Skip to main content

Tanzania: Shughulikia Haki Kabla ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa

Kukomesha Ukandamizaji; Hakikisha Uchunguzi wa Haraka, Bila Upendeleo wa Unyanyasaji

Polisi wanamzuilia mfuasi wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, Chadema, mwanzoni mwa maandamano yaliyopigwa marufuku jijini Dar es Salaam, Septemba 23, 2024. © 2024 ANTHONY SIAME/EPA-EFE/Shutterstock

(Nairobi) – Serikali ya Tanzanian inapaswa kuchukua hatua za haraka kukabiliana na kudorora kwa hali ya haki za binadamu nchini kabla ya uchaguzi ujao wa serikali za mitaa Tanzania Bara mnamo Novemba 27, 2024, Human Rights Watch imesema leo.

Tangu Juni, mamlaka zimewakamata kiholela mamia ya wafuasi wa upinzani, kuweka vikwazo kwenye mitandao ya kijamii, kupiga marufuku vyombo vya habari huru, na wamehusishwa na utekaji nyara na mauaji ya kiholela ya wakosoaji angalau wanane wa serikali.

"Mamlaka za Tanzania zimeonyesha kukosa uvumilivu kwa uhuru wa kujieleza kwa kuwabana wakosoaji wao na upinzani wa kisiasa," Oryem Nyeko, mtafiti mkuu wa Afrika kutoka Human Rights Watch. "Serikali inapaswa kukomesha haraka wimbi la ukandamizaji au kuongeza hatari ya mazingira ya kisiasa kuwa ya wasiwasi."

Juni 23, watu wanne wasiojulikana wakiwa wamevalia kiraia walimteka nyara Edgar Mwakabela, mchambuzi wa mitandao ya kijamii anayefahamika kwa jina la Sativa, jijini Dar es Salaam. Mwakabela alisema watekaji hao walimpeleka Kituo cha Polisi Oysterbay jijini Dar es Salaam, ambako walimhoji usiku mzima huku akiwa amefungwa pingu kuhusu kazi yake ya kuhamasisha wafanyabiashara kususia biashara na uhusiano wake na viongozi wa upinzani wa kisiasa.

Julai 15, polisi walithibitisha kumshikilia Kombo Mbwana, ofisa wa chama kikuu cha upinzani cha Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wilayani Handeni, mkoani Tanga, baada ya kutoweka Juni 15. Mamlaka ilimfungulia mashtaka Julai 16 kwa madai ya kushindwa kutoa maelezo ya kutosha kuhusu akaunti yake ya namba ya simu (SIM card), chini ya kifungu cha 126 cha Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta.

Kuzuiliwa kwa Mbwana bila kufunguliwa mashitaka kwa siku 30 baada ya familia yake kuripoti kutoweka kwake kunazidi kwa mbali kiwango cha saa 24 kinachotakiwa na sheria, kumaanisha kutoweka kwa lazima. Mnamo Septemba 5, mahakama ilimnyima dhamana Mbwana, na bado yuko kizuizini akisubiri kusikilizwa kwa kesi yake.

Chadema imeripoti kupotea kwa maafisa wengine wasiopungua wawili, akiwemo Dioniz Kipanya, ofisa wa Wilaya ya Sumbawanga, mkoa wa Rukwa, aliyeripotiwa kutoweka Julai 26, na Deusdedith Soka, kiongozi wa vijana ambaye kundi la watu waliripotiwa kumteka Agosti 18, pamoja na katibu wake, Jacob Godwin Mlay, na Frank Mbise, dereva wa pikipiki (bodaboda).

Wiki moja kabla, polisi walikuwa wamemkamata na kumwachilia Soka pamoja na mamia ya wafuasi wa Chadema na waandishi wa habari kadhaa, kabla ya maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Vijana iliyoandaliwa na chama hicho jijini Mbeya.

Mnamo Agosti 2, familia ya Shadrack Chaula iliripotiwa kutoweka kwake, mwezi mmoja baada ya kutiwa hatiani kwa "kumtusi" Rais Samia Suluhu Hassan na kuchoma picha yake katika video iliyowekwa kwenye akaunti yake ya TikTok. Chaula aliachiliwa mnamo Julai 8 baada ya kulipa faini hiyo iliyowekwa na mahakama.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan (katikati), akikagua walinzi wa heshima baada ya kuapishwa katika hafla iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam, Tanzania, Machi 19, 2021. © 2021 AP Photo

Septemba 7, mwili wa Ali Mohamed Kibao, afisa wa Chadema ambaye aliripotiwa kutoweka siku moja kabla, ulikutwa umepigwa na kumwagiwa tindikali. Rais Suluhu Hassan aliagiza uchunguzi ufanyike, lakini hakuna mtu aliyekamatwa. 

Mamlaka pia imekabiliana na wale wanaoibua wasiwasi kuhusu kupotea kwa watu, Human Rights Watch ilisema.

Mwezi Agosti, baada ya Chadema kutangaza maandamano jijini Dar es Salaam kupinga Serikali kutokuchukua hatua kufuatia kutekwa nyara kwa wafuasi wake, polisi walipiga marufuku maandamano hayo, wakitishia "kuwashughulikia" watu ambao hawakufuata marfuku hiyo. Mnamo Septemba 23, polisi waliwakamata na baadaye kuwaachilia kwa dhamana viongozi wa chama hicho Freeman Mbowe na Tundu Lissu, pamoja na wanachama wengine wa chama hicho, kabla ya maandamano hayo yaliyopangwa.

Mapema Septemba, shirika la ufuatiliaji la Netblocks lilithibitisha kuwa Tanzania ilikuwa imezuia upatikanaji wa mtandao wa kijamii wa X. Mtandao huo ulizuiwa wakati Watanzania wakijihusisha na mijadala katika mitandao ya kijamii kuhusu kupotea huko kwa watu.

Hatua hizi za kikandamizaji zinaakisi hali ya kabla ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 2020, wakati ambapo kulikuwa na kuzorota kwa uhuru wa kujieleza na kujumuika na haki nyingine za binadamu. Mamlaka ilikamata kiholela viongozi na wafuasi wengi wa vyama vya upinzani, kusimamisha vyombo vya habari, kukagua mawasiliano ya simu za mkononi, na kufungia mitandao ya kijamii.

Usiku wa kuamkia uchaguzi huo, polisi walifyatua risasi za moto kwa umati wa watu visiwani Zanzibar na kusababisha vifo vya watu wasiopungua tisa, huku vikosi vya usalama, pamoja na wanamgambo walioungwa mkono na serikali, wakiwapiga na kuwanyanyasa wakazi na kuwakamata kiholela wafuasi wa upinzani, wakiwaweka kizuizini na kuwatesa kwa wiki kadhaa. Uchaguzi mkuu ujao umepangwa kufanyika mwishoni mwa 2025.

Rais Suluhu Hassan, ambaye alichukua ofisi kufuatia kifo cha Rais John Magufuli mwezi Machi 2021, alichukua hatua za awali kushughulikia masuala ya haki na kufungua nafasi kwa vyama vya upinzani na vyombo vya Habari. Mamlaka za Tanzania, hata hivyo bado hazijachunguza na kufungua mashitaka dhidi ya yoyote kwa udhalilishaji wa wakati huo, hususani kwa Zanzibar.

"Katika wakati huu mgumu, mamlaka za Tanzania zinapaswa kuchukua hatua za haraka kutetea haki za binadamu na kuhakikisha kuwa uchaguzi ujao unakuwa huru na wa haki," Nyeko alisema. "Rais Samia Suluhu Hassan anapaswa kuhakikisha uchunguzi wa haraka na usio na upendeleo juu ya kupotea kwa wakosoaji wake na kukomesha vikwazo vinavyoendelea dhidi ya wapinzani wake wa kisiasa na vyombo huru vya habari."

Your tax deductible gift can help stop human rights violations and save lives around the world.

Region / Country