(Novemba 30, 2021) – Serikali ya Tanzania haijavichukulia hatua vikosi vya ulinzi na wanamgambo wanaoungwa mkono na serikali waliohusika katika kuwaua watu visiwani Zanzibar wakati wa uchaguzi mkuu wa Mwaka 2020, Shirika la Human Rights Watch limesema leo.
Utafiti wa Human Rights Watch uligundua kwamba takriban watu 14 walifariki na wengine 55 kujeruhiwa, kwenye oparesheni iliyowashirikisha maafisa wa polisi, wanajeshi na wanamgambo waliovalia mavazi ya kiraia ambapo walifyatua risasi katika makundi ya watu na kurusha mabomu ya machozi, kati ya Oktoba 26 na 30 Mwaka 2020. Watu hao wenye silaha vilevile waliwakamata na kuwaweka kizuiani pamoja na kuwatesa raia ambao ni wafuasi wa upinzani katika visiwa vikuu vya Zanzibar, Unguja na Pemba. Hadi sasa sio serikali kuu ya Tanzania au hata ile ya Zanzibar iliyokiri kufanyika kwa dhuluma hizo na hakuna uchunguzi uliofanyika kuhusu vurugu hizo licha ya kwamba malalamiko yalikuwa mengi kote nchini. Raia wengi wametaka ufanyike uchunguzi wa kina, ikiwezekana uongozwe na Kamishna wa shirika la umoja wa mataifa la haki za binadamu.
“Serikali ya Tanzania haijachukua hatua za kuhakikisha kwamba familia za watu waliouawa, na waathiriwa wa dhuluma hizo visiwani Zanzibar mwaka 2020 zinapata haki,” alisema mtafiti wa Shirika la Human Right Watch nchini Tanzania Oryem Nyeko. “Viongozi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla wanatakiwa kuonyesha kujitoa kwao katika kusimamia haki kwa kuhakikisha uwajibikaji na fidia kwa waathirika na familia za waliofariki wakiwa mikononi mwa vikosi vya ulinzi.”
Shirika la Human Rights Watch liliwahoji watu 57 kwa njia ya simu kati ya mwezi Oktoba Mwaka 2020 na Novemba Mwaka 2021. Liliwahoji waathirika, watu walioshuhudia vurugu, wanahabari, na maafisa wa vyama vya upinzani. Mahojiano yalihusu vurugu za baada ya uchaguzi na dhuluma zilizoandamana na vurugu visiwani Zanzibar.
Tarehe 26 Oktoba, Mwaka 2020, serikali ya Tanzania ilituma vikosi vya maafisa karibu 10,000 katika visiwa vya Unguja na Pemba huko Zanzibar, kabla ya siku mbili za upigaji kura kwenye uchaguzi uliofanyika Oktoba tarehe 27 na 28. Raia waliohojiwa walisema kwamba vikosi vya ulinzi vilifanya doria mitaani, vikafanya vurugu na kudhalilisha pamoja na kuwapiga watu, vikawatisha kwa bunduki huku vikiwafukuza kutoka maeneo ya umma. Vikosi vilivamia nyumbani kwa watu huku vikilipua mabomu ya machozi na hata kufyatua risasi. Maafisa wa usalama walitangaza amri ya kukaa ndani (curfew) na kuitekeleza huku wakiwapiga raia waliokiuka amri hiyo. Waliwateka wakazi, wakawazuilia wengine kwenye vituo ambavyo havikuwa rasmi kwa wiki kadhaa. Hali hii ya kuogopesha ilipelekea watu wengi kukimbia maeneo yaliyoathirika kote Zanzibar. “Wale walioshindwa kukimbia walipigwa,” alisema mkazi mmoja mwenye umri wa miaka 59, eneo la Nungwi – Unguja.
Jioni ya tarehe 26, 27 na 28 mwezi Oktoba vikosi vya ulinzi viliwafyatulia risasi makundi ya watu karibu na vituo vya kupigia kura kisiwani Pemba. Takriban watu tisa waliuawa, akiwemo mwanafunzi wa umri wa miaka 16 na mwanamke mja mzito. Oktoba tarehe 28, vurugu ziliongezeka huku Tume ya uchaguzi visiwani Zanzibar ikifanya hesabu ya kura. Wanamgambo wajulikanao kama ‘Mazombi’ waliwafukuza na kuwapiga watu wakiwemo wale waliokuwa wamefika kwenye kituo cha kuhesabu kura kushuhudia utaratibu wa kuhesabu.
Karibu watu wote walioshuhudia ambao walihojiwa walisema hawakutoa habari za mauaji hayo kwa sababu ya hofu iliyokuwa imeletwa na vurugu hizo. Wanafamilia wengine walisema hata walipotoa taarifa za mauaji kwa polisi na mamlaka nyingine hakuna kilichofanyika. Mtu mmoja alisema kwamba polisi walimpiga risasi kifuani mwanae wa umri wa miaka 25, katika kijiji cha Kangagani -Pemba kati ya saa tatu na saa nne usiku, Oktoba 27. Mtu huyo alitoa taarifa kwa kiongozi wa mtaa na vilevile kwa polisi. Alimzika mwanae siku iliyofuata, pamoja na watu wengine wawili waliokuwa wameuawa usiku ule. Shirika la Human Rights Watch limegundua kwamba hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa na polisi hadi kufikia sasa.
Serikali ya visiwani Zanzibar vilevile zilizuia na kujaribu kudhibiti usambazaji habari za mateso na dhuluma kupitia vyombo vya habari . Serikali iliwazuia wanahabari kupiga picha za vikosi vya ulinzi vikiingia katika vituo vya kupigia kura. Polisi waliwatia nguvuni na kuwazuilia wanahabari watatu waliokuwa wakifuatilia maandamano yaliyokuwa yakifanywa na upinzani. Waliwazuia kwa muda wa saa moja Oktoba 29 mjini Zanzibar, Unguja.
Oktoba 29, Tume ya Uchaguzi – visiwani Zanzibar, ilitangaza kwamba Hussein Ali Mwinyi, wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), alikuwa ameshinda uchaguzi wa urais visiwani na kwamba John Magufuli, vilevile wa CCM, alikuwa ameshinda uchaguzi wa urais nchini Tanzania.
Ishara ya pekee ya serikali kukiri kwamba kulikuwapo mauaji ilikuwa kupitia hatua ya Mkuu wa Polisi nchini Tanzania Simon Siro kuviambia vyombo vya habari Novemba 11, kwamba ni watu wawili tu ndio walifariki wakati wa ‘vurugu’ za Oktoba 26. Alisema pia kwamba wafuasi wa upinzani walimuua polisi mmoja Oktoba 28. Mkuu huyo wa polisi hakutangaza utaratibu wowote wa kushughulikia habari na tuhuma dhidi ya polisi hasa kwamba walikuwa wamehusika kwenye mauaji hayo.
Shirika la Human Rights Watch lilituma barua ofisi ya rais ya Tanzania na ofisi ya rais visiwani Zanzibar, vilevile kwa idara ya polisi ya Tanzania. Shirika lilituma ripoti za utafiti na kuuliza maswali kuhusu hatua ambazo serikali hizo mbili zilikuwa zimechukua kuchunguza madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu uliofanywa na maafisa wa polisi, wanajeshi na makundi ya raia waliojihami wakati wa uchaguzi visiwani Zanzibar na hadi sasa Shirika la Human Rights Watch bado halijapata mrejesho.
Visiwa vya Zanzibar awali vimeathirika kwa fujo za uchaguzi na hasa kwenye uchaguzi wa 2000 na uchaguzi mkuu wa 2015. “Kila baada ya miaka mitano, watu huuawa na wengine kukatwa viungo- kujeruhiwa,” alisema mkazi wa Pandani, Pemba. “Haya hufanyika katika kila uchaguzi, huwa hatulali nyumbani.”
Viwango vya haki za binadamu katika ngazi ya nchi, kikanda na kimataifa ikiwemo na sheria za Umoja wa Afrika kuhusu haki za watu hukataza vikosi vya ulinzi kutumia nguvu za kupita kiasi. Kanuni hizo vilevile zinajumuisha haki za mtu kufidiwa iwapo amedhulumiwa haki zake. Chini ya kanuni ya Umoja wa Mataifa kuhusu utumiaji nguvu na silaha (UN Basic Principles on the Use of Force and Firearms), vikosi vya ulinzi na walinda usalama wanafaa kutumia nguvu kwa kuzingatia uzito wa makossa aliyofanya mtu- kanuni hizo hutaka kwamba kutumia nguvu nyingi maksudi kunaruhusiwa tu iwapo lengo ni kuokoa maisha – yakiwemo maisha ya walinda usalama wenyewe.
“Ni muhimu kukomesha matukio ya vurugu yatokanayo na uchaguzi visiwani Zanzibar,” alisema Nyeko. “Ili haya yafanyike, mamlaka za Tanzania na Zanzibar zinatakiwa kuchukua hatua za haraka dhidi ya vikosi vya ulinzi na kuhakikisha haki inatendeka.”
Ili kupata mengi zaidi kuhusu vurugu za uchaguzi wa Mwaka 2020 visiwani Zanzibar, mfano maelezo ya waathiriwa na watu walioshuhudia, ikiwemo mapendekezo, tizama hapa.
Utawala, Polisi, na Muundo wa Haki
Visiwa vya Zanzibar ni eneo linalotambuliwa kuwa nchi inayojitawala. Nchi hiyo inavijumuisha visiwa kadhaa ambavyo vipo kilomita kadhaa kutoka ufukwe wa Tanzania bara. Visiwa vya Zanzibar vinaongozwa na serikali kuu ya Muungano wa Tanzania iliyopo jijini Dodoma pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) iliyopo jijini Zanzibar.
Matawi kadhaa ya vikosi vya ulinzi na usalama, yakiwemo makundi ya wanamgambo yanayoungwa mkono na serikali ya Zanzibar, mfano kundi la Mazombi, yalihusika kwenye oparesheni wakati wa uchaguzi wa visiwani Zanzibar Mwaka 2020. Idara ya Polisi ya Tanzania na Jeshi la Ulinzi la Tanzania (TPDF), husimamiwa na serikali kuu ya Jamhuri ya Muungano na kufanya kazi Tanzania Bara na Visiwani (Zanzibar). Idara ya polisi ya Zanzibar ni sehemu ya idara kuu ya polisi ya Tanzania. Serikali ya Zanzibar pia ina vikosi vyake vya ulinzi na usalama ambavyo vinajulikana kama ‘idara za usalama’ “Jeshi la SMZ,” au “Vikosi,” ambavyo uhudumu sambamba na idara ya polisi ya Tanzania. Kundi la wanangambo la Mazombi, au kwa jina jingine “Janjaweed,” ni la raia waliojihami, mara nyingi huficha sura zao kwa vitambaa na kuvalia mavazi meusi ya kiraia.
Tofauti na namna ambavyo idara za jeshi na polisi huongozwa, serikali za Tanzania na Zanzibar zina idara tofauti ya mashtaka ya umma ambapo kila idara huanzisha taratibu za mashtaka na kuyaongoza mahakamani na vilevile kusimamia shughuli zote za mashtaka katika maeneo yao.
Historia ya Vurugu za Uchaguzi Visiwani Zanzibar
Mwezi Januari 2001, vikosi vya ulinzi nchini Tanzania viliwaua takriban watu 35 na kuwajeruhi wengine 600 visiwani. Watu hao walikuwa wakiandamana kupinga kile walichokiita kuwa udanganyifu katika uchaguzi. Kwenye marudio ya uchaguzi wa urais Mwaka 2015 mwezi Machi Mwaka 2016, serikali visiwani Zanzibar ikitumia nguvu za kupita kiasi iliwatia nguvuni wafuasi wa upinzani, ikapiga marufuku mikutano ya hadhara, na kufunga matangazo ya redio. Uchaguzi mkuu wa Mwaka 2015 na uchaguzi wa marudio wa Mwaka 2016 vilevile uliathirika kwa oparesheni za kundi la Mazombi lililowatisha raia na watu wanaoikosoa serikali. Watu wasiojulikana, walioshukiwa kuwa mawakala wa serikali, vilevile walimtisha mwanahabari mmoja anayehudumu visiwani Zanzibar aliyekuwa akiangazia yaliyokuwa yakifanyika wakati wa uchaguzi wa marudio Mwaka 2016.
Hakuna uchunguzi wowote ulioanzishwa na serikali ya Tanzania au Zanzibar kuhusu dhuluma hizo. Ukosefu wa hatua zozote kuchukuliwa dhidi ya wanaoshiriki dhuluma hizo, wengi wakiwa wanachama wa chama tawala cha CCM umechangia kujirudia kwa vurugu katika misimu ya uchaguzi - ikiwemo uchaguzi wa hivi majuzi, Oktoba 2020.
Dhuluma za Idara za Ulinzi na Wanamgambo wa Mazombi Visiwani Zanzibar Katika Uchaguzi Mkuu Mwaka 2020
Shirika la Human Rights Watch lilipata kwamba katika uchaguzi wa mwaka 2020, vikosi vya ulinzi vya Tanzania na Zanzibar vikiwemo polisi, jeshi na wanamgambo mfano makundi ya Vikosi na Mazombi viliwapiga watu, vikawarushia mabomu ya machozi, vikawatisha na kukawapiga risasi wakazi wa visiwani (Unguja na Pemba). Dhuluma hizi zilianza kabla shughuli ya kupiga kura na kumalizika baada ya kipindi kizima cha upigaji kura. Baadhi ya wakazi walitoroka manyumbani mwao na kujificha kwenye misitu iliyo karibu kwa siku kadhaa na hata majuma kadhaa.
“Baadhi ta watu waliona kwamba hawakuwa salama iwapo watarudi nyumbani kwao [hata baada ya uchaguzi],” alisema mkazi wa umri wa miaka 33 wa kijiji cha Kangagani –Pemba. “[Hatukurudi nyumbani] kwa miezi miwili hadi hali iliporejea kawaida huku kila mtu akianza kuona kwamba sasa yupo salama kurudi nyumbani.”
Watu wengi walioshuhudia dhuluma hizi na vilevile baadhi ya familia za waathiriwa walisema kwamba hawakutoa habari kwa vyombo vya serikali kwa sababu ya kuogopa. “ Sikutoa ripoti [ya kuuawa kwake ] popote,” alisema jamaa ya mtu mmoja aliyeuawa Pemba. “Mwanzo nilibabaika — hatukutarajia haya kutendeka. Pili, ungetoa taarifa ya dhuluma hizo wapi na kwa nani? Nani angekusikiliza?”
Dhuluma za Kuwapiga Watu na Kuvunja Nyumba Zao
Oktoba 26, Mwaka 2020, maafisa wa usalama na ulinzi wakiwa wamevalia wameziba sura zao na vitambaa na kuvalia nguo za sare ambazo hazikujulikana ni za idara ipi walianza kuwasili katika eneo la Nungwi, kaskazini ya Unguja. Walitangaza amri ya kukaa ndani kuanzia saa mbili usiku. Baadhi ya walioshuhudia walisema kwamba maafisa hao waliwatisha watu, wakavunja nyumba zao karibu siku nne mfululizo huku wakiwapiga wanaume. Polisi na wanajeshi walimpiga mtu yeyote waliyemkuta akiwa nje muda wa amri ya kukaa ndani ukiwa umeanza. Waliwapiga hata wale waliokuwa wakirejea nyumbani baada ya kutoka kwenye ibada -saa mbili usiku.
Oktoba 27, siku iliyotengewa mahsusi kwa maafisa wa usalama na ulinzi kupiga kura, watu katika kijiji cha Nungwi waliagizwa kukaa manyumbani adhuhuri. Walioshuhudia hali hii walisema wanamgambo wa Mazombi walimpiga mtu yeyote aliyepatikana nje ya nyumba yake baada ya saa saba adhuhuri. Kuanzia saa tatu na nusu asubuhi hadi saa saba adhuhuri tarehe 28 Oktoba, siku iliyotengewa watu wote kupiga kura, mtu mmoja alisema kundi la Mazombi liliandaa kambi-mfano katika kijiji cha Nungwi, likawachukua watu kadhaa na kuwazuilia kwenye kambi ile na kuwapiga.
“Nilisikia sauti ya mwanamune kwa jina Haji Hajibu,” alisema shahidi wa umri wa miaka 54- “Aliletwa hapa na kupigwa. Alivuliwa nguo akabaki uchi halafu akaambiwa aelekee dukani anunue nguo.” Mtu huyo alisema pia kwamba walikuwa wamesikia habari za wanawake kunajisiwa - Shirika la Human Rights Watch halikuweza kuthibitisha haya.
Usiku ule, wakazi wa Nungwi waliandamana kupinga oparesheni iliyokuwa inawadhulumu. Waliweka vizuizi barabarani wakitumia mawe huku wakiteketeza magurudumu. Polisi walikabili hayo kwa risasi. Licha ya shinikizo za raia, polisi, wanajeshi na wanamgambo wa Mazombi, waliendelea kuvunja nyumba za watu na kuingia ndani. Walivunja maduka yao huku wakiwapiga watu. “Milango ilikuwa ikivunjwa. Maafisa waliingia kwenye nyumba na maduka kwa lazima,” alisema mkazi mmoja wa umri wa miaka 59, kijiji cha Nungwi.
Katika kijiji cha Garagara na viunga vyake, mjini Zanzibar, vikosi vya ulinzi vilimpiga mwanamume wa umri wa miaka 23 aliyekuwa akifanya shughuli zake dukani kwake. Vikosi hivyo vilimlazimisha kujigaragaza kwenye kidimbwi cha maji na kumdhalilisha kwa kukata nywele zake kwa kutumia kisu.
Kuteketeza na Kuwapiga Risasi Wakazi Wasiokuwa na Silaha
Kuanzia Oktoba tarehe 26 hadi 29 na vilevile Novemba tarehe 1, watu kadhaa walioshuhudia dhuluma walisema kwamba vikosi vya ulinzi vilirusha mabomu ya kutoa machozi bila kujali ingemwathiri nani. Vilevile viliwapiga watu risasi kwenye maeneo mbalimbali ya Unguja na Pemba, hasa katika vituo vya kupigia kura. Watu takriban 14 waliuawa.
Jioni nzima Oktoba 26, vikosi vya ulinzi viliwalilipulia mabomu ya machozi na kuwafaytulia risasi watu waliokuwa wamekusanyika katika shule ya msingi ya Chwaka, vilevile katika kituo cha kupigia kura cha Tumbe eneo la kaskazini la Pemba baada ya uvumi kusambaa kuwa wafuasi wa chama cha CCM walikuwa wamepelekwa kule kupiga kura. Kufikia usiku wa manane, Abdalla Said Abdalla, wa umri wa miaka 24, aliuawa.
Mfanyakazi wa mashirika ya haki za binadamu alielezea fujo alizoshuhudia:
Polisi wengi na wahusika katika oparesheni za wanamgambo wa kundi la Vikosi walianza kuja. Hata jeshi. [Walinda usalama] walikuwa wakitupa mabomu ya machozi na kufyatua risasi. Walifanya hivyo kana kwamba walifurahia tu kufyatua kotekote. Tulikuwa kwenye barabara kuu na tungemwona [afisa] aliyekuwa akitoa amri: fanya hivi, fanya vile.
Usiku wa Oktoba 26, vikosi vya ulinzi viliwapiga risasi watu katika eneo la Kangagani, Pemba. Watu watatu waliuawa, akiwemo Asha Haji Hassan, ambaye alikuwa mja mzito. Mwanamke mmoja wa umri wa miaka 36 aliyeshuhudia, ambaye pia alipigwa risasi kwenye paja la kushoto (na watu wenye nguo za sare anaoamini walikuwa polisi) akiwa njiani kutoka kituo cha kupigia kura cha Shule ya msingi ya Kangagani, saa tatu usiku alielezea hivi:
Niliwaona watu [waliompiga risasi Asha na mimi] - walitoka kwenye kituo cha kupigia kura, walitumia barabara kuu. Sijui walikuwa wangapi, lakini walikuwa wengi. Baadhi walichutama, wakashuka kutoka kwenye gari, halafu wakafyatua risasi. Sina shaka kwamba wale waliochutama ndio walinipiga mimi risasi na kunijeruhi. Ndio vilevile waliompiga risasi Asha Hassan aliyekuwa mja mzito.
Ndugu wa Kombo Hamad Salim, wa umri wa miaka 32, alisema kwamba vikosi vya ulinzi vikiwa kwenye lori ya polisi, dakika thelathini hivi baadaye, vilimpiga risasi Salim- ikampata kifuani. Alikuwa ameketi na marafiki kwenye uwanja wa michezo wa shule ya Kangagani. Alifariki papo hapo.
Katika kijiji cha Garagara, walioshuhudia walisema, vikosi vya ulinzi vilimjeruhi vibaya mwanamke wa umri wa miaka 73 punde baada ya kurusha mabomu ya machozi nyumbani kwake. Ikiwa tarehe 27 Oktoba saa tano hivi asubuhi, watu sita waliokuwa na silaha, ambao wanaaminika kuwa wanamgambo wa Vikosi- kwa sababu ya aina ya mavazi yao, walielekea nyumbani kwa Saada Ali Hassan. Waliiamuru familia ile iwatoe wanaume wote waliokuwa wakiishi pale. Familia ile ilipokataa, watu hao walirusha mabomu ya machozi nyumbani kule na kemikali fulani ya kuwaka moto ndipo nyumba ikawaka moto. Mama Hassan alikuwa chumbani akipumzika –alikuwa ndio ameanza kupona kutokana na maradhi. Binti yake wa umri wa miaka 50 alikielezea kisa hicho ifuatavyo:
Magodoro yalikuwa yanateketea. Milango iliteketea. Asingeweza kujiokoa. Ilibidi tujaribu kumwokoa, lakini tulishindwa kwa sababu moto ulikuwa mkubwa. Kulikuwa na moshi mkubwa tena mzito. Alikuwa akiwalilia binti zake waje kumwokoa.
Afisa mmoja wa polisi ambaye hakuwa mshirika wa wanamgambo wa Vikosi aliingia kwenye chumba hicho na kumwondoa mama Hassan. Wale watu wenye silaha walisimama tu hapo wakiangalia bila kuingilia au hata kutoa usaidizi wowote. Mama Hassan alikuwa ameungua vibaya. Kwa hivyo familia yake ikampeleka katika hospitali ya Mnazi Mmoja mjini, Zanzibar. Alilazwa hapo akitibiwa hadi alipofariki tarehe 8 Mwezi Desemba.
Punde baada ya saa sita usiku wa Tarehe 27 Oktoba, vikosi vya ulinzi ambavyo vilikuwa vinalinda masanduku ya kura katika kituo cha kupigia kura cha shule ya msingi ya Mtemani wilayani Wete, Pemba, viliwapiga risasi watu waliokuwa wakipita pale. Watu watatu walipatwa na risasi hizo akiwemo mwanafunzi wa umri wa miaka 16 kwa jina, Massoud Salim Fadhal. Babaye Masoud alisema watoto wake wengine walimwambia kwamba walimwona mtu fulani kwenye gari jeusi akitoa maagizo kwa vikosi vya ulinzi viwafyatulie risasi watu waliokuwa nje ya shule.
Mhubiri mmoja katika shule ya kiislamu karibu na hapo kwa jina Ali Kombo Omar, ambaye aliisafisha maiti ya Fadhal kabla kuzikwa alisema maiti hiyo ilikuwa ingali inatoa damu mgongoni alipokuwa akiiosha.
Wakati huo huo katika kijiji cha Kinazini, Pemba, vikosi vya ulinzi vililipua mabomu ya machozi na pia kufyatua risasi. Risasi ilimpata Ali Said Kombo, wa umri wa miaka 28. Ali alikuwa amejumuika na marafiki katika kituo cha kupigia kura cha eneo akiangalia masanduku ya kura ambayo yalikuwa yakiletwa ikiwa maandalizi ya upigaji kura. Familia yake haikumpeleka hospitalini kwa sababu ya kuogopa kutoka nje kwa sababu vurugu zilikuwapo - alifariki saa chache baadaye.
“Walikuwa wakilipua mabomu ya machozi, walikuwa pia wakifyatua risasi,” alisema rafiki mmoja wa wa Kombo. “Sikuwaona watu hao, lakini kwa kuangalia magari yaliyokuwapo na dalili zote zilizotufikia, bila shaka walikuwa vikosi vya ulinzi.” Alisema kwamba walikuwa wakiendesha magari makubwa ya Toyota, aina ambayo hutumiwa na vikosi vya ulinzi vya Tanzania.
Watu walioshuhudia visa hivi katika kituo cha kupigia kura cha shule ya msingi ya Vitongoji mjini Vitongoji, wilaya ya Chake Chake, Pemba, walisema saa saba usiku Oktoba 27, maafisa wa polisi wanaoaminika kuwa sehemu ya kitengo cha kukabili fujo - kutokana na mavazi yao ya kijani, walimuua Mohammed Khalfan Mjaka, wa umri wa miaka 35, na kumjeruhi mguuni mwanamume wa umri wa miaka 30. Walioshuhudia walisema polisi hao walimpiga Mjaka risasi sita kifuani.
Vurugu zilizofanywa na vikosi vya ulinzi ziliendelea usiku kucha. Saa nne hivi tarehe 27 Oktoba, polisi walimuua kwa kumpiga risasi Salum Ali Abdalla, wa umri wa miaka 38, akiwa katika duka la jirani yake karibu na nyumbani kwake viungani mwa Kipangani, wilayani Wete. Mtu mmoja aliyeshuhudia alisema kwamba Abdalla alijaribu kutoroka punde maafisa wawili wa polisi walipovamia duka hilo. Mmoja alimpiga risasi mgongoni alipokuwa anatoroka halafu polisi yule akafunika matone ya damu yaliyokuwa yamedondoka mchangani ili kuficha ushahidi. Polisi hao waliuchukua mwili wake na kwenda nao. Baadaye mwili huo ulipelekwa katika mochari ya hospitali ya Wete.
Watu wawili, akiwemo rafiki wa karibu wa Hamad Shehe Ali, wa umri wa miaka 35, alishuhudia kuuawa kwa rafikiye katika kijiji cha Konde, wilaya ya Micheweni, kaskazini ya Pemba. Jioni ya Oktoba 27, watu waliovalia vitambaa vilivyofunika nyuso, wakiwa na sare, na pia silaha, wakawa kwenye msafara wa magari yaliyokwenda mbio ajabu. Magari hayo hayakuwa na namba za usajili, yaliongozwa na gari la polisi na lori la wanamgambo wa Vikosi walifyatua risasi, na kuwafanya watu kukimbia na kujificha. Risasi ilimpiga Ali, aliyekuwa njiani akiwa na watu wengine wawili wakielekea katika kituo cha kupigia kura cha shule ya msingi ya Konde- risasi ilimpiga kifuani. Rafiki yake wa karibu aliyekuwa naye alisema watu waliokuwa karibu walimchukua na kumpeleka katika hospitali ya Wete ambapo alifariki akihudumiwa.
Katika eneo la Garagara, Said Makame Ali, wa umri wa miaka 18, aliondoka nyumbani kwa jamaa zake saa tatu na nusu asubuhi Oktoba 28. Alikuwa akielekea katikati ya mji akiongozana na binamu zake. Njiani walikutana na watu waliovalia sare wakivurugana na makundi ya watu huku wakilipua mabomu ya machozi. Watu hao walianza kuwafukuza. Binamu yake Makame alisimulia yaliyotokea:
Kulikuwa na ukuta ambao ilibidi tuupande, Said Makame alishindwa kuupanda ili auruke. Hivyo ndivyo walimfikia na kumshika. Alipokuwa akijaribu kupanda ukuta risasi ilimpiga. Ilikuwa risasi moja tu. Nilimwona akishikilia mguu wake kwa uchungu.
Binamu yake Ali alitoweka, lakini familia ya Ali iliipata maiti yake siku tatu baadaye katika mochari ya hospitali ya Mnazi Mmoja. Jamaa yake mwingine alisema aliona jeraha kwenye mguu wa Ali lilikuwa likivuja damu wakati walimpata.
Tarehe 29 Oktoba, ikiwa saa tatu na dakika kumi na tano, watu wenye silaha walimpiga risasi nne Mussa Haji Mussa, wa umri wa miaka 28. Risasi zilimpiga kifuani, kwenye mabega yote mawili na mguuni – alipigwa risasi akiwa nje ya nyumba yake kijijini Nungwi. Jamaa zake walimpeleka katika hospitali iliyo karibu, lakini akawa amefariki alipofika pale. Jamaa yake mmoja alisema Mussa alikuwa mgonjwa wakati wa mkasa huo na alitakiwa kuwa amepumzika nyumbani kwake. Jamaa huyo anaamini kwamba waliompiga risasi walikuwa washirika wa vikosi vya serikali na kwamba walimtoa nyumbani kwake na kumuua.
Familia ya Mussa ilitoa taarifa ya kisa hicho kwa polisi lakini inakisiwa kwa sababu ya hofu ya vurugu zaidi, walitoa ulinzi wakati wa mazishi yake. Hata hivyo mamlaka haijatoa habari zozote kuhusu iwapo upo uchunguzi wowote unaoendelea kuhusiana na mauaji hayo.
Baada ya kumalizika uchaguzi, vikosi vya ulinzi viliendelea kushika doria katika maeneo mengi yaliyoathirika kwa dhuluma. Vikosi hivyo viliendelea kuwatisha na kuwatia uoga wakazi.
Tarehe 11 Novemba, vikosi vya ulinzi kwa ushirkiano na wanamgambo waitwao Valantia Zanzibar (KVZ) ambalo ni tawi la kundi la Vikosi lilimpiga risasi Said Salum Suleiman, wa umri wa miaka 34. Ilikuwa barabarani viungani mwa Mwembe Makumbi, mjini Zanzibar, na alikuwa anasafirisha mchanga kwa mkokoteni. Nduguye Suleiman anaelezea namna walibishana na maafisa sita wa ulinzi kabla kifo cha Suleiman.
Mimi ndiye nilikuwa nazungumza na kubishana nao. Ndipo Said aliingilia kati tukaendelea kuzungumza nao. Walijaribu kumkataza Said wakitaka asiingilie akasema alitaka kujua kinachoendelea baina yao na ndugu yake. Mmoja wao alisema, “Nitakupiga risasi usije huku.” Lakini Said akasisitiza kwamba atakuja nilipo. [Afisa yule] alifyatua tu risasi na ikampiga tumboni - kwenye kitovu. Alifariki papo hapo.
Familia ya Suleiman baadaye iliambiwa kwamba afisa wa polisi aliyempiga risasi alitiwa nguvuni na kufikishwa kortini. Licha ya hiyo familia hiyo haijapokea habari zaidi kuhusu mwelekeo wa kesi – vilevile haijaalikwa kutoa ushahidi.
Kuwatesa Waliozuiliwa
Watu watatu waliokuwa wamezuiliwa, waliliambia Shirika la Human Rights Watch kwamba tarehe 26 Oktoba, watu waliovalia vitambaa nyusoni, wakiwa pia na silaha, waliwatoa nyumbani kwao, wakawafunika nyusoni kwa vitambaa, wakawapiga na kuwasafirisa karibu kwa dakika thelathini hadi kwenye nyumba moja. Waliwazuilia pale kwenye chumba kimoja, wakawa wakiwapiga mara kwa mara na kuwaonya wasiingilie ‘masuala ya siasa.”
“Mpango ulikuwa kwamba kabla chakula, ilikuwa lazima tupigwe kwanza, ndipo baadaye tungepewa chakula,” jamaa mmoja aliyekuwa amezuiliwa awali alisema. “Walitumia nyaya kutupiga na vilevile nyundo. Tulipigwa kwa nyundo magotini na kwenye kumbo.”
Siku sita kabla waachiliwe huru, kichapo kilikoma. Maafisa waliokuwa wamevaa sare za maafisa wa magereza waliwaleta madaktari kuwatibu. Kufikia Novemba tarehe 15, siku 19 tangu watekwe, wanaume wote, isipokuwa Ameir Ameir Soud, walifungwa machoni kwa vitambaa na kuanza kusafirishwa. Waliachwa kwenye maeneo tofauti tofauti.
Mchanganuzi maarufu wa masuala ya siasa, mzee wa umri wa miaka 72, Soud, ambaye pia ni mkosoaji wa serikali kutoka mjini Bwejuju, Unguja alitekwa. Mkewe alisema alitekwa akiwa pekee nyumbani kwake.
Mtu mmoja waliyezuiliwa naye alisema Soud alipelekwa katika chumba cha kuwatesa watu na hakurudi. Saa ishirini na nne tangu Soud kutekwa, familia yake ilipata habari kwamba alikuwa ameachwa katika kituo cha polisi cha Madema mjini Zanzibar. Familia ilimpata pale na kumpeleka katika hospitali iliyo karibu. Mkewe alielezea hivi:
Alikuwa katika hali mbaya ajabu. Miguu yake haikuwa na nguvu tena asingesimama au kuisongesha. Macho yake yalikuwa na matatizo pia. Alikuwa mlegevu bila nguvu mwilini. Aliniambia kwamba walikuwa wamemtesa. Alisema alikuwa amepitia maovu si haba. Singemuuliza maswali zaidi.
Alifariki siku kadhaa baadaye, tarehe 24 Novemba, Mwaka 2020 katika hospitali moja.
Mapendekezo
Ili kukomesha kurudia rudia wa vurugu na fujo misimu ya uchaguzi kisiwani Zanzibar:
- Serikali za Tanzania na Zanzibar, ikiwemo idara ya polisi nchini Tanzania na idara maalum za SMZ, zinafaa kuchunguza halafu baadaye kuondoa muundo msingi unaoyawezesha makundi ya wanamgambo kushirikiana na vikosi vya ulinzi kuendesha oparesheni visiwani Zanzibar – serikali zinatakiwa pia kufunga vituo visivyo vya kisheria vya kuwazuilia watu;
- Serikali za Tanzania na Zanzibar zinatakiwa kukomesha mwenendo wa wanamgambo kushiriki oparesheni za ulinzi na usalama na hali makundi hayo hayatambuliwi kisheria-likiwemo kundi la Mazombi.
Jamii ya kimataifa, wakiwemo washirika wa Tanzania kimaendeleo, na vilevile Umoja wa Afrika na wataalamu wao wa Haki za kibinadamu yanatakiwa yatoe shinikizo kwa serikali ya Tanzania kufanya yafuatayo:
- Ianzishe uchunguzi utakaofanywa kwa njia huru, wa kuaminika, usioegemea upande wowote kuhusiana na dhuluma za uchaguzi mkuu wa mwaka 2020;
- Baada ya uchunguzi ripoti itangaziwe umma ili kila mtu ajue kilichotokea wakati wa oparesheni za vikosi vya ulinzi msimu wa uchaguzi huo; halafu
- Ihakikishe kwamba vikosi vyote vya ulinzi vilivyohusika katika dhuluma na mateso dhidi ya raia vinachukuliwa hatua za kisheria kulingana na sheria za Tanzania na vilevile kwa mujibu wa sheria za kimataifa na haki za binadamu.