(Nairobi) – Wanawake wengi nchini Kenya wameendelea kukosa haki za kudai mali walizochuma wakiwa katika ndoa, licha ya kuwepo hatua kadhaa katika sheria zilizondikwa. Human Rights Watch na Chama cha Wanawake Wanasheria (FIDA-Kenya) wamesema katika taarifa yao iliyotolewa leo. Rufaa ya hivi majuzi mbele ya Mahakama ya juu Tarehe 21 Juni , 2020, dhidi ya uamuzi wa mahakama ya ngazi ya chini imeliweka swala hili mbele ya Mahakama. Uamuzi wa rufaa hiyo utakuwa suluhu ya shaka zilizomo katika sheria huku ukitoa ushauri wa namna ya kufafanua jinsi ambavyo mali iliyopatikana katika ndoa inafaa kugawanywa. Kenya inafaa kuongeza nguvu katika kufanya marekebisho makubwa ya kisheria ili kupata usawa wa kumiliki mali katika ndoa.
Ripoti ya kurasa 64, “Mara tu Unapoondoka, Unapoteza Kila Kitu” inaonyesha namna ambavyo Sheria ya Haki za Mali kwa Wanandoa ya 2013, ambayo inatambua kwamba wanawake walioolewa wana haki sawa na wanaume waliooa, pamoja na marekebisho mengine ya sheria yanavyopuuzwa katika utekelezaji.
Katiba ya Kenya inaendana na tafsiri ya kimataifa ya usawa na kutokuwepo kwa ubaguzi lakini inashindwa kuhakikisha mabadiliko makubwa na muhimu kutokana na ukosefu wa utekelezaji. Katika kuangalia hali halisi kwenye kaunti mbili, Human Rights Watch wamegundua kwamba sheria zenye utata ambazo pia ni za zamani na zimebaki katika vitabu pamoja na mienendo na mazoea ya ubaguzi katika jamii zinafanya iwe vigumu kwa wanawake walioolewa, walioachwa, waliotengana na waume au wajane kudai mali ambazo ni haki zao kisheria.
“Sheria za sasa zinazohakikisha haki za wanawake walioolewa juu ya mali walizochuma ndani ya ndoa hazitekelezwi inavyofaa,” anasema Juliana Nnoko-Mewanu, mtafiti wa masuala ya wanawake na ardhi katika Human Rights Watch. “Serikali inapaswa kufafanua katika sheria kipi kinachohesabiwa kuwa mchango wa mwanamke kwenye mali ya ushirika, namna ya kupima thamani yake, na mwisho namna mchango ule unavyohesabiwa kama mali inayomilikiwa kwa ushirika pale ndoa inapovunjika.”
Human Rights Watch na FIDA-Kenya walifanya mahojiano na zaidi ya watu 60, ikiwa ni pamoja na wanawake waliotengana na waume zao, wale walioachwa au wajane, na kuchambua takwimu za kesi 56 za kugawana mali baada ya kuachana. Kesi hizo zilikuwa zile zilizotolewa hukumu kati ya mwaka 2014-2019 katika mahakama za Kaunti za Kakamega na Kilifi. Human Rights Watch na FIDA-Kenya pia waliangalia mfumo wa sheria unaotumika kutoa uamuzi katika kesi kama hizo.
Human Rights Watch na FIDA-Kenya wamegundua kwamba taratibu zote za kimahakama na zile zisizo za kimahakama ambazo zinaamua ugawaji wa mali zilizochumwa katika ndoa wakati wa kuvunjika kwa ndoa iwe kupitia talaka au kifo zinabagua na kutishia wanawake kudai sehemu ya mali.
Licha ya uwepo wa mfumo wa sheria unaozingatia “masuala ya jinsia” nchini Kenya, wanawake wanakabiliana na vikwazo mbalimbali vya kijamii, kisheria na kimahakama katika kudai sehemu ya mali. Ijapokuwa sheria iko wazi kuhusu mchango wa kifedha na ule usiokuwa wa kifedha kuzingatiwa katika ugawaji wa mali pale ndoa inapovunjika, sio sheria wala Mahakama inayofafanua ni vithibitisho gani vya uchangiaji vinavyotakiwa, na namna mchango huo unavyohesabiwa katika kugawa mali.
Majaji wanaachwa kuamua wenyewe juu ya vithibitisho na hesabu ya uchangiaji. Katika kesi nyingine, majaji wamewataka wanandoa kutoa stakabadhi za kuthibitisha miaka mingi ya ndoa, kuwabagua baadhi ya wanawake ambao mchango wao mkubwa haukuwa wa kifedha. Majaji wengine hawatambui huduma ya kujali ambayo wanawake hutoa pamoja na kazi za ndani ya nyumba huku wengine wakitambua.
Sheria zilizopo pia sio thabiti. Sheria za urithi hazitimizi haki iliyomo katika sheria ya 2013 ya kupata mali ambazo zilipatikana kupitia ushirikiano kati ya mume na mke. Chini ya Sheria ya mirathi, mume au mke aliyebaki anakuwa mmiliki wa mali binafsi na za nyumbani za mwenza aliyefariki, lakini anakuwa na nguvu ya “maslahi ya maisha” katika mali nyingine kama vile ardhi na nyumba katika kipindi cha uhai wake.
Mwenza aliyebaki hawezi kuuza mali isiyoweza kuhamishwa bila ruhusa ya mahakama. Vilevile mjane anapoteza haki zake za kutumia mali hii pale anapoolewa na mtu mwingine. Sheria pia inasamehe ardhi ya kilimo, mazao na mifugo katika baadhi ya wilaya kama hakuna wosia. Suala la urithi katika kesi kama hizi liko chini ya imani za kijamii na kimila, ambazo kwa kiasi kikubwa zinawabagua wanawake na wasichana
Hata kama sheria zipo na kanuni zake zinaeleweka, wanawake wanakabiliana na vikwazo katika kupata haki kupitia mahakama. Vikwazo vingi ni pamoja na ufahamu mdogo wa wanawake juu ya haki zao, kukosa kufikia habari zinazowafaa, gharama kubwa za huduma ya kisheria, umbali wa mahakama na ugumu katika kukusanya vithibitisho vinavyotakiwa
“Pale unapotumikia jambo fulani [ndoa] kwa miaka 10 na kupoteza kila kitu kufumba na kufumbua, inaumiza mno,” anasema mwanamke mwenye umri wa miaka 40 ambaye mume wake amemfukuza nyumbani. “ Sina pesa. Mimi sio tajiri kama alivyo yeye [mume]. Nitaanzia wapi na nitaanza vipi?’
Nchini Kenya baadhi ya mila na desturi za jamii juu ya ndoa na njia zinazoongoza mahari, mila kuhusiana na watoto baada ya talaka, na imani zinazowabagua wanawake ikija katika kumiliki ardhi na mali zinaongeza ugumu kwa baadhi ya wanawake kupata mali walizochuma wakiwa katika ndoa.
Haki za wanawake juu ya ardhi na rasilimali nyingine za kuzalisha, kama vile kupata mkopo na pembejeo za kilimo zinaingiliana na umiliki wao wa mali ndani ya ndoa. Swala la kuhakikisha ugawaji ulio wa haki na ulio sawa wa mali za ndoa ni hatua muhimu ya kulinda haki za wanawake.
Sheria zilizo wazi na za haki juu ya ugawaji wenye haki na usawa wa mali za ndoa pia zinatoa utambuzi muhimu wa kisheria wa thamani ya mchango wa kiuchumi wa mwanamke katika ndoa. Wanawake hufanya kazi za nyumbani na huduma ya kujali, bila shaka zote zikiwa ni kazi wanazofanya bila malipo.
Mikataba na makubaliano ya kimataifa na kikanda ambayo Kenya imeikubali na kuitia saini inahakikisha haki ya usawa na kukataza ubaguzi kwa misingi ya jinsia. Serikali ina wajibu wa haki za binadamu kuhakikisha haki sawa kwa wanawake katika ndoa na hata wakati wa talaka. Serikali ya Kenya inapaswa kuchukua hatua muhimu kushughulikia vikwazo katika kutekeleza sheria ya 2013, itoe ufafanuzi unaoeleweka na miongozo kwa maafisa wa mahakama ili kuwe na uelewa mpana wa namna ambapo kuhusika kwa mwanamke kunaweza kupewa thamani ikija kwenye mali za ndoa ili sheria zote ziwe zinatekelezwa kuhakikisha haki na usawa.
“Serikali ya Kenya inapaswa kuchukua hatua katika misingi ya usawa, isiyobagua ili kuhakikisha kwamba haki za wanawake zinalindwa,” Nnoko Mewanu anasema. “Serikali inapaswa kuwahakikishia wanawake sehemu yao ya mali za ndoa katika sheria na katika uhalisia.”
Baadhi ya matukio yaliyotolewa katika ripoti
“Jina langu halipo popote katika mali yoyote tuliyoipata hata kama nilichukua mkopo kutoka katika chama [kikundi cha fedha cha wanawake] kulipia mali hiyo. Yeye [mume] hakuruhusu jina langu kuwepo katika hati. Alisema ‘Mimi’ ndio mwanaume wa nyumba, nilichonacho unacho. Nikimiliki, unamiliki pia.’ Kwa mujibu wa mila zao [Kisii] wanawake hawawezi kumiliki chochote katika jina lao. Nani atanisaidia mimi kupata sehemu yangu? Niko peke yangu.”
– Ruth K., mama wa umri wa miaka 40 mwenye watoto wawili kutoka Taita, Mtwapa, Kaunti ya Kilifi. Mwaka 2016 mume wake alimfukuza katika nyumba yao na kubaki bila chochote.
“Alinipiga na kunifukuza nyumbani usiku. Alichukua pesa zote zilizokuwa katika mkoba wangu na katika akaunti ya simu yangu. Nilipoteza vingi usiku ule. Nilipoteza makao na kupoteza mapato kutoka katika mali niliyoiendeleza. Na bado lazima nilipe deni la shilingi milioni 1.5 (sawa na dola $ 13,951) ambazo nilitumia kujenga nyumba ambayo [aliyekuwa mume wangu] sasa anaishi na mwanamke mwingine. Kitu cha pekee ninachotaka ni nyumba yangu.”
– Fatuma M., mwanamke wa kiislamu wa umri wa miaka 47 na mama ya watoto watano Kilifi, Kaunti ya Kilifi. Katika kipindi cha miongo miwili cha kuishi pamoja na kisha kuoana, yeye na mumewe walijipatia mali nyingi. Mwaka 2018, mume alimfukuza nyumbani bila kumpa chochote. Kwa sasa anaishi katika nyumba ya chumba kimoja inayomilikiwa na serikali. Alipewa nyuma ile na mwajiri wake.
“Katika mirathi, mke hana chochote. Vivyo hivyo katika talaka. Anachukua vitu vyake binafsi – hakuna kingine na anaacha watoto wake. Ukweli kuhusu utamaduni, pale wewe [mwanamke] unapotoka, unapoteza kila kitu.”
– Dickson Kanana, mzee wa kijiji Kirao, Malindi Kaunti ya Kilifi
“Ninajua kuna mahakama ambazo bado zinashikilia suala la mchango. Na hapo ndipo mwanamke anataabika pindi anapokuwa mama wa nyumbani. Kama utashikilia mchango wa moja kwa moja, inamaanisha wao [wanawake] wanapoteza kila kitu.”
– William Musyoka, Jaji wa Mahakama Kuu, Kaunti ya Kakamega
“Sheria inasema ninapaswa kutoa alama. Ni alama ngapi kwa kila kigezo? Vigezo vipi vina uzito zaidi? Kutokana na vipimo vya kubuni vinavyotolewa katika hesabu ninatumia kufanya mgao [wa mali]. Lakini hesabu hiyo yaweza kuwa na makosa. Ni namna gani ninahakikisha hesabu inajaribiwa katika kipindi kirefu kutokana na kanuni za msingi za mamlaka? Misingi ya usawa, haki na ugawanaji. Mwisho wa siku ugawanaji huo ni fedha kwa fedha, mita za mraba kwa mita za mraba. Namna gani unafikia hesabu za kuleta maana kwa dola au mita za mraba?”
– Reuben Nyakundi, Jaji wa Mahakama Kuu, Kaunti ya Kilifi