(Dar es Salaam, 14, Februari 2017) – Zaidi ya asilimia 40 ya vijana wa Tanzania hawapati elimu bora ya awamu ya kwanza ya sekondari (kidato cha kwanza hadi cha nne), mbali na uamuzi chanya wa serikali kufanya elimu hii ya sekondari kuwa bure, inasema ripoti iliyotolewa na shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch.
Ripoti hiyo yenye kurasa 98, “‘Nilikuwa na Ndoto za Kumaliza Shule’: Vipingamizi katika Elimu ya Sekondari Tanzania,” inaangazia vikwazo, ikiwa ni pamoja na vikwazo vitokanavyo na sera za serikali zilizopitwa na wakati, ambazo zinazuia zaidi ya vijana milioni 1.5 kupata elimu ya sekondari na kusababisha wengine wengi kuacha shule kwasababu ya hali duni ya elimu. Matatizo hayo ni pamoja na kutokuwepo kwa shule za sekondari vijijini, mtihani unaoweka ugumu wa kujiunga na shule ya sekondari, na sera za kinidhamu za serikali zinazowafukuzisha shule wasichana waliopata ujauzito au kuolewa
“Kufutwa kwa ada na michango mingine katika shule za sekondari nchini Tanzania imekuwa ni hatua kubwa katika kuimarisha ujiungaji wa elimu ya sekondari,” anasema Elin Martínez, mtafiti wa haki za watoto wa Human Rights Watch na mwandishi wa ripoti hii. “Lakini serikali inapaswa kwenda mbali zaidi na kushughulikia swala la idadi kubwa ya wanafunzi katika vyumba vya madarasa, ubaguzi na unyanyasaji wa namna mbalimbali unaoathiri elimu ya vijana wengi”
Mwaka 2016 Human Rights Watch iliwahoji wanafunzi 220 wa shule za sekondari, vijana wasiokuwa shuleni, wazazi, wataalamu wa elimu, wanaharakati, washirika wa maendeleo, na maofisa mbalimbali wa serikali wa mahala na taifa kwa ujumla katika wilaya nane ndani ya mikoa minne nchini Tanzania. Utafiti ulienda sanjali na uanzishwaji wa elimu ya bure ya sekondari kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha nne nchini kote.
Elimu imekuwa kipaumbele cha taifa kwa serikali zote za Tanzania tangu uhuru mnamo mwaka 1961, huku asilimia 22 ya bajeti ya mwaka wa fedha wa 2016-2017 ikielekezwa katika elimu. Hata hivyo, Tanzania, nchi ya kipato cha chini, ni miongoni mwa nchi zenye idadi kubwa ya vijana, ikiwa na takribani asilimia 43 ya idadi ya watu wenye umri chini ya miaka 15.
Tangu mwaka 2005, serikali imechukua hatua muhimu kuongeza kujiunga kwa wanafunzi katika elimu ya sekondari, ikiwa ni pamoja na kuahidi kujenga shule za sekondari katika kila kata. Hata hivyo, Human Rights Watch imekuta katika baadhi ya maeneo ya vijijini nchini, wanafunzi wanasafiri umbali wa hadi kilometa 25 kufika shuleni, na wengi hawana shule ya sekondari katika kata zao. Baadhi ya vijana walishindwa kufika shuleni kwa sababu ya gharama zingine zihusianazo na shule, ikiwa ni pamoja na usafiri, mavazi ya shule, vitabu au gharama za malazi.
“Shule ilianza tangu Januari 11, lakini sio kwangu, kwa sababu wazazi wangu hawana uwezo wa kununua mavazi ya shule, mkoba na vifaa vingine vya darasani,” Msichana mwenye miaka 16 aliwaambia Human Rights Watch. “Waliniambia nisubiri hadi watakapopata pesa – tunahitaji Shilingi elfu 75 (sawa na Dola 34).
Watoto wengi wanazuiliwa kwa sababu hawakufaulu mtihani wa lazima wa kumaliza elimu ya msingi. Kwa sababu wanafunzi hawaruhusiwi kurudia mtihani huo, anaposhindwa mara moja ndio inakuwa mwisho wa safari yake ya shule. Tangu mwaka 2012, matokeo ya mitihani yamekwamisha fursa za watoto takribani milioni 1.6 za kujiunga na elimu ya sekondari. Wengi wao hawajaruhusiwa kurudia mtihani wa darasa la 7, mwaka wa mwisho wa elimu ya msingi. Wanapokuwa nje ya shule, vijana wengi wanakosa namna nyingine mbadala ya kumaliza elimu yao ya muhimu au kuendelea na mafunzo ya ufundi stadi.
Kwa mujibu wa takwimu za Benki ya Dunia, idadi ndogo zaidi ya theluthi ya wasichana wanaojiunga na sekondari humaliza shule. Mara nyingi shule hizi huwafukuza wanafunzi wa kike walio wajawazito kwa sababu ya “kukiuka maadili.” Taratibu za serikali pia huwalazimisha wasichana walioolewa kwa nguvu kabla ya kufikisha miaka 18 kuacha shule. Takribani wasichana 8,000 wanaacha shule kila mwaka kwa sababu ya ujauzito.
Human Rights Watch imegundua kwamba maofisa wa shule hufanya vipimo vya lazima vya ujauzito mara kwa mara, jambo ambalo ni la udhalilishaji. Na mara nyingi wasichana hawaruhusiwi kurudi shuleni hata baada ya kujifungua au wanashindwa kwasababu ya kutotiwa moyo na jamii zao au kukosekana kwa msaada wa watoto wao wachanga.
Serikali inapaswa kupiga marufuku upimwaji wa mimba shuleni, kukomesha ufukuzwaji wa wasichana walioolewa au kupata ujauzito, na kutoa waraka wa kuamuru shule kuwaruhusu wamama hawa vijana kuendelea na elimu ya sekondari, inasema Human Rights Watch.
Elimu bora ya sekondari pia haipatikani kwa vijana wengi walemavu. Pamoja na mkakati jumuishi mkubwa wa elimu wa serikali, shule nyingi bado hazina nyenzo za kutosha kuwasaidia watoto wenye aina mbalimbali ya ulemavu. Waalimu wengi pia hawana mafunzo ya kutosha kuwahudumia walemavu. Serikali inapaswa kuhakikisha kwamba wanafunzi wenye ulemavu wanapata msaada wa kutosha kuwasaidia kujifunza vizuri kama wanafunzi wengine wasio na ulemavu.
Adhabu nyingi za viboko ambazo mara nyingi huwa za kikatili na kidhalilishaji katika shule nyingi za Tanzania zinachangia pia kuathiri mahudhurio shuleni, Human Rights Watch imegundua. Kwa mujibu wa shirika la African Child Policy Forum, adhabu za viboko bado zinaruhusiwa Tanzania, huku zikikiuka makubaliano ya kimataifa, na kutokea kwa kiwango cha kutisha. Hata katika shule ambazo Human Rights Watch ilitembelea, waalimu walikuwa wakitumia adhabu za viboko mara kwa mara, ikiwa ni pamoja na kuwapiga wanafunzi kwa kutumia mikono yao, mianzi au fimbo za mbao au kwa kutumia vitu vingine.
Wafunzi wengi wa kike pia wanakumbana na udhalilishaji wa kijinsia mara kwa mara, na katika shule zingine waalimu wa kiume huwataka wanafunzi wa kike kwa mahusiano ya kimapenzi. Ni nadra sana kwa maofisa wa shuleni kuripoti polisi visa hivi vya udhalilishaji, huku shule nyingi zikiwa hazina utaratibu wa siri wa kuripoti visa hivi. Mwaka 2011, shirika la umoja wa mataifa la watoto (UNICEF), liligundua kwamba takribani msichana mmoja kati ya 10 anakumbana na unyanyasaji wa kingono angali mtoto kutoka kwa mwalimu.
Serikali izuie adhabu za viboko shuleni, na kutengeneza mfumo wa kisiri wa utoaji taarifa ili kwamba wanafunzi wawe huru kutoa taarifa za unyanyasaji. Maofisa wa serikali wachunguze kwa kina tuhuma za unyanyasaji wa kingono ziwahusuzo waalimu na kuwachukulia hatua za kisheria watuhumiwa wote.
“Serikali imeahidi mara nyingi kutoa elimu ya sekondari kwa wote,” anasema Martinez. “Na sasa serikali ifungue mlango wa elimu ya sekondari kwa kukomesha sera za unyanyasaji na udhalilishaji na kuondoa vizuizi vilivyopo kati ya wanafunzi wengi na elimu bora.”
Baadhi ya Nukuu
“Tunapigwa sana. Wakikupiga leo, utapata nafuu baada ya siku mbili – Mwalimu mmoja anaweza kukupiga hata kwa dakika 15 ikiwa anataka.”
–Rashidi, 18, Mwanza, Kaskazini Magharibi Tanzania
“Kuna waalimu wanaojihusisha na maswala ya kimapenzi na wanafunzi – nawafahamu wanafunzi wengi wa kike ambao imewatokea – na ikiwa mwanafunzi atakataa, anaadhibiwa … sina amani. Kuna wasichana watatu waliacha shule kwa sababu ya waalimu na ngono mwaka 2015.”
–Joyce, 17, Shinyanga, Kaskazini Magharibi mwa Tanzania
“Hakuna Perkins Brailler, hakuna kabisa vitabu vya kujifunzia. Hizi mashine tunazotakiwa kuzitumia – hazifanyi kazi kabisa. Inatuzuia kufanya mazoezi yetu vizuri. Napata notsi baada ya wiki mbili au mwezi mzima kabisa baadae [mbele ya mwenzangu]. Inanirudisha nyuma katika maendeleo yangu ya kimasomo – hadi napopata notsi, nakuwa nyuma tayari katika masomo mawili au matatu.”
–Nasser, 18, mwanafunzi wa Kidato cha Nne asiyeona na anasoma shule ya kulala Shinyanga, Kaskazini Magharibi mwa Tanzania