Skip to main content

Afrika: Fanya Upatikanaji wa Elimu wa Wasichana kuwa Kweli

Ondoa Ufukuzaji wa Wanafunzi Walioolewa na Wajawazito kutoka Shule

© 2017 Marco Tibasima kwa Human Rights Watch

(Dakar)- Mamilioni ya wasichana wajawazito na walioolewa katika nchi nyingi za Afrika wananyimwa elimu kwa sababu ya sera na mienendo ya kibaguzi, Human Rights Watch wamesema leo katika siku ya Mtoto wa Afrika. Zaidi ya wasichana milioni 49 wameacha shule za msingi na sekondari Kusini mwa Jangwa la Sahara, ambapo milioni 31 kati yao wako nje ya elimu ya sekondari jambo ambalo linadhoofisha haki zao na kukwamisha fursa zao.

Ndoa za mapema na mimba za utotoni ni vikwazo vikubwa. Kusini mwa Jangwa la Sahara, asilimia 40 ya wasichana wanaolewa kabla ya umri wa miaka 18, na nchi za Afrika ni miongoni mwa nchi 15 kati ya 20 zenye kiwango cha juu zaidi cha ndoa za utotoni ulimwenguni.  Bara hili pia lina kiwango cha juu cha uwepo wa mimba za utotoni duniani. Katika nchi 14 za Kusini mwa Jangwa la Sahara, kati ya asilimia 30 na 51 ya wasichana wanapata watoto kabla ya umri wa miaka 18. Imani za kitamaduni na kidini mara nyingi zinanyanyapaa wasichana wasioolewa, wajawazito na matokeo yake wasichana wengi wajawazito hulazimishwa kuingia katika ndoa za mapema.


“Bara la Afrika lina kiwango cha juu cha mimba za utotoni duniani lakini serikali nyingi zinasisitiza kushughulikia changamoto hii ya kijamii na afya ya umma kwa kuwaadhibu wasichana na kuhatarisha maisha yao ya baadaye,” anasema Elin Martínez, mtafiti wa haki za watoto na Human Rights Watch. “Serikali zinapaswa kusaidia wasichana kujikinga na mimba zisizotarajiwa na kusaidia juhudi zao za kuendelea na masomo.”

Ijapokuwa nchi nyingi za Kusini mwa Jangwa la Sahara Afrika zimeweka ahadi ya kuhakikisha elimu ya msingi na sekondari ngazi ya chini ni lazima kwa watoto wote, nchi nyingi zinafukuza au kuwatenga mashuleni wasichana wenye mimba na wale wenye watoto.”
 

Tanzania na Sierra Leone ni miongoni mwa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara zenye sera na mienendo yenye madhara ambazo zinabagua dhidi ya wasichana wajawazito au walioolewa, tafiti ya Human Rights Watch inaonyesha. Huko Tanzania, Human Rights Watch iligundua kwamba maofisa wa shule hufanya vipimo vya mimba na kufukuza wanafunzi wenye mimba. Rita, mwenye miaka kumi na nane kutoka Kaskazini mwa Tanzania alisema alifukuzwa shule alipopata mimba akiwa na umri wa miaka 17. “Walimu waligundua nilikuwa na mimba,” anasema. “Nikagundua kuwa wanafunzi wenye mimba hawakuruhusiwa kuendelea na shule … sikuwa na taarifa [elimu ya uzazi] kuhusu mimba na kipi kinaweza kutokea.”
 

Baadhi ya nchi ikiwa ni pamoja na Cameroon, Afrika Kusini na Zambia zimepitisha sera ya “kujiunga upya” ili kuwezesha wasichana wenye watoto kurudi shule baada ya kujifungua. Hata hivyo, hata kama serikali zina sera hizi, maofisa wa shule mara nyingi hushindwa kuzitekeleza ipasavyo au kutokuzitekeleza kabisa. Wasichana wenye watoto mara nyingi hukosa usaidizi wa kujiunga na shule kutokana na ada za shule na gharama zinazohusiana, usaidizi pungufu kutoka katika familia zao, unyanyapaaji shuleni, na ukosefu wa huduma nafuu za ulezi na huduma zinazohusiana na watoto.

Wasichana wengi hupata mimba kutokana na ukosefu wa taarifa za kuwasaidia kufanya maamuzi sahihi kuhusu kujamiiana, mpango wa uzazi na afya ya uzazi, wakati wengine hulazimishwa kushiriki vitendo vya ngono na kuhitaji ulinzi na upatikanaji wa huduma za kiafya na msaada. Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, asilimia 80 ya wasichana wenye umri kati ya miaka 15 hadi 24 wenye maambukizi ya HIV ulimwenguni wanaishi Kusini mwa Jangwa la Sahara na barani Afrika kwa ujumla, na wasichana wenye umri kati ya miaka 15 hadi 19 wana uwezekano mara tano zaidi kuambukizwa virusi vya HIV zaidi ya wavulana.

Elimu ya uzazi na kujamiiana mara nyingi haijumuishwi katika mitaala ya shule kitaifa. Katika nchi chache ambazo zinajumuisha uhamasishaji wa HIV au program za “stadi za maisha” au masomo, walimu mara nyingi hukataa kufundisha masomo haya kwa sababu ya maudhui ya elimu ya kujamiiana na afya ya uzazi au kutokana na vikwazo vya muda wa kufundisha na rasilimali.

Serikali zote za Afrika zimeweka azimio kwa Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa kuhakikisha usawa wa kijinsia na upatikanaji wa elimu bure ya msingi na sekondari kila mahali kwa watoto wote ifikapo 2030. Umoja wa Afrika umetambua umuhimu wa kuondoa ndoa za utotoni na kuelewa kwamba ni kikwazo kikubwa kwa maendeleo na mafanikio ya kanda na kuondoa aina zote za ukatili wa kijinsia na ubaguzi.  

Serikali za Afrika zinapaswa kuhakikisha kwamba wasichana wanapata fursa sawa za kupata elimu bora na bure ya msingi na sekondari, na msaada wa kuendelea kuwepo shule, Human Rights Watch walisema. Serikali zinapaswa kurekebisha sera na mienendo yenye madhara ambayo inanyanyapaa wasichana ikiwa ni pamoja na vipimo vya lazima vya mimba na kanuni ambazo zinaruhusu wasichana wajawazito au walioolewa kufukuzwa shule. Serikali pia inabidi ipitishe sheria ambayo inaweka wazi miaka 18 kama kiwango cha chini cha ndoa kwa wanaume na wanawake.

Pia wanapaswa kupitisha miongozo ya wazi ambayo inatoa maelekezo kwa shule kuwasajili upya wanafunzi wenye watoto, kutoa huduma ya msaada katika shule na kuhakikisha kina mama vijana wanapata huduma za malezi ya watoto. Serikali lazima pia ihakikishe kwamba watoto wote kulingana na umri wao wanapata elimu ya kina ya kujamiiana na afya ya uzazi. Ikiwezekana, huduma za shule ziunganishwe na huduma za kiafya zilizo rafiki na vijana ili kuhakikisha kwamba vijana wanapata taarifa bila upendeleo wala kuhukumiwa.

“Serikali inawajibu mkuu wa kuhakikisha kwamba wasichana wanapata elimu bure ya msingi na sekondari bila ya kukumbana na unyanyapaaji au ubaguzi,” anasema Martínez. “Serikali zote hazina budi kutupilia mbali sera ambazo zinawatenga wasichana wenye mimba au walioolewa na kuweka hatua maalum kuhakikisha wasichana wote wanaweza kwenda shule.”

Kwa Maneno ya Wasichana Wenyewe

Malawi

Huko Malawi, takribani nusu ya wasichana wote huolewa kabla ya miaka 18. Kati ya mwaka 2010 na 2013, wasichana 27,612 wa shule za msingi na 4,053 wa shule za sekondari waliacha shule kutokana na ndoa. Katika kipindi hicho wasichana wengine 14,051 wa shule za msingi na 5,597 wa shule za sekondari waliacha shule kutokana na kuwa na mimba.

Wasichana waliwaambia Human Rights Watch kwamba ndoa ziliingilia au kusitisha elimu yao ikiwa ni pamoja na ndoto za kuwa madaktari, walimu au wanasheria. Wengi walisema kwamba hawakuweza kurudi shule baada ya ndoa kutokana na ukosefu wa fedha za kulipa ada, huduma za mtoto, mpango rahisi na rafiki wa shule au madarasa ya watu wazima na mahitaji ya kukamilisha kazi za nyumbani. Wengine walisema kwamba waume zao au ndugu wa wanaume hawakuwaruhusu kwenda shule.

Kabwila N., 17, alisema aliacha shule darasa la nane akiwa na umri wa miaka 15 kutokana na umasikini. Anasema hakuweza kurudi shule kwa sababu alijiskia aibu kutokana na mimba: “Nisingependa kurudi shule kwa sababu nilianza kufanya mapenzi na mpenzi wangu nikiwa shule. Siko sawa kurudi shule.”
 

Sudan Kusini

Huko Sudan Kusini, asilimia 52 ya wasichana wanaolewa kabla miaka 18 ya kuzaliwa. Kwa mujibu wa UNESCO, zaidi ya watoto milioni 1.3 walio katika umri wa kwenda shule za msingi wako nje ya shule na nchi hii ina idadi ndogo zaidi duniani ya uandikishaji wa shule za sekondari ambayo ni asilimia nne.


Mary K., kutoka eneo la Yambio alisema: “Baba yangu alinikataza kwenda shule. Alisema ni kupoteza fedha kumsomesha mtoto wa kike. Alisema ndoa itanifanya niheshimike katika jamii. Sasa nimekuwa na nimetambua kwamba haikuwa kweli. Siwezi kupata kazi kusaidia familia yangu na ninawaona wasichana wenye elimu wanapata kazi.”

Anyier D., 18, anasema mjomba wake alimlazimisha kuacha shule akiwa na umri wa miaka 14 mwaka 2008 ili aolewe na mwanaume mzee ambaye hakuwa anamjua: “Ningetamani kurudi shule hata kama nina watoto. Watu wanafikiri kwamba nina furaha lakini si kweli kwa sababu sina elimu. Sina kitu ambacho ni cha kwangu na nimebaki nasafisha ofisi tu. Kama ningeenda shule ya sekondari ningepata kazi nzuri.”

Tanzania

Huko Tanzania, chini ya theluthi ya wasichana ambao wamemaliza elimu ya msingi wanamaliza elimu ya sekondari ngazi ya chini na zaidi ya wasichana 15,000 wanaacha shule kwa mwaka kutokana na mimba. Human Rights Watch iligundua kwamba katika baadhi ya kesi wasichana huacha shule katika sekondari ngazi ya chini kutokana na unyonyaji wa kingono na ukatili wa walimu.

Joyce, 17, kutoka Shinyanga alisema: “Kuna walimu ambao wanamahusiano ya kimapenzi na wanafunzi – Nawajua wengi [wasichana] ambao imewatokea … kama mwanafunzi akikataa, anapewa adhabu … najiskia vibaya … hata kama utatoa taarifa juu ya jambo hili halitapewa uzito. Inatufanya tujiskie hatuko salama. Wasichana watatu waliacha shule kutokana na walimu na ngono mwaka 2015.”

Your tax deductible gift can help stop human rights violations and save lives around the world.

Region / Country