Skip to main content

(Nairobi) – Mamlaka nchini Tanzania zimeua takribani watu wanne na kutekeleza vitendo vingine vya unyanyasaji mkubwa ambao umeharibu uchaguzi wa kitaifa mwishoni mwa mwezi Oktoba na mapema mwezi Novemba 2020, Human Rights Watch wamesema leo. Mamlaka zinapaswa kuchunguza unyanyasaji huu, kukomesha udhalilishaji wa wanahabari na wanasiasa wa upinzani na kuondoa vikwazo kwa vyombo vya habari vilivyoanza kabla ya siku ya uchaguzi.

Baada ya kuanza kampeni za uchaguzi mwezi Agosti, polisi waliwakamata kiholela na kuwaweka kizuizini viongozi na wafuasi wa vyama vya upinzani. Wiki kadhaa kabla ya uchaguzi, mamlaka ilisimamisha baadhi ya vituo vya televisheni na redio, ikakagua mawasiliano ya simu za mkononi na kuzuia mitandao ya kijamii. Usiku wa kuamkia uchaguzi polisi walifyatua risasi za moto katika kundi la watu katika kisiwa cha Zanzibar na kuuwa takribani watu watatu.

“Vitendo vya serikali ya Tanzania kukandamiza upinzani na vyombo vya habari wakati wa kampeni za uchaguzi vinadhoofisha uaminifu wa uchaguzi,” anasema Oryem Nyeko, mtafiti wa Afrika na Human Rights Watch. “Mamlaka zinapaswa kuchunguza kwa uwazi matukio ya unyanyasaji yanayohusiana na uchaguzi na kumaliza vitendo vya ukandamizaji vinavyoendelea sasa.”

Uchaguzi Tanzania bara ulifanyika Oktoba 28, na Zanzibar Oktoba 27 na 28. Oktoba 30, Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilitangaza kwamba Rais John Magufuli wa chama tawala-Chama cha Mapinduzi ameshinda kwa asilimia 84 ya kura zote mbele ya mpinzani wake mkubwa, Tundu Lissu wa upinzani, chama cha Chadema.

Human Rights Watch ilifanya mahojiano ya simu na watu 16 kati ya Oktoba 15 na Novemba 9 ikiwa ni pamoja na waandishi wa habari, maafisa wa vyama na wanafamilia wa watu wanaosemekana wameuliwa na polisi.

Human Rights Watch iliweka kumbukumbu ya kukamatwa kwa takribani maafisa 18 wa vyama vya upinzani, viongozi na wafuasi ikiwa ni pamoja na Lissu pamoja na mgombea mwingine wa kiti cha urais, Seif Sharif Hamad wa chama cha ACT Wazalendo kabla na baada ya uchaguzi. Chama cha Chadema kiliripoti kuwa wanachama wao wapatao 300 wamekamatwa nchi nzima katika kipindi hiki.

Human Rights Watch waligundua kwamba polisi iliwaua takribani watu watatu na kuumiza wengine wengi usiku kabla ya uchaguzi Zanzibar. Katika taarifa ya Novemba 10, Kamishna mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa alisisitiza uchunguzi wa madai ya kuuwawa kwa takribani watu 10 Zanzibar siku mbili kuelekea uchaguzi. Mnamo Novemba 11, inspekta jenerali wa polisi, Simon Sirro aliviambia vyombo vya habari kwamba ni watu wawili tu ndio waliokufa kutokana na “vuruga za hapa na pale” mnamo Oktoba 26 na kwamba mtu wa tatu, mwanajeshi aliuwawa na wafuasi wa upinzani mnamo Oktoba 28 lakini hakugusia tuhumua za polisi kuhusika.

Catherine Ruge, mgombea ubunge wa Chadema aliiambia Human rights Watch kuwa polisi waliwakamata na kuwapiga yeye pamoja na wenzake katika ofisi ya uratibu wa kampeni kaskazini mwa Wilaya ya Serengeti mnamo Oktoba 12. Polisi mmoja baadae alimdhalilisha kijinsia kwa kumshika isivyofaa akiwa kituo cha polisi, alisema. Alisema kwamba mmoja ya maafisa ambaye alimtambua alitishia kumuua kwa kumwambia, “Uchaguzi huu hautoisha kabla sijakuua.” Siku mbili baadae, Sirro, inspekta jenerali wa polisi aliviambia vyombo vya habari kuwa polisi itachunguza tuhuma za Ruge.

Huko Zanzibar, vyombo vya ulinzi vya serikali na kikundi kilichopangwa na serikali kinachojulikana kama “Mazombi,” walinyanyasa na kupiga watu kabla na kuelekea uchaguzi. Watu watatu kisiwani Pemba walisema kwamba katika kipindi hiki vyombo vya ulinzi mara kwa mara vinadhalilisha wakazi, kujitapa na bunduki na kufukuza watu katika maeneo ya wazi.

Kuelekea uchaguzi, mdhibiti wa vyombo vya habari, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) alizuia vyombo vya habari kutoa taarifa za uchaguzi na kuweka vikwazo kwa maudhui ya mtandaoni yenye kukosoa serikali. Mwandishi wa habari Unguja, Zanzibar aliiambia Human rights Watch kuwa Oktoba 29 polisi waliwaweka kizuizini kwa muda yeye na wenzake wawili katika kituo cha polisi walipokuwa wanajaribu kukusanya habari ya maandamano dhidi ya matokeo ya uchaguzi yaliyoandaliwa na ACT Wazalendo.

Tangu Rais Magufuli achukue ofisi mwaka 2015, mamlaka zimeongeza ukandamizaji kwa vyombo vya habari na vikundi vya asasi za kiraia kwa kupitisha na kusimamia sharia kandamizi na kutishia kufuta usajili wa mashirika yanayokosoa serikali. Serikali pia imeweka vikwazo kwa vyama vya upinzani na kumpa msajili wa vyama vya siasa wigo mpana wa kisheria ikiwa ni pamoja na kufuta usajili wa vyama vya siasa.

Mamlaka nchini Tanzania zinapaswa kuchukua hatua za haraka, za wazi na zisizo na upendeleo kuchunguza tuhuma za mauaji yatokanayo na uchaguzi, vipigo na udhalilishaji uliofanywa na vyombo vya ulinzi na kuwawajibisha waliohusika, Human Rights Watch wamesema. Serikali haina budi kurekebisha mapema iwezekanavyo sharia na kanuni kandamizi na kuhakikisha ulinzi wa haki kwa wote kama ilivyohakikishiwa katika sheria za kimataifa na kikanda za haki za binadamu ikiwa ni pamoja na Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu.

“Kuzorota kwa serikali ya Tanzania kuheshimu haki za kujieleza kwa uhuru, kujiunga na chama au kikundi chochote na mikusanyiko ya amani kulikuwa wazi kabisa katika kipindi cha uchaguzi,” anasema Nyeko. “Serikali ya Magufuli inapaswa kuchukua hatua madhubuti kuboresha heshima ya haki za binadamu kwa wote.”


Kwa maelezo zaidi ya unyanyasaji utokanao na uchaguzi, tafadhali angalia hapa chini.

Uchaguzi Tanzania

Mfumo wa serikali wa Tanzania umegawanyika katika serikali ya umoja, ambayo inawajibika kwa masuala yote yanayohusu nchi nzima ikiwa ni pamoja na visiwa vya Zanzibar na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Jeshi la Polisi Tanzania linafanya kazi Tanzania bara na Zanzibar na linasimamiwa na serikali ya jamhuri. Zanzibar inasimamia na kuratibu vikosi vyake vya usalama vinavyojulikana kama SMZ “idara maalumu” au “vikosi” sambamba na polisi wa Tanzania. Kikundi kivuli cha kijeshi, kinachojulikana kama Mazombi kimedhalilisha raia na wakosoaji wa serikali katika uchaguzi uliopita.

Kati ya mwaka 1977 na 1992, baada ya kuanzishwa kwa Chama cha Mapinduzi (CCM), Tanzania ilikuwa ikiendeshwa kama nchi ya chama kimoja. Mwaka 1992 Katiba ilirekebishwa kuruhusu mfumo wa vyama vingi. Chama cha Demokrasia na Maendeleo, au Chadema, ndio chama cha siasa cha pili kwa ukubwa na mpinzani mkubwa kwa CCM bara, wakati ACT-Wazalendo ndio chama kikubwa cha upinzani Zanzibar. Wapiga kura Zanzibar wanapiga kura kuchagua rais na wawakilishi wa bunge kwa visiwani pamoja na rais wa Tanzania na bunge. Wapiga kura wa bara wanachagua wawakilishi katika bunge na rais wa Tanzania. Tume ya Taifa ya Uchaguzi inaratibu uchaguzi wa jamhuri/umoja wakati Tume ya Uchaguzi Zanzibar inasimamia masuala ya uchaguzi Zanzibar.

Uchaguzi mkuu wa 2020 uliharibiwa nchi nzima kwa serikali kukandamiza wanasiasa wa upinzani na vyombo vya habari. Zanzibar inaonekana kuathirika vibaya zaidi kwa polisi kutekeleza matukio ya ukamataji holela, udhalilishaji, na kupiga risasi kabla, wakati na baada ya uchaguzi.

Risasi na Mauaji ya Polisi

Mashuhuda wawili na ndugu wa wahanga waliwaambia Human Rights Watch kuwa usiku wa kuamkia siku ya uchaguzi huko Zanzibar, polisi walipiga risasi za moto katika vikundi vya watu na kuua walau watu watatu.

Baba wa Yussuf Shaahame Muhidini, kijana wa miaka 25 alisema polisi walimpiga risasi za kifuani kijana wake usiku wa Oktoba 26 katika uwanja wa kijiji cha Kangagani kisiwa cha Pemba, Zanzibar. Anasema kwamba alitoa taarifa za tukio hilo kwa ‘Sheha,” kiongozi wa jamii, na polisi ambao hawakufanya chochote. Alimzika mwanae siku inayofuata, sambamba na watu wengine wawili wanaosemekana kuuwawa na polisi.

Asubuhi ya Oktoba 27, polisi wanatuhumiwa kumpiga risasi na kumuua Salum Ali Abdallah, miaka 28 katika mji wa Wete kisiwani Pemba, katika duka karibu na nyumbani kwake. Shuhuda anasema polisi wawili walivamia duka. Abdallah alipogundua kuwa walikuwa polisi, alipaza sauti, “Watakuja na kutuua sisi!” na kujaribu kukimbia. Alipokuwa anakimbia, polisi mmoja alimpiga risasi ya nyuma. Shuhuda anasema kwamba polisi walijaribu kuficha kidhibiti kwa kufunika damu iliyokuwa imemwagika chini na takataka/udongo kisha wakaondoka na mwili wake. Shuhuda anasema baadae alijua kuwa mwili wa Abdallah umepelekwa hospitali ya Wete.

Polisi wa Zanzibar waliambia vyombo vya habari baadae kwamba walikuwa wanawashikilia watu 42 kwa tuhuma za kuwarushia mawe polisi waliokuwa wanasambaza masanduku ya kura. Chama cha upinzani ACT Wazalendo kiliripoti kuwa takribani watu 10 waliuwawa Zanzibar

Ukamataji Holela na Udhalilishaji

Wakati na baada ya uchaguzi, polisi wa Tanzania waliwabana wanachama wa upinzani na kuwakamata kiholela takribani viongozi na wafuasi wa upinzani18.

Ruge, mgombea nafasi ya ubunge, anasema kwamba mnamo Oktoba 12, polisi wawili walijaribu kumuondoa yeye na wenzake kutoka katika ofisi ya maafisa wanaoshughulika na uratibu wa uchaguzi wilaya ya Serengeti.  Polisi hao walipata ushirikianowa polisi wengine, ikiwa ni pamoja na maafisa waandamizi wa polisi wa wilaya, ambao anawatuhumu kwa kumpiga na kumchania nguo zake, kisha kumchukua yeye na wenzake katika gari la polisi mpaka kituo cha polisi.

Ruge anasema kwamba akiwa kituoni na wakili wake, afisa wa kiume alimdhalilisha kijinsia kwa kumshika isivyopaswa kiuno na makalio. Anasema kwamba baada ya kutolewa baadae siku hiyo, maafisa nane walimfuata mpaka katika mgahawa wa karibu ambapo walimpiga mateke na kumpiga na rungu. Mamlaka imemshtaki Ruge sambamba na wengine watano kwa makosa kadhaa ikiwemo mkusanyiko kinyume cha sheria na uharibifu wa mali.

Vyombo vya habari viliripoti kuwa mnamo Oktoba 14, polisi huko Tarime, kaskazini mwa Mkoa wa Mara, walivamia nyumba ya mgombea ubunge wa Chadema, Esther Matiko, na kumkamata mtu mmoja. Mnamo Oktoba 23 na Oktoba 28, polisi walimkamata na kumwachia mwanachama wa Chadema, Halima Mdee. Edward Bukombe, kamanda wa polisi mkoa wa Kinondoni, alisema kwamba polisi walimkamata Mdee baada ya “ugomvi.”

Mnamo Oktoba 26, polisi walimkamata afisa wa chama cha ACT Wazalendo, Hamad Masoud Hamad, muda mfupi baada ya kutua Uwanja wa Ndege wa Pemba huko Zanzibar. Aliachiwa mnamo Novemba 2 bila mashitaka..

Polisi walimkamata na baadae kumwachia mgombea urais wa Zanzibar, Seif Sharif Hamad, katika kituo cha kupigia kura huko kisiwa cha Unguja mnamo Oktoba 27, baada ya kupinga wapiga kura kupewa karatasi mbili hadi tatu za kupigia kura kwa ajili ya kupiga kura. Mnamo Oktoba 29, Hamad aliwataka wafuasi wa chama chake kupinga matokeo ya uchaguzi, ambao alisema ulikuwa umeibiwa. Polisi walimkamata yeye pamoja na wengine 40 kabla ya maandamano kuanza, lakini baadae walimuachia Hamad kwa dhamana, wakati wengine wakibaki kizuizini katika Kituo cha Polisi cha Madema.

Mnamo Novemba 1, polisi walimkamata mwenyekiti wa Chadema, freeman Mbowe, na wanachama wa chama hicho Godbless Leman a Boniface Jacob, siku moja kabla ya maandamano yaliyoitishwa na Chadema na ACT Wazalendo kupinga matokeo ya uchaguzi unaotuhumiwa kuibiwa. Mnamo Novemba 2, polisi walimshikilia na baadae kumwachia Lissu, mgombea urais wa upinzani, katika ofisi za Umoja wa Ulaya Dar es Salaam kwa kinachodaiwa ni kuhusu maandamano. Lissu baadae aliambia vyombo vya habari kutokana na tishio la maisha yake, wakati wa kukamatwa kwake alikuwa akitafuta hifadhi katika makazi ya balozi wa Ujerumani. Wiki iliyofuata, Lissu na Lema waliondoka Tanzania wakisema ni kutokana na kuendelea kutishiwa maisha yao.

Lissu, kiongozi maarufu wa upinzani na mbunge wa zamani, hapo awali ameshakuwa shabaha ya mashambulizi. Aliondoka nchini Septemba 2017 baada ya watu wasiojulikana kumpiga risasi, na kumwacha akiwa na majeraha makubwa nje ya nyumba yake katika mji mkuu wa Tanzania, Dodoma. Ijapokuwa serikali ilisema hapo awali kuwa ilikuwa ikichunguza shambulio hilo, hakuna yeyote aliyekamatwa kwa tukio hilo kwa kipindi cha miaka mitatu. Lissu alirudi Tanzania Julai 2020.

Mnamo Novemba 17, mamlaka zilimwachia naibu katibu mkuu wa ACT Wazalendo, Nassor Mazrui, baada ya kukaa siku 23 kizuizini. Katika taarifa yake ya Oktoba 28, chama kiliripoti kuwa Mazrui ametekwa akiwa nyumbani kwake usiku na kupigwa.  Baadae polisi walisema kwamba Mazrui na wengine 32 walikuwa wameshikiliwa kwa kumiliki vifaa ambavyo vingeweza kuingilia mfumo wa uchaguzi. Maafisa wa ACT Wazalendo walisema kwamba walinyimwa kuwaona wanachama wao wote waliokuwa wameshikiliwa  kwa siku kadhaa.  Siku kadhaa kabla ya kukamatwa kwake, Mazrui aliambia Human Rights Watch kwamba alikuwa ametekwa awali na kushikiliwa na saa tano na watu takribani sita wasiojulikana mnamo Oktoba 25 alipokuwa anaelekea ofisini kwake katika kisiwa cha Unguja Zanzibar.

Watu huko Zanzibar wanasema kuwa katika kipindi cha kuelekea uchaguzi na siku baada, vyombo vya ulinzi mara kwa mara vilidhalilisha watu. Mkazi wa Kangagani alisema kuwa polisi walivunja mlango wa jirani yake  usiku,wakawapiga watu na kuchukua vitu katika nyumba zao. Wengine wanasema waliona watu wenye silaha walioficha nyuso zao wakiwa katika fulana nyeusi za kikundi cha serikali cha Mazombi wakikamata watu kiholela katika mitaa ya Unguja, kuwapiga na kuwaweka kizuizini.

Uvunjifu wa Haki ya Kuzungumza; Vizuizi kwa Vyombo vya Habari

Mnamo Agosti 27, mdhibiti wa vyombo vya habari Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, iliwaagiza Clouds TV na Clouds FM kusitisha kurusha matangazo yao kwa muda wa siku saba na kuomba radhi kwa tuhuma za kurusha matokeo ya uteuzi wa wagombea ambayo hayakuwa yamethibitishwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Mnamo Oktoba 21, mamlaka ya vyombo vya habari Zanzibar ilisimamisha TV ya mtandaoni ya RVS, kituo cha mtandaoni cha televisheni, kwa kipindi cha miezi miwili kwa tuhuma za kushindwa kutangaza uchaguzi bila upendeleo.

Mamlaka pia zinaonekana kuwazuia waandishi wa habari wa kigeni kutoa habari za uchaguzi baada ya kushindwa mara kadhaa kujibu maombi ya ithibati/idhini. Waandishi wa habari wanne wa kigeni walisema kwamba waliandika kwa maafisa wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo wiki kadhaa kabla ya uchaguzi kuomba idhini lakini hawakupata majibu yoyote. Hii inafuatia kanuni za mwezi Juni za serikali zinayokataza watangazaji wa Tanzania kufanya kazi na wenzao wa kigeni bila ya uwepo wa afisa kutoka mamlaka ya udhibiti au wakala mwingine wa serikali kuwepo. Waandishi wa habari wa kigeni waliopata idhini ya kukusanya habari za uchaguzi Zanzibar wanasema maafisa wa ulinzi waliwazuia kuingia katika maeneo ya kupigia kura.

Mnamo Septemba 18, mamlaka zilimshtaki Dominic Mgaya, afisa wa Chadema, kwa kuweka maudhui katika chaneli ya chama ya Youtube, Chadema TV, bila ya kuwa na leseni inayotolewa na mamlaka ya Mawasiliano. Mamlaka ya udhibiti ina nguvu kubwa kisheria kutoa leseni kwa blogu, tovuti na mudhui ya mtandaoni. Mgaya alitolewa kwa dhamana na kesi yake bado inaendelea.

Mamlaka pia iliweka vikwazo kwa simu za mkononi na mawasiliano ya mtandaoni kuelekea uchaguzi. Mnamo Oktoba 21, TCRA iliagiza kampuni zinazotoa huduma za simu kusitisha huduma ya meseji za jumla mpaka baada ya uchaguzi, kuwazuia wagombea kuwafikia watu wengi. Siku moja kabla ya uchaguzi bara, Twitter iliripoti “kuzuiwa na kuminywa” kwa mitandao ya kijamii Tanzania.

Mashirika ya uhuru wa mtandao Open Observatory of Network Interference na NetBlocks Internet Observatory ilionyesha uwezekano wa kuwepo kwa usumbufu wa mtandao nchini ukilenga Twitter na huduma za ujumbe mfupi ikiwa ni pamoja na WhatsApp. Ili kupata mtandao na huduma za mitandao ya kijamii, Watanzania walianza kutumia mitandao binafsi (VPNs). Hata hivyo mnamo Oktoba 28, watoa huduma za VPN Proton VPN walitoa ujumbe Twitter kuwa VPNs zinazuiwa nchini.

Mnamo Septemba 25, polisi walimkamata afisa wa ACT Wazalendo, Dotto Rangimoto na wenzake Arodia Peter na Dahlia Majid katika ofisi zao na kuwashikilia katika kituo cha polisi cha Oysterbay jijini Dar es Salaam. Majid na Peter waliachiwa baadae wakati Rangimoto aliendelea kushikiliwa kwa siku 10 bila kufunguliwa mashitaka, ambapo ni uvunjifu wa sharia za Tanzania ambazo zinataka mtuhumiwa kufunguliwa mashitaka ndani ya saa 48.

Rangimoto aliambia Human Rights Watch kwamba akiwa kituo cha polisi, polisi walimpiga na kumtaka awape nywila ya barua pepe yake na akaunti zake za mitandao ya jamii. Polisi walimwambia kuwa alikuwa anashikiliwa kwa kumtukana Rais Magufuli katika mtandao wa Twitter. Rangimoto baadae alifunguliwa mashtaka ya kuvunja sheria ya Makosa ya Mtandaoni kwa tuhuma za kusambaza video za utupu mtandaoni.

Your tax deductible gift can help stop human rights violations and save lives around the world.

Region / Country