Ukandamizaji ulishamiri chini ya uongozi wa Rais alietangulia, John Magufuli, kama anavyoelewa vema Tito Magoti, mwanasheria na mwanaharakati ambaye alikamatwa mwaka 2019 na kuwekwa kizuizini bila ya kesi kwa zaidi ya mwaka mmoja. Hii ni baada ya maafisa usalama wasiokuwa na sare kumfunga Magoti kitambaa usoni na kumuingiza kwenye gari, walimshutumu kuwa gaidi. Alishikiliwa kwa mashitaka yasiyokuwa na msingi ya “uhalifu wa kiuchumi,” ikiwa ni pamoja na utakatishaji fedha na kuongoza genge la uhalifu, makosa ambayo hayana dhamana kwa mujibu wa sheria za Tanzania.
Sasa yuko huru akiishi chini ya uongozi wa Rais mpya – Samia Suluhu Hassan, ambaye alichukua ofisi hiyo mwezi Machi 2021 kufuatia kifo cha Magufuli – Magoti, 31, anaendelea na kazi zake za kutetea haki za binadamu.
Mtafiti wa Human Rights Watch wa Tanzania, Oryem Nyeko, alizungumza na Magoti kuhusu maoni yake juu ya mageuzi yanayofanywa na Rais Suluhu Hassan na mambo yaliyobadilika na yale yaliyobaki vile vile nchini Tanzania tangu awe Rais miaka mitatu iliyopita.
Historia yako ilikuaje kama mwanaharakati wa haki za binadamu kabla ya kukamatwa kwako mwaka 2019?
[Hapo awali] nilikuwa napaza sauti na kukosoa juu ya utawala na siasa nchini Tanzania. Nilifuatilia kila hotuba ya kila kiongozi mkubwa nchini na kuthibitisha kile kinachosemwa kila mara wanapoongea, kuchambua kile wanachosema na kutoa maoni yangu. Muda wowote anapozungumza Rais, nilikuwa nathibitisha kile anachokisema. Nilikuwa nahojiwa na vipindi mbalimbali vya TV na kujadili masuala yanayozungumzwa zaidi.
Vile vile kulikuwa na kazi yangu na [shirika la kiraia la masuala ya haki za binadamu Tanzania] Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu. Nilikuwa nafanya utafiti kuhusu biashara na haki za binadamu kabla sijawa afisa uhusiano wa umma ninayeshughulikia elimu ya haki za binadamu. Kazi hii ilinipa fursa ya kufundisha masuala ya haki za binadamu kwa waandishi wa habari, waangalizi wa haki za binadamu, watoa huduma za kisheria na wanafunzi wa vyuo vikuu.
Wakati huo nilikuwa nafuatiliwa. Serikali iliweka watu wa kunifuatilia. Baadhi ya maafisa hao walikuwa wakiwauliza marafiki zangu kuhusu mimi, mahali nilipo na masuala yangu binafsi. Walikuwa wakinifuatilia wakati nikiwa Dodoma [Mji Mkuu wa Tanzania]
Nilikuwa mtumiaji mzuri wa Twitter. Nilikuwa namkosoa Rais Magufuli bila uoga na [aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda] ambaye ilisemekana alikuwa mtu wa karibu na Rais aliyepita.
Nini kilikuleta katika ulimwengu huu wa uanaharakati na haki za binadamu?
Nilianza kujihusisha na uanaharakati wa haki za binadamu nikiwa shule ya sekondari, hususan kidato cha nne na tano. Nakumbuka kuwindwa kwasababu sikukubaliana na vitendo vya kikatili vilivyokuwa vinafanywa dhidi yetu na walimu.
[Uanaharakati wangu] ulishamiri nilipochagua kusoma shahada ya sheria. Nilijiunga na vyama vya haki za binadamu na nilikuwa na ari ya kusaidia watu, hususan wanafunzi wenzangu. Tulianzisha taasisi ya kusaidia vijana kufikia ndoto zao za kupata elimu. Tulijikita zaidi katika kusaidia watu wasiojiweza na wale walioko kwenye hali ngumu hususan yatima. Tulitembelea shule na vituo vya watoto yatima na kuwapatia kidogo tulichokuwa nacho kuwatia moyo na kuwasaidia vifaa mbalimbali.
Nikiwa chuo kikuu nilikuwa katibu mkuu wa kwanza wa chama cha haki za binadamu. Tulikuwa na mkufunzi mzuri wa haki za binadamu, Dkt. Isabela Warioba na chuo kikuu ndipo sehemu ambapo wakufunzi wetu waligundua kitu ndani yetu: “Kama mnaweza kuwa wanaharakati wazuri wa haki za binadamu mnaweza kuwa wanasheria wazuri wa haki za binadamu pia.” Naweza kusema ari yangu ya uanaharakati ilianzia siku hizo.
Mara ya mwisho tulizungumza mwaka 2021, miezi michache baada ya kuachiwa kutoka gerezani. Umekuwa ukifanya nini toka wakati huo?
Nimekuwa nikijaribu kurudi kwenye majukumu yangu. Nilichukua likizo na kurudi shule kujiendeleza na shahada ya uzamili, lakini niliendelea kufuatilia hali ya haki za binadamu nchini Tanzania. Mtazamo wangu umebadilika zaidi ukilinganisha na awali: Nimekuwa na mtazamo mpana zaidi kwa namna ninavyoitafsiri serikali, utawala na haki.
Nimesoma sheria na sasa naelewa namna inaweza kutumika na namna ilivyotumika vibaya dhidi yangu pindi nilipokamatwa. Sasa naweza kusimama na kusema, “Hiki kinapaswa kuwa hivi,” hususan katika eneo la haki za jinai na demokrasia. Ninajiamini kusema mambo kadhaa kutokana na uzoefu nilioupata gerezani, kama mshtakiwa mahakamani na kama wakili anaemuwakilisha mtu mahakamani.
Je, kuwekwa kwako kizuizini kumebadili vipi mtazamo wako wa uanaharakati na kazi za haki za binadamu nchini Tanzania?
Kabla ya kukamtwa kwangu sikuwa ni mtu wa kufikiria kutembelea magereza kwasababu sikuwa najua sana kuhusu yanayoendelea kule. Lakini nilichokipitia kimebadilisha hilo. Imenifundisha kiwango cha uhitaji wa msaada gerezani. Wakati mwingine naweza kuwa nafanya jambo fulani na fikra zangu zinaleta kumbukumbu na nasikia sauti za wafungwa, “Kaka, tunakuhitaji … kaka, tafadhali tutembelee.” Ninahisi wito wa mara kwa mara kuwatembelea, kuwashauri na kuwapa msaada wa kimaadili na wa mali. Nimejaribu kuwawakilisha mahakamani.
Nilipoachiliwa, nilimwandikia Rais Suluhu kuelezea kwa kina dosari zilizopo katika mfumo wetu wa kutoa haki. Nimekuwa nikishirikisha kile ambacho sasa nakijua kupitia mitandao ya kijamii. Najisikia kuwa ninao wajibu wa kuchangia kujenga nchi yetu.
Je, barua yako kwa Rais ilipata majibu gani?
Barua yenyewe ilizua gumzo nchini Tanzania. Kulikuwa na majadiliano katika vyombo vya habari, mitandao ya kijamii na katika taasisi za kufanya maamuzi ndani ya serikali. Sipendi kujichukulia sifa juu ya mambo kadhaa, lakini mwaka jana Rais alizindua kikosi kazi kilichoongozwa na Jaji Mkuu aliyepita, Mohamed Chande Othman kwa ajili ya kuangalia mfumo wetu wa kutoa haki jinai. Niliombwa ushauri na tume ilitumia barua yangu kama kielelezo. [Julai 15, 2023, tume ya Jaji Othman iliwasilisha ripoti yake kwa Rais Suluhu na kupendekeza mabadiliko kadhaa kwenye jeshi la polisi na huduma za magereza.
Ijapokuwa kumekuwa na kiu ya mabadiliko ndani ya nchi, hatujaweza kupiga hatua kubwa kutokana na kukosekana kwa utayari wa kisiasa kubadili sehemu kubwa ya mfumo wetu wa siasa – ambao ni katiba na sheria mbaya. Badala yake tumekuwa na ahadi za kisiasa kutoka kwa Rais na Mawaziri. Lakini kadri mambo yanavyobadilika ndivyo yanavyobaki vile vile. Tuna chai ile ile katika kikombe kipya.
Je unadhani "makosa yasiyokuwa na dhamana" bado yanatumika kama nyenzo ya ukandamizaji Tanzania?
Hatujawa na kesi nyingi kama ilivyokuwa kipindi cha Magufuli. Lakini hatutakiwi kufanya kazi kwa matakwa ya kila utawala. Kama Rais akiamua kufanya vibaya anao uwezo na zana za kumuwezesha katika hilo. Zaidi ya yote, Rais Suluhu ametumia sheria hizi – alimuweka jela [mwanasiasa wa upinzani] Freeman Mbowe. Anajaribu kufanya ionekane kama anaondoa maovu yaliyofanywa na Magufuli lakini bado kuna watu wako gerezani kwa kuikosoa serikali.
Ijapokuwa hatujashuhudia ukamataji mkubwa wa wakosoaji kama ilivyokuwa wakati wa Magufuli, tumeona serikali ikiwashughulikia wale wote waliokosoa mkataba wa bandari li. [Mwaka 2023, serikali ya Tanzania iliingia kwenye mkataba tata na kampuni kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu kwa ajili ya kusimamia bandari zake.] [ilikuwa] ikiwatuhumu na tuhumu kubwa zaidi nchini, uhaini [ambao hauna dhamana].
Siwezi kusema mambo yamebadilika sana. Labda tumenasa kati ya Rais Suluhu kusema anaamini katika demokrasia lakini akisuasua kujenga madaraja ya kisiasa na taasisi? Lakini unawezaje kuleta upatanishi ikiwa baadhi ya watu wetu wakike kwa wakiume wako gerezani?
Nafasi ya watetezi wa haki za binadamu na wanaharakati nchini Tanzania ilizorota sana wakati wa Rais Magufuli. Nini kifanyike kutengeneza nafasi kwa ajili ya watetezi wa haki za binadamu na wanaharakati nchini Tanzania kufanya kazi zao?
Kwa upande wa mfumo wa utoaji wa haki jinai, tunahitaji kufanya mabadiliko katika jeshi la polisi na vyombo vingine vya kusimamia sheria. Mabadiliko yanahitajika katika mafunzo, ajira na malipo.
Tunahitaji chombo cha kusimamia jeshi la polisi. Pale ambapo afisa wa polisi anakuwa ametenda uhalifu kama serikali haitamshitaki basi hakuna namna wananchi wanaweza kumshtaki. Ni pale tu ambapo serikali itataka kufanya hivyo, ndipo watakapo mshtaki. Chombo hiki cha usimamizi kitapokea malalamiko na kurejesha Imani katika mfumo wa utoaji haki.
Tunahitaji kuona mfumo wa mahakama ukiboreshwa. Serikali inapaswa kuajiri na kuwalipa maafisa wa mahakama zaidi. Tuna mrundikano wa kesi unaotokana na ufinyu wa bajeti. Hakuna bajeti ya kutosha inayotolewa kwa mahakama.
[Serikali nayo inatakiwa] kukuza zaidi uhuru wa mahakama. Kwa sasa Mkurugenzi wa Mashtka wa Umma (DPP) ndio anaendesha mashtaka nchini Tanzania – hivyo kama DPP anataka kesi iendelee, itaendelea. Kama hataki, DPP anaweza kuondoa kesi mahakamani bila ya sababu yoyote.
Utekelezaji wa mazungumzo ya rufaa [pale ambapo mtuhumiwa amekubali kosa kwa makubaliano ya kupata adhabu ndogo au kuondolewa kwa baadhi ya mashtaka] nchini Tanzania unaacha maswali mengi, hii ni kwa sababu hilo ndio chaguo pekee la kubaki huru kwa mtu aliyeshtakiwa kwa makosa yasiyokuwa na dhamana. Ni kweli kuwa ni njia mojawapo ya kupunguza mrundikano wa kesi mahakamani lakini washtakiwa wanaachwa bila ya machaguzi. Watu pia wananunua uhuru wao, ni njia mojawapo ambapo serikali inajipatia mapato [kwa maana ya malipo ya lazima yanayolipwa na mshtakiwa kabla ya kuachiliwa kutoka gerezani].
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa umepangwa kufanyika mwaka huu na uchaguzi mkuu utafanyika 2025. Kwa historia, uchaguzi nchini Tanzania umekuwa ukigubikwa na sintofahamu, hususan katika mtazamo wa haki za binadamu. Nini kifanyike kuhakikisha Watanzania wanashiriki uchaguzi ambao haujaathiriwa na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu?
Mimi sio muumini wa mabadiliko madogo. Mabadiliko ya Katiba ndio lengo kuu ili kujihakikishia uhuru wa taasisi. Kwa sasa nadhani tunaahirisha jambo hili kubwa kwa manufaa ya watawala. Hii ndio sababu Rais Suluhu anasema anataka kujikita zaidi kwenye haki za kijamii na kiuchumi. Kwangu mimi hili halina maana yoyote kama katiba itabaki kama ilivyo. [Muda mfupi baada ya kuingia madarakani mnamo 2021, Rais Suluhu alitangaza kwamba, kama ilivyokuwa kwa Magufuli atazingatia zaidi kuboresha uchumi wa nchi badala ya kuboresha katiba ya nchi].
Nina wasiwasi na mchakato wa uchaguzi unaokuja. Tume ya Uchaguzi inateuliwa na Rais. Kama hakuna kitakachobadilika, tutaona hali ile ile ya udanganyifu, utawala mbovu na ukatili. Watu wanahitaji kuona haki ikitendeka.
Ni mambo gani makubwa matatu ya haki za binadamu ambayo unaamini Rais Suluhu inabidi ayashughulikie mwaka ujao?
Uwajibikaji. Ubadhirifu wa rasilimali za umma haujapigiwa kelele sasa kama ilivyokuwa wakati wa Rais Magufuli. Lakini rushwa imeshamiri na hakuna uwajibikaji.
Utawala wa sheria. Hususan utawala wa sheria nzuri. Tunahitaji kuona dhamira ya Rais Suluhu kwa kuchukua hatua kwa vitendo kukuza uwajibikaji. Tunaona utekelezaji wa kuchagua kwa kujiamulia wa utawala wa sheria. Wanalenga wanasheria wa haki za binadamu, lakini wakati huo huo tuna kashfa kubwa zinazohusu rasilimali za umma, kama Sakata la bandari.
Suala la mwisho ni kufanya maboresho katika sheria na taasisi kama mahakama. Tunahitaji kujenga Imani kwa mahakama. Ndio njia pekee ya watu kueleza malalamiko yao. Kama watu hawatakuwa na Imani na taasisi zao, tutakuwa na taifa lenye wasiwasi na lisilozingatia sheria.
Je, kuna kitu kingine ungependa kutushirikisha?
Nalilia ulinzi wa Wamasai, kwa usalama wao na ushiriki wao katika kile kinachoendelea katika ardhi yao. Huwezi kuwahamisha watu kutoka katika ardhi ya babu zao kisha ukauza ardhi hiyo kwa wawekezaji kutoka nje ya nchi. Tunahitaji haki kwa Wamasai. [Tangu 2022, Mamlaka nchini Tanzania zimewaondoa kwa nguvu na kuwahamisha jamii za wafugaji Wamasai kutoka katika tarafa ya Loliondo na Hifadhi ya Ngorongoro iliyopo katika Wilaya ya Ngorongoro huku kukiwa na mashauriano hafifu au yasiwepo kabisa na jamii zinazoathirika.]
Hali hii inahusisha pia maeneo mengine ya nchi yenye rasilimali. Watu wamekuwa wakiuwawa na kuondolewa kwa nguvu katika ardhi zao. Kuna watu wamepotea. Wanahitaji haki.