Skip to main content

Tanzania: Uhuru hatarini kuelekea Uchaguzi

Mamlaka yavibana Vyama vya Upinzani, Vikundi vya Haki na Vyombo vya Habari

(Nairobi) – Mamlaka nchini Tanzania zimeongeza ukandamizaji dhidi ya vyama vya upinzani, taasisi zisizokuwa za kiserikali na vyombo vya habari kuelekea uchaguzi mkuu nchini humo unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28, 2020, wamesema Human Rights Watch leo.

Tangu katikati ya mwezi Juni, serikali imekamata takribani wanachama 17 wa vyama vya upinzani na wakosoaji wa serikali, kusimamisha kazi za kikundi cha watetezi wa haki za binadamu na kufuta leseni ya kikundi kingine na kuzuia vikundi vingine vikubwa vya utetezi wa haki za binadamu kuwa waangalizi katika uchanguzi ujao. Mamlaka pia zimeweka vikwazo vipya kwa vyombo vya habari, kufuta leseni ya gazeti lenye uhusiano na mwanachama wa upinzani na kuzuia vyombo vingine vya habari kutokana na kutoa taarifa juu ya Covid-19, ambayo Rais John Magufuli anasema haipo tena nchini.

 “Sio jambo la bahati mbaya kwamba serikali ya Tanzania imeongeza ukandamizaji kwa wapinzani, wanaharakati wa haki za binadamu na vyombo vya habari siku za karibu kabisa na uchaguzi mkuu,” anasema Oryem Nyeko, mtafiti wa Afrika anaefanya kazi na Human Rights Watch. “Badala ya kuzingatia haki ya kujieleza katika wakati huu muhimu, mamlaka zimeamua kuchukua hatua ambazo zinaleta mashaka juu ya uchaguzi kuwa wa huru na haki.”

Serikali imewakamata kiholela na kuwatia kizuizini kwa muda wanachama wa vyama vya siasa vya upinzani, hususan chama cha ACT-Wazalendo na Chadema ambacho ni chama kikuu cha upinzani kwa misingi kama vile “kuhatarisha amani” au mikusanyiko kinyume cha sheria. Mwezi Julai, polisi walimkamata na kumshikilia Sheikh Issa Ponda, kiongozi wa Kiislam, kwa siku tisa baada ya kufanya mkutano na waandishi wa habari kutaka uchaguzi huru na wa haki.

Serikali pia imeweka vizuizi vipya kwa vyombo vya habari na katika uhuru wa kujieleza mitandaoni. Imepitisha kanuni zinazopiga marufuku watangazaji wa Kitanzania kufanya kazi na watangazaji wa kigeni bila mtumishi kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania au wakala mwingine wa serikali kuwepo. Pia imepitisha kanuni zinazofanya kuwa ni kosa kuchapisha aina mbalimbali za machapisho mitandaoni ikiwa ni pamoja na yale yenye kuchochea kuandaa maandamano au “yanayohamasisha mapenzi ya jinsia moja.”

Mamlaka pia imetoza faini au kufungia vyombo vya habari kwa kuangazia mada nyeti za kisiasa, pamoja na virusi vya korona. Julai 6, Mamlaka ya Mawasiliano iliifungia Kwanza TV, kituo cha televisheni cha mtandaoni, kwa kipindi cha miezi 11 kutokana na chapisho lake Instagram lilitoa taarifa juu ya tahadhari ya afya juu ya Covid-19 kutoka Ubalozi wa Marekani Tanzania. Barua kutoka Mamlaka kwenda Kwanza TV ilituhumu kituo hicho kukosa “ uzalendo”.

Wahariri wawili wa magazeti yanayojitegemea na ambao hawakutaka majina yao kutumika walisema kwamba maafisa wamewajulisha isivyo rasmi kutochapisha maudhui ambayo hayataipendeza serikali. Mmoja wa wahariri alisema kwamba “wameonywa chinichini” kutokumpa muda wa hewani wa kutosha mwanachama wa upinzani Tundu Lissu na waziri wa zamani wa mambo ya nje Benard Membe ambaye amehama chama tawala, Chama cha Mapinduzi (CCM) siku za hivi karibuni.

Mamlaka pia zimechukua hatua dhidi ya mashirika makubwa yasiyokuwa ya kiserikali kupunguza uwezo wao wa kufuatilia uchaguzi. Mwezi Julai, Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilitoa orodha ya taasisi zilizoidhinishwa kuwa kama waangalizi wa uchaguzi na kutoa elimu ya mpiga kura, huku ikiacha mashirika makubwa ambayo kihistoria yamekuwa yakiratibu ufuatiliaji wa uchaguzi nchini.

Mamlaka pia zimeongeza vikwazo kwa mashirika yanayofanya kazi kutetea haki na afya za wanawake wanaovutiwa kimapenzi na wanawake, wanaume wanauvutiwa kimapenzi na wanaume, wenye kuvutiwa na jinsia zote mbili na waliobadili jinsia (LGBT) kuelekea uchaguzi mkuu. Human Rights Watch imeweka rekodi ya namna serikali inavyokandamiza watu wa LGBT na wanaharakati wao, ikiwa ni pamoja na kukamatwa kiholela na matumizi ya vipimo vya lazima vya njia ya haja kubwa, njia ambayo inapingwa ya kutafuta ushahidi wa mienendo ya mapenzi ya jinsia moja, njia ambayo ni ya kikatili na iliyokosa  utu na ambayo ni sawa na mateso, yote haya yanafanyika katika muktadha wa ukandamizaji wa kisiasa katika miaka mitano iliyopita.

Tangu Rais Magufuli aingie madarakani mwaka 2015, serikali imebana vyombo vya habari na uwanja wa raia kutoa maoni kwa kupitisha na kusimamia utekelezaji wa sheria kali na kutishia kufuta usajili wa mashirika yanayokosoa serikali. Serikali pia imeweka vikwazo kwa vyama vya upinzani na kumpa Msajili wa vyama vya upinzani mamlaka makubwa ikiwa ni pamoja na kufuta usajili wa vyama.

Mamlaka pia imeweka mipaka mipya kwa madai yenye maslahi ya umma, kitu ambacho kinaongeza wasiwasi juu ya haki ya kurekebisha ukiukwaji wa haki, wamesema Human Rights Watch. Mnamo Juni 10, bunge limepunguza uwezo wa vikundi kupinga kisheria sheria au sera ambayo inadaiwa kukiuka muswada wa haki za katiba. Hatua hii inaonyesha kuwa imelenga kuzuia vikundi kufungua kesi yenye maslahi ya umma kwa niaba ya wahanga wa dhuluma za serikali.

 “Vitendo vyote ambavyo vimefanywa na serikali katika wiki za hivi karibuni vinaathiri hali ya uwepo wa usawa katika uchaguzi,” anasema Nyeko. “Ili uchaguzi wa Tanzania uwe wa haki na usawa, serikali inapaswa kuruhusu vikundi vya watetezi wa haki za binadamu na vyombo vya habari kufanya kazi kwa uhuru na vyama vya upinzani na wakosoaji kutoa maoni yao kwa uhuru bila bughudha.”

Kwa maelezo zaidi ya vikwazo vilivyowekwa na serikali, tafadhali angalia hapa chini.

 

Vikwazo kwa Mashirika yasiyokuwa ya kiserikali; Uangalizi wa Uchaguzi; Elimu ya Mpiga kura

 

Mnamo Juni, Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilichapisha orodha ya mashirika 96 yaliyoidhinishwa kuwa waangalizi rasmi wa uchaguzi na 245 ya kutoa elimu ya mpiga kura au kuratibu mashirika yanayotoa elimu ya mpiga kura kwa uchaguzi ujao. Mashirika yalituma maombi kati ya Novemba 27, 2019 na Januari 30, 2020 kwa ajili ya kupewa kibali. 

Orodha hiyo iliyaacha mashirika makubwa ya haki za binadamu ambayo yalituma maombi, ikiwa ni pamoja na Muungano wa Watetezi wa haki za Binadamu Tanzania, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu na Jukwaa la Katiba Tanzania. Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinaratibu Muungano wa Asasi za Kiraia kwa Uangalizi wa Uchaguzi, muungano wa mashirika yasiyokuwa ya kiserikali ambayo hufuatilia uchaguzi nchini Tanzania.

Mashirika haya yanaamini kuwa yaliondolewa katika orodha kwa sababu ya uwezo wao mkubwa wa kufuatilia mchakato mzima wa uchaguzi bila upendeleo. Baada ya orodha kuchapishwa, mashirika haya yalikata rufaa kwa Tume ya Uchaguzi. Bado hawajapata majibu.

Kusimamisha/Kusitisha

Mamlaka imesimamisha mashirika kwa kudhaniwa kushiriki shughuli za kisiasa na kufanya kazi ya kulinda haki za watu wa LGBT.

Mnamo Mei 20, watu wawili waliojitambulisha kuwa maafisa kutoka msajili wa mashirika yasiyokuwa ya kiserikali walitembelea ofisi za Maendeleo Jumuishi ya Wananchi (Inclusive Development for Citizens) jijini Dar es Salaam, ambayo inahamasisha uhuru wa kujieleza na uwajibikaji wa serikali kupitia madai ya kimkakati ya haki za binadamu na uanaharakati mtandaoni. Walimhoji mfanyakazi juu ya barua isiyokuwa na jina kutoka shirika lisilokuwa la serikali inayohimiza Benki ya Dunia kuzuia mkopo kwa Tanzania kwa ajili ya programu ya elimu ya sekondari ambapo walisema utazidisha ubaguzi dhidi ya wasichana wajawazito shuleni.

Maafisa hao walimuuliza mfanyakazi kama shirika hilo limeshirikiana na mwanasiasa wa upinzani, Zitto Kabwe, ambaye ameandika barua tofauti kwenda Benki ya Dunia kupinga mkopo huo, na kuuliza kwanini shirika linafanya kazi na Maria Sarungi-Tsehai, mkurugenzi wa shirika hilo ambaye anajulikana kwa uanaharakati wake mtandaoni na ukosoaji wa wazi wa serikali na kuhusu Fatma Karume, mwanasheria na mkosoaji wa serikali.

Mnamo Mei 21, ofisi ya Msajili ilituma barua kwa Maendeleo Jumuishi ya Wananchi ikiwatuhumu kushiriki au kujihusisha na “vitendo vya siasa” kinyume na kifungu cha 29 cha marekebisho ya sheria ya Mashirika Yasiyokuwa ya Serikali ya 2019. Barua ambayo Human Rights Watch waliiona iliwapa shirika siku 30 kueleza kwanini hatua za kisheria zisichukuliwe dhidi yao. Mnamo Juni 24, msajili alisimamisha usajili wa shirika kwa kipindi kisichojulikana.

Msajili pia aliwaandikia mashirika kadhaa ya Tanzania Bara mnamo Juni 24 kuwaomba nyaraka za vyanzo vyao vya fedha, matumizi na shughuli zao au wawe hatarini kupoteza usajili wao.

Katika siku hiyo hiyo, msajili aliwaagiza muungano wa mashirika ya haki za binadamu kuwasilisha mikataba yao na wafadhali na vyeti vya usajili. Polisi pia walivamia mafunzo yaliyokuwa yakifanywa na muungano wa watetezi wa haki za binadamu jijini Dar es Salaam siku hiyo na kuwakamata wafanyakazi wawili na baadae kuwaachia baada ya masaa mawili. Polisi walisema shirika hilo halikuwa na kibali cha kufanya mafunzo na kamanda wa polisi mkoa, Mussa Taibu aliviambia vyombo vya habari kwamba polisi wanawashikilia wafanyakazi kwa sababu “walitaka kujua mada kuu za kikao hicho.”

Mnamo Agosti 17, polisi walimuita Onesmo Olengurumwa, mkuu wa muungano huo, na kumhoji juu ya kushindwa kuwasilisha mkataba wao na wafadhili kama kanuni zinavyoelekeza. Muungano huo ulisema kuwa waliwasilisha mikataba hiyo. Olengurumwa aliachiliwa siku hiyo hiyo baadae kwa dhamana ya polisi ya Shilingi za Kitanzania Milioni 200 (US$ 86,000). Siku inayofuata, shirika hilo lilisimamisha shughuli zake baada ya mamlaka kufungia akaunti zake za benki, mpaka hapo uchunguzi utakapokamilika.

Tofauti na hiyo, mamlaka pia zimeongeza ukandamizaji wa vikundi vinavyotetea haki na afya ya watu wa LGBT. Mnamo Juni16, huko Zanzibar, msajili alimuita Hamid Muhammad Ali, mkurugenzi wa Mpango wa UKIMWI Uwezeshaji Vijana na Maendeleo, kikundi cha haki za LGBT, katika kikao ambacho maafisa walimhoji na kumjulisha kuwa usajili wa shirika lake unasimamishwa kwa “kuhamasisha mapenzi ya jinsia moja”. Kikao hicho baadae kilirushwa katika runinga.

Ali aliwaambia Human Rights Watch kuwa siku nne baadae, polisi walikwenda nyumbani kwake na kupekua na kumuagiza kufanya uchunguzi wa njia ya haja kubwa katika hospitali ya Mnazi Mmoja siku inayofuata. Alisema alienda hospitali na kutakiwa kutoa alama za vidole na nakala ya kitambulisho cha taifa, lakini hakulazimishwa kufanya uchunguzi. Mnamo Agosti 10, waziri wa tawala za mikoa na serikali za mitaa na idara maalumu alifuta leseni ya kikundi hicho ya mashirika yasiyokuwa ya kiserikali kwa kwenda kinyume cha “maadili ya kidini na kijamii” ya Zanzibar

Ali na wanaharakati wengine wa haki za LGBT Zanzibar walisema wanaamini kuwa maafisa walifanya vitendo hivyo ili kupata upendeleo wa kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu.

Kukamatwa, Kuweka Kizuizini kwa Wakosoaji wa Serikali

Mamlaka zimewakamata kiholela wakosoaji wa serikali na wa mchakato wa uchaguzi. Mnamo Juni 23, polisi walimkamata Kabwe na wanachama wengine saba wa upinzani wakati wa kikao chao cha ndani cha chama cha upinzani, ACT Wazalendo huko Kilwa, mkoa wa kusini wa Lindi. Siku inayofuata polisi waliwaachia. Chama kilisema kwamba Kabwe na wenzie walituhumiwa kwa “kuhatarisha amani,” lakini hakuna taarifa zaidi juu ya kosa hilo zilizotolewa. Kabwe na wengine wametakiwa kuripoti kituo cha polisi kila baada ya majuma matatu.

Kabwe huko nyuma alikuwa amekamatwa mara kadhaa kwa kukosoa serikali, ikiwa ni pamoja na mwaka 2017, kwa kupingana na takwimu za serikali na mwaka 2018 kwa kudai kuwa watu kadhaa waliuwa wakati wa mapambano kati ya wafugaji na polisi. Mnamo Mei 26, Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Kisutu ilimpata Kabwe na makosa ya uchochezi kwa maneno yake ya mwaka 2018 na kumtaka kutokuandika au kusema chochote ambacho ni uchochezi

Mnamo Julai 11, polisi walimkamata Sheikh Issa Ponda, katibu wa Baraza la Maimamu nchini Tanzania katika ofisi zake Bungoni, Dar es Salaam. Vyombo vya habari viliripoti kuwa sababu ilitokana na “kudaiwa kusambaza nyaraka zenye viashiria vya uchochezi na kuvunja amani kuelekea uchaguzi mkuu 2020.” Baraza la Maimamu mnamo Julai 9 lilitoa nyaraka, ambayo Human Rights Watch waliiona, na kuitaka serikali kuhakikisha uchaguzi huru na wa haki, marekebisho ya sharia na usawa kwa Waislamu. Polisi walimshikilia Ponda kwa siku tisa na baadae kumtoa kwa dhamana.

Polisi waliwakamata wanachama nane wa Chadema, chama kikuu cha upinzani Tanzania, ikiwa ni pamoja na mwenyekiti wao wa baraza la vijana, Nusrat Hanje, mkoani Singida, magharibi mwa Dodoma mnamo Julai 6. Polisi waliwatuhumu kwa kuikashifu bendera ya taifa kwa kuimba wimbo wa taifa la Tanzania wakati wamepeperusha bendera ya Chadema wakati wa kikao cha chama mnamo Julai 4. Mwendesha mashtaka pia aliwatuhumu kwa kukusanyika kinyume cha sheria na “kujaribu kusambaza taarifa za siri.” Watu hao bado wako rumande huko Dodoma toka mahakama iwanyime dhamana. Mnamo Agosti 26, Mahakama Kuu iliamuru dhamana yao ishughulikiwe lakini bado wako rumande. 

Vyombo vya habari viliripoti kuwa usiku wa Juni 8, watu wasiojulikana walimvamia na kumpiga Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema, alipokuwa anarudi mji mkuu, Dodoma, na kumvunja mguu. Mbowe ambaye ni mkosoaji mkubwa wa serikali amekamtwa mara kadhaa. Mwezi Machi, mahakama ilimhukumu Mbowe na viongozi wengine nane wa chama kwa kutoa matamko ya kichochezi wakati wa mkutano wa hadhara Februari 2018 na kupewa faini ya hadi shilingi za Kitanzania milioni 350 (US$ 151,000).

Kufungiwa kwa Vyombo vya Habari na Vikwazo

Mamlaka zimesitisha leseni za vyombo vya habari na kuwaita wataalamu wa habari juu ya kuripoti vitu ambavyo vinachukuliwa vya kutatanisha, ikiwa ni pamoja na kuripoti kuhusu Covid-19.

Mnamo Julai 20, Rais Magufuli alisema hakuna virusi vya corona Tanzania. Serikali haijatoa takwimu mpya juu ya maambukizi ya Covid-19 nchini tangu Aprili na haijaweka vikwazo vya kusafiri, amri ya kutotoka nje au hatua nyingine kupambana na kusambaa kwa maambukizi ya ugonjwa huo.

Mnamo Julai 23, mkurugenzi wa Idara ya Habari kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Patrick Kipangula, alifuta leseni ya gazeti la Tanzania Daima juu ya “kukithiri na kujirudia rudia kukiuka sheria na miiko ya uandishi wa habari.”

Wafanyakazi wa gazeti hilo waliwaambia Human Rights Watch kuwa walihisi kuwa serikali iliamua kwa makusudi kuchukua hatua hiyo kuelekea uchaguzi mkuu kwa sababu gazeti hilo mara kwa mara huandika shughuli zinazofanywa na vyama vya upinzani na kwa sababu mmiliki wake ameolewa na Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema.

Mnamo Aprili 20, mamlaka za Zanzibar zilisimamisha leseni ya Talib Ussi Hamad, mwandishi wa habari anaefanya kazi na Tanzania Daima, kwa sababu ya chapisho lake katika ukurasa wake wa Facebook ambao alisema mwandishi mwingine ana virusi vya corona.

Mnamo Aprili 2, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania iliwapiga faini Star Media Tanzania Limited, Multichoice Tanzania Limited na Azam Digital Broadcast Limited ya shilingi milioni 5 za Kitanzania (US$ 2,155) kila mmoja kwa kusambaza “habari za uongo na za kupotosha kuhusu msimamo wa Tanzania juu ya Covid-19,” baada ya vituo vya televisheni wanavyomiliki kurusha habari kuhusu Covid-19.

Mnamo Aprili 16, Mamlaka ya Mawasiliano ilisitisha leseni ya toleo la mtandaoni la gazeti la lugha ya Kiswahili la Mwananchi kwa miezi sita baada ya kuweka video ya Rais Magufuli akinunua samaki sokoni, ambapo hakuheshimu maelekezo ya kuepuka misongamano na vizuizi vya Covid-19. Mamlaka hiyo ilituhumu Mwananchi kwa kuchapisha “habari za uongo,” kinyume na kanuni cha Maudhui ya Mtandaoni. Mwananchi baadae iliomba radhi kwa kuweka video ile, na kusema ilikuwa ni video ya zamani.

Mnamo Juni, serikali ilifanya marekebisho ya kanuni za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (Redio na Televisheni), kuzuia watangazaji wa redio na televisheni za Kitanzania kufanya kazi na watangazaji wa kigeni bila mamlaka ya mawasiliano au mtumishi yeyote wa serikali kuwepo, na kupendekeza kwamba watangazaji wa kigeni hawatoweza kuripoti matukio nchini Tanzania bila ya kibali cha serikali.

Kanuni za Maudhui ya Mtandaoni

Tangu Julai, serikali imepitisha vikwazo vipya juu ya mawasiliano ya mtandaoni, moja kwa moja kuzuia maudhui yanayokosoa serikali.

Mnamo Julai, serikali ilipitisha marekebisho ya Kanuni za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (Maudhui ya Mtandaoni) ambayo yanatoa adhabu za jinai kwa kuchapisha mtandaoni “maudhui kinyume na utaratibu wa Serikali na jamii,” au kuitisha maandamano, au ambayo “yanachochea au kupendelea kile ambacho kinaweza kuleta uchochezi, uhasama au ubaguzi wa rangi.”

Kanuni pia zinakataza kuhamasisha mapenzi ya jinsia moja, ambayo inaweza kutumika kushtaki watu kwa kufanya shughuli za utetezi wa haki za LGBT au kwa kuchapisha “taarifa juu ya kuwepo kwa mlipuko wa ugonjwa unaoua au kuambukiza” bila kuwa na idhini ya serikali. Wanaokiuka wanaweza kupigwa faini au kuhukumiwa kifungo kisichopungua mwaka mmoja gerezani.

Mawasiliano ya mtandaoni nchini Tanzani tayari yamebanwa vilivyo na Sheria ya Makosa ya Mtandaoni ya 2015. Serikali imetumia sheria hii kuwashtaki watu kwa kuchapisha maudhui mtandaoni au machapisho ya mtandaoni. Mwezi Machi 2018, serikali ilipitisha kanuni za Maudhui ya Mtandaoni, ambazo zimeipa Mamlaka ya Mawasiliano nguvu kubwa ya kutoa leseni kwa maudhui ya mtandaoni, ikiwa ni pamoja na blogu, na kuwataka kulipa ada ya hadi kufikia US$900, ambayo imezuia wengi kupata leseni. Kutokutii sheria ni kosa la jinai.

 

Your tax deductible gift can help stop human rights violations and save lives around the world.

Region / Country