(Nairobi) – Tangu tarehe 25 mwezi Disemba, 2019, maafisa wa polisi nchini Kenya wamewauwa kwa kuwapiga risasi watu wanane katika makaazi ya mabanda ya Mathare, Kasarani na Majengo yaliopo mjini Nairobi, shirika la haki za binadamu la Human Rights Watch limesema leo. Maafisa wa polisi wanaendelea kuwauwa washukiwa wakuu wa uhalifu na waandamanaji licha ya wito wa mara kwa mara kwao kusitisha mauaji na utumiaji wa nguvu wa kiholela.
Mauaji hayo ni ya hivi karibuni katika mtindo unaotumiwa na Polisi wa utumiaji wa nguvu na mauaji ya kiholela Mjini Nairobi hususan katika makaazi ya watu wenye kipato cha chini. Serikali ya Kenya inapaswa kufanyia uchunguzi madai yote ya mauaji mengi yakiwa yamenakiliwa na mashirika ya haki za Binadamu nchini Kenya pamoja na yale ya kimataifa, na kuhakikisha kuwa wahusika wote wanawajibika.
“Maafisa wa polisi nchini Kenya wamekuwa wakiwapiga risasi na kuwaua vijana bila kujali sheria kuhusu utumiaji wa nguvu,” alisema Otsieno Namwaya, mtafiti mwandamizi katika shirika la Human Rights Watch. “Mamlaka nchini Kenya inapaswa kusitisha mauaji haya haramu ya watu wasiojulikana na kuwafungulia mashtaka maafisa wa polisi waliohusika.”
Mnamo mwezi Januari 2020, Shirika la Human Rights Watch liliwahoji watu 23 wakiwemo mashahidi, watu wa familia ya waathiriwa, maafisa wa vyumba vya kuhifadhia maiti, wahudumu wa afya, wanaharakati na maafisa wa polisi. Shirika la Human Rights Watch lilifanya kazi kwa karibu na mashirika washirika katika maeneo ya Mathare, Majengo na Kasarani ili kutambua waathiriwa na familia zao.
Shirika la Human Rights Watch lilibaini kwamba katika vitongoji vitatu vya wakaazi wa mapato duni, maafisa wa polisi waliwaua takriban vijana wanane wiki tatu baada ya likizo ya Krimasi. Kwa mjibu wa mashahidi, mnamo tarehe 25 Mwezi Disemba, katika eneo la Mathare,muda wa saa kumi na moja unusu jioni, polisi walimpiga risasi na kumuua Peter Irungu mwenye umri wa miaka 19 na Brian Mung’aru mwenye umri wa miaka 20. Wote wawili walikuwa wamepiga magoti na kuwaomba polisi kutowaua, wakati walipopigwa risasi.
Mnamo tarehe 26 Mwezi Disemba, maafisa wa kukabiliana na ghasia walitumia nguvu kuzima maandamano kuhusu mauaji ya vijana hao kwa kutumia risasi, vitoa machozi na kuwapiga waandamanaji. Polisi waliwapiga waandamanaji na kuwajeruhi zaidi ya watu 10 na kuwakamata wengine wengi. Maafisa wa Polisi walizuia vyombo vya habari kuingia katika mtaa wa Mathare ili kuangazia maandamano hayo kulingana na mashahidi katika eneo hilo.
Wakati wa maandamano yaliofanyika katika makaazi ya Kasarani, tarehe 15 mwezi Januari kulalamikia barabara mbovu, polisi waliwafyatulia risasi waandamanaji na wakaazi. Katika kisa hicho walimpiga risasi na kumuua mfanyakazi wa magari ya usafiri mwenye umri wa miaka 19 Stephen Machurusi, walioshuhudia walimuona Machurusi akiwa amewapigia magoti na kuwaomba polisi wa kukabiliana na ghasia waliokuwa wamefunga upande mmoja wa barabara kumruhusu kupita ili akwende kazini.
Mwanaharakati wa miaka 30 katika eneo la Kasarani aliyeshuhudia mauaji hayo alisema: “Nilipokuwa nikielekea kazini nilikutana na kijana aliyekuwa akiwatoroka polisi. Hakujua kwamba kulikuwa na maandamano. Alisalimu amri kwa polisi kwa kuinua mikono juu na kusema alikuwa anaelekea kazini lakini afisa mmoja alimpiga risasi kifuani akiwa karibu.”
Katika eneo la Majengo, mnamo tarehe 16 Mwezi Januari, maafisa wawili wa polisi waliokuwa wakipiga doria walimuua Ahmed Majid mwenye umri wa miaka 24. Walioshuhudia wanasema kwamba maafisa walimpiga risasi alipokuwa akijaribu kuingilia kati wakati maafisa hao walipokuwa wakimburuza rafikiye Yassin Athuman, mwenye umri wa miaka 20 ardhini ili kumpeleka katika kituo cha polisi. Maafisa hao walikuwa wamejaribia kumulimbikizia Yassin madia ya kupatikana na mihadarati aina ya bangi dai ambalo alikataa, baada ya kukataa kuwapatia hongo, mashahidi hao walisema.
Mnamo tarehe 17 Mwezi Januari, Polisi waliwaua watu wengine wanne wakati wa maandamano yaliofanyika katika eneo hilo la Majengo wakipinga mauaji ya Majid. Mwanaharakati wa kutetea haki za binadamu katika eneo hilo la Majengo aliyenakili ghasia hizo alisema: “Polisi walitumia nguvu nyingi sana kuzima maandamano hayo. Walikuwa wakitumia risasi wakati mwingi, wakifyatua risasi ndani ya nyumba za watu ama hata kuwalenga watu ambao hawakuhusika na maandamano.” Polisi walijibu madai hayo kwa kuwaambia waandishi wa habari mnamo Janauari 18 kwa afisa aliyehusika na ukiukwaji wa sheria na aliyeshukiwa kwa mauaji ya Majid alikuwa amekamatwa.
Maujai haya ya hivi karibuni ndio mapya katika mtindo wa mauaji na utumiaji wa nguvu kupitia kiasi katika maeneo hayo. Mnamo mwezi Julai 2019, Shirika la Huma Rights watch lilinakili kesi 21 za mauaji yanayotekelezwa na polisi dhidi ya vijana na wanaume katika mitaaa ya Mathare na Dandora mjini Nairobi, bila sababu yoyote, wakidai kwamba walikuwa wahalifu. Mnamo tarehe 24 Mwezi Januari 2020, Tume huru ya Kuratibu maswala ya Polisi - IPOA ilisema kwamba imerikodi ongezeko la unyanyasaji wa Polisi ikiwemo mauaji, visa hivyo vimefikia 3200 katika mwaka wa 2019 pekee. Mnamo tarehe 23 Mwezi Januari 2019, waziri wa maswala ya ndani Fred Matiangi alisema kwamba serikali itasitisha mauaji ya kiholela ya washukiwa ambayo alidai yanatekelezwa na maafisa wadhalimu.
Vyombo vya habari nchini Kenya vimeripoti mauaji yanayotokeo mara kwa mara katika makaazi ya mabanda. Mnamo Mwezi Mei 2018, gazeti la ‘The Standard’ liliripoti kwamba maafisa wa polisi waliwaua takriban watu 10 waliokuwa kati ya umri wa miaka 18 hadi 23 katika kipindi cha juma moja. Mnamo mwezi Oktoba 2018, gazeti la ‘Daily Nation’ liliripoti kwamba karibia watu 101 mjini Nairobi waliuawa na wengine zaidi ya 180 wakiuawa nchini Kenya kwa jumla katika kipindi cha miezi tisa. Haijabainika kutoka kwa ripoti za vyombo vya habari iwapo mauaji hayo yalitekelezwa chini ya sheria au la.
Kulingana na Sheria ya Polisi nchini Kenya kifungo cha 2011, Utumiaji wa nguvu au wa silaha ni halali pale ambapo Afisa yoyote wa Polisi analazimika kulinda maisha yake au ya raia. Walinda Usalama wa Kenya pia wanapaswa kuheshimu azimio la Umoja wa Mataifa kuhusu utumiaji wa nguvu na silaha kwa watekelezaji sheria, inayosema kwamba Walinda Usalama wanafaa kutumia njia salama na zisizo na ghasia na kulazimika kutumia nguvu za silaha pale wanapokabiliw ana hali ya kushindwa kulinda usalama wa maisha. Sheria hiyo pia huzitaka serikali kuhakikisha kuwa Afisa yoyote anayetumia vibaya nguvu na silaha anaadhibiwa kama kwa kutekeleza tendo la uhalifu.
Sheria ya Polisi inawataka Maafisa wa Polisi wanaotumia silaha zao kuripoti kwa wakubwa wao, wakieleza sababu zilizowalazimu kutumia nguvu hizo. Maafisa wa Polisi pia wanatakiwa kuripoti ili kufanyiwa uchunguzi utumizi wowote wa nguvu unaosababisha kifo ama majeraha mabaya kwa Tume huru inayosimamia Maswala ya Polisi IPOA - taasisi ya Kiraia iliyoanzishwa Mwaka 2011 kuchunguza na kuwashtaki Maafisa wa Polisi wanaohusika na unyanyasaji.
Katika kesi zote zilizonakiliwa na Shirika la Human Rights Watch, Maafisa wa Polisi hawakuripoti ama hata kuanza uchunguzi kama wanavyohitajika na sheria. Katika visa vingine, polisi hawakuwaruhusu waathiriwa na familia zao kuwasilisha ripoti. Katika kisa kimoja, Polisi walionekana kukusanya mabaki ya risasi na kuyaficha badala ya kusubiri wachunguzi kuwasili kama inavyostahili katika sheria inayohitajika kufuatwa nchini Kenya.
Tume ya IPOA, ilianzisha uchunguzi kuhusu mauaji ya vijana wawili katika eneo la Mathare mnamo tarehe 25 Mwezi Disemba na mauaji ya Majid katika eneo la Majengo tarehe 16 Januari, Afisa wa IPOA aliambia Shirika la Human Rights Watch.
Hakuna uchunguzi mwengine wowote unaoendelea kuhusu mauaji hayo mengine. Tume hiyo inakabiliwa na changamoto chungu nzima wakati inapotekeleza kazi yake, ikiwemo ukosefu wa ushirikiano kutoka kwa Maafisa wa Polisi ambao hukosa kuandaa ripoti za awali kuhusu mauaji, na ambazo zinafaa kuwafichua Maafisa waliohusika. Licha ya juhudi zake uchunguzi wa Tume hiyo umeweza tu kufanikisha mashtaka kwa kesi sita pekee tangu 2013 wakati shirika hilo lilipoanza operesheni zake na kufikia sasa bado lina kesi takriban 2000 zinazoendelea kuchunguzwa.
Mauaji haya ya watu wanane tangu Disemba 25 ambayo watafiti wa HRW walinakili katika makaazi ya watu wa mapato ya chini jijini Nairobi kama vile Mathare, Majenngo na Kasarani yanaonyesha jinsi Maafisa wa Polisi wanavyotumia nguvu wakijidai kwamba wanajaribu kuweka amani katika mitaa ya mabanda ya Nairobi.
“Polisi wana jukumu la kuhakikisha kwamba maafisa wote wanafuata sheria ya kuchunguza mauaji yote na kusaidia taasisi za uwajibikaji kama vile IPOA ili kuhakisha kwamba wale wanaohusika katika mauaji wanawajibika,” Namwaya alisema. “Serikali, kuanzia kwa Rais Uhuru Kenyatta inafaa kuhakikisha kwamba mauaji yanasitishwa na kwamba wale waliohusika kwa kuwapiga risasi na kuwaua vijana wanakamatwa na kushtakiwa kwa haraka.”
Kwa maelezo Zaidi kuhusu mauaji ya hivi karibuni, tafadhali fuata maelezo yaliyo hapa chini.
Mauaji Katika Eneo la Mathare
Mashahidi katika eneo la Mathare waliambia Shirika la Human Rights Watch kwamba mwendo wa saa kumi na moja jioni mnamo tarehe 25 mwezi Disemba, Maafisa wanne waliokuwa wakishika doria wakiwa wamevalia nguo za raia waliwakamata vijana wanne nje ya Makaazi ya watoto ya Good Samaritan katika mtaa wa Mathare, mojawepo wa mitaa ya wakaazi wa mapato duni mjini Nairobi. Mfanyakazi mmoja wa nyumba hiyo alisema kwamba vijana hao walioishi katika nyumba hiyo walikuwa wamemaliza Sherehe za Krisimasi wakati maafisa hao walipowakamata hapo nje. Wakaazi wa Mathare waliwatambua Maafisa hao wanne kama wale wa Kikosi cha Polisi maarufu kama ‘Pangani six squad’. Kikosi hicho kimehusishwa katika mauaji kadhaa ya wavulana na wasichana katika eneo hilo wengine ambao vifo vyao vilinakiliwa na shirika la Human Rights watch Mwaka 2019.
Mashahidi walisema kwamba maafisa waliwakamata vijana hao na kuwapekua mwilini bila kupata silaha zozote. Afisa mmoja alimshika Brian Mungaru na Peter Irungu kwa nguvu katika mashati yao na kuwapeleka kando, huku maafisa wengine watatu wakitembea nyuma na vijana wengine wawili Felix Ouma na Daniel Gitau ambapo waliwazaba makofi, kuwapiga makonde na kuwapiga mateke wakati wakiwahoji kabla ya kuwaachilia.
Maafisa hao waliwachukua Mungaru na Irungu katika kituo cha mafuta cha Amana, takriban kilomita moja na nusu kutoka kwa nyumba waliokuwa wakiishi ya watoto na vijana mayatima na kuwapiga risasi na kuwaua wote wawili.
Shahidi mmoja, mfanyakazi wa usafiri aliyekuwa akifanya kazi katika kituo cha matatu karibu na kituo cha mafuta cha Amana anakumbuka kwamba maafisa hao kwanza walimtuhumu Irungu kwa kuwa mhalifu. Wote wawili walililia maisha yao.
“Maafisa hao walimpiga risasi Irungu katika mkono wake wa kulia,” alisema mfanyakazi huyo wa uchukuzi. “Irungu alianguka katika mfereji wa kupitisha maji taka kandokando ya barabara. Mung’aru alizimia aliposikia sauti ya mlio wa risasi.” Alisema kwamba Irungu alijaribu kutambaa ili kupanda katika sakafu ya kituo cha mafuta cha Amana kwa usalama wake, lakini maafisa hao walimpiga risasi mara kadhaa mgongoni na kumuua papo hapo. Maafisa hao baadaye walimfuata Mung’aru ambaye alionekana kama amepoteza fahamu, na kumpiga mateke hadi katika mtaro wa maji taka na kumpiga risasai mara kadhaa.
Shahidi mwengine alisema kwamba maafisa hao baadaye walikusanya mabaki yote ya risasi katika eneo hilo na kwamba gari la polisi liliwasili na kuchukua mili hiyo dakika chache baadaye. Anaamini kwamba hilo lilikuwa jaribio la kutaka kuficha ushahidi.
Uchunguzi wa miili ya wawili hao uliofanywa na Serikali ulibaini kwamba Irungu alipigwa risasi mara tano, moja katika tumbo, moja katika mkono wake wa kulia, nyengine katika taya lake la kushoto na nyingine mgongoni. Na kwamba Mung’aru alipigwa risasi kadhaa mgongoni, eneo la kiunoni na goti la kulia.
Polisi hawajachunguza mauaji hayo kama inavyohitajika chini ya Sheria ya Kenya. Tume ya IPOA imeanzisha uchunguzi, lakini polisi hawajakubalia kushirikiana, ikiwemo kukataa kutoa ripoti kuhusu uchunguzi wa Makamanda wa Kituo.
Polisi wametoa ripoti yenye maelezo yanayokinzana na mauaji hayo. Rekodi za Kituo cha Polisi cha Pangani zinasema kwamba wawili hao waliuawa katika wizi wa mabavu katika eneo la Mathare lakini sIku tatu baada ya mauaji, Kamanda wa Kaunti ya Mji wa Nairobi alitaja kuwa mauaji hayo yalikuwa ‘ufyatulianaji wa risasi kati ya maafisa wa polisi na wahalifu watatu’.
Mauaji Katika Eneo la Kasarani
Mnamo Januari 13, katika eneo la Kasarani, wakaazi na waendeshaji Magari ya “Matatu” waliandaa maandamano ya amani katika barabara za eneo hilo. Walikuwa wakilalamikia barabara mbaya. Tarehe 15 Januari, Maafisa wa kuzima ghasia walipelekwa katika eneo hilo kuzima maandamano, waliwapia watu, kuwarushia mateke na makonde na kufyatua gesi ya kutoa machozi na kuwalenga na risasi bila kujali. Baadhi ya nyumba za wakaazi pia zililengwa.
Mmoja wa waandamanaji aliyeshuhudia mauaji alisema kuwa Maafisa wa Polisi walimpiga risasi na kumuua Stephen Muchurusi mpitaji barabarani aliyekuwa na umri wa miaka 19 na ambaye alikuwa akifanya kazi ya uchukuzi. “Karibia saa saba hivi za mchana, Afisa mmoja aliyekuw akifyatua risasi alimlenga Muchurusi kiholela, Kijana huyo alikuw aamepiga magoti na kuomba aachiliwe, alipigwa risasi kwenye kifua.”
Hadi sasa hakuna uchunguzi ambao umeanzishwa na Polisi wala Tume Huru ya IPOA kuhusiana na mauaji hayo au jinsi Polisi walivyotenda kazi wakati wa kuzima maandamano hayo. Jamaa na walioshuhudia mauaji hayo wanasema hadi sasa hawajahojiwa kuhusiana na kisa hicho.
Mauaji Katika Eneo la Majengo
Shirika la Human Rights Watch lilibaini kwamba maafisa wa polisi walimpiga risasi na kumuua Ahmed Majid mwenye umri wa miaka 24 katika eneo la Majengo kwasababu aliwataka kumbeba rafikiye Yassin Athuman hadi kituo cha polisi au wamruhusu kutembea badala ya kumburuza. Mauaji hayo yalisababisha ghasia chache siku hiyo. Siku ambayo Majid alizikwa mnamo tarehe 17 Mwezi Januari, kulikuwa na maandamano makubwa ambayo polisi wa kukabiliana na ghasia walijaribu kuyazima kwa kurusha vitoa machozi na risasi katika makaazi ya watu na pia kuwalenga waandamanaji hao.
Rafiki wa karibu wa Majid ambaye alishuhudia mauaji hayo alisema kwamba dakika chache kabla ya saa sita tarehe 16 Januari, Majid alikutana na maafisa wawili wa polisi mita 10 kutoka nyumbani kwake. Maafisa hao walikuwa wamemkamata Yassin, ambaye ni mwendeshaji wa boda boda, alikuwa akisubiri abiria katika barabara moja katika eneo hilo la Majengo. Maafisa hao walisema kwamba mtu mmoja aliyewaona wakimkamata Yassin alimshutumu jamaa huyo kwa kuwa mvutaji bangi, kitu alichokana. Baadaye maafisa hao walijaribu kumwekea bangi katika nguo zake. Ndugu za Majid walioshuhudia tukio hilo walisema kwamba Polisi hao walikuwa wanamburuza Yassin aliyekuwa amefungwa pingu.
Mwanamke mwenye umri wa miaka 23 aliyeshuhudia kisa hicho alisema kwamba Majid alijaribu kuingilia kati lakini afisa mmoja akamchapa kofi na baadaye kumpiga risasi kifuani wakati alipokua ameanguka.
Shahidi mwengine alisema kwamba Afisa wa pili alijawa na wasiwasi na kumfungua Yassin na baadaye Maafisa wote wawili wakakimbilia Kituo cha Polisi wa AP kilichokuwa karibu yao ili kukwepa raia waliojawa na ghadhabu. Marafiki akiwemo Yassin walimkimbiza Majid katika zahanati ilikuwa karibu na eneo hilo, ambapo aliaga dunia.
Mchana huo, wakaazi walifanya maandamano, ambayo yaliongezeka kasi na kuwa mabaya Zaidi keshoye wakati wa chakula cha mchana baada ya mazishi ya Majid.
Mwanaharakati wa kutetea Haki za Binadamu katika eneo hilo Majengo alisema: “Maafisa wa polisi walitumia nguvu kupita kiasi kuzima maandamano . Walitumia risasi ambazo walikuwa wakifyatua wakilenga watu na makaazi yao.”
Mwanaharakati huyo alisema kwamba alinakili visa vinne vya watu kupigwa risasi na Polisi hadi kufa, watu saba walilazwa hospitalini wakiwa na majeraha ya kupigwa risasi na visa 30 vya watu kuuguza majeraha ya mashambulizi ya polisi. Shirika la Human Rights Watch lilifanikiwa kubaini mauaji hayo ya watu wanne.
Mmoja ya wale waliouawa siku hiyo alikuwa Samuel Chegero Barasa mwenye umri wa miaka 35 ambaye yeye na familia yake walikuwa wamejifungia ndani ya nyumba yao wakati walipowaona Maafisa wa Polisi wakifukuza waandamanaji vijana, wakiwafyatulia risasi na kuwarushia vitoa machozi. Risasi moja ilipita katika mabamba ya nyumba ambayo alikuwa ametumikia kama ukuta wa nyumba yake na kumpasua kichwa, alisema mkewe Alice Andeso. Aliambia vyombo vya habari kwamba alikuwa na mwanawe mwenye umri wa miaka mitatu wakati alipoona mwili wa mumewe umelala ukiwa unamwagika damu nyingi katika chumba cha wageni. “Je kichwa cha babangu kimeenda wapi?” Alisema mwanawe alimuuliza. Alisema mwanawe alishindwa kuzungumza kwa takriban wiki moja baada ya mauaji hayo.
Mashahidi waliokuwa karibu na msikiti wa Riadha wakati wa maandamano hayo walielezea mauaji ya watu watatu ambao hawakutambulika. Katika kisa kimoja muda wa saa tisa jioni Polisi walimpiga risasi kijana wa kurandaranda mjini ambaye alikuwa amelala katika eneo linalojulikana kuwa Toilet 34, nje ya msikiti wa Riadha na baadaye wakaubeba mwili wake na kuondoa maganda ya risasi yaliokuwepo.
Human Rights Watch waliutafuta na kupata mwili wake katika chumba cha kuhifadhia maiti cha City ambapo ulipelekwa na Polisi na kusajiliwa kama “mwanamume mwenye asili ya Ki-Afrika asiyejuliakana aliyepigwa risasi wakati wa maandamano ya ghasia katika eneo la Majengo.” Maafisa wa chumba cha kuhifadhia maiti walisema Kwamba mtu huyo alikuwa na kitambulisho kwa jina Victor Omondi Wanyama, lakini polisi walisema kwamba hawakuwa na hakika kilikuwa cha kijana huyo.
Watu wawili waliokuwa ndani ya msikiti wa Riadha walioshuhudia mauaji hayo walisema kwamba muda mfupi baada ya polisi kumuua kijana huyo walimuua mtu mwengine ambaye alikuwa amelala katika barabara kati ya msikiti wa Riadha na duka la jumla la Mumbai. Maafisa hao kwa haraka waliubeba mwili wake huku wengine wakikusanya maganda ya risasi. Katika chumba cha kuhifadhi maiti cha City, mwili huo ulipelekwa kama “mwanamume mwenye asili ya Ki-Afrika asiyejuliakana aliyepigwa risasi wakati wa maandamano ya ghasia katika eneo la Majengo.”
Human Rights Watch pia lilipata katika chumba hicho cha kuhifadhia maiti mwili wa mtu aliyepigwa risasi wakati wa maandamano hayo naye pia alikuwa amesajiliwa kama, “mwanamume mwenye asili ya Ki-Afrika asiyejuliakana aliyepigwa risasi wakati wa maandamano ya ghasia katika eneo la Majengo.” Shahidi mmoja aliyekuwa katika eneo la Majengo la Rokongo alisema kwamba “ Mwanamme huyo alikuwa akikimbia katika eneo lilowazi wakati tulipoona ameanguka ghafla.” Wale walioona mwili wake kabla ya Polisi kuuchukua wanasema kwamba alikuwa amepigwa risasi shingoni.