Skip to main content

Upembe wa Afrika: Ukiukaji wachochea Unyanyasaji

Raia Wastahimili Mzigo wa Kutochukua Hatua Ulimwenguni kwenye Ukatili wa Wakati wa Vita, Migogoro ya Kibinadamu

Moshi wafuka kutoka kwenye ghala la kuhifadhi mbao katika mji mkuu wa Sudan Kartoum, wakati wa hali ya vita tarehe 7 Mwezi Juni Mwaka 2023. Vita hivyo ambavyo vilikuwa vimeingia juma la nane, vinawashirikisha Mkuu wa Jeshi la Sudan Abdel Fattah—Burhan na naibu wake awali Mohamed Hamdan Daglo ambaye anaongoza Jeshi la Rapid Support (RSF) @2023 Picha za AFP kupitia Getty Images © 2023 Picha za AFP kupitia Getty Images

(Nairobi) – Serikali za Upembe wa Afrika zilikabiliana na ukatili wa wakati wa vita na migogoro ya kibinadamu iliyokithiri mwaka wa 2023 huku jamii ya kimataifa ikitoa usaidizi mdogo, Shirika la Human Rights Watch limesema leo katika ripoti yake ya Dunia ya mwaka 2024.­­ Malalamiko kuhusu madhila ya miaka mingi ambayo hayajashughulikiwa na kutokuadhibiwa kwa uhalifu mkubwa kuliendelea kuchochea ukiukaji mkubwa kwa raia katika eneo hilo.

Migogoro ya Sudan na Ethiopia imekuwa na athari kubwa kwa raia. Imesababisha hasara kubwa ya maisha, uharibifu wa mali na watu wengi kuhama makazi yao. Badala ya migogoro hii kupewa kipa-umbele kwa ajili ya kusuluhishwa, serikali zenye ushawishi na Umoja wa Mataifa pamoja na mashirika ya kikanda mara kwa mara zimetafuta mafanikio ya muda mfupi na hivyo kutatiza kupatikana kwa suluhu zinazoendana na haki za binadamu.

"Sudan na Ethiopia zinatoa mifano ya kutisha ya vikosi vya serikali na makundi yenye silaha kwa kukiuka sheria za kimataifa huku adhabu ikiwa ndogo kwa matendo yao," alisema Mausi Segun, mkurugenzi wa Afrika Shirika la Human Rights Watch. "Hatua kubwa zaidi ya kimataifa na kikanda inahitajika kulinda raia na kumaliza marudio ya unyanyasaji na kutokujali sheria hali inayowaweka raia hatarini."

Kwenye ripoti hiyo yenye kurasa 740, toleo lake la 34, Shirika la Human Rights Watch lilitathmini na kukagua namna ambavyo masuala ya haki za binadamu yanaendeshwa katika nchi zaidi ya 100 duniani. Kwenye utangulizi wa ripoti hiyo Mkurugenzi Mkuu Tirana Hassan anasema kwamba mwaka 2023 ulikumbwa na masuala mengi si tu yanayohusu ukiukaji mwingi wa haki za binadamu na madhila ya vita lakini pia hapa na pale serikali mbali mbali zilihusika katika kuchukulia masuala kwa njia za kidiplomasia ambazo ziliwaathiri wengi waliokuwa wamedhulumiwa na hawakushirikishwa kwenye harakati hizo. Hata hivyo Hassan anasema kwamba kumekuwapo dalili za matumaini, zinazoonesha mwamko mpya, kwa hivyo ameziomba serikali kuendelea kutimiza majukumu yao kuhusiana na haki za binadamu.

Nchini Sudan, mzozo wa silaha kati ya Jeshi la Sudan na Jeshi la Rapid Support ambalo limekuwa jeshi huru tangu Aprili limekuwa na madhara mabaya kwa raia.

Pande zinazopigana mara kwa mara zimetumia silaha nzito katika maeneo yenye watu wengi na kuharibu miundombinu muhimu ikiwa ni pamoja na vituo vya matibabu. Maelfu ya raia wameuawa na kujeruhiwa, huku mamilioni wakikimbia makwao, hivyo kuzua mgogoro wa kibinadamu. Baadhi ya dhuluma mbaya zaidi zimefanyika Darfur Magharibi, ambapo Jeshi la Rapid Support na wanamgambo washirika wamelenga kwa makusudi raia wasio Waarabu, kushiriki katika mauaji ya halaiki, unyanyasaji wa kijinsia, na uteketezaji wa vitu katika miji.

Baada ya pande zinazohusika katika mzozo wa Kaskazini mwa Ethiopia kutia saini makubaliano ya kusitisha mapigano Novemba mwaka 2022, juhudi ndogo za kimataifa za kukuza umuhimu wa uwajibikaji na kukomesha unyanyasaji zilitoweka haraka.Washirika wa Ethiopia kama vile, Marekani na Umoja wa Ulaya na nchi wanachama wa umoja huo, walianza kurekebisha uhusiano na serikali ya Ethiopia licha ya uhalifu dhidi ya ubinadamu na unyanyasaji mwingine mkubwa, hasa katika maeneo ya Amhara, Tigray, na kwingine.

Migogoro na matukio yanayohusiana na hali ya hewa yamehamisha mamilioni ya watu katika eneo lote. Mzozo wa Sudan umewalazimu watu zaidi ya milioni 1.2  kukimbilia nchi jirani. Miongoni mwao walikuwamo wakimbizi wanaoishi nchini Sudan, ambayo tayari inawahifadhi zaidi ya wakimbizi zaidi ya milioni 2 wa Sudan Kusini, na mamia ya maelfu ya Waeritria, Waethiopia na wengineo. Licha ya mengi, maombi ya msaada katika eneo hilo yanasalia kuwa duni.


Katika eneo lote, hatua za makusudi za pande zinazopigana zimezidisha migogoro ya kibinadamu. Nchini Ethiopia, vikosi vya Eritrea vilizuia msaada wa kibinadamu kufikia jamii katika sehemu za Tigray chini ya udhibiti wao, wakati mapigano makali, usumbufu wa mara kwa mara wa mawasiliano ya simu, na mashambulizi dhidi ya wafanyakazi wa misaada  yalizuia oparesheni za misaada huko Amhara.

Nchini Sudan na Ethiopia, oparesheni za kibinadamu zimeathiriwa pakubwa na kushambuliwa kwa wafanyakazi wa misaada, uporaji mkubwa wa misaada, na mahitaji ya ukiritimba pingamizi ikiwa ni pamoja na kupiga marufuku usambazaji. Tangu Aprili, mamia ya maelfu ya watu wanaokimbia mgogoro wa Sudan wamewasili Sudan Kusini, wakiwamo waliorejea Sudan Kusini pamoja na wakimbizi. Hili limezidisha mzozo mkubwa wa kibinadamu ambao tayari umekithiri nchini humo, unaochochewa na migogoro, uhaba uliopo wa chakula na unaoendelea, na hali mbaya ya anga, pamoja na kupunguza ufadhili wa kibinadamu.

Mwitikio wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya kuwaharibia raia maisha na kuwafukuza makwao nchini Ethiopia na Sudan umekuwa mdogo. Wanachama wa Umoja huo watatu kutoka bara la Afrika hawakuendeleza mashauri thabiti na muhimu kuhusiana na kuwalinda raia katika nchi zote mbili.

Jambo zuri, Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa lilipiga kura ya kuanzisha tume huru ya kimataifa ya kutafuta ukweli ili kuchunguza ukiukaji wa haki nchini Sudan. Bado, Baraza la Usalama na serikali zinazohusika, pamoja na wahusika wa kikanda, hasa Umoja wa Afrika na chombo chake cha haki za binadamu, wanapaswa kutanguliza uwajibikaji katika utatuzi wowote wa kisiasa kwenye mgogoro huo.

Ni ajabu kwamba juhudi za kukuza uwajibikaji nchini Ethiopia zilipata pingamizi kubwa. Umoja wa Ulaya- EU, ambao ni kiungo muhimu kwenye maazimio ya awali ya Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa kuhusu Ethiopia , mwezi Septemba ilisitisha uchunguzi wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya haki za binadamu, licha ya ripoti muhimu ya Tume ya Kimataifa ya Wataalamu wa Haki za Kibinadamu iliyopewa mamlaka na Baraza la Haki za Kibinadamu nchini Ethiopia(ICHREE). Nchi wanachama zilishindwa kushinikiza kuanzishwa upya kwa tume hiyo, huku utaratibu wa haki za Umoja wa Afrika ukaacha uchunguzi wake huru kusitishwa wakati huo. Serikali zilikubali upinzani wa utawala wa Ethiopia kuendelea kuchunguzwa kimataifa ili kusaidia juhudi zake za kuanzisha mchakato wa haki wa mpito wa ndani. Waathiriwa wa unyanyasaji mwingi walionesha kutokuwa na imani kabisa  na taasisi za Ethiopia, ambazo zimeshindwa kutoa uwajibikaji  kwa unyanyasaji unaofanywa na Ethiopia na wengine, hasa vikosi vya Eritrea.


"Katika Upembe wa Afrika, waathiriwa wa unyanyasaji mwingi na familia zao pamoja na wanaharakati wamedai mara kwa mara kulindwa kwa raia, kukabiliwa kwa ukiukaji, na uwajibikaji kwa wale waliohusika, ikiwa ni pamoja na watu wenye mamlaka," Segun alisema. "Mashirika ya kimataifa na ya kikanda na serikali zenye nguvu zimekatisha tamaa sana kwa wahitaji kwa mtazamo wao mbaya wa haki za binadamu na migogoro ya kibinadamu inayoendelea.”

Your tax deductible gift can help stop human rights violations and save lives around the world.

Region / Country