipita chini. Kwa hivyo, sikusikia mlio wa risasi, bali nikashituka kukuta mguu wangu ukiwa umekufa ganzi."
Mamlaka ilikamata zaidi ya watu 2,000, wakiwemo watoto, wakiwashutumu wengi kwa uharibifu wa mali za serikali na uhaini, ambao adhabu yake ni kifo. Sheria za kimataifa zinakataza kukamatwa na kushikiliwa kiholela.
Mwanaume wa miaka 39 anayefanya kazi kama dereva wa boda boda alisema polisi jijini Dar es Salaam walimkamata Oktoba 30 alipokuwa akipeleka mteja. Alisema walimshutumu kwa uongo kushiriki katika maandamano, walimpiga vibaya, na kumshtaki kwa uhaini.
Hatimaye aliachiliwa pamoja na mamia ya wengine mnamo Desemba 24, baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kusema kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma apitie kesi za waliokamatwa. Dereva huyo alisema kuwa hawezi kufanya kazi kutokana na majeraha ya mguu yaliyosabaishwa na kupigwa.
Kufutia shinikizo la kimataifa, mnamo Novemba 18, Ofisi ya Rais iliunda "tume huru" yenye wakuu wa zamani na watumishi wa umma waliostaafu ili "kuchunguza matukio yaliyosababisha uvunjaji wa amani wakati na baada ya uchaguzi mkuu." Haijaeleweka wazi kama wigo wa tume unahusisha watu waliouawa au kujeruhiwa wakiwa hawashiriki maandamano na kukamatwa kiholela. Tume imepangwa kumaliza kazi yake mnamo Aprili 3, 2026.
Mnamo Machi 6, Shirika la Uangalizi wa Haki za Binadamu liliandika barua kwa Jeshi la Polisi Tanzania na Tume ya Uchunguzi kushirikishwa katika matokeo na kuomba taarifa, lakini haijapokea majibu.
Viwango vya ndani, kikanda, na kimataifa vya haki za binadamu, ikiwemo Katiba ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu, ambayo Tanzania ni mwanachama, vinakataza matumizi ya nguvu kupita kiasi na vinatoa haki ya kupata fidia kwa ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu.
Kulingana na Kanuni za msingi za UN kuhusu Matumizi ya Nguvu na Silaha, maafisa wa usalama wanapaswa kutumia nguvu tu pale njia zisizo za nguvu zinaposhindwa kuwa na ufanisi na nguvu inayotumika iwe na uwiano na ukubwa wa kosa na lengo halali linalotakiwa kufikiwa. Maafisa wasimamizi wa sheria wanapaswa kutumia silaha kujilinda au kulinda wengine dhidi ya tishio linalokaribia kusababisha kifo au la kujeruhiwa vibaya, au katika nyakati ambapo ni lazima, kwa ajili ya kuchukua hatua dhidi ya uhalifu mkubwa unaohusisha tishio kubwa kwa maisha. uhalifu mkubwa unaohusisha tishio kubwa kwa maisha. Matumizi ya makusudi ya silaha za moto yanaruhusiwa pale tu ambapo haiwezi kuepukika katika kulinda maisha.
Serikali zinazoguswa na washirika wa maendeleo wa Tanzania wanapaswa kuitaka serikali kwa uwazi ichunguze kwa kina unyanyasaji huu, kumshtaki yeyote anayehusika, na kuhakikisha fidia, Shirika la Uangalizi wa Haki za Binadamu limesema. Pia wanapaswa kusaidia jukumu la asasi za kiraia katika kuhifadhi taarifa za matukio ya ukiukaji wa haki za binadamu.
“Mamlaka za Tanzania zinapaswa kutambua kuwa ulinzi dhidi ya wakiukaji wa haki kunachochea vurugu za kisiasa zaidi,” alisema Nyeko. “Zinapaswa kutokomeza ukandamizaji wa kisiasa unaoendelea na kushikiliwa kwa wakosoaji wa serikali, asasi za kiraia, na vyombo vya habari.”
Kwa maelezo zaidi kuhusu matokeo haya, tafadhali angalia hapa chini.
Serikali ya Tanzania iliongeza ukandamizaji wa upinzani wa kisiasa, wakosoaji wa serikali, na vyombo vya habari kabla ya uchaguzi wa Oktoba 2025.
Mnamo Aprili 9, polisi walimkamata Tundu Lissu, mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wakimshtaki kwa uhaini na kuchapisha “habari za uongo” mtandaoni, kufuatia maoni yake ya ukosoaji katika mkutano. Chama cha Lissu kilihamasisha kugomea uchaguzi baada ya serikali kushindwa kutekeleza mageuzi ya uchaguzi.
Siku chache baada ya kukamatwa kwake, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) ilizuia Chadema kushiriki katika uchaguzi, kwa kudai kuwa chama hakijasaini kanuni ya maadili iliyoamriwa na serikali.
Kabla ya uchaguzi, mamlaka walikamata waandamanaji na kuzuia vyombo vya habari vilivyoandika kuhusu masuala haya. Mamlaka pia walihusishwa katika utekaji na mauaji ya kiholela ya angalau wakosoaji 10 wa serikali.
Baada ya wiki kadhaa za wito kutoka kwa wanaharakati wakihamasisha maandamano kuhusu masuala haya, asubuhi ya siku ya uchaguzi maandamano yalianza katika mji mkuu wa kibiashara wa Tanzania, Dar es Salaam, pamoja na katika miji mingine, hususan Mwanza na Arusha.
Majira ya saa saba mchana (7:00 mchana), serikali iliweka vizuizi vya matumizi ya mtandao nchi nzima, na saa kumi na moja jioni (11:00 Jioni), Inspekta Jenerali wa Polisi, Camillus Wambura, alitangaza amri ya kutotoka nje (lockdown) katika jiji la Dar es Salaam kuanzia saa kumi na mbili jioni (12:00 Jioni). Aliwataka wakazi kubaki majumbani mwao bila kikomo cha muda, huku polisi na vyombo vingine vya usalama pekee wakiruhusiwa kuwa mitaani.
Licha ya vizuizi hivyo, waandamanaji walirejea mitaani siku iliyofuata katika Dar es Salaam na maeneo mengine, ikiwa ni pamoja na Namanga mpakani mwa Kenya. Huduma ya mtandao ilirejeshwa kwa muda mfupi kisha ikasitishwa tena.
Maandamano yalipungua kwa kiasi kikubwa baada ya tarehe 30 Oktoba, na tarehe 1 Novemba, Tume ya Uchaguzi ilitangaza kuwa Samia Suluhu Hassan ameshinda urais. Aliapishwa kwa muhula wa pili tarehe 3 Novemba, na msemaji wa serikali, Gerson Msigwa, alitangaza “kuanza kurejea taratibu kwa shughuli za kawaida,” huku huduma ya mtandao ikirejeshwa kidogo kidogo na wakazi kuruhusiwa kutoka majumbani mwao siku iliyofuata.
Dar es Salaam, October 29-30
Majira ya saa nne asubuhi (4:00 Asubuhi) siku ya uchaguzi, waandamanaji katika Dar es Salaam walifunga barabara za Mandela, Bagamoyo na Morogoro zinazoelekea katikati ya jiji kwa kuchoma matairi na kuweka vizuizi, kulingana na taarifa za vyombo vya habari.
Mwanamke mwenye umri wa miaka 20 aliliambia Shirika la Uangalizi wa Haki za Binadamu kuwa yeye na mama yake walikuwa wameketi nje ya nyumba yao katika wilaya ya Ubungo walipopigwa risasi miguuni majira ya saa nane mchana (8:00 Mchana), walipojaribu kuingia ndani:
Sikuona polisi walipokuwa, lakini waliowaona wanasema walikuwa barabarani wakifyatua risasi hata huku ndani ya makazi. Sijui kama walikuwa barabarani tu au walikuwa wamekaribia zaidi eneo letu, sikujua kwa sababu niliona watu wanakuja wakikimbia, nami nikaingia ndani, ndipo risasi ikanipata.
Yeye pamoja na mama yake walieleza kuwa walishindwa kufanya kazi baada ya tukio hilo kutokana na majeraha waliyoyapata.
Mwanaume mwenye umri wa miaka 39 alisema kuwa majira ya saa kumi alasiri (10:00 alasiri), askari polisi waliokuwa kwenye gari jeupe walimpiga risasi na kumjeruhi akiwa katika biashara yake ya usukaji vikapu huko Ubungo. Alisema machafuko hayo yalimzuia kupata matibabu hospitalini, hivyo alilazimika kupata msaada kutoka kwa mfanyakazi wa duka la dawa. Katika kipindi cha wiki tatu za kupona,hakuweza kufanya kazi, jambo lililosababisha mzigo mkubwa wa ugumu wa kifedha kwa familia yake.
Chama cha wanasheria cha Tanganyika kiliripoti kuwa majira ya saa kumi na mbili na nusu jioni (12:30 Jioni), askari polisi walimpiga risasi na kumuua wakili, Peter Elibariki Makundi, katika Barabara ya Shekilango alipokuwa akirejea nyumbani kutoka kufanya manunuzi.
Siku iliyofuata, vyombo vya habari viliripoti kuwa maafisa wa jeshi na polisi waliweka vizuizi vya ukaguzi (checkpoints) kwa madereva na watembea kwa miguu. Pia iliripotiwa kuwa, licha ya vizuizi hivyo, waandamanaji walirejea mitaani katika maeneo ambayo polisi walikuwa wametawanya umati siku iliyotangulia kwa kutumia risasi na mabomu ya machozi.
Katika wilaya ya Temeke, Dar es Salaam, majira ya saa kumi alasiri (10:00 alasiri) tarehe 30 Oktoba, mwanaume mwenye umri wa miaka 49, Master Tindwa Mtopa, alipigwa risasi nje ya nyumba yake. Mkazi mmoja wa eneo hilo alisema kuwa ingawa mtaa wao ulikuwa tulivu, polisi waliokuwa doria waliwaamuru watu kurejea majumbani, kisha wakaanza kufyatua risasi.
Wanafamilia walieleza kuwa vikosi vya usalama vilivyokuwa katika kizuizi cha barabarani viliwazuia kumpeleka Mtopa hospitalini. Baada ya saa mbili, waliweza kufanya hivyo pale ndugu mmoja aliyekuwa mwanajeshi alipowasindikiza. Hata hivyo, Mtopa alifariki dunia hospitalini.
Mkazi mmoja wa Temeke mwenye umri wa miaka 57 alisema kuwa alipigwa risasi mgongoni akiwa amepanda pikipiki karibu na kituo cha polisi cha Buza, baada ya kuvuka kizuizi cha kijeshi. Alieleza kuwa alifanyiwa upasuaji kutokana na majeraha hayo.
Mwanaume mwenye umri wa miaka 27 alisema kuwa askari wawili wa polisi walimkamata huko Buza tarehe 30 Oktoba, baada ya kuvuka kizuizi cha barabarani akiwa na abiria kwenye pikipiki yake ya biashara. Alisema kuwa askari hao walimpeleka katika kituo cha polisi kilicho karibu, wakamtuhumu kwa kuchoma matairi barabarani, na kumpiga makofi huku wakirudia rudia na kumpiga kwa kiti cha chuma, hali iliyosababishia majeraha makubwa miguuni mwake. Alizuiliwa hapo usiku kucha na kuhamishwa mara mbili katika wiki iliyofuata, alisema.
Alieleza kuwa maafisa walimlazimisha kusaini hati ambayo hakuielewa, wakampiga picha, na kumpeleka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu. Yeye pamoja na wengine walishitakiwa mahakamani kwa shitaka la uhaini na kuwekwa rumande katika Gereza la Segerea hadi kesi yao iliposikilizwa tarehe 19 Novemba.
Tarehe 24 Desemba, alipelekwa mahakamani ambapo mashtaka yalifutwa na akaachiwa huru. Alisema kuwa ingawa alipata matibabu gerezani, hakuweza kufanya kazi kutokana na majeraha yake.
Mwanza, Oktoba 30-31
Mashahidi watano huko Mwanza walisema kuwa polisi walifyatua risasi kwa watu katika soko la Buhongwa, kusini mwa jiji la Mwanza, tarehe 30 Oktoba.
Mkazi mmoja alisema kuwa watu walikuwa wametoka majumbani mwao kwenda kazini au kufanya manunuzi bila kufahamu uwepo wa amri ya kutotoka nje, au wakiamini kuwa amri hiyo ilihusu Dar es Salaam pekee. Tangazo la awali la polisi lilitaja Dar es Salaam, kisha baadaye kupanuliwa nchi nzima.
Mashahidi walieleza kuwa majira ya saa mbili asubuhi (2:00 Asubuhi), takribani askari polisi 20 walifika sokoni hapo kwa magari ya polisi na kuwaamuru watu—hasa wafanyabiashara—kuondoka. Walipochelewa kuondoka, askari hao waliwapiga kwa fimbo.
"Watu walichelewa kuondoka kwa sababu walikuwa wanakusanya bidhaa zao,” alisema mwanaume mmoja aliyekuwepo. “Polisi walianza kuwapiga watu waliokuwa wamebeba mizigo yao. Baada ya takribani dakika 40, walianza kufyatua risasi za moto. Walikuwa wakilenga moja kwa moja kwa watu, siyo kupiga hewani.”
Mashahidi kadhaa walielezea kuuawa kwa wafanyakazi watano sokoni hapo: dereva wa pikipiki aitwaye Hassan; Masanja Kabo, muuza viatu aliyeripotiwa kupigwa risasi kifuani alipokuwa akifunga biashara yake; mtu aitwaye Chacha, mwenye takribani umri wa miaka 24, pia mfanyabiashara; mwanaume wa kabila la Kimasai aliyekuwa akiuza dawa za asili, aliyepigwa risasi akiwa ameketi karibu na soko; na James Ijide, fundi cherehani ambaye mashahidi walisema alipigwa risasi kutoka nyuma alipokuwa akikimbia na wengine kujinusuru.
Shahidi mmoja alisema kuwa askari walimpiga Kabo risasi akiwa umbali wa takribani mita 10: “Walipoanza kufyatua risasi, Masanja alianza kukusanya vitu vyake,” alisema shahidi huyo. “Alipopigwa risasi alikuwa anakimbia kuelekea zahanati ya Buhongwa. Alipigwa karibu na lango la kuingilia. Walimpiga risasi nyuma kichwani.”
Mashahidi walisema kuwa tukio la kupigwa risasi kwa Hassan lilisababisha ghasia hadi wanajeshi walipowasili kwa gari la kijeshi na kutuliza hali. Baada ya wao kuondoka, vurugu ziliendelea. Shahidi mwingine alisema:
Wakati huu, polisi walikuwa wanawapiga risasi moja kwa moja makundi ya watu. Hapo ndipo (James Ijide) fundi cherehani alipigwa risasi. Askari aliyempiga risasi alikuwa amejificha katika majengo ya shule ya Buhongwa. Aliwaona watu wakikimbia katika uwanja wa karibu na shule hiyo, akamlenga na kumpiga risasi mguuni huyo fundi cherehani. Hakuna aliyekwenda kumsaidia kwa sababu kila mtu alikuwa anakimbia. Baada ya tukio hili, watu walikasirika na kuanza kuharibu na kuchoma mali.
Shahidi mmoja alisema kuwa Ijide alifariki nyumbani baada ya kushindwa kufikishwa hospitalini kutokana na kufungwa kwa barabara.
Shirika la Uangalizi wa Haki za Binadamu lilipokea picha nne zikimuonesha Ijide kama alivyotambuliwa na mashahidi. Picha moja inaonesha akiwa kati ya watu wawili juu ya pikipiki, takribani mita 375 kaskazini mwa soko, karibu na shule. Katika picha nyingine, amelala chini akiwa na damu miguuni na kifuani, huku mtu mmoja akiwa amefunga kitambaa kama kitanzi cha kuzuia damu na kumshinikiza juu ya paja lake.
Kiongozi mmoja wa jamii alisema watu saba waliuawa na takribani watu 50 walijeruhiwa. Miili ya waliouawa ilibaki eneo hilo hadi polisi walipowaambia wananchi waichukue saa kumi na mbili jioni (12:00 Jioni).
Wanajamii walijibu kwa kulipiza kisasi kwa kuchoma kituo cha polisi kilicho karibu, kituo cha mafuta, pikipiki na magari mengine, alisema mwandishi wa habari aliyekuwepo eneo hilo: “Kilichowachochea kufanya hivyo ni tukio la Buhongwa ambapo watu waliuawa bila sababu yoyote.”
Shahidi mwingine alisema:
Baadhi ya watu walijificha kwa hofu, kwa sababu ikiwa wanaweza kuwapiga risasi watu wasiokuwa waandamanaji, basi lolote linawezekana. Pia kulikuwa na taarifa za maeneo mengine kuwa watu walikuwa wakivamiwa majumbani mwao na kuchukuliwa. Watu walihisi kuwa hata kuwa majumbani mwao haikuwa salama.
Mashahidi walisema kuwa majira ya saa mbili na nusu usiku (2:30 Usiku) tarehe 31 Oktoba, takribani askari saba wa polisi waliovaa sare walifika katika kituo cha Mjimwema, umbali wa kilomita 16 kaskazini mwa Buhongwa, ambapo watu walikuwa wakitazama mpira wa miguu katika mgahawa mdogo. Shirika la Habari la Reuters iliripoti kuwa mapema jioni hiyo, polisi waliokuwa doria katika eneo hilo waliwaamuru watu waliokuwa mitaani kurejea majumbani kwao.
Shahidi mmoja alisema kuwa askari hao walianza kuwafyatulia risasi watu waliokuwa wameketi nje, na kuwaua wawili. Wengine walikimbia kwa taharuki kuelekea pande mbalimbali, baadhi yao wakiingia ndani ya mgahawa. Askari waliwaamuru waliokuwa ndani kutoka nje na kulala kifudifudi. Shahidi aliyekuwa amejificha baada ya milio ya risasi ya awali alisema:
“Mmoja wa wale waliokuwa wamelala chini alisimama huku akiinua mikono yake juu, akiwaomba polisi wasiwaue. Hawakumsikiliza, na yeye ndiye aliyekuwa mtu wa kwanza kuuawa. Baada ya kumpiga risasi, waliwapiga risasi wote waliokuwa wamelala chini.”
Dakika chache baadaye, askari walirusha bomu la machozi na kuondoka eneo hilo. Mashahidi walisema watu 14 waliuawa na angalau wawili walinusurika.
Siku sita baadaye, video tatu zilizosambazwa mtandaoni zilionyesha tukio hilo. Katika moja ya video hizo, miili 13 inaonekana imelala chini, wengi wao kifudifudi katika madimbwi ya damu—mmoja ndani ya baa, wawili mlangoni, na 10 barabarani nje. Video hizo pia zinaendana na picha iliyoshirikishwa moja kwa moja na shahidi kwa Shirika la Uangalizi wa Haki za Binadamu alisema ilichukuliwa dakika tano baada ya shambulio hilo.
Deutsche Welle iliripoti tarehe 14 Januari kuwa ilipata na kuchambua risasi kutoka katika tukio hilo ambazo zilifanana na zile zinazotumiwa na silaha ndogo na nyepesi, zinazofanana na bunduki za kivita za aina ya Kalashnikov zinazotumiwa na polisi wa Tanzania. Shirika la uangalizi wa haki za binadamu halikufanya mapitio ya risasi hizo.
Mkazi mmoja wa Ilemela, Mwanza, alisema kuwa alipokuwa akikaribia nyumbani kwake, aliwaona askari wawili wa polisi wakifyatua risasi kuelekea nyumbani kwake walipokuwa wakiwafukuza waandamanaji. Alipofika nyumbani, alimkuta ndugu yake mwenye umri wa miaka 16, aliyekuwa ndani pamoja na ndugu wengine watatu, akiwa amejeruhiwa kwa risasi kwenye paja:
“Niliona risasi ikigonga mlango. Risasi ilimpiga paja, ikapenya mwilini mwake na kugonga jokofu. Baada ya tukio hilo, niliwaona askari wakiondoka kuelekea walipoacha gari lao.Nilikwenda moja kwa moja kwenye nyumba yangu na kusukuma mlango nilipofika hapo,nilimkuta amelala chini huku akivuja damu nyingi ".
Alisema alimtoa nje na kuwaomba polisi wampeleke hospitalini, lakini walikataa na kumtishia kumpiga. Hatimaye walikubali kumchukua lakini walimwacha yeye alipokuwa akijaribu kuingia ndani ya gari. Yeye pamoja na ndugu mwingine walitumia saa saba kumtafuta hadi mfanyakazi wa hospitali alipowaambia kuwa alikuwa amefariki dunia. Baadaye waliupata mwili wake katika chumba cha kuhifadhia maiti.
Arusha, Oktoba 29-30
Katika jiji la Arusha, maandamano yalizuka asubuhi ya siku ya uchaguzi katika maeneo ya Mianzini na Sakina. Mkazi wa Sakina ambaye hakushiriki maandamano alisema aliona takribani askari 20 wa polisi wakiwa wamevaa sare, pamoja na wengine wasio na sare aliowahisi kuwa ni polisi, wakifyatua risasi kuelekea kwenye umati mkubwa uliokuwa ukiandamana kupinga gharama ya maisha na uongozi wa nchi.
“Kila mtu alikuwa akitafuta mahali pa kukimbilia,” alisema. “Nilikimbia pia kuelekea nyumbani kwangu. Hata baada ya kukimbia, bado nilikuwa nasikia milio ya risasi.”
Katika eneo la Mianzini, mwanaume aliyeshiriki maandamano alisema yeye kwa macho yake mwenyewe alishuhudia watu tisa wakiuawa na polisi pale kwenye maandamano:
Mtu wa kwanza alipigwa risasi usoni, mwingine kifuani na akafa papo hapo. Watu watatu waliuawa wakiwa juu ya pikipiki iliyogongwa na gari la polisi. Mwanamke mjamzito alipigwa risasi mgongoni.
Shahidi huyo aliongeza kuwa watu wengi walijeruhiwa kwa risasi au kupigwa na askari kwa marungu, haikujalisha kama ulikuwa ni sehemu ya maandamano au la" alisema. Ndugu na mashahidi walielezea mauaji ya jamaa zao jijini Arusha siku hiyo.
Majira ya saa kumi Alasiri (10:00 Alasiri), polisi walimpiga risasi na kumjeruhi mwanaume mwenye umri wa zaidi ya miaka 40 alipokuwa akitoka msikitini katika kata ya Ngarenaro, kaka yake alisema.
Mkazi mwingine alisema alipata taarifa kuwa mume wake mwenye umri wa miaka 47 alipigwa risasi na polisi waliokuwa wakitawanya umati katika eneo la Uswahilini la Arusha alipokuwa akirejea nyumbani kutoka kupiga kura jioni. Baadaye familia ilipata mwili wake katika hospitali ya Mount Meru ukiwa na majeraha mawili ya risasi kichwani.
Mwanamke mwenye umri wa miaka 32 alipigwa risasi mgongoni tarehe 29 Oktoba alipokuwa akitoka sokoni Mianzini. Ndugu aliyekuwa naye alisema alikuwa mjamzito:
“Katikati ya vurugu, niliona mtu mwingineo akipigwa risasi upande mwingine. Nilipokimbilia kumsaidia, upande mwingine nilimuona ameanguka chini. Nilimbeba na kumpeleka hospitalini, lakini tayari alikuwa amefariki. Hali ilikuwa mbaya sana. Watu walivunjika miguu, wengine walifariki pale Mianzini. Rafiki yangu tunayefanya naye kazi ya kutengeneza matofali pia alipigwa risasi kwenye paja, na bado ana jeraha.”
Wanafamilia walipata shida kubwa kuupata mwili wake katika chumba cha kuhifadhia maiti kutokana na wingi wa miili:
Tulifanikiwa kuupata mwili, japo tulipata shida kubwa. Ilituchukua siku nne za usumbufu kuupata mwili. Hospitalini kulikuwa na miili mingi kiasi kwamba haikuwa rahisi kumtambua mtu wako. Miili ilikuwa imepangwa hadi mlangoni, na hatukuruhusiwa kuingia na simu. Hatimaye nilimpata pale kwenye kona, chini ya miili mingine.
Mwanaume mwenye umri wa miaka 41 alipigwa risasi kichwani Mianzini alipokuwa katika shughuli zake za kawaida. Mke wake alisema walimkuta akiwa katika hali mbaya lakini bado anapumua. Tulipofika pale tulimkuta amefunikwa na nguo,nilimfunua nguo,na alikuwa amepigwa risasi kisogoni. Hakukuwa na usafiri tulimpeleka kwenye kituo cha afya kwa kumbeba na tulipofika, tulimkuta kaka yake pia pale (ambaye pia alikuwa amepigwa risasi mara mbili).
Familia iliwapeleka wote wawili katika hospitali ya Mount Meru, ambapo wafanyakazi wa hospitali waliwaambia waondoke na baadaye walijulishwa kwamba alikuwa amekufa. Kaka yake alipata nafuu baada ya upasuaji.
Katika maeneo ya pembezoni mwa jiji, wananchi pia waliripoti vifo vya ndugu zao.
Mwanamke mmoja mwenye umri wa miaka 27 aliuawa kwa kupigwa risasi langoni mwa nyumba yake eneo la Ngulelo, kaskazini mashariki mwa jiji la Arusha majira ya saa tisa alasiri (9:00 Alasiri). Familia ilieleza kuwa ndugu zake walisema kwamba ndugu walipouchukua mwili wake kutoka hosipitalini maafisa wa polisi waliwaonya wasionyeshe kwenye fomu kuwa alipigwa risasi.
Kaka wa mwanaume mwingine mwenye umri wa miaka 27 alisema alipata taarifa kuwa ndugu yake alipatikana akiwa amepigwa risasi kichwani katika kituo cha mabasi cha Kilala, barabara ya Arusha–Moshi,kwenye saa 9 za alasiri katika vitongoji vya jiji.
Mama wa mwathirika mwingine mwenye umri wa miaka 37 alisema mwanawe fundi pikipiki na mkazi wa kilala alipigwa risasi alipokuwa akirejea nyumbani kutoka kazini,polisi walipokuwa wakiwakabili waandamanaji na baadaye alifariki hospitalini.
Maandamano kaskazini mwa Arusha yalisambaa hadi Namanga mpakani mwa Tanzania,na Kenya na asubuhi ya siku iliyofuata ya uchaguzi wa tarehe 30 Oktoba. Mashahidi walisema polisi walifyatua risasi za moto na mabomu ya machozi kutoka kituo cha polisi upande wa Tanzania kuelekea waandamanaji waliokuwa wakirusha mawe, wengi wao wakiwa upande wa Kenya umbali wa takribani mita 20. Angalau watu wawili waliuawa na polisi.
Ndugu wa mwanaume mwenye umri wa miaka 32 kutoka mkoa wa Arusha walisema alipigwa risasi na kujeruhiwa vibaya mdomoni alipokuwa akila katika mgahawa upande wa Kenya.
Watafiti walipokea picha tano zilizopigwa na waandishi wa habari zilizomuonesha akiwa amejeruhiwa na amekaa katika kiti cha nyuma cha pikipiki. Shirika la Uangalizi wa Haki za Binadamu zilng’amua kuwa picha hizi zilipigwa katika mji wa Namanga eneo la mpaka wa Kenya, takribani mita 75 kutoka mpaka wa Tanzania. Watafiti pia walipokea picha za video zikimuonyesha akiwa kituo cha afya. Katika picha hizo zote alionekana akivuja damu kutoka katika jeraha kubwa kidevuni kwake.
Mamlaka za Kenya zilimpeleka yeye pamoja na watu wengine wawili waliopigwa risasi katika hospitali ya Nairobi kwa matibabu. Familia yake ilisema waliogopa kumpeleka hospitali nchini Tanzania kutokana na taarifa kwamba majeruhi walikuwa wakikamatwa.