(Nairobi) – Mwenendo wa polisi kutumia nguvu kupita kiasi na kuharibu mali kwenye oparesheni ya kuwaondoa wakazi katika msitu wa Mau, eneo la Rift Valley, na ukosefu wa msaada kwa waliofurushwa vimesababisha vifo na hangaiko kwa wakazi wengi waliondolewa, Shirika la Human Rights Watch (HRW) limesema leo.
Tangu mwaka 2018 serikali ya Kenya imewaondoa kwa lazima watu wapatao elfu hamsini katika maeneo yaliyoko msitu wa Mau. Kati ya watu hao, elfu arobaini wamefurushwa mnamo mwezi Julai Mwaka 2018. Wengine waliondolewa kati ya mwezi Agosti na Novemba mwaka jana (2019). Kati ya idadi hiyo watu elfu sita ambao waliondolewa hivi karibuni wanaishi katika mazingira magumu, kwenye makazi ya muda yaliyo katika kaunti ya Narok. Watu hao hawajapewa ardhi wala kufidiwa sawa na inavyotakiwa chini ya Sheria za Kenya.
“Utumiaji wa nguvu kuwaondoa wakazi katika maeneo ya misitu ni jambo lisilokubalika, na, kusikitisha zaidi ni kwamba watu hao hawakupata msaada wowote iwe makao mapya au usaidizi mwingine wakati huu wa janga la virusi vya Corona (COVID-19), amesema Otsieno Namwaya, mtafiti mkuu wa kanda ya Afrika, Shirika la Human Rights Watch. “Serikali inapaswa kuchukua hatua za haraka kutatua mgogoro huu, kwa kufanya uchunguzi wa madai kwamba polisi wametumia nguvu za kupita kiasi na kuwadhulumu wakazi hao wakati wa kuwaondoa. Serikali inapaswa kufahamu kwamba shughuli zote za kuhamishwa kwa lazima zinafuata taratibu na sheria za nchi.”
Shirika la Human Rights Watch lilizuru kambi mbili za watu waliofurushwa makwao. Shirika vilevile lilifika katika mji wa Narok mnamo mwezi Machi 2020. Liliwahoji watu 37, wakiwemo wakazi waliofurushwa na maafisa wa serikali ya kaunti hiyo. Baada ya kutangazwa kutokea kwa ugonjwa wa Virusi vya Corona (COVID-19) nchini, watu wengine 7 walihojiwa katika kambi ya Sagamian, wawili kati yao wakiwa wawakilishi wa kundi hilo. Mahojiano yalikuwa kwa njia ya simu.
Katika mahojiano hayo ilibainika kuwa kati ya mwezi Agosti na mwezi Novemba mwaka 2019, maafisa wapatao 150 kutoka vikosi vya askari wa kulinda mbuga (KWS), askari wa kulinda misitu (Kenya Forest Service) polisi wa utawala (Administration Police), polisi wa kawaida, na walinda mbuga wa kaunti ya Narok walitumia nguvu kuwahamisha wakazi hao kutoka vijiji kumi katika eneo la kaskazini mwa msitu wa Mau, yakiwemo maeneo ya Kitoben, Olaba, Kapkoros na Kirobon. Walioshuhudia pamoja na familia za waathiriwa waliripoti kwamba yamkini watu 7 waliuawa katika operesheni hiyo hiyo. Serikali ya Kenya bado haijafanya uchunguzi wowote kufuatia vifo hivyo. Vilevile haijachunguza vitendo vingine vya dhuluma na badala yake imeendelea kutoa vitisho vya kufungwa kwa lazima kwa kambi za waliofurushwa.
Vikosi hivyo pia viliharibu maghala ya kuhifadhi chakula, vilipora chakula, vikawapiga watu kwa kutumia mitutu ya bunduki na magogo. Wakazi wengi waliopigwa waliachwa na majeraha mabaya. Maafisa hao waliteketeza baadhi ya nyumba, na hapa na pale waliwalazimu wakazi kuteketeza nyumba zao wenyewe huku wakiwa wametisha kuwafyatulia risasi.
Katika uchunguzi wa awali uliofanywa na Shirika la Human Rights Watch kufuatia kuondolewa kwa wakazi mnamo mwaka 2018, Shirika hili liligundua kwamba dhuluma sawa na hizi zilitendwa, na kusababisha vifo vya watu 9 huku wengine wengi wakijeruhiwa.
Maafisa wa serikali walilielezea Shirika la Human Rights Watch kwamba waliwafurusha wakazi katika awamu mbili chini ya mpango wa kuhifadhi mazingira katika msitu huo. Msitu huo ni chemchemi ya maji ya mito 12 ambayo ni vyanzo vya maji ya maziwa matatu katika ukanda wa Afrika Mashariki. Msitu huo unasemekana kuwa katika hatari ya kuangamia kutokana na ujenzi wa makazi yasiyo halali, kukatwa kwa miti kiholela, miongoni mwa sababu nyingine. Shughuli ya kuondolewa kwa wakazi ya Mwaka 2018 na 2019 iliwalenga watu ambao walikuwa wamejenga makazi katika msitu wa Maasai Mau, ambao ni sehemu ya msitu wa Mau unaosimamiwa na serikali ya kaunti ya Narok kwa niaba ya Wakfu wa Mau. Maeneo mengine 21 yako chini ya usimamizi wa Shirika la kulinda Misitu la Kenya (Kenya Forest Services).
Serikali ilisema familia zilizoondolewa zilikuwa zimejenga makao haramu katika msitu huo kwa zaidi ya miaka thelathini na kuchangia katika uharibifu wa msitu. Licha ya kuwa baadhi yao walikuwa na hati za kumiliki ardhi, serikali ilidai kutozitambua. Serikali ilikiuka sheria za nchi na mikataba ya kimataifa kwa kusisitiza kwamba, haitawafidia au kuwapa makao mapya, wale waliofurushwa, kwa kuwa walijenga katika ardhi hiyo au kumiliki ardhi kwa njia zisizo halali.
Licha ya kuibuka kwa taarifa kwamba polisi waliwadhalalisha na kuwatesa wakazi katika awamu ya kwanza ya kuwafurusha, na wito kwamba shughuli hiyo isimamishwe, huku kukiwa na kesi inayoendelea mahakamani mjini Nakuru, serikali iliendelea kuwaondoa watu katika awamu ya pili ya shughuli hiyo mwaka 2019. Haya yalifanyika bila kuzingatia Mwongozo wa Kuwafurusha Watu wa 2010, unaoitaka serikali kuwapa waathiriwa notisi ya muda wa siku 90, pamoja na kuitaka ichapishe katika Gazetti rasmi la serikali notisi hiyo, na kuweka matangazo katika sehemu za umma kuwalenga waathiriwa. Mwishoni mwa mwezi Agosti, aliyekuwa kamishna wa kaunti ya Narok, George Natembeya, alitoa ilani ya siku 60, na kisha kuruhusu wakazi hao kuondolewa makwao siku moja baada ya kuchapisha notisi hiyo.
Shirika la Human Rights watch lilibaini kwamba maafisa wa vikosi mbali mbali vilivyopelekwa kutekeleza shughuli hiyo walitumia vurugu na nguvu ya kupita kiasi. Watu wawili waliuawa katika vurugu hizo, wakati wa kuondolewa au punde tu baada ya shughuli kukamilika, wengine walipata majeraha mabaya. Takriban watu wengine 5 walifariki miezi kadhaa baadaye kutokana na mazingira magumu kama vile ukosefu wa chakula na baridi kali. Hata hivyo serikali ya Kenya inakanusha habari za kufariki mtu yeyote.
Sally Kipchirchir Langat, mwenye umri wa miaka 33, alielezea kwamba alipoteza mimba mnamo Agosti 25, baada ya maafisa kumi wa polisi kuingia kwa lazima nyumbani mwake akiwa mja mzito wa miezi saba. Walivunja mlango wa nyumba yake, na kumlazimisha alale kwenye sakafu. Alisema:
“Nilianza kuhisi maumivu tumboni, baada ya kuanguka kwenye sakafu. Nilipoenda hospitalini siku iliyofuata daktari aliniambia mwanangu alikuwa amefariki tumboni, na nilitakikana kupasuliwa haraka ili kuyaokoa maisha yangu. Nilimpoteza mwanangu.”
Mwanamke mwenye umri wa miaka 35 alikariri jinsi akiwa na babake mzazi mwenye umri wa miaka 65, Joseph Ruto, walishinda bila kula kwa siku kadhaa baada ya maafisa wa polisi kuteketeza ghala lao la chakula na kuharibu mimea yao shambani katika kijiji cha Loliondo kwenye msitu huo mwezi Septemba. Ruto alifariki siku tano baada ya tukio hilo.
Chini ya Sheria za kimataifa, kuondolewa kwa nguvu kwa wakazi ni ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu. Mataifa yote yanatakiwa kuchukua hatua za kuzuia kufurushwa kwa wakazi. Serikali pia zina wajibu wa kuwafidia waliohamishwa kutoka makao yao, iwe wana hati za kumiliki ardhi au hawana. Serikali inapaswa kutambua haki za raia mhusika kumiliki mali, familia au jamii, ikiwemo wale wanaomiliki ardhi kupitia sheria zinazotokana na desturi na tamaduni.
Pale ambapo kuondolewa kwa watu lazima kutendeke, kutokana na sababu za kipekee, kama vile kwa maslahi ya umma, huku kuondolewa kukiwa ndio njia ya pekee inayofaa basi kutekelezwe kuambatana na viwango vya kimataifa. Hatua ya kuwaondoa itekelezwe kwa kufuata sheria, kuwapa waathiriwa fursa ya kupinga mpango wa kuwaondoa makwao, mpango utekelezwa kwa njia ya uwazi, bila mapendeleo, na kwa kujali maslahi ya wanyonge na wale wanaotoka katika jamii zilizotengwa.
Serikali ya Kenya inajukumiwa chini ya mikataba ya kimataifa ya haki za binadamu kuhakikisha kwamba kila mkenya ana kiwango cha wastani cha maisha anayofaa kuishi ikiwemo kumudu chakula cha kutosha na makao.
Mnamo mwezi Aprili, ikiwa mojawepo ya mbinu za kukabiliana na janga la virusi vya Corona, Rais Uhuru Kenyatta alitangaza mpango wa kuwapa fedha za msaada baadhi ya wakongwe na makundi yaliyokuwa hatarini ili kuwawezesha kupata chakula. Lakini shirika la Human Rights Watch liligundua kwamba mpango huo haujawafaidi wakongwe na wengine walio katika hatari kwenye makundi ya watu waliofurushwa kutoka msitu wa Mau.
Serikali ya Kenya inatakiwa kuwapa maelfu ya watu hawa msaada wa haraka wa chakula, na usadizi mwingine kama vile wa fedha. Serikali inatakiwa kuhakikisha kwamba kila aliyefurushwa kutoka msitu wa Mau amelipwa pesa za fidia, hasa ikizingatiwa kwamba watu hao wana hati za kuthibitisha kwamba walinunua na kulipia ardhi hizo yapata miaka thelathini iliyopita. Serikali pia inafaa kuchunguza dhuluma na mateso waliotendewa wakazi wa eneo hilo wakati wakifurushwa kutoka msitu huo. Wale wote waliohusika na visa hivi wawajibishwe kwa kushtakiwa na kuhukumiwa.
“Serikali ya Kenya inapaswa kuchukua hatua za haraka kuwaepushia mauti yanayotokana na ukosefu wa chakula miongoni mwa wakazi wa kambi za waliofurushwa huko Mau,” Namwaya alisema. “Viongozi wasipuuze shida zinazowakumba watu hao, hasa wakati huu ambapo tunapaswa kuwasaidia wale walio katika hatari ya kuathirika kwa makali ya ugonjwa wa virusi vya Corona vinavyoenea.”
Kwa maelezo zaidi, tafadhali tizama.
Kuondolewa kwa makazi katika msitu wa Mau
Msitu wa Mau ndio chemchemi kubwa ya maji nchini Kenya. Unajumuisha maeneo 22 yenye ukubwa wa hekari 400,000 zilizosambaa katika kaunti saba nchini, ikiwemo kaunti ya Narok.
Msitu huo una vyaanzo vya angalau mito 12 inayomwaga maji yake katika maziwa matatu ya ukanda wa Afrika Mashariki. Mojawepo wa maziwa hayo ni ziwa Victoria, ambalo linatambulikana kuwa ziwa la pili kwa ukubwa ulimwenguni lililo na maji yasiyo ya Chumvi.
Serikali ya Kenya inadai kwamba imewaondoa wale wote waliokuwa wamenyakua ardhi ya msitu huo katika kaunti ya Narok. Shughuli ya kuwafurusha watu hao ilianza mwaka 2004 na kukamilika mwaka jana (2019). Maafisa wa serikali wanasema wameokoa na kuhifadhi hekari 40,000 ambazo tangu mwaka 1974 zilikuwa zimemilikiwa kwa haramu na zaidi ya watu 150,000.
Katikati mwa mwaka 2019, maafisa wa serikali katika kaunti ya Narok waliliambia Shirika la Human Rights Watch kwamba ujenzi wa makazi yasiyo halali na ukataji kiholela wa miti katika msitu wa Mau ulikuwa umeathiri vibaya mazingira ya eneo hilo. Uharibifu huo ulikuwa umesababisha ukame, kukauka kwa mito, na vifo vya wanyama pori katika mbuga ya Maasai Mara. Serikali ilijaribu kwa mara ya kwanza kuwaondoa wakazi wapatao 100,000 mnamo mwaka 2004, lakini ikalazimika kusimamisha shughuli hiyo baada ya amri ya Mahakama. Mnamo mwaka 2018, serikali ilipata idhini ya Mahakama kuendelea na shughuli hiyo na katika hatua hiyo ikawaondoa watu wapatao 50,000 ambao walikuwa wamesalia katika ardhi hiyo. Watu 40,000 waliondolewa mwaka 2018 na wengine 10,000 kufurushwa mwishoni mwa mwaka 2019.
Tangu Mwaka 2019, wakazi wengi waliofurushwa wamekuwa wakiishi katika kambi mbili zilizoko katika kijiji cha Ol Megenyu na kijiji cha Sagamian. Serikali imekataa kusajili au kutambua maeneo hayo kama hifadhi. Hali hiyo imekuwa changamoto kwa mashirika ya misaada hasa katika kuwapa misaada waathiriwa hao. Serikali ilitangaza kwamba kambi hizo sio halali huku ikiwataka wakazi waondoke mara moja. Serikali haijawapa msaada wowote na iliwaambia watafiti wa Human Rights Watch kwamba mashirika yoyote yanayokusudia kuwasaidia watu hao yatahitaji kuomba ruhusa ili kupewa vibali maalum.
Wakazi wa kambi hizo sasa wanajikimu kwa kutafuta kazi za vibarua au kutegemea msaada kutoka kwa watu binafsi ama wanasiasa. Tangu mwezi Machi wakati Kenya ilipotangaza taratibu za kuzuia kuenea kwa ugonjwa wa Virusi vya Corona, watu hao waliofurushwa, waliliambia Shirika la Human Rights Watch kwamba, wamekabiliwa na wakati mgumu wanapotafuta kazi au msaada. Familia nyingi zimewapoteza jamaa zao wa karibu au zimekabiliwa na magonjwa yanayotokana na ukosefu wa chakula au utapia mlo.
Utumiaji nguvu kupita kiasi katika oparesheni ya kuwaondoa wakazi wa Mau 2019
Shirika la Human Rights Watch limerekodi angalau vifo vya watu saba. Haya ni kwa mujibu wa mahojiano na wanafamilia, mashahidi, rekodi za matibabu. Vifo viwili vilisababishwa na oparesheni za polisi, ilhali vifo vilivyosalia vitano viliambatanishwa na kufurushwa kwa wakazi hao au mazingira magumu ya kuishi katika kambi za wakimbizi. Aidha ilisemekana kwamba wakazi wengi walipata majereha wakati wa kuhamishwa kwa mabavu. Maafisa wa serikali walikanusha madai kwamba vifo hivyo vilitokea wakati wa kuondolewa kwa watu hao kutoka msitu huo.
Mwanamme mwenye umri wa miaka 53 alisema kwamba kundi la maafisa wa polisi waliokuwa wakiwaondoa waliingia kwa lazima katika nyumba yake katika eneo la Sierra Leone katika msitu huo mwezi Novemba. Walitisha kuwapiga risasi, wakatisha kuwapiga na kuteketeza makazi yao. Mwanamume huyo alielezea kwamba polisi waliwaamuru kwa kusema, “teketeza nyumba yako la sivyo tutakufyatulia risasi.” Aliongezea kwamba, Mamake mwenye umri wa miaka 73 alishtuka aliposhuhudia vitendo hivyo, akapatwa na msongo wa mawazo. Alifariki siku chache baada ya kisa hicho.
Mwanamume mwingine mwenye umri wa miaka 42 anayeishi katika kambi ya Sagamian alielezea kwamba polisi waliwaandama akiwa na familia yake kwa siku kadhaa. Hatimaye waliwafurusha kutoka nyumbani kwao, wakateketeza nyumba yao, na baadaye kuteketeza maduka yao katika kituo cha kibiashara cha Sierra Leone. Hatua hii iliwaondolea uwezo wao wa kujitafutia riziki. Alikariri: “Afya ya mke wangu mwenye uja mzito iliathirika sana. Tulilazimika kulala nje kwenye baridi, na mara nyingi hatukupata chakula.” Mke wake hakula chochote kwa siku kadhaa."
Jamaa huyo alielezea kumpoteza mwanawe mchanga alipokuwa akizaliwa. Madaktari walimwambia yeye na mkewe kwamba kifo cha mtoto kilisababishwa na mama kuathirika sana na utapia mlo, hakuwa na nguvu za kujifungua.
Familia nyingine katika kambi hiyo ilizungumzia vifo vya takriban wenzao watatu waliokufa walipojaribu kukimbia na kujificha msituni walipofumaniwa na polisi waliokuwa wakiwafurusha.
Mnamo mwezi Septemba katika kisa kimoja kwenye kijiji cha Kapkoros, mwanamume mwenye umri wa miaka 39 alilazimika kwenda mafichoni msitumi, akiwa na mkewe na wanawe, baada ya polisi waliokuwa wamejihami kwa bunduki kuvamia nyumba yao. Alisema kwamba yeye na familia yake waliishi katika mazingira magumu yaliyosababisha mwanawe wa mwaka mmoja kufariki kutokana na maradhi ya homa ya mapafu. Alielezea: “Tuliishi msituni kwa mwezi mzima, tukilala kwenye mapango au nje kwenye nyasi. Tulikuwa na hofu sana kutoka nje kwa kuwa polisi walikuwa kila mahali, na walikuwa wakatili sana.”
Mnamo mwezi Agosti katika kisa kingine kwenye kijiji cha Olaba, bibi kikongwe alielezea kukimbilia msituni akiwa na mwanaye wa kike na wajukuu wake watatu, wajukuu wawili waliathirika na maradhi ya homa ya mapafu, na wakafariki. “Tulilala nje kwenye baridi,” alisema.
Mmoja wa waliofurushwa mwenye umri wa miaka 42, na ambaye ni mojawepo ya maafisa wa kundi la waliofurushwa kutoka msitu wa Mau wanaoishi katika kambi ya Sagamian aliarifu kwamba mnamo Juni 16, mwaka huu (2020), mwenzake mwenye umri wa miaka 60, Joseph Kilel, alizirai baada ya kukosa chakula kwa wiki nzima. Alikimbizwa hospitalini kwa matibabu. Madaktari waliwaambia kwamba utumbo wake ulikuwa umejikunyata na kushikana kwa kukosa lishe. Kilel ni mmoja tu wa wakazi wengi katika kambi za waliofurushwa kutoka msitu wa Mau wanaioshi kwa shida nyingi. Changamoto kuu ni kutafuta chakula na wakikosa wamo katika hatari ya kufa, hasa tangu kuanza kwa janga la virusi vya Corona nchini.
Uporaji na uharibifu wa mali
Wakazi waliofurushwa wameliambia Shirika la Human Rights Watch kuwa polisi walipora mali yao ikiwemo vifaa vya nyumba, kuwaibia pesa, kuteketeza maghala ya kuhifadhi chakula, na kuharibu mimea iliyokuwa shambani. Vilevile waliwaua mifugo wao. Vitendo hivi vinakiuka taratibu za kuongoza shughuli za kuondolewa kwa lazima kwa wakazi zilizowekwa na serikali, ambazo zinahimiza kwamba, hatua mahsusi zinapaswa kuchukuliwa kuhakikisha kwamba “hamna anayepokonywa mali yake au kunyimwa haki ya kumiliki mali wakati wa shughuli ya kuondolewa kwa wakazi. Aidha sheria inasema mali yoyote inayoachwa nyuma wakati wa shughuli hii inafaa kulindwa dhidi ya kuharibiwa, kupewa mtu mwingine au kukaliwa na kutumiwa na mtu mwingine.”
Licha ya maafisa wakuu wa serikali katika kaunti ya Narok kudai kwamba waliwaruhusu wakazi waliofurushwa kuondoa mali yao, waathiriwa hao walisema kuwa, hawakuruhusiwa kuvuna mazao yao shambani, wala kuondoa chakula chao katika maghala, na hata walinyimwa fursa ya kubeba mali iliyokuwepo katika nyumba zao. Badala yake, maafisa wa polisi waliharibu mimea iliyokuwa imekomaa, na kuteketeza mashamba na nyumba za waathiriwa, walisema.
Katika kambi ya Ol Megenyu, tulikumbana na Purity Chebet mwanamke mwenye umri wa miaka 30. Purity, hajazungumza kwa muda wa miezi tisa. Hii ni baada ya kukumbwa na kiharusi (stroke) wakati polisi walipovamia makazi ya familia yake yaliyokuwa katika eneo la Sierra Leone kwenye msitu wa Mau. Polisi hao walipiga kelele, wakateketeza nyumba, wakapora mali na kufyatua risasi huku wakiwatisha kuwaua Purity na familia yake.
Mwanamume mmoja mwenye umri wa miaka 56, ambaye ni baba ya watoto wanne aliyeondolewa katika kijiji cha Kirobon alisema alikuwa mgonjwa siku hiyo na akashindwa kuondoa mali yake. Alielezea:“Niliporejea baada ya muda, nilipata nyumba zangu tatu zikiwa zimeteketezwa, pamoja na mali yangu yote iliyokuwemo. Nilipoteza kila kitu.”
Mtu mwingine mwenye umri wa miaka 47, aliyefurushwa kutoka kijiji cha Kitoben, alisema kwamba hakuwa amepata mlo kwa muda mrefu, na ilibidi alazwe kwa wiki nzima katika Hospitali ya Tenwek katika kaunti ya Bomet, yapata kilomita 70 kutoka kambini anamoishi. Ilikuwa baada ya polisi kuteketeza na kuharibu hifadhi zake za chakula wakati wa oparesheni hiyo. Alikariri kilichotokea:
“Sikuwa na chakula kwa muda mrefu, afya yangu ilidhoofika, ilibidi nilazwe hospitalini. Daktari alinielezea kwamba utumbo wangu ulikuwa umeathirika kwa kujikunyata na kufungana tumboni.”
Wakimbizi hao waliliambia Shirika la Human Rights Watch kuwa polisi waliwazuia waliokuwa wakitaka kurejea makwao kuchukua mali yao au hata kuvuna mazao yao.
Mmoja wao, mwanamume mwenye umri wa miaka 42, aliyeondolewa kutoka kituo cha kibiashara cha Sierra Leone alisema alimiliki nyumba na duka, lakini alitishwa na maafisa wa usalama kwamba atafyatuliwa risasi alipojaribu kurejea nyumbani kwake:
“Kila mara tulipojaribu kurejea, polisi walitufukuza, kuturushia gesi ya kutoza machozi na kututisha kwamba watatufyatulia risasi. Wale waliopatikana katika eneo hilo walipigwa na polisi hao.”
Wakazi wengine waliorejea walikamatwa na kushtakiwa kwa makosa kadhaa ikiwemo kupatikana na silaha kama vile mishale na nyuta. Mnamo mwezi Machi, mwanamume mwenye umri wa miaka 26, ambaye sasa anaishi katika kambi ya Ol Megenyu alielezea kukamatwa kwake mnamo mwezi Novemba 2019: “Maafisa wa polisi kituoni walipekua mifuko yangu na kuchukua simu yangu ya rununu na pesa taslimu Shilingi 8,000. hawakunirejeshea.” Alisema kwamba, licha ya polisi kumkamata kwa sababu ya kuwapiga picha wakiwa kazini, alipofikishwa mahakamani alisomewa mashtaka ya kupatikana na nyuta na mishale. Hadi sasa hajarejeshwa mahakamani kujibu mashtaka. Mlinzi mmoja wa mkuu katika Shirika la Kuwalinda Wanyama Pori (KWS) aliliambia Shirika la Human Rights Watch mnamo mwezi Machi kwamba watu hao waliwashambulia polisi kwa kutumia mishale na nyuta.
Watu waliohojiwa katika kambi zote walidai polisi walipora mali yao ya nyumba wakati wa shughuli hiyo, walipora maghala yao na kuteketeza kilichosalia. Mwanamume mwenye umri wa miaka 65 anayeishi katika kambi ya Sagamian alielezea kisa kilichotokea mwezi Agosti mwaka jana, kwamba maafisa wanane wa polisi walivamia nyumba yake, na kuchukua redio yake na vifaa vingine vya elektroniki, vyombo vya jikoni, na kumpiga mkewe mwenye umri wa miaka 50. Mwanamke huyo alivunjika mguu alipojaribu kutoroka kichapo vya polisi hao.
Mnamo mwezi Juni, kuliripotiwa mlipuko wa maradhi katika kambi hizo mbili, wakazi wengi waliathirika, na wengine huenda walifariki kwa sababu ya utapia mlo wakati huu wa kuenea kwa ugonjwa wa virusi vya Corona (COVID-19). Wakazi hao wameelezea kupata mwili wa Selina Toweett, alikuwa katika miaka ya hamsini hivi, Selina alifariki katika makazi ya muda katika kambi ya Sagamian. Inaaminika alikuwa na maradhi yanayotokana na utapia mlo, kwa kuwa alikuwa amezunguka kambi hiyo kwa kipindi kirefu akiomba msaada wa chakula.
Hali katika kambi za waathiriwa wa oparesheni
Watu waliofurushwa kutoka kwenye ardhi zao walikumbwa na wakati mgumu hata kabla ya kuanza kwa janga la kuenea kwa virusi vya Corona mnamo mwezi Machi wakati wachunguzi wa Shirika la Human Rights Watch walizuru eneo hilo. Wengi wao walitegemea misaada kutoka kwa wahisani, hasa wanasiasa, au kwa kutafuta kazi ya vibarua.
Kutokana na kuharibiwa kwa mazao yao, waathiriwa hao hawakuwa na chakula walipopata hifadhi katika kambi ya muda iliyo umbali wa kilomita mbili kutoka msitu wa Mau. Watu 5 waliohojiwa walisema kuwa hawakupata chakula kwa siku kadhaa baada ya kufurushwa. David Kipng’eno Rono, mwenye umri wa miaka 47, alisema kuwa hakula kwa siku saba, alilala nje kwenye baridi mwezi wa Septemba, baada ya polisi kumfurusha kutoka kijiji cha Kapsilbwa kwenye msitu huo ambapo pia waliharibu mazao yake yote.
Licha ya matatizo haya yote yanayowakabili waathiriwa hawa, maafisa wa serikali katika kaunti ya Narok wameendelea kusisitiza kuwa kambi hizo sio halali, na kwamba shirika lolote la msaada linalotaka kusaidia lazima liwe na ruhusa ya serikali kufanya hivyo.
Na hadi sasa watu hao waliofurushwa wamepata msaada wa chakula mara moja tu, mnamo mwezi Aprili, huu ukiwa ni msaada kutoka kwa mbunge wa eneo hilo. Kazi za vibarua hazipatikani kwa sasa, tangu kufungwa kwa biashara nyingi kulipotokea janga la virusi vya Corona (Covid-19) lililofwatiwa na vikwazo vya serikali kuzuia maradhi kuenea.
Kutotolewa kwa Ilani ya kuondolewa
Maafisa wa serikali walitekeleza shughuli hii bila kuzingatia Mwongozo wa Kuwafurusha Watu wa 2010, unaoitaka serikali kuwapa waathiriwa notisi ya muda wa siku 90. Aidha huitaka ichapishe katika Gazetti rasmi la serikali notisi hiyo, na kuweka matangazo katika sehemu za umma kuwalenga waathiriwa. Mwishoni mwa mwezi Agosti, aliyekuwa kamishna wa kaunti ya Narok, George Natembeya, alitoa ilani ya siku 60, na kisha kuruhusu wakazi hao kuondolewa makwao siku moja baada ya kuchapishwa kwa notisi hiyo. George Natembeya, alitoa tangazo hilo kwa vyombo vya habari alipozuru eneo hilo la msitu wa Mau mnamo Agosti 28, 2019. Polisi walianza kuwafurusha wakazi Agosti 29.
Kamishna wa sasa katika kaunti hiyo Samuel Kimiti, alikiri kwamba serikali haikuchapisha na kusambaza notisi hiyo kwa waathiriwa. Maagizo ni kwamba notisi ichapishwe na kuwekwa katika vituo kadhaa vinavyoweza kufikiwa na waathiriwa. Pia notisi inafaa kutoa maelezo zaidi ya siku, wakati na jinsi shughuli ya kuwaondoa watu itakavyotekelezwa na mbinu za kuzuia madhara kwa wahusika.
Kutowafidia na kuwapa makao mapya waathiriwa
Shirika la Human Rights Watch lilipata kwamba serikali haikuwafidia au kuwapa makao mapya watu hao. Kwa hivi sasa wanaishi katika mazingira mabaya na magunu yasiyo na maji safi wala usafi katika kambi hizo.
Kabla ya shughuli hiyo na baada ya kuhamishwa kwa wakazi hao serikali ilisisitiza kupitia vyombo vya habari kwamba haitawafidia wala kuwapa makao mapya wale waliokuwa wamejenga makazi haramu, kwa kuwa walikuwa wamenyakua ardhi hiyo na kuishi katika eneo la msitu. Hii ni licha ya kwamba baadhi yao walikuwa na hati halali za kumili ardhi zilizotolewa na Wizara ya Ardhi.
Kamishna wa kaunti ya Narok Samuel Kimiti, alisema:
“Tukiwa serikali hatuna mipango yoyote ya kuwafidia. Unawezaje kumfidia mtu ambaye amekalia ardhi isiyo yake, ardhi ambayo ni ya serikali? Na hata wale wanaodai kuwa na hati-miliki lazima wangeelewa kwanza sheria kabla ya kukabidhiwa hati hizo.”
Katika mikutano kadhaa na waandishi wa habari mnamo mwaka 2019, waziri wa mazingira, Keriako Tobiko, alisisitiza msimamo wa serikali, akiongeza kwamba haitawafidia wale walio na hati-miliki kwa kuwa hati hizo zilikabidhiwa kwa njia zisizo halali.
Afisa mmoja wa idara ya upelelezi wa jinai- CID, mjini Narok, alielezea Shirika la Human Rights Watch kwamba polisi wamekuwa wakichunguza kwa muda mrefu visa vya kuuza na kunyakuliwa kwa ardhi ya Mau lakini hadi sasa hakuna aliyekamatwa au kushtakiwa.
Mwongozo wa Kenya ya mwaka 2010 kuhusu kuwahamisha watu, unaelezea kwamba:
“Serikali itachukua hatua zote zinazotakikana, kadri ya uwezo wake, na pale raslimali itaruhusu, kuhakikisha kuwa inawapa waathiriwa wote wasiojiweza, makazi, kuwapa makao mapya, na uwezo wa kumiliki ardhi, kwa kila anayestahili kadri inapowezekana.”